Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mussa Ramadhani Sima (24 total)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, naitwa Mwalimu Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika huu mpango wa Serikali wa kutoa elimu bure, napenda kufahamu Serikali ina mpango gani sasa kuboresha maslahi ya walimu kwa mpango utakaoitwa elimu bure na maslahi bora kwa walimu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua umuhimu wa ualimu, lakini vilevile tunatambua umuhimu wa watumishi wote wa umma. Lakini kwa kutambua umuhimu huo wa walimu kama Serikali, kwa miaka takribani nane tumeshapandisha takribani asilimia 160 ya mshahara wa walimu. Ukiangalia hivi sasa mwalimu wa chini kabisa anapata shilingi 419,000/=, na wa juu anapata shilingi 719,000/=. Tunatambua bado mazingira ya kuishi gharama ni kubwa na wanahitaji kuongezewa kipato na tutafanya hivyo kwa kadri hali ya uchumi itakavyokuwa ikiruhusu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naomba niulize swali dogo. Kwa kuwa Mkoa wa Singida tumejenga Hospitali ya Rufaa na mpaka sasa haijaanza kufanya kazi, je, Serikali iko tayari sasa kuhakikisha hospitali ile inaanza kazi kwa kupeleka vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli na katika ziara yangu hospitali hiyo ni miongoni mwa hospitali nilizozitembelea wakati wa ziara zangu mikoani na siku ile tulikuwa na Mheshimiwa Mbunge, miongoni mwa majengo makubwa sana yaliyojengwa ni lile pale Singida Mjini. Nilitoa maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo kipindi kile na kwa Mganga Mkuu wa Mkoa kuhakikisha hospitali ile inafanya kazi. Ukiangalia inawezekana ikawa Hospitali ya Kanda kutokana na ukubwa wake kwa sababu kuna center kubwa ya akinamama kujifungulia.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha jana nilipata taarifa kwamba kuna watu wanataka kutoa vile vitanda kurudisha mjini, natoa agizo hakuna kuondoa kitanda au kitu chochote katika hospitali ile. Wiki ijayo nitakwenda Singida nataka niikute Hospitali ya Singida inafanya kazi. Sitaki kusikia hospitali ambayo uwekezaji wake ni mkubwa na wa mfano, watu wanatoa vitanda kupeleka sehemu zingine, tutawashugulikia watu wote wanaotaka kufanya ubadhirifu katika sekta ya afya.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Singida mjini kwa asilimia kubwa ya wakazi wanajishungulisha na biashara za mazao hususani biashara ya vitunguu. Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga Soko la Kimataifa la Vitunguu pale Misuna ambalo linawahusisha mpaka wenyeji wa nchi za Afrika Mashariki na Kati?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imeonyesha ina hisa nyingi kwenye Makampuni ya Umma, je Serikali ina mpango gani wa kuongeza hisa lakini pia hold share na kuongeza uzalishaji katika makampuni hayo? Ahsante.
HARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Sima kwa anavyoshughulikia masuala ya masoko na viwanda hapo Singida, hakuna asiyejua kwamba Singida ni wakulima wa vitunguu na wakulima maarufu sana wa zao la alizeti. Serikali inachofanya pamoja na mambo mengine ni kuhakikisha kwamba sasa hivi inawasiliana na Halmashauri ya Singida ili kuona sasa zao la vitunguu linapewa kipaumbele na kuanzisha soko la kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa Singida pamoja na mambo mengine hadi sasa kwa kilimo cha vitunguu pamoja na alizeti nadhani ni Mkoa unaongoza kwa Tanzania kwa sasa ukifuatiwa na Mkoa wa Iringa. Hivyo Serikali inaona kuna umuhimu kweli wa kuanzisha soko la Kimataifa kama ambavyo tumeanzisha masoko mengine mipakani kwa ajili ya kuimarisha mazao ambayo yanalimwa hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Mbunge ni kuhusiana na hisa za Serikali. Ni kweli kabisa Serikali ina miliki hisa katika makampuni mengi sana. Kwa sasa hivi kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi Serikali ina hisa katika makampuni 61 na katika makampuni yale asilimia kubwa ya hisa za Serikali ni chini ya 50. Kama mnavyotambua tuna asilimia kwa sasa hivi kwa mfano Tanzania Oxygen tuna asilimia 9.59, ukienda Kilombero Sugar tuna asilimia 25, ukienda Tanelec tuna asilimia 30. Lakini hata ukienda kwenye makampuni mengine kama migodi Mwadui tuna asilimia 25.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mkakati wa kuongeza za Serikali katika mipango ya kimkakati, mipango ya kimakakati kwa mfano mathalani kwa sasa hivi viwanda vyetu vya nguo kama Urafiki Serikali ina asilimia 49. Serikali inajaribu kuangalia uwezekano wa kuongeza hisa zake ili iweze kuwa na maamuzi ya uzalishaji katika viwanda vile.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiongeza suala lingine kuhusu uongezaji wa hisa katika kuweka asilimia za Serikali, katika mipango na miradi na viwanda vya kimkakati kama viwanda vya chuma cha Liganga, kama viwanda vya Kiwira, Serikali inaona kuwa na asilimia nyingi ili iweze kuwa na uwekezaji yenyewe kama ambavyo inaweza kufanya kwa maendeleo ya wananchi wake.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru. Naomba kuuliza swali la nyongeza, Serikali ina mkakati gani sasa kwa watumishi ambao wamestaafu kwa hiyari ama wengine wamebadilisha kazi kwa mfano kuwa Wabunge, ili kuendelea kuchangia Mfuko huu wa PSPF badala ya kuwaondoa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati uliopo kati ya Serikali na watumishi hawa, nadhani ni ndani ya mtumishi yeye mwenyewe kwamba kama anaona anaweza kuendelea kulipa anaweza kuongea na watumishi wa mfuko huu, Wakurugenzi wetu wote na wote wako tayari na wanapenda kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mussa Sima nikwambie mimi ni mmoja wa waliokuwa watumishi wa Serikali na sasa naendelea kuchangia malipo yangu baada ya mimi kwenda kuongea na Mkurugenzi wa Mfuko wa PSPF na sasa mimi naendelea kuchangia.
Kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, Waheshimiwa Watumishi wote na Watanzania kwa ujumla wanaoona wanaweza kuendelea kulipa basi waende wafike kwenye mifuko hii na wataweza kuendelea kulipa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa niwapongeze Waheshimiwa Naibu Mawaziri wote wawili kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama tu kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sheria hizi za malipo ya pensheni na mifumo ya kuchangia katika mifuko ya pensheni zimehuishwa na sasa kila mtumishi wa umma ama mtumishi katika sekta binafsi anapohama kiajira kutoka ajira moja kwenda ajira nyingine ama anapotaka kuhamisha mafao kutoka mfuko mmoja kwenda katika mfuko mwingine kwa mujibu wa sheria sasahivi anaruhusiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni suala tu kila mtu kufikiria na kuona ni namna gani anataka kuendelea kuhuisha mafao yake na anaweza kuhusiaha katika mfuko wowote kwa kuhamisha kutoka mfuko mwingine kwenda mwingine kama anabadilisha ajira ama anaamua kufanya hivyo na sheria sasa hivi zinaturuhusu. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, niulize maswali madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa kila mwaka mwezi Julai kunakuwa na ongezeko la mshahara, kupanda vyeo ama madaraja kwa watumishi, lakini mpaka sasa Serikali haijafanya chochote.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi katika kuhakikisha kwamba hakutakuwa na mlundikano tena wa madai kwa kupandisha mishahara ya watumishi?
Pili, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha madai haya hayatakuwepo tena? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimhakikishie tu kwamba tunaendelea kulipa madeni haya kwa kadri yanavyojitokeza na kwa kweli ukiangalia tangu mwaka 2013 tulipoanza kutumia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara, madai haya yamekuwa yakiendelea kupungua kwa nyakati mbalimbali.
Vilevile kwa upande wa madeni yanayotokana na kupandisha mishahara na kwa madeni yanayotokana na upandishwaji wa vyeo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari tulishatoa maelekezo kwamba ni lazima madai haya yalipwe kupitia mfumo pindi watu hawa wanapopandishwa vyeo pamoja na madai haya yanapokuwa yamejitokeza ili kuhakikisha kwamba hatuleti milundikano ya madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunakikisha tunakuwa na mkakati endelevu, yapo madai mengine yanatokana na watumishi kuhama, tumeshaelekeza tuhakikishe kwamba mtumishi hahamishiwi kama hakuna fedha za uhamisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai mengine ambayo yamekuwa yakijitokeza kwa wingi ni masuala au madai ya posho ya kukaimu. Tumeshaelekeza pia na yenyewe, pindi barua ya kukaimishwa na marekebisho ya mshahara yanapotoka, basi mtumishi aingiziwe marekebisho hayo mapema na marekebisho ya mshahara yaweze kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukishuhudia baadhi ya waajiri wamekuwa hawatengi fedha kwa ajili ya matibabu, likizo na posho zao nyingine, matokeo yake imekuwa inasababisha sasa pindi mtu anapotakiwa kwenda likizo, inaleta madeni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaagiza waajiri wote, wanapokuwa wanapanga bajeti zao za kila mwaka, wahakikishe stahili za msingi na za kisheria na za kanuni za kudumu za Utumishi wa Umma zinatengwa ili kuhakikisha kwamba hawasababishi madeni, lakini vilevile kuhakikisha tunazingatia haki za msingi za watumishi hao. Nakushukuru.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba sasa niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali tayari imekiri kusambaza mabomba na kupeleka pampu, napenda kujua ni lini sasa utekelezaji wake unaanza kufanyika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la maji ni kubwa katika Jimbo la Singida Mjini hususani kata za pembeni, Serikali inawaambia nini wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwa ajili ya kuhakikisha tatizo hili linaisha?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini mradi wa kusambaza maji katika Mji wa Singida utafanyika, tunahitaji shilingi milioni 730 na tayari tuna vyanzo viwili vya kupata hiyo fedha. Kwanza tumeshaomba fedha kutoka BADEA, lakini pili tumetoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Mamlaka wa Singida kuna fedha kidogo ambazo zipo, kwa hiyo wakati wowote mradi huu utaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua ni lini tutakuwa na mkakati wa kuhakikisha kwamba Mji wa Singida unakuwa na maji ya kudumu. Kama nilivyojibu wakati wa bajeti kwamba tunaanza kujipanga ili tuweze kufanya usanifu wa kutoa maji Igunga kuyaleta Mji wa Singida ili kuhakikisha kwamba sasa tatizo la maji katika Mji wa Singida tunalimaliza. Tutamuagiza Mhandisi Mshauri, aanze kufanya kazi hiyo ili kuona ile pressure iliyoko Igunga inaweza ikafika Singida? Kama itakuwa inapungua basi wataalam watatushauri tufanyeje lakini Mji wa Singida ni mkame tutahakikisha kwamba tunawapa chanzo cha maji chenye uhakika.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Wakati wa kampeni, Mheshimiwa Rais aliwaahidi wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwamba atajenga barabara kwa kiwango cha lami ya kuunganisha Kata zote za pembeni. Sasa, je, mchakato huu wa kujenga barabara utaanza lini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tumepewa ahadi zote ambazo viongozi wetu, Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, walizitoa sehemu mbalimbali za nchi, ahadi zote tunazo. Tulichowekea fedha ili tuweze kuanza kutekeleza katika mwaka huu wa kwanza tunaoanza ni zile barabara ambazo zilishaanza kufanyiwa kazi toka zamani na wakandarasi wako site.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tutakubaliana kwamba ni vyema tukamaliza kwanza ile kazi iliyoanza siku nyingi za nyuma ili wakandarasi wasiendelee kupata fedha bila kufanyia kazi kwa kutopewa fedha za ujenzi na hivyo wanaendelea kukaa pale bila kufanya kazi na tunalazimika kuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kipaumbele cha kwanza ni kukamilisha barabara ambazo zilianza. Nawahakikishieni Waheshimiwa Wabunge kwamba barabara zote ambazo Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais waliziahidi na bahati nzuri tumeshazipata, tutahakikisha tunazipangia ratiba ya utekelezaji katika kipindi kitakachofuata.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika nashukuru sana kwa kuniona, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza. Askari wetu wanafanya kazi kwenye mazingira magumu sana na wanafanaya kazi kwa muda mrefu bila kupanda vyeo mpaka kustaafu. Je, Serikali haioni haja sasa ya kutathmini upya vigezo vya kuwapandisha vyeo ili kuongeza ufanisi wa kazi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa kutumia weledi wake kama mtumishi wa umma na kutambua umuhimu wa motisha inayoambatana na upandaji wa vyeo kwa askari kama ilivyo kwa Mtumishi mwingine ili kuweza kuongeza ufanisi. Wazo lake ni zuri, tumelipokea na Mheshimiwa Rais alishaongelea kuhusu kuongeza motisha kwa watumishi wa umma wote hapa nchini mara baada ya kuwa ameshamaliza marekebisho na kutoa dira ya Serikali yake. Sisi wasaidizi wake tunatembea kwenye miguu yake, tunatembea kwenye maneno yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwahidi Mheshimiwa Mussa Sima taratibu hizo zitakapoanza kufanyika tutatoa kipaumbele kwa vijana wetu wazalendo wanaolitumikia Taifa kwa uzalendo na kwa moyo wao kwa ajili ya kuhakikisha raia wa Tanzania na mali zao wako salama.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Singida Mjini imejaaliwa kuwa na rasilimali ya vyanzo vya umeme kwa maana ya upepo na jua na yako makampuni tayari yamekwishajitokeza kwa ajili ya kuzalisha umeme huo. Sasa na sisi wananchi wa Jimbo la Singida Mjini tumejitokeza kwa maana ya kutoa maeneo yetu kwa ajili ya uzalishaji. Serikali sasa ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba umeme huo unazalishwa ili Singida Mjini iweze kupata viwanda vya kutosha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Singida Mjini kunapita umeme wa kilovoti 40 kuelekea Shinyanga na Namanga na wananchi tayari wametoa maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi huo na wako ambao wameshalipwa fidia na wengine hawajalipwa fidia. Serikali inatoa tamko gani sasa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanalipwa fidia kwa ajili ya kupisha umeme huo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa, Serikali ina mpango mahususi wa kuendeleza wawekezaji binafsi katika umeme mbadala hasa katika maeneo ya Singida ambako kuna umeme wa upepo. Hata hivyo, mkakati wa Serikali wa kwanza, Serikali imetenga kupitia mradi wake wa REA shilingi milioni 42 kwa ajili ya kuendeleza wawekezaji binafsi watakaofanya katika uzalishaji wa umeme pamoja na mambo ya miradi ya maji. Kwa hiyo, wananchi wa Singida watapata pesa hizi kupitia mradi wa REA ambapo watawezeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mkakati mwingine badala ya kupitia mradi wake umeshafadhili sasa, nikizungumzia kwa nchi nzima miradi ya Lukonda kule Njombe pamoja na Ndoya kule Mbinga kama wajasiriamali wa Kitanzania ambao wanawezeshwa kupitia miradi ya Serikali, miradi ya REA. Kwa hiyo, miradi ya Serikali kupitia miradi ya REA kutoa mahususi kwa ajili ya kuendekeza wawekezaji. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Sima na kama kuna wawekezaji wengine kule Singida Mheshimiwa Sima basi walete wataalam wetu watashirikiana na watu wa REA ili waweze kushirikiana zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili kuhusiana na mkakati wa Serikali kulipa fidia kwenye Mradi wa backbone wa kilovoti 400. Kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Sima alivyoshirikiana na Serikali mpaka wananchi takriban 200 wakalipwa fidia awamu ya kwanza. Awamu ya pili nimhakikishie Mheshimiwa Sima, hivi sasa vijiji vyake 13 ambavyo vinaingia kwenye mradi ule vitalipwa fidia jumla ya shilingi milioni 722.7, malipo yataanza mwezi Februari mwaka huu na yatakamilika mwezi Machi na nimhakikishie kwamba vijiji vyake vya Misuna ambavyo vilipitiwa na umeme pamoja na Mtipa pamoja na Kisaki pia vitalipwa fidia kwa utaratibu huo.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti,
nishukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa Singida Mjini ni mji ambao unakua kwa kasi sana kwa sababu Serikali imehamia Dodoma, Serikali haioni haja
sasa ya kutenga fedha kwenye bajeti ya mwaka huu ili uweze kuwalipa fidia wananchi wa kwenye hilo eneo la Manga na Uhamaka ilitoe hilo eneo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa
Serikali imeanza ukarabati kwenye uwanja wa ndege wa sasa, je, Serikali itamaliza ukarabati huo lini ili na sisi tuweze kuutumia uwanja huo kwa kupanda ndege? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Sima na wananchi wa Mji wa Singida wawe na subira, tupate taarifa ya mwisho ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili hatua ya pili ifuate. Si rahisi tukaanza
kutenga fedha kwa mwaka huu na hasa vipaumbele ambavyo tulipitisha mwaka huu, mtakumbuka ambavyo tulipitisha katika mpango wa mwaka huu wa fedha, vinahitaji rasilimali fedha nyingi na hivyo hii kazi tutaifanya mara badaa
ya kazi hii ya upembuzi yakinifu kukamilika. Itakuwa sio rahisi kwa mwaka huu, mnafahamu kwamba bajeti ya mwaka huu tumeshaipitisha katika ngazi ya Kamati na hivi sasa tunaanza kuingiza katika hatua za Bunge Zima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu ukarabati;
nimhakikishie Mheshimiwa Sima kwamba kazi hii ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itakapokamilika suala la ukarabati litafuata.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, namwomba Mheshimiwa Waziri awahakikishie wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kwamba miradi hiyo aliyoitaja, miradi 33 iliyosajiliwa yenye kutoa ajira zaidi ya 4,000 itaanza lini?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Serikali imehamia Dodoma na yako Mashirika ndani ya Wizara, Ofisi za Kanda zipo Dodoma: Je, Mheshimiwa Waziri, sasa upo tayari Mashirika hayo kwa mfano TFDA, TBS na mengine kuanzisha Ofisi za Kanda Singida Mjini ili kuweka ufanisi wa kazi hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ile miradi 33 niliyoisema, nimesema kuanzia mwaka 1996 mpaka Aprili, 2017, miongoni mwa viwanda hivyo ni kiwanda cha mafuta cha Mount Meru, kimeshaanza kazi. Viwanda hivyo vimeshaanza kazi; na mojawapo ya viwanda hivyo ni Kiwanda cha Maziwa anachokijasiria Mheshimiwa Kingu. Tumeshaanza kazi. Tanzania sasa tunajenga viwanda. Sasa labda anieleze wapi anataka mimi nisukume kwa nguvu kusudi mambo ya nchi yetu yaendelee vizuri na yeye yamnyookee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuanzisha kanda za TBS na TIRDO, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna tija kuwa Dodoma ukaanzisha Branch Singida, kwa sababu unaweza kuondoka asubuhi ukafanya kazi Singida, ukarudi hapa, ukarudi tena, ukarudi tena. Kwa hiyo, itabaki Dodoma na itakuwa rahisi hata Mheshimiwa Waziri kwenda na Mheshimiwa, rafiki yake wakaweza kuhamasisha shughuli za viwanda.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa hatua hiyo. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna ongezeko lolote la mshahara kwa watumishi. Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi hawa ambao wamekuwa na moyo mkubwa sana wa kujitolea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna kupandishwa daraja kwa mtumishi yeyote hususan Mwalimu. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kulipa malimbikizo ya mshahara kwa Mtumishi ambaye alistahili kupanda mwaka 2016 mpaka sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya rejea ya takriban siku mbili, Mheshimiwa Waziri anayehusika na mambo ya Utumishi (Waziri wa Utumishi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma) alitoa maelekezo hapa kwamba katika hoja yetu ya Bajeti Kuu ilivyokuwa inapita watu walikuwa wanasema kwamba kwa nini sasa fungu hili la mshahara halipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba Mheshimiwa Rais alizungumza wazi alipokuwa katika viwanja vya Mkoa wa Kilimanjaro katika siku ya Mei Mosi. Jambo hili limezingatiwa katika bajeti yetu hii tunayokwenda nayo hivi sasa. Ndiyo maana hata juzi Waziri wa Utumishi wa Umma alikuwa anatoa maelekezo kwamba kuna nyongeza ya fedha hapa ambayo itaenda ku-address jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la kupanda madaraja, hali kadhalika eneo hilo madaraja yalisimamishwa kutokana na zoezi maalum la uhakiki hasa wa vyeti feki na watumishi hewa. Vile vile naomba nifanye rejea ya Waziri wetu wa Utumishi wa Umma alipozungumza wazi kwamba suala la kupanda madaraja sasa limewekewa utaratibu mzuri, kila mtu atapanda kwa stahiki yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie kwamba kila mtu atapata stahili yake kwa kadri inavyotakiwa na hili Mheshimiwa Waziri amelizungumza wazi kwa sababu yeye ndiyo anahusika na Utumishi kwamba kila mtu atapata stahiki yake na jambo hili sasa hivi linakamilika na kila mtu atapanda daraja kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Waziri kwa majibu mazuri naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa mwaka jana tuliomba fedha kwa ajili ya ukarabati Hospitali yetu ya Rufaa takribani shilingi bilioni 1.7 na tumekwishapata shilingi bilioni moja, je, fedha iliyobaki itakuja lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali la pili, nimuombe Mheshimiwa Waziri aseme kama atakuwa tayari kuambatana nami kwenda kuangalia hali ya Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa na Kituo cha Afya cha Sokoine. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika mpango wa bajeti ilitengwa karibuni shilingi bilioni 1.7 na ndiyo maana kwa mujibu wa Serikali kwa sababu mipango yake ni kuhakikisha miradi hii inatekelezeka tayari tumeshapeleka shilingi bilioni moja. Nishukuru sana wakati naongea na Sekretarieti ya Mkoa mwezi mmoja uliopita walikuwa katika michakato ya kuona ni jinsi gani fedha zile ziweze kutumika vizuri zaidi kuhakikisha kwamba jengo lile linakamilika. Hata hivyo, ni mpango wa Serikali kuhakikisha kwamba hospitali hii inakamilika. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutajitahidi kadri iwezekanavyo fedha zipatikane, mpango ule wa ujenzi wa Hospitali yetu ya Rufaa ya Mkoa wa Singida iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili kwamba ikiwezekana tuweze kuongozana, nimwambie Mheshimiwa Mbunge tujipange ikiwezekana hata kesho mchana, tutoke hapa mara moja tukafanye kazi turudi tuendelee na kazi za Bunge kwa sababu ni lazima tuhakikishe kwamba tunawafikia wananchi kuweza kuwahudumia kwa karibu zaidi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika nakushukuru sana. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, pamoja na kazi nzuri sana inayofanywa na Serikali lakini bado kuna changamoto kubwa kwa akina mama wajawazito wanapokwenda hospitali za umma kwa ajili ya kupata vipimo na matibabu mengine, vifaa havipatikani. Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Serikali inafanya kazi nzuri sana ya zoezi la ukusanyaji damu salama na imetoa mwongozo mzuri kwa Halmashauri zetu kutenga bajeti kwa ajili ya kukusanya damu salama, lakini bado ziko Halmashauri zimeshindwa kutenga bajeti hiyo. Je, Serikali pia inatoa tamko gani kwenye Halmashauri hizi zilizoshindwa kufanya kazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la nyongeza na mwenyewe amekiri jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Serikali ili kuhakikisha kwamba vifaa tiba vinapatikana na kuondoa adha na hasa kwa akinamama kama ambavyo na yeye mwenyewe amekuwa mdau mkubwa kuhakikisha kwamba akinamama hawapati adha hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee naomba niendelee kupongeza Halmashauri yake ambayo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akihakikisha kwamba vifaa tiba vinanunuliwa. Nizitake Halmashauri zingine wahakikishe kwamba vifaa tiba vinatengewa pesa na vinanunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na Halmashauri yake kwa sababu katika hizi pesa ambazo zimelipwa milioni 41 niliyotaja ni pamoja na kitanda cha upasuaji kimeshalipiwa, mashine ya kutolea dawa ya usingizi, jokofu la kuhifadhia damu kama ambavyo amesema Halmashauri zingine hazifanyi, wao wanafanya vizuri sana; mashine ya kufulia moja, vitanda vya kujifungulia vinne, mfumo wa hewa ya oxygen, vitanda vya kubebea wagonjwa. Kwa hiyo, kwa ujumla nizitake Halmashauri zingine zote nchini waige mfano mzuri ambao wenzetu wanafanya ambako Mheshimiwa Mbunge amesemea.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa fedha hizi zimeleta mgogoro sana zinapowekwa kwenye akaunti ya pamoja, je, Serikali haioni haja sasa kuzielekeza Halmashauri kuanzisha akaunti maalum kwa ajili ya hii asilimia 10 peke yake? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliahidi Bunge lako Tukufu kwamba tumechukua maoni ya Mheshimiwa Sima ambayo naamini ni maoni ya Waheshimiwa Wabunge wote na tutalifanyia kazi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Kwa kuwa Tanzania ina wachezaji wachache sana wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi na kwa kuwa vijana wetu wa Serengeti Boys Under 17 walionesha kiwango kikubwa sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwekeza kwa vijana hawa ili tuwe na wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba timu yetu ya Taifa ya Serengeti imefanya vizuri sana katika historia ya nchi yetu na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Sima kwamba juhudi za Serikali sasa hivi ziko katika maeneo mawili. Moja ni kuhakikisha timu hii tunaendelea kuilea kwa sababu hawa ndiyo wawakilishi wetu katika michuano yetu ya olympiki mwaka 2020, kwa hiyo hatuwezi kuwaacha tunaendelea kuwalea kwa karibu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba nimhakikishie kwamba tuko kwenye mazungumzo na wadau mbalimbali, tumepata watu wengi nje ambao sasa hivi tunashirikiana kwa karibu kama Sport Pesa na timu ya Everton FC ambayo iko Premier League ya Uingereza ambao tuna mahusiano mazuri, tumeanza kuongelea kuhusu uwezekano wa kuweza kuchukua baadhi ya vijana wetu. Hayo ni mazungumzo bado hatujapata guarantee nisije nikasikia kesho magazeti yakesema sasa wanakwenda huko, tuko kwenye mazungumzo na tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho nikuhakikishie Mheshimiwa Sima katika kipindi changu cha uongozi wa Wizara hii sitaruhusu kijana yeyote kwenye timu ya Serengeti achukuliwe na timu ambayo ina historia ya uchovu uchovu kiweledi hata kipesa na mimi mwenyewe nitasimamia katika kuangalia mikataba yao. Niwahakikishie tunawaangalia vijana wetu na wataendelea kutusaidia katika kuinua jina letu kwenye ulimwengu wa soka. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naishukuru Serikali kwa hatua hiyo. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna ongezeko lolote la mshahara kwa watumishi. Serikali inatoa tamko gani kwa watumishi hawa ambao wamekuwa na moyo mkubwa sana wa kujitolea?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; tangu mwaka 2016 mpaka sasa hakuna kupandishwa daraja kwa mtumishi yeyote hususan Mwalimu. Je, Serikali itakuwa tayari sasa kulipa malimbikizo ya mshahara kwa Mtumishi ambaye alistahili kupanda mwaka 2016 mpaka sasa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya rejea ya takriban siku mbili, Mheshimiwa Waziri anayehusika na mambo ya Utumishi (Waziri wa Utumishi na Menejimenti ya Utumishi wa Umma) alitoa maelekezo hapa kwamba katika hoja yetu ya Bajeti Kuu ilivyokuwa inapita watu walikuwa wanasema kwamba kwa nini sasa fungu hili la mshahara halipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba Mheshimiwa Rais alizungumza wazi alipokuwa katika viwanja vya Mkoa wa Kilimanjaro katika siku ya Mei Mosi. Jambo hili limezingatiwa katika bajeti yetu hii tunayokwenda nayo hivi sasa. Ndiyo maana hata juzi Waziri wa Utumishi wa Umma alikuwa anatoa maelekezo kwamba kuna nyongeza ya fedha hapa ambayo itaenda ku-address jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la kupanda madaraja, hali kadhalika eneo hilo madaraja yalisimamishwa kutokana na zoezi maalum la uhakiki hasa wa vyeti feki na watumishi hewa. Vile vile naomba nifanye rejea ya Waziri wetu wa Utumishi wa Umma alipozungumza wazi kwamba suala la kupanda madaraja sasa limewekewa utaratibu mzuri, kila mtu atapanda kwa stahiki yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie kwamba kila mtu atapata stahili yake kwa kadri inavyotakiwa na hili Mheshimiwa Waziri amelizungumza wazi kwa sababu yeye ndiyo anahusika na Utumishi kwamba kila mtu atapata stahiki yake na jambo hili sasa hivi linakamilika na kila mtu atapanda daraja kama ilivyokusudiwa. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru na niipongeze Serikali kuwa wazi kwenye swali hili. Pia ni-declare interest, mimi ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka, Mkoa wa Singida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Na. 12 ya mwaka 1967 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1971 na Kanuni za Usajili wa Vyama vya Michezo, Namba 442 ya mwaka 1999, kifungu cha 7(2)(c)(ii), inatambua mamlaka ya Waziri na Waziri ndiyo mwenye maamuzi ya mwisho ya vyama vya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini viko baadhi ya vyama katiba zao hazitambui mamlaka ya Waziri na vyenyewe ndiyo vyenye mamlaka ya mwisho ikiwemo TFF. Mheshimiwa Waziri, nikuombe sana, ikikupendeza kama utakuwa tayari kulinda, kuheshimu na kusimamia sheria hii iliyotungwa na Bunge na kuhakikisha vyama hivi kwenye katiba zao zinatambua role ama wajibu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, Serikali imekiri wazi katika ruzuku ambayo inatolewa TFF ni zaidi ya bilioni 10 na ile dola milioni tatu tunazungumzia karibu bilioni saba, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana, kama utakuwa tayari uiombe TFF ilete mpango kazi kwenye mikoa yetu ili tuweze kujua fedha hizi zinatumikaje. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Sima kwa sababu amekuwa ni mwanamichezo mahiri na vilevile ni mdau mkubwa sana wa michezo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na kujibu swali lake la kwanza ambalo ametaka kujua kama kuna vyama vya mpira ambavyo havitambui mamlaka ya Waziri. Mimi niseme kwamba tunatambua kabisa kwamba TFF pamoja na viongozi wake wote wanapaswa, wanalazimika na hivyo wanatambua mamlaka ya Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Ukisoma Katiba ya TFF, Ibara ya 1(2) inasema kwamba TFF ni chombo cha mpira ambacho kimesajiliwa chini ya Sheria ya Baraza la Michezo ya mwaka 1967 kama ambavyo umesema na marekebisho yake ya mwaka 1971. Kwa maana hiyo sasa, kimsingi kwa sababu Baraza la Michezo ambalo ndiyo ambalo linasajili TFF liko chini ya Wizara ya Habari, kwa maana lipo chini ya Waziri husika mwenye dhamana ya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwa sababu TFF iko chini ya Baraza la Michezo, kwa hiyo, kimsingi ni kwamba TFF inapaswa kutambua mamlaka ambayo Waziri kwa maana ya Serikali inayo. Naamini kabisa kwamba TFF inatambua mamlaka ya Waziri kwa sababu ni takwa la kikanuni na kikatiba na wanapaswa kufanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikija kwenye swali lako la pili ambapo unataka kujua hizi fedha za FIFA Forward ambazo zimetolewa, unaiomba Serikali iweze kuishauri TFF iweze kutoa mchanganuo wa fedha hizo mapema. Mheshimiwa Sima natambua kabisa kwamba wewe ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu katika Mkoa wa Singida na kwa jinsi mimi ninavyotambua ni kwamba humu ndani tuna Wabunge wengi ambao ni viongozi wa vyama vya mipira. Kwa hiyo, najua kabisa kwamba ninyi kama Wenyeviti pamoja na Makatibu ndiyo mhimili mkubwa kabisa wa TFF lakini kimsingi ninyi ndio washauri wakubwa wa TFF. Kwa hiyo, kwa sababu TFF ina taratibu zake, ina mikutano yake ambayo huwa mnakaa na kila mwaka huwa mnakutana, mna mkutano wa robo mwaka, nusu mwaka pamoja na wa mwaka, naamini mtakapokutana ninyi mna nafasi kubwa kabisa ya kuweza kuishauri TFF ili kuweza kuandaa huo mchanganuo wa fedha.
Niseme kabisa sisi kama Serikali tumelipokea wazo lako na tunakubaliana kabisa na wazo lako kwa sababu tunajua kwa namna moja au nyingine litasaidia kuweka uwazi wa mapato na matumizi na kuondoa sintofahamu ambazo zilikuwepo siku za nyuma. Ahsante. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru Serikali kwa majibu yake mazuri. Kwa kuwa hawa Makatibu Wasaidizi wa Tume wote hawajawahi kuteuliwa na hawatambuliki kisheria.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwateuwa hawa ili waweze kufanya kazi yao ipasavyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mashauri mengi ya walimu yamekaa kwa muda mrefu kwa sababu ya ukosefu wa fedha na fedha nyingi haziendi, na leo Serikali imekiri imetenga shilingi bilioni 4.6; Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje viongozi hawa kwamba fedha hizi zitaenda kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama nilivyosema katika swali la kwanza kuhusu uteuzi. Uteuzi huwa ni hatua ya mwisho ya mchakato, na mchakato wenyewe huanza na upekuzi, kumpekua yule mtu unayempendekeza kwenye nafasi fulani. Kwa hiyo mchakato huo uko katika hatua za mwisho.
Napenda kulithibitishia Bunge hili na Mheshimiwa Mbunge kwamba mchakato huo wa upekuzi ambao Idara ambazo zinazofanya upekuzi anazifahamu Mheshimiwa Mbunge zitakapokamilisha upekuzi huo, Makatibu Wasaidizi wote katika Wilaya watateuliwa kwa mujibu wa mapendekezo ya huo upekuzi utakapokamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili naomba nimhakikishie kwamba wakati wa mazungumzo yetu wakati wa bajeti tumehakikishiwa na Waziri wa Fedha kwamba kwa mwaka ujao wa fedha, fedha hizi zitatoka kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ligi yetu ya Tanzania imekuwa ikitumia gharama kubwa sana hata kwenye usajili wa zaidi ya shilingi bilioni moja kwenye timu kadhaa, lakini wanaenda kupokea shilingi milioni 86 na wamecheza kwa mwaka mzima.
Je, Serikali ina mkakati gani kuifanya ligi hii ya Tanzania kuwa ina ushindani? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kama nimemwelewa vizuri Mheshimiwa Sima kuhusu usajili na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimweleze Mheshimiwa Sima kwamba sisi kama Wizara bado hatujaona tatizo la usajili na ushindani katika ligi, lakini kama ni matumizi ya pesa, kwa kweli soka la leo ni la pesa. Usipokuwa na pesa, huwezi kabisa ukaendesha mchezo wowote wa mpira. Ndiyo maana unaweza kuona maendeleo mazuri ya timu kama Singida United, nao naomba niwapongeze kwa kazi nzuri ambayo wameifanya Kenya na tuwaombee kama ambavyo tunawaombea Simba waweze kufanya vizuri wawe washindi wa tatu katika mashindano ya Kenya.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naomba niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto kubwa inajitokeza kutokana na uhaba wa hawa Maafisa Utamaduni kwenye halmashauri zetu. Sasa Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri Maafisa Utamaduni ili kuweza kukidhi haja ya Sanaa. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba, hapo nyuma kulikuwa kuna changamoto kubwa sana ya Maafisa Utamaduni kwenye halmashauri zetu, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, halmashauri nyingi zilishaandika barua ya kuomba vibali kutoka Utumishi vya kuweza kuajiri Maafisa Utamaduni. Mpaka sasa hivi karibu halmashauri nyingi zina Maafisa Utamaduni.
Mheshimiwa Spika, kama haitoshi sisi kama Wizara, tunaendelea na mchakato wa kuonesha kwamba tunaajiri Maafisa Utamaduni wapya, hususani katika Mikoa na Halmashauri ambazo ni mpya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tatizo hilo kwa kiasi kikubwa sana limeshashughulikiwa na Wizara yetu ya Habari, nadhani hata Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Singida Mjini tumeanza programu ya kupandisha hadhi shule zetu za sekondari kuwa kidato cha tano na sita ikiwemo Shule ya Sekondari ya Mungumaji. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutusaidia kukamilisha programu hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikirejea majibu yangu ya awali ambayo nimeyatoa, kwanza yeye kama mwalimu namsifu kwa juhudi zake za kuendeleza sekta ya elimu katika jimbo lake lakini vilevile kutoa mawazo mazuri kwa ajili ya nchi nzima. Napenda kusisitiza kwamba maagizo ambayo tumeyatoa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri ambao wanasimamiwa na Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ni kwamba kipaumbele lazima waendelee kukiweka katika shule zote ambazo wameziteua kwa ajili ya kuzipandisha hadhi kuwa za kidato cha tano na sita kwa maana hizo zitakuwa ni shule za nchi. Waweke kipaumbele kuhakikisha kwamba miundombinu inayohitajika yote kwa mujibu wa vigezo vilivyotolewa na Wizara ya Elimu inakamilika mapema iwezekanavyo ili kusudi shule hizo ziweze kutusaidia kupokea watoto wengi zaidi au vijana wengi zaidi wa kidato cha tano na sita.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kabisa kwenye ligi ya Uingereza ilijulikana kama Backlays English Premier League na siyo Backlays Premier League, pia hata Kagame Cup haikujulikana kama Kagame Cup inajulikana kama CECAFA Kagame Cup. Serikali haioni haja sasa kwamba umefika wakati wa kuitangaza Tanzania kwenye michezo na league yetu ikaitwa Tanzania Vodacom Premier League? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Kampuni ya Azam wameanzisha mashindano makubwa sana yanaitwa Azam Sports Federation Cup, nichukue fursa hii kuwapongeza sana, je, Serikali haioni haja sasa ya kushawishi na makampuni mengine yaweze kuanzisha mashindano ili ku-promote soko la Tanzania? (Makofi
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwalimu Mussa Sima kwa kifupi sana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pendekezo la kuweka jina la Tanzania kabla ya jina la mdhamini lina mashiko, tutalifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la kampuni nyingine kuiga mfano wa Azam, nami naunga mkono suala hilo. Natoa wito kwa makampuni mengine yajaribu kuiga mfano wa Azam ili tuweze kukusa soka katika nchi yetu.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Serikali inatoa elimu bila malipo kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne, wanafunzi wachache ambao hawajabahatika kwenda kidato cha tano wanaenda vyuo vya ufundi. Vyuo vya ufundi, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema wanalipia ada ya Sh.60,000/= na Sh.120,000/= kwa wale wa boarding. Je, Serikali haioni haja sasa kuondoa ada pia kwenye vyuo vya ufundi ili kuwawezesha watoto wengi kuweza kupata ujuzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya mwanzo kwamba Serikali inatoa ruzuku ya kutosha. Kwa hiyo, hili alilolileta Mheshimiwa Sima ni pendekezo, tunaomba twende tukalifanyie kazi tuweze kuangalia namna gani aidha kwa kupunguza au kwa kuondoa wakati huo huo tukiangalia wigo wa bajeti ya Serikali unavyokuwa.