Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mussa Ramadhani Sima (12 total)

MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Malengo ya Dira ya Taifa 2025, inaeleza kwamba ifikapo mwaka 2025 Tanzania itakuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda.
(a) Je, Serikali imeweka mkakati gani wa kuinua wananchi wa tabaka la kati (middle class) kuweza kujitegemea?
(b) Je, ni kampuni ngapi zilizowekeza nchini na Serikali ina hisa kiasi gani kwenye kampuni hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda yaani Integrated Industrial Development Strategy 2020 unahimiza ushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda ambapo malighafi zake zinapatikana hapa nchini. Mikakati mingine ni pamoja na mkakati wa pamba mpaka mavazi, mafuta yatokanayo na alizeti lakini ngozi bidhaa pamoja na ngozi yenyewe pamoja na mkakati wa mazao ya jamii ya kunde.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati hiyo ni utekelezaji wa mpango elekezi wa miaka 15 wa Dira ya Taifa ya Maendeleo mwaka 2025 unaolenga kutanzua vikwazo vya uchumi hapa nchini. Mpango wa pili una dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Mpango wa tatu unalenga kuimarisha ubunifu na ushindani wa Kimataifa. Msukumo wa mipango hii ni kuhakikisha kuwa na rasilimali za fursa za nchi zinatumika vizuri katika uchumi wa viwanda vya kati hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Taarifa za Ofisi ya Msajili wa Hazina kuna jumla ya makampuni 61 yaliyowekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji na utoaji wa huduma hapa nchini. Ukitoa makampuni 21 ambayo Serikali inamiliki asilimia 100; lakini makampuni mengine manne Serikali inamiliki hisa asilimia 50, na makampuni meninge manne pia asilimia 50 pamoja na makampuni asilimia 32 yanayomilikiwa asilimia 50.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Kumekuwa na mlundikano wa madeni ya watumishi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuyalipa madeni hayo?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuwa hakuna madeni tena?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Jimbo la Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kupokea na kuhakiki madai ya watumishi wa umma yanayohusu mishahara na kuyalipa kwa kadri ya uwezo wake wa kifedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Serikali ililipa madai ya malimbikizo ya mshahara ya shilingi 56,293,372,627.37 ambayo yalilipwa kwa watumishi 55,688 waliokuwa na madai yaliyotokana na kupandishwa vyeo, ajira mpya na sababu nyinginezo.
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali imeendelea kulipa madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi wa umma ambapo hadi kufikia mwezi Juni, 2016 watumishi 31,032 walilipwa jumla ya shilingi 28,929,095,373.89.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 7,871 yenye jumla ya shilingi 13,754,462,429.29 tayari yamehakikiwa na yameshaingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara na yanasubiri kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya watumishi 8,776 yenye jumla ya shilingi 15,590,586,474.69 yanaendelea kuhakikiwa ili yaweze kuingizwa kwenye mfumo tayari kwa kulipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika shughuli za kila siku madeni huzalishwa, lakini ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba madeni haya yanalipwa mara yanapojitokeza.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Miradi ya kuboresha huduma ya maji inayofadhiliwa na Benki ya Kiarabu (BADEA), Shirika la Mafuta Ulimwenguni (OFID) na Serikali ya Tanzania katika Kijiji cha Mwankoko na Kisaki katika eneo la Irao inaleta changamoto kubwa.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kulipa fidia kwa wananchi waliopisha miradi hiyo ambapo tayari uthamini ulishafanyika kwa mara ya pili ambapo Mwankoko wanadai shilingi 1,510,427,634 na uthamini ulifanyika tarehe 13 Machi, 2014 na mradi wa Irao shilingi 2,932,001,058/=?
(b) Mradi wa maji wa Irao katika visima vyake vyote viwili vinapoteza uwezo wa kutoa maji kutoka Q250-170 kwa saa na kisima cha pili ni Q150-70 kwa saa. Je, Serikali ina mpango gani juu ya kukabiliana na tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha uhakiki wa fidia kwa eneo la Mwankoko na imetuma kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kulipa fidia ya eneo hilo. Kwa upande wa Irao inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 2.9 zitahitajika kulipia fidia katika eneo hilo. Serikali inaendelea na tathmini ya uhakiki wa gharama za fidia hiyo na uhakiki huo ukikamilika fidia hizo zitalipwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa mradi wa maji safi Mjini Singida, kumejitokeza tatizo la kushuka kwa viwango vya uzalishaji maji katika visima viwili vya Irao. Kutokana na tatizo hilo, Serikali imechukua hatua za haraka ikiwemo kusafisha visima hivyo, kushusha pampu za visima vyote ili kuongeza kina cha kuchota maji. Baada ya jitihada hizo, imeonekana uwezo wa visima kutoa maji uliongezeka kwa kiasi. Aidha, Serikali imepanga kubadilisha pampu hizo ili kuongeza uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma ya maji, Serikali imepanga kufunga pampu kwenye visima vitatu vya akiba vilivyochimbwa awali wakati wa utekelezaji wa mradi mkubwa katika Manispaa ya Singida. Kazi hii itatekelezwa pamoja na shughuli ya ulazaji wa mabomba kutoka kwenye visima hivyo vitatu hadi kwenye tanki dogo la kukusanya maji yanayovutwa na kusukumwa kwenda kwenye matenki makubwa katika eneo la karakana.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Kuna mahitaji makubwa ya umeme katika Jimbo la Singida Mjini hususani katika kata za pembezoni kama vile Kisaki, Mtama, Mtipa, Mwankoko, Uhamaka, Unyambwa, Unyamikombi na Unyianga.
(a) Je, Serikali ina mpango gani kuvipatia umeme vijiji katika mwaka huu wa fedha?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia rasilimali ya nguvu ya upepo iliyopo Singida ili kuongeza nishati ya umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Kisaki, Mtama pamoja na Mtipa pamoja na Mwankoko zimejumuishwa katika mradi kabambe wa REA III unaoanza mwezi Machi, 2017. Katika kazi hizi, maeneo haya yatapelekewa mradi kupitia desification, grid extension pamoja na renewable utakaoanza mwezi huo nilioutaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo inajumuisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 105, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 126.9, ufungaji wa transfoma 31, pamoja na kuwaunganishia wateja wa awali 1,111. Kazi hii itagharimu shilingi bilioni 8.15.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa muda mrefu wa Serikali ni kutumia vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme ikijumuisha upepo uliopo katika eneo la Singida ambapo katika mpango kabambe wa kuendeleza sekta ya umeme wa mwaka 2016, mradi huu umepangwa kuanza kuzalisha megawati 50 za awamu ya kwanza mwaka 2018. Mradi huu unakadiriwa kugharimu dola za Marekani 136 na utatekelezwa katika maeneo ya Kisasida, Ipungi, Mughamo na Unyankhyanya. Kampuni ya Geo Wind pamoja na Acciona wameingia exclusive agreement kwa ajili ya kipindi cha miezi minne ambayo itaishia mwezi Februari mwaka huu kwa ajili ya kujiridhisha kwa wananchi kama watakubaliana na utekelezaji wa mradi huu ili waweze kupata umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni mbalimbali binafsi zimeonesha nia ya kuzalisha umeme kwa kutumia upepo katika Mkoa wa Singida ikiwa ni pamoja na Kampuni ya Wind East-Africa iliyojitokeza kuzalisha umeme wa megawati 50 kwa awamu ya kwanza na baadae kufikisha megawati 100. Mradi huu utatekelezwa katika eneo la Kititimo. Gharama ya mradi huu ni dola za Marekani milioni 264.77.
MHE. MUSSA R. SIMA Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa uwanja wa ndege katika eneo lililotengwa katika Kijiji cha Manga kwa msaada wa Benki ya Dunia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipata mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo sehemu ya mkopo huo imetumika kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa viwanja 11 vya ndege vya Iringa, Njombe, Songea, Lindi, Kilwa Msoko, Tanga, Moshi, Lake Manyara, Musoma, kiwanja kipya katika Mkoa wa Simiyu na Singida kwa ajili ya ukarabati, upanuzi na ujenzi wa viwanja hivyo kwa kiwango cha lami.
Ninapenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa kiwanja cha Singida unafanyika katika eneo la kiwanja cha sasa na si katika eneo jipya la Manga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utafutaji wa fedha za kazi za ukarabati, upanuzi na ujenzi kutoka vyanzo mbalimbali utaanza baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao kwa sasa upo katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kazi hii ya usanifu ikiendelea, Wizara yangu ilipata maombi ya Mkoa wa Singida ya kutaka wataalam kwenda kufanya tathmini ya awali ya eneo jipya linalopendekezwa katika eneo la Uhamaka karibu na kijiji cha Manga kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo hilo la Uhamaka limependekezwa kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja kipya cha ndege cha Mkoa wa Singida katika mpango kabambe wa uendelezaji wa Manispaa ya Singida kwa mwaka 2015 – 2035. Tathmini ya awali iliyofanywa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mnamo Februari, 2016 kuhusu eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2400 (kilometa sita kwa kilometa nne) imeonesha kuwa eneo pendekezwa linafaa kwa ujenzi wa kiwanja cha ndege.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia matokeo ya tathmini, hatua zitakazofuata ni utwaaji rasmi wa eneo hilo unaohusisha ulipaji fidia ya mali za wananchi waliomo ndani upimaji wa eneo kwa ajili ya hatimiliki, usanifu wa miundombinu ya kiwanja, utafutaji wa fedha za ujenzi wa kiwanja na hatimaye ujenzi wenyewe.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Singida Mjini ni Mji unaokuwa kwa kasi sana na tumetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji:-
Je, Serikali iko tayari kuleta wawekezaji?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhamasishaji wa uvutiaji wa uwekezaji ni jukumu la msingi la Serikali. Katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016/2017 –2020/2021 imeelezwa wazi kwamba malengo ya Serikali ni kuongeza kasi ya kuvutia wawekezaji wa ndani na wa nje katika sekta zenye tija kwa Taifa. Hivyo, Wizara yangu imekuwa ikihamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza nchini ikijumuisha Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya kivutio cha msingi
cha uwekezaji ni uwepo wa maeneo ya uwekezaji. Hivyo, Serikali imeendelea kuhamasisha Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Mikoa na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji. Kutokana na juhudi hizo, hadi kufikia Aprili, 2017, jumla ya Mikoa 13 imewasilisha taarifa ya utengaji wa maeneo katika mikoa yao. Napenda kuchukua fursa hii kuupongeza Mkoa wa Singida kwa kuitikia wito huo na tayari wametenga hekta 6,595.6.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jitihada hizo, katika kipindi cha kuanzia mwaka 1996 hadi Aprili, 2017, Serikali kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania, imefanikiwa kuandikisha miradi 33 kwa ajili ya Mkoa wa Singida yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 997.879. Kwa muhtasari huo, kazi iliyofanyika katika uhamasishaji uwekezaji Mkoani Singida, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Singida kuwa Serikali itaendelea kuvutia wawekezaji kuwekeza katika Mkoa wa Singida. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa vifaa tiba kwenye Hospitali ya Wilaya ya Singida Mjini au kituo cha afya Sokoine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sima, Mbunge kutoka Singida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanikiwa kununua vifaa tiba vyenye thamani ya Sh.102,939,700.00 kwa kutumia fedha za Mfuko wa Afya wa Pamoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya. Vifaa vilivyonunuliwa ni vitanda vitatu
(a) vya kujifungulia, mitungi mitano (5) ya kuhifadhia gesi, vitanda ishirini (20) vya hospitali na mashine tatu (3) za kutakasia vyombo vya hospitali. Vifaa vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na mashine moja (1) ya kutolea dawa ya usingizi (anaestheric machine), kitanda kimoja (1) cha upasuaji (operation table) na mashine ya kutakasia vifaa tiba vyenye ujazo wa lita 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imetenga jumla ya Sh.160,866.466.01 kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwenye kituo cha afya cha Sokoine. Kati ya fedha hizo, Sh.41,451,400 zimeshalipwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)kwa ajili ya vifaa tiba. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Serikali imekuwa na dhamira ya dhati ya kuboresha maslahi ya Watumishi hususan Walimu kwa kutoa nyaraka mbalimbali ikiwemo Waraka wa Utumishi wa Serikali Na. 3 wa tarehe 20/10/2014 unaohusu mishahara na Posho ya Madaraka kwa Viongozi wa elimu (Responsibility Allowance):-
• Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutekeleza waraka huo?
• Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa Posho ya Kufundishia (Teaching Allowance) ili kuleta ufanisi wa kazi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Serikali ilianza kutekeleza Waraka Na. 3 wa mwaka 2014 tangu tarehe 1 Julai, 2016 kuhusu Posho ya Madaraka kwa Walimu Wakuu, Wakuu wa Shule na Waratibu wa Elimu Kata. Walimu Wakuu wanalipwa sh.200,000/= kila mwezi na Wakuu wa Shule na Waratibu Elimu Kata wanalipwa sh.250,000/= kila mwezi. Kwa mwezi mmoja, Serikali inatumia takriban shilingi bilioni 5.01 kwa ajili ya kulipa Posho za Madaraka kwa viongozi hao kwa ajili ya kuimarisha uongozi na usimamizi wa elimu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, posho ya kufundishia ilijumuishwa katika Mshahara wa Walimu ili kuboresha maslahi ya Walimu wanapostaafu. Hata hivyo, Serikali hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora inafanya mapitio ya kazi kwa watumishi wote nchini ili kuboresha maslahi kwa kuzingatia uzito wa kazi.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Tunatambua kuwa michezo duniani kote imekuwa chanzo cha mapato na kuinua uchumi wa Taifa husika, lakini nchini Tanzania michezo hususan soka imebaki kuwa burudani tu.
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuinua Soka la Tanzania?
(b) Je, kuna mahusiano gani kati ya Serikali na TFF
katika kuimarisha soka la Tanzania kuanzia ngazi ya Wilaya?
(c) Je, Shirikisho la Mpira wa Tanzania (TFF) linapata fedha za ruzuku kiasi gani toka FIFA na Wadhamini kama TBL na Serengeti Breweries?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhan Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kuhakikisha kuwa michezo ikiwepo soka inaimarika nchini, imeendelea kuendesha mashindano mbalimbali ya michezo mashuleni kitaifa ikiwepo UMISETA pamoja na UMITASHUMTA ili kuibua vipaji mapema na imeteua shule 56, mbili kwa kila mkoa hadi tatu kwa kila mkoa ili ziwe shule za michezo kwa ajili ya kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo ikiwepo mchezo wa soka.
Aidha, Serikali kupitia Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, imeendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi na mafunzo ya muda mrefu kwa wakufunzi wa michezo mbalimbali ukiwepo mchezo wa mpira wa miguu.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, TFF, vyama vya michezo pamoja na mashirikisho mengine ya michezo vimesajiliwa na kufanya kazi chini ya Sheria ya Baraza la Michezo (BMT) Na. 12 ya mwaka 1967 na marekebisho yake ya mwaka 1971. Aidha, TFF inaendelea na uboreshaji wa viwanja vya soka nchini, mfano ni viwanja vya Kaitaba na Nyamagana mkoani Mwanza. Vilevile TFF inatoa msaada wa kiufundi katika viwanja mbalimbali ili kuhakikisha kwamba viwanja vinakuwa katika ubora unaotakiwa. Wizara yangu inaunga mkono programu mbalimbai za TFF katika kukuza mchezo wa mpira wa miguu wilayani na mikoani zikiwemo programu mpya kabisa za grass root pamoja na programu ya live your goals kwa wanawake ambazo zilizinduliwa Mkoani Kigoma Februari, 2018. BMT nayo inaendelea kusimamia utekelezaji wa Katiba, Kanuni na Sheria zinazosimamia michezo mbalimbali nchini.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato ya TFF; kwanza TFF ina udhamini wa miaka minne (2015-2018) kutoka FIFA kwenye programu ya FIFA Forward ambayo hutoa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1.25 kwa mwaka ambapo kati ya hizo dola za Kimarekani 750,000 hutumika kwa ajili miradi ya maendeleo na dola za Kimarekani 500,000 hutumika kwa ajili ya gharama za kuendeshea ofisi, timu za Taifa pamoja na ligi. Fedha hizi za maendeleo hazikuwahi kutolewa na FIFA tangu mwaka 2015, hivyo, TFF wanatarajia kupokea kiasi fedha cha dola za Kimarekani milioni tatu kwa ajili ya kutekeleza miradi husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, TFF iliingia mkataba na Kampuni ya Bia ya TBL mwaka 2013-2017 kwa thamani ya Dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya Timu ya Taifa ambap kwa sasa mkataba huo umeshamalizika. Hivyo, TFF imeingia mkataba wa ufadhili na Kampuni ya Bia ya Serengeti wa miaka mitatu (2017-2019) wenye thamani ya shilingi milioni 700 kwa ajili ya timu ya Taifa ya wanaume na shilingi milioni 450 kwa ajili ya ligi kuu ya wanawake nchini.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, Serikali haioni haja sasa ya kuziagiza rasmi Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwezesha Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kutekeleza baadhi ya majukumu yake ili walimu wapate huduma stahiki kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Utumishi wa Walimu ilianzishwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 2015 ili kuwahudumia walimu wa shule za msingi na sekondari za umma Tanzania Bara. Aidha, Tume ya Walimu ina fungu lake (Fungu 2) linalojitegemea na watumishi wake kupitia wasimamizi wao huripoti moja kwa moja kwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Makao Makuu ya Tume. Hivyo Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina bajeti za kuwawezesha uendeshaji wa siku kwa siku wa kazi za TSC zilizoainishwa na sheria kwa kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa ziko chini ya mafungu mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Bunge limeiidhinishia Tume ya Utumishi wa Walimu jumla ya shilingi bilioni 12.515; kati ya hizo shilingi bilioni 4.622 ni matumizi mengineyo ili tume ipate vitendea kazi kama magari, samani za ofisi na pia kugharamia vikao vya mashauri ya nidhamu na rufaa. Hata hivyo, kwa kutambua umuhimu wa Tume, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimewapatia Makatibu Wasaidizi wa Tume katika Wilaya zote nchini Ofisi na baadhi ya vitendea kazi. Serikali itaendelea kuiimarisha Tume ya Utumishi wa Walimu ikiwemo kutatua changamoto za kiutendaji ndani ya wigo wake wa kisheria ili itekeleze majukumu yake vizuri zaidi.
MHE. MUSSA R. SIMA aliuliza:-
Je, ni vigezo vipi ambavyo Serikali imeviweka juu ya kampuni zinazowekeza kwenye michezo nchini kuruhusiwa Ligi husika kubeba majina ya kampuni hizo kama vile Vodacom Premier League badala ya Tanzania Premier League?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mussa Ramadhani Sima, Mbunge wa Singida Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kuongezeka kwa gharama za mfumo wa uendeshaji wa Mpira wa Miguu Duniani, Shirikishao la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limelazimika kutafuta wadhamini au wafadhili wa kusaidia kuendesha shughuli za mpira wa miguu nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya makubaliano yanayofikiwa kati ya Shirikisho na Wadhamini ni mdhamini kujitangaza kupitia mchezo wenyewe. Kwa mfano, ligi kuu ya Uingereza wakati ikifadhiliwa na Benki ya Backlays, ligi ilijulikana kwa jina la Backlays English Premier League. Hapa Afrika Mashariki kuna mashindano ya Kagame Cup ambayo mfadhili wake ni Rais wa Rwanda, Mheshimiwa Paul Kagame na yanajulikana kama CECAFA Kagame Cup.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo suala la ligi kuu ya Tanzania kutumia jina la Mdhamini wa ligi hiyo, Kampuni ya Vodacom, linatokana na makubaliano ya kimkataba baina ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na mdhamini wa ligi hiyo ambayo ni kampuni ya Vodacom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkataba huo, miongoni mwa masuala waliyokubaliana ni pamoja na mdhamini kuwa na haki ya kutumia jina lake (Naming Right) katika uendeshaji wa ligi hiyo.