Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mussa Ramadhani Sima (31 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza leo, naomba nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua na kuendelea kuniamini kuwa Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira).

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kumshukuru Makamu wa Rais, Mama yetu, Mama Samia Suluhu kwa maelekezo na ushauri mzuri ambao amekuwa akiutoa kwenye Wizara na tumekuwa tukiufanyiakazi. Nichukue fursa hii pia kumshukuru Waziri Mkuu wa ushauri ambao ameendelea kutupatia. Nimshukuru pia Waziri wangu Mheshimiwa Januari, amekuwa ni mstari wa mbele sana kunipa mwongozo mzuri wa kuhakikisha natekeleza majukumu yangu, nimshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote katika Wizara yetu, tumefanya kazi kwa pamoja vizuri na hatimaye tunaendelea vuzuri. Vile vile nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wote, Mwenyekiti na Wenyeviti wengine kwa kazi kubwa ambayo tumeendelea kuifanya kwa pamoja. Mwisho lakini siyo kwa umuhimu, niwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Singida Mjini, wamekuwa wavumilivu kwa kipindi chote ambacho nikitekeleza majukumu ya Serikali. Mwisho kabisa niwashukuru pia Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira wametupa ushirikiano mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia na wengine wamechangia kwa maandishi, lakini nijikite kwenye maeneo machache hasa yahusuyo mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia hotuba ya bajeti ya Kambi Rasmi ya Upinzani ukurasa wa 10 wamegusia suala la Stiegler’s Gorge kwamba misitu inafyekwa sawa na ukubwa wa Dar es Salaam nzima. Jambo hili likisemwa hivi kwa Watanzania linaweza kuleta sura tofauti. Mtanzania anayeifahamu Dar es Salaam anaweza akaona eneo lile linalokatwa miti litabaki kuwa jangwa, lakini ni wajibu wetu sasa kufika mahali kueleza faida ya ule mradi wa Stiegler’s Gorge ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Mbuga ya Selou ina kilometa za mraba zaidi ya 50,000 lakini ni asilimia tatu tu ambapo ule mradi unaotarajiwa kujengwa na umekwishaanza ndiyo zitatumika kwa ajili ya kuhakikisha tunapata umeme wa megawatts 2,100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunahitaji umeme na tunahitaji umeme rafiki wa mazingira. Sisi ambao tuko kwenye eneo hili la mazingira, huu umeme kwetu ndiyo umeme rafiki wa mazingira kuliko umeme wa mafuta. Kama umewasikia Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa wakizungumza kwenye bajeti iliyopita ya TAMISEMI wanataka umeme wa REA na mambo mengine yote, lakini umeme ule wanaouhitaji wanahitaji wapate umeme rafiki na hapa nilitarajia na mimi kuona Waheshimiwa Wabunge kwanza wanampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa na hatua kubwa ya ujasiri ya kuhakikisha kwanza tunapata umeme rafiki wa mazingira ambao tunapata megawatts 2,100. Eneo hili linahitaji ushirikiano wa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini faida kubwa sana tunaipata. Unapozungumzia tu ile miti ambayo sisi hatukati asilimia 3, ile miti ni kama 1.8 lakini faida ya ule umeme ni kubwa kwa nchi nzima na duniani. Wamezungumzia habari ya mabadiliko ya tabianchi kwamba tuwe na umeme rafiki lakini leo wananchi wetu wanawekewa umeme ama umeme unaofika vijijini unahitaji kuwa wa gharama nafuu ambapo ni lazima tuwe na umeme unaotokana na maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la umeme kumekuwa na mambo mengi watu wanayaeleza lakini wanaeleza kwenye eneo la kukata misitu lakini waeleze faida ya kile kinachopatikana pale. Mbali ya faida ya ule mradi kwenye umeme pia kuna ajira, kilimo, ufugaji na mambo mengi ambayo tunahitaji tushirikiane na wenzetu kwa ajili ya kuhakikisha kwanza tunaweza kupata umeme huu ambao utatusaidia kufikia malengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mengine wenzetu wamejaribu kuzungumzia lakini nieleze jambo moja kwenye eneo la taka ngumu na taka hatarishi, wakati nafanya ziara kwenye Mikoa sita ya Nyanda za Juu Kusini moja ya hoja ilikuwa ni hiyo ya vyanzo vya maji lakini nyingine ya taka. Vyanzo vya maji Mto Rufiji wenyewe unaunganishwa ama unalishwa na mito mikuu mitatu: Mto Rwengu, Mto Kilombero na Mto Ruaha Mkuu. Nimeenda kuangalia vyanzo vya maji na namna vinavyohifadhiwa, nataka niwahakikishie Watanzania tunayo maji ya kutosha na Watanzania ni waadilifu wametunza vyanzo vya maji na tunahitaji kuendelea kuwapa elimu waendelee kutunza vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimeangalia eneo la taka ngumu na taka hatarishi, Kamati yangu imelizungumza vizuri, moja ya eneo ambalo linaleta changamoto ya taka, nimemsikia Mheshimiwa Hawa Mwaifunga pia amezungumza eneo hili la taka, ni eneo ambalo ni vizuri kwa kweli tukashirikiana kwa pamoja. Nimeendelea kutoa elimu kwenye mikoa yote ambayo nimepitia, nimetembelea madampo na kuona namna ambavyo wanateketeza zile taka zinapotoka majumbani na kupelekwa kwenye madampo, eneo lile tumewaomba wenzetu wa Serikali za Mitaa walioko chini viongozi wale tunashirikiana kwa pamoja japo tunajaua kwenye Sheria yetu ya Mazingira ya mwaka 2004, Ibara ya 6 kwamba jukumu la usafi ama la utunzaji wa mazingira ni la kila Mtanzania ama ni la kila mwananchi ambaye anaishi Tanzania. Eneo hili niwaombe Waheshimiwa Wabunge tushirikiane pamoja, suala la uhifadhi wa mazingira siyo la Wizara moja ama la Serikali peke yake ni suala la kila Mtanzania na kila kiongozi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Genzabuke amezungumza vizuri na niseme tu kwamba tumepokea ushauri wake juu ya kushirikiana na wenzetu hasa mashirika yale yanayo-deal na wakimbizi. Nimefika mpaka Kagera Nkanda nimeona uharibifu mkubwa wa miti na maeneo mengine. Nimuahidi Mheshimiwa Genzabuke jambo hili tumelipokea na tutalifanyia kazi ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mtolea nikuahidi tu kwamba baada ya Bunge hili nadhani nitakapokwenda Jimboni sasa niwasalimie wananchi wangu, nitakwenda kufanya ziara Dar es Salaam. Jambo kubwa hapa siyo tu kutoza faini na hili tuliweke wazi, kwanza tunahitaji watu wale wapewe elimu. Kwa sababu kama Watanzania kwenye gereji na maeneo mengine hawajapewa elimu na tukakimbilia faini, hili kwa kweli hatutakubaliana nalo. Nikuahidi kwamba nitafika mwenyewe nifanye ziara na pia tuwashirikishe wananchi ambao wameamua kuwa wajasiliamali kwenye maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamezungumza suala la elimu, kwa kweli tunakubaliana nalo, suala la elimu halina mwisho hata kama tunaendelea kutoa inawezekana bado elimu inahitajika sana. Nimshukuru sana Mheshimiwa Saada Mkuya amesema elimu ya Muungano inayotakiwa sasa ianzie Bungeni. Hili tunakuunga mkono, tutaanza nalo, najua Mheshimiwa Waziri ataeleza vizuri suala la Muungano.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala la elimu ni jambo kubwa sana na siyo jambo la Wizara au Serikali peke yake, kila Mtanzania anayeelewa juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira anapaswa kuwaelimisha na wengine. Pia anayejua umuhimu wa Muungano anapaswa kuwaelimisha na wengine. Sisi tutakuwa mstari wa mbele, tutaendelea na majukumu na mikakati yetu ya kuhakikisha kwamba elimu hii inatolewa kadri inavyotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kuendelea kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kadri ambavyo wametupongeza waendelee kutupa ushirikiano wa dhati na sisi kama ambavyo mnafahamu tunafikika na tuko tayari kufanya kazi wakati wote. Pale tunapobanwa mtuwie radhi inawezekana tusifike kwa wakati lakini tunaweza kushauriana na kusaidiana, majukumu haya yote ni yetu pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, nichukue fursa hii kuishukuru sana familia yangu, mke wangu na watoto ambao nao wamenivumilia kwa kipindi chote hiki nimeendelea kutekeleza majukumu yangu vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini pia niungane na Wabunge wenzangu kwamba sasa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Profesa na Naibu Waziri kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. Pia, nampongeza kaka yangu Katibu Mkuu wa Wizara hii, Profesa Kitila Mkumbo na watendaji wake wote kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza mazingira bila kutaja uhifadhi wa vyanzo vya maji, maana yake mazingira yatakuwa hayajatimia. Nawapongeza Waheshimiwa Wabunge na ni ukweli usiopingika kwamba wameongea kwa hisia kubwa sana juu ya uhitaji wa maji na hili ni jambo jema sana. Mjadala huu unatuonesha picha ni nini ambacho Serikali tunapaswa kukifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna vita itatokea duniani leo itakuwa ni vita ya kugombania maji. Kwa bahati mbaya sana Tanzania inaweza ikawa nchi ya kwanza ya kuathirika na vita hii. Kwa nini? Asilimia 35 ya maji safi na salama duniani yanapatikana Tanzania. Tunayo maziwa makubwa, tunalo Ziwa Viktoria, Ziwa Tanganyika na maziwa mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa inayojitokeza hapa ni namna ya kuhifadhi vyanzo vya maji na hili ndiyo jukumu letu. Hata kwenye mjadala ukiusikiliza, wote tunazungumzia water supply. Sasa una-supply water wakati unajua kabisa hujahifadhi vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niliseme hili kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kwamba jukumu la kuhifadhi vyanzo vya maji ni jukumu la kila Mtanzania, siyo jukumu la Serikali peke yake. Eneo hili linahitaji tushirikiane kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunahifadhi vyanzo vya maji ili tuweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imejitahidi sana kupeleka fedha za kutosha, inapeleka fedha za mradi, lakini mradi kwenye maeneo mengine hata kwangu kule Singida wanaenda kluchimba wanakosa maji na geological physical survey imefanyika inaonesha kwamba hapa kuna maji. Watakapochimba tu wakaenda hata mita 200 wanakosa maji. Hapo ndiyo kwenye changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayojitokeza hapa ni uhifadhi wa vyanzo vya maji ambalo hili ni jukumu letu kuwaelimisha watu wetu, tukirudi kuitaka Serikali itupatie fedha za miradi, tuwe tumetoa elimu ya kuhakikisha watu wetu wanajua namna ya kuhifadhi vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukirudi nyuma mwaka 1961 Watanzania walikuwa takribani milioni 10, ukiweza kugawa unapata mita za mraba kama 7,862, lakini leo milioni 55 Watanzania mita za mraba unapata kama 2,300. Vyanzo vya maji ni vilevile na vingine toka mwaka 1961 vimeshakufa na leo vyanzo vinaendela kufa. Maana yake tunakoelekea ni kwenye vita kubwa ambayo tutashindwa kukabiliananayo. Vita hii inatuhitaji sisi wote Watanzania tuungane kwa pamoja, tusiiachie Serikali peke yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefanya ziara kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kuangalia vyanzo vya maji vya mito mikuu mitatu; Mto Luengo nimeenda kule Namtumbo, nimepanda ile milima zaidi ya kilometa 10, nimeenda kuona chanzo cha maji. Kwenye chanzo cha maji pale hakuna tatizo, lakini inapoanzia pale kwenda maeneo mengine, maji kote njiani Watanzania wanafanya shughuli za kibinadamu na eneo hilo lote wame-tap maji wanayatumia kwa wingi kiasi kwamba maji yale kule yanakotoka mpaka yanakofika, yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda Mto Ruaha Mkuu kuna shida kubwa sana. Watu wamevamia kwa kiwango kikubwa. Hili ni eneo ambalo tunahitaji sisi Watanzania tushirikiane kwa pamoja kulisimamia. Hivi vyanzo vya maji tusipovisimamia hapa tutakuja kudanganyana. Tukizungumza lugha ya water supply peke yake na Serikali kweli ikawa na fedha ikapeleka, unapeleka fedha unaenda kuchimba maji wakati hayapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la mazingira nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge tushirikiane kwa pamoja. Tunayo fursa na tunayo nafasi kwenye mikutano yetu ya Majimbo ya kuwaeleza Watanzania kwamba tunahitaji kutunza vyanzo vya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado kuna fedha ya miradi mbalimbali inayopelekwa na Serikali kwenye Halmashauri zetu. Tusiposimamia kuanzia hatua ya kwanza mpaka ya mwisho na baadaye tunaenda; hapa umesikiliza mjadala wa Waheshimiwa Wabunge, mijadala mingi inasema mradi umeenda umeisha, shilingi milioni 500 zimeenda, lakini hakuna maji. Jukumu ni la nani? Wizara imepeleka fedha. Fedha tunatakiwa tuzisimamie sisi, ndiyo wajibu wetu na kuwaelimisha watu wetu. Kamati za Maji zishirikishwe kuanzia initial stage. Hili ni jukumu letu kule chini. Hili eneo nilitaka niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tusibaki tu kulalamika na tukaiachia Serikali ikasimamia mpaka kule chini. Huu ni wajibu wetu na hatuwezi kurudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine Serikali imeweka mkakati mzuri sana. Yako maeneo iko miradi ya nyuma ambayo tayari miradi ile ime-collapse kwa uzembe wa watendaji na kwa uzembe wa kutokushirikisha jamii. Mkakati huu uliowekwa uwe mkakati ambao unahitaji na sisi kushiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la mita 60, mita 500 limezungumzwa; eneo hili sisi kwenye Sheria yetu ya Mazingira mwaka 2004 kifungu cha 57(1) kimezungumza mita 60, lakini kifungu cha 57(2) kimeeleza ufafanuzi kwamba Waziri anayo dhamana ya kutengeneza kanuni za mita 60 itumikeje. Nataka niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba kanuni tayari zipo na hazielekezi moja kwa moja, kila mazingira yana tofauti yake; kuna eneo ambalo halihitaji mita 60, mengine yanahitaji mita 10 tu, tukapanda miti mita 10 kuhifadhi kile chanzo cha maji lakini mita zingine wakaweza kuzitumia ama mita 20. Kanuni tumeziweka wazi na hatuna muda mrefu kanuni hizi zitafika mpaka kwenye Local Government kuhakikisha kwamba suala hili linaweza kusimamiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo mengi tunaweza kuzungumza juu ya uhifadhi wa maji, maeneo haya yote hasa visima ukizingatia visima hivi ambavyo vimechimbwa na wadau mbalimbali; mdau akishachimba kisima watu wanaamua kuacha kiendelee. Jukumu la kutunza visima na jukumu la kutunza vyanzo vya maji ni jukumu letu sote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na haya ya kuweza kushauri/kuwashauri wenzangu na kuunga mkono bajeti. Nampongeza sana Mheshimiwa Profesa na Naibu Waziri kwa kazi kubwa anayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nami nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kutoa mchango wangu katika Bunge hili, nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Singida Mjini walionipa ridhaa hii na mimi niwaahidi utumishi uliotukuka.
Pia nichukue fursa hii kushukuru Chama changu cha Mapinduzi, lakini pia niishukuru Kamati yangu ya Viwanda na nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri ambapo mambo mengi ambayo na mimi niliyatarajia sasa nimeyaona yakiwa humo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye kuchangia hoja ya viwanda. Nianze na EPZA kwa maana ya pale Kurasini, eneo lile ni muhimu sana na niipongeze sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao unaendelea pale. Mambo yaliyomo mule ni mengi sana na nimejifunza vitu vingi mle ndani na ni vizuri sana Watanzania wakajua kwamba leo hii Serikali yetu kwenda kwenye viwanda wala haijakosea. Kuna uwekezaji mkubwa na pale wanatengeneza jeans ya grade A, suruali ile inauzwa Marekani, Uingereza na German, ina-compete kwenye soko la Kimataifa. Hali kadhalika pale wanatengeneza mpaka ATM card mpaka voucher tunayoweza kuitumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu ni nini hapa? Hatuwezi kuendelea kuwa-entertain wawekezaji halafu wakawekeza na sisi tukabaki tu kutumika. Niiombe Serikali ifike mahali tuwe na mpango wa ku-adopt teknolojia kutoka kwa wenzetu hawa wageni lakini isitoshe ku-adopt kama inawezekana kuinunua teknolojia ifike mahali tuinunue teknolojia. Baada ya huo muda wakiweza kuondoka na sisi tuweze kuendesha hivyo viwanda ambavyo vipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni la ajira. Tumezungumzia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi asilimia 40% ya ajira. Nataka jambo hili tuliweke wazi. Tunao vijana zaidi ya 800,000 wanaingia mtaani kila mwaka na wote hawa tunazungumzia ajira. Hapa palihitaji ufafanuzi mpana kidogo. Najua utafiti ulifanyika ndani ya chama changu na Serikali yangu wanajua kabisa kwamba ajira hii inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuliweke vizuri, ni vizuri tukaliweka katika mazingira ambayo yanaeleweka. Tunayo service industry, tuna kiwanda cha huduma, kote huku unakokuona hotelini, kwenye masoko, usafirishaji, mazingira haya yote yanazungumzia ajira ya Watanzania. Hoja yangu hapa ya msingi ni lazima sasa Serikali ijikite kwenda kuangalia mikataba ya hawa Watanzania wanaoajiriwa kwenye haya maeneo. Ni namna gani wanafaidika na namna gani wanaweza kujikimu kwenye maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wenzangu walizungumza awali lazima Serikali ijikite kwenye agro-product. Tuna kila sababu sasa ya kuwekeza zaidi kwa wakulima wetu ambao tunajua kila mkoa sasa hivi unazalisha na hiyo ago-product itatusaidia sasa kuboresha viwanda vyetu. Connectivity ionekane ya mkulima, ya mchuuzi na mtumiaji, hii pia inaongeza wigo wa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya kulinda viwanda vyetu vya ndani. Amejaribu kuizungumza Mheshimiwa Waziri namna ya kulinda viwanda vyetu vya ndani, mimi nilitaka nishauri na lazima tuliweke wazi. Ufafanuzi hapa ulitakiwa uwekwe bayana, tunapovipeleka viwanda vyetu vya ndani kwenye tenders kwa maana kwamba tumetangaza tender na vyenyewe vinakwenda ku-compete, kazi ile ni ngumu sana. Tunatakiwa katika asilimia 100% tuwape kwanza viwanda vya ndani asilimia 40% halafu asilimia 60% waingie kwenda ku-compete na viwanda vingine vya nje, hapa tutakuwa tumeweza kulinda viwanda vyetu vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mdogo, tuna Kiwanda cha TANALEC kinachotoa transformer bora East Africa na sisi Serikali mle ndani ni wabia. NDC wana 10% lakini TANESCO wana 20%, sisi ni wabia, maana yake sisi ni member wa Bodi ya TANALEC lakini kwa bahati mbaya sana tunaagiza transformer kutoka India. Ukiagiza transformer kutoka India, wenzetu Serikali ya India inatoa ruzuku ya 10% kwenye viwanda vyake vya ndani, kwa hiyo, uzalishaji unakuwa mkubwa inafikia mahali wanatafuta masoko kwa cheap price. Kwa hiyo, ukija ukiwaingiza TANELEC kwenda ku-compete wenzetu wanakuwa chini halafu hawa wa TANALEC wanakuwa wako juu na ukizingatia TANALEC wako Tanzania na sisi tunamiliki percent ya TANALEC. Kwa hiyo, niwaombe sana tunapokwenda kuhakikisha tunalinda viwanda vyetu vya ndani ni lazima tuzingatie mambo haya ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, tuna kiwanda cha Urafiki, tuna asilimia 49% pale kwenye kiwanda kile na Wachina wana asilimia 51%, ndiyo wasemaji wakubwa wa kiwanda, lakini uzalishaji wa pale ni hafifu na Kamati imeeleza pale kuna madeni ya kutisha. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tufike mahali kama ambavyo tumeshauri sisi ndiyo tu-hold share ya Kiwanda cha Urafiki. Sasa leo tunavaa khanga na vitenge kutoka China lakini tuna Kiwanda cha Urafiki, niombe sana Serikali iliangalie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahali siku za nyuma tulijaribu kulinda viwanda, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, tuna Mufindi Paper Mills. Kiwanda hiki cha Mufindi kinatumia rasilimali za Tanzania na ikumbukwe miaka ya nyuma 2007 cubic meter moja walikuwa wanauziwa nusu ya bei badala ya 28,000 wanauziwa 14,000 na bado ile pulp wanaisafirisha kwenda Kenya na wakitoka Kenya importation ya huku tumewapunguzia mpaka 10% Serikali inaingia hasara. Wakenya hawana misitu, misitu iko Tanzania. Kwa hiyo, niiombe Serikali iende ikaliangalie hili, hili jambo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja nizungumzie sekta ya ngozi. Mheshimiwa Waziri amezungumzia sekta ya ngozi hapa kwamba wataiangalia na wataboresha mpaka kufikia kiwango cha wet blue. Wet blue jamani ni sawa na kutengeneza raw material, ni sawa na kutengeneza ghafi. Leo hivi viwanda vilivyopo vya wet blue tunazungumzia temporary turning maana yake ni sawa na mtu anakwenda kwenye harusi unamuogesha tu halafu anaenda hana viatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi leo tumepeleka fedha kwenye SIDO nimeona pale, zaidi ya shilingi bilioni sita lakini tunasafirisha ngozi hatuwezi kwenda huko. Mheshimiwa Waziri ni shahidi maghala yamejaa ngozi. Niombe sana Serikali sasa ichukue hatua ya haraka kuhusu suala hili. Vile viwanda ni temporary, umezungumzia viwanda nane hakuna viwanda nane Mheshimiwa Waziri, kama vinazidi sana ni vinne na bado ni temporary kwa hiyo Tanzania bado hatuna viwanda hivyo. Niombe sana jambo hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nishukuru tumezungumzia habari ya regulatory bodies, tu-harmonise vifanye kazi kwa pamoja kuondoa mlolongo mrefu ambao hauna tija. Jambo lingine tumezungumzia model, nimeona kwenye kitabu hapa, wenzetu wa Vietnam, China, Korea Kusini na wengine wote walianzia hapa tulipo. Kwa hiyo, niombe sana tuangalie hili tabaka la kati kwa maana ya middle class ndiko mahali ambapo tunatakiwa kujikita zaidi kuhakikisha kwamba Watanzania wanaweza kujikimu na maisha yao juu ya uwepo wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapozungumzia SIDO lazima tuweke connection na VETA. Hivi vitu lazima vihusiane, SIDO na VETA. Hatuwezi kuishia tu SIDO, VETA inafanya nini ili iweze kutusaidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri jambo la mwisho kwamba sasa wakati umefika kama tumeamua Tanzania iwe nchi ya viwanda, tuwe na siku ya viwanda Tanzania. Jambo hili litawarahisishia wafanyabiashara na wenye viwanda kukutana na kujadili changamoto wanazokutana nazo hata kila mwaka, hata kila baada ya miezi sita, jambo hili litatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende mbali zaidi. Leo wenzetu wa Rwanda wanazalisha alizeti. Singida sisi ni maarufu sana kwa alizeti na bahati mbaya sana sijaona kama tunaenda kuanzisha kiwanda cha alizeti Singida, niombe sana suala hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisi Singida ni wafanyabiashara wazuri sana wa vitunguu. Mheshimiwa Waziri karibu sana tuje tuanzishe soko la Kimataifa pale Singida ili tuweze kuwasaidia wananchi wa pale. Rwanda leo wameweka 25% ya kodi hata Kenya wenyewe nao wanaweka lakini sisi tukitaka kuweka hapa mpaka tukaulize East Africa. Mheshimiwa Waziri naomba agenda hii uilete vizuri ili tuweze…
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza pongezi kwa kuteuliwa kwake Mheshimiwa Waziri na hongera kwa uwasilishaji mzuri, naomba nizungumzie mambo machache yafuatayo:-
Kwanza, Serikali ilitoa waraka wa responsibility allowance, lakini mpaka sasa haijaanza kutekelezwa ili kuwawezesha viongozi wetu kwenye Idara ya Elimu.
Pili, kumekuwa na tatizo kubwa sana la madeni ya walimu, Serikali lazima ije na Mpango wa kukomesha madeni ya walimu.
Naomba soko huria la vitabu lidhibitiwe kuendana na mitaala ya elimu. Nashauri kuwe na formality moja nchi nzima ya vitabu.
Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya SADC ya Usimamizi wa Mazingira kwa ajili ya Maendeleo Endelevu (The Southern African Development Community SADC – Protocol on Environmental Management for Sustainable Development)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Namshukuru Mheshimiwa Waziri Mbarawa, nawashukuru Kamati na Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamechangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ijikite hasa katika kujibu hoja za wenzetu wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Wamesema yawezekana taasisi ambazo tunazo ni taasisi ambazo hazina viwango, hazina ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze tu kwamba, tunaporidhia mkataba kama huu, maana yake Serikali inapata teknolojia, lakini tunapata fedha kwa ajili ya kufanya capacity building. Kwa hiyo, eneo hili tunakuwa tumelimaliza kulingana na utaratibu huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mwanya wa rushwa, wamesema kuna grand corruption, siyo kweli. Sisi tuna focal point, maana yake hizi nchi wanachama ziko focal point, hakuna bidhaa inaingia kabla Mkurugenzi wa Mazingira hajaridhia. Akisharidhia, maana yake ile bidhaa haina tatizo. Kwa hiyo, hakuna compromise ya kampuni yoyote itakayoingiza bidhaa yake bila sisi kama Serikali na Ofisi ya Makamu wa Rais kukubali kwamba iingie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamepewa semina. Kam mmemsikiliza Mwenyekiti hapa, ameeleza vizuri kwamba Kamati imeshapata semina na wamekuwa na uelewa mkubwa; na kwa semina hiyo uelewa huo maana yake wametuwakilisha sisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili halijaanza leo, nchi imeridhia Mkataba huu wa Vienna tangu mwaka 1993 na kuanzia hapo marekebisho yameendelea. Huu ni mkataba wa sita; tumefanya wa kwanza, wa pili, mpaka wa tano na huu ni wa sita. Kwa hiyo, kama nchi tuna uelewa mkubwa sana kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Nirejee kwa Mheshimiwa Janeth Mbene; ni kweli fungu lipo kama alivyoeleza, linaendelea kwa utaratibu ule ule. Pia namshukuru Mheshimiwa Jitu Soni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Zungu ameeleza hoja yake ya msingi sana ambayo nataka kueleza Bunge lako kwamba tunaendelea na utekelezaji kuhakikisha nchi inapata fidia kulingana na uharibifu wa mazingira wa viwanda vya wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Juma Hamad, kwa kweli ametoa elimu ya kutosha sana, Mungu ambariki. Nadhani sasa watu wote wamepata uelewa wa juu ni nini kifanyike. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa dakika zako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza sana juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Waziri katika kuboresha na kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima. Niiombe Wizara mambo yafuatayo:-
(1) Ije na mfumo mpya wa pembejeo ili kuondoa upotevu wa fedha na itasaidia kutathmini hali ya kilimo nchini.
(2) Mkoa wa Singida ni maarufu kwa kilimo cha alizeti na vitunguu, naiomba Wizara ituletee mbegu bora ili tukidhi bidhaa ghafi nchini.
(3) Cattle holding ground iliyoko Singida Mjini takribani kilomita tano toka centre, naiomba Wizara itupatie heka 21 ambayo ni sehemu ya eneo hilo ili tuweze kutengeneza Trading Area na kuboresha Mji wetu wa Singida, ukizingatia eneo limepitiwa barabara kuu.
(4) Naiomba Wizara iwasaidie wafanyabiashara wa ngozi kupata soko la uhakika la ndani na nje ya nchi, hasa Afrika Mashariki kwani sasa hivi soko hakuna na bei imeshuka kutoka 2000 kwa kilo mpaka 100 kilo. Wizara ije na mpango maalum wa kuboresha suala hili.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri kwa uwasilishaji mzuri. Kwa kuwa Serikali kupitia Wizara hii ilitoa agizo la kuwauzia MPM miti kwa nusu ya bei, that is cubic meter 1 – 14,000 badala ya 28,000 tangu mwaka 2007 mpaka sasa hivi Serikali inaingia hasara isiyopungua shilingi bilioni 2.8 kila mwaka. Naomba Wizara ije na mkakati wa kuondokana na tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa karatasi inatengenezwa Kenya, lakini misitu iko Tanzania na bado importation ya karatasi ina punguzo la kodi la asilimia10 badala ya asilimia 25 ninaiomba Serikali ije na mpango wa kuhimiza viwanda vyetu kama MPM kutengeneza karatasi badala ya mifuko peke yake na tuongeze kodi ya importation iwe asilimia 25.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru sana, pia nichukue fursa hii kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi yake kubwa anayoifanya, ama hakika amepita Singida, amefungua kiwanda kikubwa sana cha alizeti na ni kiwanda kikubwa East Africa, niwaombe yale maelekezo aliyotoa sasa yatekelezwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru pia na kumpongeza mzee wangu Mkuchika alivyoweza kuzingatia agizo la kuwarudisha wale watumishi wa darasa la saba, tunakushukuru sana. Nimshukuru kaka yangu Mheshimiwa Selemani Jafo na Naibu Mawaziri ama hakika TAMISEMI imetulia. Yapo mambo mengi sana ambayo wameyafanya sina sababu ya kuyaelezea, lakini mambo machache niwashukuru tumepata fedha shilingi milioni 500 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Sokoine na ujenzi unaendelea vizuri. Kama haitoshi mmekwenda mbali na hata majirani zangu mmewapa pia fedha za kujenga Hospitali za Wilaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkalama mmewapa shilingi bilioni 1.5 wanajenga Hospitali ya Wilaya, lakini pia hata Singida DC wanajenga Hospitali ya Wilaya kule eneo la Ilongero, nawashukuru sana ndugu zangu mmetupunguzia mzigo mkubwa, ama hakika sasa mmepanua wigo wa watu kupata huduma ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la afya ndugu zangu Singida Mjini tunalo tatizo hatuna hospitali ya Wilaya, tumepewa fedha zaidi ya shilingi bilioni 2.3 za kujenga Hospitali ya Rufaa tayari fedha zile zimeshakwenda na Hospitali ya Rufaa inaendelea vizuri. Ninawaomba, hili nilishalieleza kwenye Wizara ya Afya kwamba majengo ama Hospitali ya Mkoa iliyoko pale sasa hivi itakapohamia kwenda Hospitali ya Rufaa ni vizuri yale majengo tukayatumia kama Hospitali ya Wilaya ikishindikana basi mtupe fedha ya kujenga Hospitali ya Wilaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende eneo lingine, katika hotuba ya Waziri ukurasa wa 58 umezungumzia programu za kujengea uwezo Halmashauri za Miji na tayari Halmashauri ya Manispaa ya Singida tumeshaweka mpango kabambe tunayo master plan. Ninaiomba Serikali iende mbali zaidi tunapoweka master plan nini malengo yake, malengo yake ni kuelekea kwenye Jiji, sasa mtupe mwongozo wa kupanua ule Mji wa Singida ili tuweze kuwa na Jiji. Mnajua tayari Serikali imeshahamia Dodoma sehemu ya kupumulia ambako ni karibu na Dodoma ni Singida. Tukuombe Mheshimiwa Waziri hili tuliwekee mkakati, Mkoa wa Singida uwe mkoa wa kimkakati kwa ajili ya kuisaidia Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niangalie eneo lingine ambalo ni vizuri pia nikalielezea la asilimia 10; asilimia tano kwa vijana na asilimia tano kwa akina mama. Ninashauri eneo dogo, nishukuru Serikali imeondoa riba, lakini hapa tatizo kama ambavyo wamesema wenzangu haikuwa kwenye riba, tatizo ilikuwa ni utoaji wa hizi fedha.

Sasa naomba nishauri ni vizuri Serikali ikawa makini mtupe mwongozo na mzielekeze Halmashauri zifungue akaunti maalum ili kuweza kuweka fedha hizo moja kwa moja hili litatusaidia sana, lakini tuweke sheria kali kwa sababu hata marejesho yake, mpango wa kuleta marejesho ya zile fedha haueleweki na hii ndiyo inatupa mazingira magumu ya kuweza kuwapa na wengine fedha hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naenda haraka kwa sababu yako mambo mengi ya kuzungumza, tunalo soko kubwa la vitunguu. Nilishaomba awali hapa tujengewe soko lile na Serikali iliji-commit kujenga lakini mpaka sasa haijajengwa. Umezuka mgogoro, yako maelekezo ambayo wanaelekezwa wafanyabiashara wetu kwamba sasa waende wakafungashe ule mzigo (packing) shambani badala ya kwenye soko. Sasa tunataka kujua maana ya soko ni nini? Kama sasa watu wanaamua kwenda kufungasha shambani mwekezaji anatoka Kenya, Uganda aende shambani kwa mkulima, tunachojua akienda shambani maana yake atamuonea mkulima, tunataka mapato. Tunataka kuona maana ya soko yaani umuhimu wa soko uonekane. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka nikuombe Mheshimiwa Waziri uje Singida, tufanye mkutano tuweze kuondoa mgogoro huu wa soko na ikiwezekana soko hili la vitunguu liweze kujengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko eneo lingine la Waheshimiwa Madiwani kwa kweli ni jambo jema sana na wanafanya kazi kubwa sana, ni vizuri Serikali ikafikiria namna ya kuwaongezea posho yao ili waweze kufanya kazi yao vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuna eneo moja hapa ni vizuri nikawakumbusha Serikali, miaka minne, mitano nyuma alitokea Mzee Loliondo tulimwita Babu wa Loliondo, tulikuwa tunaenda kupata kikombe cha babu. Watanzania wote walielekea kwenda Loliondo na Serikali iliamua kuhakikisha inatengeneza miundombinu ya barabara inayoenda huko na kujenga minara ya simu, lakini hatukugundua tatizo nini la Loliondo. Hatukugundua tatizo ni nini Watanzania wameamua kuondoka kwenye hospitali zetu tulizozitegemea wamekwenda Loliondo. Anamtoa mgonjwa yuko ICU anapelekwa Loliondo!

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitarajia kuiona Serikali inatathimini ni wapi tumefeli mpaka Watanzania wote wameamua kwenda kwenye tiba mbadala. Nataka kusema nini hapa, tumeamua sasa kuhakikisha kila kata iwe na kituo cha afya na kila kijiji kiwe na zahanati na Hospitali za Wilaya. Serikali imejikita kwenye Hospitali za Wilaya naomba ije na mkakati tusirudi kule kwenye tiba mbadala, ije na mkakati wa kuhakikisha kwamba huu utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambao tumeuelekeza ili uweze kutekelezeka kwa umakini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajifunza hapa Loliondo ninajifunza pia na utawala bora leo. Nataka nilieleze kidogo eneo hili la utawala bora, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ametoa tamko na ameweza kufanikiwa akina mama wamekwenda pale zaidi ya 2000, jambo hili nilitaka Serikali itusaidie Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amefanya jambo jema sana.

Mimi nataka nimpongeze kwenye eneo hili, lakini nataka nifike mahali nishauri, ninampongeza kwa sababu ameonesha kabisa iko mifumo ya Serikali imeshindwa kufanya kazi yake. Kama tunayo Mabaraza ya Kata, tunalo Dawati la Kijinsia, tunao Ustawi wa Jamii mifumo hii yote imeshindwa kufanya kazi yake, tunazo taasisi za dini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, akatokea mtu mmoja akasema na watu wakafika wakaitikia, hapa tunajifunza jambo, mifumo hii ime-collapse. Sasa Serikali inachukua hatua gani? Lakini nataka kujifunza jambo lingine, anapata wapi legal authority ya kuamua kutekeleza haya ambayo wanayasema leo. Kama ni jambo jema Serikali itusaidie, iamue sasa na Wakuu wa Mikoa wengine waamue kufanya utaratibu huo alioufanya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kama ni jambo jema tumpe legal authority aweze kutekeleza kama ambavyo amefanya, lakini tukiacha hivi akafanya, maana yake tunataka kuwapa mzigo wanafamilia hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo anatoa bima za afya, jambo jema sana lakini tunao watoto yatima hawana baba wala mama, hakuna mtu aliyetoka akasema watoto hawa nao wapewe bima ya afya. Niiombe sana Serikali iliangalie jambo hili, jambo hili litatuletea mgogoro mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa pili niwakumbushe pia alitokea mama mmoja wa Tanga, Mheshimiwa Rais aliamua kufanya natural justice ya kumsikiliza. Yule mama mjane alisikilizwa na alieleza mambo yake yote pale kwenye ule mkutano, lakini Mheshimiwa Rais hakuamua, alichokiamua ni kupeleka kwenye mfumo rasmi na leo yule mama yupo jela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hiki kinachofanyika maana yake umeshawasikiliza watu, ukishawasikiliza warudishe kwenye mifumo rasmi iliyowekwa na Serikali, ikiendelea hivi ilivyo maana yake kila mtu atakuwa naamka leo anafanya jambo tumekaa kimya. Nataka niiombe Serikali kwenye eneo hili tuwe makini sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wetu ameonesha uwezo mkubwa sana na hata wa kuendelea kusimamia matatizo ya wananchi. Ametambua utawala bora maana yake nini na ameweza kutekeleza. Sasa wasaidizi wake nao watambue utawala bora, ile mifumo hata kama ime-collapse na yeye ndiye anayoisimamia, arudi kwenye mifumo rasmi, awarudishe kule ifanyike natural justice wasikilizwe kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira mengine atusaidie pia, likiisha hili la akina mama lakini pia akina baba nao waliachiwa watoto akina mama wameondoka nao pia waitwe waweze kusikilizwa, tutakuwa tumeweza ku-balance suala la equality, tunazungumzia usawa. Usawa haupo upande mmoja tu, usawa upo pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka niiombe Serikali kwenye eneo hili tusilichukulie mzaha, nchi leo kila mama leo ameelekea kule. Sisi tuliozaliwa na kulelewa kwenye single mother family tunajua uchungu wake. Kauli tu ya Mkuu wa Mkoa mama anashangilia hajapewa chochote, kauli tu ya kusikilizwa, maana yake mifumo yetu huku chini haisikilizi, mifumo yetu huku chini yawezekana haiwezeshwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Nishati
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru lakini nimshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema ambaye ametuwezesha tunaendelea na mjadala wa bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuwapa pole ndugu zangu wa Ikungi kwa kufiwa na Katibu wao wa Wilaya wa Chama cha Mapinduzi. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya marehemu mahali pema peponi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kuipongeza Wizara ya Nishati, ama hakika ndugu zetu hawa wa Wizara ya Nishati wanaonesha vision na mission ya Tanzania kuwa na umeme wa uhakika, kwa kweli niwapongeze sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kupitia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kabisa na kwa mara ya kwanza naona wameweka fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya asilimia 66.7, ni fedha nyingi sana haijawahi kutokea. Humo ndani wameelekeza vizuri, iko miradi mikubwa ambayo imeelekezwa kupewa fedha nyingi ikiwemo Stiegler’s Gorge lakini pia na mradi wa REA, ni jambo jema sana. Kote huku tunalenga kuwa na umeme wa uhakika. Eneo hili tuna kila sababu ya kumsifu sana na kumtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na Naibu wake waweze kufikia malengo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hofu yangu, siku zote lazima tuiweke hofu hii kwamba fedha hizi hazifiki kwa wakati. Tunataka tuiombe Serikali tusiwe watu wa kulalamika kila siku fedha hazifiki, mikakati yote iliyowekwa hii haiwezi kutekelezeka kama fedha hazijaenda. Niiombe sana Serikali ihakikishe inawapa fedha ili hii mikakati waliyoiweka ya kuhakikisha tunapata umeme wa uhakika tuweze kupata huo umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nielezee eneo hili la Stiegler’s Gorge. Wako watu wametolea mfano kwamba eneo hili wanakata miti ambapo unafananisha sasa ukataji wa eneo lile la miti na kilometa za mraba za Dar es Salaam yaani unafananisha na Jiji la Dar es Salaam. Ndugu zangu, Selous ina kilometa za mraba zaidi ya 50,000, Dar es Salaam ina kilometa za mraba 1,300, maana yake Dar es Salaam pale Selous inaweza ikaingia mara 35 mpaka 40. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilieleze jambo hili vizuri, Watanzania wanahitaji kuelezwa vizuri na ukweli. Tukisema zaidi ya Dar es Salaam kwamba tunaangalia ile miti lazima uangalie value ya mradi na ile miti inayokatwa, lakini lazima uangalie multiplying effect ya ule mradi, tunatarajia huu mradi utusaidie nini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunajenga reli kwa kiwango cha standard gauge, reli hii inatarajiwa kuwa na umeme wa kutosha, utatoka wapi? Malengo haya yaliyowekwa na Wizara ya kuhakikisha kwamba tunapata megawatt 2,100 maana yake yatatusaidia sasa hata miradi mingine ambayo inatarajia kuhitaji umeme iweze kutekelezeka, ikiwemo reli. Pia tunahitaji kuwa na viwanda vya kutosha vinahitaji umeme, Stiegler’s Gorge inaweza ikawa ndiyo suluhu ya hiyo miradi ambayo tunatarajia iweze kutekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wote tunalalamika juu ya kutokuwepo kwa umeme wa uhakika. Pale Singida Mjini tunayo sub-station nadhani ina megawatt zaidi ya 600 lakini hata pale ilipo kuna mtaa unaitwa Kimpungua, wananchi hawana umeme. Nimuombe Mheshimiwa Waziri, maeneo haya ambayo yako mjini na wako tayari kulipia gharama za umeme, maeneo haya madogo madogo ni vizuri sana Wizara ikawa makini kuhakikisha watu wanapata umeme lakini viko vijiji karibu 13 na mitaa 13 yote haina umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma kitabu cha Mheshimiwa Waziri wameomba fedha kwa ajili ya usambazaji wa umeme mijini, wameomba, hawana fedha. Sasa kama wameomba fedha maana yake sisi tutaendelea kusubiri maombi ya fedha, yanaweza yakakubalia au yakakataliwa ni lazima tuwe na mkakati madhubuti. Hatuhitaji kusubiri fedha zinazokuja sisi tunao umeme wa kutosha ni kuwaongezea tu bajeti ndugu zetu wa TANESCO pale wahakikishe kwamba vijiji vile na mitaa wanaweza kupata ule umeme wala hakutakuwa na tatizo lolote Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo mengine, Singida tumejaaliwa na rasilimali ya umeme wa jua, rasilimali nyingine ya upepo, nashukuru Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri kwenye kitabu chake na ziko fedha wametenga zaidi ya shilingi bilioni 888 kwa ajili ya umeme wa jua, niwaombe sana eneo hili sasa waliangalie na ni vizuri tukaharakisha, mchakato ufanyike mapema kwani jambo hili halijaanza leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, tunao upepo, nashukuru Waziri ametambua. Kwenye kitabu ukurasa wa 32 kama sikosei ametambua kwamba tunao upepo ambapo tunaweza kupata mradi wa umeme wa upepo na ametambua kampuni moja ya Wind East Africa, walikuja na kampuni nyingine ya Power Project, eneo kubwa sana la Singida ukiacha Kisaki, Mungumaji tunaenda mpaka Unyambo kule Kisasida kote kule kunafaa kwa mradi wa umeme wa upepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niiombe Serikali eneo dogo hapa, kampuni hii tumekuwa nayo zaidi ya miaka 10 sasa lakini hakuna utekelezaji, sijajua kulikuwa na mazingira gani, lakini Waziri ameeleza vizuri kwamba mchakato wa kusaini ile Power Purchasing Agreement umefikia hatua ya mwisho, well and good lakini muwape time-frame, wakimaliza huo mchakato tuwape time-frame ni lini wataanza sasa kuhakikisha mradi huu unafanyika. Kama jambo hili linashindikana niiombe Wizara itangaze rasilimali hii hadharani. Wako wawekezaji wengi watatusaidia na watahakikisha tunapata umeme, zaidi ya hii megawatt tuliyoizungumza hapa 100 tunaweza kupata hata megawatt 200 na tukaondokana na tatizo la umeme Mkoa wa Singida. Niiombe sana Serikali, tunayo maeneo mengi tunahitaji kuwa na uwekezaji wa viwanda, hatuwezi kuwa na uwekezaji wa viwanda kama hatuna umeme wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejaliwa kuwa na rasilimali kama hii, liwe eneo muhimu sana. Naomba Waziri atakapokuja ku-wind up ni vizuri tukawapa timeframe hawa wawekezaji tulionao kwa muda mrefu na sasa hivi wananchi wanalalamika sana, tufikie mahali tuweke rasilimali hii hadharani kila mtu mwenye uwezo wa kuwekeza kwenye eneo hili aje awekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko eneo lingine, Watanzania hawa tunaowapelekea umeme hasa vijijini uwezo wao wa ku-afford unit 350 ni mdogo sana. Unit moja ina takriban 350, kesho tutakwama kwenye hili. Nataka niiombe Serikali, tunapoweka mkakati wa kuhakisha watu wanapata umeme kwenye vijiji vyote basi tuweke na mkakati wa kupunguza gharama hii, kwa sababu watakuwa watu wengi ambao wanatumia umeme. Tukipunguza gharama hii itatusaidia pia watu waache kutumia mkaa kwa wingi, tutaanza kutumia umeme kwenye shughuli zetu. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Waziri tuweke mkakati wa kupunguza hii gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini watu wanapohitaji kuingiza umeme, tumepunguza gharama za uingizaji umeme. Kwa mjini tumeweka Sh.321,000 bado ni fedha nyingi sana, akiweka nguzo moja tu anaenda Sh.515,000 lakini vijijini tumeweka Sh.177,000, kwa nini tusiwaweke wote sawa kwa sababu wote wanatumia umeme sawa, wote wafanane kwa nini itofautiane? Kama inatofautiana, kwa nini tuweke kipaumbele kwenye REA tukaacha hapa kwenye maeneo ya miji, maeneo ya miji hayana umeme, tumewekeza kwenye maeneo ya vijijini. Niiombe Serikali iliangalie eneo hili itasaidia wananchi wengi kupata umeme na wanaweza kutumia ule umeme kwa gharama nafuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vision hii ya Wizara itatufikisha mahali ambapo lengo ama utekelezaji wa Ilani yetu ya uwepo wa viwanda vya kutosha na watu kuweza kutumia umeme kwa uhakika itatusaidia sana. Tumepitia bajeti nyingi hapa lakini mkakati kwenye bajeti hii ukiusoma vizuri na watu wakipewa fedha utatufikisha mahali ambapo tunapahitaji. Tuna kila sababu ya kuwaaunga mkono watu wa Wizara hii ili waweze kutusaidia sisi kuweza kupata umeme wa uhakika na wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimalizie kwa kuendelea kuishukuru Serikali, mambo mengi tumekuwa tukiyasema hapa, nimuombe Waziri tunaposhauri ni vizuri mkayasema hapahapa msisubiri Rais aseme. Tulishauri kwenye maji hapa kesho Rais akatolea majibu lakini sisi hatukuweza kusema. Sasa niwaombe tuwe tunamaliza humu humu tusisubiri Rais alione hili, Rais wetu anafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na naiunga mkono bajeti.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu lakini pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa bajeti hii ambayo mipango yake imekaa vizuri, yapo maeneo ambayo tunapaswa kuishauri Serikali vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuliweke jambo moja sawa, unajua mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, Mheshimiwa Dkt. Mpango alisema vizuri sana, amesoma vitabu vya viongozi hawa amejifunza best practice na worse practice sasa afute nini? Mheshimiwa Dkt. Mpango nikupongeze sana. Nadhani mimi nilikuelewa vizuri wakati umezungumza na hiyo itakuwa imetusaidia sana lazima ujifunze sehemu zote mbili.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejikita katika uchumi wa viwanda utakaochochea ajira na ustawi endelevu kwa jamii. Likisemwa hivi kwenye bajeti maana yake lazima tuone indicator za kuelekea kwenye uchumi wa viwanda. Serikali imeeleza vizuri imepunguza Corporate Tax kwenye kilimo lakini kwenye bidhaa za ngozi, nataka nijielekeze kwenye bidhaa za ngozi. Tukizungumzia bidhaa za ngozi ni lazima tujue kama viwanda vyenyewe vya kutengeneza ngozi vipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka hapa tujielekeze vizuri sana, tulikuwa na viwanda vya ngozi mimi sidhani kama vipo. Leo Mwanza hatuna kiwanda cha ngozi, ile Mwanza Tannery imebaki kuwa go-down. Ukienda Arusha kipo kiwanda kimoja kazi yake kubwa ni kutengeneza wet blue, inalainisha tu ile ngozi na kuisafirisha kwenda nje. Tuna Himo Tannery na tuna Kiwanda cha Moshi Leather ambacho kimefungwa. Morogoro tulikuwa na kiwanda pale na chenyewe kimefungwa kilikuwa kinafanya temporary.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka kujiuliza tumepunguza kodi kutoka asilimia 30 kwenda 20 kwenye bidhaa za ngozi wakati viwanda hamna. Nataka Serikali itusaidie hapa na nishauri vizuri, leo bidhaa ya ngozi hii tunayoizungumza ngozi yenyewe imeshuka thamani. Ngozi leo kilo moja inauzwa Sh.200 mpaka Sh.500 lakini hivyo viwanda viwili vinavyofanya finishing kwa maana ya Himo na Moshi Tannery, Himo tu kinaweza kununua ngozi tani 100 peke yake, Dar es Salaam peke yake inazalisha kwa siku ngozi tani 45 maana yake Dar es Salaam peke yake inaweza ikalisha hivi viwanda viwili basi, kwa hiyo, mikoa yote hii ikiwemo na Singida ngozi yetu imekosa thamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa lazima tuishauri Serikali vizuri na iwe makini kwenye jambo hili. Tunapotaka kuonesha indicator kwenda kwenye viwanda kuna eneo la muhimu sana, tunataka mashine ziingie humu lakini kwenye Customs Duty ni lazima tuondoe Import Duty na VAT asilimia 18. Itakuwa imetusaida mno kwenye eneo hili ili viwanda na mashine ziingie ili tuweze kuanzisha hivi viwanda tofauti na hapo hatuwezi kuwa na uchumi wa viwanda lakini bidhaa tunazo. Ngozi hii tunayoizungumza ukitaka kuitoa nje unalipa kodi asilimia 80 maana yake ngozi ambayo umeinunua kilo Sh.500 unalipa kodi Sh.1,200 utaenda kuiuza wapi lakini ngozi inateseka leo. Nataka niiombe Serikali wakati tunajiandaa kuweka viwanda hivi iruhusu ngozi hii iuzwe ili Serikali ipate mapato na wananchi waweze ku- survive. Kwenye eneo hili nilikuwa nataka niombe Serikali iliweke vizuri sana taarifa hii haiko sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata kwenye kilimo, nchi yetu leo kilimo ni uti wa mgongo kuondoa Corporate Tax kwa asilimia 10 peke yake haitoshi. Nashauri tuweke zero tu kabisa walau kwa miaka miwili itatusaidia sana ku-promote eneo hili la kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko Regulatory Authority TFDA, TBS, TPRI, NEMC, Vipimo na wengine wengi. Tumezungumza sana kwenye bajeti iliyopita kwamba ifike mahali tu-harmonize hizi Regulatory Authority zote zinafanya kazi moja. Kila mmoja anakwenda kwa mfanyabiashara anatoza ada. Sasa tukaomba tufanye One Shop Stop Center nataka kusema leo hii nayo haiwezekani hawa wote wanafanya kazi ya Serikali, niiombe Serikali ilipwe ada moja tu ya mfanyabiashara kulingana na kiwango; kama mfanyabiashara ana mtaji wake wa Sh.100,000 mpaka Sh.10,000,000 whatever alipe ada moja tu hawa kazi yao waende wakatoe certificate, basi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, aende kwenye kiwanda kwa mfanyabiashara akague atoe taarifa Serikalini siyo na yeye aende akatoze faini na yeye anataka ada, hatuwezi kufika. Tunataka indicator hizi ziwekwe sawa. Kama tunataka uchumi wa viwanda hizi Regulatory Authority ni sehemu ya kumomonyoa hatuwezi kufika, ilipwe ada moja tu Serikalini. Mtu akilipa ada moja hawa kazi yao waende wakafanye auditing kuangalia kama hiyo bidhaa ni halali ama sio halali watoe taarifa Serikalini. Wanalipwa mshahara na Serikali lakini hawana sababu ya wao kuanzisha vyanzo vya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwenye eneo moja la betting, amezungumzia Sheria ya Michezo ya Kubahatisha (sport betting) imeongeza kodi kutoka asilimia 6 mpaka 10 lakini kwenye slot mashine Sh.35,000 mpaka Sh.100,000. Tukizungumzia sport betting maana yake tunazungumzia Watanzania sasa wameamka na mwamko huu ni wa eneo la soka, wapenzi na wanachama wa soka wameona sasa kuna haja ya kuingia kwenye eneo hili na Serikali inapata mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa isiishie hapo, nataka nioneshe na eneo lingine kila mchezo wa soka unaochezwa Tanzania kwenye viwanja vyetu tunalipa VAT baada ya kutoa yale mapato yote get collection wanatoa asilimia 18 inayobaki ndiyo wanaita asilimia 100 wanaanza kugawana. Naiomba Serikali kwenye eneo hili tunataka kuboresha michezo Tanzania na tuboreshe mchezo huu wa soka ili tupate mapato zaidi maana yake hii asilimia 4 na hii shilingi sabini na kitu inayoongezeka tuwape Baraza la Michezo la Taifa ili liweze kujielekeza kuhakikisha kwamba tunapata viwanja na kuboresha mchezo huu wa soka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania hii leo hata ukipewa msaada wa vifaa vya michezo kutoka nje maana yake unalipa kodi. Sasa niiombe Serikali vifaa vya michezo hivi hebu viingie bure hatuna sababu ya kulipa Import Duty wala VAT sababu tunaboresha michezo Tanzania. Nataka niiombe sana Serikali eneo hili iliangalie vizuri sana. Hata ile asilimia 18 ya get collection ambayo inapatikana kwenye viwanja wapeni Baraza la Michezo waweze kuboresha michezo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo lingine la wafanyakazi hapa, niipongeze Serikali kwa kuweka single digit kwenye Income Tax lakini single digit tunayoizungumza hapa inazungumzika kwenye eneo la kima cha chini, hao wengine inaendelea kama kawaida. Serikali izungumze single digit kwenye Income Tax kwenye mshahara wote bila kujali kima cha mshahara cha mtu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu alifafanua vizuri sana kuhusu mishahara ya wafanyakazi, sina sababu ya kurudia eneo hili kwa sababu ya muda lakini nataka niombe eneo moja muhimu sana. Tangu Serikali imeingia madarakani mwaka 2015 tulianza zoezi la uhakiki la wafanyakazi tukasimamisha madaraja ya watumishi wakiwemo walimu, madaraja haya yamesimama mpaka leo. Maana yake mtu aliyeanza kazi 2015 na 2012, 2018 tutawakusanya pamoja waweze kulipwa daraja moja, this is unfair, halitakubalika. Niombe kama alistahili kupanda daraja 2015 kama anaenda daraja D, mwaka 2018 alipaswa kuwa daraja E apewe daraja lake la sasa E na tusirudi huko kumpa daraja D, tutakuwa tumemuonea. Nataka niiombe sana Serikali kwenye eneo hili itusaidie ihakikishe watumishi wetu wanapata haki yao. Hawa watumishi hawana kosa lolote, uhakiki ulikuwa ni wa kwetu wenyewe Serikali siyo wa watumishi, tutoe mwongozo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie eneo lingine la PPP (Public Private Partnership). Nataka niende haraka hapa nitolee mfano, leo eneo la UDART pale Dar es Salaam kwenye usafirishaji mwendokasi mradi ule unakufa lakini Serikali tuna asilimia 49, mtu anaye-hold share na sisi ana asilimia 51, mradi unakufa. Mradi unakufa kwa sababu gani na Serikali imekaa kimya?

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mingi tunaendelea nayo, juzi Mheshimiwa Rais amezindua Agricultural Sector Development Program Phase II lakini Phase I hatujaitathmini ikoje. Hapa tunazungumzia PPP, hata tunapokwenda kwenye standard gauge tunatarajia kwenda kwenye PPP tutakwendaje? Niombe Serikali ituletee taarifa kuhakikisha miradi hii ya PPP inatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Wizara hii kwa kazi nzuri ya barabara iliyofanyika Singida Mjini. Naipongeza TANROADS kwa usimamizi mzuri wa barabara hizi hususani Singida Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimetazama bajeti ya Wizara hii sijaona utekelezaji ama mkakati wa utekelezaji wa ahadi ya bypass kilometa 84 kwa kuanzia tungeanza na kilometa 46 hali itakayotusaidia kupunguza msongamano wa magari makubwa kupita katikati ya mji. Naomba Serikali kuzingatia maombi haya.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kazi kubwa ya kuendelea kulinda amani na utulivu nchini. Naomba Jeshi la Polisi liendelee kuboresha maslahi ya watumishi wake ili waweze kuitenda kazi yao kwa haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba askari wa barabarani (traffic) wachukue muda mwingi kufanya kazi ya kuwaelimisha wananchi badala ya kutafuta makosa na kutoza faini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iweke mkakati wa kujenga Vituo vya Polisi kila Kata hususan Kata za Singida Mjini.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini pia niishukuru kamati kwa kusoma taarifa yao vizuri ambayo imesheheni mambo ya msingi na kwa sehemu kubwa imetushauri sisi tunaohusika na suala la mazingira. Yako baadhi ya mambo machache ambayo naweza kuyatolea ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati imehitaji ili tujiimarishe zaidi katika usimamizi wa suala la mazingira. Ni kweli ziko changamoto ambazo zinajitokeza kwenye mzingira kulingana na wakati tulionao. Tumefanya maboresho ya sera yetu ya mwaka 1997, ili iweze kuendana na wakati uliopo sasa, ili iweze kutatua changamoto zinazojitokeza kwenye suala la mazingira, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, lakini pia, bio teknolojia:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati imegusia suala la ufinyu wa bajeti; nilitaka nilieleze tu Bunge lako kwamba, kulingana na ongezeko la mapato ya ndani sasa tunafanya mawasiliano na wenzetu wa Wizara ya Fedha, ili tuweze kuongezewa fedha, lakini jambo jingine kukwama kwa Mfuko wa Taifa wa Mazingira. Nakubaliana na kamati kwamba, huu ndio muarobaini wa matatizo ya mazingira ambayo yanajitokeza na ulikwama na sasa tunatengeneza waraka maalum kulingana na sheria yetu ya mazingira ya mwaka 2004, ili kuhakikisha kwamba, tunapeleka waraka huu kwenye mamlaka zinazohusika na kuweka ufanisi wa mfuko huu wa mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni uelewa mdogo juu ya mambo ya mazingira:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu imeendelea kufanya kazi hii kwa kina zaidi, kwenye vyombo vya habari, lakini pia kwenye semina, midahalo mbalimbali na tutaendelea. Tunaishukuru kamati kuendelea kutukumbusha juu ya suala la uelewa wa mazingira bado ni mdogo kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine ni vyuma chakavu, biashara ya vyuma chakavu ambayo sisi tunazungumzia suala la udhibiti wa taka hatarishi, tumetengeneza Kanuni ya Mwaka 2019 ya Usimamizi wa Udhibiti wa Taka Hatarishi na kanuni hii imeanza kazi rasmi. Kwa hiyo, nilitaka niwatoe hofu wafanyabiashara wa biashara hii ya vyuma chakavu kwamba, Wizara imeweka utaratibu maalum kushirikiana na Wizara ya Fedha, lakini kushirikiana na Wizara ya Viwanda na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha tunalinda miundombinu yetu ya ndani isiweze kuharibiwa kupitia biashara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati imezungumzia urasimu wa kutoa vibali:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, yawezekana ni kweli, lakini jambo hili tumelichukua kama lilivyo tuende tukakae na wataalam wetu kuweka njia iliyo sahihi kuondoa urasimu uliopo. Tunatambua tumetengeneza, tumebadilisha kanuni, lakini tunatambua pia, katika suala la vibali leo tunatoa Provision License Clearance, tunatoa vibali vya muda mfupi ndani ya siku saba mtu anapata kibali wakati anasubiri kibali cha tathmini ya athari ya mazingira. Kile cheti cha athari ya mazingira kinachukua muda mrefu na ndio maana inawezekana wawekezaji baadhi wanaona kama vibali hivi vina urasimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunao wataalam elekezi nao tumeboresha kanuni yao. Wataalam elekezi ambao wanatambuliwa na Baraza la Hifadhi ya Mazingira kwamba, tumeboresha kanuni yao na kanuni yao itaanza kazi rasmi mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye hoja ya Mheshimiwa Mbunge Mwita Getere,Mheshimiwa Mwita Getere amezungumza vizuri na ushauri wake tumeupokea kama Wizara kwamba, sasa ifike mahali Wizara ya Mazingira isiwe mambo mengi yanafanywa na Wizara za kisekta. Mheshimiwa Mwita Getere ametoa ushauri kwamba, sasa Wizara ijitegemee kufanya mambo hayo, ili kukabiliana na changamoto kubwa inayojitokeza. Na sisi tunakubaliana na hilo na tunalichukua kwa ajili ya kulifanyia kazi, ili tuone huko tunakokwenda tuboreshe maeneo ambayo tunaona yana changamoto, ili Wizara hii isiendelee kukabiliana na changamoto hizi na matokeo yake inaleta kutokuwa na ufanisi ndani ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utekekelezaji wa agizo la kupiga marufuku mifuko ya plastic:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kamati imeeleza vizuri. Na kwa ushirikiano mkubwa wa kamati mifuko ya plastic leo nchini kwa sehemu kubwa sisi hatuitumii, lakini wako wafanyabiashara wababaishaji wanaopitisha mifuko hii kwa njia za panya, lakini iko mifuko ambayo haizingatii viwango na wenzetu wa TBS wameshatoa viwango na mifuko inahitaji kuwa na standard.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuja na mpango huu mzuri wa maendeleo, yapo maeneo ambayo Serikali imefanya vizuri sana:-
(1) Elimu bure licha ya changamoto inayojitokeza. Elimu ya juu hususani mikopo naiomba Serikali itatue changamoto hiyo.
(2) Afya ya mama na mtoto mpango huu umewekwa vizuri sana.
(3) Tulipitisha bajeti ya sh. 50,000,000 kila Kijiji naomba isomeke kila Kijiji na kila Mtaa.
(4) Ongezeko la bajeti ya maendeleo toka trilioni 11.5 mpaka trilioni 13.1 hali hii itatusaidia kuharakisha maendeleo.
(5) Mkakati wa ukusanyaji mapato ikiwa ni pamoja na udhibiti wa upotevu wa mapato.
Naiomba Serikali ipunguze utitiri wa tozo na kero kwa wananchi itawapa unafuu wa kufanya biashara na kuinua pato la Taifa. Serikali iboreshe huduma za maji, afya, umeme, barabara pia na reli.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nikushukuru na niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wetu wa Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, imezungumzwa vizuri juu ya mradi wetu wa kufua umeme wa Rufiji. Ni kweli kabisa kwamba mradi huu una umuhimu mkubwa sana katika uchumi wetu, lakini hatua tuliyofikia ni point of no return.

Mheshimiwa Spika, hofu ambayo imejengwa ni juu ya vyanzo vya maji, na mimi niseme tu nimefanya ziara katika Mikoa sita ambayo inapatikana mito mikuu mitatu inayolisha Bonde la Mto Rufiji. Mto Luwengu ambao unachangia zaidi ya asilimia 19, Mto Ruaha Mkuu unachangia asilimia 15.5 na Mto Kilombero ambao unachangia asilimia 65.5. Vyanzo vya maji vya mito yote hii mitatu viko salama. Ningeomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwamba maeneo yote ambayo mito hii imeanzia vyanzo viko salama. Kazi tuliyonayo sasa ni ku-maintain vile vyanzo vya maji, lakini maji yanakopita mpaka kwenda kwenye Bonde la Mto Rufiji ndiko kazi tunayoifanya kuanzia sasa. Kwa hiyo nimefika mpaka Stiegler’s Gorge kwenyewe kwa kweli maji yapo ya kutosha na mradi huu utakuwa ni mradi wa mfano na utakuwa ni mradi endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mazingira Serikali imeweka utaratibu mzuri sana. Vile viumbe hai tunavi-reserve; tukishamaliza mchakato mzima wa lile bwawa maana yake viumbe hai vile vinarudishwa na shughuli inaendelea kama ilivyo. Vilevile bado pale kutakuwa na faidi nyingi, wameeleza Waheshimiwa Wabunge vizuri; utalii, kilimo na vitu vingine vyote.

Mheshimiwa Spika, pia imezungumzwa tutavunja mkataba wa World Heritage, kitu ambacho siyo kweli. Mkataba huu wa World Heritage umekuja baada ya program hii kuanza, sasa program hii ikishaanza Selou kuwa World Heritage maana yake ule mkataba unakubaliana na program iliyokuwepo. Kwa hiyo nisingependa jambo hili lizungumzwe kwa kupotosha Bunge hili; kwamba tayari mkataba huu umekuja wakati program yetu ya Stiegler’s Gorge ilishakuwepo before. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaandaa master plan kwa ajili ya ku-maintain vile vyanzo vya maji kama Wizara ya Mazingira na sisi tayari tumefungua ama tumeshaweka Ofisi ya Baraza la NEMC pale pale. Yuko mratibu ambaye atakuwa anashughulika na mazingira, pale pale kwenye eneo la Stiegler’s Gorge. Kwa hiyo nilitaka niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba suala hili la mradi huu …..

T A A R I F A

SPIKA: Kwa nusu dakika, Mheshimiwa Msigwa.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, yeah, nilitaka nimwambie rafiki yangu nimpe taarifa kwamba Selous kuwa ni World Heritage si leo, hata Bunge lililopita Serikali ilipotaka kuchimba Uranium ilitutuma baadhi ya wajumbe kwenda Urusi kuomba UNESCO itoe kibali tuchimbe Uranium.

Sasa ukisema Selous hiyo World Heritage imeanza leo, nilikuwa nakupa taarifa kwamba tulianza muda mrefu, huu mradi wetu umeikuta Selous tuko World Heritage tayari. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri malizia dakika moja.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, nimsaidie kaka yangu Mheshimiwa Msingwa, nimefika Iringa bahati mbaya hukuwepo lakini ningeweza kukupa elimu zaidi, mradi umeanza tangu Nyerere kaka, si Bunge lililopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee, nilitaka nimsaidie kwenye hili. Unapokuwa na umeme wa kutosha sisi watu ambao tuna-deal na eneo hili la mazingira ni msaada mkubwa sana, huwezi kuzungumzia asilimia tatu ya Selous. Watu wanapopata umeme leo wamesema Waheshimiwa Wabunge, sasa tutaacha kutumia kuni, mkaa na vitu vingine vyote, watu wata-transform kutoka kwenye matumizi haya wanaanza kutumia umeme. Nilitaka niwaondoe hofu mradi huu tunauhitaji sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ya bajeti imegusa kila nyanja ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, pamoja na kazi inayofanywa na Serikali kwenye sekta hii zipo changamoto nyingi lakini niiombe Serikali kuja na mpango mahsusi wa kuondokana na madeni ya walimu. Niiombe Serikali kuja na mpango wa teaching allowance ili iwe motisha kwa walimu
kama inavyotoa kwa viongozi yaani responsibility allowance.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji; naishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Jimbo la Singida Mjini. Naomba nizungumzie miradi ya vijijini 10 inayofadhiliwa na Benki ya Dunia changamoto kubwa inayojitokeza katika Jimbo la Singida Mjini ni kuwa miradi yote imekamilika
akini wananchi hawapati maji tatizo kubwa ni kwamba umefanyika uchakachuzi mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini tumejaliwa rasilimali ya vyanzo vya umeme:-
(i) Umeme wa upepo na makampuni mawili yaliyojitokeza ni:-
(a) Power pool
(b) Wind East African Company.
(ii) Umeme wa jua (solar power) na kampuni ya Synohydro ya China wamejitokeza kuzalisha umeme huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba TANESCO ipunguze urasimu katika kutoa PPA na pia TANESCO inapaswa kuyaacha makampuni kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 50 kila kijiji, naiomba Serikali yafuatayo; kwanza isomeke shilingi milioni
50 kila kijiji na kila mtaa ili kutoa fursa kwa majimbo ambayo hayana vijiji bali ni mitaa kama Singida Mjini na pia fedha hiyo itoke mapema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kwa uwasilishaji wake mzuri, lakini kwa kazi yake. Hakuna ubishi kwamba mzee huyu kwa kweli ana-fit kwenye nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na umeme; katika Jimbo langu la Singida Mjini ninavyo vijiji 13 na mitaa 13 ambayo haina umeme. Katika taarifa yake Mheshimiwa Waziri, imeonesha wazi kwamba kutakuwa na KV 400 zinapita Singida kwenda Shinyanga, lakini pia kwenda Namanga. Nimuombe sana tusiwe watazamaji, lakini tusiwe watu wa kupisha mradi unapita unaenda kwa wengine na sisi tuwe sehemu ya mradi. Naomba Mheshimiwa Waziri utushirikishe na ikiwezekana sasa vijiji vyangu vyote hivi nilivyovitaja na mitaa viweze kupatiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeguswa kidogo na suala la vinasaba. Kabla sijaendelea na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuweka vinasaba ambavyo vimetusaidia kwa kiasi kikubwa sana; vimepunguza uchakachuaji wa mafuta kwa asilimia kubwa na kama haitoshi vimedhibiti mafuta ya magendo (smagling product). Vinasaba hivi vimedhibiti pia on transit product. Yale mafuta yanayopita hapa kwenda nchi za jirani vimedhibiti, lakini pia hata yale mafuta ambayo yanasamehewa kodi, vinasaba hivi vimetusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi vimeongeza makusanyo ya kodi na vimeleta ushindani kwa wafanyabiashara wa mafuta nchini. Nikuombe sana na niwaombe Waheshimiwa Wabunge na wananchi tufike mahali tuiunge mkono Serikali, tuwe waadilifu na kama haitoshi kwa wale wafanyakazi wetu ambao tunawatuma kwenda kubeba mafuta haya sasa wawe makini na kazi hii kwa sababu Serikali kwa kweli ina mkono mrefu na nikuombe Mheshimiwa uifanye kazi yako vizuri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la madini. Kwa kweli, kwa Mkoa wangu wa Singida tunayo madini mengi sana na ya kutosha, lakini hali tuliyonayo pale haifanani na yale madini tuliyonayo pale. Nataka niiombe Serikali sasa iwaangalie wale wachimbaji wadogo waweze kupewa fedha na kama haitoshi, wachimbaji wadogo wale waweze kupewa elimu, kwa maana sasa waendane na teknolojia ya uchimbaji ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo ninaloliona pale, naliona tatizo kubwa moja, GST. Mamlaka ya GST siyaoni, GST wanavyoonekana kwa sasa kazi yao haina meno. GST wakati umefika sasa wafanane kama EWURA kwa sababu, na wao nao ni wakala, wapewe hatimiliki. Sasa hivi makampuni yote tunayoyaona makampuni makubwa ndio ambayo yanafanya utafiti na wakishamaliza utafiti ule hawako tayari kutupa hali halisi ya madini tuliyonayo pale kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejionea, nitoe mfano wa Shanta Company Limited pale Singida walitoa eneo la Mwintiri kwa wachimbaji wadogo, lakini eneo lile wachimbaji wadogo wameshindwa kuliendeleza kwa sababu hawana utafiti, hawajapewa ramani nzima ya eneo lile lililopo pale. Sasa kwa hali hii ni lazima Serikali ije na mpango kama ni sheria, kama ni nini, ije tuweze kuisimamia. GST wapewe mamlaka wawe mawakala ambao wanaweza kusimamia raw data na sio watu wa kupewa processing data. Huu sio wakati wa processing data. Wawe ni watu ambao wana raw data na wawekezaji wote wanaokuja waanzie GST, hii inaweza kutusaidia sisi na wale wachimbaji wetu wadogo walioko kule wanaweza kupata mwelekeo wa kuchimba madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo alitangulia msemaji mmoja tuko naye kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara alizungumzia namna ambavyo TANELEC, kiwanda ambacho sisi tuna hisa, kiwanda ambacho kimefika mahali sasa Serikali imekitelekeza. Mimi nizungumzie upande mdogo wa REA. REA waliwapa kazi Symbion, Symbion wamekwenda kuomba kutengenezewa transfoma TANELEC, hivi tunavyozungumza zimetengenezwa transfoma za zaidi ya shilingi bilioni mbili zimekaa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia kama Kamati transfoma ambazo Symbion walizi-order ziko pale TANELEC, kwa hiyo, wametuingizia hasara Serikali. Nikuombe Mheshimiwa Waziri na kuna taarifa kwamba ulifika pale na ukatoa maagizo. Na sisi tukuombe ifike mahali sasa hawa watu wanaopewa tender, tender hizi lazima ziangalie kwanza viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati nachangia kwenye viwanda nilitoa ushauri kwamba kabla hatujaenda kwenye kutangaza tenda ya kuingiza viwanda vyetu kwenye tender ni lazima kwanza ikiwezekana 40% ibaki kwetu, 60% waende wakashindanishwe kwenye tender, hali hii itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia wenzetu wa Symbion wanaagiza transfoma kutoka India. Na nilitoa mfano siku ile wenzetu kule wanatoa ruzuku kwenye viwanda vya ndani 10% kwa kila kiwanda. Uzalishaji unakuwa mwingi kwa hiyo, wanatafuta sehemu ya dumping, sasa sisi hatuwezi kuendelea kuwa dumping place. Niombe sana na sisi sasa tufike mahali tuone umuhimu wa viwanda vyetu vya ndani, hali hii itatusaidia kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa nchi yenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini tumejaaliwa kuwa na chanzo cha umeme ambacho ni upepo na mpaka sasa sioni juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba rasilimali hiyo ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia tunaweza kuitumia ipasavyo, sioni. Maana tunakoelekea tunaelekea kwenda ku-misuse rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niuone mpango wa Serikali wa kuhakikisha rasilimali ile iliyojitokeza kwenye eneo letu la Singida Mjini ya umeme wa upepo, Serikali inakuja na mpango wa kuwekeza ama kutafuta wawekezaji. Na kwa bahati nzuri tayari walishajitokeza wawekezaji, kwa bahati mbaya sijajua wameishia wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wind East African Company walijitokeza, lakini kama haitoshi wako Power Pull nao walijitokeza. Sasa niiombe Serikali, kama wawekezaji walijitokeza na wameonesha nia, kama kuna mahali tunaweza kuwa-support basi tuwa-support waje wawekeze umeme pale Singida. Tunajua umuhimu wa umeme kwenye maeneo yetu, sisi tumejaaliwa hilo na maeneo yetu tuna uzalishaji mkubwa sana. Tunauhitaji umeme huu kwa kasi kubwa, utatusaidia kuinua uchumi wetu hasa kwa maeneo yale ya Kisasida ambayo tayari pale tuna uzalishaji na ndio tuna kilimo cha umwagiliaji cha mboga mboga.
Mheshimiwa Waziri nikuombe sana ifike mahali, sisi ndugu zetu wa Singida Mjini pale tunakutakia kila la heri, tunakuomba ufike ili uweze kutuwezesha na sisi kuweza kuupata huu umeme na uchumi wetu uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya na mimi nimalizie kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli kumteua baba huyu ametusaidia sana sisi. Ameionesha dhamira ya dhati ya nchi yenye viwanda kwamba inawezekana kwa sababu tayari tuna uwezo wa kupata umeme kwa kila eneo. Baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji na mikakati mizuri inayomkomboa Mtanzania wa hali ya chini. Niombe mambo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za upimaji ardhi zipungue zaidi ili kumuwezesha mwananchi kuweza kumiliki ardhi. Niiombe Serikali itusaidie kupima ardhi ya maeneo yaliyo pembezoni ya Singida Mjini, karibu kata nane, mfano, Mwankoko, Uhamaka, Kisaki na kwingine ili kuwezesha mwananchi kukoposheka na kuinua uchumi wa maeneo hayo, hali hii itatusaidia kuwa na mpango mzuri wa ujenzi na makazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri.
Niende moja kwa moja katika Wizara hii ya Maji, nadhani umefika wakati sasa Serikali ijielekeze na ielekeze nguvu zake zote pale. Nimeona wametutengea shilingi bilioni mbili point nne, niombe sana kama walivyoomba wenzangu kwamba, fedha hizi sasa ifike wakati zije zote, ili tuweze kukamilisha miradi yetu ya maji iliyoko pale katika Jimbo la Singida Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishukuru Serikali kwa mradi wa maji mkubwa ambao uko pale katika Kata yangu ya Mwankoko. Changamoto kubwa iliyopo pale, mradi ule uko pale, lakini wananchi wa Mwankoko hawafaidiki na ule mradi ulioko pale. Kama hiyo haitoshi, wananchi wale walipisha ule mradi kwa maana kwamba, sasa walipaswa kulipwa fidia; uthamini umefanyika mara ya kwanza zaidi ya milioni 800 hawakulipwa! Umekwenda umefanyika mara ya pili, sasa hivi tunazungumzia bilioni moja na milioni 500 hazijalipwa mpaka sasa! Nilitarajia kuziona kwenye makabrasha haya ambao Mheshimiwa Waziri ametuletea au kwenye kitabu hiki kwamba, shilingi bilioni moja point tano wananchi hawa sasa wanakwenda kulipwa fedha zao za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuwasilisha awaeleze wananchi wa Mwankoko kwamba, watalipwa fedha zao lini, ili kuondokana na hii adha ambayo inaendelea sasa. Na unafahamu kabisa kuchelewa kulipa zaidi ya miezi sita maana yake unakoelekea sasa wafanye uthamini wa tatu tunaenda kuzungumzia shilingi bilioni tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uko mradi mwingine wa maji ambao uko eneo la Kisaki unaitwa mradi wa ILAO. Kwa bahati mbaya sana pale nako kuna zaidi ya shilingi bilioni tatu wananchi wanatakiwa walipwe, kwa ajili ya fidia wamepisha mradi wa maji wa ILAO. Vimechimbwa visima viwili pale Kisaki, vile visima viwili kwa hali iliyoko sasa tunakoelekea maana yake wananchi watakosa maji! Kisima kimoja kilikuwa kinatoa maji cubic metre 250 kwa saa na sasa zinashuka mpaka zimeenda 170 kwa muda wa mwaka mmoja! Kwa mwaka mwingine unaofuata, miaka miwili maana yake wananchi wa eneo lile wanaotegemea maji ya Mradi wa ILAO watakosa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, anapokuja ku-wind up lazima atueleze kwamba, kwa namna gani sasa wananchi hawa tunaweza kuwakomboa na hii adha ambayo inajitokeza kwenye hili eneo la Kisaki. Kwa sasa wananchi wa eneo lile hawafaidiki na ule mradi! Wanalinda mradi, wanalinda maji na visima vilivyoko pale, lakini wao hawapati maji! Niiombe sana Serikali ifike mahali iwaonee huruma wananchi ambao wamepisha eneo lile kwa ajili ya mradi wa maji na wao wafaidike na yale maji, lakini waweze kulipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mfumo wa maji taka. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunayo maabara ya maji, sasa hebu zipewe nguvu hizi maabara za maji zitusaidie kuchunguza kwa sababu tukiacha sasa mfumo wa maji taka huu ukaenda holela hatutakuwa na uhakika na maji ambayo tunayapata sisi kwenye eneo lile! Bahati nzuri tayari tumekwishakaa, tumeandaa mradi mzuri ambao umeshafanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya mfumo wa maji taka, unahitaji fedha. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tunahitaji fedha, sisi tumeshajiwekea utaratibu mzuri juu ya ule mfumo wa maji taka, ili tuondokane na hili tatizo ambalo liko pale katika Jimbo la Singida Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia juu ya Wakala; Wakala wa Maji Vijijini nadhani ndiyo suluhu. Pia Waheshimiwa Wabunge wameonesha hapa Mheshimiwa Waziri fedha atazipata wapi, fedha hizi wameeleza kwenye mafuta, tuongeze pale kama wanavyofanya EWURA shilingi 50, tuweke 50 nyingine, lakini kama haitoshi wamekwenda kwenye simu! Wala hakuna tatizo hatuhitaji kulijadili jambo hili! Nimwombe Mheshimiwa Waziri aliweke mezani, fedha zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ninaporudi mimi kule Jimboni swali hili linakuwa swali gumu sana; wananchi wangu hawana maji, tumewatengea shilingi bilioni mbili point nne! Bilioni mbili hizi tunaomba zifike, ili tuweze kuzisimamia na hizi fidia ambazo nimezizungumza za Mwankoko naomba nazo pia ziweze kuletwa.
MWENYEKITI: Ahsante.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoendelea. Katika sera ya zahanati kila kijiji/mtaa na kituo cha afya kila kata, pia hospitali ya wilaya na mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini kwa asili ya mji ulivyo karibu kata nane za mjini zinategemea Hospitali ya Mkoa. Hivyo ninaiomba Serikali kuharakisha kuanza kazi kwa Hospitali ya Rufaa ili Hospitali ya Mkoa ihamie kwenye Hospitali inayojengwa sasa hivi na eneo/majengo ya Hospitali ya Mkoa yatumike kama Hospitali ya Wilaya, tutakuwa tumemaliza tatizo la Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu damu salama, mpango huu ni mzuri sana na unasaidia sana wananchi hususani Singida Mjini. Changamoto inayojitokeza hapo ni kama ifuatavyo:-

(i) Mwamko mdogo kwa wananchi kuchangia damu;
na
(ii) Halmashauri hazitengi bajeti kwa ajili ya zoezi hilo
hususan Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwezi Juni, 2016 hadi Februari, 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Singida imekusanya unit 12 tu out of 2300 za mkoa mzima. Hivyo tunaishi kwa kutegemea Wilaya nyingine au tunatumia damu isiyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ifanye tathmini kwenye jambo hili. Pia Mganga Mkuu wa Mkoa awe na mamlaka ya kuisimamia Halmashauri katika kutekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fedha za dawa, ninaishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha Singida Mjini takribani shilingi 203,100,000 ambayo ni sawa na asilimia 93. Tatizo tunalolipata dawa hazionekani, nakosa majibu ya kuwaambia. Naiomba Serikali itusaidie kusimamia upatikanaji wa dawa.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru sana, lakini nikupongeze kwa ukakamavu ambao unauonesha hapa Bungeni, Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na ama hakika Watanzania sasa wanasubiri kuona mabadiliko ambayo tumewaahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja, nianze na reli ya kati. Tunajenga reli ya kati kwa standard gauge lakini liwe jambo jema sana tuzingatie vituo vyote. Nafahamu pale Singida itapita Manyoni, Itigi na kuendelea mbele, lakini reli ya kati ilikuwa inakwenda mpaka Singida Mjini. Sehemu pekee ambayo ndiyo sehemu ya kibiashara iko pale mjini. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri katika vituo vyake asiache kituo cha Singida Mjini, almaarufu reli yetu ile tulikuwa tunaiita Kamnyampaa maana yake ndiye mzee mwenyewe yule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, kwenye bajeti tumezungumzia ongezeko la kodi ya mitumba kutoa 0.2 mpaka 0.4. Ni lazima tuwe wakweli, Watanzania bado hatujawa na maandalizi ya kutumia viwanda vyetu vya ndani, ya kutumia nguo zilizoko ndani badala ya kutumia mitumba ambayo ni bei rahisi. Leo hii ukitazama vizuri sisi wote tunatumia sana mitumba kuliko nguo za dukani. Tukiongeza kodi maana yake tunaongeza thamani ya mitumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri amezungumza kuna tatizo la kiafya na mambo mengine. Mpaka tunafikia umri huu kwa kweli wajibu wa Serikali ni kuwaelimisha Watanzania juu ya afya kuliko kuongeza kodi. Kama hiyo haitoshi, tumezungumzia ngozi, kwamba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itakuja na mpango madhubuti wa ku-deal na sekta ya ngozi, ni mpango gani huu? Tunazungumzia sekta ya ngozi wakati hatuna viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vinavyozungumzwa hapa vyote hivi vinatengeneza wet blue, ni temporary turning, ndivyo viwanda tulivyo navyo. Viwanda vinavyofanya finishing, utazungumzia Himo na Moshi Tanneries kule, viwanda viwili haviwezi kukidhi haja ya kutengeneza bidhaa kwa Watanzania wote milioni 50. Tunazungumzia sekta ya ngozi ambayo leo ngozi inaoza kwenye ma-godown, tuna tani karibu 5,000 zinaoza, halafu tunasema tutakuwa na mpango madhubuti. Nilitarajia mpango madhubuti ni kufungua milango, tuondoe ile kodi ya zaidi ya asilimia 80 ya exportation ili hawa watu waweze kuuza ngozi yao East Africa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeua kiwanda cha Mwanza Tanneries kwa sababu ya ukaribu wa ziwa, kitu ambacho siyo kweli. Hebu twende tukaangalie ile Jinja Tannery, ni mita 200 tu pale lakini kiwanda kinafanya kazi, leo tunaendelea kuua viwanda. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, kwenye suala hili la ngozi, huu mkakati madhubuti unaozungumzwa ni vizuri ungeletwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara na nimeshiriki kwenye kikao cha wadau, wachuuzi wa ngozi na wale wenye viwanda vya ngozi, hakuna majibu thabiti yaliyotolewa ni namna gani tuna-deal na viwanda vya ngozi. Leo hii ngozi inaoza, ngozi imeshuka bei imefika mpaka Sh.100, inatupwa, lakini tunasema tumempa Waziri sasa aje na mkakati. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hakuna mkakati na kama upo uletwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mafuta, tumeweka asilimia 10 kwenye importation ya crude palm oil, lakini mafuta yaliyoko ndani leo bado VAT inatutesa. Nilitarajia kuiona Serikali sasa inaondoa VAT katika bidhaa inayosindikwa. Tumendoa VAT katika bidhaa ambayo haisindikwi lakini mkulima yule yule ambaye analima alizeti, anaipeleka kiwandani, ikishatoka pale inalipiwa kodi asilimia 18, maana yake utakuwa hujamsaidia. Kwa hiyo, niombe sana tuondoe VAT pia kwenye mafuta yetu haya ya alizeti ambayo tunayatumia sasa, tutakuwa tumemsaidia mkulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya kwenye mashudu wameondoa VAT na sisi tunategemea sana haya mashudu yatusaidie. Niombe na sisi tuondoe VAT kwenye mashudu. Hii nayo itasaidia wakulima wetu wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini na mimi nichangie kwenye zile shilingi milioni 50 ambazo Serikali inazitoa vijijini. Kuna mambo mawili hapa, tunazungumzia shilingi milioni 50 vijijini lakini hatuzungumzii shilingi milioni 50 kwenye mitaa. Kama sababu kwamba vijiji vina mamlaka ya kisheria, yawezekana mnatutofautisha hapo, mimi nina mitaa 50 na vijiji 20, sasa tunakwenda kuleta mgawanyiko katika jamii ambayo inaongozwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kama sababu ni kwa sababu vijiji vina mamlaka ya kisheria, basi ni vizuri sasa na mitaa hii ipewe mamlaka hayo hayo na wenyewe wapewe mgawanyo huo sawa, unless otherwise tuzungumzie shilingi milioni 50 vijijini kwenye vijiji na mitaa, hapo tutaelewana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini shilingi milioni 50 hii, wenzangu wamejaribu kuchangia nami naomba nishauri, tujifunze katika yale mabilioni ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, tusije tukazalisha mgogoro ambao hatukuutarajia. Tumekwenda na nia njema ya kuwakomboa Watanzania, lakini namna ya kwenda kusimamia zoezi hili la shilingi milioni 50 linaweza likawa mwiba mchungu sana kwetu hapo kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niombe, kama tutashindwa kuanzisha Community Bank basi ni vizuri tutumie NMB kwa maana iko kila halmashauri, tuweke dawati litakalo-deal na hii shilingi milioni 50 li-act kama Community Bank. Tukiweka dawati pale NMB tayari usimamizi wa fedha zile utakuwa uko salama. Sisi wanasiasa tuwe sehemu ya kuwahamasisha watu wetu kuanzisha vikundi na kwenda kufungua akaunti, lakini watakaotoa elimu hiyo wawe ni watu wanao-deal na fedha, jambo hili litakuwa limetuokoa na tunaweza kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie usajili wa pikipiki. Asilimia 50 ya Watanzania leo wanatumia usafiri wa pikipiki. Vijana wetu leo wote unaowaona wamejiajiri kwenye usafiri wa pikipiki. Wanaolipa kodi na wanaochangia matibabu leo ni hao hao waendesha boda boda lakini tumeongeza thamani ya usajili wake kutoka Sh. 45,000 mpaka Sh. 95,000. Nilitarajia kuona utapungua badala ya kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia Watanzania kupata ajira, wako ambao tayari wamejiajiri. Ni lazima tuwatengenezee mazingira bora ili waweze kuboresha sehemu zao hizo za kazi. Naomba jambo hili pia nalo tulitafakari kwa kina tuone ni namna gani tunaweza kuwasaidia hawa waendesha boda boda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na property tax. Nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa hatua madhubuti ambazo wameamua kuchukua kwenye property tax. Yawezekana tukalitazama kwamba halmashauri zetu sasa zinakwenda kufa kwa sababu sehemu hii maalum imechukuliwa na TRA, la hasha! Ule mpango ambao tumejiwekea, kwenye Halmashauri yetu katika zile bilioni tatu ambazo tutakusanya ndani ni pamoja na property tax.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu kwenye mpango huu kile kiasi ambacho tumekipanga TRA kwa maana Serikali itatuletea kama kilivyo, sasa silioni tatizo la property tax hapa, kwa sababu kama tumekubali kukusanya shilingi milioni 100 kwenye property tax Serikali inatuletea zile shilingi milioni 100, imetupunguzia mzigo. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuipongeza kwa dhati Serikali kwa hatua hii ambayo wamechukua kwa kweli property tax itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sehemu nyingine, tumeweka kodi ya asilimia 10 kwenye importation ya karatasi. Awali wakati nachangia kwenye viwanda nilisema, Mufindi Paper Mills walipewa jukumu la kutengeneza karatasi na si mifuko, lakini wamekuwa wakisafirisha pulp na kupeleka Kenya badala yake karatasi huku kwetu inaingia bure. Leo Serikali imeweke asilimia 10, naipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetuwezesha leo tupo hapa, lakini nichukue fursa hii pia kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya, niwapongeze pia nimpongeze Waziri Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya kuzungumza, jambo la kwanza ndani ya Singida Mjini leo tunajenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Mheshimiwa Ummy alifika pale na alitoa maagizo na nimshukuru sana. Naomba nisisitize, tunayo changamoto kubwa ya Hospitali ya Wilaya ya Singida Mjini, eneo kubwa ambalo tunalitegemea ni ile hospitali ya Mkoa tuliyonayo iweze kuhamia iende Hospitali ya Rufaa ambayo ipo Mandewa na ile hospitali ya Mkoa iwe hospitali ya Wilaya. Ninamuomba sana Mheshimiwa Ummy wakati ana wind up atusaidie kutoa tamko hili ili tuweze kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa na ile hospitali ya Mkoa iliyopo pale iwe Hospitali ya Wilaya. Tutakuwa tumetatua tatizo kubwa sana Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie zoezi la damu salama. Niipongeze Serikali inatumia gharama kubwa leo na katika mpango huu wa damu salama imetusaidia sana. Mkoa wa Singida, tangu Juni , 2016 mpaka Februari, 2017 wamekusanya unit takribani 2,300, bahati mbaya sana Singida Mjini zilikusanywa unit 12 tu, changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira mengine inaonesha kabisa Singida Mjini tunawanyonya wenzetu wa Halmashauri zingine kwa ajili ya kutumia zile damu salama. Naiomba Serikali ifanye tathmini na iweze kusimamia zoezi hili kikamilifu kwa kila Halmashauri ili tujue tatizo lipo wapi. Kwa sababu kama unakusanya unit 12 maana yake watu waliochangia damu ni watu 12 tu. inawezekana mwamko ni mdogo au yawezekana watendaji wetu Serikalini wanashindwa kufanya kazi hii vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifanyika tathmini itatusaidi kuweza kupata damu salama kwa wingi, zoezi hili litatusaidia sana. Niombe sana Serikali iweze kulisimamia jambo hili kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kuishukuru Serikali, imetupatia fedha za dawa na mpaka sasa ni takribani milioni 200 tumepata Singida Mjini fedha za dawa, nimpongeze sana Dada yangu Ummy. Karibu asilimia 93 ya fedha za dawa zilizokuja Singida Mjini, asilimia 93 siyo jambo dogo Serikali inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoipata mwananchi anapokwenda kupata huduma na akaambiwa dawa hamna, nami nasimama kwenye majukwaa kuwaambia kwamba Serikali imeleta fedha za dawa asilimia 93, ninakosa ni mazingira gani ninaweza kuwaeleza, matokeo yake itanilazimu sasa na mimi nigeuke kuwa muuguzi au kuwa daktari au kuwa mhasibu ili niweze kusimamia fedha hizi namna zinavyoweza kutumika. Kwa hiyo, niiombe Serikali, tunapotoa fedha na mkatuachia tu tuendelee kuratibu jambo hili sisi wawakilishi wa wananchi mnatupa mtihani mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninaona kwenye vitabu tumepata fedha na kweli fedha zimefika, lakini hakuna dawa. Mwananchi anapokwenda akakosa dawa huwezi kueleza, utaeleza kitu gani? Tuna kila sababu sasa ya kusaidiana ni namna gani tufanye kuweza kusimamia utekelezaji wa hizi fedha zinazoletwa. Kama dawa zimenunuliwa ni lazima tujue dawa zipo na wananchi wetu wasipate matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali Watumishi wetu wanapata wakati mgumu sana, leo tumefika mahali call allowance hamna, extra duty hamna, kazi ni kubwa. Daktari anamaliza shughuli zake, nurse anamaliza shughuli zake lakini ataitwa kwa sababu ni wito na atakuja, atakapokuja kufanya ile kazi halipwi, wanayo madeni makubwa sana watumishi wetu.

Ninaiomba sana Serikali iweze kulisimamia jambo hili, hatuna tatizo hilo, tuna tatizo tu la Menejimenti linalosababisha watumishi wasiweze kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itaua morali ya watumishi. Sisi tunapokaa nao, unapozungumza nao, unafanya mikutano unaona kuna mahali wanajitoa wao kufanya kazi lakini sisi tumeshindwa kuweza kutimiza kile ambacho walistahili kupewa ni haki yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali imeendelea kupunguza tatizo la maji nchini. Singida Mjini katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tulipewa shilingi bilioni mbili mpaka sasa hivi fedha hizo hazijaja. Naiomba Serikali ituletee fedha hizo tuweze kukamilisha miradi ya maji iliyopo. Bajeti hiyo ya mwaka 2016/ 2017 Serikali pia iliahidi kutupatia fedha za fidia shilingi bilioni tatu kwa wananchi wa eneo la Irao - Kisaki waliopisha mradi wa maji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya vijiji kumi vya maji vinavyofadhiliwa na Benki ya Dunia, miradi hii imejengwa Singida Mjini bahati mbaya wananchi hawana maji mpaka sasa hivi. Naomba Serikali ije ifanye tathimini ya miradi hiyo na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa waliohusika kukwamisha miradi hiyo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetuwezesha leo tuko hapa kujadili Bajeti hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika mchakato mzima wa kazi ambayo tumempatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri; nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Hakuna ubishi kwamba Serikali inafanya kazi kubwa na mchango wake ni mkubwa sana kwenye eneo hili la elimu, hakuna ubishi kwenye hilo. Sina sababu ya kuelezea mafanikio ya elimu ambayo yapo na kila Mtanzania anajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu hiki cha Bajeti ya Elimu. Nina Shule kongwe ya Sekondari ya Advance ya Mwenge. Katika ukarabati ambao Serikali inaufanya sasa hivi, lakini shule yangu ya Mwenge haipo kwenye ukarabati huo. Nataka nimweleze Mheshimiwa Waziri, shule hii mwaka 2016 ilifaulisha kwa asilimia 93, licha ya kwamba miundombinu hiyo hiyo tunaendelea nayo lakini Walimu wangu wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Singida, ni Manispaa ya Singida Mjini pekee ambayo haina Shule ya Sekondari ya Kidato cha Tano na sita na ndiyo tunaitegemea Shule ya Sekondari ya Mwenge na ndiyo Shule ya Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nilieleze hili bayana ili Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa ukarabati wa shule hii kongwe ya Mwenge Sekondari. Kwa mazingira haya haya, sisi Singida Mjini tunalazimika sasa kuanza ujenzi wa shule nyingine za Advance ili kuweza kuwapunguzia mzigo wazazi na vijana ambao wanafaulu kwenda shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipewa fedha hii, ikikarabatiwa Shule hii ya Mwenge Sekondari itatusaidia katika mazingira ya kuanzisha hata Mwenge Day kwa sababu tunao uwezo huo. Yataongezwa madarasa, tunaanzisha advance ya Mwenge Day. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana utupunguzie mzigo wazazi, nasi tuwe na kauli ya kuweza kuzungumza kwa wananchi waone umuhimu wa uwepo wa Advanced Level Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hii inao wazabuni mle ndani, wanadai zaidi ya shilingi milioni 500 na hao wazabuni ndio tunawategemea kutuchangia kwenye maabara na kwingine kwenye ujenzi kwa namna yoyote ile. Sasa Serikali lazima ione umuhimu wao, itusaidie na hao wazabuni wakilipwa wataendelea kutusaidia kwa kadri watakavyojaaliwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri na hili nalo aliwekee umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Singida Mjini, Kata ambazo hazina Sekondari, wameanza kujenga na tayari Kata yangu moja ya Unyanga wamejenga Sekondari, inahitaji usajili Mheshimiwa Waziri. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri; tumeshakamilisha majengo ya maabara, naomba sana Shule hii ya Unyanga nayo iweze kupata usajili na tuweze kuwapa morale wazazi wa kuweza kuendelea kuchangia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie juu ya elimu bora (quality education). Hakuna ubishi kwamba Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa na elimu bora. Tayari tunayo elimu bila malipo, tayari kuna Responsibility Allowance inatolewa kwa ajili ya viongozi wetu, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Waratibu; hakuna ubishi kwenye hili. Katika mazingira haya haya, ziko changamoto ambazo hatuwezi kuziepuka ili kufikia malengo hayo. Hii ina-create gap kati ya wale viongozi kwa maana ya Walimu Wakuu, Waratibu wa Shule na Walimu wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu anayeingia darasani leo hakuna allowance yoyote anayoipata, lakini kiongozi anayemwongoza, anayo allowance. Serikali lazima ioneshe ni namna gani inam-promote na huyu Mwalimu anayeingia darasani ili tuweze kufikia quality education. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia kulipa madeni ya Walimu yasiyokuwa ya mishahara. Sasa hayo yaliyokuwa na mishahara ni nani aliyasababisha na ni nani ataenda kuwalipa? Naomba Serikali isibague, tunahitaji kulipa madeni yote na tuondokane na mpango huu wa Walimu kuendelea kudai, inashusha morale ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu leo haendi likizo, fedha ya likizo haipo. Mwalimu anahamishwa, hapewi fedha ya uhamisho, haipo. Mwalimu anawezaje kufanya kazi fedha ya matibabu haipo? Naiomba Serikali ilete fedha kwa wakati Walimu waweze kwenda likizo, Mwalimu anayehamishwa apewe fedha, tuondokane na mpango huu wa madai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la madaraja. Habari ya madaraja miaka mitatu, sijui OPRAS, kila kitu kimeletwa hapa, lakini hakina msaada kwa Mwalimu. Walimu lazima wapandishwe madaraja kwa wakati. Hii ndiyo motisha yetu sisi Walimu wala hatuna kitu kingine. Serikali inapaswa izingatie. Kama tumeamua kwenye Open Performance Appraisal System, basi tuamue. Habari ya kukaa miaka mitatu na yenyewe haitimiii, jambo hili linatupa mzigo mkubwa sana. Naiomba Serikali iliangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa iangalie teaching allowance, hatuwezi kuepuka. Huwezi kutoa allowance kwa Walimu hawa ambao ni viongozi, subordinate wao ukawaacha. Hatuwezi kuepuka hili! Serikali lazima ije na mpango huu, itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Nidhamu; tunazungumzia elimu bora. Tumeunda Tume ya Utumishi ya Walimu hapa kwa Sheria Na. 25 ya Mwaka 2015, wameizungumza Kambi ya Upinzani pale. Ni ukweli usiofichika, tumefuta Mikoa, Halmashauri, tukapeleka Mamlaka ya Nidhamu hii Tume ya Utumishi kwenye Wilaya. Leo watumishi watatu kwenye Wilaya ambayo ina Halmashauri mbili, wameshindwa Walimu 1,200 watawezaje Walimu 3,000? Mamlaka ya Nidhamu haijapewa kipaumbele. Niiombe Serikali iliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo mamlaka, TSC kwenye Ofisi zao haina vitendea kazi, haina fedha, haina chochote. Sasa unatarajia inawezaje kusimamia jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tujue umuhimu wa quality education, tunahitaji kuwashirikisha wadau wote wakiwemo TSC. Kama inashindikana, tuwape semina Waratibu na Walimu Wakuu waweze kuifanya kazi hii kwa pamoja ili tuhakikishe kabisa kama tunazungumzia uadilifu kwenye utumishi uwe ni uadilifu ambao unawagusa watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TSC kama imeshindikana, tuirudishe sheria hapa ili tuweze kuirekebisha. Leo wale maafisa wa TSC wanafanya kazi, hawana vyeo. Haieleweki mishahara yao ikoje, wanafanyaje kazi hii? Naomba sana Serikali iliangalie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni community participation. Serikali ina kila sababu ya kuwashirikisha wazazi na wananchi kuweza kushiriki kwenye hili. Baada ya kuanzisha elimu bila malipo, wengi wamerudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kuanzisha programu maalum ambayo itainua ubora wa elimu. Training; kutoa mafunzo maalum kwa ajili ya wazazi. Tutoe mafunzo maalum kwenye Kamati za Shule, tutoe mafunzo maalum kwa Walimu; hii itatusaidia kufikia malengo ambayo tumeyakusudia ya kuwa na elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuiomba Serikali ione elimu ndiyo kila kitu. Tusipomwangalia Mwalimu huyu kama stakeholder namba moja, hatuwezi kufanikiwa malengo ya kufikia elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja ya Serikali.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu lakini nipongeze sana Wizara, Waziri na Naibu wake kwa kutuletea bajeti nzuri ambayo inajali maisha ya Watanzania wa hali ya chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli ameonesha dhamira yake ya dhati ya kuwatumikia Watanzania. Nimpe moyo tu hata Mitume nao wakati wanakuja walitokea watu ambao hawakuwaunga mkono lakini leo bado tunaendelea kuwaabudu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti yetu ni nzuri sana, kwa kweli inatufanya tutembee kifua mbele. Yako mambo machache ambayo nami napenda niyazungumzie. Nianze na eneo ambalo bajeti imelizungumzia na nipongeze sana Wizara kwa kuondoa kodi kwenye mazao ya biashara na kilimo. Kwenye eneo hili yametajwa mazao hapa kama vile chai, pamba na mengine lakini alizeti halijaangaliwa na Mkoa wa Singida sisi ni maarufu sana na ndiyo waasisi wa zao hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumza nini hapa? Takwimu inatuambia Tanzania tunatumia karibu tani laki nne za mafuta, lakini tani laki mbili na themanini ni (importation) yanatoka nje, palm oil zinazobaki ndizo tani ambazo sisi tunatumia kama laki moja na ishirini. Serikali leo tunazungumza kuwekeza katika viwanda vyetu vya ndani na lazima tujikite katika kuwakomboa wakulima wetu na ni lazima tuhakikishe kwamba mazao ya kwetu tunayapa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mkulima akilima alizeti yake akishaisindika tu maana yake analipa VAT asilimia 18. Huyo huyo mkulima tunamtarajia aende akaongeze angalau heka moja, mbili hawezi, matokeo yake wakulima wote wa alizeti wanaiuza alizeti ikiwa shambani, ndiyo maana uzalishaji unakuwa mdogo. Mafuta ya alizeti tukiyaangalia na ndiyo mafuta bora yana cholesterol ndogo ya asilimia 17 kulinganisha na mafuta mengine yote ambayo yana zaidi ya cholesterol asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mafuta yanayoagizwa nje ni asilimia 70, yanayobaki ni asilimia 30 mafuta yetu ya ndani. Sasa kama Serikali ina lengo la ku-promote tuweze kutumia mafuta yetu ya ndani hasa alizeti tulikuwa na kila sababu ya kuhakikisha tunaondoa hii kodi ya VAT. Serikali imeongeza asilimia 10 kwenye importation ya mafuta yanayotoka nje, mwenzangu aliyepita amesema iongezwe iwekwe hata asilimia 15 na mimi namuunga mkono kwenye hilo, kwa sababu kama tuna lengo la kulinda viwanda vyetu vya ndani basi niiombe Serikali iondoe kodi hii ya asilimia kumi na nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwomb sana Mheshimiwa Waziri, sisi tunaotoka kwenye maeneo haya alizeti ndiyo zao kuu Mkoa wa Singida ambalo uzalishaji wake unashuka kila kukicha, kwa sababu wametuwekea VAT bila sababu ya msingi. Mwaka 2010 tulikuwa na zero rate lakini tumekwenda mwaka 2014 wametuwekea VAT lakini hakuna sababu ya msingi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri awajali wakulima hawa wa zao hili la alizeti ili tuweze kuwasaidia Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pale Singida tunalima sana kitunguu na kitunguu bora kinatoka Singida. Wakati nauliza swali mwanzoni Serikali iliji-commit kwamba itakwenda kutujengea soko la kisasa la vitunguu. Sisi tumekwishatenga eneo na Mheshimiwa Rais alianza ziara yake ya kwanza Mkoa wa Singida namshukuru sana na katika ziara ile aliwaahidi Wanasingida kwamba sasa anahitaji vile vitunguu tuweze kufanya packing pale pale Mkoani Singida badala ya kubeba kitunguu kikiwa raw kiende kufanyiwa packing Kenya na maeneo mengine. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, tumeshaandaa eneo, tuna vitunguu vya kutosha, waje mtusaidie kujenga lile soko liwe soko la kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali imewatambua wafanyabiashara wadogo wadogo, mama lishe, Wamachinga na wengine. Hata hivyo, nilikuwa najaribu kuangalia hawa bodaboda na bajaji ni wafanyabiashara wa namna gani? Mkoa wa Singida hususan Singida Mjini tunao vijana wengi sana na eneo hili la usafirishaji wameturahisishia sana sisi, lakini jambo la kushangaza, Mheshimiwa Waziri vijana wangu leo wanatozwa (income tax) kodi ya mapato ya Sh.150,000/= kwa mwaka bila sababu ya msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naanza kulalamika kwa nini wanatozwa nilimwandikia barua Meneja wa TRA, nashukuru sana kijana yule ni msikivu, lakini ananijibu kwa pikipiki moja bwana tutaacha lakini mmiliki wa pikipiki mbili atalipa Sh.150,000, tunakwenda wapi? Tunataka vijana hao wajiajiri na ajira Serikalini hamna, sasa leo kama watalipa income tax maana yake vijana wale watafanya kazi usiku, madhara ya usiku tunayajua, akishindwa kupata fedha ya kununua mafuta maana yake ataanza kufanya shughuli nyingine. Naomba tusiwaweke kwenye majaribu, Mheshimiwa Waziri hili ni eneo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii Sheria ya Mapato mwaka 2014 ya kukusanya kila mahali sidhani kama ina tija kwa vijana wa bodaboda. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri vijana wangu pale mjini wako wengi, wamejiajiri na mimi ni sehemu ya shughuli zao na mimi ni mlezi wa eneo lao, niombe sana hili eneo kwa kweli kwangu wanatozwa Sh.150,000/= bodaboda na bajaji, hebu tuiondoe kodi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo lingine la maji. Nami niungane na wenzangu kwa kuongeza Sh.50/= kwenye maji lakini tunayo miradi ya vijiji 10 ambayo imekuja Singida lakini utekelezaji wake ni hafifu sana. Niombe eneo hili pia mtaenda kuliangalia kwa sababu ya muda nisieleze sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kwenye milioni 50, kila Mbunge anasimama na vitabu vinaandika milioni 50 kila kijiji. Mheshimiwa Waziri hebu tuliweke vizuri hili sisi wengine tuna mitaa, sasa ukizungumza milioni 50 kila kijiji, mimi naenda kusimama naambiwa naletewa milioni 50 na sheria imekuja inasema milioni 50 kila kijiji, mitaa haipo. Naomba tuiweke vizuri wala hapa hakuna mgogoro, tuweke milioni 50 kila kijiji na kila mtaa ili wananchi wangu kote wapate, kwa sababu hii categorization ya vijiji na mtaa ni ya Kiserikali wala siyo ya kwetu, Watanzania ni wale wale tu. Nimwombe Mheshimiwa Waziri hili pia nalo aliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la REA, tunazungumzia umeme vijijini. Sisi tunaoishi mjini maana yake ni kama unaambiwa wewe unaishi mjini umeme hauwezi kuja. Mimi nina vijiji 20 na mitaa havina umeme, Mheshimiwa Waziri hebu na jambo hili tuliangalie, tutazungumza lugha gani? Kama tunasema Serikali inaleta umeme lakini umeme unakwenda vijijini sisi tunaishi mjini, hatukuzaliwa kuishi mjini ili tukose hizi fursa ambazo Serikali inazitoa, wote tunaishi maisha sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni lazima Wizara iliangalie vizuri ituletee umeme, tusiwe watu wa kulalamika kwenye maeneo haya. Kama wenzetu wanapata umeme na sisi tupate umeme bila kujali vijijini wala mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida una rasilimali ya madini, eneo la Singida Mashariki, Singida Magharibi hali kadhalika Iramba kuna madini. Wako wawekezaji wanaitwa Shanta Gold Mine, wananchi kwa ridhaa yao wamepisha eneo lakini hawajalipwa fidia. Bahati mbaya sana kaka yangu Mheshimiwa Tundu Lissu hili hakuliona lakini naomba mimi niliseme kwa sababu mimi naishi mjini nahitaji waje wawekeze mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wale wawekezaji, Shanta Gold Mine sasa wana miaka mingi, wananchi wangu sasa wamebaki kuvamia kuanza kuchimbachimba kidogo kidogo yale madini yako ya kutosha, wanahitaji kulipwa fidia na ule uchimbaji uweze kuonekana. Mheshimiwa Rais keshatuonyesha njia sasa hatuna sababu ya kurudi nyuma. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pia nami nachukua fursa hii kuwapongeza sana mabingwa wa Tanzania Dar Yanga Afrika, wameweza kutuwakilisha vyema Kimataifa na sasa wameingia kwenye makundi. Pia nichukue fursa hii kuwapongeza vijana wetu wa Singida United ambao wamefanya vizuri na sasa wameingia fainali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na taarifa nzuri sana ya Mheshimiwa Waziri, nampongeza yeye na Naibu wake; pia yako maeneo tuna kila sababu ya kushauri. Wizara kama ambavyo wameeleza wenzangu, kwa sasa kuna eneo muhimu sana, tunazungumzia entertainment industry. Kwenye eneo hili la kiwanda, nilitarajia kuiona Wizara inatambua kwamba hapa tuna kiwanda. Tukishazungumza kiwanda, content za kiwanda zinajulikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya vizuri, iko Bodi ya Filamu ya Tanzania, iko Baraza la Sanaa (BASATA), lakini iko BMT. Vyombo vyote hivi vya Serikali havijaonesha ni namna gani vinawekeza kwenye kiwanda hiki? Havijaweka mazingira wezeshi ya wawekezaji kuja kuwekeza, badala yake kwa asilimia kubwa vime-deal sana na maadili ambalo ni jambo jema sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwakumbushe kidogo. Kwenye tasnia hii ya filamu, tulikuwa na Marehemu Kanumba, alifanya kazi kubwa sana kuitangaza Tanzania; lakini hata baada ya kutangulia mbele ya haki, kazi zake zinaonekana. Leo nilitaka kuona Mpango Kazi wa Serikali wa kutuwezesha sasa kuwa na akina Kanumba wengine ili kuweza kui-promote Tanzania. Hatujauona Mpango Kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tukumbuke, sasa hivi kijana wetu Diamond anakwenda kutumbuiza kwenye World Cup. Ni fahari ya Tanzania. Najua wakati anaondoka tutamkabidhi bendera na wakati anarudi tutampokea vizuri, tutapiga picha na vitu vingine. Tunajifunza nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Diamond haendi kuwakilisha Wasafi Record, anaenda kuwakilisha Tanzania. Tunatarajia kwa uwakilishi wake duniani wawekezaji watataka kuja Tanzania. Je, mazingira ya kuwekeza tumeyaweka? Wale wawekezaji hawawezi wakaja wakaenda Wasafi Record, watakuja kwenye Wizara ya Habari na Utamaduni kujua mazingira ya kuwekeza kwenye sanaa hii yakoje? Hakuna mazingira yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, consistency hii haipo. Maana yake hatuna watu wengine ambao tunaweza kuwaandaa wakaweza kuitangaza Tanzania, lakini badala yake tumeweza kusimamia kwenye eneo la maadili ambalo mimi naliunga mkono. Ila tulipaswa kutambua, tusitazame tulipoangukia, tunatakiwa tutazame tulikojikwaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka maadili yamepotoka, mpango huu wa maadili kupotoka Serikali ilipaswa iangalie wapi ambapo maadili yamepotoka? Siyo kurudi kuanza kufunga tu kuangalia maadili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ni ushindani na mazingira haya ya ushindani yanawapa wakati mgumu sana wasanii. Ili aweze kutoka na mazingira magumu aliyopitia, ni lazima aangalie nchi nyingine wamefanya nini ili aweze kushindana na hilo soko. Katika ushindani huo, lazima tuingie kwenye mazingira haya. Nasi Watanzania tunataka kuangalia kwa sababu tayari jamii yetu imekuwa ina mtazamo huo, lazima turudi, Serikali ikae na wasanii hawa, ikae na wanamichezo wote, izungumze nao. Wanapitia mazingira magumu sana! Kwa mazingira hayohayo, iwekeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuangalia kazi ya Bodi ya Filamu, eneo kubwa sana ni tamasha, makongamano na kadhalika. Sijaona mahali ambapo inaenda kuwekeza kwa hao wasanii. Itatupa mazingira magumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie eneo hili la soka. Sisi wadau wa soka, tunafika mahali tunajivunia eneo ambalo Shirikisho la Michezo la Taifa imelisimamia, tumewapa mzigo mkubwa sana na TFF wanafanya kazi kubwa sana, lakini taarifa yote hii ya Serikali haijatambua hata mchango wa TFF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipaswa kwenye bajeti hii na taarifa ya Serikali ioneshe ni namna gani inaweza kuwasaidia TFF kufikia malengo yaliyotarajiwa. Sasa TFF haiwezi kufika mahali ikaandaa na viwanja ama ikajenga viwanja. Serikali ilipaswa ituoneshe mpango thabiti hapa wa kujenga viwanja, lakini ilipaswa itoe maelekezo kwenye Halmashauri zetu, itenge maeneo ya viwanja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo viwanja ambavyo unaviona, vingi ni vya Chama cha Mapinduzi. Nilitarajia kuiona Serikali iingie ubia na CCM katika uboreshaji wa vile viwanja ili viweze kusaidia kwenye eneo hili la soka. Sasa kama huna viwanja na viwanja vimesimamiwa na mapato ya kiwanja kwenye gate collection ni asilimia 15.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Baraza la Michezo la Taifa lenyewe linapata asilimia moja na wanaridhika. Kwenye gate collection wanapata asilimia moja wanaridhika. Sasa utaendeleza michezo Tanzania? Maana yake inaonesha kabisa hakuna link hapa ya Serikali na Chama cha Mpira kwa maana ya Chama cha Soka. Hamna link yoyote! Serikali lazima ilitazame hili; inawezajie kusaidia kwenye eneo hili la soka? Tofauti na hapa, hatutaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wetu wa Ngorongoro Heroes na Serengeti Boys, nichukue fursa hii kuwapongeza sana. Hizi ni juhudi binafsi za wazalendo, wanafanya kazi kubwa sana. Nilitarajia kuona mpango wa Serikali utakaowezesha vijana hawa under 17 wengine under 21kwa miaka ijao tuwe na timu ya Taifa bora. Sijaona mpango wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri kama inawezekana, ni vizuri vijana hawa tukawapeleka nje hata kwenye Academy za wenzetu ambako soka limeendelea, lakini tukawapeleka kwa mkopo kwenye timu za nje hata kama ni za daraja la nne na kuendelea wakapikwa kule, hata kama Serikali ikigharamia wale vijana wakaa kule. Wakiwaacha huku wakaja kwenye timu zetu, watakuwa polluted na wala hawatawaona. Nasi Timu yetu ya Taifa hata siku moja hatuwezi kufika mahali tukaweza kuingia kwenye mashindano makubwa tukasema sasa timu yetu ya Taifa itafanya vizuri, hapana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iliangalie eneo hili. Kwa mazingira haya tunazungumzia uchumi wa nchi. Uchumi wa nchi, hauwezi kujengwa tu na viwanda vingine. Natarajia kumwona na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, anatambua kwamba kuna entertainment industry katika viwanda vyake 3,600.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kiwanda kikubwa kuliko viwanda vyote; na kwa sababu najua huwa anaweka machanganuo mzuri kwamba kuna viwanda vikubwa, vya kati, vidogo na vidogo sana, maana hata kiwanda cha juisi anakiita kiwanda kidogo. Sasa entertainment industry ni kiwanda kikubwa sana. Kimeajiri vijana wengi. Lazima tuwe na mpango kazi na lazima tujitathimini wenyewe kabla ya kuamua kukwamisha kazi zao. Ndugu zangu, kazi hii ni ngumu mno. Sisi wanamichezo tunajua huko tunakoelekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejikita kwenye UMISETA na UMITASHUMTA. Sisi Walimu tunajua lile ni somo, lakini je, Serikali kama inajua hili ni somo na imesimamia kule, imewezesha kwa kiwango gani maeneo haya hizi shule zikafanya vizuri? Siyo tu kufanya vizuri, mwisho wake nini? Wale vijana wanapoenda kwenye mashindano yale wakamaliza, mwisho wake nini? Maana siyo wanaenda kwenye mashindano wanarudi, biashara imeisha. Ni lazima kuwe na mpango kazi wa Serikali utakaoendeleza michezo mashuleni. Watoto wale wakimaliza wanaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitarajia kuona hata kama hatuwezi kujenga Academy, uwepo mpango tu kwamba Serikali imeweka mpango wa kuwa na Academy, watoto wanatoka shule wanaingia kwenye Academy tunaendeleza vipaji vyao. Leo tutakuwa tunazungumza habari ya eneo hili la michezo, tutalizungumza tu, lakini...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MUSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru na nikupongeze sana kwa Tulia Marathon.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri wanayoiendelea kuifanya kwenye Wizara yao ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue hii kuwashukuru kwenye taarifa yake ya kwenye kitabu hiki Singida Mjini walau tumeonekana, ninamshukuru sana. Eneo langu la Irau pale Kisaki limetengewa fedha kama shilingi milioni 900 na kama haitoshi kuna fedha zingine za upanuzi wa miundombinu ya maji kama shilingi bilioni moja, kwa ujumla yake tumepata kama shilingi bilioni tatu. Nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuieleza hofu yangu ya upatikanaji wa fedha hizi, inanitia mashaka kidogo kama fedha hizi zitakuja, kwa sababu bajeti ya mwaka 2016/2017 nilitengewa shilingi bilioni 2.4 fedha hizi hazikuwahi kuonekana mpaka leo. Mheshimiwa Waziri alifika Singida akasema tumetengewa fedha, lakini akiwa bado anachangia Mpango wa Maendeleo hapa Bungeni alitolea mfano wa Singida kwamba tulitengewa fedha na hatukuziomba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kulisema hili kwa sababu katika mazingira ambayo ninayaona Wizara inatenga fedha zinazokwenda Halmashauri na mimi nakwenda kuongea na wananchi wangu kuwaambia tumetengewa fedha za maji zinakuja, lakini fedha haziji na Mkurugenzi anaulizwa anasema hana taarifa ya fedha zinazoletwa na Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto hii imekuwa kubwa sana ndiyo maana hofu hii naileleza wazi. Lakini nimeendelea kuifuatilia na katika kufuatilia kwangu nimegundua uzembe mkubwa sana unaofanywa na Halmashauri zetu hizi, ukiangalia malalamiko makubwa ya miradi ambayo haitekelezwi kwenye Halmashauri ni miradi ambayo inasimamiwa na TAMISEMI. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tuliweke jambo hili wazi, Wizara ya Maji inatenga fedha, lakini fedha zinazokwenda Halmashauri zinasimamiwa na TAMISEMI na TAMISEMI tumekwishamaliza bajeti yao hapa, sasa niiombe Serikali iangalie jambo hili na ninaiomba Idara ya Maji kwenye Halmashauri isibaki kwenye Halmashauri, isimamiwe na Wizara ya Maji na Umwagilaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweza kutofautisha leo Wizara ya Afya, hospitali za Rufaa za Mikoa zinasimamiwa na Wizara ya Afya, kwa nini Idara za Maji za Halmashauri zisisimamiwe na Wizara ya Maji ili kuweka utaratibu mzuri wa kuweza kulisimamia jambo hili. Eneo hili linatupa mkanganyiko mkubwa sana na TAMISEMI imeshakuwa kubwa, hebu tuipunguzie mzigo yenyewe ibaki kufanya monitoring, suala la maji libaki kwenye eneo la Wizara ya Maji, nimuombe Mheshimiwa Waziri akija alione eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naungana na wenzangu kuomba kuundwe tume ili kuweza kufatilia miradi ya maji ambayo imeshindwa kutekelezeka na mikataba mibovu iliyotengenezwa huko nyuma imefanya wananchi wetu wasipate maji, niombe sana Bunge lako liweze kuliangalia hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo fidia ya maji kwenye maeneo yetu, ninamshukuru Mheshimiwa Waziri alitupatia fedha kwenye Kata yangu ya Mwankoko shilingi 1,500,000,000 lakini bado kuna fedha zingine wananchi wanadai nimuombe ili aweze kutupa hizo fedha. Lakini tunalo eneo la Irao ambalo lipo Kisaki wananchi wanadai fedha ya fidia shilingi bilioni 2.1, bado kule Misaki Mandeo wanadai shilingi milioni 200, jumla ni takribaki shilingi bilioni 2.5 nimuombe Mheshimiwa Waziri hili nalo aliangalie wananchi hao wanahitaji kulipwa fidia ya maji ili iweze kuwasaidia kwa sababu wananchi walikuwa waungwana kupisha vyanzo vya maji tuweze kupata maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida unakua kwa kasi sana, tunataka tuendane na kasi ya ujenzi wa viwanda. Viwanda haviwezi kujengwa kama hatuna maji ya kutosha, kuendelea kutegemea visima maji yanayochimbwa maana yake hatutafikia malengo. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, ule mkakati wa maji ya kutoka Ziwa Victoria unaokwenda mpaka Simiyu usiishie Simiyu, utoke Simiyu uingie Mkalama, utoke Mkalama uende Kiomboi, uingie Singida DC, uje Singida Mjini, Ikungi, Manyoni na Itigi, Mkoa mzima utakuwa umeweza kuingia kwenye mtandao wa maji wa Ziwa Victoria. Ninamuomba sana Mheshimiwa Waziri eneo hili ni muhimu mno hatuwezi kuendelea kutegemea visima peke yake tukawa na viwanda vya kutosha, watusaidie wasiishie Simiyu waje moja kwa moja mpaka Mkoa wa Singida na wote tutaweza kuendana na kasi hi ya ujenzi wa viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Manispaa ya Singida inakua kwa kasi mnoo, kumekuwa na ongezeko kubwa la watu lakini kama haitoshi watu wanajenga kwa kasi kubwa lakini miundombinu ya maji taka haiwezi kutosheleza mazingira tuliyonayo. Wameshafanya feasibility study kwenye eneo la Manispaa, tunahitaji fedha ili kuweza kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya maji taka. Eneo hili litatusadia sana, tukiacha hivi ilivyo tutakuwa na mazingira magumu sana ya kesho kuendelea ku-solve tatizo hili kwa kutumia magari ya maji taka. Pale Singida hatuhitaji magari ya maji taka, tunahitaji kuhakikisha kwamba kuna miundombinu rafiki kwa ajili ya kuondoa majitaka yale na kwenda kwenye Maziwa yetu tunayo mabwawa mawili pale ya Singidani na Kindai. Ni lazima Serikali ije na mkakati wa uvunaji wa maji, hatuwezi kuendelea kutegemea visima kama nilivyosema awali na Singida tunalo eneo ambao tulikwisha lipanga kwenye master plan yetu, eneo hili linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Mheshimiwa Waziri atusaidie kushirikiana na Wizara hii, lile eneo tulilolitenga maalum eneo lile tuweze kupewa kwa ajili ya kuchimba bwawa ili tuweze kuyavuna maji haya. Itatusaidiasana kupunguza tatizo la maji katika Jimbo la Singida Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, wamesema wenzangu kwamba lazima kuwe na Wakala wa Maji Mijini na Vijijini, lakini walio wengi wanazungumza Wakala wa Maji Vijijini, hapana! Tuzungumze Wakala wa Maji Mijini na Vijijini. Tumefanya kosa kwenye REA, tumezungumza Wakala wa Umeme Vijijini peke yake na leo wa Mjini tunahangaika na suala la umeme. Sasa tuzungumzie Wakala wa Maji Mjini na Vijijini, tukiliweka hivi maana yake tutaondoa shaka tunaoishi Mjini. Ninamuombe Mheshimiwa Waziri aliweke kwenye mazingira hayo, litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wamezungumza wenzangu kuhusu nyongeza ya shilingi 50 kwenye lita ya mafuta ya petroli na dizeli nami nataka niwaunge mkono, ukifanya hesabu ya haraka unaongeza kwenye bajeti hiyo isiyopungua bilioni 160, siyo fedha ndogo. Niwaombe sana Wabunge wenzangu na niiombe Serikali ione umuhimu huu wa kuweza kuweka nyongeza hii. Tutaondokana na tatizo la maji kwenye mazingira haya ambayo yanatukabili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nichukue fursa hii kuunga mkono bajeti na nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri, ama hakika kitabu hiki walimu tuliozoea kusoma kitabu hiki kina mikakati ya kutosha na kitabu hiki kinajitosheleza. Tukiweza kukisoma vizuri nadhani tutatumia muda wetu mzuri kuweza kutatua matatizo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana. Nami nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema. Pia nikishukuru chama changu, niwashukuru pia wananchi wa Jimbo la Singida Mjini kuniamini tena kwa mara nyingine ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nijikite ukurasa wa 25 eneo ambalo linazungumzia kukuza ujuzi. Kulikuwa na Tume imefanya utafiti iliyokuwa inaitwa Tume ya Mipango mwaka 2014 ilifanya utafiti wa kuangalia hali ya soko la ajira nchini, lakini matokeo ya utafiti ule umeonesha iko tofauti kubwa ya uhitaji wa ujuzi kwenye soko lakini na ujuzi unaotolewa katika vyuo vyetu vya elimu ya ufundi. Wameenda mbali zaidi wakaamua kufanya reference kwenye nchi za wenzetu za China, India, South Africa na nyingine, lakini huko wamekwenda mbali sana walipaswa watueleze tulikwama wapi kabla ya kwenda kufanya reference. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nieleze hapa, tulikuwa na vyuo vya kati (FDCs) ambavyo leo tumezi-transform kuwa university. Mtu anapopata degree unamuandaa kuwa manager, kuwa administrator, lakini hawezi kuwa mtu mwenye ujuzi ambaye anahitaji kusimamiwa, sasa tumehama kwenye eneo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri hapa na nitoe mfano. Naibu Waziri kule China, wenyewe wanaita Vice Minister, anaitwa Lu Xin, mwaka 2014 aliamua kwa dhati kuridisha universities 600 kuwa polytechnic. Sisi leo tunatoa hivi vyuo vya kati tumevipeleka kuwa university, kitu ambacho sio sawa lakini hatujachelewa. Nataka niombe Mpango huu sasa uamue vile vyuo vilivyokuwa vya kati vimekuwa university virudi kuwa vyuo vya kati, tutakuwa tume-solve tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Korea Kusini alikuwepo Rais anaitwa Park Chung-hee amefariki mwaka 1979 alikuja na mpango maalum, mpango huu aliamua wawekeze kwenye chuma. Korea Kusini population yake inafanana na sisi lakini ardhi yake asilimia 70 ni milima, asilimia 30 tu ndio wanayoitumia kwa makazi, lakini hawana resource yoyote, resource tulizonazo sisi hata hizo Asian countries hazina, sisi tunazo za kutosha sana; wakaamua kuwekeza kwenye chuma na chuma hiki wana-import. Sisi tuna Mchuchuma na Liganga kwenye Mpango hauelezwi, hatuweki mkakati wa Mchuchuma na Liganga tunategemea kufanya mapinduzi gani ya viwanda? Tunategemea kufanya mapinduzi gani ya kilimo kama hatuwekezi kwenye chuma na chuma tunacho, wala hatuhitaji ku-import chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niiombe Serikali kwa nia njema kabisa, huu ndio wakati sahihi wa kutumia Serikali zetu kwa sababu uwekezaji mkubwa umefanyika na tunatumia vitu vya nje wakati sisi tunavyo ndani. Naomba tufanye mabadiliko kwenye eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri eneo moja dogo sana; leo kilimo chetu hiki wanaotuwezesha ni wakulima wadogowadogo na wanaofaidika na kilimo hiki ni makampuni makubwa. Lazima tutengeneze ukuaji wa dhana ya pamoja, shared growth principle na lazima tuwe na authority tutengeneze mamlaka ambayo itasimamia ukuaji wa dhana ya pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumaanisha nini? Makampuni makubwa ni lazima tuwe na mamlaka ya kuya- control kuyalazimisha yafanye biashara na makampuni madogo. Natoa mfano mdogo, leo nenda Lushoto, Muheza kote kule, matunda yanazagaa lakini Azam yule anaweza kuyanunua yale matunda yote na tukainua kile kilimo cha watu wetu wa chini. Nenda Singida kule leo alizeti inazagaa, lazima aje mchuuzi ndiyo aweze kuuza alizeti, tunawezaje ku-promote hii peasant economy? Hapa ndipo tunafanya wakulima wetu wanafeli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba sana Serikali, umefika wakati wa kuanzisha mamlaka itakayosimamia mikataba ya makampuni makubwa na kwa ajili ya makampuni madogo ili kuweza kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Wizara kwa hotuba iliyoeleza uhalisia na changamoto zinanojitokeza katika kukamilisha utekelezaji wa miradi. Naiomba Serikali ifuate yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, iongeze bajeti ya kilimo hasa kwenye miradi ya maendeleo kwa sababu bajeti iliyopo ni ndogo kulinganishwa na ya mwaka 2017/2018. Mazao yote ya kibiashara yapatiwe masoko ndani na nje ili kukidhi mahitaji ya wakulima na kuinua uchumi wa nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na uhaba wa pembejeo na mbegu bora, kwa mfano zao la alizeti. Tunaiomba Serikali kuhakikisha inaondoa uhaba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uhaba mkubwa wa maafisa ugani pamoja na vitendea kazi. Tunaiomba Serikali iajiri na kuleta vitendea kazi.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na watendaji wote. Narejea ukurasa wa 37 wa hotuba ya Waziri kuhusu matumizi ya mkaa. Nampongeza kwa kutambua umuhimu wa matumizi ya mkaa na kuja na mkakati mzuri. In short ingependeza zaidi kama elimu hii ya matumizi ya mkaa ingehusisha viongozi wote wa ngazi ya chini kama watendaji (VEOs/WEOs) ambao wana jukumu la kutoa elimu hiyo na ujumbe kufika kwa haraka. Kwa kuwa teknolojia hiyo ya gesi bado wananchi hawana uwezo wa ku-afford kununua gesi ni vizuri Serikali ikaendelea kuruhusu matumizi ya mkaa.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Maafisa Maliasili na Utalii kwenye Halmashauri zetu ikiwemo Manispaa ya Singida kuwa na mpango kazi wa kuboresha eneo hili. Kwa mfano Singida tunavyo vyanzo vya utalii vingi ikiwa na fukwe. Niombe Serikali itoe maelekezo ya kila Halmashauri kupitia mikoa yao waandae na kuleta taarifa ya maliasili na utalii. Hii itasaidia kubaini maeneo hayo na kuongeza wigo wa utalii.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa Muswada wa Mabadiliko ya Tasnia ya Habari kuelekea kuwa muhimili wa nne. Kifungu cha (7), wajibu na haki ya media lengo ni kuimarisha National Security. Kifungu cha 8(1) kwamba kutakuwa na leseni ya kuchapisha ama kuuza. Hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji, kufanya tathmini kila mwaka, ni source ya revenue na pia itaongeza uadilifu.
Kifungu cha 14(2) kuhusu sifa za Director General, naomba tuongeze awe na uzoefu usiopungua miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha (1) kuhusu Mfuko wa Mafunzo ya Habari, mafunzo ya wanataaluma ya habari, kukuza na kuendeleza program na kuongeza utafiti. Naipongeza Serikali kwa kifungu hiki kwani kitasaidia kuwafanya wanahabari waende na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 23 kuhusu Baraza Huru la Habari; mwanahabari aliyethibitishwa atakuwa mwanachama, utakuwa na uwezo wa kujisimamia, italetea haki ya wanahabari. Vile vile Baraza hili litakuwa na uwezo wa kuishauri Serikali na kusimamia vyema tasnia ya habari.