Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ahmed Ally Salum (5 total)

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Tatizo hili linafanana sana na tatizo la maji ambalo liko kwenye Jimbo la Solwa. Tumekuwa na mradi wa World Bank ambao Serikali kama Serikali, Wizara ya Maji ilitupa approval ya kuendelea na miradi kumi, lakini mpaka leo mwaka wa pili sasa kuna fedha ambazo hatujazipata na kwenye bajeti sijaziona. Naomba Serikali au Waziri wa Maji atuhakikishe leo kwamba tatizo hili linakwisha, fedha zije na watu wanywe maji. Nashukuru sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, tumekamilisha program ya kwanza ya miradi ambayo iliitwa ni ya World Bank Desemba mwaka 2005, lakini miradi hiyo si ya World Bank kama ambavyo tunaitaja, ni miradi ambayo wale wadau wanaotusaidia fedha katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye ile programu ya kwanza waliamua kwamba miradi hii isimamiwe na World Bank kwa sababu ya uzoefu wa World Bank, lakini ni miradi ambayo inachangiwa fedha na Serikali pamoja na wadau wengine wakiwemo ADB, Benki za Ufaransa pamoja na World Bank yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini programu ya kwanza tumemaliza Desemba 2015, sasa hivi tumeingia kwenye programu ya pili ambayo imeanza Januari mwaka 2016. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba miradi ile ambayo haikukamilika au miradi ambayo haikuanza utekelezaji katika kipindi kile lakini ilikuwa imepangwa, basi katika awamu ya pili tutahakikisha kwamba tunakamilisha ili wananchi waweze kupata maji.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nashukuru sana kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri yenye matumaini kwa wananchi wa Jimbo la Solwa na hasa Hospitali yetu ya Wilaya katika Kata hii ya Salamagazi, Makao Makuu ya Wilaya yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali hii imechukua muda mrefu, sasa imefika miaka karibu sita na nguvu ya Halmashauri yetu ilifika mahali ikawa haiwezekani kuikamilisha; na kwa kuwa tumeomba fedha hizi kwa muda mrefu; na kwa kuwa Serikali sasa imeahidi kulikamilisha: Je, fedha tunazozihitaji tunaweza tukazipata zote katika bajeti hii inayokuja ya 2017/2018? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Mheshimiwa Naibu Waziri, Jafo mdogo wangu, namwamini, naiamini Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, yeye mwenyewe na Serikali yake yote kwa ujumla, anaweza akawa tayari kuja kutembelea hospitali hii akajionea hatua na nguvu ya Halmashauri yetu tuliyoiweka na kwa nini tunaomba fedha hizo ili Hospitali yetu ya Wilaya iweze kukamilika na kutoa huduma kwa wananchi wetu wa Jimbo la Solwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Ahmed kwa sababu amekuwa akizungumzia sana hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme wazi kwamba nami nilifika katika Mkoa wa Shinyanga, nimebaini changamoto zinazoukabili mkoa huu, hasa ukiangalia kwanza pale tuna Hospitali ya Mkoa, lakini ukiangalia katika eneo hili la Shinyanga Vijijini hakuna hospitali ambayo itaweza ku-accommodate idadi kubwa sana ya watu. Kwa hiyo, kinachotokea ni kwamba, wagonjwa wengi sana wanakwenda pale katika hospitali ile. Kwa hiyo, ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, katika mpango huu wa bajeti ya mwaka huu wa fedha tutahakikisha kwamba, zile shughuli za awali za kuhakikisha kwamba hospitali inasimama, tutajikita nazo hizo. Naomba nimtoe hofu kabisa, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo. Leo hii asubuhi nilikuwa nafanya mawasiliano na Mkurugenzi kule Shinyanga Vijijini kuona jinsi gani wanajipanga na kuwapa agizo na sisi huku Serikali Kuu tuweke nguvu ya pamoja ili wananchi wa eneo hili waweze kupata huduma ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kiujumla ni kwamba Serikali itajitahidi kwa kadri iwezekanavyo; na katika mchakato wa bajeti nami nitatoa kipaumbele sana kwa sababu nimefika eneo lile, nimebaini changamoto na Mheshimiwa Mbunge muda mrefu alikuwa analipigia kelele eneo hili, lakini kwa bahati nzuri ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ambayo wananchi wana imani kubwa katika hilo na kwa kuwa Mheshimiwa Rais ameahidi, lazima litekelezwe. Ni jukumu letu sisi Serikali kuhakikisha tunafanya, tusimwangushe Mheshimiwa Rais, ahadi ile iweze kutekelezeka na wananchi wapate huduma ya afya iliyo bora.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, ya kuuliza swali la nyongeza; kwa kuwa sera hii ya kupeleka maji ndani ya vijiji vyote ambavyo vinapitiwa na bomba hili la Ziwa Victoria ziwe ndani ya kilometa 12 imepelekea baadhi ya vijiji katika maeneo yanayopita hasa kwenye Jimbo la Solwa ambalo bomba hili kuu kutoka Solwa linakwenda kwenye maeneo mengi katika Mikoa ya Shinyanga na Tabora. Je, kwa nini sasa Wizara isione namna bora ya kuweza kupeleka maji haya zaidi ya kilometa 12 kwa sababu vijiji vingi vimeachwa kwa kuongeza tenki dogo kuongeza gravity ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na maji haya?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtandao wa bomba la KASHWASA umeacha matoleo katika maeneo mbalimbali na ndiyo maana matoleo yaliyopo Shinyanga sasa tunapeleka maji Tinde. Kwahiyo, kwenye mradi hizi kilometa 12 ni yale maeneo ambayo yatachukua maji moja kwa moja kutoka kwenye hili bomba kuu, mradi unaoendelea kupeleka kwenye vijiji vya kilometa 12. Lakini kupitia kwenye matoleo yaliyopo tunaweza tukaenda hata kilometa 50 na tumeanza kufanya hivyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hiki ni chanzo cha maji tutaendelea kupeleka maji mpaka zaidi ya kilometa hata 100 kutoka kwenye hili bomba.
MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante, pamoja na majibu yasiyoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri na ni mepesi mepesi sana, naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hivi, katika Jimbo la Solwa tuna maboma 158, kati ya hayo maboma 40 ni zahanati kwa maana zahanati 32 na nyumba za watumishi ni 10 na maboma 50 ni shule za msingi, 58 tupo kwenye sekondari kwa maana ya maabara. Fedha zinazohitajika ni zaidi ya bilioni 4.7 lakini sijaona commitment ya Serikali ya kuniambia kwamba katika mwaka huu wa fedha au mwaka unaofuata tutatenga kiasi fulani kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma haya. Kwa majibu haya, ninaona kabisa kwamba hata miaka kumi hatuwezi kukamilisha maboma haya ambayo ni nguvu za wananchi tulikwenda kuyakamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa Serikali inatoa commitment majibu sahihi kwa wananchi wa Jimbo la Solwa kwenda kukamilisha maboma haya hata kwa awamu tatu polepole ili tukamilishe maboma haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, kwanza haya siyo majibu mepesi, kwa sababu Serikali imepeleka fedha shilingi bilioni 29.9 nchi nzima, siyo jambo dogo ni jambo kubwa na la kupongeza. Na Majimbo yote yamepata na Mheshimiwa Mbunge tumetaja kiasi cha fedha ambazo amepata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kumalizia maboma haya ya zahanati, msingi na sekondari ni jambo mtambuka, tunahusisha wadau mbalimbali wa elimu, Serikali yenyewe, Mheshimiwa Mbunge, halmashauri yake na wadau wengine, kwa hiyo hili jambo ni la pamoja. Niseme tu kwamba commitment kwa mfano Halmashauri ya Shinyanga wametenga fedha mapato ya ndani milioni 140 kumalizia maboma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapozungumza niseme tu kwamba wiki iliyopita Serikali hii ya Chama cha Mapinduzi ya Awamu ya Tano imepeleka fedha shilingi bilioni 68.48 kumalizia maboma ya shule za msingi na halmashauri yake imepata. Kwa hiyo, hii ni commitment kubwa, tunaomba hizi fedha zitumike vizuri, cha muhimu wakurugenzi wa halmashauri wanapoleta maboma kule TAMISEMI wawasiliane na Wabunge wao ili wawe kwenye lugha moja, fedha zikienda Wabunge wajulishwe ili waweze kusimamia utekelezaji, fedha iweze kutumika vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
MHE. AHMED ALLY SALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana yanayopendeza kuhusu Bwawa la Ishololo. Lakini kwa kuwa tayari andiko lilishafanyika kwa maagizo yake mwenyewe Mheshimiwa Naibu Waziri mwezi nne liko mezani kwake na kwa kuwa mradi huu umechukua muda mrefu na ni muhimu sana kwenye Kata ya Usule Kijiji cha Ushololo na kwa kuwa tayari hapo ameonyesha commitment kwamba 2021/2022 inaweza likajengwa sasa bwawa hili na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ikiendelea kutafuta fedha.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utakubaliana na mimi kwamba katika mradi huu uwe ni mradi wa kwanza kabisa pale ambapo Tume itakapopata fedha katika mwaka 2021/ 2022?

Mheshimiwa Spika, swali lingine ningependa sana Mheshimiwa Naibu Waziri aweze kutembelea bwawa hili tukienda pamoja ili kuweza kutoa matumaini mapya kwa wananchi wa Kijiji cha Ishololo na Kata ya Usule?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Ahmed Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kwenda kutembelea katika eneo la Ishololo nataka tu nimwahidi kwamba niko tayari na tutakwenda Pamoja. Pili nataka tu nimhakikishie kwamba mradi wa Ishololo, Mradi wa Nyida ambao mradi huu unahusisha vile vile Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini na Nzega District Council kwa maana ya ambayo inahudumia majimbo 3, jimbo la kwake, jimbo la Mheshimiwa Kigwangala na Mheshimiwa Selemani Zedi. Nataka nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba ni miongoni mwa miradi ya priority katika Wizara katika mwaka huu wa fedha na tumeshaanza kufanya visibility study na tutatumia wataalamu wetu wa ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hii fedha ikipatikana.