Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Hawa Mchafu Chakoma (29 total)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Warizi kwa majibu mazuri. Napenda nimwulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ya Naibu Waziri yanaonyesha dhamira ya Serikali ya kupunguza kodi ya Pay As You Earn kwa wafanyakazi wa kima cha chini, napenda kujua sasa kama Serikali ina mpango wowote kwa wafanyakazi ambao wana makato ya kiwango cha juu cha asilimia 30.
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Rais amesisitiza ukusanyaji wa mapato katika kila source ambayo inatakiwa kulipa kodi, je, hatuoni wakati umefika sasa kuwapunguzia kodi hawa wafanyakazi wenye kiwango cha juu? Ahsante.
MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI - WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali la kwanza kwenye kuangalia kama Serikali ina mpango gani wa kupunguza kodi hii ya mapato kwa watumishi ambao wanapata zaidi ya hii shilingi 500,000/= ambapo wanatozwa asilimia 30; niseme tu kwamba kwa upande wa Serikali na kupitia Ofisi ya Rais (Utumishi) tayari tumekwishawasilisha mapendekezo katika Kamati ya Tax Workforce ambayo inaifanyia kazi. Katika Kamati hii wako Wajumbe kutoka Hazina na Wajumbe kutoka TRA.
Mheshimiwa Spika, ni imani yangu kwamba tutakapokutana na sasa ana Baraza Kuu la majadiliano katika Utumishi wa Umma mwaka huu baadaye, tutaweza kuweza kutoa feedback ni kwa kiasi gani suala hili limeweza kuzingatiwa. Aidha, Serikali inaona kwa kweli ni suala la msingi, ikizingatiwa kwamba na wenyewe wanatozwa kodi ya mapato iliyo kubwa.
Mheshimiwa Spika, nadhani nimeshajibu yote, nimeunganisha. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba awe specific kama Serikali ina mkakati wowote kuhakikisha inaijengea SIDO uwezo ili iweze kutoa mafunzo ya biashara pamoja na masoko kwa wafanyabiashara wadogo wadogo ama wajasiriamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa wajasiriamali wadogo wadogo waliokuwa wengi, mitaji kwao ni tatizo na kwa kuwa nchi za wenzetu huko nje zina kawaida ya kutoa kipindi fulani kwa wajasiriamali wadogo wadogo ili kuwasamehe kodi waweze kuwa na nguvu ya kimtaji na waendelee zoezi la kulipa kodi. Napenda kujua kama Serikali yetu ya Tanzania ina mkakati wowote wa kutoa grace period kwa hao wajasiriamali wadogo wadogo. Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO pamoja na kutoa mafunzo kwa wajasiriamali, inao Mfuko Maalum unaohusisha kutoa pesa. Hata hivyo, SIDO kwa kushirikiana na TBS wanakwenda mbali kwa kuwaongoza wajasiriamali namna ya kutengeneza bidhaa zao ziweze kufaa kwenda sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ndiyo swali ambalo Waziri wa Fedha ametujibu hivi punde. Si kivutio, si uwezeshaji, ni msamaha wa kodi tu. Mazingira bora ya biashara ni kivutio kikubwa kuliko ile kumpa pesa. Kwa hiyo, Serikali itahakikisha mazingira bora ya biashara yanapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeanzisha incubators na Serikali ya India inakuja kutusaidia kuwawezesha wajasiriamali wadogo waweze kumudu shughuli, waweze kufanya packaging, waweze kwenda kwenye masoko na tutaanzisha mitaa huko vijijini, small industries street kusudi muweze kufanya kazi kule badala ya kudondosha pesa au kuwapa msamaha ya kodi. Misamaha ya kodi mwenye pesa ameshasema kwamba haitakuwepo ila tutaboresha mazingira.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri Jafo mpaka sasa tunavyoongea baadhi ya shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ikiwemo Shule ya Sekondari Magindu, Shule ya Ruvu Station na Shule ya Dosa Aziz katika kutii agizo la Serikali Kuu la kujenga maabara katika shule zetu za sekondari inakabiliwa na madeni makubwa ya wazabuni pamoja na mafundi. Swali langu la kwanza, ninaomba kauli ya Serikali, je, itakuwa tayari ku-clear madeni hayo ili kutua mzigo Halmashauri zetu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni lini sasa Serikali Kuu itaacha kubebesha mizigo Halmashauri kwa kutoa maagizo nje kabisa ya bajeti ya Halmashauri ya kuzitaka zitekeleza maagizo ya Serikali kuu ikiwemo hili agizo jipya la kila mtoto kukalia dawati pasipo kuwatengea fungu maalum. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa agizo la ujenzi wa maabara na agizo lile lilikuwa ni agizo la kimkakati. Kwa sababu shule nyingi sana katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa hizi shule za kata zilikuwa zina upungufu wa maabara. Sambamba na hiyo watoto walikuwa wakienda shuleni wanakosa fursa ya kupata masomo ya sayansi, kwa mtazamo ulio makini ndiyo maana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
16
alitoa agizo hilo. Lakini naomba niseme wazi kwamba agizo lile limeleta manufaa makubwa sana kwa watoto wetu wanaosoma shule za kata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili niwapongeze Watanzania wote kwa ujumla wamejitahidi katika kila eneo moja kufanya fursa, hata Halmashauri ya Kibaha najua walikuwa na mchakato wa kujenga takribani maabara nane, changamoto iliyokuwepo ni upatikanaji wa fedha ilikuwa ni changamoto kubwa kwa sababu Kibaha peke yake walichanga shilingi milioni 218. 6 lakini bahati mbaya upelekaji wa fedha haukuwa vizuri.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie suala la upelekaji wa fedha lilikuwa sio suala la sekta ya elimu peke yake, mnakumbuka hata miradi ya maji ilisimama ndiyo maana ajenda kubwa ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliposhika madaraka aliazimia kuhakikisha kwamba kodi inakusanywa ili mradi kulipa madeni ya wakandarasi wa aina mbalimbali. Hili naomba niseme pale kuna wakandarasi wanadai na niseme Serikali inalitambua hilo na juhudi ya Serikali itaendelea kukusanya kodi ili mradi kulipa madeni ya wakandarasi kwa kadri iwezekanavyo kuweza kutatua tatizo hilo.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ni lini Serikali sasa itaacha kutoa maelekezo haya. Naomba niwaambie ndugu zangu, Serikali inapima nini kifanyike katika muda gani na hivi sasa mnakumbuka kuna maagizo mbalimbali yametoka lakini lengo lake kubwa ni kuisaidia jamii.
Kwa hiyo, naamini maagizo yote yaliyotolewa na Serikali ni maagizo na kuona ni uhitaji wa kiasi gani uweze kufanyika kwa ajili ya kutatua matatizo ya Watanzania. Lakini hili nililosikia kwamba kila mtoto achangie dawati, hili nadhani ngoja tutalifanyia kazi kwa sababu maagizo yetu ya Serikali kama watu watachangia ni wadau wenyewe katika maeneo husika wanajihamasisha kama tunavyoona hivi sasa, na juzi nishukuru nilikabidhi madawati hapa Dodoma. Watu/wadau waliamua kuchangia madawati lakini siamini kama kuna watu wanalazimishwa kuchangia madawati kwa sababu hizo ndiyo miongoni mwa kero tuliamua kuzitatua katika Jamhuri ya Muungano ya Tanzana ili mradi mwananchi wa kawaida aweze ku-access elimu ya mtoto wake. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya Nane ya World Bank kuhusu Uchumi wa Tanzania inaonesha Watanzania milioni 12 wanaishi katika umaskini wa kutupwa, wengi wao ni vijana na kila mwaka takribani vijana laki nane wanaingia katika soko la ajira. Napenda kujua Serikali ina mpango wa kuzalisha ajira ngapi kwa mwaka?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Mkoa wa Pwani ni wa kimkatati unaounganisha kati ya Bara pamoja na Bandari za Mtwara, Dar es Salaam pamoja na Tanga, hata hivyo vijana wengi wa mkoa huu hawana ajira. Je, Serikali ina mpango gani wa kuelekeza viwanda Mkoani Pwani na ni viwanda vya aina gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma kwa jitihada zake kubwa ambazo amekuwa akizionesha na mapenzi ya dhati aliyonayo kwa maendeleo ya vijana hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ameuliza ni mipango ipi sasa Serikali imeweka ili kuzalisha ajira zaidi. Katika majibu yangu ya msingi nilieleza wazi kabisa kwamba pamoja na kuwa nafasi nyingi za ajira zinatengenezwa ndani ya Serikali lakini Serikali imekwenda mbele zaidi kuzipa umuhimu sekta za kipaumbele ambazo zitakuwa zinachukua vijana wengi zaidi. Lengo ni kuhakikisha tunawachukua vijana wengi zaidi kwa sababu asilimia kubwa ya wanaotafuta kazi wanajikuta wako katika informal sector, formal sector yenyewe inachukua watu wachache sana. Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kuhakikisha inaongeza fursa zaidi za ajira ili vijana wengi waweze kupata nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hizo za kipaumbele ni pamoja na kilimo kama nilivyosema pale awali lakini vilevile na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo vitakuwa ni labour intensive ili kuchukua vijana wengi zaidi. Hata katika Global Employment Trend ambayo ILO wameitoa mwaka jana inaonesha kwamba moja kati ya maeneo ambayo yanaweza yakachukua vijana wengi kwa wakati mmoja ni eneo la viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali imeweka msisitizo na mkazo katika eneo hili na tunajenga uwezo huo ili kuona kwamba vijana wengi wanapata ajira kupitia viwanda vidogo vidogo. Pia kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) Serikali imekuwa na mikakati na mipango mbalimbali ya kuhakikisha kwamba inawasaidia wajasiriamali wadogo kuanzisha viwanda vidogo vidogo hasa vile ambavyo vina-link ya moja kwa moja na sekta ya kilimo ambapo tunapata forward and backward linkage.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili anauliza Serikali ina mpango gani kwa vijana wa Mkoa wa Pwani? Katika kuongeza ajira siku zote tumekuwa tukisema moja kati ya kazi kubwa ya kwanza kabisa ambayo tunaifanya ni kuhakikisha tunawashawishi vijana wengi sana wakae katika vikundi. Kupitia katika vikundi vyao ni rahisi Serikali kuweza kuanza kusaidia kutokana na mahitaji ya maeneo husika. Kwa mfano, vijana wengi wa Mkoa wa Pwani wanafanya shughuli za uvuvi na shughuli nyingine za viwanda vidogo vidogo. Kwa hiyo, ni vyema Mheshimiwa Mbunge pamoja na ujana wake ajitahidi basi kwenda kuwahamasisha vijana wengi wakae katika vikundi ili baadaye Serikali iweze kusaidia katika uanzishwaji wa viwanda lakini vilevile na kusaidia mikopo na mitaji kwa ajili ya vijana hawa.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya Jimbo la Mlimba inafanana kabisa na hali ya Mkoani Pwani kuwa na vyanzo vingi na vikubwa vya maji ikiwemo Mto Ruvu na Mto Rufiji lakini bado wananchi wake wa Wilaya za Kibiti, Rufiji, Mkuranga na Kisarawe wanakabiliwa na adha kubwa ya maji safi na salama.
Je, ni lini sasa Serikali itaanzisha mradi wa kuyavuta maji ya Mto Rufiji ili kuwanufaisha wanawake wa Mkoa wa Pwani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze, Mheshimiwa huyu mara nyingi sana amekuwa ananifuata na kuniuliza maswali mengi kuhusu miradi ya maji na ameniuliza pia hata kuhusu DAWASCO au DAWASA wanapelekaje maji Pwani, lakini nikuhakikishie kuhusu swali lako moja hili tayari tumeanza mazungumzo ya kufanya utafiti wa kutoa maji kutoka Mto Rufiji kuyaleta Dar es Salaam ikipitia na maeneo uliyoyataja ya Ikwiriri, kuja Kibiti, kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapata maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati huo huo tufahamu kwamba tunataka pia kufanya mradi mkubwa wa kujenga bwawa la Kidunda wa kuleta maji. Sasa kama tutakamilisha huu mradi wa Kidunda basi tutaangalia uwezekano kwamba tufanyaje je, tupeleke maji kutoka Kidunda kupeleka huko kwako au tufanye mradi wa Rufiji kwa sababu wakati mwingine unaweza ukafanya miradi miwili mikubwa yale yakawa mengi sana mpaka watu wakashindwa kuyatumia au taasisi za Serikali zikashindwa kuyatumia. Lakini ni kwamba swali lako la msingi ni kwamba ni kweli Serikali sasa hivi inaanza kujiweka tayari kufanya utaratibu wa kufanya utafiti wa kutoa mto Rufiji na kuyaleta Mikoa ya Pwani pamoja na Dar es Salaam.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ya msingi amezungumzia juu ya kuleta sheria hii kufanyiwa marekebisho kwa kuzingatia uzoefu wa nchini nyingine juu ya nyara hii muhimu. Swali langu ni kwamba, je, ni lini sheria hii italetwa hapa Bungeni ili iweze kufanyiwa marekebisho?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali inachukua hatua gani ya kuwanyang’anya Diplomatic Passport watu ambao hawana tena sifa ya kuwa nazo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwamba ni lini sheria hii muhimu italetwa hapa Bungeni? Ni pale ambapo Taasisi husika zitakapomaliza kuirekebisha na kupitia process zote. Kwa sababu kurekebisha inahitaji wadau wazungumze, wajadili na ipitie katika Wizara mbili husika na kuwatumia wadau ambao kwa namna moja au nyingine wanahusika moja kwa moja. Kwa hiyo, itakapokuwa tayari, italetwa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pili, kwamba tunachukua hatua gani kuwanyang’anya passport wale ambao hawastahili; pale ambapo wanapokuja kubadilisha zile passport, hawarudishiwi tena, wanapewa passport ambazo ni za kawaida kutokana na sheria. Huo ndiyo utaratibu ambao unafanyika.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Nina swali la nyongeza eeh.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilikuwa nasubiri umalize kwanza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya Maendeleo ya Dunia ya mwaka 2010 inaitaja Tanzania kama nchi yenye malikale adimu na urithi wa utamaduni wa Taifa ambao ungeweza kuongezea nchi yetu kipato na kukuza uchumi wetu. Nataka kujua sasa, Tanzania inafanya nini katika kutumia malikale zake hizo adimu kama Olduvai Gorge, Laetoli, Kolo na Kilwa Kisiwani ili iweze kuiongezea nchi yetu kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuzingatia umuhimu na mchango wa malikale za Taifa letu katika kukuza uchumi, mnamo mwaka 2007 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, aliagiza nyayo hizo ziweze kufukuliwa ili watalii wengi zaidi waweze kutembelea eneo hilo na nchi yetu iweze kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, anasema hakuna kusuasua kwa ufukuzi wa nyayo hizo ilhali sasa hivi inapita miaka 10 tangu agizo hilo litolewe na hadi hivi sasa tunavyozungumza, bado nyayo hizo hazijafukuliwa. Kwa hiyo, ninachotaka kujua, wananchi wa maeneo yale ambao wanazungukwa na ile historical site wananufaikaje kwa uwepo wa hiyo historical site? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Chakoma kwamba Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba maeneo yetu haya ya urithi wa Taifa yanaletwa katika kiwango ambacho kinaweza kutumika na kutuzalishia mapato katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Ngorongoro, eneo hilo limefukuliwa na wataalam kutoka Tanzania, Spain pamoja na Marekani na kuvumbua nyayo nyingine ambazo zinaonesha kwamba wanadamu hao wanaitwa Zamadamu, walikuwa wanaishi pale wakiwa wanatembea upright miaka milioni 3.6 iliyopita. Nyayo hizo mpya ambazo ziligundulika, zilifunguliwa mwezi Machi, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo pia linajenga museum kubwa, eneo la mapokezi, maktaba na kuonesha vitu mbalimbali ambavyo vitavutia sana watalii watakaotembelea eneo hilo. Aidha, Serikali inaendelea kuyafufua na kuyakarabati maeneo mengi ya Malikale ambayo Mheshimiwa Chakoma ameyataja na kwamba maeneo haya yakiwekwa katika utangazaji wetu wa utalii yatakuwa na mvuto mkubwa na yataongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa sana.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri anasema alishatuma wataalam wake toka katika Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, kwenda katika Kituo cha Kibiti, ili watoe maelekezo sasa namna ya kutoa huduma kwa ngazi ya Hospitali ya Wilaya. Swali langu nataka kujua sasa ceiling ya kituo hicho imekuwaje, ni kwamba, tumeongezewa mgawo wa fedha wa uendeshaji ili ufanane na hadhi ya ngazi ya Hospitali ya Wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali langu la pili; atakubaliana Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, kutambulika kituo cha afya kuwa Hopsitali ya Wilaya kunasababisha kuongezeka mgawo wa fedha na ukomo wa bajeti. Hadi hivi tunavyozungumza Kituo cha Afya Kibiti kina changamoto kubwa ya ukosefu wa vifaa tiba muhimu kama X-Ray Machine na Ultra Sound. Nataka kujua sasa ni upi mkakati wa Serikali kuhakikisha tunapatiwa vifaa hivyo muhimu, ili kuimarisha afya ya wana-Kibiti? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, binti yangu, kwa jitihada kubwa anayoifanya ya kupigania afya za wananchi wa Mkoa wa Pwani kwa ujumla. Kwa pamoja naomba nijibu swali lake la kwanza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa bado hatujapandisha hadhi Kituo cha Afya Kibiti kuwa Hospitali ya Wilaya na kwa msingi huo bado hatujaanza kuwapelekea mgawo wa fedha ambao unaendana na mgao ambao vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo katika ngazi ya hospitali ya wilaya vinapata kwa hivyo mgawo wao bado ni wa kituo cha afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nakubaliana na yeye kwamba, kama kituo cha kutolea huduma za afya kikipanda ngazi kutoka ngazi ya kituo cha afya kwenda kwenye ngazi ya hospitali ya wilaya ni wazi mgawo wa fedha utaongezeka, bajeti yake itaongezeka, idadi ya watumishi itaongezeka, lakini pia idadi ya vifaa tiba vya kufanyia uchunguzi wa magonjwa pia, itaongezeka ili kuendana na huduma zinazopaswa kutolewa katika ngazi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu changamoto ya vifaa tiba, naomba nimtaarifu Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba changamoto hii tunaifahamu na ni kati ya changamoto kubwa tatu kwenye sekta ya afya nchini na mkakati wetu kama Serikali kwa sasa ni kutekeleza mradi unaojulikana kama ORIO ambapo tuko katika hatua za mwisho za kufanya utekelezaji wa mradi husika mkandarasi amekwishapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutakapoanza tunakusudia kupeleka vifaa tiba kama Ultrasound, X-Ray Machines, CT Scans na vifaa tiba vingine mbalimbali kwenye hospitali nyingi nchini ambazo zipo katika ngazi tofauti tofauti; ngazi ya hospitali za rufaa za mikoa, ngazi ya hospitali za wilaya, lakini pia ngazi ya vituo vya afya. Kwa hivyo kwa sasa hivi sina kumbukumbu sahihi kama Kituo cha Afya Kibiti, kipo katika mgawo husika, lakini nitafutilia na nitampa taarifa.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Waraka wa SSRA Namba 1 wa mwaka 2006 unasema kwamba mstaafu atakayecheleweshewa mafao yake, Mfuko husika wa Hifadhi ya Jamii utatakiwa kumfidia, waraka huo unaonekana kutokuwa na nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini sasa mkakati kabambe wa Serikali kuhakikisha tabia ya ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu inakoma? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha kwa majibu yake mazuri na nampongeza sana.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa waajiri wengi lakini na mifuko kwa maana nyingine wamekuwa wakichelewesha ulipaji wa mafao ya wastaafu wetu kwa namna moja ama nyingine. Kupitia SSRA tumeweka sasa mkakati maalum na kupitia maboresho pia ya Sheria za Kazi ambayo yalifanyika ndani ya Bunge lako hili Tukufu, tumewapa nguvu pia Maafisa Kazi wetu ambao sasa wamepata ya kukagua, wanapokwenda kukagua masuala ya kazi, wanakwenda pia kukagua compliance ya mifuko na waajiri katika kushughulikia pensheni za wastaafu na michango ya waajiri kwenye mifuko ya pensheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba Serikali inalisimamia hili kupitia SSRA lakini pia kupitia ofisi zetu za kazi tutaendelea kuhakikisha kwamba waajiri na mifuko ya pensheni inafanya compliance katika sharia zote tulizonazo na wastaafu wetu wapate mafao yao kwa wakati na waajiri wapeleke michango yao kwa wakati.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, visima vilivyopo Kibiti vinazalisha maji kidogo tu, lita 4,000; na kwa kuwa, mahitaji ya maji kwa sasa kwa wananchi wa Kibiti ni zaidi ya lita 8,000 hivi ni kwa nini Serikali isianzishe mradi mkubwa wa maji kutoka Mto Rufiji ili uwafae wananchi wa Rufiji, Kibiti, Kisarawe, Mkuranga na Dar-es-Salaam?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, kuungua-ungua kwa mota mara kwa mara husababishwa na kukatika kwa umeme mara kwa mara. Nini sasa mpango wa Serikali katika kumaliza kadhia hiyo ili wananchi wa Kibiti waweze kunufaika na mradi huo wa Kibiti? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli anavyosema kwamba uzalishaji ni mdogo kuliko mahitaji na hili ni jambo ambalo liko maeneo mengi; lakini tunayashughulikia yote haya kwa awamu kulingana na bajeti inayotengwa na Serikali. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuangalia namna ya kuongeza uwezo wa uzalishaji wa maji, ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Hata hivyo, tumeipangia kwamba, kwa sasa hivi uzalishaji wa pale unakidhi asilimia 70 ya wananchi wa Kibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali tunataka ikifika mwaka 2020 tufikishe asilimia 85 kwa hiyo, tutaongeza vyanzo vingine ili kusudi tuweze kufikisha lengo ambalo tumelipanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kuungua-ungua kwa mota. Hili ni tatizo la mahitaji na uendeshaji ni lazima vitu kama hivyo vinaweza vikatokea. Kuungua kwa mota inawezekana pengine ni matatizo ya umeme unapo-flactuate kuwa mkubwa sana kuliko capacity ya zile mota, zitaungua. Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na Wizara ya Nishati kurekebisha ule umeme unaopatikana pale uwe angalau hauleti madhara ya kuunguaungua kwa mota ambazo zimewekwa.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Nabu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kuvunwa kwa maji ya Mto Rufiji ni pasi moja ndefu mpaka golini, na ushindi huo unanufaisha akinamama kutua ndoo kichwani. Sasa ni kwa nini Serikali inapata kigugumizi kuanza kuyavuna maji haya ili kupoza kiu ya Mheshimiwa Rais ya kuwatua akinamama ndoo kichwani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa mradi huu hauna dalili ya kuanza leo wala kesho. Na kwa kuwa, mradi wa maji ya visima uliopo haukidhi mahitaji ya Wana Rufiji. Ni nini sasa kauli ya Serikali juu ya upatikanaji wa maji safi na salama ndani ya mita 400 kama ilivyo kwenye sera? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimpongeze dada yangu Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake wa Mkoa a Pwani na wananchi wa Rufuji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa Serikali kuutumia Mto Rufiji, nikubalianenae, kutumia Mto Rufiji kutaweza kuondoa tatizo kabisa la maji katika mji wa Rufiji, lakini kikubwa katika lengo na nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba, inawapatia wananchi wake maji. Si maji tu, ni maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa lengo na mkakati wa Rais wetu ni kuwatua ndoo akinamama kichwani na kwa kuwa hii ni Serikali ya Hapa Kazi Tu, kazi ya kuhakikisha kwamba mtaalamu mshauri kwa ajili mya kufanya upembuzi yakinifu wa/ya Mto Rufiji imeshaanza katika utaratibu. Kwa hiyo, subira yavuta heri, namuomba tusubiri kuhakikisha kwamba, tunatekeleza mradi ule wa Mto Rufiji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kuhusu suala zima la kuondoa tatizo la majni katika Mji wa Rufiji; ikumbukwe katika Bunge lako Tukufu katika Mji wa Rufiji tumetenga kiasi cha shilingi milioni 630,977,000 kwa ajili ya kuondoa tatizo la maji kwa kipindi hiki wanasubiri katika suala zima la kutumia Mto Rufiji. Ahsante sana.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa naomba nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi ni kwa muda mrefu sasa Sera ya Matibabu Bure kwa mama wajawazito ya mwaka 2007 imeendelea kuwabagua akina mama wanaopata miscarriage kwa kuwatoza gharama za kusafishwa.
Je, Serikali haioni kwamba hii ni ajali kama ajali nyingine, hivyo basi akinamama hawa ambao walikuwa wana kiu ya kupata watoto wanastahili kufarijiwa kwa kusafishwa bila malipo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni ipi sasa kauli ya Serikali juu ya mabadiliko ya kisera ili ianze kuwa- include akina mama wanaopata miscarriage na wale ambao mimba inatunga nje ya kizazi kuanza kupata matibabu bure na sio kuwaweka kwenye group (orodha) ya magonjwa ya akina mama ambayo kimsingi yanalipiwa kwa asilimia 100? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza lilikuwa limejielekeza kwa nini akina mama ambao mimba zao zinaharibika ama kwa lugha ya kitaalam miscarriage, kwa nini nao wasipate matibabu bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu langu la msingi nilisema kwamba huduma za akinamama wajawazito kuanzia mwanzo wa mimba mpaka mwisho ni bure, hii inakwenda sambamba na tiba ambayo inaambatana na mimba kuharibika. Ninaomba tu niseme kwamba huduma hii ni bure kwa mujibu wa sera yetu lakini kama suala hili halitekelezeki kama inavyotakiwa katika sera niseme tu kwamba tutalichukua na kutoa maelekezo katika mamlaka husika ili sasa hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sambamba na hilo, sasa hivi Serikali tunafanya mapitio ya Sera ya Afya, tutaweka utaratibu mzuri wa kuweza kulisimamia jambo hili.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. La kwanza, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, atakumbuka mnamo mwaka 1981 Serikali ilikitangaza Kisiwa hiki cha Kilwa Kisiwani kuwa Urithi wa Dunia. Hadi kufikia mwaka jana Serikali ilipokea bilioni saba kutoka kwa wafadhili kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miundombinu iliyopo Kilwa Kisiwani ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Mheshimiwa Spika, nitapenda kupata majibu ya Serikali ni kwa nini sasa ujenzi wa miundombinu hii haujafanyika ilhali wameshapokea bilioni saba kutoka kwa wafadhali na pengine Serikali ingeweza kuongeza fedha ili huu ukarabati wa magofu unaoendelea uweze kwenda sambamba na ukarabati wa miundombinu?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri atakubaliana na mimi, watalii wengi zaidi kutoka nchi mbalimbali duniani wangependa kutembelea urithi huu wa dunia, lakini hadi hivi tunavyozungumza hakuna kivuko cha kueleweka cha kuwavusha watalii kutoka Kilwa Masoko kwenda Kilwa Kisiwani, kitu ambacho kingeweza kuingizia mapato Serikali yetu. Nataka kujua sasa ni lini kivuko hicho kitajengwa kutoka Kilwa Masoko kwenda Kilwa Kisiwani ili kuinua kasi ya uchumi katika sekta hii ya utalii? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Kilwa Kisiwani tumepokea fedha zaidi ya bilioni saba kwa ajili ya ukarabati wa majenzi yaani ukarabati wa magofu yote ambayo yapo Kilwa Kisiwani. Naomba nilitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba Kisiwa cha Kilwa Kisiwani kina magofu mengi sana na hizo bilioni saba bado ni kidogo.
Mheshimiwa Spika, hizi tulishaanza kuzifanyia kazi tayari, tumeanza ukarabati na hao vijana ambao wameshapata mafunzo mbalimbali kwa ajili ya kukarabati hayo majenzi wako kazini. Mimi mwenyewe tarehe 9 Machi, nilikuwa kule nikashuhudia jinsi kazi nzuri ambayo inaendelea kufanywa na wale vijana. Kwa hiyo, siyo kwamba zile fedha zimekaa, fedha zile zinaendelea tayari kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu kivuko ni kweli kabisa nimeshuhudia katika lile eneo kwamba tukipata kivuko cha kisasa, kizuri kinaweza kikasaidia sana katika kuwavutia watalii ili waweze kufika katika lile eneo. Hivi sasa Serikali inaendelea kujipanga pale hali itakaporuhusu ya kifedha basi tutaweza kupata kivuko hicho ili kiweze ku- promote utalii katika aneo hilo la Kilwa Kisiwani.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, je, ni hatua gani kali na za kisheria zinazochukuliwa dhidi ya wafanyabiashara wanaosafirisha vijana wa Kitanzania hususan vijana wa kike kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kufanya biashara isiyo rasmi ikiwemo kuuza miili yao?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni ipi sasa kauli ya Serikali dhidi ya madai ya kusikitisha sana kuwa baadhi ya Watanzania wanasafirishwa kwenda nje ya nchi kuuzwa figo zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Hawa Mchafu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu hatua gani kali za kisheria zimechukuliwa kwa wafanyabiashara ambao wamewapeleka wasichana nje na kwenda kufanya biashara ya kuuza miili yao, kwa kweli niseme tu kwamba kama taarifa hiyo ikijulikana hatua za kisheria za nchi yetu zitachukuliwa. So far mimi sina data za aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Watanzania ambao wamepelekwa nje na kwamba figo zinachukuliwa pia hiyo tutaifuatilia ili kama kuna ukweli, basi hatua kali zitachukuliwa kwenye nchi husika.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, stadi zinaonesha lipo jaribio linalohusisha utolewaji ama utumiaji wa ARV kwa watu wasio kuwa na maambukizi ya VVU ama UKIMWI ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia maambukizi mapya endapo mtu huyu aliyetumia ARV pasipo kujamiana na mtu ambaye tayari ana maambuki ya VVU ama UKIMWI.
Ningependa kusikia kauli ya Serikali hali ipoje nchini Tanzania juu ya matumizi hayo ya ARV kwa mtu ambaye hana maambukizi ili kumzuia asiambukizwe endapo atajaamiana na mtu mwenye maambukizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kufuatia mikakati inayofanywa na Serikali ambayo mengi wameainisha kwenye majibu yao ningependa kujua jambo moja mahususi. Je, Serikali inashughulikiaje swala zima la ongezeko la watoro ambao tayari wako kwenye kujiunga na utumiaji wa matibabu ya HIV and AIDS? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, sayansi katika matibabu ya ugonjwa wa UKIMWI yameonesha kwamba mtu asiyekuwa na maambukizi ya UKIMWI anaweza akapatiwa dawa ambazo zinaweza kumsadia kumkinga dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa lugha ya kitaalamu inaitwa pre-exposure prophylaxis.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuweke msisitizo hadi hivi sasa hatuna tiba ya ugonjwa wa UKIMWI, tunachokifanya hichi ni dawa kinga, na sisi kama Tanzania tunalitambua hilo na tumeshaanza katika ngazi ya majaribio na lengo letu ni kwamba baada ya majaribio haya tuweze roll out nchi nzima na tunalenga makundi mahususi ambayo ni pamoja na wanaofanya biashara ya ukahaba, kwa wale ambao wanajidunga madawa ya kulevya na wale ambao wanajamiiana kwa jinsia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nisisitize kwamba kinga hii inaendana sambamba na kutumia njia nyingine za kujikinga na wala sio suluhu ya kutopata maambuzi ya UKIMWI, nilitaka niliweke msisitizo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana wale ambao wanaacha dawa.
Sasa hivi Serikali tumeanza mchakato wa kuwabaini na changamoto ambayo tumeiona ni kwamba siyo kwamba wengi wanaacha ni mtu amekuwa eneo moja anachukua dawa baada ya hapo anahamia katika nyingine na kule anaenda kujisajili kama mteja mpya na sisi tumekuwa hatuna kumbukumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa hivi tuna kitu ambacho tunachokifanya ni kuweka utaratibu wa kutumia mifumo wa biometric kwamba mtu akipata matibabu sehemu moja akienda tena sehemu nyingine atatambulika kama ni mtu ambaye tayari tunaye kwenye database na hili tunalifanyia kazi na hivi karibuni tutali-introduce. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa nitapenda nikuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi, chini ya Rais John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kabisa kutoa elimu bure kwa watoto wote; na kwa kuwa, wazazi wengi wa jamii ya kifugaji hawajajitokeza kuwaandikisha watoto wao badala yake wanaamua kuanzisha shule zao ama kufungua shule zao na kuwapeleka watoto wao. Napenda kujua sasa je, Serikali mna taarifa na uwepo wa shule hizi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini swali langu la pili, kama Serikali inafahamu uwepo wa hizo shule ni nini sasa mkakati wa kuhakikisha mnazisaidia shule hizo, ili ziweze kufanya vizuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilikuja na mpango wa elimu bure. Lengo ni kuhakikiksha kwamba kila mtoto wa Kitanzania anapata fursa ya kuendelezwa kwa mujibu wa sheria kupitia nyanja ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la msingi ambalo aliuliza kwamba, je, tuna ufahamu wa hizi shule bubu, ambazo naziita shule bubu;-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge kama ana taarifa ya hizi shule basi na sisi atujulishe kwa sababu shule zetu zote za msingi ni shule ambazo zinatambuliwa Kiserikali na zimesajiliwa na Serikali na zinapata ruzuku na sisi tunapeleka walimu. Kama kunakuwa na shule bubu napata shida kuelewa kwamba hizo shule zimesajiliwa wapi? Hao walimu wanawapata wapi na aina ya elimu ambayo wanaitoa ni elimu ya namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimuombe sana Mheshimiwa Mbunge kama ana taarifa ya hizi shule, basi atujulishe Serikali, ili tuweze kuzitambua. Na kama tukiona kwamba, zina mazingira ambayo na sisi kama Serikali tunaweza kuzichukua, basi tutaweka utaratibu wa kuzirasimisha rasmi.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mkoani Mwanza kuna eneo la wananchi limechukuliwa kwa ajili ya matumizi ya Ikulu ndogo ikiwemo na lile eneo lenye mradi wa UWT. Napenda kujua sasa ni lini Serikali itawafidia wananchi hao pamoja na taasisi ambazo maeneo yao yamechukuliwa ikizingatiwa wananchi hao wamesitisha shughuli za maendeleo kwa ajili ya kupisha zoezi hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili eneo la Bugosi, Kata ya Nyandoto, Wilayani Tarime, kuna eneo la wananchi limechukuliwa na Jeshi takribani miaka mitano ama zaidi. Napenda kujua sasa ni lini Serikali itawafidia wananchi hao ilhali tathmini ya eneo hilo tayari ilishafanyika? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mchafu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analitaja ingekuwa vizuri tukapata fursa ya kwanza kujua chanzo cha tatizo kwa kujiridhisha ili pande zote tujue nini kinatakiwa kifanyike ili haki iweze kutendeka. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba hakuna kipande cha ardhi cha mwananchi kitachukuliwa bila kupata fidia. Kwa hiyo, katika hilo eneo ambalo amelitaja ni vizuri tukajiridhisha hasa tatizo ni nini ili wananchi kama wanastahili fidia waweze kupata.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anaelezea eneo ambalo liko Tarime anasema kwamba eneo hilo limechukuliwa na Jeshi. Itakuwa ni ngumu sana unless kama tumejiridhisha kwa sababu Jeshi maeneo ambayo imekuwa ikitwaa ardhi kuna utaratibu ambao unawekwa juu ya fidia na fidia imekuwa ikitolewa. Katika hili ambalo ni jipya ni vizuri Mheshimiwa Mbunge akatoa fursa Serikali tukajiridhisha hasa nini ambacho kimetokea mpaka Jeshi ikaonekana limetwaa eneo hilo bila fidia. Maana inawezekana wananchi ndiyo wamelifuata Jeshi au Jeshi limekuja baada ya eneo la wananchi. Kwa hiyo, ni vizuri kutizama pande zote mbili ili kuweza kutoa majibu ambayo ni sahihi.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Barabara ya Vigwaza - Kwala - Kimaramasale inayounganisha Majimbo matatu ya Mkoa wa Pwani, Jimbo la Bagamoyo, Kibaha Vijiji na Kisarawe, ni lini itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ikizingatiwa kule kuna bandari kavu? Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nimshukuru Mheshimiwa Hawa Mchafu kwa swali lake.
Mheshimiwa Spika, niseme tu barabara hii inahudumiwa na TANROADS na katika ule mpango mkakati wetu tunao utaratibu wa kuitengeneza. Kwa sasa tunajitahidi kuhakikisha barabara hii inapitika wakati wote na kwa umuhimu wa kipekee kwa sababu ya kuwa na hii bandari kavu tutaipeleka kwenye kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge avumilie kidogo utaratibu upo wa kuifanya hii barabara iwe nzuri zaidi. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kinachoendelea kwa sasa katika Kituo cha Afya cha Mlandizi ni kuelemewa na lundo la wagonjwa, hususan upande wa afya ya uzazi. Ndani ya mwezi mmoja kuna wanawake zaidi ya 250 wanaojifungua. Idadi hii ni mara tatu ya walengwa wa Kituo hiko cha Afya cha Mlandizi, kitu ambacho kinapelekea kituo chetu kuwa na mahitaji makubwa ya matumizi ya dawa, vifaa tiba na huduma za kujifungua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, sasa napenda kujua, wakati huu ambao hatuna Hospitali ya Wilaya na Serikali haina mpango wa kujenga Hospitali hiyo ya Wilaya: Je, Serikali itakuwa tayari kutupatia fungu maalum la fedha kila mwaka kwa ajili ya huduma hii ya afya ya uzazi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kufuatia ongezeko hilo la wagonjwa kuwa mara tatu ya walengwa wa Kituo hicho cha Afya na kupelekea kituo chetu kuwa na deni kubwa takriban shilingi milioni 83 linalojumuisha matumizi ya dawa, vifaatiba, huduma ya uzazi na huduma nyingine, nangependa kujua, sasa Serikali itatusaidiaje ku-clear deni hilo, ukizingatia idadi hiyo ya fedha au kiasi hicho cha fedha ni mara mbili, tatu, nne mpaka tano ya mapato yote ya Kituo cha Afya cha Mlandizi? (Makofi) Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE): Mheshimiwa nakushukuru. Katika jibu langu la msingi, nimesema kwamba Serikali imeona uhitaji wa kujenga Hospitali ya Wilaya na tayari katika bajeti ya 2018/2019 tumetenga shilingi bilioni 1.5, ni kwa sababu tunatambua umuhimu na uhitaji mkubwa sana wa wananchi kwa suala zima la Afya. Kwa hiyo, tuko tayari na ndiyo maana tunajua kabisa kuna kuelemewa ndiyo maana tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anauliza, tunafanyaje katika kuwasaidia deni la jumla kama shilingi milioni 80? Ni vizuri kwanza tukajua chimbuko la deni hili nini na tukikaa baada ya kipindi cha maswali na majibu, tujue tatizo ni nini ili tuweze kusaidiana ili wananchi waendelee kupata huduma, lakini wakiwa wamevuta subira, Serikali yao ya CCM inawajali na ndiyo maana tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hangamoto ya umeme iliyopo manispaa ya Tabora inafanana kabisa na ile ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga katika Kata ya Tambani, Mwandege na vijiji vyake. Je, ni lini sasa umeme utawaka kwenye Kata hizi ikizingatiwa mradi wa REA I na REA II tayari ulishapita? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nikiri kwa kweli kwa Mbunge wa Mkuranga, Mheshimiwa Ulega pamoja na Mheshimiwa Mchafu wamekuwa wakifuatilia sana masuala ya nishati ya umeme katika Wilaya ya Mkuranga. Na ninaomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, mkandarasi wa Mkoa wa Pwani Sengerema tumezungumza naye na Jumapili hii atapeleka nguzo kwa ajili ya maeneo hayo ya Tambani, Mwandege ambapo pana ongezeko kubwa la wananchi na hususani Kijiji cha Mlamleni katika Wilaya ya Mkuranga. Nataka nimthibitishie kazi kuanzia Jumamosi hii nguzo zitafika na itaendelea katika Mradi huu wa REA Awamu ya Tatu. Ahsante sana.
MHE. HAWA MCHAFU CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri sasa ningependa nimuulize maswali wadogo wawili yangongeza. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuikabidhi miradi ya serikali kwa DAWASA ikiwemo mradi wa Bokomnemela Vikuruti na Ngeta.

(i) Ni lini sasa DAWASA itakamilisha zoezi la ufangaji maji majumbani ikizingatiwa wananchi wanauhitaji mkubwa wa maji na hivi tunavyozungumza ni nyumba 30 tu zilizofungwa kati ya wananchi wote walojaza fomu?

(ii) Nataka kujua ni kwanini DAWASA wanafanya ucheleweshaji wa kijiji cha kipangege Kata Soga. Kijiji hakipati maji ya kuridhisha presha yake ni ndogo na wakati mwingine hakuna kabisa maji nataka kusikia kauli ya Serikali inasema nini juu ya uchelewashi huu unaofanywa na DAWASA?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma ni miongoni mwa Wabunge makini katika ufuatiliaji na kupigania maendeleo ya watu wake katika Mkoa wa Pwani. Lakini kikubwa maji hanaya mbadala sasa niagize Mkurugenzi wa Mamlaka wa Majisafi na Usafi wa Mazingira DAWASA Eng. Luhemeja katika kuhakikisha suala la ufungaji mita kwa wananchi lakini pia mradi huu wa Soga uwezi kukamilika kwa wakati ahsante sana.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza; kabla sijauliza swali niruhusu nimshukuru Mheshimiwa Spika na Wabunge kwa ujumla kwa namna ya kipekee walivyonifariji mara baada ya kumpoteza mama yangu duniani, nawashukuru sana Waheshimiwa, nakushukuru sana Mheshimiwa Spika kwa faraja yako. Swali langu ninalopenda kumuuliza Naibu Waziri changamoto ya mawasiliano ilipo kwenye visiwa vidogo vya Tumbatu inafafana kabisa na visiwa vya delta Wilayani Kibiti.

Je, ni upi mpango wa Serikali kuhakikisha wananchi wa delta Kibiti wanawasiliana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli changamoto ta mawasiliano katika visiwa vya delta inafahamika na kwa kule tumeunda kikosi maalum kwa ajili ya kwenda kutembela maeneo yote ya visiwa vidogo vidogo ambavyo havina huduma ya umeme, pia kufika kwake kuna changamoto. Tumeunda kikosi maalum kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, lakini kwa kushirikiana na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote kwenda kutembelea maeneo hayo kwa ajili ya kuangalia namna nzuri ya kufikisha umeme, kwa sababu tumegundua kwamba ukifikisha mawasiliano kama hakuna umeme kunakuwa na changamoto kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunapelekaga kule solar ambazo sio za kufanya kazi muda mrefu. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya tathimini ya kina ya kiufundi kuhakikisha kwamba sehemu hizo zinakuwa na huduma nzuri ya mawasiliano. Nikuhakikishie kwamba mwezi wa kwanza mwaka huu sehemu mbalimbali za visiwa na sehemu maalm za Kanda ambazo ni za mipakani zote zitashugulikiwa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata mawasiliano.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Kanuni za Utumishi wa Umma hazikuainisha waziwazi mtumishi mwanamke anayezaa watoto zaidi ya wawili ama mtoto njiti anaongezewaje siku; na kwa kuwa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini imetoa fursa ya kuingia mikataba ya hali bora mahali pa kazi, je, Serikali haioni umefika sasa wakati kwa kutumia hii fursa ya kutengeneza ama ya kuingia mikataba ya hali bora ya kazi kwa watumishi wanawake wanaopata watoto zaidi ya wawili ama kwa mwanamke anayezaa mtoto njiti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa mdogo wangu Mheshimiwa Hawa Mchafu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wakati najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Anatropia nimesema kwamba Serikali inatambua na inajali wanawake wote ambao wanajifungua watoto zaidi ya wawili na ndiyo maana kama Serikali tumeweza kuongezea zile siku 14 ili kwa pamoja ziweze kuwa siku 98 kwa sababu likizo ya uzazi ni siku 84. Kwa maana hiyo wale wote wanaojifungua watoto njiti au watoto zaidi ya wawili tumewaongezea siku 14. Hii iko kisheria ili kuthibitisha na kuhakikisha kwamba huyu mama mzazi anastahili kupewa haki yake.

Mheshimiwa Spika, hili jambo naomba niwaambie Wabunge wote kwamba liko kisheria na tumeongeza hizo siku 14 zaidi kwa ajili ya akina mama wote wanaojifungua mtoto zaidi ya mmoja. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, mgao wa fedha wa kununulia dawa kwa mwaka huu wa fedha zimeenda mara moja tu katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu na isitoshe fedha hizo zinakatwa juu kwa kwa juu kwenda kulipia deni sugu lililopo Bohari ya Dawa. Swali langu kwa Serikali, je, Serikali inamkakati gani kuhakikisha deni linalipwa na dawa zinapatikana katika zahanati na vituo vyetu vya afya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka kujua Serikali inampango gani kuhakikisha kwamba mgao wa fedha wa kununulia dawa haukatwi juu kwa juu kwenda kulipia deni hilo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO:-Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Mheshimiwa Waziri amesimama, Mheshimiwa Waziri, sijui mlivyokubaliana lakini tuanze na lile la kwanza.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, yes.

SPIKA: Aliuliza kwa nini dawa za shinikizo la damu hazitolewi katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya na wewe umejibu vizuri kwamba sasa hivi hata watu wenye Shahada za Udaktari sasa wanapangwa kwenye vituo vya afya, kwa hiyo mmekubali kwamba sasa dawa za shinikizo la damu zitatolewa katika vituo vya afya au bado hamjakubali?

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, msisitizo uliowekwa nikwamba dawa za shinikizo la damu zinatolewa kulingana na zinavyofanya kazi, lakini na athari zake. Kwa sababu kuna dawa ambazo zinaenda kugusa moyo moja kwa moja na kuna dawa ambazo hazigusi moyo. Sasa utoaji wake unazingatia utaalam na uwezo wa wataalam wenyewe. Kwa hiyo, wakati tunaamuliwa ndiyo maana sasa utaona wakati kunadawa sasa hivi mpaka sasa zinatolewa kwenye zahanati, vituo vya afya, lakini inakwenda mpaka kufika rufaa.

Mheshimiwa Spika, kuna dawa zingine haziwezi kutolewa huko kulingana na utaalam ulioko katika sehemu husika. Kwa hiyo, sasa tunakwenda kuboresha kushuka chini kuhakikisha sasa wataalam ambao walikuwa wanapatikana tu katika hospitali za wilaya na za mikoa wanaanza kushuka chini sasa kuwepo kwenye maeneo hayo. Pia kuna mwongozo mpya ambao umetengenezwa ambao utaenda sasa kusaidia hizo dawa ziweze kupatikana kila mahali, ndicho ambacho tulimaanisha.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la nyongeza, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Hawa Mchafu kwa sababu katika meseji nyingi ambazo nimekuwa nikirushiwa na Waziri na ambazo nilikuwa nazipata, tumepata meseji zake sana zinazokwenda kwenye service delivery. Bado narudi pale pale kwamba tunahitaji, ukiangalia nilieleza na nikasema kwamba umeona nimetoa mfano wa hospitali, nitoe Hospitali ya Katavi, tumekwenda Hospitali ya Katavi nao wamepewa dawa zenye thamani ya milioni 41, lakini wakauza hizo dawa pamoja na kuhudumia akinamama na watoto wakapata milioni 112, mwisho wa siku wakaenda kununua dawa za milioni…

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri swali alilouliza Mheshimiwa Hawa Mchafu kama la nyongeza ni national problem.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Yes.

SPIKA: Hela zinakatwa juu kwa juu…

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, sawa, nakuja hapo. Kwa hiyo ukiangalia dawa za milioni 22 maana yake amenunua chini ya pesa aliyopata MSD, kwa maana hiyo ni kwamba utakuta utekelezaji kule chini kuna uwezekano wa hospitali zetu kuuza dawa na kupata pesa ya kutosha kupeleka kule na kuweza kuhudumia wananchi. Sasa…
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri hujamsikia swali lake naomba ukae ulisikie tena swali lake. Mheshimiwa Hawa Mchafu nakupa nafasi uulize tena swali lako. Ngoja aulize tena swali ili wamsikie,issue siyo majibu,issue ni kumjibu swali ambalo mtu ameuliza. (Makofi)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa hii nafasi tena. Mheshimiwa Waziri mgao wa fedha wa kununulia madawa kwa mwaka huu wa bajeti tuliokuwa nao, umeenda mara moja tu kwenye vituo vyetu vya afya na zahanati zetu na isitoshe fedha hizo zinakatwa juu kwa juu kwenda kulipa deni sugu lililopo Bohari ya Madawa.Nataka kujua sasa mkakati wa Serikali juu wa ulipaji wa deni lililopo MSD na dawa ziendelee kuwepo katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu.

Mheshimiwa Spika, la pili, wanampango gani kuhakikisha mgao wa fedha unaopangwa kwenda kununulia madawa haukatwi juu kwa juu kwenda kulipia deni?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kusimama kwenye Bunge lako tukufu kujibu swali naomba kwanza nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kuifanya siku ya leo iwepo katika ramani ya mipango yake.

Mheshimiwa Spika, pili naomba kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kuona kwamba natosha kuwa sehemu ya chombo hiki tukufu cha kuleta maendeleo katika nchi yetu. Tatu naomba nimshukuru sana familia hususani mume wangu Advocate, wakili msomi Metusela Gwajima Mpenzi wangu sana pamoja na watoto wetu…(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, sasa majibu ya maswali ya nyongeza.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Evelyn, Mary Mkubwa, Mary Mdogo na Victoria Gwajima.

Sasa Mheshimiwa Naomba nijielekeze kwenye swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu kuhusu dawa.

Mheshimiwa Spika, kweli dawa katika kipindi cha mwaka huu wa fedha zimekwenda mara moja, lakini katika mfumo huu wa sekta ya afya tunapopeleka dawa kutoka MSD, sheria ni cash na carry kwamba ulipe ndiyo upewe hizo dawa, kwa kipindi kirefu vituo vyetu vimekuwa havitekelezi vizuri usimamizi wa cost sharing ile user fees pamoja na bima ili zirejeshe zile pesa huko. Hata hivyo, Serikali imeendelea kupeleka hizi dawa kule kwao, baada ya kuona kwamba wana madeni tukaweka utaratibu kwamba wao sasa wanaruhusiwa kwenda pale MSD wakasaini contract kwamba hizi pesa zisikatwe kwanza tupeleke kule tukafanye ule mzunguko turejeshe. Wengine wamefanya hivyo wanapelekewa hizo dawa kwa utaratibu huo wa makubaliano watalipaje deni, wengine hawafanyi hivyo. Kwa hiyo, nimelipokea, nimelichukua naomba nikawasiliane huko kwenye halmashauri tukaone tatizo liko wapi wa kutekeleza hiyo offer.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la nyongeza la kwamba tutaendeleaje kuhakikisha kwamba pesa zinaenda na Serikali inaendelea kulipa hilo deni. Serikali inampango na mipango yake ni mipana kuimarisha makusanyo ambayo yamekuwa yakivuja sana kule kwenye hivi vituo, lakini pia kufuatilia matumizi ya zile bidhaa tunazopeleka kule. Hivi sasa ninavyosema kuna timu zetu ziko kule zinafanya ukaguzi. Kwa hiyo, msingi mkubwa hapa ni kwamba tunavitaka vituo viende MSD viingie makubaliano lile deni halitakatwa kiasi cha kuwanyima zile bidhaa zao, watachukua bidhaa tutaendelea kuimarisha ili nao watekeleze sheria ya cash and carry.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninalo ninakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ningependa kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwa kuwa, Serikali inayafahamu kwa kuyataja kabisa madhara yanayotokana na kemikali ya zebaki lakini pia kwa kuwa, kutumia njia hii kuchenjulia dhahabu tunapata asilimia kidogo tu kama ambazo ametaja asilimia 30, ni kwanini sasa Serikali isitumie cyanide kuchenjulia madini hayo ya zebaki na kuachana na kemikali hatari ya zebaki? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, kibali cha ku-import kemikali ya zebaki nchini kinatolewa na Mkemia Mkuu wa Serikali. Wataalam kutoka Wizarani wanatuambia kwamba Mkemia Mkuu wa Serikali hakupokea maombi ya ku-import zebaki nchini. Cha ajabu ni kwamba, kemikali hiyo ipo ya kutosha tu huko mtaani, sasa ni nini kauli ya Serikali juu ya njia hizi za panya zinazoingiza kemikali hii kiholela? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, cyanide pamoja na baadhi ya acids ndio njia sahihi ambayo inafaa kwa ajili ya uchenjuaji dhahabu kwa sasa na ndio teknolojia ambayo aaah! Kama Mheshimiwa Mchafu atakumbuka kwamba, ndio teknolojia mpya ambayo imetumika na ndio imeleta hasa manufaa kwa wachimbaji wadogo. Sema, kwa kutumia cyanide pamoja na vat leaching inakuwa inahitaji kidogo mtaji uwe mkubwa ili mchimbaji mdogo aweze kuitumia. Sasa kitendo cha kuhitaji mtaji mkubwa kidogo ndicho kinachofanya wengine bado wanaendelea kutumia mercury.

Mheshimiwa Spika, lakini ni kweli kwamba, wengi wameshaanza kuhama na ndio msisitizo wa Wizara tunawasisitiza watoke kule kwasababu ya madhara ambayo yanaonekana. Nikweli kwamba, kwa kutumia vat leaching ambayo inatumia cyanide ni kwamba, hata recovery inakuwa ni kubwa na kwa hiyo tumuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kama Wizara tutaendelea kufanya jitihada za kutoa elimu. Kwanza, wachimbaji wadogo wajue madhara makubwa yanayotokana na kutumia mercury, lakini pia ikiwezekana hata kama ni kujiunga kwa vikundi waende katika teknolojia ambayo inafanya recovery kubwa lakini pia haina madhara makubwa.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kweli kwamba mercury inapatikana kwa wachimbaji wadogo wakiitumia na kwasababu, kibali kilipaswa kutoka kwa Mkemia Mkuu kama ambavyo anatoa kuhusu kemikali zingine zozote zile. Lakini Mheshimiwa Mbunge anathibitisha kwamba sio kweli kwamba yeye ametoa vibali. Tulichukue kama Serikali kwasababu tunatamani kulinda mazingira yetu, tunatamani kuwalinda wachimbaji wetu ili tuingie katika mnyororo na ikiwezekana badala ya kutoa elimu kwenye matumizi, basi twende pia kuangalia hata source ya mahali ambapo zebaki inaingilia. Nadhani kwa jinsi hiyo tutaweza kuwasaidia maana yake ni kwamba tuanze udhibiti tangu kwenye source kuliko kule kwenye matumizi yenyewe kwa kujali afya na mazingira yetu. Ahsante (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kuniona hali ya barabara ya Lumecha kilosa inafanana kabisa na ile ya Bungwi Nyamisati je, ni lini sasa Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami ikizingatiwa ni muhimu kwa wananchi wa Mafia, Mkuranga na Kibiti yenyewe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri barabara ya Bungwi Nyamisati nimefika na tukiwa tumeongozana na Mheshimiwa Mbunge Mpembenwe naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba hii ni barabara ambayo ni ahadi ya viongozi wa Kitaifa lakini pia ipo kwenye Ilani ambayo inaunganisha wananchi wa Mafia na wanaokuja bara, kwa hiyo ipo kwenye mpango, fedha itakapopatikana barabara hii itajengwa ili kuifanya wananchi waweze kupata huduma bora ya barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, hali iliyopo Halmashauri ya Mji wa Mbulu ya ukosefu wa walimu wa sayansi inafanana kabisa na hali ya Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kuwa na uhaba wa walimu wa sayansi.

Je, ni lini sasa Serikali itatupatia walimu hawa wa sayansi ili kuweza kukidhi mahitaji? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Naibu Waziri Mheshimiwa Silinde kwa majibu mazuri, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Hawa Mchafu kutaka kujua ni lini Serikali itapeleka walimu wa sayansi katika shule za sekondari za Mkoa wa Pwani.

Mheshimiwa Spika, kama ulivyosema, tunakiri tunayo changamoto ya uhaba wa walimu wa sayansi na uchambuzi ambao tumeufanya ndani ya miezi mitatu kuna shule takribani 1,000 za sekondari wanafunzi wetu hawajawahi kukutana na mwalimu wa physics face to face, lakini tuna shule takribani 400 watoto wetu wa sekondari hawajawahi kumuona mwalimu wa hesabu akiingia darasani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tatizo hili tumeliona na tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutupa kibali cha kuajiri walimu katika mwaka huu wa fedha wa 2020/2021. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge tunakamilisha uchambuzi wa maombi ya walimu ambao wameomba nafasi hizi za ajira tulizozitoa na kipaumbele kama tulivyosema ni kutatua changamoto hii ya walimu wa sayansi hususan pia katika masomo ya hesabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongeze, sambamba na kuendelea kuomba kibali cha ajira kutoka kwa wenzetu Ofisi ya Rais - Utumishi tumeona ipo fursa ya kutumia maendeleo ya Information Communication and Technology (ICT) ili pia kuwawezesha wanafunzi wetu kupata masomo au walimu wa sayansi na hesabu kupitia mtandao.

Kwa hiyo, hili ni jambo ambalo tumeliona, tutaweka walimu wazuri watarekodi mada zote muhimu halafu wanafunzi wetu watakuwa pia wanaweza kusoma masomo ya sayansi kwa kutumia njia ya mtandano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wapo wafanyabiashara ambao hawalipi ushuru, wamejitoa kwenye kodi na leseni kwa kisingizio cha kukosekana kanuni za vitambulisho vya mjasiriamali.

Ni nini kauli ya Serikali juu ya upotevu wa mapato unaosababishwa na wafanyabiashara hawa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa namna hali ilivyo huko site, vitambulisho hivi inaonekana kama ni hiyari, zoezi lake ni gumu na kwa wale wanaovikataa hakuna hatua yoyote ya kuwachukulia kikanuni.

Sasa ni lini Serikali itatoa kanuni hizo za vitambulisho vya mjasiriamali ili kuondoa mkanganyiko huo na kuweka bayana masharti na utaratibu wa vitambulisho hivyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza niseme kimsingi vitambulisho hivi vilitolewa kwa nia njema ya kuhakikisha wajasiriamali na
wafanyabiashara wadogo wanafanyabiashara kwa utulivu kwa kuwa na kitambulisho kinachowawezesha kutoa huduma zao za biashara bila kulipa gharama nyingine kama ilivyokuwa siku za kule nyuma.

Kwa hiyo, kanuni zimetolewa wazi kwamba kwanza ni mfanyabiashara mdogo, mwenye mzunguko wa biashara usiozidi shilingi milioni nne kwa mwaka lakini mfanyabiashara ambaye kimsingi anapatikana katika eneo husika linalofanyabiashara, lakini anaweza kufanya biashara sehemu nyingine; lakini kanuni nyingine ni kwamba kinatumika kwa miezi 12 tangu tarehe ile ya kukatwa kitambulisho kile.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawalipii vitambulisho hivi, maana yake watakuwa tayari kulipa gharama zilizopo kisheria za kufanya biashara kwa maana ya ushuru mbalimbali na gharama zingine. Kwa hiyo, tunaendelea kuwaelimisha na walio wengi kwa kweli wanaona hii ni njia bora zaidi kwa sababu wanapata nafuu ya kulipa ushuru kila siku kwa kulipa kitambulisho kwa mwaka mmoja.

Mheshimiwa Spika, pili, vitambulisho hivi ni vya hiyari, lakini elimu inaendelea kutolewa ili walio wengi waweze kuona umuhimu wake na kuvitumia, ahsante.