Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hawa Mchafu Chakoma (19 total)

MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 inalenga kuwapunguzia wafanyakazi kodi ya mapato (PAYE) kutoka asilimia 11 hadi kufikia tarakimu moja.
Je, Serikali imejipangaje kutekeleza jambo hilo muhimu kwa ustawi wa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kodi ya wafanyakazi uliopo sasa una viwango vya kodi kwa kuzingatia kipato cha mfanyakazi ambapo kiwango cha kodi hupanda kadri ya kipato cha mfanyakazi kinavyopanda. Kwa sasa, kima cha chini kisichotozwa kodi ya mfanyakazi ni kipato cha mshahara kisichozidi shilingi 170,000/=. Watumishi Waandamizi wanalipa kodi kubwa kutokana na mishahara yao mikubwa na kwa asilimia kubwa zaidi ya wale watumishi wa hali ya chini.
Mheshimiwa Spika, watumishi wa ngazi za chini wataendelea kuboreshewa maslahi yao kwa kupunguza kiwango cha chini cha kodi. Kiwango cha chini cha kodi kinachotozwa kwenye kipato cha zaidi ya shilingi 170,000/= ni asilimia 11; na cha juu zaidi ni asilimia 30. Serikali imekuwa ikishusha kiwango cha chini cha kuanzia kutoza kodi kwa mfanyakazi hatua kwa hatua, kutoka asilimia 18.5 mwaka 2006/2007, asilimia 15 mwaka 2008/2009 na kufikia asilimia 14 mwaka 2010/2011. Mwaka 2012/2013 tumefikia asilimia 13; asilimia 12 kwa mwaka 2013/2014 na sasa kufikia kiwango cha asilimia 11. Lengo la kuendelea kushusha kiwango hiki ni kufikia kiwango cha asilimia 10 kwa mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufikia kiwango hicho cha asilimia 10 Serikali itaendelea kujadiliana na Vyama vya Wafanyakazi kwa lengo la kupunguza kodi hii ya Pay As You Earn (PAYE) hadi kufikia tarakimu moja kutegemea na hali ya uchumi itakavyokuwa inaimarika mwaka hadi mwaka.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 imelenga kuanzisha Mfuko Mkubwa kwa ajili ya kutoa mkopo kwa wafanyakazi na wajasiriamali wadogo kwa masharti nafuu.
Je, Serikali imefikia hatua gani katika utekelezaji wa jambo hilo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nianze kwa kunukuu Ibara ya 57(e)(v) ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, inayosema; “Kuanzia Mfuko Mkubwa wa Kitaifa wa wajasiriamali wadogo na wakati kwa kushirikiana na Mifuko ya Jamii na Asasi nyingine za Kifedha. Hivyo ibara hiyo iliyorejewa imewalenga wajasiriamali wote bila kujali kama ni wafanyakazi au si wafanyakazi.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutekeleza maelekezo ya Chama Tawala, chini ya Ibara ya 57(e)(v) Ilani ya Uchaguzi itawajengea wananchi uwezo wa kuanzisha, kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi ili waweze kushiriki kikamilifu katika kuendesha uchumi wa Tanzania. Serikali inategemea kuanza mazungumzo na wadau wa Mifuko ya Kijamii pamoja na asasi nyingine za kifedha mwezi Februari mwaka huu ili kujadili namna bora ya kuanzisha na kuendesha Mfuko huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inatarajiwa taratibu za kuanzisha Mfuko huo zitakamilika katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kuweza kuanza kwa Mfuko huo katika mwaka wa fedha 2017/2018, baada ya Serikali kutenga fedha za kutosha.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Utekelezaji wa maagizo ya Serikali Kuu kwa Halmashauri imekuwa ni changamoto na mzigo mkubwa kwa Halmashauri hizo hususan Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambapo maagizo mengi hayamo kwenye Mpango wa Bajeti na hivyo utekelezaji unakuwa mgumu.
Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha maagizo hayo yanatengewa bajeti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa kwa nyakati tofauti Serikali imekuwa ikitoa maagizo ya kiutendaji katika Halmashauri zetu nchini na si kwa Halmashauri ya Kibaha pekee ikiwa na lengo la kuhakikisha kuwa inatatua changamoto ambazo Halmashauri zinaikabili kwa kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya maagizo hayo ya hutolewa na Serikali huhitaji fedha. Maagizo hayo huingizwa kwenye mipango na bajeti ya Halmashauri yanapotolewa kabla ya bajeti kupitishwa, hata hivyo baadhi ya maagizo na maelekezo hutolewa na Serikali katikati ya mwaka wa bajeti, maagizo na maelekezo ya Serikali ambayo hukosa kabisa fedha katika mwaka husika huingizwa katika bajeti za Halmashauri ya mwaka wa fedha unaofuata kwa ajili ya utekelezaji au Halmashauri hufuata utaratibu wa kurekebisha bajeti.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuzihimiza Halmashauri zote nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuendelea kutenga fedha katika mpango na bajeti yao ili ziweze kutatua changamoto zinazowakabili.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Moja ya tatizo kubwa nchini ni ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali imeweka vipaumbele vya kuanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuajiri vijana wengi wa Kitanzania:-
Je, Serikali ina mikakati ipi kuhakikisha azma hiyo njema inafikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ukuzaji ajira ni mtambuka na linahitaji juhudi za wadau mbalimbali katika kukabiliana nalo. Serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) imekuwa mstari wa mbele kuendeleza sekta ya viwanda vidogo vidogo nchini ili kuajiri na kujiajiri kwa vijana wengi. Shirika hili limekuwa likikuza utaalam katika sekta mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga yafuatayo kuhakikisha viwanda vidogo vidogo vinatoa ajira kwa vijana:-
(i) Kuanzisha na kukuza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuwaajiri vijana wengi kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Mpango huu utawezesha uanzishwaji wa viwanda vidogo kama vile viwanda vya kuunganisha vifaa na bidhaa za teknolojia ya habari na mawasiliano na vya kielektroniki, viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo, viwanda vya kuongeza thamani ya madini na viwanda vya kutengeneza bidhaa za ujenzi.
(ii) Kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi katika sekta za kipaumbele ambazo ni chachu ya ukuaji wa uchumi na ajira. Sekta hizo ni kilimo na biashara, nishati, utalii na huduma za ukarimu, usafiri na usafirishaji, huduma za ujenzi na TEHAMA.
(iii) Kuimarisha Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo linadhamini wahitimu wachanga kupata mikopo nafuu katika benki kwa njia ya ushindani ili waweze kufanya shughuli za kujiajiri ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo na makampuni.
MHE. HAWA M. CHAKOMA, aliuliza:-
Tarehe 25 Oktoba, 2016 Kituo cha Televisheni cha Mlimani TV kilirusha Kipindi cha Urithi Wetu kilichozungumzia Malikale za Taifa letu na namna ambavyo agizo la Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete la ufunguzi wa nyayo za Laetoli linavyosuasua kutekelezwa kwa kisingizo cha ukosefu wa wataalam.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuajiri wataalam hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nyayo za Laetoli zilizogunduliwa na mtafiti Dkt. Mary Leakey mwaka 1978 katika eneo la Laetoli katika Hifadhi ya Ngorongoro ni ushahidi wa pekee duniani usiopingika kwamba binadamu wa umri wa miaka milioni 3.6 iliyopita waliweza kutembea wima kwa miguu miwili katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2007 aliagiza Wizara yangu kufukua nyayo hizo na kuzihifadhi kwa njia ya kisasa itakayoruhusu matumizi ya elimu na utalii kwa Watanzania na wageni na kwamba Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro igharamie kazi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unakadiriwa kugharimu takribani Dola za Marekani milioni 50 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 105. Fedha hizo zitatumika kuwasomesha wataalam, kuandaa michoro ya ujenzi wa makumbusho, kufukua na kuhifadhi nyayo, kusimamia ujenzi na kuweka mifumo ya uhifadhi. Fedha hizo ni nyingi ukilinganisha na mapato na majukumu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Hivyo Wizara yangu inaendelea na jitihada za kutafuta vyanzo vingine vya fedha ili kugharamia utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kwamba hakuna hali ya kusuasua katika katika utekelezaji wa mradi huu muhimu na kwamba baadhi ya kazi zimekwishakamilika na nyingine ziko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zilizokamilika ni pamoja na kuundwa kwa Idara ya Urithi wa Utamaduni, kukamilika kwa michoro ya awali ya jengo la mapokezi, jengo la utafiti na jengo la elimu kwa umma, kuwasilishwa kwa tathmini ya athari kwa mazingira kwa mamlaka husika ikiwa ni pamoja na UNESCO kwa uchambuzi wa kina kwa lengo la kutoa idhini na mafunzo ya shahada ya uzamivu kwa watumishi wawili.
Kazi ambazo zinaendelea kutekelezwa ni pamoja na kukamilisha taratibu za ajira kwa baadhi ya wataalam wanaopatikana nchini na ukusanyaji wa takwimu sahihi kuhusu mazingira rafiki ya nyayo hizo kazi ambayo inafanywa na wataalam kutoka nje ya nchi na inatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2017 na kwa maana hiyo, napenda kusema kwamba kazi hii imekwishakamilika kwa sababu tulikuwa tumepanga ikamilike mwezi huu, mwaka 2017.
MHE. DKT. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. HAWA
M. CHAKOMA) Aliuliza:-
Je, kwa nini Serikali haitumii mfumo wa Ubia na Sekta Binafsi (PPP) kwenye mipango yake ya ununuzi wa vifaa tiba vya bei kubwa kama MRI, CT-Scan na X-Ray?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kukua kwa kasi ya sayansi na teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa, Wizara inakubaliana kabisa na wazo la Mheshimiwa Mbunge juu ya kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na Sekta Binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara imeanza hatua za awali za uainishaji wa gharama, uandaaji wa mfumo mbadala (Option Development) na upembuzi wa kina wa aina ya ubia ambapo Wizara kwa kuanzia inafikiria ushirikiano kwa kupitia ukodishaji wa vifaa (lease agreement) ambapo Serikali itakodisha mashine hizo ambazo zitakuwa za mbia na Serikali haitahusika na ununuzi, ufungaji na matengenezo kinga ya mashine hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mfumo huu, Wizara itakuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma na itapata gawio lake kutokana na makusanyo yatokanayo na uchangiaji wa huduma kulingana na mkataba. Ni imani ya Wizara kuwa kutumia mfumo wa Ubia na Sekta Binafsi (PPP) huduma za uchunguzi wa
magonjwa zitaimarika na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama.
MHE. MBARAKA K. DAU (K.n.y- MHE. HAWA M. CHAKOMA) aliuliza:-
Kisiwa cha Mafia kina vivutio vingi vya utalii kama viumbe wanaoishi kwenye maji, mikoko na kadhalika lakini vivutio hivyo havijatangazwa vya kutosha:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza utalii wa Kisiwa cha Mafia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Chakoma Mchafu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sasa Wizara kupitia Bodi ya Utalii, Shirika la Hifadhi za Taifa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikielekeza juhudi zaidi katika kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia tovuti, mitandao ya kijamii, Ofisi za Ubalozi, kuteua Mabalozi wa hiari kwa ajili ya kuitangaza Tanzania, kutumia Watanzania waishio nchi za nje yaani (diaspora), kuendesha mafunzo ya utalii kwa njia ya mtandao kwa mawakala wa utalii na kuandaa majarida, vipeperushi, CDs na DVDs.
Mheshimiwa Spika, aidha, jitihada zaidi zimewekwa katika matangazo kupitia redio, magazeti, runinga, mabango kwenye maeneo ya mipaka na vituo vya mabasi, kudhamini matukio mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, kuwa na wawakilishi wa kutangaza utalii kwenye masoko ya utalii pamoja na kutumia watu mashuhuri.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kuboresha utangazaji wa vivutio vya utalii Wizara imeanzisha mkakati wa kutangaza kwa pamoja kati ya Bodi ya Utalii na Taasisi nyingine ikishirikisha Sekta Binafsi. Mkakati huo umeonekana kuwa na tija na unasaidia kutangaza vivutio vya utalii nchini ikiwemo Kisiwa cha Mafia na hivyo kuitangaza Tanzania kwa ujumla na kwa gharama nafuu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kutangaza Kisiwa cha Mafia pamoja na matangazo yaliyoainishwa hapo juu, Bodi ya Utalii iliingia mkataba na kampuni ya kutengeneza filamu nchini ijulikanayo kama Aerial Tanzania kutengeneza filamu maalum ya Kisiwa cha Mafia ambayo ilizinduliwa mwezi Machi, 2017. Filamu hii itachangia kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaotembelea Kisiwa cha Mafia sambamba na kuongezeka kwa shughuli mbalimbali za utalii katika kisiwa hicho.
Mheshimiwa Spika, utangazaji wa vivutio vya utalii Kisiwani Mafia unaojumuisha viumbe vinavyoishi majini kama Papa Potwe na aina nyingine za samaki adimu wa aina mbalimbali ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, ule wa mwaka wa 2016/2017 - 2020/2021 unaosisitiza juu ya utangazaji wa vivutio na uibuaji wa vivutio vipya vya utalii katika maeneo mbalimbali nchini.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete, aliahidi kupandishwa hadhi Kituo cha Afya Kibiti kuwa Hospitali ya Wilaya:-
Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Wilaya ni Kituo kinachotoa huduma za afya ndani ya wilaya na ambacho hupokea wagonjwa kutoka zahanati na vituo vya afya ili kuwapatia huduma ambazo hazipatikani kutokana na uwezo mdogo uliopo katika vituo vidogo, yaani zahanati na vituo vya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutekeleza maagizo ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, kwamba Kituo cha Afya Kibiti kipandishwe hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, Wizara ilituma wataalam wake kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani ambao walifanya ukaguzi mnamo tarehe 13 – 16 Novemba, 2015 na kuwasilisha taarifa kwetu iliyotoa ushauri na maelezo pamoja na maelekezo ya kufanyiwa kazi ili kukiwezesha Kituo cha Afya Kibiti kumudu vema majukumu yake ya kutoa huduma katika ngazi ya hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla taarifa ilionesha kuwa, mazingira ya kituo yalihitaji maboresho kadhaa ili kituo hiki kifikie uwezo wa kutoa huduma za hospitali ya wilaya. Wizara inajiandaa kwenda kufanya ufuatiliaji ifikapo Oktoba, 2017 endapo itahakikishiwa kuwa upungufu uliobainishwa na ukaguzi ule utakuwa umefanyiwa kazi ili kituo hicho sasa kiweze kutangazwa rasmi kuwa Hospitali ya Wilaya.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Kwa muda mrefu chanzo cha maji cha Ruvu Chini na Ruvu Juu kimekuwa chanzo pekee cha maji katika Mkoa wa Pwani. Lakini kimsingi chanzo hicho hakitoshelezi mahitaji na hivyo kushindwa kumaliza tatizo la maji.
Je, ni lini Serikali itatumia chanzo cha maji cha Mto Rufiji kuwapatia maji safi na salama wananchi hususan wa Wilaya ya Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Kisarawe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa Niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Kuanzia mwaka 2005 hadi 2007 Serikali ilifanya uchunguzi wa vyanzo 26 vya maji kwa ajili ya matumizi ya Jiji la Dar es Salaam na Miji ya Kibaha na Bagamoyo kwa miaka 2025 hadi 2032. Uchunguzi huo ulibaini kuwa wakati ule vyanzo vya maji vya mto Ruvu na visima vya Kimbiji na Mpera vilikuwa vinatosha kwa matumizi ya Jiji la Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani hadi mwaka 2032. Chanzo cha maji cha Mto Rufiji hakikuchaguliwa wakati huo kwa sababu ilionekana gharama za kusafisha na kusafirisha maji kutoka Mto Rufiji hadi Dar es Salaam zilikuwa kubwa ukilinganisha na vyanzo vingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati uchunguzi huo unafanyika, Serikali ilifanya uchunguzi wa vyanzo mbadala kwa ajili ya miji ya Utete, Ikwiriri, Mkuranga na Kisarawe. Uchunguzi ulibaini kuwa miji hiyo inaweza kupata maji ya visima. Miradi mikubwa ya visima ilitekelezwa katika miji hiyo na kunufaisha wakazi wa maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukidhi mahitaji ya maji kwa Jiji la Dar es Salaam pamoja na maeneo ya Mkoa wa Pwani hususan Wilaya za Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Kisarawe, Serikali imeanza taratibu za kumwajiri mtaalam mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na utayarishaji wa vitabu kwa kutumia chanzo cha Mto Rufiji. Kazi hiyo inatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2018/2019. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Je, Serikali ilimaanisha nini kusema kuwa matibabu ni bure kwa kinamama wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mama wajawazito ni moja ya makundi maalum wanaostahili kupata huduma za matibabu bure kama ilivyoainishwa katika Mwongozo wa Uchangiaji wa Huduma za Afya wa mwaka 1997. Aidha, mwongozo umeweka bayana kuwa akina mama wajawazito ni haki yao kupewa huduma zote bila malipo na sio zile tu zinazohusu huduma za ujauzito.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwongozo uliopitiwa mwaka 2009/2010, imetamkwa bayana kuwa huduma ya afya kwa mama wajawazito ni bure ikiwa na maana kwamba mara tu mwanamke anapokuwa na ujauzito, huduma zote kuanzia kliniki ya ujauzito, pale atakapougua maradhi yoyote pamoja na huduma ya kujifungua, sanjrari na kumuona daktari, kupatiwa vipimo, kupewa dawa na kufanyiwa upasuaji pale utakapohitajika kufanyiwa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kuondoa adha kwa wananchi, Wizara imeanzisha utaratibu wa kutenga bajeti itakayotumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vinavyohitajika wakati wa kujifungua (delivery parks), delivery parks hizo watapewa akina mama wajawazito wanapokaribia kujifungua ili wawe wanatembea na vifaa hivyo. Hii itapunguza kero kwa akina mama kujinunulia vifaa vyao wao wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali inazikumbusha halmshauri kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sera hii ili akina mama wajawazito wapate huduma za matibabu bure kama Mwongozo wa Uchangiaji wa Mwaka 1997 na Sera ya Afya ya Mwaka 2007 inavyoelekeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, wananchi wanaombwa kutoa taarifa kuhusu hospitali zinazotoza fedha kwa ajili ya matibabu kwa akina mama wajawazito ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya urithi wa Dunia wa Kisiwa cha Kilwa Kisiwani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kisiwa cha Kilwa Kisiwani kinapatikana katika Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi. Kisiwa hiki kina utajiri wa magofu ya kale yaliyoorodheshwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia mwaka 1981 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni yaani UNESCO.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha urithi wa Dunia wa Kilwa Kisiwani unaendelea kuwepo, Serikali imetekeleza mipango ifuatayo:-
(a) Kukarabati majenzi yaliyoorodheshwa kwenye Urithi wa Dunia. Ukarabati unafanywa na vijana wa Kitanzania kutoka Kisiwa cha Kilwa Kisiwani ambao wamepata mafunzo kutoka kwa wataalam wa UNESCO. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara itajenga Ofisi itakayotumiwa na watumishi wa Urithi wa Dunia wa Kituo cha Magofu ya Kilwa Ksiwani na Songo Mnara.
(b) Kutangaza magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ndani na nje ya nchi ili kuvutia watalii. Serikali imeandaa jarida la karibu Kilwa (Kilwa District heritage resources) linaloonyesha picha na maelezo ya vivutio vya utalii vilivyopo Wilayani Kilwa yakiwemo magofu ya Kilwa Kisiwani. Jarida hili linatolewa kwa wageni wanaotembelea Kilwa pamoja na kutumika kutangaza utalii wa Kilwa katika maonyesho ya ndani ya Sabasaba na Nanenane.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali sasa imeandaa mpango wa kuuza utalii wa malikale na wanyamapori kwa pamoja yaani one package. Kilwa Kisiwani itanufaika na mpango huu kwa kuunganishwa na package ya Pori la Akiba la Selou.
(c) Kushirikisha jamii ya Kilwa Kisiwani kuhifadhi na kujipatia kipato kupitia malikale zilizopo kwenye Urithi wa Dunia. Serikali itawapa fursa za ajira na mafunzo katika fani ya ukarabati wa majenzi, kuongoza wageni, huduma za chakula na fani nyingine za ujasiriamali. Elimu waliyoipata itawasaidia kuanzisha ofisi ya kuongoza wageni Kilwa Masoko na wengine wanafanya kazi za ukarabati wa magofu ya Urithi wa Dunia Kilwa Kisiwani.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza ugonjwa wa UKIMWI kufikia mwaka 2030 kama Azimio la Umoja wa Mataifa linavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumaliza ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoazimiwa na Umoja wa Mataifa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kama ifuatavyo:-
Moja, ni kuendelea kutekeleza mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI Tanzania wa mwaka 2018 mpaka 2023. Mkakati huu umeainisha maeneo saba ya kimkakati yatayowezesha kufikia malengo ya sirufi tatu ikiwa ni ya kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kuratibu mipango ya sekta zote katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Pili, kuhamasisha upatikanaji na utumiaji wa kondomu; tatu, kutokomeza maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, nne, kuendeleza tohara ya hiari ya kitabibu kwa wanaume kwenye mikoa yenye kiwango kidogo cha tohara; tano, kinga ya tiba, matumizi sahihi na endelevu ya ARV’s na sita ni mkakati wa kuzuia maambukizi mapya ya UKIMWI kwenye makundi yaliyo katika hatari ya kuambukizwa. Makundi haya ni pamoja na wasichina balehe na wanawake vijana, wanaojidunga dawa za kulevya, wasichana wanaouza ngono, wafungwa, wavuvi, wachimbaji wa madini kwenye migodi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuendeleza usimamizi wa Mfuko wa Dhamana wa UKIMWI (AIDS Trust Fund) ili kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali fedha na nyingine kupitia vyanzo vya ndani vya nchi ikiwa ni jitihada za kupunguza utegemezi wa fedha za wafadhili nje. Tatu, kurekebisha Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 pamoja na sera nyingine husika. Vilevile sheria mbalimbali ili zitoe miongozo ya programu na mifumo ya kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI nchini. Na mwisho ni kuhamasisha wanaume kupima VVU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kuwa UKIMWI ni janga linalotukabili zote kama Taifa. Hivyo sisi tukiwa kama wawakilishi wa wananchi tunao wajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia katika kupunguza na hatimaye kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Kituo cha Afya Mlandizi kimetimiza vigezo vyote vya kuwa Haspitali ya Wilaya:-
Je, ni lini sasa Serikali itapandisha hadhi Kituo hicho kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Malandizi bado hakijakidhi vigezo vya kukifanya kiwe Hospitali ya Wilaya. Hata hivyo, Serikali haina mpango wa kukipandisha hadhi Kituo hicho kuwa Hospitali ya Wilaya. Serikali imeamua Kituo hicho kiendelee kutoa huduma kama Kituo cha Afya. Hata hivyo, Serikali iliiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha itenge eneo kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali Wilaya.
Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshatenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 1.5 katika mwaka wa 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi huo. Pia Halmashauri imeshatenga eneo la ekari 32 lililopo katika Kitongoji cha Disunyala, zamani lilikuwa shamba la United Farming Cooperation kwa ajili ya ujenzi huo.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y MHE. HAWA M. CHAKOMA) aliuliza:-
Je, Serikali inatekelezaje Mpango wa UKIMWI wa 90-90-90?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mpango wa 90-90-90 kwa kufanya mambo yafuatayo:-
(a) Serikali imeridhia Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kupima VVU na kutibu bila ya kuzingatia kiwango cha kinga mwilini (CD4);
(b) Serikali imetoa Waraka unaoagiza utekelezaji wa mkakati huu tangu Oktoba, 2016;
(c) Utaratibu umewekwa wa kuhakikisha watu wote wanaogundulika kuwa na VVU wanaanzishiwa dawa za kufubaza VVU (ARV) mara moja; na
(d) Serikali baada ya kubaini mapungufu ya wananchi kujitokeza kupima maambukizi ya VVU kupitia utafiti, imeandaa kampeni mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU ili kujua hali zao na hasa mkazo mkubwa utaelekezwa kwa wanaume ambao utafiti umeonesha kuwa hawajitokezi sana kupima na kujua hali zao. Kampeni hii inategemewa kuzinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 19 Juni, 2018 hapa Mjini Dodoma. Aidha, kampeni hii itahusisha kusambaza ujumbe wa uhamasishaji kupitia vyombo vya habari, mabango, vipeperushi na makongamano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa wananchi wote kuendelea kupima afya zao ili watambue hali zao na kuchukua hatua stahiki. Pia natoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo mara itakapoanza kwa nchi nzima.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. HAWA M. CHAKOMA) aliuliza:-

Kuna miradi mikubwa ya maji katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambayo hadi sasa haijakamilika. Miradi hiyo ipo Kijiji cha Mperamumbi Kata ya Kwala, Kijiji cha Boki Mnemera Kata ya Bokomnemera, Kijiji cha Vukunti Kata ya Mlandizi na Kijiji cha Dutumi Kata ya Dutumi:-

Je, ni lini miradi hiyo itakamilika ili kuwaletea matumaini wananchi wa maeneo hayo, hususan akinamama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2013, Serikali ilianza kutekeleza miradi ya maji mikubwa katika Vijiji vya Mperamumbi, Kata ya Kwala, Boko Mnemela, Kata ya Bokomnemela na Vukunti, Kata ya Mlandizi vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha. Utekelezaji wa miradi hiyo imekamilika mwaka 2018 na tayari inatoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi. Miradi hii ina changamoto ya uendeshaji inayosababisha maji kukatwa mara kwa mara kutokana na bili ya maji kuwa kubwa. Kwa kuwa eneo la Kibaha linapatiwa maji na DAWASA, Wizara inaangalia uwezekano wa mradi huo kusimamiwa na DAWASA na si Jumuiya ya Watumiaji Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji wa Dutumi umekamilika na unatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi na kwa sasa mradi huo unafanyiwa upanuzi kutoka vituo sita (6) hadi kufikia vituo tisa (9) vya kuchotea maji.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-

Miradi ya maji katika vijiji vya Lupunga, Ruvu Dosa na Kipandege Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha bado inasuasua mpaka sasa.

Je, ni lini miradi hiyo itapatiwa fedha ili iweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji Lupunga uliopo Kata ya Kikongo ulianza kutekelezwa Novemba, 2013 na ulikamika mwaka 2016 na unaendelea kutoa huduma ya maji katika vitongoji tisa vya Ngeta, kikongo, Lupunga, Mwanabwito, Makongotopola, Kisabi, Madimula, Msongola na Makazi Mapya kwenye mamlaka ya mji mdogo wa Malandizi. Mradi huo ulikuwa na changamoto za kiundeshaji ambapo kamati ya Maji ya awali ilivunjwa na kuundwa kamati mpya inaendelea kutoa huduma ya maji maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji Ruvu kwa Dosa uliopo katika Kata ya Matambani ulianza kutekeleza mwaka 2013 na kukamilika mwaka 2016 kutoka bomba kuu la DAWASA. Kwa sasa mradi unaendelea kutoa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi 1800 kwa eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa Maji kipandege uliopo katika Kata ya Soga ulianza kutekelezwa Novemba, 2013 na kukamilika mwaka 2017. Mradi huo kwa sasa una changamoto za kiufundi ikiwa ni msukumo mdogo wa maji toka bomba la DAWASA. Tayari Mkandarasi na Mhandisi Mshauri aliyesanifu wanashukulikia tatizo hilo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha miradi yote inatoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa maeneo hao.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-

Je, ni kwa nini dawa za shinikizo la damu hazitolewi katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma,Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dawa za kutibu shinikizo la damu zimegawanyika katika makundi kulingana na namna zinavyofanya kazi na athari zake,hivyo basi utoaji wake unazingatia utaalam na uwezo wa kitaaluma, ndiyo maana kuna dawa hutolewa katika ngazi za Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa na Hospitali ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ushauri mzuri wa Mheshimiwa Mbunge unatekelezeka, Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli imepeleka wataalam wengi wenye shahada ya udaktari mpaka ngazi ya kituo cha afya kwa lengo la kuhakikisha huduma nyingi na bora kama ulivyoshauriwa na Mheshimiwa Mbunge zinapatikana kuanzia ngazi ya chini na pia dawa hizi zimehusishwa katika mwongozo mpya wa matibabu nchini ili ziweze kutumika mpaka ngazi ya kituo cha afya na zahanati.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -

Je, ni kwa kiasi gani Serikali inafahamu madhara yatokanayo na madini ya zebaki?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma (Mbunge wa Viti Maalum) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba, Serikali inatambua madhara makubwa ya kiafya kwa binadamu, mimea na mazingira yanayosababishwa na matumizi ya kemikali ya zebaki na hasa katika shughuli za uchenjuaji wa madini. Na miongoni mwa madhara ya kemikali hiyo kwa binadamu, ni kuathiri mifumo ya fahamu, uzazi, upumuaji na kusababisha magonjwa mbalimbali kama vile ya figo, moyo na saratani. Aidha, kemikali hiyo pia, huathiri viumbe hai vya majini na nchi kavu pindi zebaki inapotiririka na kuingia kwenye vyanzo vya maji ambavyo hutumiwa kwa matumizi mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za kibinadamu.

Mheshimiwa Spika, na njia zinazopelekea kemikali ya zebaki kuingia mwilini ni kushika, kuvuta hewa na kula vyakula vyenye viambata vya kemikali hiyo. Pamoja na athari hizo kiafya, matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu yameonesha uwezo mdogo wa kutoa dhahabu ambao ni chini ya asilimia 30, hali ambayo imekuwa ikipelekea wachimbaji wadogo kushindwa kuzalisha kiwango cha kutosha na hivyo kupata faida kidogo.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa wachimbaji wadogo kuhusu athari za kemikali hiyo na kutoa njia salama za utumiaji, ikiwa ni pamoja na usakafiaji wa mialo na utumiaji wa retorts kiswahili chake ni (vigida) wakati wa uchomaji. Aidha, Serikali kupitia STAMICO itaendelea kutoa elimu ya matumizi ya njia mbadala ya uchenjuaji dhahabu kupitia vituo vyetu vya mfano vilivyoko maeneo ya Lwamgasa, Katente pamoja na Itumbi. Nakushukuru.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kurasimisha vitambulisho vya wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mwezi Machi 2018, Serikali kwa kuwathamini na kuwajali wajasiriamali na watoa huduma wadogo ilianzisha utaratibu wa vitambulisho ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira bora na tulivu zaidi. Vitambulisho hivi vilirasimishwa kutumiwa na wajasiriamali wenye mitaji yao na mauzo ghafi yasiyozidi shilingi milioni nne kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2021 vitambulisho vya wajasiriamali wadogo vimefanyiwa maboresho kadhaa ikiwemo kuwekwa picha na jina la mjasiriamali mdogo aliyepatiwa kitambulisho hicho pamoja na ukomo wa muda wa kutumia kitambulisho hicho. Muda wa matumizi ni mwaka mmoja tangu tarehe ya kupatiwa kitambulisho badala ya mwaka wa kalenda kama ilivyokuwa awali.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali wadogo kadri itakavyohitajika, ahsante.