Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Additional Questions to the Prime Minister from Hon. Hawa Mchafu Chakoma (1 total)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Nina swali la nyongeza eeh.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nilikuwa nasubiri umalize kwanza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba sasa nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ripoti ya Maendeleo ya Dunia ya mwaka 2010 inaitaja Tanzania kama nchi yenye malikale adimu na urithi wa utamaduni wa Taifa ambao ungeweza kuongezea nchi yetu kipato na kukuza uchumi wetu. Nataka kujua sasa, Tanzania inafanya nini katika kutumia malikale zake hizo adimu kama Olduvai Gorge, Laetoli, Kolo na Kilwa Kisiwani ili iweze kuiongezea nchi yetu kipato? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuzingatia umuhimu na mchango wa malikale za Taifa letu katika kukuza uchumi, mnamo mwaka 2007 aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, aliagiza nyayo hizo ziweze kufukuliwa ili watalii wengi zaidi waweze kutembelea eneo hilo na nchi yetu iweze kujipatia kipato.
Mheshimiwa Naibu Spika, inasikitisha sana katika majibu ya Mheshimiwa Waziri, anasema hakuna kusuasua kwa ufukuzi wa nyayo hizo ilhali sasa hivi inapita miaka 10 tangu agizo hilo litolewe na hadi hivi sasa tunavyozungumza, bado nyayo hizo hazijafukuliwa. Kwa hiyo, ninachotaka kujua, wananchi wa maeneo yale ambao wanazungukwa na ile historical site wananufaikaje kwa uwepo wa hiyo historical site? Ahsante.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Chakoma kwamba Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kwamba maeneo yetu haya ya urithi wa Taifa yanaletwa katika kiwango ambacho kinaweza kutumika na kutuzalishia mapato katika maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Ngorongoro, eneo hilo limefukuliwa na wataalam kutoka Tanzania, Spain pamoja na Marekani na kuvumbua nyayo nyingine ambazo zinaonesha kwamba wanadamu hao wanaitwa Zamadamu, walikuwa wanaishi pale wakiwa wanatembea upright miaka milioni 3.6 iliyopita. Nyayo hizo mpya ambazo ziligundulika, zilifunguliwa mwezi Machi, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hilo pia linajenga museum kubwa, eneo la mapokezi, maktaba na kuonesha vitu mbalimbali ambavyo vitavutia sana watalii watakaotembelea eneo hilo. Aidha, Serikali inaendelea kuyafufua na kuyakarabati maeneo mengi ya Malikale ambayo Mheshimiwa Chakoma ameyataja na kwamba maeneo haya yakiwekwa katika utangazaji wetu wa utalii yatakuwa na mvuto mkubwa na yataongeza mapato ya Serikali kwa kiwango kikubwa sana.