Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Salome Wycliffe Makamba (10 total)

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri hayaridhishi. Anaongea habari ya gesi asili Shinyanga yaani mpaka gesi asili ije kufika hizi ni ndoto na kwa kweli tutaendelea kuumia na bei ya maji. EWURA hawajaenda kufanya consultation, hawajaenda kuongea na wananchi, wamepandisha bei ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Maji ya Shinyanga na Kahama wametengeneza muungano wakaweka kitu kinaitwa SHUWASA na kazi ya SHUWASA ilikuwa ni kuboresha usambazaji wa huduma ya maji katika Wilaya hizi mbili. Badala yake SHUWASA sasa hivi wanauzia maji Mamlaka ya Kahama na ya Shinyanga ambapo watumiaji wa mwisho wanaumizwa na bei kubwa kwa sababu ya kuwepo na mtu wa katikati. Waziri ana mpango gani wa kujaribu ku-standardize suala la bei ya maji katika wilaya hizi mbili kwa sababu hali hii inawaumiza wadau na wawekezaji wanakimbia kwa sababu hakuna huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nikimnukuu Mheshimiwa Rais Magufuli kwenye kampeni zake alisema atahakikisha akiingia madarakani nchi nzima tutapata maji na kama tukikosa maji atawageuza ninyi Mawaziri kuwa maji, lakini mpaka leo hamjawa maji. Shinyanga ni Kata nane tu za Wilaya ya Kahama Mjini ndiyo zina maji wakati Kata 12 zote mpaka leo hazijapata maji, watu wanahangaika wanatumia maji taka na inatishia kuleta milipuko ya magonjwa. Ni lini watatimiza mpango wa kutandaza mtandao wa maji katika Wilaya hizi mbili ili watu waepukane na magonjwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge pamoja na jazba aliyokuwa nayo wakati akiongea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimfahamishe kwamba masuala ya kupandisha bei yapo kisheria. Huyu mdhibiti ambaye anaitwa EWURA ipo procedure ambayo lazima aifuate. Kwa hiyo, procedure ya kupandisha bei ilifuatwa, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Spika, pia naomba afahamu kwamba jurisdiction ya SHUWASA ni katika Mji wa Shinyanga kule Kahama wana mamlaka nyingine ambayo inashughulikia Kahama. Kwa hiyo, tunayo mamlaka ambayo inaleta maji SHUWASA kwa bulk halafu SHUWASA sasa ndo inafanya distribution.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja kubwa hapa ungesema tu kwamba unaona bei iliyowekwa ni kubwa, hilo ni jambo ambalo tunaweza tukazungumza. Ndiyo maana kwenye majibu tumesema kwamba nusu ya gharama za uendeshaji wa SHUWASA ni kulipa bili za umeme. Kwa hiyo, bili za umeme zikishushwa definitely na bili ya maji itashuka. Tukasema kwamba uzalishaji wa umeme kwa mfano kama tunatumia nishati ambayo inalazimisha bei ya umeme ishuke basi hata bei ya maji itashuka, ndiyo hoja ambayo ulikuwa umeuliza kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia ukielezea suala la kwamba mpaka sasa upatikanaji wa maji maeneo mengi hakuna, lakini ni lazima Mheshimiwa Mbunge afahamu tulipitisha bajeti mwaka huu na tumepanga fedha za kutekeleza miradi na kila Wilaya inaendelea kutekeleza. Sasa akilizungumza kwa ujumla inakuwa vigumu kuelewa swali lake tulijibu vipi. Nataka awe specific na swali kwamba ni Wilaya ipi na ni mradi upi ambao haujakamilika. Serikali inaendelea kukamilisha miradi kulingana na mpango ambao Wabunge mlipitisha.
Mheshimiwa Spika, naomba nitambue Mheshimiwa Masele ndiye aliyeuliza swali kwa Mheshimiwa Rais kuhusu bei za maji.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI.
Mheshimiwa Waziri umetuaminisha kwamba mmetupatia shilingi milioni 600 kwa ajili ya kujenga barabara na pia mmetupa shilingi milioni 320 kwa ajili ya kukarabati barabara hizi. Mheshimiwa Waziri barabara ya Phantom-Majengo, ni barabara ya muhimu kweli na barabara hii inachangia pato la Halmashauri kwa asilimia 25. Barabara hii ina urefu wa mita tano na tunasema tunataka tufanye Serikali ya viwanda, kule kuna viwanda vidogo vidogo vya mazao ya mpunga na mahindi.
Mheshimiwa Waziri, hauoni kama kuna umuhimu wa kuingiza barabara hii katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha ili tuweze kutekeleza mpango huu wa Tanzania ya viwanda kwa kuendelea kuzalisha na magari yaweze kupita? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Ushetu, Mheshimiwa Waziri mmetenga shilingi milioni 181 tu kwa ajili ya barabara na tena ni kwa ajili ya ukarabati tu wa barabara, lakini nikufahamishe kwamba kule hakuna barabara hata moja ya lami, barabara zote ni za vumbi na fedha mliyotenga ni kidogo na ile ni Halmashauri mpya. Unawaambia nini Watanzania wa Ushetu, watawezaje kupata barabara nzuri za lami ilihali mmewatengea fedha kidogo namna hii, nini mpango wa Serikali kwa Halmashauri hii mpya?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilimaanisha kilometa tano.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Mji wa Kahama kimkakati tunafahamu na ndio maana hata ninyi katika Mji wa Kahama mlikuwa mnapeleka maombi kwa Mheshimiwa Waziri wa Nchi kwamba Mji ule sasa uwe Manispaa kwa kadri unavyokua. Ukiangalia barabara ya Phantom - Majengo ina kilometa 5.2 ni barabara ya kimkakati ina jukumu kubwa sana, ndiyo maana tumesema mwaka huu tumeanza kutenga fedha hizo. Hata hivyo, unafahamu Mji wa Kahama siyo barabara hii tu ndiyo tunaanza kujenga, kuna miundombinu ya barabara za lami pale zilikuwa zinaendelea na mimi nilifika pale miezi michache iliyopita kuja kukagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu letu kubwa tunajua kwamba eneo hili ni eneo la mkakati, kama Serikali tutafanya kila liwezekanalo, lakini siyo Mji huu peke yake. Serikali tumejipanga kuna ahadi za Mheshimiwa Rais katika maeneo mbalimbali, hivi sasa ukiangalia katika Halmashauri mbalimbali, juzi Mheshimiwa Rais alikuwa kwa ndugu yangu pale Mheshimiwa Mbowe, alikuwa akiangalia miundombinu ya barabara. Pia nchi nzima hata kwa Mzee Lubeleje kule Mpwapwa kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunachotaka kufanya ni kwamba ndani ya miaka mitano tufanye mabadiliko makubwa sana katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hasa katika ujenzi wa barabara za lami.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaondoe hofu Waheshimiwa Wabunge, siyo kwa Mji wa Kahama peke yake isipokuwa katika miji mbalimbali katika Halmashauri zetu hizi tutahakikisha ujenzi wa barabara za lami hasa kutumia fedha za World Bank ambayo Serikali imechukua commitment ya kutosha kubadilisha miji yake yote iweze kubadilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninyi ni mashahidi mnafahamu sasa hivi, Halmashauri za Miji nyingi sasa hivi na Manispaa zimebadilika katika suala la ujenzi wa barabara za lami TAMISEMI imeamua kufanya hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu eneo la Ushetu kama ulivyosema ni kwamba tunafahamu Ushetu ni Halmashauri mpya na ndiyo maana, ndugu yangu hapa Mheshimiwa Elias Kwandikwa kila siku anapambana na Jimbo lake la Ushetu, kama unavyopambana Mheshimiwa Mbunge hapa. Naomba kuahidi kwamba kwa kutumia Mfuko wa Barabara, nikuahidi tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo tutahakikisha maeneo ya Ushetu na maeneo mengine tutaweka nguvu za kutosha na hasa hizi Halmashauri mpya tutaweza kuzifungua ili wananchi kule waweze kupata huduma wajisikie huru kama wananchi wenzao wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza kwa Waziri Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi takribani wiki mbili inakwenda ya tatu sasa Shinyanga, Kahama maji hayatoki. Wale watu wanatumia maji ya kununua hakuna maji kabisa. Tatizo inasemekana kwamba hamjalipa bili ya umeme kama Mheshimiwa Rais alivyoagiza. Mheshimiwa Waziri wale watu wanapata shida, hivi ni lini mtarudisha yale maji ili watu waendelee ku-enjoy tunu za Taifa hili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wiki mbili zilizopita Mamlaka nyingi za maji zimekumbwa na tatizo la kukatiwa umeme hivyo kufanya mitambo ya kuzalisha maji isifanye kazi, hii ni kwa Shinyanga pamoja na maeneo mengine pia. Kutokana na tatizo hilo, tarehe 8 Wizara ya Maji, Hazina na Mkurugenzi wa TANESCO walikaa kikao na kuna makubaliano ambayo yamefikiwa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya muda mfupi suala hili litatuliwa ili liwe na ufumbuzi wa kudumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini napenda Mheshimiwa Mbunge ajue kwamba ni kweli kabisa kwamba Mamlaka zimekuwa hazilipi bili za umeme na kama Mamlaka hazilipi bili za umeme TANESCO itakufa. Kwa hiyo, tumeweka utaratibu kwamba tuhakikishe tunalipa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wamekuwa na nia nzuri kabisa ya kuwatetea wananchi wao, wengine wanasema kwamba bili ni kubwa na kadhalika lakini bila kuweka bili ya kiwango ambacho kitawezesha hizi Mamlaka ziweze kujiendesha wenyewe tatizo hili tutaendelea kuwa nalo. Kwa hiyo, naomba sana EWURA wanapopita kufanya hesabu za maji tuwe waangalifu tunapojaribu kuziingilia zile kwa sababu zinatusababisha tufike kwenye hii hali ambayo tumefika.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniona na ningependa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Kahama nyumba za Polisi zina hali mbaya kweli, na nimewahi kuuliza hapa na kumuomba Mheshimiwa Waziri akaniahidi kwamba watatusaidia kukarabatai zile nyumba. Kwanza hazitoshi na zina hali mbaya.
Je, ni lini Mheshimiwa Waziri atakuja kutusaidia kuweza kukarabati nyumba zile ili anglau polisi nao waweze kuishi katika mazingira mazuri? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Salome kwa kuleta jambo hili. Nilishazungukia Wilaya ya Kahama. Kama tunavyojua Kahama ni moja ya eneo potential sana katika nchi yetu, hata kimakusanyo; kwa hiyo hata vijana wetu wanaokaa kule na wanapokabiliana na changamoto za eneo husika wanatakiwa wawe katika mazingira mazuri. Tunalitambua jambo hilo na kwa sababu limekuwa likiletwa mara kwa mara. Niseme tu kwamba tutalipa kipaumbele, tutalipa uzito ili hadhi za nyumba za askari wetu ziweze kulingana na eneo husika.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Kahama, Kata ya Mwendakulima kuna mgogoro wa muda mrefu sana kati ya Kanisa la Katoliki na Kijiji cha Mwendakulima na sasa ni mtaa juu ya ardhi ambayo Kanisa hili limemiliki.
Mheshimiwa Waziri, je, uko tayari kwenda na mimi katika Jimbo hili na Kata hii kuweza kutatua mgogoro huu maana umekuwa ni wa muda mrefu na unaleta hali ya kutoelewana kati ya Kanisa na wananchi wa Mwendakulima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimahakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kwenda naye katika eneo hilo na ikiwezekana kuwashirikisha wenzetu wa Wizara ya Ardhi tuone mgogoro huo namna ya kusuluhisha, lakini kwa kuanzia hata leo niko tayari tukutane mimi na yeye tujadiliane kuhusu hili.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri, tunafahamu kwamba sekta zisizo rasmi zinachangia sana Pato la Taifa na wengi wao wako kwenye hatari ya kupata ajali na magonjwa kama watu wa bodaboda. Serikali ina mpango gani wa kurasimisha na kuwaweka katika mpango wa bima ya afya sekta isiyo rasmi, hasa vijana wetu wa bodaboda? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tunatambua kwamba sekta isiyo rasmi nayo ina mchango mkubwa sana katika ukuaji na kuchangia katika uchumi wa nchi yetu, lakini sisi kupitia bima ya NHIF na CHF tunatambua makundi haya na kwa kupitia vikundi vyao kuna mfumo wa bima ambao wanao ambao wanaweza kukata kwa kupitia vikundi vyao. Lakini hata hivyo, kwa mtu mmoja mmoja sasa hivi tunakuja na utaratibu wa CHF iliyoboreshwa ambayo nayo itakuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kutoa huduma kwa mtu mmojammoja ambaye atakuwa anahitaji.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya viwanda Tanzania ni gharama kubwa za uzalishaji katika viwanda hivi. Serikali ina mpango gani wa kuweka mazingira wezeshi ili kupunguza gharama kama kuboresha miundombinu na kutengeneza mazingira mazuri ya kilimo cha malighafi kama pamba kwa ajili ya uzalishaji wa viwanda hivi? Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira hayo ili wawekezaji hasa kwenye viwanda vya nguo waweze kupata gharama nafuu za uzalishaji zitakazopelekea wao kupata faida?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, viwanda vingi vimekuwa vikikwama kwa sababu ya kukosa mitaji. Je, Wizara ina mkakati gani wa kuzungumza na mabenki ambayo yanatoa mikopo kuweka riba nafuu kwenye viwanda ili waweze kupata pesa kwa ajili ya kufanya biashara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza hapo awali, Serikali kwa kutambua changamoto zilizopo ndiyo maana ilikuwa imeitisha kikao na wadau ili kujadili na kuweza kubaini changamoto hizo na hivyo ipo mbioni katika kuzifanyia kazi ikiwemo kuangalia mazingira ambayo yanafanya bidhaa hizo zisiwe na ushindani wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mitaji, ni kweli kwamba kuna baadhi ambao wanahitaji kuwekeza lakini suala la mitaji hasa katika uwekezaji binafsi ni jukumu la mwekezaji mwenyewe. Kwa upande wa Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaweza kulima pamba iliyo bora zaidi, lakini pia wanastahili wapate faida inayostahili kutokana na kilimo chao.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Uti wa mgongo wa nchi hii uko kwenye kilimo. Tunategemea kilimo ili tuweze kupata maendeleo kwenye nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza swali. Shinyanga na Kahama tunaongoza kwa kilimo cha mpunga na mahindi. Mpaka sasa ninapoongea ruzuku imepungua kwa zaidi ya 50%. Nini mpango wa Serikali kuongeza ruzuku ili tuweze ku-improve kwenye kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amezungumzia kwenye zao la mpunga na mahindi na juu ya kuongeza ruzuku. Nilipokuwa najibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Hongoli nimesema kabisa kwamba hatutakuwa na ruzuku kwa mwaka huu kwa sababu mazao yote yawe ya kimkakati, yawe yale ya nafaka, wote watakuwa wananunua isipokuwa kwa bei elekezi.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mradi wa bomba la Ziwa Victoria umeshafika katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, lakini usambazaji katika Kata nyingi bado haujafanyika, Kata ya Mwenda kulima, Kagongwa, Iyenze, Isagee maji hayajafika. Je, Serikali ina mpango gani wa kusambaza maji ya Ziwa Victoria ili wananchi waweze kunufaika? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza tutambue jitahada kubwa zilizofanywa na Serikali, tunatambua kabisa tulikuwa na changamoto kubwa sana, katika Mji wa Kahama na Shinyanga na Serikali ikaona haja sasa ya kuyatoa maji Ziwa Victoria kwa ajili ya kutatua matatizo haya ya maji, kikubwa maji yale yamekwishafika lakini imebaki changamoto tu ya usambazaji. Hivyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Mbunge, wali wa kushiba unaonekana kwenye sahani, sisi tumekwishawaita Wakurugenzi wote na tumekwishawaagiza katika mapato yao wanayoyakusanya watenge asilimia katika kuhakikisha wanasambaza maji kwa wananchi ili waweze kupata maji safi salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, lipo tatizo la msingi la ajali za barabarani kwa bodaboda na vyombo vingine vya usafiri. Tatizo hili ni Kitengo cha Usalama Barabarani kugeuza kitengo hiki kama chanzo cha mapato. Watu wanakwepa matrafiki, wanakimbia kwa sababu ukikamatwa hakuna onyo, ni faini. Bodaboda siku hizi wanakamatwa kwa kukimbizana na trafiki. Nadhani hii inasababishwa na uzee wa sheria hii ni ya mwaka 1973. Ni lini Serikali italeta mabadiliko ya Sheria ya Usalama Barabarani ili tufungue mjadala wa namna gani tutaiboresha ili kupunguza ajali za barabarani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDAIN YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nimtoe hofu Mheshimiwa Salome, Muswada huu uko njiani, muda wowote tutauleta tuje tuujadili tuone namna ambavyo tunaweza tukafanya mabadiliko ya baadhi ya sheria hizi. Mheshimiwa asiwe na wasiwasi, tuko mbioni kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.