Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Halima James Mdee (30 total)

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hivi karibuni tumeshuhudia kwa ukatili kabisa na pasipo kuzingatia haki za binadamu kwa kisingizio cha kutunza mazingira, Serikali ya Chama cha Mapinduzi imebomolea wananchi ambao wanaishi kwenye mabonde na pembezoni mwa mito. Hata hivyo, tuna taarifa vilevile kwamba miaka minne iliyopita, wananchi hao walitakiwa wahamishwe kutoka mabondeni kupelekwa Mabwepande.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna taarifa vile vile kwamba mgawanyo wa viwanja vya Mabwepande ulifanyika kinyume na utaratibu. Je, Serikali iko tayari kumuagiza Mkaguzi Mkuu wa Serikali afanye uhakiki wa viwanja vya Mabwepande ili tujue nani alipata nini na kama kuna tatizo lolote hatua muafaka zichukuliwe ili wananchi waliotarajiwa kupata viwanja hivyo waweze kupata haki yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MUUNGANO NA MAZINGIRA (MHE. LUHAGA J. MPINA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zoezi la bomoabomoa lililofanyika Dar es Salaam - Msimbazi, sheria na taratibu zote zilifuatwa. Nataka kusisitiza tu hapa kwamba hakuna tatizo lolote katika zoezi hilo. Kumtumia Mkaguzi wetu wa Hesabu za Serikali kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge anaomba kama kuna mambo ya kutaka kujiridhisha sisi tuko tayari afanye hiyo kazi lakini sheria zote zilizingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie Waheshimiwa Wabunge, sasa hivi dunia imefikia kwenye wakati mgumu sana katika suala hili la mabadiliko ya tabia nchi. Ni lazima sisi viongozi wote tujipange na tuwe mstari wa mbele kuwaambia wananchi wetu waondoke mabondeni. Kwa sababu mafuriko sasa ni suala ambalo litaendelea kuwa permanent kulingana na madhara ambayo yapo sasa hivi yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa hiyo, ni lazima sisi viongozi wote tuwe firm kuwaambia wananchi wetu bila kumumunya maneno, waondoke wote mabondeni kwa sababu ni kwa ajili ya afya na maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sisi tupo tayari Mkaguzi afanye kazi hiyo kwa sababu jambo hili lilifanyika kwa mujibu wa Sheria yetu ya Mazingira kwa maana ya kifungu cha 57(1) ambapo wananchi hawapaswi kuishi ndani ya mita 60 kutoka kwenye mabonde, mito au bahari. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwenye majibu ya Waziri anasema uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi umekamilika. Labda tu nimpe taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri hizi barabara kwa miaka ya fedha miwili mfululizo, 2014/2015, 2015/2016 zilitengewa fedha, zikatangazwa, tatizo ilikuwa fedha zilizotolewa na wakandarasi walichokuwa wakihitaji zilikuwa ni ndogo hivyo licha ya matangazo mara tatu hakuna kilichofanyika. Ukiangalia bajeti ya ujenzi zimetengwa kiasi kilekile cha fedha, barabara ya Mlimani City - Goba imetengewa shilingi bilioni 2.5, fedha ambazo mwaka jana ilishindikana, halikadhalika Tegeta Kibaoni - Goba. Nataka tu Naibu Waziri aniambie kiukweli tu kabisa, anawahakikishia vitu wananchi wa Jimbo la Kawe kwamba kwa bajeti hii iliyotengwa ujenzi utaanza kufanyika kwa mwaka huu wa fedha? Hilo ni la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili barabara muhimu sana ya New Bagamoyo Road, tunafahamu kwamba kwa miaka miwili iliyopita pia zilitengwa shilingi bilioni 88, zilitolewa na Wajapan through JICA. Madhumuni yalikuwa ni kujenga barabara ya Mwenge - Tegeta (double road), kujenga barabara ya Mwenge - Morocco (double roads), 88 billion akiwa Waziri wa Ujenzi ni Magufuli. Sasa leo kile kipande cha Mwenge - Morocco inaonekana kama kimekufa kuna ukarabati wa kienyeji unaendelea pale. Nilitaka Naibu Waziri aniambie zile shilingi bilioni 88 zimekwenda wapi na kile kinachoendelea pale Mwenge - Morocco ndiyo permanent ama ni temporary kukidhi mahitaji ya sasa ya barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge wa Kawe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Kawe na wananchi wake wote wa Kawe kwamba nilichokieleza katika jibu langu la msingi kuhusu kuanza kwa ujenzi wa hizi barabara mbili alizozitaja ni sahihi na tutajenga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili kwamba shilingi bilioni 88 zilikwenda wapi, nadhani anafahamu kwamba hiyo double road anayoongelea kuna sehemu yake imeshajengwa, kilichobaki ni kama anavyosema ni hiki kipande cha kati ya Mwenge - Morocco, upande ule mwingine umeshajengwa na hizo hela ndiko zilikoenda. Zimekwenda huko, zimetumika kujenga barabara hiyo na namhakikishia kazi inayoendelea sasa hivi pale, inaendelea kwa kiwango.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye (b) ya swali langu niliuliza, ni miradi gani inayotarajia kutekelezwa, muda wa utekelezaji, gharama za kila mradi na nani anayewajibika katika utekelezaji? Sasa majibu ya Serikali hayajanielezea mradi, ila ameelezea maeneo ambayo mradi utatekelezwa. Sasa nataka niambiwe katika maeneo haya ambayo miradi itatekelezwa, kuna miradi gani specifically, kuna Kampuni gani specifically? Hilo la kwanza.
La pili, zimetajwa dola bilioni 32, nami nilivyouliza swali, nilikuwa nataka nijue gharama za kila mradi kwenye Jimbo langu. Sasa swali langu la pili: Je, hizi bilioni 32 ndiyo zote zinaenda kwenye mradi wa Jimbo la Kawe na kama siyo, nataka nijue Jimbo la Kawe specifically katika hii dola bilioni 32 mgao wake ni kiasi gani na kwa miradi ipi? Nadhani nimeeleweka.
Swali langu nataka uchambuzi ili wananchi wangu wanaosikia kila mmoja ajue kwake anastahiki gani. Sasa Serikali ikinipa kiujumla jumla nitashindwa kuja kuwabana.
Kwa hiyo, nataka uchambue, siyo unajibu kiujumla jumla.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa katika jibu la msingi, tumeshasema mradi ambao unaendelea, Mkandarasi anaitwa Jain Irrigation Company na tumesema gharama ya mradi ni US Dollar milioni 32. Tunapokuwa tunapanga miradi, huwa hatupangi Kijimbo. Tunapanga mradi kwa ajili ya Jiji la Dar es Salaam na sehemu kubwa ya mradi huu uko kwenye Jimbo lake.
Ndiyo maana tumetaja hayo maeneo ya Kawe, Mabwepande, yote yote yako kwenye Jimbo la Kawe. Kwa hiyo, tumelijibu kikamilifu kama alivyouliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sehemu yake ya pili alikuwa anataka kujua kama hizo US Dollar milioni 32 ni kwa Jimbo la Kawe tu peke yake? Hapana, siyo kwa Jimbo la Kawe peke yake, ni pamoja na bomba kubwa ambalo litaenda baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Bagamoyo.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya asilimia 70 ya nguvu kazi ya kilimo ni wanawake, lakini ni kwa bahati mbaya sana inapokuja suala la umiliki wa ardhi, wanawake wanaomiliki ardhi ni pungufu hata ya asilimia 20. Na hata ninavyozungumza hati za kawaida na hati za kimila haziwanufaishi wanawake kwasababu sheria za nchi yetu zinatambua Sheria za Kimila ambazo zina ubaguzi.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka Wizara inisaidie katika mpango wenu mpana wa kuweza kufanya maboresho kwenye sekta ya ardhi mna mikakati gani ya kuweza kuondokana na sheria kandamizi ili umiliki wa ardhi usiwe na ubaguzi hivyo shughuli za uchumi zinufaishe makundi yote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimhakikishie Mheshimiwa kwamba sheria zetu tulizo nazo sasa pamoja na kanuni pamoja na kwamba Sera ya Ardhi pia inapitiwa upya, hazikandamizi wala hazibagui mwanamke kuweza kupata hati. Ndio maana zoezi linaloendelea sasa la kutoa hati miliki za kimila kuna mahali ambapo unakuta mke na mume wote wanakabidhiwa hati kwa pamoja, aidha wanakubaliana iandikwe jina la mke au iandikwe majina yote mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tumeshaanza kuangalia kwa sababu wengi walikuwa wakinyanyasika katika hilo. Kwa hiyo, tunajaribu kupitia upya pia sera tuweze kuona lakini haya yote yanawezekana katika kufanyika ili kuweza kuhakikisha kwamba akina mama nao pia hawako nyuma katika umiliki wa ardhi. Ni kweli lilikuwepo tatizo hilo lakini limeanza kuondoka kwa taratibu.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumalizia kazi la Mheshimiwa Mdee, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri kwamba ni kweli sheria hazibagui, lakini pia hata kama akipata mwanaume hati ya kimila au hati ya muda mrefu, wakati wowote ule mwanamke ajue ile hati ni salama. Hii ni kwa sababu kwa utaratibu wa sasa mwanaume akitaka kuuza au kubadilisha ile hati hatumkubalii mpaka tumuulize mkewe na vilevile mwanamke akitaka kuuza lazima tumuulize mumewe ili kuonyesha kwamba mali haipotei whether imeandikwa mwanaume au mwanamke wakati wa kupoteza lazima yoyote aulizwe. Kwa hiyo, mwanamke amelindwa sana katika sheria za sasa. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya Waziri yanaonesha kwamba watajenga mtaro mkubwa Mbezi Samaki lakini kuna eneo lingine ambalo ni hatarishi na sasa hivi kutokana na mvua zilivyonyesha liko kwenye hali mbaya sana na barabara inaweza ikakatika, ni eneo la Afrikana - Salasala - Kinzudi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo hili tumeshafanya ziara mara kadhaa na Mkurugenzi wa TANROADS Mkoa tukashauriana kwamba wauweke mtaro mkubwa, lakini vilevile waweke utaratibu wa kujenga hata mita mia za lami kwenda mbele kwa sababu ile barabara inahudumiwa na Halmashauri ili kuweka mapokeo makubwa ya maji vilevile kuokoa ile barabara. Sasa napenda Mheshimiwa Naibu Waziri anijibu mahsusi kwa eneo la Afrikana - Salasala - Kinzudi ambapo sasa hivi barabara imechimbika sana?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni mwaka wa
tatu mfululizo Manispaa ya Kinondoni haijapata fedha za Mfuko wa Barabara kutokana na makosa yaliyofanywa na ma-engineer wetu ambao walijenga barabara chini ya kiwango. Matokeo yake ni kwamba wananchi wa Kinondoni ikiwemo Jimbo la Kawe wanaathirika kwa sababu barabara ziko katika hali mbaya sana. Hawa ma-engineer wameshapewa adhabu zao, wengine wamesimamishwa kazi, wengine wamehamishwa vituo. Nataka Waziri atuambie ni lini fedha husika za miaka mitatu zitakuwa released ili maboresho ya barabara za Kinondoni yaweze kufanyika na kupunguza kero ya wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO): Mheshimiwa Naibu Spika, kuna tatizo la tafsiri ya mradi, nini maana ya mradi? Mradi unaanza na basic concept, feasibility study, detail design, ujenzi lakini mradi pia una operation na wakati wa operation ni operation and research. Nikiri kwamba Mheshimiwa Mbunge aliyoyasema ni kweli, ile barabara na mimi naitumia. Kwanza yeye ni Mbunge wangu maana nakaa Kinondoni. Tangi Bovu, Afrikana, Kilongowima na maeneo mengine maji yanapita pale lakini kipindi cha operation and research tayari mpaka sasa hivi Wizara imeshatambua maeneo hayo na inaanza kuingia mikataba. Kwa mfano, eneo la Tangi Bovu mkandarasi amepatikana kwa maana sasa ya kuboresha na kupanua ile sehemu ya kupitisha maji katika eneo la barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo tatizo lingine kwamba TANROADS inashughulikia eneo la hifadhi yake na kwa eneo lile hifadhi ni mita 80, 40 kila upande kutoka katikati ya barabara, nje ya hapo ni eneo la Halmashauri. Kipindi cha mvua kutokana na mabadiliko haya, mimi huwa nasema ni mabadiliko ya binadamu, storm water yanapotembea yanakuja na takataka nyingi sana zinaingia kwenye yale makalavati zinaziba, matokeo yake sasa maji hayapiti katika dizaini iliyotakiwa yanapita juu ya barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja yake pia amezungumzia kuhusu street light, nazo katika hiki kipindi cha operation and research need imeshaonekana. Kwa hiyo, Serikali italifanyia kazi ili wananchi wanaotembea usiku waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lipo hili suala ambalo mwenyewe amekiri kwamba kulikuwa na ubadhirifu na uzembe ama wa wahandisi ama wa watu gani kuhusiana na ujenzi wa barabara, wakajenga barabara ambazo haziko katika standard inayotakiwa. Ni kweli, kwani yeye Mheshimiwa Mbunge anapenda? Mtu ambaye anafanya kitu ambacho hakiko kwenye standard inayotakiwa lazima achukuliwe hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala kwamba fedha za Mfuko wa Barabara hazijaja mfululizo kwa miaka mitatu kwangu ni geni. Naomba nilichukue, nitaliwasilisha kwa wahusika ili waweze kuliangalia.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya ukatili na unyanyasaji mkubwa wa watoto wa kike ni wa kuwanyima fursa ya kurudi shuleni pale ambapo wanapata ujauzito kwa kuzingatia mazingira mbalimbali ambayo yanapelekea watoto wetu wa kike kupata mimba wakiwa watoto wadogo. Sasa ninatambua kwamba kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na cabinet yake, kuna initiative mbalimbali walizozifanya hali iliyopelekea kuanza utekelezaji wa re-entry policy, kwamba mtoto anapata mimba, anapata fursa ya kurudi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka tu Serikali iniambie, kwa kuzingatia kwamba kama viongozi, tuna wajibu wa kujali mustakabali wa mtoto wa kike; na kwa kuzingatia kwamba katika nchi yetu kuna mazingira mengi ambayo nikiyataja hapa siwezi kuyamaliza, yanayopelekea mtoto huyu kushindwa kusoma na kushindwa kuzuia hivyo vishawishi ama kushindwa kukabiliana na nguvu kubwa za nje ambazo zinamzidi uwezo wake wa akili; ni lini sasa Serikali itafanya utekelezaji wa ile kazi kubwa ambayo mlifanya katika kipindi cha miaka 10 iliyopita mpaka kipindi cha awamu ya Mheshimiwa Jakaya kilipoisha? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji kujua utekelezaji tu.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kulikuwa na maandalizi ya re-entry policy lakini utekelezaji wake sasa umepitwa na wakati kutokana na maagizo ambayo yametolewa na Serikali kwamba mtoto ambaye amepata ujauzito hataruhusiwa kurudi tena katika shule ambayo alikuwa anasoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maagizo haya hayajamzuia mtoto wa kike ambaye amepata ujauzito kutoendelea na masomo. Naomba tuelewane vizuri, imezuia mtoto wa kike kurudi shule ambayo alikuwa anasoma, lakini haijazuia mtoto wa kike kuendelea na masomo. Kwa hiyo, ndani ya Serikali tunajaribu njia mbadala ya kuhakikisha kwamba watoto hawa ambao wamepata ujauzito wanaendelea na masomo.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa maelezo yake mazuri kuhusiana na suala la watoto ambao wanapata ujauzito kurudi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama alivyosema ni kwamba Serikali imekwishaeleza kwamba mwanafunzi anayepata ujauzito hawezi kurudi shuleni, lakini mwanafunzi huyo anaweza akaendelea na masomo kwa kupitia njia mbadala ambazo tuna vituo vya elimu, zipo Taasisi zetu za Elimu ya Watu Wazima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, msimamo wa Serikali ni kwamba mwanafunzi hawezi kurudi shuleni lakini anaweza akapata masomo kupitia njia mbalimbali ambazo Serikali inazitoa. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, kufuatia ugunduzi wa gesi, Serikali ya CCM iliwahakikishia Watanzania na wananchi wa Mtwara kwamba maisha yetu kwa kiwango kikubwa yatabadilika. Ikumbukwe kwamba bomba la gesi lilijengwa kwa mkopo usiopungua shilingi trilioni 1.5 kwenda shilingi trilioni 2. Hivi tunavyozungumza na kwa taarifa za Serikali inaonesha kwamba tunatumia asilimia 5 tu ya gesi katika bomba husika. Nataka tu Serikali ituambie, Deni la Taifa linakua, tulikopa tukajenga bomba tukajua kwamba tunapata suluhu lakini sasa hivi tunatumia bomba asilimia 5, ni nini kimetokea hapo katikati kilichopelekea kushindwa kulitumia kwa asilimia 95 ? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaambiwa tena kuna mpango Stigler’s Gorge wa kuzalisha umeme. Sasa mtuambie bomba la gesi limekwamia wapi katika uzalishaji wa umeme na hii Stiegler’s Gorge inaanzia wapi ili kama Taifa tuwe na taarifa, maana tunaona tunapelekwapelekwa tu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa Halima Mdee, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilitekeleza mradi mkubwa huu wa ujenzi wa bomba la gesi la Mkoa wa Mtwara. Kama alivyoeleza kwenye swali lake, kwa sasa matumizi ya kusafirisha gesi kwa kupitia bomba hili kwa mwaka huu unaoendelea imefika lita za ujazo milioni 175 kutoka milioni 145 za mwaka 2016/2017, ni wazi ongezeko linatokana na mahitaji makubwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nimthibitishie tulipokuwa tunajenga bomba hili na ahadi tulizotoa kwa wana Mtwara, ahadi zile ni sahihi kwa sababu kuna miradi mbalimbali ambayo inayoendelea. Kwa mfano, Mtwara peke yake tunajega mradi wa kuzalisha umeme wa megawatts 300 kwa kutumia gesi asilia ya Mkoa wa Mtwara. Sambamba na hilo, pia kuna mpango wa kujenga mradi wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia Somanga Fungu, kwa kuzalisha megawatts 330 kwa kutumia gesi hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi yoyote lazima izalishe umeme kwa vyanzo mbalimbali, huwezi kutumia gesi asilia peke yake ukatosheleza mahitaji ya nchi nzima. Ndiyo maana tunazalisha umeme kwa kutumia maji na gesi. Sasa hivi zaidi ya asilimia ya 50 megawatts zinazozalishwa zinatumia gesi. Kwa hiyo, ni wazi kwamba gesi ambayo iligundulika Mtwara imeleta tija katika uzalishaji wa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kama tunavyofahamu umuhimu wa kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo vingine, Serikali imetafakari, kwa sababu lengo la Serikali ni kuzalisha umeme wa bei nafuu na kumfikia mtumiaji kwa bei nafuu. Ndiyo maana Serikali imekuja na mradi wa Stiegler’s Gorge utakaozalisha megawatts 2,100. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimewahi kusema ndani ya Bunge lako Tukufu kwamba uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji una unafuu zaidi, unatumia shilingi 36 ukilinganisha na gesi ambayo ni shilingi 147. Kwa nchi inayotarajiwa kujenga viwanda nchi nzima na kazi inayoendelea lazima tuzalishe umeme kwa wingi. Kwa kuwa lengo la Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli ni kuzalisha megawatts 5,000 mradi wa Stiegler’s Gorge ndiyo wakati wake muafaka. Mheshimiwa Spika, nashukuru. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, zalio la vyeti feki ni Chama cha Mapinduzi na Serikali yake, Mheshimiwa Rais akiwa ni sehemu ya CCM kwa kipindi chote hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Walimu ama Watumishi wengi walianza na cheti cha mtu wakaenda wakasomea taaluma, wakafaulu taaluma zao, wakaenda kulitumikia Taifa hili kwa miaka mingi sana. Serikali ya watu ni Serikali yenye ubinadamu. Sasa nauliza, hivi ni kweli Serikali ya CCM inadhani ni sahihi kwa watu ambao wametumikia hili Taifa kwa miaka 20, wengine mpaka miaka 40 wengine miaka 30, waondoke hivi hivi bila hata kupata kifuta jasho, wanadhani ni sahihi?
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri dada yangu ama mdogo wangu naye ni Mwanasheria. You cannot benefit from your own wrong, suala hili lilikuwa ni jinai, huwezi ukanufaika hata kama uliweza ku-penetrate katika mfumo ikafikia hapo na ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliweza kutoa amnesty na amnesty hii haikuweza kutoka bure.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Halima aweze kuelewa suala hili halijazalishwa tu hivi na Serikali ya CCM ni Criminal Offence na ilikuwa ni lazima kufanya hivyo. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Mheshimiwa Kalanga na Mheshimiwa John Mnyika, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; moja kati ya barabara muhimu za ring road ama barabara za pete ambazo zimeainishwa hapa ni barabara ya Goba kwenda Makongo – Chuo cha Ardhi, barabara hii kama ambavyo mnafahamu kwa siku yanapita magari zaidi ya laki moja (100,000) lakini vilevile ni barabara yenye umuhimu mkubwa sana pale ambapo tutakuwa tunajenga interchange ya pale Ubungo kwa sababu magari mengi yatahitaji barabara za kuweza kuchopoka kwenda Mbezi na hatimaye Morogoro Road.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nataka nipate majibu ya Serikali, kwa sasa zimejengwa kilometa nne tu halafu zinaonekana zime-stuck hakuna kitu kinachoendelea. Naomba majibu ya Serikali ni lini uendelezaji wa barabara kwa kilometa tano zilizobaki utafanyika kwa kiwango cha lami? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, maelezo ama majibu ya Mheshimiwa Waziri yanaainisha kama vile barabara ya Goba – Madale – Tegeta Kibaoni imekamilika, lakini ukweli ni kwamba barabara iliyokamilika ni kipande cha Goba, kipande cha Goba – Madale ndiyo kinajengwa sasa hivi kwa kilometa tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi nzuri ambayo inaanza sasa kufanywa, swali langu ni dogo, kiwanda cha Twiga kimekuwa kinafanya matumizi mabovu ya hii barabara kwa kupaki magari yake barabarani, hali ambayo inahatarisha uhai wa barabara, lakini inahatarisha uhai wa wananchi wetu. Kama Serikali ya mtaa imejaribu kuingilia kati, Serikali ya Kata imeingilia kati, Mbunge nimeingilia kati, lakini kiwanda kinaonekana ni kiburi. Nataka commitment ya Serikali kwamba itafuatilia kiwandani ili matumizi ya barabara yaachwe kwa ajili ya barabara na isihatarishe uhai wa wananchi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nashukuru kuona kuwa, Mheshimiwa Halima Mdee anatambua juhudi kubwa ambazo Serikali hii inazifanya katika kujenga barabara na kuweza kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyopitisha kwenye bajeti barabara zinazohusiana na kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam ziko kama kilometa 156, baadhi ya barabara zimekamilika lakini baadhi ya barabara juhudi zinaendelea kuweza kukamilisha. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Mheshimiwa Halima, hii barabara ambayo unaizungumzia barabara ambayo inapita Madale kwamba kuna kipande cha kilometa tano kinaendelea kukamilishwa, ni mpango wetu na hata ukiangalia kwenye bajeti ni kuweza kuikamilisha barabara hii nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimwombe tu avute subira na wananchi wavute subira, tunafahamu umuhimu na uharaka wa kutengeneza barabara katika Jiji la Dar es Salaam kupunguza msongamano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko awamu nyingi zitakuja, kila awamu ikikamilika ni fursa ya kuanza awamu nyingine ili hatimaye tumalize kabisa msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, amezungumza juu ya barabara kipande ambacho unasema kilometa tano kutoka Makongo Juu kwenda Chuo cha Ardhi, najua tunafanya juhudi ya kumaliza tatizo la compensation eneo lile ili wananchi waweze kupisha barabara ikamilike. Niseme tu kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam na watumiaji wa barabara kwamba, ni mkakati wa Serikali kwamba wakati wa ujenzi wa interchange ya Ubungo barabara hiyo anayoitaja Mheshimiwa Mbunge ni muhimu sana. Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba tunapunguza msongamano kipindi chote cha ujenzi wa barabara pale Ubungo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana hiyo Serikali tunaona uko umuhimu na kwa haraka sana kukamilisha barabara hii. Kwa hiyo avute tu subira, barabara hii tutaitengeneza pamoja na barabara zingine. Iko mipango mingi tu mizuri katika kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Halima, akisoma pia kwenye hotuba ya bajeti ambayo Mheshimiwa Waziri aliwasilisha hapa ukurasa wa 17 hadi wa 18 na ukurasa wa 25 ataona mambo mazuri yaliyoko huku. Angepitia tu ili aone namna tulivyojipanga kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inabakia vizuri barabara zinakuwa zinawasaidia wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiwanda cha Twiga Cement kupaki magari, naomba nilichukue hilo, lakini niseme tu kwamba tunao mpango kabambe wa kuwashughulikia wanaotumia barabara vibaya katika Jiji la Dar es Salaam, pia tunafanya patrol na kwenda na mizani ile ya kuhama.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe tu watumiaji wa magari, siyo hao wa barabara hii lakini na maeneo mbalimbali ambao na wengine wanatumia wakati wa usiku. Tumeshaliona hilo tunalifanyia kazi ili kuhakikisha kwanza magari yanaegeshwa vizuri kwa ajili ya usalama, lakini pia kwa ajili ya kufanya barabara zetu zisiweze kuharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hili nimelichukua nakushukuru tutaendelea kulifanyia kazi ili tuweze kuondosha hili tatizo. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya barabara ambazo zina changamoto ya muda mrefu, lakini ni muhimu sana ni barabara ya Makongo kwa mantiki ya kwamba UCLAS, Makongo Juu kwenda Goba, hii barabara nimeuliza kwenye swali la TAMISEMI kwa sababu ni barabara ya halmashauri, lakini ina hudumiwa na TANROADS kwa mantiki ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba zoezi la tathimini ya kulipa fidia wananchi limeshakamilika, lakini lime stuck kwa muda mrefu. Sasa kwa sababu ya umuhimu wa hii barabara na ni barabara ya kimkakati kwa sababu inasadia kupunguza foleni wakati wa ujenzi wa madaraja pale njia ya Ubungo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka sasa Waziri aniambie; ni lini ujenzi wa barabara hii utakamilika kumalizia kipande ambacho kimeshaanzwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba katika ujenzi wa barabara kuna hatua mbalimbali na katika huu mradi wa DMDP lazima ipatikane no objection kwa kila hatua. Pale ambapo fidia inatolewa nafasi ili kama kuna malalamiko mengine ambayo yatakuwa yame-raise, baada ya kuwa sorted out ndipo tunaendelea na hatua ya pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Halima, na bahati nzuri swala hili tumekuwa tukiwasiliana hata na Mheshimiwa Susan Lymo naamini na yeye labla anaishi maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea na Meneja wa TARURA kwanza kufanya marekebisho kwa muda wakati wa ujenzi mwingine unasubiriwa. Naomba avute subira, ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa; lakini pia kusiwe na malalamiko kutoka kwa wananchi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya maeneo ambayo kulikuwa kuna viwanda vya Tanganyika Packers ni Jimbo la Kawe, Kata ya Kawe ambayo miaka sita iliyopita kwa kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nne tulifanikiwa kuliokoa eneo husika kutoka kwa waliokuwa wawekezaji uchwara na hatimaye Shirika la Nyumba la Taifa likakabidhiwa kupewa jukumu la kujenga Kawe Mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tokea Awamu ya Tano imeingia madarakani…
Mheshimiwa Mwenyekiti, tokea Awamu ya Tano imeingia madarakani, mradi ule ambao ulikuwa unahusisha nyumba zaidi ya 50,000 ni kama vile umekwama, matokeo yake eneo lile linakuwa kama sehemu ya genge la majambazi na wahalifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka Serikali iniambie, ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba ujenzi wa Kawe Mpya ya kisasa unafanyika kama ambavyo ilikuwa ni katika mpango wa miaka mitano na mwaka mmoja mmoja wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mpango wa Serikali kujenga nyumba kama ilivyokuwa imepangwa kwa National Housing ulikuwa umepangwa na ulikuwa unaendelea vizuri, lakini mpango ule ulisimama baada ya kuja kuongeza nguvu katika ujenzi wa nyumba za Makao Makuu hapa Dodoma. Hata hivyo, kwa sababu suala zima la ujenzi wa nyumba za hapa Dodoma unaendelea vizuri, miradi mingine yote iliyokuwa imesimama sasa hivi wataanza kuitekeleza kwa sababu utaratibu tayari umeshawekwa vizuri.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya barabara ambayo nimeizungumza sana na Mheshimiwa Waziri pamoja na TAMISEMI wanajua, ni Barabara ya Chuo cha Ardhi – Makongo - Goba. Imekwama kutengenezwa kwa sababu ya fidia, sasa nataka Waziri aniambie, ni lini kipande hicho kitalipwa fidia ili wananchi wa Makongo waweze kujengewa barabara ya lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali na nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa sana imefanyika kuboresha miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam na Mheshimiwa Mbunge anafahamu. Changamoto ambazo zimebaki ni kulipa fidia kwa hizi kilometa nne zilizobaki. Barabara hii ni muhimu kwa sababu tunavyojenga barabara ya juu pale Ubungo, barabara hii itatumika pia kupunguza msongamano ili kufanya ujenzi uende kwa haraka. Tunatambua umuhimu huo, kwa hiyo nimwombe tu Mheshimiwa Mdee avute subira, suala hili tunalifuatilia kwa umakini kuhakikisha kwamba kipande hiki kinatengenezwa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri wakati anatoa majibu yake ametaja kama mamlaka nne hususan kwenye suala la mchanga. Ametaja Wizara ya Mazingira ambayo kuna NEMC, ametaja Wizara ya Nishati na Madini, ametaja halmashauri lakini vilevile kuna kitu kingine kinaitwa Bonde ama Pwani Ruvu Bonde.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ya usimamizi wa mito yetu ni kutokana na ukweli kwamba si NEMC, si halmashauri, si Wizara ya Nishati na Madini ina mamlaka ya moja kwa moja ya ku-deal na masuala ya mchanga. Ni Pwani Ruvu Bonde ambayo ofisi zake ziko Morogoro ndiyo inaingia mikataba na watu wa kuchimba mchanga kwenye halmashauri zetu. Wananchi wetu wakipata mafuriko wanaenda halmashauri wakijua halmashauri inaweza ikawasaidia, wanajua NEMC inaweza ikawasaidia lakini ukweli ni kwamba Pwani Ruvu Bonde ndiyo inafanya kila kitu na kuchukua mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu kwa Serikali, kwa kuzingati hizo changamoto nilizozizungumza ni lini sasa mtabadilisha sheria zilizopo ili kuwe na mamlaka moja yenye usimamizi ili hili suala liweze kudhibitiwa vizuri? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, takataka za Dar es Salaam pamoja na maelezo yote mazuri na matamu uliyoyeleza ni ukweli kwamba Dar es Salaam yenye wakazi wasiopungua milioni tano, yenye majimbo kumi ya uchaguzi, yenye wilaya kubwa tano lina dampo moja tu ambalo liko Pugu Kinyamwezi; na dampo hilo liko katika hali mbaya sana. Sasa nilitaka Serikali ilieleze Bunge hili Tukufu ina mkakati gani wa kuhakikisha…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Halima malizia swali lako.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Serikali katika majibu yake inipe majibu serious, kwamba ina mpango gani wa kujenga madampo mengine makubwa. Kama inashindwa kujenga katika kila jimbo basi at least kila wilaya iwe na dampo kubwa ili taka ziweze kwenda kutupwa kwa uharaka na kuzuia uchafu. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile ni mara yangu ya kwanza nasimama kwenye upande wa Serikali, kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetujalia wote viumbe vyake. Nimshukuru Mheshimiwa Rais kuwa na imani kubwa sana na mimi kuniweka kwenye wizara nyeti kama hii, lakini mafanikio yangu na mafanikio yetu wote ni kushirikiana, tufanye kazi kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nitajibu swali namba mbili la Mheshimiwa Mbunge Halima Mdee. Ni kweli crisis ya taka katika Mkoa wa Dar es Salaam ni kubwa, si ndogo na Dar es Salaam inakuwa sasa hivi kwa asilimia kubwa sana. Kwa miaka miwili ijayo Dar es Salaam itakuwa na population siyo chini ya watu milioni nane mpaka tisa na dampo ni moja. Juzi mimi nimekwenda kwenye dampo, hali ya dampo ni mbaya lazima tukiri ni mbaya, miundombinu ni mibaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, hatua zimeshachukuliwa. Halmashauri ya Jiji imeshatoa fedha kujenga barabara ya lami katika eneo lote la dampo lakini baada ya hapo kuna mradi ambao unafadhiliwa na donors wa bilioni 75 fedha ambazozimeshakuja. Fedha hizi zimeshawekwa ili ziweze kuboresha dampo jipya la kisasa ambalo litaweza kubeba taka zote za Mkoa wa Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nim-assure Mheshimiwa Mbunge, Serikali iko kazini na Serikali iko makini kuhakikisha kuwa dampo hili linajengwa na fedha ziko tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu haya namwambia akae chini sasa. (Makofi/Kicheko)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali dogo la kwanza la Mheshimiwa Halima Mdee. Kwanza nakubaliana naye, wanaotoa kibali na siyo cha kuchimba mchanga cha kusafisha mto ni Bonde. Ukishautoa ule mchanga kwenda nje maana yake Wizara ya Madini wanatoa kibali kingine kwa hiyo unapaswa kulipia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Ofisi ya Makamu wa Rais kwa maana ya kupitia NEMC tunaowajibika sasa kusimamia athari ya mazingira na uhidhi wa maeneo hayo. Sasa nakubaliana naye kwamba umefika wakati lakini pia Ofisi ya Makamu wa Rais ilishaunda Kamati na kamati hii ilijumuisha wadau wote na imekuja na mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya mapendekezo ni kuwa sasa na mbadala wa mchanga, hasa kwenye maeneo ya ujenzi sasa hivi, kwenye kokoto ile vumbi ya kokoto ianze kutumika barabarani ili iweze kutumika badala ya mchanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, hata tunapojenga haya majengo yetu sasa tunaanza kutumia vyuma; na baada ya hapo kamati ile pia imependekeza iwepo sasa sheria maalumu na kuwe na bodi moja mbayo inaweza kusimamia zoezi hili. Kwa hiyo nakubaliana naye. Nashukuru.

NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri mwenzangu wa Wizara ya Mazingira nipende tu kumtaarifu Mheshimiwa Halima Mdee, Mbunge kwamba hata sisi kwa upande wa Wizara ya Madini tunatoa leseni za uchimbaji wa mchanga tofauti na leseni nyingine. Leseni nyingine tunatoa miaka kumi ya uchimbaji wa madini mengine na leseni nyingine tunatoa kwa muda wa miaka saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa leseni ya uchimbaji wa mchanga tunatoa kwa muda wa mwaka mmoja mmoja. Maana yake nini; ni kwamba kila tunapotoa leseni katika maeneo fulani basi tunaangalia vilevile na athari za mazingira kwa kushirikiana na Wizara ya Mazingira, na tunapoona kwamba eneo hili halifai basi kwa mwaka unaofuata hatutaweza kutoa leseni hiyo. Kwa hiyo tunatoa muda mfupi mfupi huku tuki- monitor mazingira yanavyokwenda katika maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunapotoa sisi leseni za uchimbaji tunategemea kabisa na mamlaka nyingine ikiwemo mamlaka za halmashauri na mamlaka nyingine ambazo zinalinda mabonde, tunashirikiana kwa pamoja katika kutoa vibali. Tunapokuwa tunaona kwamba eneo hili tunakubaliana kwamba mtu achimbe mchanga tunakuwa tumekubaliana kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoona kwamba kuna athari inaweza kutokea katika uchimbaji wa mazingira, basi mamlaka ile nyingine tunashirikiana nazo kuhakikisha kwamba tunafuata maamuzi ambao wanaona na wao kwamba kuna athari au hakuna athari katika maeneo yale ya uchimbaji wa mchanga. Ahsante sana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni mara ya 15 nauliza kuhusiana na barabara muhimu sana ya Chuo cha Ardhi – Makongo – Goba. Mara ya mwisho nilijibiwa tukiwa tunaelekea kwenye Uchaguzi wa Serikali ya Mtaa ambapo Mkuu wa Mkoa alienda na mkandarasi wakaweka vifaa pale wakawaambia wananchi barabara itajengwa watalipwa fidia. Leo baada ya uchakachuzi mkandarasi ameondoka, ile lami kilometa moja ambayo tulijenga Halmashauri imekwanguliwa, wananchi hawajui mustakabali wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi kama mwakilishi wao, naomba Waziri anipe jibu na jibu liwe la ukweli na uhakika, ni lini barabara ya Makongo inayoanzia Chuo cha Ardhi – Makongo Juu – Goba itajengwa kwa kiwango cha lami na wananchi kulipwa fidia yao wanayostahili? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara ya Makongo tayari tumeanza kuijenga, kama unavyosema ni kweli mitambo ilienda lakini huwezi ukajenga barabara katika kipindi cha mvua nzito, huo ndiyo utaratibu, hiyo ndiyo sayansi yake, kwa sababu udongo unakuwa umeloana, kuna kiwango maalum kinachohitajika kwenye maji ya ujenzi wa barabara, huwezi ukafanya ushindiliaji kama moisture content iko high.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuhusiana na suala la fidia, kwa vile tumeshasaini mikataba tayari fidia ni lazima ilipwe. Huwezi ukajenga barabara bila kulipa fidia lakini pia fidia italipwa kwa mujibu wa sheria. Kama kuna mtu alijenga ndani ya hifadhi ya barabara hatuwezi kumlipa lakini yule ambaye tumemfuata, alikuwa yuko nje ya hifadhi ya barabara, huyo lazima tutamlipa, kwa hiyo fidia italipwa kwa mujibu wa sheria.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, Moja kati ya barabara ambazo ni muhimu sana hasa katika foleni za Dar es Salaam ni barabara ya Chuo cha Ardhi - Makongo – Goba. Ninatambua kwamba baada ya kero ya muda mrefu sana hatimaye barabara itaanza kujengwa. Sasa swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, changamoto kubwa iliyopo ni fidia ya wananchi ya shilingi bilioni 3 na tumekuwa tukizungumza kwa kipindi kirefu sana.

Mheshimiwa Spika, nilitaka nipate commitment ya Serikali ni lini wananchi hawa ambao wako tayari kuachia maeneo yao watalipwa fidia yao stahiki ili barabara ijengwe kwa viwango ambavyo ilikuwa imetarajiwa kujengwa?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja la Mheshimiwa Mbunge Halima kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeanza kujenga ile barabara ya Makongo lakini kuhusiana na swali lako fidia italipwa kwa mujibu wa sheria, sheria ipo ilitungwa na Bunge. Kwa hiyo, siyo commitment ya mtu hapana, kwa mujibu wa sheria.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, wakati Mheshimiwa Naibu Waziri anajibu maswali amezungumzia neno elimu bure, lakini najua anajua tofauti kati ya elimu bure na elimu bila kulipa ada. Nazungumza hivi kwa sababu kinachofanyika mashuleni huko wanafunzi na wazazi wanatozwa fedha ama za kulipa mlinzi ama za kulipa maji ama za kulipa walimu wa sayansi ambao wanawatafuta wa ziada ama masomo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nataka Serikali iweke hoja wazi kabisa hapa mezani, kinachofanyika ni elimu bila kulipa ile ada ya Sh.20,000 na Sh.70,000 na siyo elimu bure, ili wazazi wanapochangia huko wajue kwamba wao kwenye mchakato wa elimu ya Tanzania wana-stake yao ya kuchangia na Serikali ina stake yake ya kuchangia. Kwa hiyo, aweke wazi hapa ni elimu bila ada na sio elimu bure. Sasa kwa tafsiri ya kamusi bure ina maana yake na ada ina maana yake. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza kwenye majibu yangu ya msingi, Waraka Namba 5 wa mwaka 2015 ulikuwa unaeleza kwamba elimu bila malipo kwa elimu ya awali mpaka kidato cha nne.

Mheshimiwa Spika, lakini kuna michango ambayo huenda ikawa inatokea huko ambayo ni michango ya hiari…

SPIKA: Ngoja Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa hiyo, ni elimu bila malipo siyo elimu bure.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, elimu bila malipo. (Makofi)

SPIKA: Nisikuwekee maneno mdomoni Mheshimiwa Naibu Waziri, nilitaka tu uweke vizuri, hebu rudia wewe mwenyewe.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, nilikuwa nazungumzia Waraka Namba 5 wa mwaka 2015 unaeleza kwamba elimu ya awali mpaka elimu ya kidato cha nne itakuwa ni elimu bila malipo, tafsiri yake ni elimu bure. Kwa hiyo, waraka huo unaeleza hivyo.

Mheshimiwa Spika, katika muktadha huo, amezungumzia kwamba kuna michango wazazi wanachangishwa ya walinzi, usafi au ya vitu vingine, naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kuwa Serikali katika Waraka ule imebainisha wazi kwamba michango ile yote ambayo mzazi alikuwa anachangia katika kipindi cha nyuma katika maeneo haya ya elimu ya awali kwa hivi sasa haipo na gharama hizo zinakwenda Serikalini.

Sambamba na hilo, nadhani keshawahi kusikika Mheshimiwa Waziri wa Elimu lakini Mheshimiwa Rais ameshawahi kuzungumza mara nyingi sana, kama mzazi au mlezi ana mchango wa aina yoyote ambao anaona bora au inafaa mchango huo autoe ni vema aufikishe au auwasilishe kwa Mkurugenzi ambapo yeye atapanga kitu gani cha kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikijinasibu kwamba mikopo hii inalenga kusaidia watoto wa familia maskini lakini kimsingi mikopo hii inakuwa ni mzigo kwa watoto wa familia maskini. Muuliza wa swali msingi amezungumzia asilima 15 ya makato kila mwezi, amezungumzia asilimia 10 ya interest rate kwa watu ambao ndani ya miezi 24 wameshindwa kulipa, kuna asilimia 6 ya interest kwa watu ambao wanalipa. Sasa matokeo yake ni kwamba badala ya kuwa ni mkopo wa kusaidia watoto unakuwa ni mkopo wa kibiashara.

Sasa ni lini Serikali italeta hapa Bungeni mabadiliko ya kisheria ili kile kinachosemwa kusaidia watoto maskini kithibitike kwa maneno na kwa vitendo na isiwe lugha za kisiasa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, katika urejeshaji wa mikopo hii mnufaika anapaswa kukatwa asilimia 15 katika gross salary yake ambayo makato haya yalipitishwa katika Bunge lako hili Tukufu. Lakini vilevile kuna hizo alizozitaja Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna hiyo asilimia 10 kwa wale watakaochelewa na asilimia sita.

Lakini kama nilivyojibu katika maswali ya nyongeza yaliyopita, kwamba tunakwenda kufanya review ya kanuni hizi na kuweza kuangalia namna gani tunaweza aidha kuondoa au kupunguza. Kwa hiyo, tunaomba tuachie ili jambo hili tukalifanyie kazi; na tuwe watulivu ili kuhakikisha mikopo hii haiendi kuwa kero kwa watumishi wetu maskini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza na mpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa maswali mengi ambayo yameelekezwa na ameyajibu kwa ufasaha. Jambo dogo tu nilikuwa nataka niweke kumbukumbu ili kwenye Hansard ikae vizuri.

Nilikuwa nataka tu kueleza kwamba, katika mkopo wa mwanafunzi analipa asilimia sita kama tozo ya kutunza thamani, lakini hakuna riba ya asilimia 10 kama ambavyo ilikuwa imeelekezwa, na hiyo asilimia 6 ndiyo hiyo ambayo tunaifanyika kazi. Nilikuwa ninaomba kumbukumbu zikae vizuri. Asilimia 15 ni makato ya mshahara kila mwezi, lakini ile riba iliyokuwa inatajwa ya asilimia 10 niombe niweke kumbukumbu vizuri hiyo haipo. Ahsante sana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, miaka ya mwanzo ya 2000, Serikali kupitia Wizara ya Ardhi ilikuwa na miradi ya viwanja 20,000, ambapo kwenye Jimbo la Kawe ilihusisha Kata ya Mbweni na Kata ya Bunju.

Mheshimiwa Spika, wananchi wakati wanalipia viwanja moja kati ya ahadi ya Serikali ilikuwa ni kutengeneza barabara za ndani. Hata hivyo, mpaka sasa hivi barabara nyingi za ndani za Kata hizi za Mbweni na Bunju kwenye mradi wa viwanja 20,000 bado ipo katika hali mbaya. Ninataka tu commitment ya Serikali kama itaenda kufanya uchunguzi na kuweza kwenda kufanya utaratibu wa kutengeneza barabara moja baada ya nyingine, kwa sababu wananchi walilipia kwenye viwanda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima James Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge alichokuwa anakitaka hapa ni ahadi ambayo ilitolewa na Serikali katika miaka ya 2000 ya kutengeneza barabara za ndani katika maeneo ya Bunju na Vijibweni. Mimi nimwambie tu kwamba tumepokea kile alichokisema, kwamba anataka commitment ya Serikali, na sisi tunakubali kwenda maeneo hayo, tutakwenda kufanya tathmini kujionea hali ili tuone na bajeti jinsi ambavyo tutakavyopanga kutekeleza ahadi ya Serikali ambayo ilikuwa imepangwa kwa wakati huo. Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nimshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, nataka tu nimfahamishe Mheshimiwa Mdee kwa swali lake kwamba, ni kweli mradi huo ulikuwepo, lakini baadaye miradi yote kutoka kwenye Wizara tumeirudisha kwenye mamlaka za upangaji. Kwa hiyo ni jukumu pia la Halmashauri husika kuwasiliana na watu wa TARURA kwasababu zile zinakuwa zipo chini ya TARURA ili TARURA waweke kwenye mpango ili ziweze kufunguliwa kama ambavyo ilistahili kuwa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, upungufu wa vifaa tiba ulioko Geita upo vilevile kwenye hospitali nyingi kama sio zote za wilaya, za mikoa, rufaa katika kukabiliana na janga la Covid - 19 hususan mitungi ya oxygen wananchi wengi wanakufa kwa kukosa mitungi ya oxygen. Sasa nilitaka Serikali iniambie wana mkakati gani wa dharura wa kuhakikisha hospitali hizi zinapata mitungi ya oxygen ili wananchi wenye uhitaji wa oxygen wasife kwa kukosa oxygen?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima James Mdee Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na upungufu wa baadhi ya vifaa tiba katika vituo vyetu na hospitali zetu za kutolea huduma za afya na Serikali katika mida tofauti na katika bajeti tofauti imeendelea kuweka mikakati ya kutosha kwanza kwa kuongeza sana bajeti ya dawa, vitendanishi na vifaa tiba. Kwa mfano katika miaka mitano iliyopita mpaka sasa tumeongeza bajeti kwa zaidi ya mara tisa kutoka bilioni 30 mpaka bilioni 270.

Mheshimiwa Spika, lakini tunatambua kwamba kweli bado kuna changamoto ya vifaa tiba na hususan mitungi ya oxygen kama ulivyotamka na tumeweka mpango mkakati sasa wa kuhakikisha kwamba hospitali zetu za halmashauri zinakuwa na mitambo ya kusindika gesi ya oxygen pia kuhakikisha hospitali za rufaa za mikoa zote nchini zinasimika mitambo ya kuzalisha gesi ya oxygen ili tuweze kuondokana na changamoto ya upungufu wa mitungi hii pia kuhakikisha tunaboresha huduma za afya kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo mpango huu utakwenda kutekelezwa nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafanyia kazi hayo ili kuhakikisha tunaboresha huduma za afya, ahsante sana.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anajibu swali alisema kwamba, kesi zinachelewa kwa sababu kuna vyombo mbalimbali vinachakata. Lakini labda nikuulize Mheshimiwa Waziri, hivi kuanzia mwaka 0 mpaka miaka 7, vyombo kuendelea kuchakata wakati watu wako magereza, unadhani ni sawa? na kama si sawa, kwanini sasa, badala ya kutoa maagizo hapa Bungeni usiwe ni wakati muafaka kwa Serikali kufanya kazi ya ziada kwenda kuchunguza kinagaubaga ili kuja na majibu ambayo yatasaidia wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, muda wa kukaa mahabusu utategemea mwenendo wa upelelezi, na hivyo ni halali kabisa wakati mtu anapelelezwa, ambaye atakuwa yuko nje ya vigezo vya dhamana kuendelea kuwa chini ya Magereza. Kwa hiyo muda unaangaliwa na uzito.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, kuhusu uchunguzi, kwamba tuunde timu ambayo itasaidia kuangalia kwa ukaribu na kwenda kufanya utafiti wa kina badala ya kutoa maagizo Bungeni; hapa nilikuwa natoa kama msisitizo tu lakini ukweli Serikali tulishaanza hiyo kazi na ukweli kwa kipindi hiki cha kuanzia Januari mpaka sasa naamini wazi watu wote mnaona kasi ya kuondoa mahabusu wasiokuwa na kesi zenye mashiko imeongezeka sana na mahabusu zimeanza kupumua. Ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri kabla haujawa Mbunge na hatimaye Naibu Waziri tulikuwa wote Manispaa ya Kinondoni; na unafahamu kwamba tulikuwa tuna mpango wa kujenga stendi Kata mashuhuri ya Kawe yenye wananchi wengi sana. Sasa, sasa hivi umeshakuwa Naibu Waziri upo huko kwenyewe huko. Sasa naomba uniambie, kwa sababu mkakati wa Kinondoni unaujua, ni lini tutajenga Stendi ya Kawe? Kwa sababu tuna eneo la iliyokuwa Wizara ya Mifugo na eneo la Tanganyika Packers. Ni lini tutajenga stendi Kata ya Kawe? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri Dkt. Dugange kwa majibu mazuri, lakini nimshukuru Mheshimiwa Halima Mdee kwa swali lake, kwamba lini tutajenga stendi katika Kata ya Kawe.

Mheshimiwa Spika, nimesimama, tulipata maelekezo kutoka kwa Kamati yako ya Bajeti lakini pia Kamati ya Utawala na TAMISEMI kwamba tufanye mapitio ya mwongozo wa kutekeleza miradi ya kimkakati nchini, kwa sababu inavyoonekana mwongozo ule unazipendelea Halmashauri zenye mapato makubwa na kuzifanya Halmashauri zenye mapato madogo kutopata rasilimali fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, halafu fedha hizi ni grant, ukipewa hazirudi; kwa hiyo tulijadili, na sisi tumekubaliana na ushauri wa Kamati. Unamuacha Makete, unampa Kawe, Kinondoni ambaye ana mapato ya zaidi ya bilioni 30. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge, Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha tunapitia mwongozo ili halafu sasa tuweke vigezo vya jinsi ya ku-finance miradi ya kimkakati ili hata Halmashauri zisizo na fedha na mapato ya kutosha waweze kupata fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa stendi, masoko na vitega uchumi vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Kawe itasubiri kwa kuwa kipaumbele chetu tutaangalia uhitaji wa Halmashauri maskini au zenye mapato madogo Zaidi. Ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nina maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza. Sekta ta kilimo ni sekta ambayo inaajiri kati ya asilimia 65 hadi 70 ya Watanzania, hii ni robo tatu ya Watanzania wanategemea hii sekta moja kwa moja, directly ama indirectly. Lakini sasa ukiangalia mikopo iliyotolewa kwa sekta binafsi kwa mwaka huu uliopita eneo la kilimo ambalo linategemewa na asilimia 65 mpaka 70 ya Watanzania limepata asilimia 8.7 tu ya mikopo yote iliyotolewa kwa sekta binafsi. Sasa na hii inajumuisha Benki ya Kilimo yenyewe pamoja na hizi benki nyingine. Sasa hiki ni kiashiria kwamba, mazingira ya kibenki sio rafiki kwa wakulima.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, kwa kuzingatia haya, Serikali ina mikakati gani, mosi kuiongezea mtaji benki ya kilimo, lakini pili kuzungumza sasa na mabenki haya mengine ya biashara ili kuwe kuna riba rafiki ili wakulima waweze kukopa mikopo? Hilo la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili, Benki ya Kilimo ni miongoni mwa benki ambayo ina mikopo chechefu sana, na taarifa ya CAG iliyopita imeonesha kwamba, kati ya mikopo chechefu ya shilingi bilioni 129 iliyorekodiwa ni mikopo chechefu ya shilingi bilioni 2.1 tu iliyoweza kukusanywa. Sasa Serikali ina mkakati gani basi, kuhakikisha kwamba, hii mikopo inakusanywa ili kutoa nafasi kwa wakulima wengine kuweza kukopa na benki kuendelea kama kwaida? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali maswali aliyoyasema. Na kipengele cha pili cha swali lake ndio kinatoa majibu ya kipengele cha kwanza kwamba, ni kwa nini inaonekana mikopo inayokwenda kwenye sekta hiyo ni kidogo:-

Mheshimiwa Spika, sababu yake ni hiyo ambayo umeweza kuona kwamba, hata Mdhibiti, CAG, aliweza kuonesha kwamba, sekta hiyo inaongoza kwa mikopo chechefu.

Mheshimiwa Spika, na sababu kubwa na ameuliza mkakati ni nini wa Serikali:-

Mheshimiwa Spika, utasikiliza mara kwa mara Waziri wa Kilimo amelisemea ni kuibadilisha sekta nzima, ili itoke kwenye ubahatinasibu kwenda kwenye uhakika. Na sehemu ya kwanza ambayo Mheshimiwa Waziri wa kilimo ameweka mkazo, kama ambavyo Mheshimiwa Rais ameelekeza nguvu ielekezwe, ni kuanzia na mbegu bora zenyewe. Kwamba, mtu anapokopa halafu akaenda kuwekeza kwenye kilimo, halafu akatumia mbegu bora ana uhakika wa kupata kutokana na kile kilichowekezwa. Kwa maana hiyo sekta nzima ikibadilishwa ikawa sekta ya uhakika, mbegu bora, kilimo cha umwagiliaji, matumizi bora ya zana za kilimo pamoja na uhifadhi pamoja na masoko, ukiukamilisha ule mnyumburisho wote maana yake unamfanya yule aliyekopa akawekeza kwenye kilimo awe na uhakika wa kurejesha.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo utaratibu ule utakapokuwa umekamilika kwa kuanzia na hilo la mbegu bora pamoja na vingine ambavyo viko kwenye mpango wa sekta ya kilimo vitawezesha sekta hiyo iwe ya kutabirika na ya uhakika na hivyo, itawezesha mtu aweze kukopa. Na ikishakuwa ya uhakika hata benki zitakuwa na uhakika wa kukusanya kutokana na hiyo kwa hiyo, riba zitakuwa rafiki.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali kuiwezesha, kuiwekea nguvu; tutaendelea kuliangalia kwa sababu ni moja ya kipaumbele ambacho tunalenga ili kuweza kuwezesha uchumi wa viwanda, lakini pia kukuza kipato cha kila Mtanzania, ili tuweze kusonga mbele kiuchumi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto wanazokabiliana Maafisa Ugani mbali na kwamba hawana vifaa, mbali na kwamba wapo wachache lakini wengi hawana ujuzi wa kukabiliana na mazingira ya kisasa. Na tafiti mbalimbali za Serikali zimeonesha kwamba asilimia zaidi ya 90 ya Maafisa Ugani wanatumia zile skills ambazo walikuwa wamepewa shuleni.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilitaka Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie ni lini basi Serikali itakuwa na mkakati madhubuti wa mafunzo ya maafisa Ugani wetu ili waendane na mazingira ya sasa ya ushindani wa Kilimo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kwa muda mrefu maafisa ugani wetu kuna gape kati ya technology advancement na elimu waliyonayo. Kwa hiyo, kama Wizara hatua ya kwanza tuliyochukua na mtaiona katika Mpango wetu wa bajeti mwaka huu ni pamoja na kuwapatia vitendea kazi, tutawapatia soil kit kila Afisa ugani ambaye anafanyia kazi katika eneo lake, tutampatia pikipiki lakini training ambayo tutaifanya, tutafanya training ya darasani kwa ajili ya kuwa-equip na technology na knowledge za sasa hivi kutokana na mazao na ecology ya eneo ambalo anafanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vile vile kila afisa ugani atakuwa na shamba darasa yeye mweyewe ambalo yeye Afisa Ugani atalisimamia lile Ushamba katika eneo lake kutokana na zao linalozalishwa pale ili liwe ni sehemu ya kufundisha wakulima na gharama za uwekezaji zitatolewa na Serikali katika eneo hilo kwa kumwezesha mbegu, kumwezesha madawa na kumwezesha… ili kuwe kuna- practical experience ambayo wakulima wanaiona na yeye mwenyewe anai-practice kwa hiyo, training ni sehemu ya muhimu na tumeanza repair ya chuo chetu cha Bihawana hapa sasa hivi ambacho kitatumika kwa ajili ya kuwafundisha Maafisa Ugani continues kutokana na mahitaji ya soko na dunia.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa mujibu wa taarifa ya TCRA asilimia 68 ya Watanzania wako kwenye maeneo yenye mtandao wa kuweza kutoa huduma ya internet, lakini ni asilimia 26 tu wenye simu janja ama vifaa vingine vyovyote vinavyoweza kuwapa access ya internet. Sasa na changamoto kubwa ni kwa sababu ya kodi na vitu vinavyofanania hivyo, sasa kwa kuzingatia kwamba Wizara inataka kuifanya Tanzania iwe katika utaratibu wa kidijitali, wana mkakati gani basi wa kuhakikisha huduma hizi zinapatikana kwa gharama nafuu, ili Watanzania wengi waweze na kuwa na hivi vifaa na hatimaye kuweza kushiriki katika dunia ya TEHAMA na kidijitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge alivyosema tuna changamoto hiyo kwa sasa, lakini sasa Serikali tunafahamu kwamba tunaenda kwenye uchumi wa kidijitali, lakini tunapoenda kwenye mfumo wa kidijitali maana yake ni kwamba tunahitaji kuwa na internet penetration na mpaka 2025 tufikie tuwe tumeshafikia asilimia 80 kutoka asilimia 43 ya sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, maendeleo ya dijitali yoyote yanaendana na vifaa ambavyo vita-support matumizi halisi ya teknolojia husika. Mheshimiwa Mbunge pia anafahamu kwamba, tuko kwenye mchakato wa kuangalia namna bora ambayo itasababisha vifaa hivi vitakapokuwa vinaingia nchini, basi viwe vina bei ambazo zitawavutia Watanzania wengi kununua hizi simu ili waweze kutumia teknolojia ambayo itakuwa inatumika. Ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, nikiwa mwakilishi wa Jimbo la Kawe mwaka 2010 mpaka 20 tulifanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kupunguza tatizo la maji, lakini kuna kata kadhaa ambazo zimebaki bado ni sugu sana. Kata ya Wazo, hususan maeneo ya Nyakasangwe, Mivumoni, Salasala, Kata ya Mbezi Juu eneo la Mbezi Mtoni na Sakuvede. Sasa nataka tu commitment ya Waziri ni lini changamoto hii itafikia ukingoni? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nijibu swali na ninashukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kukiri kwamba kuna jitihada kubwa ambayo Serikali imefanya katika Jiji la Dar es Salaam na nikiri bado kuna changamoto katika eneo la Mivumoni na maeneo ambayo ameyataja ya Wazo, lakini kuna kazi kubwa ambayo inafanywa juu ya utandazaji wa miundombinu na usambazaji wa maji inayofanywa na DAWASA, zaidi ya kilometa 1,600 ambazo tutaenda kutekeleza. Nataka nimhakikishie sisi kama Wizara tutasimamia kuhakikisha maeneo haya yanapata maji kwa haraka na wananchi waweze kupata maji, ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika nashukuru, changamoto ambayo inakumba Sikonge ya ujenzi holela inakumba pia jiji la Dar es Salaam sasa tofauti na Sikonge Dar es Salaam tayari tuna Dar es Salaam City Master Plan ya 2012 mpaka 2032 ambayo tumeshaipitisha katika ngazi zote inasubiri tu utekelezaji. S nataka waziri uniambaie ni lini Serikali itaanza kutekeleza mkakati wa Dar es Salaam City Master Plan ili mji wetu upangike vizuri na uonekane na changamoto zote za mji kutokupangwa?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Dar es salaam tayari inayo master plan na ilishapitia katika nganzi zote lakini changamoto iliyopo pale katika utekelezaji wake bado katika halmashauri zinazohusika katika kufanya kazi ile kwa sababu ule utekelezaji unakwenda awamu kwa awamu kutegemeana na utaratibu wa mpangilio wa majenzi waliyoyaweka.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa utekelezaji unaoendelea hawaruhusu pia hata katika ujenzi unaoendelea kuweza kujenga nyumba pengine katika maeneo ambayo master plan inazungumzia habari ya kwamba pana magorofa kadhaa, ukiomba kujenga nyumba ya kawaida unazuiliwa. Kama ni eneo la viwanda ukiomba kujenga nyumba ya kawaida unazuiliwa. Kwa hiyo, utekelezaji umeanza japokuwa space yake ni ndogo kutegemea jinsi mtu mji wenyewe wa Dar es Salaam ulivyokuwa umejengeka katika taratibu ambazo si ki mipango miji katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lazima twende nao taratibu namna ya kuweza adapt kile ambacho tayari kimepangwa na wenye halmashauri zao ili kuweza kuhakikisha ile master plan inatekelezwa. Kwa hiyo, sisi kama wizara tutaendelea kushirikiana na TAMISEMI ili kuweza kuona ni jinsi gani ile master plan inatekelezwa bila kuleta athari kwa wananchi.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu za Serikali zinaonesha kwamba maji vijijini yanapatikana asilimia 74 na mijini ni asilimia 85 kwenda 90; lakini uhalisia unaonesha kwamba mnasema watu wamepata maji kutokana na kuweka miundombinu na sio nyumba kwa nyumba.

Kwa kuwa sasa hivi tunaenda kwenye sensa ya Taifa ambapo watu wataenda kufanyiwa hesabu nyumba kwa nyumba. Kwa nini msitumie utaratibu huu wa sensa ili kuweza kupata takwimu halisi ya kila nyumba ambayo inapata maji nchi hii? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze na nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge dada yangu Halima, sisi Wizara yetu ya Maji inafanya mageuzi makubwa sana na moja ya eneo ambalo eneo unalizungumzia sisi tumeshalifanyia kazi. Tumekutana na watu wetu wa takwimu ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kwenye hilo hilo. Lakini tunataka tujiongeze mbali zaidi. Badala ya kusema tu asilimia ngapi watu wanapata maji, tunataka twende mbali zaidi, tunataka tujue Tanzania kuna vijiji vingapi, vingapi vimepata maji, vipi havijapata maji ili tuhakikishe tunaviongezea nguvu maeneo ambayo hayana maji ili waweze kupata huduma ya maji safi na salama. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani sasa hivi tunavyozungumza ambayo inahudumiwa na mitambo ya Ruvu Chini, nazungumzia Bagamoyo, nakuja Jimbo langu la Kawe pale, nakwenda Kinondoni, Temeke, kuna uhaba mkubwa sana wa maji.

Mheshimiwa Spika, Serikali inasema kwa sababu kuna upungufu wa maji, yaani kina cha maji kimepungua. Sasa ninataka Serikali iniambie, kwa sababu kupungua kwa maji kwa vyovyote vile kuna uhusiano na mabadiliko ya tabianchi, dunia nzima sasa hivi inazungumzia climate change. Leo nimemsikiliza Rais anasema anataka Serikali mtenge fedha za climate change.

Mheshimiwa Spika, nataka nipate majibu sahihi ili tatizo hili lisiwe la kudumu, kuna mkakati gani wa muda mfupi na muda mrefu kuweza kukabiliana na upungufu huu wa maji ili wananchi wa maeneo husika waepukane na kero hii? Hasa kwa kuzingatia miradi husika tumejenga kwa fedha za mikopo za mabilioni ya shilingi ambayo Taifa linalipa sasa hivi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Halima Mdee kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli mitambo yetu ya Ruvu Chini hapa katikati ilipata hitilafu ya kupata maji kwa upungufu lakini kama Wizara tuna mabonde tisa ambayo yanafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana kuona kwamba tunadhibiti tatizo hili. Tatizo hili ni kwamba matumizi ya shughuli za kibinadamu kwa sehemu kubwa ndiyo yameathiri.

Mheshimiwa Spika, huwa tunatoa vibali kwa wenzetu kufanya umwagiliaji maeneo karibu na vyanzo vyetu vya maji lakini vina muda. Muda ambao unapaswa kutumika ni muda ule wenye high season, maji yanakuwa mengi na muda huu wa kiangazi vile vibali huwa vina-expire. Sasa wale wamwagiliaji wamekuwa wakiendelea.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa hivi kama Wizara tayari tumeweka task force kuhakikisha hakuna atakayetumia maji yale kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji na shughuIi nyingine yoyote isipokuwa kuelekeza maji katika mitambo yetu kwa ajili ya kuchakata kwenda kwenye matumizi ya kibinadamu.

Mheshimiwa Spika, mkakati mwingine wa Wizara yetu ni kuona tutaendelea kutoa elimu ya kutosha, matumizi sahihi ya maji katika maeneo yote yenye mito tiririka ili vyanzo vyetu vya maji visiweze kuathirika kama ulivyosema. Tayari tumeshatumia fedha nyingi kujenga miundombinu ambayo Serikali inatarajia wananchi waweze kupata maji ya kutosha, safi na salama wakati wote. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ili mtu aweze kuwa bilionea, wengi wanaanza katika biashara ndogo ndogo. Kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema, unaanza na biashara ndogo ndogo, unafika kati na hatimaye unakuwa mkubwa ukiacha wale ambao wanarithi. Sasa imekuwa ni utamaduni wa Serikali ya Chama cha Mapinduzi kuwafukuza Wamachinga ambao wanatumia kipato chao kidogo kwenye maeneo yao ya biashara na kuwapeleka pembezoni na maeneo ambayo hayajaandaliwa na mazingira ambayo siyo wezeshi kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuthibitisha kwamba Serikali haijali kundi hili la wafanyabiashara wadogo wadogo, hapa kwenye mpango ambao Waziri ameusoma jana, hakuna maeneo ambayo anazungumza atawapanga vipi hawa vijana wetu? (Makofi)

Sasa nataka Waziri aniambie, kwa kuwa anatambua ili uweze kuwa milionea na hatimaye bilionea, lazima uanzie chini; na kwa kuwa anatambua...

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Halima.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakuja, ninakuja. Serikali...

NAIBU SPIKA: Aah, uliza swali, kwa sababu umepewa nyongeza.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina uwezo wa kuajiri asilimia mbili tu: Je, sasa ana mpango gani rasmi wa kuingiza eneo hili muhimu katika Mpango wetu ambao tutakuja kuufanyia kazi Januari, kwa kundi hili kubwa la vijana ambalo sasa hivi wanahangaika mtaani?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Halima kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni Serikali inayowajali sana wafanyabiashara wadogo. Mfano na uthibitisho mmoja ni kwamba mabilionea wote walioko katika nchi hii, ni zao la Chama cha Mapinduzi kwa sababu hakuna chama kingine kimewahi kuongoza. Kwa hiyo, mabilionea wote unaowaona katika nchi hii na wengine wame-spill over mpaka nchi za SADC na nchi nyingine kwa ukombozi wa Chama cha Mapinduzi. Ni zao la Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hawa ambao wako hapa, amesema Mpango haujasema watapangwa vipi? Mpango wa nani akae wapi, ni suala la kisekta ambalo litafanywa na Serikali za Mitaa. Kwa upande wa Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Rais ana mpango mzuri sana na kundi hili ambalo Mheshimiwa Halima amelisema la wafanyabiashara wadogo wadogo. Kwa sababu ndiyo kwanza bado tunaendelea kuchambua huu Mpango, tutawapa undani wake Waheshimiwa Wabunge, ni kwa sababu tu hatukusema kwa kuwa bado tuko kwenye mazungumzo ya awali. Hata hivi tunavyoongea, tunaendelea kuongea na wenzetu wa Benki ya Dunia, lakini pia tunaendelea kuongea ndani ya Serikali kutengeneza utaratibu ambalo lengo lake kubwa hasa ni kuwafanya hawa ambao tumewataja kwa jina la Wamachinga waweze ku- graduate, wapige hatua kwenda kwenye hatua nyingine inayofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, habari njema hii mtaiona katika Mpango huu na mtaona katika bajeti hii inayokuja na wenyewe Wamachinga watakuwa mashahidi kwamba kumbe kweli huu Mpango ulikuwa ni mwema ambapo umetufanya tu-graduate. Kwa sababu katika hali ya kawaida, hakuna Mmachinga anayetaka aendelee kuwa Machinga katika maisha yake yote. Hata wao wanataka siku moja wawe kama GSM wafanye mambo ya kweli na yanayoonekana katika nchi hii. Ahsante. (Makofi)
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali yangu ya nyongeza, siafiki takwimu za Serikali kwa sababu Covid ilisambaa nchi nzima na kwa watu 725 ukigawanya tu kwa mikoa 31 maana yake kila mkoa wamekufa watu 23 ambayo haina mantiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama nchi tulisimamisha mwaka mzima, Machi, 2020 mpaka Machi, 2021 kutoa takwimu. Kwa hiyo, hizi taarifa za takwimu siyo za ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maswali yangu ya nyongeza mawili; la kwanza, moja kati ya changamoto kubwa ilikuwa ni upimaji, kwa sababu ilikuwa lazima upime ndiyo ujue huyu mtu amekufa na Covid ama hajafa na Covid; sasa Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana juu ya mkopo wa shilingi bilioni 466 toka IMF, lakini hivi vitu alivyoviainisha hapa hakuna hata sentensi moja inayozungumzia ujenzi wa maabara ama uwepo wa maabara kwa ajili ya kupima Covid ama virusi vingine vinavyoashiria ama vinavyofanania na hivyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka aniambie, kwa sababu tunaishi na Covid-19 na virusi vinavyofanania na hivyo vitakuja, ni fedha kiasi gani katika mkopo huu wa shilingi bilioni 466 tutapeleka kwenye eneo la maabara specifically; na siyo hizi maabara sijui X-Ray, hizo zinatoa viashiria tu, kwamba kuna homa ya mapafu? Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na dawa, nili-intend hapa kuuliza, tiba za asili za Tanzania kwa kiwango kikubwa sana zimechangia kutibu madhara yanayotokana na Covid. Imesaidia sana; na hizi ni fursa kwa watu wa tiba za asili kwa nchi, kwa ukanda na dunia: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Serikali iniambie, mpaka sasa, kwa sababu kila siku mnajibu mnafanya tafiti, mmeshagundua ni tiba gani za asili ambazo ni sahihi kwa Watanzania watakaopata maradhi ama Virusi vya Covid ili wakiugua tujue protocol ya matibabu ni hii; na siyo sasa hivi kila mtu anakunywa kivyake mpaka tunakunywa sumu? Ni lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie tu rafiki yangu kwamba hii ni sayansi. Kama ni sayansi, inahitaji akili kubwa kuweza kuyaona hayo na siyo hisia za kwenye ma-corridor. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu kwamba Bugando, Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia amepeleka vifaa vya maabara vya kupima Corona vyenye thamani ya shilingi bilioni nne na mlinisikia nikisema. Kibong’oto ambayo ndiyo taasisi yetu ya magonjwa ambukizi, imepelekewa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni sita na maabara inajengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 14. Maabara yetu ya Taifa nayo inayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujue virus siyo mdudu mpya. Ni mdudu mpya kwenye genetic makeup lakini sayansi ni ile ile. Kwa hiyo, maabara ni zile zile, mashine ndiyo zimetofautiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kuhusu tiba ya asili. Kwanza hatujaacha tiba ya asili. Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 1.2 imeenda NIMR kwa ajili ya kuchakata dawa zetu zilizoonekana kwamba zinatusaidia na kuziweka vizuri. Vilevile kwenye fedha hizi ambazo nilikuwa nazitaja, shilingi bilioni 466, imetengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya utafiti ule mkubwa na mgumu kwa ajili ya kuja na chanjo yetu ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa ninachoweza kumwambia Mheshimiwa, haya ya kisayansi huwa ni magumu, nawaachia wanasayansi. Unahitaji super computing system kubwa kuziona; hii siyo ngwini yaani, unajua. Kwa hiyo tulia. (Makofi)