Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwita Mwikwabe Waitara (10 total)

MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Zahanati ya Kitunda inahudumia wananchi wa Kata za Kitunda, Kivule, Kipunguni, Msongola na baadhi ya wananchi toka Chamazi na Tambani katika Mkoa wa Pwani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuifanya zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya ili kiweze kumudu mahitaji makubwa ya wananchi wa maeneo yaliyotajwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Kitunda iliyopo Kata ya Kitunda haina eneo la kutosha kukidhi ongezeko la miundombinu inayohitajika kuwa kituo cha afya jambo ambalo litalazimu Serikali kuwaondoa wananchi na kulipa fidia. Ili kuboresha huduma za afya katika Kata ya Kitunda, Kivule, Kipunguni na Msongola na maeneo jirani, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Kata ya Kivule.
Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 zimetengwa shilingi milioni 900 na tayari ujenzi uko katika hatua ya msingi. Vilevile katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni moja ili kuendelea na ujenzi.
Mheshimiwa Spika, sambamba na ujenzi wa hospitali, Serikali imepanga kujenga zahanati mpya na kuimarisha zilizopo. Kutokana na juhudi za kufanikisha jambo hilo muhimu Serikali imepanga kutumia shilingi milioni 600 katika mwaka wa fedha 2015/2016 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati ya Lubakaya, Mbondole na Luhanga pamoja na nyumba za watumishi zilizopo katika Kata ya Msongola.
Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa jumla ya shilingi milioni 659.13 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na nyumba za watumishi katika Kata mpya ya Mzinga na Kipunguni B katika Kata ya Kipunguni.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Kumekuwa na utaratibu mbovu na Mawaziri wa Elimu kuingilia shughuli za mitaala kwa kubadilisha mitaala, mfumo wa madaraja na hata aina ya mitihani hasa kuweka maswali ya kuchagua katika somo la hisabati:-
Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya NECTA ili Bunge libadili Sheria ya Baraza kifungu cha 30 ili kuondoa nguvu ya Waziri ya kutoa maelezo bila kuhoji na hata bila kushirikisha wataalam wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania haina kifungu cha 30 kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, Wizara inaona kuwa maudhui ya swali hili yanapatikana katika kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania. Kifungu hiki kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Elimu kufanya maamuzi kwa niaba ya Serikali pale inapolazimika kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya jamii kulingana na wakati, mazingira halisi na matokeo ya tafiti mbalimbali kutoka kwa wataalam pamoja na maoni ya wadau wa elimu. Kwa kuzingatia matakwa ya sheria hii, Baraza la Mitihani Tanzania hutakiwa kuyatekeleza maamuzi hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kukifanyia marekebisho kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania kwa kuwa kinamwezesha Mheshimiwa Waziri kufanya marekebisho mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yanayojitokeza kwa wakati husika.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Suala la Mpango Miji ni jema na mtu aliyepimiwa ardhi na kupata hati ya eneo lake huweza kutumia hati hiyo kukopa kirahisi lakini gharama za kupima ardhi ni kubwa sana kiasi kwamba wananchi walio wengi wanashindwa kupima maeneo yao.
Je, Serikali ina mpango gani wa dharura wa kupunguza gharama za upimaji ardhi ili wananchi wengi zaidi waweze kupima maeneo yao na kuyaongezea thamani?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 12 la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa ardhi hapa nchini unafanywa na Wapima wa Ardhi wa Serikali walioajiriwa na Serikali na Wapima Binafsi walioajiriwa na Bodi ya Wapima Ardhi na kupewa leseni za biashara ya upimaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Serikali, gharama za upimaji rasmi kwa sasa ni shilingi 300,000 kwa hekta ya shamba moja na kiwanja kimoja. Gharama hizi zilipunguzwa na kuridhiwa na Bunge lako Tukufu kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambapo kabla ya hapo zilikuwa shilingi 800,000 kwa hekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa za upimaji zinatokana na sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, Halmashauri nyingi hazijajengewa uwezo wa wataalam na vifaa na jukumu la kuajiri wataalam na kununua vifaa ni la Halmashauri yenyewe hivyo upungufu wa vifaa pamoja na wataalam ni mkubwa kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili ni kwamba gharama za vifaa vya upimaji ni kubwa sana na upatikanaji wa seti moja ya kawaida ya upimaji kwa kutumia darubini ni shilingi milioni 18 kwa seti moja na GPS ni shilingi milioni 48. Ukubwa huu wa gharama na vifaa husababisha wapima wengi kutokuwa na uwezo wa kununua vifaa na hivyo kutegemea kukodi kwa gharama kubwa hivyo kufanya pia upimaji kuwa ghali ili kuweza kurejesha gharama za vifaa kwa sababu ni vya kukodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ongezeko la gharama za upimaji nchini, Serikali ina mpango wa kusogeza huduma zote zinazotolewa Wizarani kwenda kwenye kanda. Hatua hii itawezesha kanda hizo kujengewa uwezo na hivyo kuchangia kupunguza gharama. Katika kuzijengea uwezo, Serikali inategemea kununua vifaa vya upimaji katika mradi wa World Bank na kuvigawa katika kanda zake ambavyo vitasaidia Halmashauri katika kanda husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nitoe rai kwa Halmashauri zote nchini kutenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya upimaji pamoja na kuajiri wataalam wa kutosha katika kada hii ya upimaji na wengine wa sekta ya ardhi ili kuondokana na gharama kubwa za kukodisha vifaa hivyo kutoka katika taasisi binafsi.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Baadhi ya wakazi wa Ukonga wanafuga kuku wa mayai na wengine wanatengeneza chakula cha mifugo, shughuli zinazowainulia kipato na kuweza kupata mahitaji muhimu ya kimaisha, lakini shughuli zao zimeathiriwa na watu wanaoingiza mayai toka nje ya nchi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia uingizaji wa mayai toka nje kwa sababu unaharibu soko la ndani la bidhaa hiyo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia malighafi ili chakula cha mifugo kiendane na bei ya mayai na kuku?
(c) Je, Serikali ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo toka nje ambao wengi wao hufa na kusababisha hasara kwa wananchi wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 2006, Serikali iliweka katazo la kuingiza kuku na mazao yake nchini ili kudhibiti Ugonjwa hatari wa Mafua ya Ndege. Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2007 na 2010 zinatumika kudhibiti na kukagua uingizwaji katika maeneo ya mpakani, bandari na viwanja vya ndege. Hakuna mwekezaji yeyote anayeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au mayai nchini kwa ajili ya biashara na katika kusimamia hili kuanzia mwaka 2013 hadi 2017, vifaranga 67,500 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria viliteketezwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inasimamia ubora wa malighafi za kusindika vyakula vya mifugo kupitia Sheria ya Maeneo ya Nyanda za Malisho na Rasilimali za Vyakula vya Wanyama Na. 13 ya Mwaka 2010. Changamoto katika kusindika vyakula hivyo ni gharama kubwa ya viinilishe vya protini kutokana na matumizi ya maharage aina ya soya. Maharage haya huagizwa kutoka nje ya nchi hususan Zambia na India. Wizara inaendelea kuhamasisha uzalishaji wa soya hapa nchini katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza nchini mayai au vifaranga wa kuku wazazi (parent stock) tu. Ukaguzi kwa ajili ya kudhibiti uingizaji wa vifaranga na mayai unaendelea na hatua kali zinachukuliwa kwa yeyote atakayekamatwa kwa kukiuka utaratibu.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya umeme katika Kata zifuatazo; Kata ya Chanika (Ngwale, Nguvu Mpya, Virobo, Kidugalo, Yongwe, Lukooni, Vikongoro na Tungini); Kata ya Zingiziwa (Zogoali, Zingiziwa, Ngasa, Ngobedi, Somelo na Gogo, Lubakaya na Kimwani); Kata ya Majohe (KIvule na Viwege); Kata ya Buyuni (Zavala, Buyuni, Mgeule Juu, Nyeburu, Mgeule Chini, Kigezi, Kigezi Chini na Taliani); Kata ya Pugu Station (Bangulo, Pugu Station na Kichangani); Msongola (Yangeyange, Mbondole, Kidle, Mkera, Sangara, Kiboga, Uwanja wa Nyani, Kitonga, Mvuleni na Mvuti) na Kata ya Kivule (Bombambili). Maeneo hayo yote yanahudumiwa na Wilaya ya Kisarawe kama maeneo ya vijijini. Je, ni lini maeneo hayo yatapata umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swai la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Kidole, Bangulo, Kitonga, Mvuti na baadhi ya maeneo mengine pamoja na Msongole yalipatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Pili uliokamilika mwezi Disemba, 2016. Kazi ya kupeleka umeme katika maeneo hayo ilijumuisha pia vijiji vilivyokuwa vinatoka katika Wilaya ya Kisarawe ambapo pamoja na mambo mengine vimefungiwa transfoma 55 za kVA 50, kVA 100 na kVA 200; ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 pia umejengwa kwa urefu wa kilometa 187.22 lakini njia ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 239.7 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 1,083. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 5.3.
Mheshimiwa Spika, mitaa mingine iliyobaki ya Kata za Chanika, Zingiziwa, Majohe, Buyuni, Pugu Station pamoja na Msongola, zitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Urban Electrification chini ya ufadhili wa Maendeleo wa Benki ya Dunia.
Mheshimiwa Spika, kazi hizi zinajumuisha ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 66.3, msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 336.7 pamoja na ufungaji wa transfoma 73 za kVA 200 na kVA 100. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 10.73 na utaunganishia wateja 7,083.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Jimbo la Ukonga lina shida kubwa ya maji.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi ya maji ya Kata za Chanika, Kipunguni na Majohe ili wananchi wa Kata hizo na maeneo ya jirani wapate maji ya uhakika?
(b) Je, ni lini Serikali itachimba bwawa kubwa katika Mnada wa Kimataifa wa Pugu ili ng’ombe wanaouzwa hapo wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kukamilisha miradi ya maji katika Kata za Chanika, Kipunguni na Majohe. Miradi mingi imekamilika na inahudumia wananchi na mingine ipo katika hatua za mwisho za ujenzi. Miradi iliyokamilika ni pamoja na Kipunguni B, Kwa Mkolemba, Chanika Shuleni, Majohe, Nyang’andu na Msongola. Miradi inayoendelea kujengwa ni bomba mbili za Kipunguni B, ambao unatekelezwa na Manispaa ya Ilala. Aidha, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji kulingana na upatikanaji wa fedha ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kuleta maji katika maeneo ya Pugu kutoka katika mradi mkubwa wa visima virefu vilivyopo Mpera katika Wilaya ya Mkuranga. Kazi ya uchimbaji wa visima hivi inaendelea na matarajio ni kukamilisha uchimbaji mwaka huu wa fedha na baada ya hapo Serikali itatekeleza mradi wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha maji hayo hadi Pugu na kuyasambaza maeneo yote ya Pugu, Chanika, Ukonga, Gongolamboto, Kinyerezi, Kitunda, Kipawa, Yombo na maeneo ya barabara ya Nyerere kuanzia Pugu hadi TAZARA.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Katika Mtaa wa Mongolandege, Kata ya Ukonga, kuna daraja la Mongolandege ambalo huunganisha Jimbo la Ukonga na Jimbo la Segerea. Aidha, daraja la Mto Nyebulu huunganisha Kata ya Buyuni na Kata ya Chanika Magengeni.
Je, ni lini Serikali itajenga madaraja hayo muhimu ili kurahisisha huduma za kijamii katika maeneo yaliyotajwa?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Mongolandege linatakiwa kujengwa katika Bonde la Mto Mzinga ambalo awali palijengwa makalavati kwa nguvu za wananchi. Kalavati hizo zilishindwa kufanya kazi kwa ufanisi baada ya mkondo wa mto kupanuka.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mwaka 2012, Manispaa ya Ilala ilijenga box culvert ili kuwezesha eneo hilo kupitika. Hata hivyo, mvua zilizonyesha kwa wingi katika kipindi hicho zilileta madhara makubwa ambapo bonde hilo lilitanuka na kalavati hiyo kusombwa na maji na kusababisha kukosekana mawasiliano katika eneo hilo. Daraja la Nyebulu linatakiwa kujengwa katika Mto Vikorongo na litakuwa na wastani wa upana wa mita 30.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala itatenga fedha katika mpango wa matengenezo ya barabara na madaraja kwa mwaka wa fedha 2018/2019 za kufanyia usanifu wa kina kwa ajili ya madaraja yote mawili. Aidha, baada ya usanifu huo kukamilika, gharama halisi za ujenzi wa madaraja hayo zitafahamika na kutengwa kwenye bajeti.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Hospitali ya Amana imepelekwa Wizarani, hivyo Wilaya ya Ilala kwa sasa haina Hospitali ya Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia Hospitali ya Kivule itumike kama Hospitali ya Wilaya ya Ilala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imeandaa mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa inapata Hospitali ya Wilaya ikiwa ni pamoja na kutenga fedha jumla ya shilingi bilioni tatu katika mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Kivule. Kati ya hizo shilingi 2,000,000,000 ni mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi 1,000,000,000 ni ruzuku ya Serikali Kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi wa Hospitali ya Kivule, Serikali inaendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mzinga, Kinyerezi na upanuzi wa Kituo cha Afya Buguruni. Lengo la kuimarisha vituo hivyo ni kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya na kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika ngazi za msingi.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kukipatia Kituo cha Chanika gari la patrol?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kipolisi ya Ukonga ipo katika Mkoa wa Kipolisi Ilala na Kituo Kikuu ni Kituo cha Polisi Stakishari ambacho kinasaidiwa na vituo vingine vidogo kama vile Pugu, Chanika, Msongola, Gongolamboto, Mazizini, Karakata, Kinyerezi, Tembo Mgwaza na Kitunda. Vituo hivi vyote huhudumiwa kwa magari saba toka katika Kituo cha Stakishari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha katika Kituo cha Polisi cha Chanika lipo gari Na. PT 1889 Toyota Land Cruiser Pickup, ndilo hutumika kufanya doria katika eneo hilo likisaidiwa na magari mengine toka katika Kituo cha Stakishari, kwani kituo hiki ni kikubwa ukilinganisha na vituo vingine vilivyotajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi litaangalia uwezekano wa kuongeza gari katika Kituo cha Polisi Chanika na kuzingatia vigezo kama vile hali ya uhalifu, idadi ya watu, sababu za kiutawala na kijiografia kwa kulinganisha na maeneo mengine yenye mahitaji kama haya.
MHE. LUCY S. MAGERELI (K.n.y. MHE. MWITA M. WAITARA) aliuliza:-
Jimbo la Ukonga katika Kata za Msongola, Chanika, Zingiziwa, Buyuni na Pugu kuna shida kubwa sana ya maji.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuondoa kero ya maji katika kata hizo?
(b) Je, ni lini miradi viporo vya maji na visima vyenye pampu mbovu vitafanyiwa matengenezo ili kupunguza kero ya maji Ukonga?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara Mbunge wa Jimbo la Ukonga lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa muda mrefu wa kuondoa kero ya maji katika Jiji la Dar es Salam na viunga vyake kwa kutumia maji ya visima virefu 20 vilivyochimbwa katika Manispaa ya Kigamboni eneo la Kimbiji na Mpera vyenye uwezo wa kutoa kiasi cha maji cha mita za ujazo 350 mpaka 700 kila kimoja. Kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza maji katika maeneo hayo. Kukamilika kwa mradi huu kutaondoa kero ya maji katika Jiji la Dar es Salam na viunga vyake zikiwemo Kata za Msongola, Chanika, Zingiziwa Buyuni na Pugu. Mradi huu unatarajiwa kuanza katika mwaka wa fedha 2018/2019.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) Serikali imeweka kipaumbele cha kukamilisha miradi viporo kabla ya kuanza miradi mingine mipya. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepanga kukamilisha miradi viporo na kukarabati visima vyenye pampu mbovu kwa kutumia fedha za Mpango wa Malipo kwa Matokeo (Payment by Result). Mpaka sasa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imekarabati na kumalizia ujenzi wa miradi viporo sita ya maji katika Jimbo la Ukonga kwenye Kata za Msongola, Pugu, Mzinga na Pugu Stesheni.