Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Catherine Valentine Magige (51 total)

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya maji yaliyoko Hydom yanafanana kabisa na matatizo ya maji yaliyoko katika Mkoa wangu wa Arusha hasa Longido na Monduli. Kwa kuwa Monduli walikuwa na mabwawa matatu ambayo yamepasuka na sasa hivi wananchi wa Monduli wana tabu kubwa sana ya maji, wana-share maji na mifugo. Kwa kuwa kuna maji yanamwagika Engaruka na Mto wa Mbu, je, Serikali haioni umuhimu wa kuwasaidia wananchi hawa wa Monduli kwa kuyatumia maji yale kuliko yanavyomwagika bure? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru ametupa taarifa kuna mabwawa ambayo yamepasuka katika Jimbo la Mbulu. Naomba kuchukua nafasi hii kuagiza Mkoa wa Arusha wakatembelee eneo hilo na waipe taarifa Wizara ili hatua mahsusi ziweze kuchukuliwa.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, napenda kufahamu kuanzia mwaka 2009 mpaka sasa ina maana Serikali ilikuwa inawekeza katika kiwanda cha General Tyre bila andiko la kitaalam? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama kiwanda kitaendeshwa bila kuwa na ruzuku ya Serikali, je, maslahi ya wananchi wa Mkoa wa Arusha yatalindwa vipi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, ni kwamba tumekuwa tukiwekeza bila kuwa na andiko la kitaalam, hapana, lilikuwepo, lakini hii ni biashara, biashara siyo static. Kilichobadilika ni kwamba huwezi kuendesha kiwanda kile kwa kutegemea ruzuku. Ule mradi ni bankable, ni rahisi ukaelezea kwamba una kiwanda kile, Tanzania kuna soko la matairi 44,000,000 kwa span ya miaka mitatu, soko lenye uwezo wa trilioni 1.18.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunataka andiko, TIB ihusishwe, pesa zikopwe kwenye benki za nje zinazotoa riba ndogo, twende kwa mtazamo huo. Ndiyo maana nataka kuitoa kwenye ruzuku, huwezi kuendesha kiwanda kwa ruzuku. Amezungumza Mheshimiwa Bashe jana hapa, ruzuku ya Serikali iende kwenye mambo ya jamii.
Mheshimiwa Spika, namba mbili, maslahi ya watu wa Arusha. Maslahi ya Watanzania wote yatazingatiwa. Maslahi yanakuja wapi, kiwanda kikishatengenezwa kwa menejimenti ni mali ya Serikali. Tunakolenga maslahi ya Watanzania wote yatapatikana, moja kwa ajira lakini pili kiwanda kile kinaweza kuuza hisa Watanzania mkaki-own kama mnavyo-own TBL, mnavyo-own cement.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa tatizo la makazi ya polisi yamekuwa makubwa sana haswa katika Mkoa wangu wa Arusha, polisi wamekuwa wakiishi katika nyumba mbovu na chafu na wengine kuishi uraiani. Kwa kuwa tuna ekari 30 tulizopewa na Magereza kwa ajili ya makazi haya ya polisi. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutumia zile ekari 30 tulizopewa na Magereza kwa ajili ya kujenga makazi haya ya polisi Mkoa wa Arusha?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mpango wa kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali. Nilizungumza jana kwamba tuna mpango wa kujenga nyumba 4136 kwa awamu ya kwanza katika mikoa 17 ikiwemo Arusha. Lakini wazo lake la kutumia eneo la Magereza basi tutalichukua tuone tunalifanyia kazi kwa kiasi gani.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutuhakikishia kuwa Karatu watapata umeme, maana Karatu ni katika Mkoa wangu. Vilevile katika Mkoa wa Arusha kuna maeneo mengi sana wana tatizo la umeme. Mfano wa Arumeru wananchi walitoa mashamba yao, wakachimba mashimo kwa ajili ya umeme wa REA, lakini mpaka sasa hivi wananchi wale wa Arumeru hawajapata umeme. Kuna malalamiko kuwa pesa zinazopangwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo hazifiki na hata zikifika hazifiki zote.
Je, Serikali itatatua vipi tatizo hilo la umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Katherine na nimpongeze sana, amehangaika sana hata kwenye ununuzi wa transformer tumeamua tununue hapa ndani kwa sababu ya juhudi zake, nakupongeza Mheshimiwa Catherine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kumuhakikishia tu wananchi wa Arusha watapata umeme, ni kweli kuna matatizo ya umeme Arumeru na kuna vijiji vingi sana kama vya Urojora pamoja na vingine havijapata umeme naelewa. Lakini kumhakikishia Mheshimiwa Magige kwenye Jimbo lote tumetenga bilioni 13.7 kwa ajili ya wananchi wa Arusha. Ili kuhakikisha kwamba, REA awamu III matatizo yote yanaisha. Sambamba na hilo yapo matatizo ya umeme hasa kwenye eneo la Arusha la kukatika katika kwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nilishazitaja lakini nidokeze tu, kwa sasa hivi Serikali kupitia TANESCO pamoja na wakandarasi tunaboresha sasa miundombinu ya umeme. Kuanzia leo, tumesema tatizo la low voltage tunakwenda kulikamilisha kwa sababu sasa tunasafirisha nguvu kubwa, tunasafirisha nguvu kubwa yenye kilovoti 400 kwa upande wa Arusha kutoka Dar es Salaam kupitia Chalinze kwenda Bagamoyo, kwenda Arusha mpaka Namanga, kilomita 664.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa upande ule tatizo la kukatika kwa umeme litakwisha kabisa, lakini juhudi nyingine pamoja tumeamua sasa kukatika kwa umeme kuna sababisha pia uharibifu wa transfomer na hii inasababisha wakati mwingine na utaratibu wa kununua transfomer kutoka nje. Sasa hivi kama mlivyokwisha kusikia tumetangaza na naendelea kusema tena, awamu inayokuja sasa na transfomer tutakuwa tumenunua hapa nchini kwa sababu TANALEC wana uwezo wa kutengeneza.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi nyingine za kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme wakati mwingine ni matatizo ya nguzo. Sasa hivi TANESCO imeunda kampuni tanzu ambayo itakuwa inatengeneza concrete pole kwa ajili ya kutengeneza nguzo hizo hapa nchini. Hivyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi kwamba, sasa tatizo la umeme litakwisha mara moja.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini tatizo lililoko Hospitali ya Rufaa ya Mbeya ni dogo sana ukilinganisha na tatizo kubwa sana lililoko katika Hospitali ya Mkoa wangu wa Arusha, Hospitali ya Mount Meru. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Mount Meru hatuna CT-Scan, hatuna MRI Machine, hatuna X-Ray Processor na Ultrasound with Doppler. Kwa hiyo, wananchi wa Mkoa wa Arusha wamekuwa wakitaabika sana kwa sababu Hospitali ya Mount Meru ndiyo hospitali yetu tegemezi. Je, Serikali ina mpango gani wa kushughulikia tatizo hili katika Hoapitali ya Mount Meru haraka iwezekanavyo?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niseme, tuna mradi wa kuboresha huduma za kiuchunguzi katika Hospitali zetu zote za rufaa za kanda na hospitali za rufaa za mikoa. Kwa hiyo, katika bajeti yangu ya 2016/2017 tumetenga kiasi cha takriban shilingi bilioni 9 kwa ajili ya kununua vifaa hivyo na kati ya hospitali ambazo tutazipa kwa mfano kama CT-Scan ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru - Arusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, niweke wazi, vifaa kama X-Rays ni kwamba hospitali zenyewe nazo zina wajibu wa kununua vifaa tiba na sasa hivi wanaweza wakatumia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya kuomba mkopo na kununua vile vifaa tiba ambavyo gharama yake siyo kubwa. Vifaa kama CT-Scan na MRI tutaweza kuwapatia kwa kupitia mradi wa Orion.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa vijana hawa wa Arusha ambao wamekuwa wakitumiwa na Mbunge huyu huyu kuandamana hawana ajira lakini inapofikia wakati wa kuwasilisha matatizo yao Bungeni Mbunge huyu akatolewa kwa ajili ya utovu wa nidhamu, je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuwasikitikia vijana wa Arusha kwa kuwapatia mafunzo na mitaji ili waendelee kutoa kura kwa Serikali hii sikivu ya Chama cha Mapinduzi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nataka niwaondoe hofu vijana wa Arusha. Pamoja na kwamba wamekosa kisemeo chao humu ndani kwa maana yule ambaye walimpa dhamana hayupo kwa ajili ya kuwasilisha matatizo yao lakini Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kuwajali vijana bila kubagua. Sisi katika utekelezaji wa majukumu yetu mbalimbali tutahakikisha vijana wa Arusha kama vijana wa maeneo mengine na wenyewe wanapata fursa za elimu ya ujasiriamali, mikopo na mitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi nimeshafika pale Arusha na nimeshakutana na vijana wa SACCOS katika soko la Korokoroni na nimewaahidi kwamba nitarudi kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia katika kupata mitaji na mikopo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nikuondoe tu wasiwasi ya kwamba kama Serikali vijana hawa tutaendelea kuwaangalia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Catherine kuwa kisemeo kipya cha vijana wa Arusha na hasa kuendelea kuwa daraja la kutu-link kati ya Serikali na vijana wa Arusha ili waweze kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 25 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasisitiza sana kwamba kazi ndiyo kipimo cha utu wa kila Mtanzania. Kifungu cha 28(b) cha Sheria ya Mwenendo ya Mashauri ya Jinai na chenyewe kinasisitiza sana masuala ya kila Mtanzania kuwajibika na apimwe kwa kuwajibika na aweze kukidhi riziki zake kwa kuwajibika yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, kama kuna Mheshimiwa Mbunge anawatumia vijana na kuwahamasisha wasifanye kazi anaenda kinyume na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo basi kukiuka misingi yote ya utawala bora. Kwa hiyo, naomba kuwaambia Waheshimiwa Wabunge na vijana wote maelekezo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais wetu ni sahihi. Vijana wanaweza kucheza pool katika saa ambazo si za kazi lakini saa za kazi kila mtu awajibike ili kuweza kupata riziki yake na kuweza kujenga uchumi wa nchi yetu ya Tanzania.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa hospitali inayotegemewa na wananchi wa Loliondo, Mkoani Arusha ni Hospitali ya Misheni ya Waso ingawa hospitali hii ina changamoto nyingi sana; na kwa kuwa hatuna Hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kujenga Hospitali ya Wilaya ili wakazi wa maeneo yale wapate huduma ya matibabu ipasavyo maana wakazi wengi wa maeneo yale ni wafugaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue ombi hili kutoka kwa Mheshimiwa Catherine Magige kwamba Ngorongoro ijengwe Hospitali ya Wilaya na nikitambua kwamba katika maeneo haya kuna changamoto kubwa sana. Juzi juzi nilikuwa na Mbunge wa eneo hilo akishirikiana na wananchi wake na Madiwani ambapo walikuja ofisini kwangu kuelezea changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.
Kwa hiyo, jambo kubwa kama nilivyosema katika miradi kama hii, naomba Mheshimiwa Mbunge kwa sababu yeye ni wa mkoa mzima ashirikiane na Mbunge wa Jimbo na najua ni mpambanaji mkubwa sana katika sekta ya afya, wafanye mchakato mpana wa kuliibua vizuri jambo hili ili badala ya kutumia Hospitali ya DDH ambayo ni ya Misheni tuhakikishe wananchi tunawapatia Hospitali yao ya Wilaya ili mradi na wao waweze kunufaika na huduma ya afya katika nchi yao.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nimeona katika jibu la msingi la Naibu Waziri amesema viongozi wa vijiji vya Ngorongoro hawakutoa ushirikiano. Nataka kufahamu, kama viongozi hao hawakutoa ushirikiano ina maana Serikali ndiyo imekata tamaa? Kwa sababu wananchi wale wamekuwa wakipata shida sana, nyumba zao zimekuwa zikichomwa moto na mifugo yao imekuwa ikiuliwa. Nataka jibu la Serikali kuhusiana na kumaliza mgogoro huu wa Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa migogoro mingi imekuwa ikichangiwa na wafanyakazi wa wanyamapori. Je, Serikali inawachuja vipi maafisa wake wale wasiokuwa na maadili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la kwanza kama Serikali imekata tamaa au laa, jibu la moja kwa moja ni kwamba, Serikali haijakata tamaa na wala Serikali haiwezi kukata tamaa katika kushughulikia changamoto ambazo zinawahusu wananchi wake. Kwa nyongeza tu ni kwamba, kwenye jibu langu la msingi nimetaja wilaya ambazo zinahusika na mgogoro ukizihesabu ni wilaya saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika wilaya sita mgogoro huu ulishughulikiwa baada ya kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi na Serikali zao za Wilaya na Wizara ya Maliasili na Utalii. Changamoto zilizojitokeza kwenye vijiji hivi vya Wilaya ya Ngorongoro ni kama hivyo nilivyozieleza lakini kama nilivyotangulia kusema hapo awali tumeuorodhesha mgogoro huu ambao unahusu vijiji hivi vya Wilaya ya Ngorongoro kuwa miongoni mwa migogoro ya hifadhi ambayo haijashughulikiwa kikamilifu na nimesema Serikali inaenda kumaliza changamoto hizo katika zoezi linaloenda kufanyika hivi karibuni kimkakati zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili linalohusiana na wafanyakazi wa wanyamapori, nashukuru ameweza kuweka vizuri kabisa kwamba ni baadhi ya wafanyakazi. Jambo la kwanza kabisa wako wafanyakazi walio wengi wa wanyamapori wanafanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa na kwa kuzingatia maadili, miiko, kanuni na taratibu na miongozo ya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale wafanyakazi wachache ambao wanatumia vibaya nafasi zao, kwa kutumia mwanya wa kutekeleza sheria kwa kuvunja sheria na kufanya vitu ambavyo ni kwa kinyume kabisa na kanuni na taratibu hao wanafanya hivyo wakiwa wanavunja sheria. Kwa hiyo, sasa tunajipanga zaidi kwenda kuwashughulikia mmoja mmoja na kwa makundi ili waweze kukomesha kabisa tabia hiyo na wananchi waweze kutii sheria kwa kuongozwa na kanuni na taratibu na sheria zenyewe badala ya matumizi mabaya ya sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitumie tu fursa hii pia kutoa wito kwa askari wote wa wanyamapori kwa ujumla wao kwamba wale ambao hawahusiki na vitendo hivi vibaya watumie nafasi zao kuwashauri wenzao lakini wale ambao wana tabia hii wakumbuke tu kwamba katika Serikali ya Awamu ya Tano mambo ya kufanya kazi kwa mazoea, kwamba ulikuwa unafanya namna fulani ulivyozoea tangu huko nyuma sasa imepitwa na wakati na sasa tumefungua ukurasa mpya kabisa wa kutaka kwenda kufanya vitu kwa mujibu wa kanuni na taratibu. Wajiepushe na taratibu za kujificha nyuma ya pazia la utekelezaji wa sheria kuonea wananchi kwa kuwachomea nyumba moto, kuwapiga na vitendo vingine vyote visivyofaa.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa katika suala zima la ulinzi tunategemea sana askari wetu, lakini tumekuwa tukishuhudia askari wetu wakipoteza maisha wakiwa kazini wakati mwingine kwa kupambana na majambazi au wakipata ajali kwenye misafara mbalimbali. Nataka kufahamu Serikali ina utaratibu gani wa kuhudumia familia za askari hawa wanaopoteza maisha wakiwa kazini kama kusomesha watoto na huduma na huduma nyingine muhimu?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Catherine kwa kulileta jambo hilo. Ni kweli kumekuwepo na matatizo hayo na sisi kama Wizara niliwaelekeza wataalam wangu kuangalia maeneo ambayo yanahusu sheria na yale yanayohusu sehemu ya bima kwa ajili ya askari wetu ili kuweza kusaidia askari kwanza akiwa bado yuko kazini, pale anapopata ajali kazini kuweza kuhudumiwa katika maumivu anayoyapata. Nilipozunguka nilipata taarifa kwamba kuna askari wanaumia kazini wanaambiwa bima haiingii kwenye baadhi ya vipimo ama katika baadhi ya dawa wanazotaka.
Kwa hiyo, hili la kuzihudumia familia wanapokuwa wamepata ajali tunaliangalia kwa mapana kisheria ili familia hizo zisiyumbe baada ya kuwa askari wetu amepata ajali.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa Wilaya ya Longido Mkoa wa Arusha ni mojawapo kati ya Wilaya ambazo zina changamoto kubwa ya maji, wakazi wa eneo hili wamekuwa wakitumia asilimia 90 ya muda wao kwenye kutafuta maji na kuna tuhuma ya kuwa kuna pesa zaidi ya milioni 400 zilitolewa lakini hazijulikani zimeenda wapi na wananchi wa Longido wanaendelea kuteseka. Je, ni lini Serikali sasa itatekeleza ahadi yake ile ya mradi mkubwa wa maji wa bilioni 13 katika Wilaya hii ya Longido?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli katika bajeti ya mwaka huu tumeweka fedha kwa ajili ya kuanza kujenga mradi huo mkubwa wa kupeleka maji katika Wilaya ya longido. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira, Serikali inaendelea na taratibu za manunuzi ili tuweze kupata mkandarasi wa kujenga mradi huu.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Kitumbeini na Namanga, Wilayani Longido, Mkoa wa Arusha wamekuwa hawapati huduma ya afya, hakuna vituo vya afya imefikia hata wanavuka mipaka kwenda nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kupata matibabu. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wananchi hawa waondokane na tatizo hili ukizingatia Wilaya ya Longido haina hata hospitali ya Wilaya.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MTAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nyakati mbalimbali nilikuwa nikirejea kwamba ni kweli katika vituo vya afya tunavyohitajika kuvipata sasa hivi bado tuna upungufu mkubwa sana.
Katika mpango mkakati wetu sasa hivi tumejielekeza kwamba at least kila Halmashauri tuweze kuwa na hospitali ya Wilaya na katika hili naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, nakumbuka jambo hili muda mrefu sana linapigiwa kelele na kweli haipendezi, katika eneo hili wananchi wanakosa huduma mpaka wanakwenda nchi za jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali, lakini kama Halmashauri ya eneo hilo, nitaomba katika mchakato wa bajeti ya mwaka huu unaokuja kwa sababu tumeweka kipaumbele na kila Halmashauri tuna mpango mpana ambao tutakuja kuu-present baadaye hapa, at least tuwe na kituo cha afya katika kila Wilaya kwanza, kituo cha afya kimoja kimoja kwanza na umaliziaji wa magofu. Nadhani Wilaya ya Longido tutaipa kipaumbele hasa katika Kata ambayo ameikusudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie, Serikali haitawatupa na iko tayari kushirikiana na wananchi wa Longido na kushirikiana na Mbunge ambaye yuko mahiri kutetea eneo hilo.
MHE. CATHERINE C. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa, malalamiko juu ya Polisi yamekuwa mengi sana. Wamekuwa wakinyanyasa raia kila siku, kila mkoa. Hivi tu majuzi wiki iliyopita nimeshuhudia Polisi anaejulikana kwa jina la Msafiri akimpiga raia hapa Dodoma kwa amri ya bosi wake. Je, nataka kujua hivi hawa Polisi wako juu ya sheria kwa sababu wanapopiga raia wanapokwenda Polisi wenyewe ndiyo wamekuwa wakiandika kesi. Je, haki itatendeka kweli?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, linapotokea tukio la Askari mmoja ama wawili kufanya jambo hilo si jambo la Jeshi la Polisi linakuwa la Askari mhusika, mtu mmoja na sio utaratibu wa Kiutumishi wa Kipolisi. Polisi kama Jeshi la Polisi Waheshimiwa Wabunge wote tunakubaliana kwamba wanafanya kazi nzuri kwa Taifa letu na ndiyo maana usalama upo. Kwa maana hiyo, inapotokea jambo mahsusi kama hilo tuendelee kuwasiliana na Mheshimiwa Mbunge ni mmoja wa pioneers wa mambo ya haki kutendeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu wetu inapotokea jambo la aina hiyo tuna vitengo ambavyo vinasimamia malalamiko hayo ili haki iweze kutendeka na uzoefu unaonesha haki imekuwa ikitendeka na hata hatua zinachukuliwa katika baadhi ya maeneo na ninyi ni mashahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Catherine aendelee kusukuma hivyo utaratibu wa haki kutendeka na kwa hilo ambalo amelitaja tutalifuatilia ili haki iweze kutendeka.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kwa kuwa Wilaya ya Ngorongoro ni kubwa kuliko
Mkoa wa Kilimanjaro, hali inayopelekea jiografia ya Wilaya hiyo kuwa ngumu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kugawa Wilaya hii ya Ngorongoro au kuweka Halmashauri mbili ili kuwasogezea wananchi wa Ngorongoro huduma kwa karibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli na Mheshimiwa Mbunge pale wa Jimbo hio la Ngorongoro ambalo Naibu Waziri wa Kilimo na yeye alinialika niweze kufika kule jimboni kwake juzi juzi hapa nilikuwepo kule. Kwa
umbali kweli jiografia ya Ngorongoro ina changamoto kubwa sana kwa sababu ukianzia hapa getini ukitoka hapa Karatu mpaka unafika Makao Makuu kule Loliondo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nilipata fursa ya
kutembelea mpaka Ziwa Natron kwenda shule ya sekondari ya Ziwa Natron. Jiografia ya Ngorongoro kweli ni kubwa zaidi, lakini mara nyingi sana maeneo haya yanagawanywa kutokana na population.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia eneo kubwa la Ngorongoro ni hifadhi, lakini kama kutakuwa na haja ya kuweza kugawanya basi kwa mchako ule ule wa kisheria wananchi wa aeneo hilo watafanya hivyo na Serikali itaangalia kama kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inawezekana
tunaweza tukaangalia mbali kwa sababu Ngorongoro na Serengeti ukiangalia jiografia yao ina changamoto kubwa sana. Hili sasa tuwaachie wenye maeneo hayo mkaweza kufanya maamuzi sahihi kama ulivyo Mheshimiwa Catherine Magige unavyokuwa na wazo hilo, basi na Serikali itaangalia nini cha kufanya kwa maamuzi sahihi kwa maslahi mapana kwa wananchi wa Ngorongoro.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yasiyoridhisha ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa katika jibu la msingi Mheshimiwa Naibu
Waziri amesema wafanyakazi hao wa Seventy Seven walilipwa, siyo kweli walilipwa awamu ya kwanza, awamu ya pili haikuwafikia wafanyakazi hawa na baada ya malalamiko Wizara ilituma wakaguzi mwaka 2003 wakakagua wakajua kuna tatizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa watu hao wamekuwa wakihangaika muda mrefu kutafuta haki zao waliandika barua Ofisi ya Rais, tarehe 17 Machi, 2016 walijibiwa barua kutoka Ofisi ya Rais ikienda kwa Waziri wa Maliasili kuwa ashughulikie tatizo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, vilevile walilalamika Ofisi ya Waziri Mkuu na kuna barua ilikuja ya tarehe 4 Novemba, 2016 kuwa tatizo hili lishughulikiwe.
Je, Serikali haioni kwamba wanyonge hawa wanapoteza muda mwingi wakitafuta haki yao huku yenyewe ikidai imewalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Maliasili alishapewa agizo kutoka Ofisi ya Rais ashughulikie, ni kwa nini wanasuasua wananchi wakiendelea kupata taabu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni swali la nyongeza ambalo limejitokeza na hoja ambayo nimeisikia kwa mara ya kwanza hapa, basi nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge anipe fursa katika kipindi cha mapumziko leo hii nilifanyie kazi halafu nimpe majibu ambayo yatakuwa ni ya uhakika zaidi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro, Mkoani Arusha, wamekuwa wakipata shida sana ya usafiri kutokana na ubovu wa barabara.
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ambayo ilikuwa kwenye bajeti ya 2016/2017 ya kujenga barabara ya lami inayoanzia Loliondo hadi Mto wa Mbu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu kumhakikishia Mheshimiwa Magige na Mheshimiwa Olenasha kwamba mkandarasi tunatarajia kumpata muda siyo mrefu kwa sababu taratibu za kumpata mkandarasi zipo katika hatua za mwisho na mara tutakapompata mkandarasi barabara hii itaanza kujengwa.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa kumekuwa na tabia mbaya kwa baadhi ya askari kudhalilisha raia na hata kuwatolea kauli mbaya ikiwemo hata sisi Wabunge tumekuwa tukikutana na kauli mbaya kutoka kwa baadhi ya askari lakini inapokuja kwenye kutetea maslahi yao sisi ndiyo tumekuwa wa kwanza kuwatetea. Je, Serikali inatoa kauli gani? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja, askari wetu wa Jeshi la Polisi pamoja na askari wengine ni Watanzania na wanafanya kazi kwa gharama za maisha yao. Kwa hiyo, tuna wajibu wa kutimiza kama Taifa kwa kutambua kwamba askari wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria na hakuna haki isiyo na wajibu. Sisi kama Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na taasisi zingine tuna utaratibu wa kuchukua hatua punde inapotokea askari amefanya kazi kinyume na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna wajibu ambao Watanzania, wananchi kwa ujumla wanatakiwa watimize wanapokuwa wamekutana na askari wetu. Kwa mfano, afadhali sisi ni viongozi, wengi wetu tunatoa uongozi tunapokutana na askari lakini kuna watu wengine ambao hawatoi heshima inayostahili kwa vyombo vyetu vya dola. Sasa vyombo vyetu vya dola vimepitia mafunzo na mimi kama kiongozi wao nisingependa kuona Jeshi la Polisi linafanana na green guard, blue guard au red brigade.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Watanzania watambue kwamba vyombo vyetu vya dola vina heshima, vinafanya kazi kubwa na vinastahili kupewa heshima kama vyombo vya dola. Ukitaka kupambana na vyombo vya dola wana sehemu ambayo wanaruhusiwa kutumia nguvu wanapoona kile kinachofanywa na raia kinaweza kikahatarisha ama kikaleta athari iliyo kubwa zaidi. Kwa kuwa Waheshimiwa Wabunge tunakutana na watu wetu, tuendelee kuitoa elimu hiyo ili vyombo vya dola katika nchi yetu kama ilivyo katika nchi zingine viweze kupewa heshima vinavyostahili.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Je, Serikali baada ya kupata repoti iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuhusu Pori Tengefu la Loliondo inampango gani wa kutoa suluhu ya kudumu kwenye mgogoro huu uliodumu zaidi ya miaka 20?
Swali la pili, je, Serikali inaweza kuahidi nini juu ya mgogoro huu wananchi wa Loliondo ili waweze kuendelea na kazi zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Catherine Magige Mbunge wa viti maalum Mkoa wa Arusha ambaye kwa kweli licha ya swali hili amekuwa akifuatilia kwa karibu sana juu ya masuala yanayohusiana na changamoto za Pori la Loliondo moja kwa moja akija kuhoji ofisini, lakini kuhusu maswali yake mawili ya nyongeza yote yanafanana kwamba hatua ambayo Serikali inaenda kuchukua ili kuwawezesha wananchi wa maeneo haya waweze kuendelea na shughuli zao kama ambavyo ameuliza.
Mheshimiwa Spika, Kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kamati iliyoundwa imefanya kazi kubwa ya kina kazi ambayo imezingatia maslahi ya pande zote upande wa wananchi lakini pia upande wa maslahi ya Taifa, lakini kwa kuwa ile ni taarifa ambayo ni ya kitaalam lakini pia iliyozingatia kama nilivyosema maslahi ya pande zote na kwa kuwa nimesema tayali iko kwenye dawati la Mheshimiwa Waziri Mkuu basi nimuombe Mheshimiwa Mbunge avute subira Waziri Mkuu bila shaka atakuwa anaipitia kwa kutumia wataalam chini ya ofisi yake baada ya pale taarifa itakayotolewa itakuwa na maelekezo ya namna gani tunaweza kusonga mbele katika kutatua mgogoro huu. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mbali na madini ya Tanzanite kuwa chanzo cha mapato kikubwa kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, lakini pia kuna madini ya aina ya Rubi yanapatikana katika Kijiji cha Mundarara, Wilayani Longido Mkoani Arusha.
Ningependa kujua Serikali, inajipanga vipi ili madini haya aina ya Rubi iweze kuwanufaisha wananchi wa Longido? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kutetea wachimbaji wadogo wadogo Mkoani Arusha na kazi nzuri anayoifanya na wananchi wa Arusha wanaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini ya Rubi yanapatikana katika Kijiji cha Mundarara katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha. Madini hayo yanapatikana na eneo hilo kwa pembeni yake kuna leseni ya mtu anayeitwa Mheshimiwa Mareale. Sasa hivi ni kwamba kuna wachimbaji wadogo wanavamia eneo lile. Sisi kama Serikali tunawapenda wachimbaji wadogo, lakini tunataka wafuate taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokitizama sasa hivi ni kwamba lile eneo ambalo ni la mtu ambaye anayelimiliki na haliendelezi, tutaangalia namna bora ambayo tunaweza tukawatafutia wale wachimbaji wadogo waweze kuchimba na tuwatambue na wachimbe katika vikundi ili tuweze kuwatambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanapochimba, basi tuweze kama Serikali kupata kodi zetu pale, tupate mrahaba pale, Halmashauri ya Longido ineemeke na Serikali kwa ujumla ineemeke na zile fedha tupeleke kwa wananchi wengine ambao wako nje na maeneo ya uchimbaji, waweze kuneemeka kupata huduma za maji, barabara na huduma za afya. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kuna Kamati ya Maudhui, siku za karibuni tumekuwa tukishuhudia wasanii wetu wengi wakifungiwa nyimbo zao, wasanii ambao wamehangaika kutafuta pesa za kurekodi kwa shida na ukizingatia kuna uhaba wa ajira.
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuambia Kamati hiyo ya Maudhui imeshindwa kazi, kwa sababu wamekuwa wanaachia mpaka nyimbo zinatoka ndiyo wanakuja kuwafungia wasanii wetu? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kila Taifa lina utamaduni wake na lazima liulinde kwa udi na uvumba. Tunachokifanya sio kwamba tuna vita na wasanii wetu, hapana! Lengo letu ni kulinda maadili ambayo katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo ya kasi ya kiteknolojia na habari, kuna mmomonyoko mkubwa sana wa maadili katika nchi yetu ni lazima tuchukue hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachokifanya hapa siyo kitu cha pekee duniani, kila mtu anafanya hivyo na hawa wasanii wetu tumeshawasamehe wasirudie tena. Nitoe mfano mmoja mdogo…

Mheshimiwa Naibu Spika, mwanamuziki Rick Ross ambaye amepiga muziki pamoja na kijana wetu nyota wa muziki Diamond hapa, wimbo wao huu wa wakawaka, huyo mwanamuziki miezi michache iliyopita amepata matatizo Marekani kwa kuimba wimbo unaoitwa U.O.E.N.O ambao maudhui yake yanaleta picha ya kwamba anaunga mkono ubakaji. Marekani nzima akina mama walikuja juu, wimbo ukaondolewa kwenye televisions zote, lakini na yule kijana akaomba radhi kwa wanawake wote kwamba amewaudhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tumekuwa kokoro, tupokee kila kitu, kwa sababu hatuna utamaduni. Baba wa Taifa alisema mwaka 1962, Taifa lisilo na utamaduni wake ni Taifa mfu nasi hatuwezi kukubali kuwa Taifa mfu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yanayotokea Tanzania yanatokea duniani kote. Nitoe tu maelezo kidogo, maana Viongozi wetu hapa wanalalamika ni kwa sababu dunia pana hawajaielewa. Davido mwanamuziki maarufu duniani ambaye amepiga na kijana wetu Diamond hapa kafungiwa nyimbo zake mbili na Nigerian Broadcasting Corporation mwaka huu. Siyo huyo tu, Wizkid kafungiwa nyimbo zake, Nine Eyes kafungiwa nyimbo zake, sijasikia Wabunge wa Nigeria wakilalamikia sheria zao wenyewe, sisi ni Wabunge kazi yetu kubwa ni kuhakikisha jamii inaheshimu, inalinda sheria za nchi na tutaendelea... (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa mwisho, Koffi Olomide amepiga wimbo unaitwa Ekotite, huu wimbo ni marufuku kupigwa Congo (DRC)…

Mheshimiwa Naibu Spika, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge mnaosafiri kwenda Congo, unaambiwa tukupigie wimbo gani ukisema Ekotite watakushangaa! Huo wimbo ni matusi wameufungia. Sisi hapa Wabunge tunakuwa wa kwanza kuruhusu nchi yetu iwe kokoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, BBC ambayo iko Uingereza ambako ndugu zangu wanadhani ndiko mwanzo wa ustaarabu, wamefungia nyimbo 237 katika historia yao, hapa tunalalamika nyimbo mbili kufungiwa. Tutaendelea kufungia kulinda utamaduni wa nchi yetu. Ahsante. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Kwa kuwa mwaka huu tumebarikiwa mvua lakini mvua hizi zimeleta madhara sehemu mbalimbali na kuharibu miundombinu ya barabara.
Ningependa kujua, je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na majanga haya ya barabara hususani zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA)? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Serikali tumejipanga na kama ilivyo kawaida kila mwaka tunatenga fedha kwa ajili ya kutibu dharura kwa maana ya emergency, kwa sasa hivi maeneo mengi ambayo barabara hazipitiki tumewaagiza Meneja wa TANROADS washirikiane na TARURA ili kuweza kuokoa sehemu hizi ambazo hazipitiki na Wizara tunaendelea kuratibu na kufuatilia ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma wanapita kwenda kwenye shughuli zao za maendeleo. Ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa umeme wa 400KV ni mkubwa sana na unahitaji transfoma zenye ubora wa hali ya juu. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutumia transfoma zetu za kiwanda cha TANELEC cha Arusha ambazo zina ubora wa hali ya juu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa na ninamshukuru sana Mheshimiwa Catherine na ninampongeza pia kwa kufuatilia masuala ya nishati akiwa pia ni Mjumbe wetu wa Kamati ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba umeme unaosafirishwa kwa njia hii ya msongo wa 400KV ni mkubwa na kwa kuwa ni mkubwa, Wizara yetu ya Nishati ilishatoa maelekezo kwamba kuanzia sasa vifaa vyote vinavyotumika kwenye miradi ya umeme vinatakiwa kutoka kwenye viwanda vyetu vya ndani na kimojawapo ni Kiwanda na TANALEC-Arusha. Mara kadhaa takribani kama zaidi ya mara mbili Mheshimiwa Waziri amefanya ziara katika kiwanda kile. Kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha transfoma kama 10,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kutoa wito kwa Wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya umeme nchini pamoja na Shirika la umeme, TANESCO kwamba bado agizo letu liko pale pale, vifaa vyote vitoke ndani ya nchi na viwanda vyetu vina uwezo na mara kadhaa tumekutana navyo na vimetuthibitishia. Ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza; katika Wilaya ya Karatu mkoa wa Arusha kijiji cha Mang’ola kuna biashara kubwa ya kimataifa ya vitunguu ambapo robo ya mapato ya Halmashauri ya Karatu yanatokana na kilimo hiki cha vitunguu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea mabwawa na mifereji ya umwagiliaji wananchi hawa wa Mang’ola ili kuongeza tija kuwainua kimaisha wananchi wa Karatu hasa akina mama waliowekeza katika kilimo hiki cha vitunguu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu asilimia kubwa zaidi ya 70 wanaishi vijijini na wanategemea kilimo cha kudra za Mwenyezi Mungu kwa maana ya mvua. Kwa hiyo sisi kama Wizara ya Maji tukaona haja sasa ya kuwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kuhakikisha kilimo chetu kinakuwa bora na tija katika suala zima la uzalishaji, kwa maana ya kupata malighafi za viwandani na hata katika suala zima la biashara. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji hatutokuwa kikwazo katika kuhakikisha tunatengeneza miundombinu ya umwagiliaji eneo hilo ili wananchi wale waweze kunufaika na kilimo cha kisasa.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa uongozi wa Mkoa wa Arusha chini ya Mkuu wa Mkoa Ndugu Mrisho Gambo, anafanya jitihada mbalimbali za ujenzi wa vituo vya afya na zahanati katika Mkoa wetu wa Arusha. Mfano tu katika Jiji la Arusha kuna ujenzi wa Kituo kikubwa cha Afya cha Murieth pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Arusha Mjini unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu, Serikali imejipanga vipi kutuletea watumishi mara tu vituo hivi vitakapokamilika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba uniruhusu nichukue fursa hii kuupongeza Mkoa wa Arusha kwa kazi nzuri ambayo wanafanya katika suala zima la ujenzi wa vituo vya afya na hasa hicho Kituo cha Afya cha Murieth maana na mimi nimeenda kukitembelea, ni miongoni mwa Vituo vya Afya ambavyo vimejengwa vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba Vituo vya Afya vinapokamilika huduma ziweze kutolewa na hakuna Kituo cha Afya hata kimoja ambacho kitakamilika Serikali ikakosa kupeleka watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie, immediately baada ya kwamba Vituo vya Afya vyote vya Arusha na maeneo mengine vikishakamilika, Serikali itapeleka watumishi pamoja na vifaa ili huduma za afya ziweze kutolewa kama ambavyo Serikali imekusudia. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana Watanzania wamekuwa wakilipa Concession Fee sawa na wageni. Je, ni kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuwa-charge Concession Fee Watanzania tofauti na wageni?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumjibu Mheshimiwa Catherine Magige, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Concession Fees inalipwa katika hoteli za kitalii na ni kwa wageni wanaotoka sana sana nje ya nchi, kwa wenyeji hawatozwi. Katika hilo, zile hoteli ambazo zinamilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa hazitozwi hiyo Concession Fee. Kwa hiyo, hii ni specifically kwa zile hoteli za kitalii.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum wamekuwa na majukumu makubwa sana ndani ya mikoa yao; je, ni lini sasa Serikali itaanza kuwapatia Wabunge wa Viti Maalum Mifuko ya Jimbo kama walivyo Wabunge wa Majimbo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mapendekezo yamekuwepo mengi nje na ndani ya Bunge kuhusu Wabunge wa Viti Maalum nao kupewa sehemu ya fedha kama Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa maelekezo yaliyoko kwenye sheria hiyo, mpaka sasa hivi bado Wabunge wa Viti Maalum hawajaingizwa kwenye huo mfumo. Sasa kwa sababu ni pendekezo ambalo linahitaji majadiliano ya awali ndani ya Serikali kwanza, naomba nalo nilichukue.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi kwa kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa waajiri wengi nawapotoa nafasi za ajira, wanahitaji waombaji ambao wanaomba wawe na experience na wanachuo wengi wanaomaliza vyuo wanakuwa hawana uzoefu. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia wanavyuo wanapotoka vyuoni waajiriwe bila kuulizwa experience?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, siyo kazi zote zinahitaji uwe umepata uzoefu. Kuna kazi ambazo zinatangazwa ambazo wanachukuliwa wanafunzi waliotoka vyuoni moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kama nilivyosema lengo la kuanzisha mfumo wa elimu ambao vilevile unafundisha stadi za kazi ni kuhakikisha kwamba hata tunapokuwa mashuleni tayari kuna uzoefu ambao tumekuwa tumeupata. Ndiyo maana hata Serikali kwa sasa inawekeza sana kwenye elimu ya ufundi ili wanafunzi wanapokuwa mashuleni na vyuoni wawe tayari wameshaanza kufanya practicals ili wakienda kwenye ajira kwamba wawe tayari wanaweza kuajiriwa. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mkoa wa Arusha jiografia yake ni pana sana na mkoa huu upo mpakani, hivyo unahitaji uangalizi mkubwa kiusalama, lakini magari mengi ya polisi ni mabovu. Je, ni lini Serikali inafikiria kutuletea magari ya polisi mapya ndani ya Mkoa wa Arusha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Arusha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya magari iliyopo katika Mkoa wa Arusha nayo tunaitambua. Katika mkakati wetu siyo tu kupeleka magari mapya lakini tunajitahidi kuangalia uwezekano wa kuyafanyia matengenezo yale magari ambayo yanaweza yakarekebishika. Kazi hiyo imewezwa kufanywa katika baadhi ya mikoa na Arusha tutaangalia uwezekano wa kuweza kukarabati magari hayo lakini wakati huohuo magari yatakapokuwa yamepatikana tutaweza kuyasambaza katika mikoa yote nchini ikiwemo Mkoa wa Arusha.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba nianze kwa kuwapongeza Wakurugenzi wote nchini akiwemo Kayombo wa Ubungo na Arusha Mjini kwa kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa kuwa ili kuwa thabiti katika utumishi wa umma ni pamoja na kuwajali watumishi; na Mheshimiwa Rais alianza kuonyesha mfano kwa kuwajali walimu wa shule za msingi kwa kuwapatia tablets, napenda kufahamu, je, Serikali ina mikakati gani kuwajali watumishi wa umma katika maslahi yao? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anataka kujua Serikali inafanyaje katika kuwajali watumishi. Tarehe 1 Mei, 2018 Mheshimiwa Rais alipohutubia Uwanja wa Samora pale Iringa alipokuwa mgeni rasmi, alipokuwa anajibu risala ya wafanyakazi alisema; Serikali yake inatumia fedha kadri zinavyokusanywa. Kwa hiyo, ataboresha maslahi ya watumishi wa umma kulingana na uwezo wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alisema;“mimi sitangoja May Day, siku yoyote nitakapotosheka kwamba hali ya Mfuko wa Serikali inaniruhusu kufanya nyongeza, kuboresha maslahi ya Watumishi wa Umma nitafanya hivyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niseme kwamba Serikali inawajali watumishi, inawapeleka mafunzo, wanapewa mikopo, wengine tunawadhamini katika kupewa mikopo, tunawapeleka kusoma nchi za nje katika taaluma mbalimbali, hiyo yote ni kujali watumishi, maana kumjali mtumishi siyo lazima kumpatia fedha tu, hata ukimpeleka mafunzo, unamjali mtumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo yote niseme kwa kifupi kwamba tunaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wa umma, lakini kwa upande wa mishahara kama nilivyosema tutapandisha mishahara pale hali ya nchi itakaporuhusu.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mkoa wa Arusha ni Mkoa ambao una shughuli nyingi sana haswa za kipolisi, zikiwemo na ku-escort viongozi mbalimbali, lakini inasikitisha sana Mkoa wa Arusha RPC wetu hana gari la polisi kutokana na gari lake lilipata ajali muda mrefu. Je, Serikali haioni ni muhimu kulichukulia jambo hili kama la dharura na kumpelekea RPC wetu wa Mkoa wa Arusha gari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna umuhimu mkubwa RPC kuwa na gari. Nataka tu nimthibitishie kwamba kama gari la RPC limepata ajali basi tutaangalia uwezekano wa kulifanyia ukarabati gari hilo, likishindikana basi RPC wa Tabora tutampatia gari nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Samahani ni RPC wa Arusha.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha imetengwa kimawasiliano kwa muda mrefu sana, hata imefikia stage Mkurugenzi wa Halmashauri anashindwa kuwasiliana kwa njia ya email katika shughuli zake za kikazi. Je, ni lini Serikali itaunganisha Wilaya ya Ngorongoro na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Catherine Magige kwa jinsi ambavyo anafuatilia sana huduma mbalimbali zinazotakiwa kupatikana katika mkoa wake na hasa eneo alilolitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna baadhi ya wilaya hapa nchini bado hazijaunganishwa lakini ni chache. Kati ya Wilaya 187 bado hatujaunganisha Wilaya 16 na tumeshawaelekeza TTCL waende wakaunganishe Mkongo ili huduma hizo ziweze kupatikana. Ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kilimo cha mbogamboga na matunda hukubali kuzalishwa sana katika Ukanda wa Kaskazini na Nyanda za Juu Kusini; je, ni nini mkakati wa Serikali katika kuimarisha kilimo hiki.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuwapongeza wakulima wote nchini ambao wamegundua umuhimu wa kilimo hiki ambacho tunaita tasnia ya horticulture. Sisi kama Serikali ni kweli tumeona kuna umuhimu sana wa tasnia ya horticulture, ndiyo maana hata pale katika Wizara yetu ya Kilimo sasa hivi tumeamua kuweka mtu ambaye atakuwa anashughulikia tu masuala ya horticulture, kwa maana ya focal person.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile tunasisitiza kwamba tasnia hii ya horticulture iendelee kuwa ni kilimo cha kibiashara. Kwa sababu licha ya kwamba ni afya katika mwili vile vile kinaliingizia Taifa pato kubwa sana. Pia niziase tena halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba wanakuwa na kitalu nyumba kwenye kila halmashauri na kuweza kufanyika hayo mavitalu nyumba kama shamba darasa. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati alifanya ziara katika Jiji la Arusha tarehe 18 Machi na alifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Mkonoo, Kata ya Terat na kuwaahidi hadi kufikia mwezi Aprili, umeme wa REA utakuwa umeshaanza kushughulikiwa, lakini sasa ni Mei hakuna chochote kinachoendelea, je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake kwa wananchi hawa wa Mkonoo, Kata ya Terat? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa, ni kweli Mheshimiwa Waziri alifanya ziara katika Kata hiyo ya Terat na kwa kuwa Mkoa wa Arusha Mkandarasi wake NIPO ambaye anafanya kazi vizuri alitoa maelekezo hayo na kwa kuwa mkandarasi NIPO ni mmojawapo wa Wakandarasi ambao wamefunguliwa Letter of Credit na ameagiza vifaa, ninaamini kwamba kazi itafanyika. Kwa hiyo, napenda nimwagize Mkandarasi NIPO wa Mkoa wa Arusha atekeleze agizo la Mheshimiwa Waziri na kwamba mwezi huu wa tano unaoendelea mpaka mwezi wa sita umeme uwe umewaka katika maeneo haya ambayo yameainishwa. Nampongeza sana Mheshimiwa Catherine. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza Swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha hususani Loliondo wamekuwa wakitegemea hospitali ya Waso kwenye matibabu na hali hii inapelekea msongamano mkubwa katika hospitali ya Waso. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga hospitali ya Wilaya ya Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Magige ni shuhuda kwamba tumeweza kujenga hospitali ya Wilaya Arusha pale na Vituo vya Afya vingi ikiwepo na Murieti na yeye ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakipigania suala zima la afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie tumeanza na hospitali 67, tukishamaliza hizo 67 tutaenda maeneo yale ambayo hakuna hospitali za Wilaya ili kupunguza mlundikano kwa wananchi kupata huduma.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa tumekuwa tukishuhudia ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika Mkoa wangu wa Arusha, Wilaya mbalimbali kama Longido, Monduli na nyinginezo na upanuzi mkubwa wa vituo vya afya ukiendelea, nataka kufahamu; Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha wanaleta wataalam wa kutosha hasa wa dawa za usingizi ili wananchi wa Arusha wapate huduma, hasa ya mama na mtoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali imewekeza katika uboreshaji wa vituo vya afya takribani zaidi ya 300 nchi nzima. Hata hivyo tunatambua kwamba uboreshaji huu unaendana sambamba na kuongeza huduma za upasuaji. Sisi kama Serikali sasa hivi tumeshapeleka watumishi zaidi ya 200 kwenda kusomea masuala ya usingizi. Tunatumaini ndani ya muda mfupi huu watumishi wale watakuwa wamekamilisha mafunzo hayo na tutawasambaza katika vituo vya kutolea huduma.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza, kwanza naipongeza Serikali kwa kutupatia pesa katika kituo cha Afya cha Sakala milioni mia nne na Usunani milioni mia nne katika Wilaya ya Ngorongoro Mkoa wa Arusha. Nilitaka kufahamu katika kwa kuwa vituo hivi vinakamilika siku si nyingi je Serikali imejipangaje, kuhakikisha inatuletea vifaa tiba na raslimali watu katika vituo hivi viwili vya Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Catherine jinsi ambavyo amekuwa akiwapigania wananchi wa Mkoa wa Arusha hususani kuhusiana na suala zima la Afya, baada ya pongezi hizo naomba nimjibu Mbunge na kwa Wabunge wote ambao wana maswali kama hayo kuhusiana na lini vifaa na wataalam watapelekwa ili hayo majengo ambayo yamekamilika yaanze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ambayo tunaikaribia 2019/2020 sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI, fedha nyingi tumetenga ili tuweze kuhakikisha kwamba tunapata vifaa vyote ili Vituo vya Afya vianze kufanya kazi iliyokusudiwa. Kwa sababu utakubaliana na mimi kwamba ukiwa na majengo mazuri bila kuwa na vitendea kazi itabaki kuwa White elephant na sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI hatutaki kuwa sehemu ya mzigo huo. Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge mchakato uko katika hali nzuri ili tuhakikishe kwamba Vifaa vinapatikana na Watumishi wa kutosha wanapatikana ili majengo yakishakamilika huduma ianze kutolewa.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wafanyakazi hawa hawakulipwa kama ambavyo jibu linasema lakini walikuwa wakikatwa mishahara yao kila mwezi na pesa hazikuwasilishwa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kinyume na utaratibu wa kisheria na ni wajibu wa Serikali kuhakikisha makato ya wafanyakazi yanawasilishwa kwenye mifuko na si wajibu wa wafanyakazi. Je, Serikali inatoa tamko gani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa madai ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakidai mafao yao yamekuwa mengi sana ikiwepo hata iliyokuwa Hoteli ya Sabasaba ya Mkoani Arusha mpaka leo hawajaliwa mafao yao na nimekuwa nikifuatilia kwa mrefu sana. Je, nini tamko la Serikali?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali hilo lakini naomba nichukue nafasi hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Catherine Magige katika maswali yote mawili ya nyongeza amelihakikishia Bunge hili kwamba bado lipo tatizo kwanza la kulipwa kwa pensheni kwa wafanyakazi hao lakini lipo tatizo la mwajiri kutopeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko iliyokuwa inachangiwa na hao wafanyakazi. Naomba nitumie nafasi hii kuagiza viongozi watendaji wa Mifuko iliyokuwa inahusika na wafanyakazi wa taasisi zote hizi mbili na kwa mujibu sheria mpya tuliyonayo ni wajibu wa Mfuko wenyewe kuhakiksha michango ya mwajiri inapelekwa kwenye mifuko husika, hivyo basi mifuko hiyo ifanye haraka kukutana na wafanyakazi hao na zilizokuwa taasisi zinazosimamia mafao ya wafanyakazi hao ili tuweze kujua nini kilichojiri na kama wanazo stahili zao kwa mujibu wa sheria waweze kulipwa mapema sana na kuweza kuondoa adha kwa wafanyakazi wote katika Taifa letu.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Tunashukuru Serikali kwa kujenga Kituo cha Afya cha Kaloleni katika Jiji la Arusha pamoja na kutujengea jengo la mionzi lakini kituo hiki hakina mashine ya X-ray. Je, ni lini Serikali itatuletea mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya cha Kaloleni katika Jiji la Arusha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi Serikali iko katika maandalizi ya mpango wa kufanya uboreshaji wa huduma za mionzi nchini na tumeanza kwanza katika Hospitali za Rufaa za Kanda, Mikoa na baadhi ya Wilaya. Tutakapomaliza hapo tutakuja sasa kuangalia vituo vya afya ambavyo vina uwezo kuweza kupata hizo huduma na wataalamu ambao wanaweza kutoa hizo huduma.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa tumeona shule nyingi kongwe zilizotoa viongozi mbalimbali zimekuwa zikikarabatiwa. Kwa Mkoa wangu wa Arusha, kuna Shule ya Arusha Sekondari ambapo miundombinu yake ni mibovu na chakavu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutenga pesa kwa ajili ya kukarabati shule hii kongwe ya Arusha Sekondari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, msemaji mzuri sana wa Mkoa wa Arusha na Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni nia ya Serikali kukarabati shule zote kwa wakati mmoja kama ingewezekana lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti jambo hilo halijawezekana, tutakarabati kulingana na uwezo lakini pia kuna vigezo mbalimbali. Kwa hiyo, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Mbunge, tufanye tathmini, tumeshamaliza awamu ya kwanza tupo kwenye mpango wa awamu ya pili, huenda kwenye awamu ya tatu Shule ya Arusha Sekondari ikaingizwa kwenye mpango huu wa Serikali wa kukarabati shule hizi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa imekuwa ni ahadi ya muda mrefu ya Serikali kujenga Soko la Mto wa Mbu Wilayani Monduli Mkoani Arusha, lakini mpaka sasa hakuna chochote kinachoendelea na wananchi wa Mto wa Mbu wamekuwa wakipata taabu: Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Soko la Mto wa Mbu Mkoani Arusha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ni kweli hili suala hata Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mheshimiwa Julius Kalanga ameniuliza jana. Kama nilivyosema, namwomba Mheshimiwa Mbunge wakae na Halmashauri yao, fedha zipo kama ulivyosema. Ni kuandika andiko na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tupo tayari kusaidia utaalaam na namna ya kuboresha pamoja na Hazina ili andiko likamilike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua kuna wapiga kura wengi sana pale Mto wa Mbu, tungependa wapate soko zuri, wapate kipato, pia wachangie kodi katika maendeleo ya Watanzania wenzetu. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane hili jambo liweze kufanyiwa kazi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuwa vituo hivi vya ukaguzi wa magari barabarani siyo tu muhimu kwa wananchi vilevile ni muhimu sana kwa Askari wetu. Tunatambua kazi kubwa wanayofanya Askari wa Barabarani, lakini Askari hawa mara nyingi wanapopata ajali kulipwa haki zao inachukua muda mrefu. Kwa mfano tu, katika Mkoa wangu wa Arusha kuna Askari wengi waliopata ajali wakiwa kazini, lakini mpaka sasa hivi hawajalipwa stahiki zao.

Je, ni lini Serikali italipa maaskari ambao wamepata ajali kazini haki yao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza lazima nikiri kwamba kulikuwa na changamoto za baadhi ya malipo ya stahiki mbalimbali za Askari wetu nchi nzima ikiwemo hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameizungumza, lakini lazima nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano, lazima tujipongeze kwa pale ambapo tutafanya vizuri.

Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya malimbikizo haya yameanza kulipwa na tunaamini kwamba kama kutakuwa kuna maeneo ambayo bado hayajakamilika, kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amezungumza, hii fidia ya Askari ambao wanapata ajali barabarani, basi tutakamilisha pale michakato mingine ikiwemo uhakiki pamoja na bajeti itakapokaa sawa.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama ana maombi mahususi ya Askari ambayo anafahamu, basi aweze kutupatia ili tufuatilie tujue ni tatizo gani lililosababisha mpaka leo wawe hawajapatiwa stahiki zao?
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa ndege zetu za Air Tanzania zimekuwa zikishindwa kutua katika Uwanja wa Ndege wa Arusha kwa kuwa kiwanja hiki ni kidogo na tunaelewa kabisa Arusha ni kitovu cha utalii na nimekuwa nikiongea kila mara na…

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Serikali imekuwa ikiniahidi lakini haitimizi, mpaka sasa hivi nimechoka kufuatilia. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupanua Kiwanja cha Ndege cha Arusha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Arusha, kama ifutavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri ukweli kwamba Mheshimiwa Catherine Magige amekuwa akifuatilia sana suala la upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Arusha na nimpongeze kwa sababu kwa kupitia juhudi zake nimtaarifu rasmi kwamba TANROADS sasa hivi wanaandaa BOQ kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo kwa mita 200 zaidi lakini pia wanashirikiana na TAA katika kuhakikisha kwamba uwanja huo unaendelea kupanuliwa pamoja na kuwekewa apron nyingine mpya. Hivi karibuni mkandarasi ataingia site kwa ajili ya upanuzi wa uwanja huo ili ndege kubwa ziweze kuanza kuruka.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza, kwa kuwa hivi karibuni kumekuwa na malalamiko ya Viwanda vya ndani kukosa masoko kikiwemo na Kiwanda cha marumaru. Je, nini Mkakati wa Serikali kuhakikisha Viwanda vya ndani vinapata masoko ya uhakika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa kumekuwa na malalamiko ya bidhaa nyingi zisizo na ubora kuingizwa katika Nchi yetu. Je, ni nini Mkakati wa Serikali kuhakikisha bidhaa ambazo hazina ubora yaani bidhaa feki hazingii katika nchi yetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kwamba Viwanda vya ndani vinapata masoko ya uhakika ikiwemo hivi vya marumaru kama ambavyo umesema ni kweli kabisa kama ambavyo nimejibu kwenye jibu la msingi ni kwamba marumaru zinazozalishwa nchini sasa hivi ni takribani mita za mraba 32.4 milioni na matumizi yetu ni takribani mita za mraba 30 milioni lakini unakuta bado ni kwamba bidhaa kama hizo zimeendelea kuingia toka nchi za nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na kwamba Viwanda hivi vinatumia malighafi takribani asilimia 95 ambazo zinapatikana hapa nchini kimsingi tunastahili kuvilinda ili viweze kuhakikisha kwamba vinapata masoko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kama ambavyo nimesema kwamba tutaongeza Kodi kwa hizo bidhaa zinazotoka nje ili kuhakikisha kwamba hizi za ndani zinakuwa na bei yenye ushindani. Hata hivyo, napenda kutoa angalizo kwa wenye Viwanda hivyo pamoja na wenye Viwanda wengine, si tu kwamba kwa sababu Serikali imeamua kuongeza Kodi kwenye hizo bidhaa wao sasa wakae tu bila kufanya majukumu yao ya msingi ikiwemo kuandaa business strategies nzuri na marketing strategies ili kuweza kuwafahamisha watumiaji juu ya ubora wa bidhaa zao ili hayo hatuyaendekeza sana kwa sababu tungependa pia walaji wapate bidhaa zilizo nzuri na wanazozitaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuhusu bidhaa feki kupitia TBS, TBS imeendelea kufanya ukaguzi kwa bidhaa zote zinazotoka nje ya nchi na hata zile za ndani kwa mfano kuanzia mwaka 2015 mpaka sasa ni kwamba jumla ya sampuli sabini na nne elfu mia sita tisini na saba zimefanyika na kuzitambua bidhaa ambazo zimefikia viwango vinavyotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa bidhaa zinazotoka nje zinakaguliwa kutoka huko nje kabla hazijaingizwa na hata zikitokea kwamba hazikukaguliwa nje tunakagua hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe watanzania kuzingatia Viwango ambavyo vinastahili. Ahsante sana.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Catherine Magige kwa swali zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, mkakati wa Serikali sio tu kulinda viwanda vya ndani, lakini pia mkakati wa Serikali ni kusaidia viwanda vya ndani na wafanyabishara waweze kufanya biashara nje ya nchi, ndani ya SADC, Jumuiya ya Afrika na hivi sasa tunafanya uchambuzi wa kuhakikisha nchi yetu inajiandaa vizuri na Soko la Pamoja la Afrika yaani Africa Continental Free Trade Area.

Kwa hiyo mpango wa Blue Print, hivi sasa Serikali tumeanda Muswada kwa ajili ya kuja hapa Bungeni, Muswada ambao utasaidia kuweka mazingira ya kirafiki kwa Watanzania kufanya biashara si tu ndani lakini kwenye bara la Afrika na maeneo mengine ya dunia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mkakati wetu ni kulinda viwanda vya ndani lakini pia kuvipa fursa ya kufanya biashara za kimataifa. Nashukuru sana.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa barabara ya Karatu - Mang’ola katika Mkoa wa Arusha imekuwa ikitengenezwa mara kwa mara na kuisababishia Serikali gharama kubwa. Je, ni lini Serikali itajenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa sababu eneo la Mang’ola ndilo linalotegemewa kwa uchumi wa Karatu kwa sababu lina ulimaji Mkubwa wa zao la vitunguu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tumejipanga vizuri kuijenga barabara hii. Barabara hii ni muhimu inaunganisha Mkoa wa Arusha pamoja na Mikoa mingine Ukanda wa Ziwa, kwa hiyo, tuko katika hatua za mwisho kwa sababu kazi ya kufanya usanifu katika barabara hii ilishafanyika tunafanya review na mara tu tutakapopata fedha barabara hii itajengwa kwa kiwango cha lami. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuwa kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu katika Wilaya ya Arumeru katika kijiji cha Ngalinanyuki na hifadhi ya Taifa ya Mumera, na mpaka sasa hivi wananchi wale hawajafikia muafaka wa mgogoro huo.

Je, Serikali sasa ni wakati muafaka wa mimi na Mbunge aliyeapishwa leo na Mheshimiwa Waziri kuongozana mpaka Kijiji cha Ngalinanyuki kwenda kusikiliza wananchi wale ili kero yao ifikie muafaka?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa hapa Bungeni na Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu swali na nyongeza na Mheshimiwa Catherine Valentine Magige kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwamba kwanza katika eneo la Arusha National Park ususani katika sehemu hiyo ya Momera hakuna mgogoro per se hakuna mgogoro unaoweza kuita mgogoro. Lakini kwa sababu wananchi walienda mahakamani na walishindwa, kwa hivyo eneo lote lile ambalo walikuwa wanalidai ni eneo la Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini pamoja na malalamiko ya wananchi na pamoja na kwamba wameshinda kesi mahakamani. Serikali imeona ikate sehemu ya eneo la Arusha National Park ambalo lilikuwa ni miongoni mwa mashamba yaliyokuwa ya settlers wa eneo lile ili kuwagaia wananchi waweze kuishi kwa raha na amani zaidi. Kwa hiyo, wakati process hiyo itakapokamilika wananchi wa Momera watapata eneo ambalo tunazungumzia.

Mheshimiwa Spika, kuhusu kuongozana nae kwenda kutoa maelezo hayo nitaomba aongozane na Mheshimiwa Naibu Waziri baada ya Bunge hili.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa maonesho ya madini yaliyokuwa yanajulikana kama Arusha Gem Fair yalikuwa yanafanyika kuanzia mwaka 1992 na mwaka 2017 maonesho haya yalisimamishwa. Maonyesho haya yalikuwa muhimu kwa kuwa yalikuwa yanaitangaza Tanzania na kuonesha Tanzania ina madini yenye ubora wa hali ya juu ya kuweza kuitangaza Tanzania katika soko la kimataifa na kuingiza Tanzania katika ushindani wa soko la kimataifa. Je, ni lini Serikali itarudisha maonesho haya ya madini ya Arusha Gem Fair? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kuwapigania wachimbaji wa madini wa Arusha, anafanya kazi kubwa sana na kwa kweli tunampongeza kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nipende tu kusema kwamba baada ya mabadiliko ya Sheria ya Madini tuliyoifanya hapa Bungeni, ile Sheria ya Madini ya mwaka 2010, tukafanya mabadiliko mwaka 2017 ni kwamba tuliweza kuzuia utoaji wa madini ghafi (raw minerals) ni kwamba mpaka yaongezewe thamani ndiyo tuweze kuyatoa. Vilevile, ni kwamba maonesho haya mara nyingi yalikuwa yanafanyika pamoja na uuzaji wa madini hayo, kwa hiyo, wale organizer wa maonesho haya walikuwa wanatuomba kwamba kipindi cha maonesho haya waweze ku-export au kuweza kutoa nje madini ghafi na sheria ilikuwa inazuia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sasa hivi tumekwenda vizuri, nadhani kufikia mwaka huu mwezi Julai mpaka wa Septemba tutakuwa tumefika sasa mahala pazuri tumekwisha kuelewana na hawa organizer wa haya maonesho na uzuri wa maonesho haya huwa yana kalenda ya kidunia.

Kwa hiyo, kalenda yetu ya mwaka ambao ukifika kwa maana ya Tanzania kupata zamu ya kuweza ku-organize maonesho haya, basi tunaweza tukaanza kukaribisha wawekezaji, waoneshaji na waoneshaji wakatoka katika maeneo/nchi zingine lakini vilevile kuweza kuonesha madini yetu ya Tanzanite ambayo kwa kweli sasa hivi wadau wengi wamekubali kuyaongezea thamani kwa maana ya kukata na sasa wapo tayari kwa ajili ya kuweza kupeleka kwenye maonesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tupo tayari sasa kuyaridisha maonesho hayo wakati wowote ratiba ikishakuwa sawasawa, basi tutaweza kuyarudisha maonesho hayo na wananchi waweze kushiriki, ahsante sana.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuwa barabara inayoanzia King’ori, hadi Ngarenanyuki imekuwa kero kubwa sana kwa wananchi wa Jimbo la Arumeru Mashariki, na Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi kujenga barabara ii katika kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kufahamu ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi yake kwa wananchi wa Arumeru Mashariki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Magige kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba ni lini barabara ya Kilole kwenda Ngarenanyuki itajengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hizi zote ambazo zimeainishwa tuna uhakika tutazikamilisha katika kipindi hiki cha miaka mitano. Lazima kutakuwa na mahali tutaanza na barabara chache lakini tutamaliza zote. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara zote ambazo zimeainishwa na ambazo zimeahidiwa zipo kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Kipaumbele ni zile barabara ambazo zinaunganisha mikoa na mikoa, wilaya na wilaya. Ahsante.
MHE. CATHERINE MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza tunaishukuru Serikali kwa mradi mkubwa wa maji wa shilingi bilioni 520 katika Jiji la Arusha. Mradi huu changamoto yake kubwa unapita katika maeneo ya mjini, lakini maeneo ya pembezoni kwenye Kata kama Olmoti, baadhi ya sehemu za Muriet, Moshono na Olasiti hazifiki. Je. Serikali haioni sasa kuna umuhimu mkubwa wa mradi huu wa maji kuhakikisha unapita katika Kata za pembezoni mwa Jiji la Arusha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mji wa Arusha una bahati kubwa sana, kwa sababu una mradi wenye fedha nyingi sana na ni mradi ambao tunautarajia umalize kero ya maji katika Jiji la Arusha. Katika maeneo haya aliyoyataja, ni jana tu nimekuwa nikiongea na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Arusha, aliyeongozana na timu iliyotoka kule ikiwa pamoja na Mheshimiwa Diwani Miriam, tayari nimeshafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, maeneo ambayo yako pembezoni, wenzetu wa Mamlaka ya Maji ya Arusha, pale tayari na wenyewe wanaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuona namna bora ya kuendelea kutanua mitandao ya mabomba kuwafikia wananchi. Hili nalo tutalisimamia kwa karibu kabisa kuhakikisha maeneo yote ya pembezoni, Mamlaka pamoja na RUWASA wanawajibika ili maji yaweze kuwafikia wananchi. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, katika Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha kuna mradi mkubwa wa maji wa vijiji (8) maarufu kama Mradi wa Magehe, mradi huu unagharimu bilioni 8, upembuzi yakinifu umeshafanyika kilichobaki ni utekelezaji tu. Nilitaka kufahamu ni lini Serikali itatekeleza mradi huu mkubwa kwa wananchi wa Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imezingatia mradi huu wa maji wa Magehe kwa umuhimu wake na tunaona kabisa ni mradi mkubwa ambao utakwenda kugharimu Serikali shilingi bilioni 8. Nikutoe hofu Mheshimiwa Catherine namna ambavyo umeweza ukafatilia suala hili muda mrefu na umekuwa ukiliuliza mara kwa mara kwangu pamoja na kwa Mheshimiwa Waziri, tutatekeleza mradi huu kwa awamu katika mwaka wa fedha ujao.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, iliyokuwa benki ya FDME, sasa ni zaidi ya miaka minne tangu BOT waifunge. Wananchi wa Arusha na sehemu mbalimbali waliokuwa na akaunti katika benki hiyo hadi leo hawajui hatima ya pesa zao. Nini kauli ya Serikali?
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa swali zuri. Na mara zote amekuwa kinara wa kuwatetea wananchi wa Tanzania, hasa wa Arusha, nadhani ndio maana huwa wanamchagua mara kwa mara:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwepo na zoezi hilo la kuichukua iliyokuwa benki ya FDME na kilichochelewesha ni ule utaratibu ambao ni wa kawaida unapoikabiodhi kwa mufilisi kwa hatua zile. Kwamba, unatoa kile cha kwanza ambacho kiko kisheria kwa wale ambao walikuwa na akiba zisizozidi kiwango kilichowekwa kisheria, lakini kwa wale ambao viwango vyao vilikuwa zaidi ya kiwango kinachogawanywa kwa awamu ya kwanza huwa ni lazima zoezi la mufilisi likamilike kwanza.

Mheshimiwa Spika, na zoezi hilo linahusu uhakiki wa mali zote zilizopo zikusanywe, ziuzwe, halafu zikishauzwa zikageuzwa kuwa fedha ndio watu wale waweze kugawanywa, wale ambao akiba zao zilikuwa zinazidi kiwango cha kwanza ambacho kilikuwa kimegawanywa. Sasa kwa kuwa zoezi hilo kukamilika linachukua muda, kuhakiki mali uzipate zote, lakini pia uzibadilishe ziwe fedha linachukua muda, hicho ndicho ambacho kimechelewesha.

Mheshimiwa Spika, sasa ni lini itakamilika?

Mheshimiwa Spika, nakumbuka utaratibu huu ulikuwa bado unaendelea na ulikuwa hatuia nzuri. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge tutakapokuwa tumemaliza zoezi lako la hapa Bungeni nitapata taarifa ambapo imeshafikia hatua gani ili niweze kujua ni lini watakuwa wameshakamilisha kwasababu, zoezi lilikuwa linaendelea.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa swali hili linalohusiana na Kiwanda cha General Tyre limeulizwa kwa muda mrefu sana na sisi tumekuwa tukifuatilia muda mrefu sana tangu Mheshimiwa Gambo akiwa Mkuu wa Wilaya, amekuwa Mkuu wa Mkoa, hadi leo hii yupo ndani ya Bunge, lakini Serikali imekuwa ikitoa majibu yaleyale. Wananchi wa Arusha wanataka kufahamu ni lini Kiwanda cha General Tyre kitaanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA
NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Serikali dhamira tunaelewa na frustration iliyoko kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na umuhimu wa Kiwanda cha General Tyre. Hili jambo ni la wazi, ni dhamira ya Serikali kuona kwamba Kiwanda cha General Tyre kinafanya kazi. Ndiyo maana Serikali mara zote imekuwa ikitangaza nia ya kumtafuta mwekezaji yeyote mwenye uwezo wa kuwekeza na kuwapa fursa wananchi wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla waweze kuwekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni muhimu vilevile Waheshimiwa Wabunge wakaelewa, unapowekeza katika kiwanda kuna dhana ya comparative advantage. Hii ina maana kwamba tunapotengeneza tairi Tanzania, tairi hilohilo linazalishwa na nchi nyingine, tunapoenda sokoni litanunuliwa kwa bei gani? Kwa hiyo, suala la teknolojia ni muhimu sana. Nitumie nafasi hii kuwahamasisha Watanzania kwamba Serikali iko open kumruhusu Mtanzania yeyote mwenye uwezo ama mwekezaji kutoka nje kuja kuendesha kiwanda hiki. Mkoa wa Arusha unakaribishwa kama kuna uwezekano tunaweza kukutana nao kama Serikali tujadiliane ni namna gani tunaweza ku-revive Kiwanda cha General Tyre. Pia siyo lazima kizalishe matairi tu, kinaweza kuzalisha jambo lingine lolote ambalo litaweza kuleta manufaa katika nchi na uchumi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa barabara hii ya kutokea Wasso kwenda Mto wa Mbu ina kilometa 206, lakini kwa miaka minne barabara hii imejengwa kilometa 49 tu; na barabara hii imekuwa inaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi wa Ngorongoro. Hivi juzi tu kuna mama amefia njiani akiwahishwa hospitali kujifungua na tumeona Mheshimiwa Mama Samia akitangaza utalii na barabara hii inahusu utalii. Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara hii? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: Kwa kuwa mkandarasi huyu anadai shilingi bilioni 21 na walimwongezea muda, alikuwa amalize kujenga barabara hiyo Oktoba, 2019: Je, hamwoni kwamba mnaingiza Serikali katika hasara ya kulipa penalty? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Catherine kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kweli kwamba Mkandarasi anadai shilingi bilioni 21; na anapokuwa amewasilisha hati ya madai, lazima kuna kazi ya kuhakiki madai yao yanafanyika. Kazi hiyo imeshafanyika na Juni mwaka huu 2021, Mkandarasi huyo amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 12. Kwa hiyo, mchakato unaendelea, wakikamilisha uhakiki huko Wizara ya Fedha atalipwa fedha ili kazi iweze kuendelea. Mimi mwenyewe nimefika katika barabara hii na nilipata shida kweli barabarani, anachokisema ni kweli, ni barabara ngumu sana, tulipata pancha za kutosha, lakini Serikali imeweka nguvu barabara hii ikamilike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali lake la pili, barabara hii ni kweli ina urefu wa kilometa 206, inavyo vipande vinne. Kwa hiyo, tunaanza na hiki cha kwanza; kutoka Wasso kwenda Sale na twende mpaka Mto wa Mbu. Tuna- engage vyanzo mbalimbali kupata fedha ili barabara hii iweze kukamilika. Mheshimiwa Mbunge ambaye pia ni Naibu Waziri wa Serikali hii ya Awamu ya Sita tulikuwa pamoja na anajua tulifanya juhudi kubwa. Tukifanya mpango kumaliza barabara hii, itabadilisha uchumi wa wale watu wa Ngorongoro, itapeleka huduma za kijamii na pia itafungua milango ya watalii na pato la Taifa kwa ujumla wake litaongezeka katika eneo hili. Ahsante.