Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Catherine Valentine Magige (15 total)

MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itafungua rasmi Kiwanda cha kutengeneza Matairi cha General Tyre ambacho kilikuwa ni mkombozi mkubwa kwa uchumi wa Taifa na ajira kwa wananchi wa Arusha?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Kutengeneza Matairi cha General Tyre Arusha kilisimamisha shughuli zake mwaka 2009 kutokana na Serikali kukosa fedha kwa ajili ya kukiendesha. Wakati huohuo, aliyekuwa mbia mwenza (Kampuni ya Continental AG) hakuwa tayari kuendelea kuwekeza katika kiwanda hiki.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuona kiwanda hiki kinaanza kuzalisha matairi mapema iwezekanavyo. Hii inadhihirishwa wazi katika Mpango wa Serikali wa Miaka Mitano 2016/2017-2020/2021 na tumepanga kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 2016. Aidha, Serikali tayari imenunua hisa 26 zilizokuwa zinamilikiwa na mbia mwenza. Kiwanda hicho kwa sasa kinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Vile vile, Serikali imeamua kuweka dhamana ya kusimamia na kuendesha kiwanda hiki chini ya NDC na Tangazo la Serikali (GN) juu ya uamuzi huo litatolewa wakati wowote.
Mheshimiwa Spika, mradi wa Kiwanda cha Matairi, Arusha una maslahi mengi kwa Taifa kuanzia wakulima wa mpira, wafanyakazi kiwandani na maduka ya bidhaa hiyo, usalama wa vyombo vya usafiri vitumiavyo matairi, kodi kwa mamlaka mbalimbali na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza matairi nje ya nchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa mradi huo, Wizara imeiagiza NDC kuandaa andiko la kitaalam ambalo pamoja na kujibu masuala ya kiuchumi, kiufundi, kijamii, lazima lizingatie maoni ya wadau wa sekta.
Mheshimiwa Spika, mradi huo ambao ni kielelezi tunataka ujiendeshe kwa kuwa na menejimenti huru yenye watu wenye weledi katika shughuli na bila kutegemea ruzuku ya Serikali.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-
Je ni lini mradi mkubwa wa maji Wilayani Longido utaanza rasmi, ambao utakuwa ni mkombozi kwa wananchi wote wa Wilaya ya Longido.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi mkubwa wa Maji Wilayani Longido ambao chanzo chake ni Mto Simba uliopo ndani ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, ulifanyiwa usanifu wa kina na kazi hiyo ilikamilika mwezi Machi mwaka 2015. Mradi umekisiwa kugharimu sh. 13,998,791,270.40 na utaweza kuhudumia watu 21,666. Serikali imepanga kujenga mradi huu na kuukamilisha katika awamu ya pili ya Program ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 4.61 kwa ajili ya kuendelea kukamilisha miradi ya Vijiji 10 katika Halmashauri ya Longido. Pia imetenga kiasi cha shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Longido.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-
Mgogoro wa mipaka kati ya Hifadhi ya Serengeti na Vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro ni wa muda mrefu na sasa umekuwa sugu na kusababisha kero kwa wananchi wa maeneo hayo:-
Je, ni lini Serikali itaainisha mipaka ya maeneo hayo ili kumaliza mgogoro huu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa muda mrefu sasa kumekuwepo na migogoro ya mipaka baina ya Hifadhi ya Serengeti na baadhi ya vijiji katika Wilaya za Serengeti, Bunda, Ngorongoro, Tarime, Busega, Bariadi na Meatu.
Kwa upande wa Wilaya ya Ngorongoro, Vijiji vinavyohusika ni pamoja na Ololosokwani, Soitsambu, Maaroni, Arashi, Piyaya, Orelian na Magaidulu. Kwa kiasi kikubwa migogoro ya mipaka katika vijiji hivi imechangiwa na kutohakikiwa kwa mipaka ya hifadhi baada ya Tangazo la Serikali Na. 235 la tarehe 21 Juni, 1968, zoezi ambalo lingefuatiwa na uwekaji wa alama za kudumu chini ya usimamizi wa kitaalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya mipaka katika Vijiji vya Wilaya za Serengeti, Bunda, Tarime, Busega, Bariadi na Meatu ilipatiwa ufumbuzi baada ya zoezi shirikishi miongoni mwa wadau wa pande za migogoro na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pamoja na jitihada zote zilizofanyika ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi na viongozi wa vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro ambavyo eneo lake kwa ujumla lina umuhimu mkubwa na wa kipekee kiikolojia, wananchi hawa walikataa kutoa ushirikiano na hivyo kukwamisha zoezi hilo. Wizara yangu imeorodhesha mgogoro huu wa mpaka baina ya Hifadhi ya Serengeti na Vijiji vya Wilaya ya Ngorongoro vilivyotajwa hapo juu kwenye orodha ya migogoro yote ya ardhi hususani inayohusu mipaka ya Hifadhi za Taifa na misitu inayopangwa kushughulikiwa kimkakati zaidi zaidi na Serikali hivi karibuni.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE Aliuliza:-
Waliokuwa wafanyakazi wa Hoteli ya Seventy Seven ya Arusha hawajalipwa mafao yao hadi sasa:-
Je ni lini watalipwa mafao yao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, waliokuwa wafanyakazi wa Hoteli ya Seventy Seven - Arusha wapato 238 waliachishwa kazi mwaka 2000 na kulipwa mafao yao kwa mujibu wa taratibu na sheria. Katika zoezi la ulipaji wa mafao ya wafanyakazi hao, Serikali kupitia iliyokuwa PSRC ilitoa na kulipa kiasi cha shilingi 217,366,296 mwezi Januari, 2000 kama mafao ya wafanyakazi hao. Baada ya malipo hayo watumishi hao waliwasilisha malalamiko kuwa wamepunjwa. PSRC ilihakiki madai hayo na baada ya kujiridhisha mwezi Agosti, 2000 Serikali ilitoa idhini ya kulipa tena kiasi cha shilingili 273,816,703 kugharamia mapunjo ya mishahara na mafao ya wafanyakazi hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, wafanyakazi hao tayari walishalipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria na taratibu na hawastahili kudai malipo yoyote ya nyongeza.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo uliodumu zaidi ya miaka 25?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALI: alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwezi Desemba, 2016 Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Wilaya ya Ngorongoro pamoja na mambo mengine, alitoa maelekezo ya jinsi ya kupata ufumbuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu Loliondo ambao unahusisha wananchi, wawekezaji na wahifadhi. Katika utekelezaji wa agizo hilo, Kamati Maalum Shirikishi inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha iliundwa ili kupata mapendekezo ya namna ya kutatua mgogoro huo. Kamati hiyo maalum ilifanya kazi yake kwa njia mbalimbali zikiwemo kufanya vikao na wadau mbalimbali, kutembelea eneo lenye mgogoro ili kujua hali halisi na kuandaa taarifa yenye mapendekezo ya jinsi ya kutatua mgogoro husika. Mapendekezo ya Kamati hiyo yamewasilishwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hatua zaidi.
MHE. DKT. STEPHEN L. KIRUSWA (K.n.y. MHE. CATHERINE MAGIGE) aliuliza:-
Serikali ilishatoa ahadi ya kujenga barabara ya Mto wa Mbu hadi Loliondo kwa kiwango cha lami.
Je, mchakato wa mradi huo umefikia hatua gani na ujenzi wake utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J.KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Stephen kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na ninamtakia kila la heri katika kuwatumikia wananchi wa Longido. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa ujenzi wa barabara ya Mto wa Mbu – Longido kwa kiwango cha lami na imeshaanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Mkataba wa awamu ya kwanza ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii unaohusisha kilometa 49 kutoka Loliondo (Waso) hadi Njiapanda ya Sale tayari umesainiwa na utekelezaji ulianza tarehe 18, Oktoba, 2017. Ujenzi wa sehemu hii ya barabara unaotekelezwa na mhandisi aitwaye Ms China Wu Yi Co. Ltd. kwa gharama ya shilingi 87,126,445,712.35 unasimamiwa na TECU (TANROADS Engineering Consulting Unit). Mradi huu unaogharamiwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 unatarajiwa kukamilika baada ya miezi 24.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa Wizara yangu itaendelea kutekeleza ahadi ya Serikali na miradi iliyowekwa katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MARTHA M. MLATA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati ipi kisheria kushughulikia suala la ulinzi wa maeneo ya vyanzo vya maji ili kunusuru maeneo hayo dhidi ya uvamizi na matumizi mengine yasiyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na. 20 ya mwaka 2004 katika Ibara ya 7 imeweka misingi ya kisheria ya ulinzi na usimamizi wa mazingira ikiwemo mazingira ya vyanzo vya maji.
Aidha, kifungu cha 57(1) kinaweka katazo la kufanya shughuli za binadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji na kifungu cha 60(3) kinaelekeza Bodi za Maji ya Bonde kuhakikisha kunakuwa na maji ya kutosha kwa mazingira.
Aidha, Sheria ya Usimamizi wa Rasilimali za Maji Na. 11 ya Mwaka 2009 inaelekeza umuhimu wa kutunza na kulinda vyanzo vya maji na rasilimali za maji. Vilevile Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020 Ibara ya 152(d) nayo inasisitiza kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji kwa kuendelea kufanya tathmini ya vyanzo vya maji vilivyohifadhiwa, kubaini vyanzo vipya na kufufua vilivyopotea ama kuharibika ili kuwa na uhakika wa kuwa na maji safi na salama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa kuzingatia sheria hizi na maelekezo haya, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkakati wa kuhifadhi mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji kwa mwaka 2006 na mkakati wa hatua za haraka za kuhifadhi mazingira ya bahari ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa wa mwaka 2008.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mikakati hii, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhamasisha jamii zinazozunguka vyanzo vya maji; Serikali za Mitaa na Vijiji kushiriki kikamilifu katika jitihada za kuhifadhi vyanzo vya maji; kutoa elimu juu ya umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji; kuvitambua vyanzo vya maji na kuviweka mipaka; kuondoa watu waliovamia vyanzo vya maji; kupiga marufuku au kusitisha shughuli zisizo endelevu katika maeneo ya vyanzo vya maji; kuondoa miti isiyo rafiki kwa mazingira; kuondoa mifugo katika maeneo ya vyanzo na kuandaa mipango ya matumizi endelevu ya ardhi katika maeneo ya mabonde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Tanzania ni mwanachama wa Makataba wa Kimataifa wa Ardhi Oevu (Ramsar Convention) kwa mwaka 1971 na Mkataba wa Kimataifa wa Baioanuai wa mwaka 1992 ambayo moja ya lengo lake ni kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa ili kuwa na maji ya kutosha kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha shughuli za hifadhi ya mazingira hususan kutunza vyanzo vya maji kwa kuendelea kutoa miongozo ya utekelezaji wa sheria na mikakati inayohusiana na kutunza vyanzo vya maji. Aidha, Sekta Binafsi na Mashirika yasiyo ya Kiserikali wataendelea kuhamasishwa kutekeleza mikakati inayolenga kuhifadhi mazingira ya vyanzo vya maji kwa vizazi vya sasa na vya baadaye. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi 55 wa Kata za Oldonyosambu na Mateves Wilayani Arumeru Mkoani Arusha waliopisha ongezeko la barabara ya Arusha- Namanga toka mwaka 2013.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tathmini ya mali za wananchi 55 wa Kata ya Oldonyosambu walioathiriwa na ujenzi wa barabara ya Arusha - Namanga ilifanyika mwaka 2013 na kiasi cha shilingi milioni 281.501 kilihitajajika kwa ajili ya kuwalipa fidia. Uhakiki wa tathmini hiyo ulifanyika na umekamilika, tayari Serikali imeshatoa Shilingi milioni 66.821 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya kulipa sehemu ya fidia hiyo.
Mheshimiwa Spika, malipo ya fidia yatafanyika kwa pamoja kwa wananchi wote mara baada ya Wizara yangu kupokea fedha zote zinazohitajika kwa ajili ya kulipa fidia hiyo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa wananchi wote wanne (4) kwa Kata ya Mateves wameshalipwa fidia yenye jumla ya shilingi bilioni 2.225, hivyo hakuna mwananchi wa Kata ya Mateves anayeidai Serikali fidia.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa wafanyakazi 545 wa KILTEX – Arusha ambao bado wanadai pensheni toka kiwanda hicho kilipofungwa baada ya Mwajiri wao kutowasilisha michango yao kwenye Mfuko wa Kijamii wa PPF?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Nguo cha KILTEX, kilisimamisha shughuli za uzalishaji mwaka 1994 na kuwekwa chini ya ufilisi na PSRC mwaka 1995, kutokana na tatizo la ukosefu wa mtaji na malimbikizo ya madeni. Kwa mujibu wa ripoti ya Mfilisi, kiwanda kilishindwa kutekeleza takwa la kisheria la kuwasilisha mchango wa mwajiri na waajiriwa kwenye Mfuko wa Pensheni wa PPF kati ya mwaka 1986 na 1994 na hivyo kusababisha PPF kushindwa kuandaa malipo ya mafao ya wafanyakazi kulingana na matakwa ya kisheria mara baada ya kiwanda kufungwa na kufilisiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kumbukumbu na nyaraka za ufilisi zilizopo, taratibu za ufilisi zilikamilika na wafanyakazi wa KILTEX walilipwa stahili zao. Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi walilipwa mafao ya kiinua mgongo kwa mkupuo na wengine walirejeshewa michango yao kwa kadri walivyochangia. Utaratibu huu wa malipo ulifanyika baada ya Mfilisi kushindwa kulipa riba, adhabu na malimbikizo ya michango kwenye Mfuko wa Pensheni wa PPF. Uamuzi huo ulifikia kutokana na ukweli kwamba mauzo ya mali za kiwanda yalikuwa kidogo ikilinganishwa na jumla ya madai na gharama halisi za ufilisi.

Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba watumishi wa Kiwanda cha KILTEX walilipwa stahili zao kwa mujibu wa Sheria ya Makampuni Na. 46 ya mwaka 1931 ambayo ilitumika kufilisi kiwanda mwaka 1995. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Mfilisi alitakiwa kuuza mali za kiwanda na kutumia fedha za mauzo kulipa madai mbalimbali ikiwa ni pamoja na stahili za watumishi ndani ya muda maalum kulingana na tangazo la ufilisi. Kufuatia tangazo la Mfilisi kwenye vyombo vya habari, wadai waliwasilisha madai yao na Mfilisi alilipa madeni hayo kulingana na fedha mauzo zilizopatikana.
MHE. ANNA R. LUPEMBE (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kulinda biashara za wazalishaji wa ndani ili kuwajengea uwezo kuelekea uchumi wa viwanda?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha biashara za wazalishaji wa ndani zinalindwa, Serikali imeendelea kutoa msamaha wa kodi kwa baadhi ya bidhaa zinazozalishwa ndani na kutoza kodi zaidi kwenye bidhaa zinazoingia nchini katika kiwango cha asilimia 10 kwa bidhaa ghafi na asilimia 25 kwa bidhaa zilizo tayari kutumiwa na mlaji. Aidha, viwango hivi vinaweza kutozwa zaidi ya asilimia 25 kulingana na umuhimu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali iliongeza kodi kati ya asilimia 25 hadi 35 kwenye mafuta ya kula yanayoingizwa nchini. Aidha, ili kulinda wazalishaji wanaotumia malighafi za ndani Serikali imeongeza kodi kwa bidhaa zinazotoka nje kwa mfano, mvinyo wa zabibu ulioingizwa toka nje ya nchi kutoka shilingi 2,349/= hadi shilingi 2,466/= kwa lita wakati unaozalishwa ndani ukitozwa shilingi 200/= tu kwa lita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeweka udhibiti na usimamizi maalum kwa kutoa vibali na leseni kwa baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini kama vile sukari, maziwa ya mtindi, mitumba na magunia au viroba vya kufungashia bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha vituo vya pamoja mipakani katika maeneo ya kuingiza bidhaa nchini. Aidha, udhibiti na ukaguzi umeimarishwa katika viwanja vya ndege na bandari ili kudhibiti bidhaa za magendo, hafifu, bandia kuingizwa nchini. Vilevile kupitia taasisi zake za mamlaka ya udhibiti, Serikali imeendelea kusimamia ubora wa bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani pamoja na zinazotoka nje ya nchi kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara. Lengo ni kuhakikisha kwamba, bidhaa zinazoingia sokoni zinakidhi matakwa ya viwango husika ili kulinda afya, usalama, mazingira na kulinda biashara na viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mikakati ya kisera, kisheria na kiutendaji niliyoeleza, Serikali imeendelea kuwawekea mazingira wezeshi wafanyabiashara wa ndani ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika soko, kuandaa na kutekeleza mpango wa kuboresha mfumo wa kudhibiti biashara nchini (blue print), kuanzisha vituo vya ushauri wa biashara ili kutatua changamoto zinazowakabili (Business Clinics) na Vituo vya Ushauri wa Kikodi, (Tax Clinic) ambavyo vinatoa elimu kuhusu namna bora ya kuanzisha kufanya biashara na aina ya kodi zinazohusiana na kila aina ya biashara nchini.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kulinda biashara za wazalishaji wa ndani ili kuwajengea uwezo kuelekea uchumi wa Viwanda?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimwia Naibu Spika, katika kuhakikisha biashara za wazalishaji wa ndani zinalindwa, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya Kisera, Kisheria na Kiutendaji. Mikakati hiyo ni pamoja na kuwawekea mazingira wezeshi wafanyabiashara wa ndani ili waweze kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika soko; kuandaa na kutekeleza Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara Nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kutoza kodi kwenye bidhaa zinazoingia nchini katika kiwango cha asilimia 10 kwa bidhaa ghafi na asilimia 25 kwa bidhaa zilizo tayari kutumiwa na mlaji. Aidha, viwango hivyo vinaweza kutozwa asilimia zaidi ya 25 kulingana na umuhimu wa bidhaa ili kulinda viwanda vya ndani. Kwa mfano, katika mwaka 2018/2019, Serikali iliongeza kodi kwenye mafuta ya kupikia yanayoingizwa nchini na kuweka vibali na leseni za udhibiti na usimamizi kwa baadhi ya bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kama vile vibali vya kuagiza sukari, mtindi, mitumba na magunia au viroba vinavyotumika kufungashia bidhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa marumaru, utafiti uliofanywa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania ulipendekeza Kiwango cha Ushuru wa Forodha kwa marumaru zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kiongezwe kutoka asilimia 25 na sasa hadi kufikia asilimia 35. Dhumuni kuu la kuongeza ushuru huo ni kuongeza tofauti ya bei ili kuvilinda viwanda vya ndani dhidi ya bidhaa zinazotoka nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuimarisha Vituo vya Pamoja Mipakani yaani One Stop Border Post katika maeneo ya kuingiza bidhaa nchini. Aidha, udhibiti na ukaguzi umeimarishwa katika Viwanja vya Ndege na Bandari ili kudhibiti bidhaa za magendo, bidhaa hafifu na bandia kuingizwa nchini.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa ulipwaji fidia kwa wananchi zaidi ya 2,000 wa Wilaya ya Longido na Monduli ambao maeneo yao yalipitiwa na Mradi wa Umeme Vijijini (REA)?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini inatekeleza mradi wa kupelea umeme katika vijiji vyote nchini ifikapo mwezi Juni, 2021. Lengo la mpango huu ni kuhakikisha kuwa Watanzania zaidi ya asilimia 85 wanatumia umeme ifikapo mwaka 2025. Ili kuhakikisha lengo hili linafikiwa, Serikali inagharamia miundombinu, ujenzi na gharama ya kufikisha huduma hii ya umeme kwa wananchi kwa asilimia 100 na wananchi kulipa shilingi 27,000 tu ikiwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya huduma hiyo. Hivyo, miradi ya umeme vijijini haina fidia.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kuwaomba wananchi wa Longido, Monduli na Watanzania wengine kutoa ushirikiano katika utekelezaji mradi huu ikiwa ni pamoja na kutodai fidia, nakushukuru.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA (K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE) aliuliza:-

Je, Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuongeza bajeti ya TARURA Wilayani Ngorongoro ili kukabiliana na uharibifu wa barabara uliotokana na mvua kubwa zilizonyesha msimu wa mwaka 2019 na 2020?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya barabara inayotokana na mvua kubwa zilizonyesha msimu wa mwaka 2019 na 2020, Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro katika mwaka wa fedha 2019/2020, ulifanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 94.4, vivuko 15 na daraja moja kwa gharama ya shilingi bilioni 1.08. Aidha, hadi kufikia Aprili, 2021, Serikali imeipatia TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro shilingi milioni 917.64 kati ya shilingi bilioni 1.05 zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2019/2020 sambamba na matengenezo ya kawaida, Serikali iliipatia TARURA Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro shilingi milioni 276.68 kwa ajili ya matengenezo ya dharura katika barabara zilizoharibiwa na mvua. Barabara zilizotengenezwa ni pamoja na kipande chenye urefu wa kilomita 1.2 na makalavati manne katika barabara ya Oldonyowas - Ormania mpaka Pipaya, ujenzi wa makalavati manne na madrifti matano katika barabara ya Mdito – Digodigo – Oldonyosambu na matengenezo ya kipande chenye urefu wa kilomita 1.5 na drifti moja katika barabara za Ormania mpaka Oldonyorock.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi bilioni 1.04 zimetengwa kwa ajili ya matengenenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 105, mifereji yenye urefu wa kilomita 1.1 na makalavati 30. Serikali itaendelea kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA K.n.y. MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kubadili Shule za Msingi za Tarafa ya Ngorongoro kuwa bweni ilikunusuru maisha ya wanafunzi ambao wamekuwa wakitembea umbali mrefu na kuhatarisha maisha yao kutokana na wanyamapori kwani eneo kubwa la Tarafa hiyo ni sehemu ya hifadhi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Shule za Msingi za Tarafa ya Ngorongoro kuwa za bweni. Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali wa elimu imeanzisha shule tatu za bweni ambazo ni Nainokanoka, Enduleni na Olbalbal zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,014 wakiwemo wavulana 590 na wasichana 424. Shule hizo zinachukua wanafunzi wanaotoka maeneo ambayo yana wanyama wakali na yaliyo mbali na maeneo ya shule na hivyo kuwawezesha wanafunzi kuhudhuria masomo bila vikwazo vyovyote.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza mabweni katika shule hizo ili kuziwezesha kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itamlipa Mkandarasi anayetengeneza kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Loliondo hadi Mto wa Mbu ili iweze kukamilika na kurahisisha maisha ya Wakazi wa Ngorongoro?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Valentine Magige, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa barabara ya Loliondo – Mto wa Mbu sehemu ya Wasso – Sale yenye kilometa 49 ulianza Oktoba, 2017 ambapo hadi kufikia Julai, 2021 utekelezaji wa kazi ulikuwa umefika asilimia 83. Serikali inaendelea kumlipa Mkandarasi wa mradi huu pamoja na Makandarasi wa miradi mingine ya maendeleo inayoendelea hapa nchini kulingana na hati za madai zinazowasilishwa na kuhakikiwa na Wizara ya Fedha na Mipango. Hadi kufikia Juni, 2021, Mkandarasi wa ujenzi wa barabara hii amelipwa jumla ya shilingi bilioni 38.07. Ahsante.