Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Bupe Nelson Mwakang'ata (17 total)

MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa tatizo hili limeikumba pia hospitali ya Namanyele - Nkasi Kusini na kwa bahati nzuri Serikali imejenga majengo ya wodi. Je, ni lini sasa Serikali itakabidhi na kufungua majengo haya?
Swali la pili, azma ya Serikali ni kuwa kila kata kuwa na kituo cha afya na kila kijiji kuwa na zahanati, je, ni lini vijiji hivi vinavyotegemea hospitali ya Kirando vitapatiwa zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipende kushukuru kama facilities zimekamilika, sasa bado kuweza kufunguliwa nadhani kikubwa zaidi tutawasiliana na uongozi wa mkoa kuangalia utaratibu tukishirikiana na wenzetu wa Wizara ya Afya, vifaa hivyo vikishakamilika basi hospitali hiyo iweze kufunguliwa. Hilo ni jambo ambalo tunasema kama Serikali tunalichukua kwa ajili ya kwenda kulifanyia kazi ili wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ajenda ya pili ni jinsi mchakato wa ujenzi wa vituo vya afya ya zahanati ni kweli sasa hivi tuna karibuni ya kata 3390, lakini vituo vya afya tulivyonavyo ni vituo 484 maana yake tuna gap kubwa sana ya kufanya. Ndiyo maana leo hii Waziri wa Afya ata-table bajeti yake hapa ikionyesha mikakati mipana kwa ajili ya kufikia maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijua wazi kwamba katika hao wenzetu wa eneo hili wanachagamoto kubwa sana na nikifanya rejea ya Mheshimiwa Keissy hapa alishasema mara nyingi sana. Hiki hasa kituo chako cha Kirando na yeye alikuwa akiomba ikiwezekana iwe Hospitali ya Wilaya kwa mtazamo wake. Lakini alikuwa akifanya hivi ni kwa sababu wenzetu wa kule wa pembezoni wakati mwingine wanapata wagonjwa wengine mpaka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Serikali naomba tuseme wazi kwamba tutashirikiana vya kutosha na mimi naomba nikiri kwamba katika maeneo yangu ya mchakato wa kuanza kutembelea nina mpango baada ya Bunge hili la Bajeti kutembelea katika mkoa huu ili kuangalia changamoto zinazowakabili ili kwa pamoja tuweze kuzitatua tukiwa katika ground pale tuone ni lipi linalowakabili wananchi wetu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa asilimia kumi iliyopo sasa hivi imepitwa na wakati, na wanawake na vijana wanakuwa kwenye makundi ya watu watano, watano, wanagawana hiyo asilimia 10 wanagawana shilingi laki moja, pesa ambayo haiwezi kukidhi matakwa ya mahitaji yao. Je, serikali ina mpango gani wa kuongeza asilimia kumi iliyoko sasa hivi? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa asilimia kumi iliyoko sasa hivi haitoki kwa wakati na wakati mwingine inasubiri matukio muhimu kama vile Mwenge. Je, ni lini Serikali itafanya sasa asilimia hii itoke kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Bupe, kwa sababu nimeona akiguswa sana na kinamama na vijana katika maeneo yake. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge hiyo ni credit kwako, kwa sababu naona unawatumikia wananchi wako wa Mkoa wa Rukwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awali asilimia kumi ni mgao katika mapato ya ndani, na asilimia kumi hii inatofautiana kutoka Halmashauri moja na kwenda Halmashauri nyingine. Kwa mfano, Halmashauri ambayo collection yake kwa mwezi ni shilingi milioni 200, unapozungumzia asilimia kumi maana yake unazungumzia shilingi milioni 20. Lakini tujue kwamba kiwamba kiwango hiki ni (own source) mapato ya ndani ya Halmashauri, na katika yale mapato ya ndani kuna mgawanyiko wa aina mbalimbali kutoka mapato ya ndani, kuna mingine kutoka miradi ya maendeleo, kuna vitu mbalimbali. Kwa hiyo, hii asilimia kumi kiundani ni asilimia yenye kutosha kabisa katika mchakato wa own source, kwa sababu ile pesa ya ndani bado kuna mahitaji mengine ya miradi ya maendeleo inatakiwa ifanyike katika Halmashauri.
Kwa hiyo, hii asilimia kumi siyo ndogo, isipokuwa lengo kubwa ni kila Halmashauri iweze kujipanga ikusanye mapato ya kutosha kutoka katika vyanzo vya ndani. Kuna Halmashauri zingine kwa mwezi wanakusanya shilingi milioni 500, asilimia kumi ni shilingi milioni 50; ni imani yangu kubwa kama kila Halmashauri imejipanga vizuri wanapofanya collection zao mfano hata shilingi milioni100, asilimia kumi yake ni shilingi milioni kumi, wakiamua kuzigawa zile vizuri, wakipanga mpango mkakati vizuri, zitawasaidia kina mama na vijana katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu kubwa lilikuwa pesa tulizozipanga katika own source ten percent ilikuwa haiendi kwa akina mama na vijana, na ndiyo maana katika Kikao cha Bunge kilichopita nilisema kwamba kipindi kilichopita own source peke yake ambazo hazikupelekwa kwa kina mama na vijana zaidi ya shilingi bilioni 39; maana yake ni kwamba Madiwani na sisi tulivyokuwa katika Kamati ya Fedha hatukutimiza wajibu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, tafadhali naomba ufupishe majibu, tafadhali! (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka angalau kidogo tuelezane hili, suala la asilimia kumi halitoki, nilikuwa nakuja asilimia kumi kutoka maana yake ni maamuzi ya wenyewe Wabunge na Madiwani, ndiyo tunakaa katika Kamati ya Fedha tunapanga kwamba asilimia kumi zitoke. Ina maana sisi tukishindwa kutimiza wajibu wetu, zitakuwa bado haziwafikii vijana, kwa sababu ten percent inafanywa katika Kamati ya Fedha ya Halmashauri husika.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja
na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali
la kwanza; kwa kuwa, wananchi wale walifanyiwa tathmini ya nyumba zao
muda mrefu na kwa kuwa, pesa inapanda thamani kila kukicha. Je, Serikali ipo
tayari kuwafanyia tathmini upya na kuwalipa kwa wakati?
Swali la pili; kwa kuwa, wananchi hawa wamepoteza imani na matumaini
ya kulipwa fidia zao kwa wakati na kwa kuwa, jitihada za Mbunge wa Jimbo
Mheshimiwa Aeshi Hilaly, amekuwa akifanya juhudi muda mrefu. Je, Mheshimiwa
Waizri yupo tayari kuongozana nami mpaka kwa wananchi ili akajionee
mwenyewe nyumba zinavyobomoka? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa
Naibu Spika, kama ambavyo nilieleza katika jibu la swali la msingi kwamba hivi
tunavyoongea suala la uhakiki wa mali za wananchi ambao wataathirika na
mradi huu lipo katika hatua za mwisho. Kwa maana hiyo, taarifa kamili ya nani
na nini watalipwa inatarajiwa kupatikana hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kwenda kujionea madhara ambayo
wananchi wale waliosimamishwa muda mrefu kuendeleza nyumba zao,
naomba sana uwasiliane na Mheshimiwa Aeshi ili Mheshimiwa Aeshi aniruhusu
niongozane naye. Kwa sababu, nina uhakika Mheshimiwa Bupe Mwakang‟ata
na Mheshimiwa Aeshi wanafanya kazi moja ya kuwatetea wana Sumbawanga,
nimhakikishie tu kwamba nitakuwa tayari kuongozana na yeye akiwa na
Mheshimiwa Aeshi.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Pamoja
na majibu mazuri ya Serikali, sote tunajua kazi za Wenyeviti, wamekuwa wanafanya kazi nzuri sana katika mitaa na vijiji vyetu, lakini hakuna hata siku moja wamelipwa posho.
Nataka Serikali iniambie leo ni lini itapanga kiwango cha kuwalipa Wenyeviti hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Wenyeviti hawa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira
magumu sana, wakati huo hawa ndio wasimamizi namba moja wa usalama katika vijiji na vitongoji vyetu, wanatatua migogoro kila siku, watoto wa mitaani wakipotea, wanapelekwa kwenye Wenyeviti, tukigombana usiku break ya kwanza kwa Wenyeviti, sote tunajua kazi za Wenyeviti.
Je, Serikali ipo tayari kuwapa hata usafiri angalau baiskeli za kuwasaidia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Bupe, Wenyeviti wetu wanafanya kazi kubwa sana katika vijiji, hili jambo halipingiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema lini? Naomba nizungumze wazi, kwa sababu tulikuwa na changamoto
kubwa hapa nyuma, hata ukija kuangalia Halmashauri zetu, hata kupeleka zile fedha, Halmashauri nyingine ilikuwa
inaonekana kama ni hisani. Ndiyo maana sasa hivi tunafanya haya marekebisho na muswada huu utaingia Bungeni wakati wowote. Hivi sasa umeshaiva na wadau wameshiriki vya kutosha. Katika Sura ya 290 kifungu cha 54 kinafanyiwa marekebisho na Waziri mwenye dhamana sasa atapewa utaratibu wa kuweka kama misingi ya kisheria, kuzielekeza Halmashauri sasa kupeleka zile fedha. Mwisho wa siku ni kwamba aidha, Halmshauri wataweza kupata hasa Wenyeviti wetu wa vijiji ambao tunatambua kwamba wanafanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la usafiri, ni kweli kama nilivyosema ni kwamba utakuta sehemu nyingine
Mwenyekiti wa Kijiji anatoka kitongoji kimoja anakwenda kitongoji kingine, changamoto yake ni kubwa. Vilevile kwa sababu kama tutaweka utaratibu mzuri wa kisheria na hata ukiangalia sheria, sehemu inayozungumza mambo ya expenditure pale, inazungumza kama kuna matumizi ya fedha nyingine zinazoweza kutumika kwa maslahi mapana ya kujenga eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utaratibu huo tukishafanikiwa vizuri, basi tutatoa maelekezo ya kutosha kuona jinsi gani tutafanya, tutaangalia na rasilimali fedha zilizopatikana angalau kama itawezekana baadhi ya vipando hasa baiskeli, lakini maelekezo hayo yatakuja baada ya kurekebisha sheria yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge jambo, lako ni la msingi na Serikali tunalifanyia kazi kama nilivyozungumza.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mojawapo ya shida inayowapata wanawake ni mitaji na Serikali imeweka pesa nyingi sana kwenye mabenki ili wakope, lakini wanapotaka kwenda kukopa kwenye mabenki wanaambiwa wapeleke hati, wanapokwenda kutafuta hati kwenye Ofisi za Ardhi wanahangaishwa sana; wanaambiwa wapeleke vitu vingi sana na wanaambiwa milolongo ya mambo mpaka wanaamua kuacha, zaidi ya mwaka mtu anafuatilia hati. Ni lini sasa Serikali itaweka gharama halisi za kupata hati?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Benki ya Wanawake ipo Dar es Salaam tu, ni lini sasa Serikali itaamua kufungua matawi mengine katika mikoa mingine ili wanawake wapate huduma hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna usumbufu katika kupata hati na hasa hizi Hakimiliki za kimila ambazo tunazizungumzia kwasababu shughuli yote inafanyika katika maeneo husika na katika vijiji husika. Kwa hiyo, mimi niseme pale ambapo Halmashauri yoyote inaonekana kwamba ni kikwazo katika kuwapatia wananchi hati za Hakimiliki za kimila tuwasiliane kwa sababu lengo la Serikali ni kuhakikisha kwamba mwananchi wa Kijijini tunamuwezesha kuweza kupata hati yake ya Hakimiliki ya kimila.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwasababu ndio sehemu pekee ambayo inaweza kumkomboa na mpaka sasa kama nilivyosema hati 400,761 zimeshatoka ni kwasababu tu ya ushirikiano wa karibu sana na wenyewe baada ya kuwa tumewaelimisha kwamba hati zile zinakwenda kuwakomboa katika shughuli za kimaendeleo. Kwa hiyo, pale wanapokwama naomba tuwasiliane ili tushughulikie.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; naomba kujibu swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata na ninaomba majibu yangu yaende kwa wanawake wote wa Tanzania kwamba Benki ya Wanawake ilianzishwa kwa malengo ya kuwahudumia, lakini kwa sasa ina changamoto kubwa za kimtaji na tutafungua matawi mikoani pindi ambapo uwezo wetu wa kimtaji wa Benki ya Wanawake utakavyoimarika. Ila kwa sasa tulichokifanya ni kuhakikisha tunafungua vituo vya kuwahudumia na kuwawezesha wanawake kwenye mikoa zaidi ya 18 nchini ili kuwapa elimu ya ujasiriamali lakini pia mikopo midogo midogo isiyo na dhamana ambapo wanawake wanadhaminiana wao kwa wao. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini maswali mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Sera ya Afya inasema itajenga zahanati kila kijiji na pia itajenga vituo vya afya kila kata na pia itajenga Hospitali za Wilaya kila wilaya. Je, ni lini sera hii itatekelezwa kikamilifu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa afya ni kipaumbele cha mwanadamu hasa kwa mama na mtoto, je, Serikali haioni umuhimu wa kuupa kipaumbele Mkoa wa Rukwa kwa kuwa hauna Hospitali ya Wilaya hata moja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli sera yetu inatueleza hivyo na ndiyo maana ukiangalia mchakato wa Serikali kwa kushirikiana na ninyi Waheshimiwa Wabunge, wananchi na wadau mbalimbali mnaona ni jinsi gani tunajitahidi kwa kadri iwezekanavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli naomba nitoe pongezi zangu za dhati, katika maeneo mbalimbali nilikopita nimekuta Wabunge wengi sana na wengine wakitumia Mfuko wa Jimbo na kuungana nguvu na wananchi katika suala zima la ujenzi wa zahanati na vituo vya afya. Nilishawahi kuzungumza hapa siku za nyuma kwamba katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga shilingi bilioni 251 lakini katika hizo shilingi bilioni 68 ni kwa ajili ya ku-top up shughuli hizo za ujenzi wa zahanati huko tunakokwenda kumalizia haya maboma.
Kwa hiyo, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba tunafanya kila liwezekanalo sera hii iweze kutekelezwa. Najua kila jambo lina time frame, katika miaka hii mitano mtaona mabadiliko makubwa sana katika sekta ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mahsusi katika Mkoa wa Rukwa, ni kweli kuna changamoto kubwa sana ndiyo maana Serikali tukaona katika Halmashauri zake kutokana na changamoto lazima tuboreshe kwanza vituo vya afya vilivyopo. Leo hii kwa kaka yangu Mheshimiwa Ally Keissy kule Nkasi amepigia kelele sana Kituo chake cha Kirando, tumefanya utaratibu tunaenda kujenga theatre na majengo mengine. Ukienda pale Sumbawanga DC halikadhalika kuna suala la ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mirepa lakini hilo tutafanya kwa kadri iwezekanavyo na ndiyo maana katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo hivi sasa tumepeleka karibia shilingi milioni 340 kwa ajili ya zoezi la ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Kwa hiyo, ni jukumu la Serikali kuhakikisha Mkoa wa Rukwa nao uweze kujengewa miundombinu ili wananchi wa kule waweze kupata huduma nzuri za afya.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini ya muda mrefu mpaka sasa hawajalipwa, nataka kujua, je, ni lini Serikali sasa itawalipa wananchi hawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wananchi hawa walifanyiwa tathmini muda mrefu ya nyumba zao na wameshindwa kuziendeleza na kufanya maendeleo. Je, Serikali iko tayari kuwaongezea tathmini ya fidia ili walipwe kiasi kikubwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia maendeleo mbalimbali kwa wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba hivi karibuni Mheshimiwa Waziri alitembelea eneo hili walizungumza na alipata pia taarifa kwamba muda siyo mrefu, wakati wowote wananchi watalipwa hizi fidia. Kwa hiyo, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira wakati wa hatua za kukamilisha ili tuweze kuwalipa wananchi wale na ujenzi uweze kuanza basi avute tu subira na wananchi wa Sumbawanga nawashukuru kwa uvumilivu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kulipa kwa ziada inategemea na sheria yenyewe na utaratibu wenyewe. Kwa hiyo, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge labda kama kuna suala la ulazima basi tuzungumze tuone kwamba je, wanastahili kulipwa ziada kutokana na kuchelewa au iko katika hali gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa wanawake wengi wamehamasika sana kuanzisha VICOBA na wengine wameanzisha vikundi mbalimbali kwa lengo la kujikwamua kimaisha lakini wamekuwa wakiangaishwa sana kwa kupata hiyo asilimia 10; sasa ni lini Serikali itaweka mazingira mazuri ili hata kama hiyo asilimia 10 ipo lakini wawekewe mazingira mazuri ya kupata mikopo kwenye mabenki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa asilimia 10 ya wanawake, walemavu na vijana inachelewa sana kuwafikia walengwa; sasa basi kwa nini Serikali isipunguze masharti ya kukopa kwenye mabenki ili wanawake waweze kukopa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kwamba ukilinganisha masharti yaliyopo katika upatikanaji wa hii asilimia tano ambayo imekusudiwa kwenda kwa wanawake na vijana masharti yake ni rahisi sana ukilinganisha na masharti ambayo yanatolewa na taasisi za fedha kama mabenki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachoomba kumekuwa na dhana potofu kama vile fedha hizi zinatolewa kama vile ni pesa ambayo haitakiwi kurejeshwa, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba tunasimamia ili pesa hizi zinazotolewa ziweze kurejeshwa na wengine waweze kukopeshwa, vizuri tukawa na mfumo ambao ni rasmi ili kuhakikisha kila shilingi ambayo inatolewa inarudi ili wakinamama wengine waweze kukopeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili angependa masharti ya benki yakapunguzwa ili wakina mama waweze kuna access ya kwenda kukopa kwenye taasisi hizi za fedha. Hili ambalo lipo ndani yuwezo wetu kama ofisi ya Rais TAMISEMI ni kuhusiana na asilimia tano kama ambavyo swali lake la msingi lipo ni vizuri kwanza tuhakikishe kwamba fedha hizi ambazo zinakusanywa asilimia tano inatengwa na zile zinazotengwa zinakopwa ikionekana kwamba kuna gap ya uhitaji hapo ndio twende kwenye taasisi zingine za fedha.

NAIBU WAZIRI VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sambasamba na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI ni kwamba katika mwezi huu wa tatu Mheshimiwa Rais alikaa na wadau mbalimbali wenye masuala ya kibiashara na viwanda katika moja ya jambo ambalo alizungumza ni kuwashauri watu wa mabenki kuweza kupunguza riba na kuweka masharti ambayo yatawasaidia zaidi wafanyabiashara. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa gharama za maisha zimepanda na asilimia 10 ni sawa na milioni moja, sasa je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 50? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Benki ya Wanawake iko Dar es Salaam tu, wanawake wa mikoa ya pembezoni wanaisikia tu hiyo benki. Je, ni lini Serikali sasa itafungua Tawi la Benki ya Wanawake Mkoa wa Rukwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swai lake la kwanza kuhusu kuongeza asilimia 10 hadi 50, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali yetu inatambua mchango wa wanawake katika kujenga uchumi wa Taifa letu. Hili ni pendekezo, tunalichukua kama Serikali. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kufuatia kuwatambua wanawake kwenye uchumi wa Taifa letu, ndiyo maana tulipopitisha bajeti ya TAMISEMI tuliondoa riba ambayo ilikuwa inachajiwa katika hii asilimia 10 ya mikopo waliyokuwa wanakopeshwa wanawake, hii ikiwa ni hatua ya kwanza kuhakikisha kuwa akina mama na vijana wanaendelea kupata mitaji inayopatikana na bila kurejesha kwa gharama nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, napenda kumwambia Mheshimiwa Bupe na Bunge lako tukufu kwamba Benki ya Wanawake Tanzania ilikumbwa na changamoto na sasa Serikali inaisimamia vizuri na tunatengeneza mfumo mzuri wa kuweza kufanya iweze kusimama. Moja ya mikakati ya kuiwezesha kusimama ni kupata mtaji wa kutosha, ndiyo maana kwa sasa kuna mapendekezo, wanafanya kazi kwa karibu na Benki yetu ya TPB na itakapoimarika ni nia ya Serikali kuona kwamba Benki ya Wanawake inaendelea kuwafikia wanawake kule walipo.
MHE. BUPE N. MWAKANG‟ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Kiongozi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Kwa kazi kubwa ya kuweza kumtua mama ndoo kichwani. Serikali hii imewaza kutuliza hata ndoa za wanawake wa Tanzania, wameweza kutulia kwa sababu maji yanapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizi sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza;

(i) Wilaya ya Nkasi ina takribani ya vijiji 35 wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Tanganyika, na wanatumia maji ya ziwa Tanganyika ambayo yanawasababishia kupata magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu na magonjwa ya kuhara. Sasa ni lini sasa Serikali itawajengea visima virefu ambavyo vitawasababisha wapate maji salama?

(ii) Wilaya ya Nkasi imegawanyika katika sehemu mbili, Nkasi Kusini na Nkasi Kaskazini. Naishuruku Serikali imeweza kujenga visima 9 ambavyo sasa hivi vinaendelea kujengwa, lakini bado Nkasi Kusini ambavyo havijajengwa visima takribani 7 ambavyo tuliomba kijiji cha Masolo, Kijiji cha Milindikwa, Malongwe, Sintali, Nkana na vijiji vingine bado havijachimbiwa visima.

Je, nili sasa Serikali itachimba visima hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amekuwa mpiganaji mkubwa hususani kwa kina mama wa Mkoa wake wa Rukwa. Lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge sisi kama Wizara ya Maji hatuta kuwa kikwazo kwa Mkoa wa Rukwa na Nkasi katika kuhakisisha wanapata maji. Ziara ya Mheshimiwa Waziri katika Jimbo la Nkasi kwa Mheshimiwa Kessy alilia sana pale Mheshimiwa Mbunge na tumetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa katika mji wa Kilando pamoja na Namanyele zaidi ya milioni tano kwa ajili ya miradi ile mikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepata fedha za PforF zaidi ya bilioni nne kwa Mkoa wa Rukwa, tumepeleka bilioni 1.3 katika Wilaya ya Nkasi katika kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji. Naomba Waheshimiwa Wabunge waende kusimamia miradi ile katika kuhakikisha wakinamama wanaendelea kutua na ndoo kichwani na ndoa zao zinaendelea kuimarika. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Shida iliyopo Mwanza ni sawa na shida iliyopo Mkoani Rukwa, Wilaya Sumbawanga Vijijini Kata ya Kaengesa katika vijiji vya Mkunda, Kaengesa B, Kaengesa A na Italima na vijiji vyote vya wilaya Sumbawanga vijiji.

Ni lini sasa Wizara itapeleka maji katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake, lakini kubwa ambacho ninachotaka kusema jukumu la wananchi kupata maji ni jukumu letu sisi Wizara ya Maji na nilishasema si mara moja si mara mbili, sisi ni Wizara maji si Wizara ya ukame tumepata fedha ambazo tumetengewa zaidi ya shilingi bilioni 301 na uwanzaishaji huu wa wakala wa maji vijiji kwa maana ya RUWASA tumejipanga miradi mingi katika kuhakikisha tunaitekeleza kutumia wataalamu wetu wandani, nimhakikishie Mheshimiwa Bupe sisi kama Wizara ya maji vijiji ambavyo ameainisha tunajipanga kuhakikisha tunavitatua ili wananchi wake waweze kupata huduma maji. Ahsante sana.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kuipongeza Serikali kwa kazi kubwa ambayo imeifanya katika Mkoa wa Rukwa kutujengea Hospitali za Wilaya. Wakati nauliza swali hili tulikuwa hatujajengewa hospitali hata moja lakini ndani ya kipindi kifupi hospitali na vituo vya afya zimejengwa. Kwa hiyo, naipongeza Wizara na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, hakika kazi ameifanya, Mwenyezi Mungu ambariki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo, sasa naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, ni lini sasa hospitali hizi zitaanza kufanya kazi na kuletewa vifaa tiba ikiwemo X-ray, MRI na vifaa tiba vingine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali sasa ina mpango gani wa kutuletea madaktari bingwa, manesi na wafanyakazi wa kada nyingine zote katika hospitali hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali tunazipokea pongezi ambazo zinatoka kwa Mbunge na naamini na Wabunge wote wanatoa pongezi hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anataka kujua ni lini sasa hospitali hizo ambazo zimejengwa zitafunguliwa ili zianze kutoa huduma kama zilivyokusudiwa. Naomba nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine, ni azma ya Serikali na ndiyo maana tulianza na majengo 7 yakamilike na yakishakamilika yaanze kutoa huduma wakati tunaongezea fedha zingine kwa sababu ili hospitali za wilaya zikamilike yanahitajika majengo yasiyopungua 22. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale ambapo majengo yakishakuwa tayari, vifaa vikipelekwa tutapeleka watumishi ili wananchi wapunguziwe adha ya kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kufata huduma za afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba wanakuwepo watumishi wa kutosha. Ndiyo maana tunaenda kuajiri hao 550, ni njia ya kuanza kupeleka wengine sio kwamba 550 ndiyo mwisho, hapana, tutaajiri na wengine kwa kadri bajeti itakavyoruhusu. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kutujengea hospitali za wilaya tatu katika Mkoa wa Rukwa, lakini katika hizo wilaya tatu bado wilaya moja ya Sumbawanga mjini haijapatiwa hospitali ya wilaya. Je, ni lini sasa itajengewa hospitali ya wilaya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni lini Serikali sasa itapeleka fedha za ukarabati hospitali hii ya mkoa ambayo inatumika kwa sasa?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Bupe Mwakangata kwa kazi nzuri ambayo anafanya katika kufuatilia upatikanaji wa huduma za afya katika Mkoa wa Rukwa hasa huduma ya afya ya mama na mtoto naamini wanawake wa Mkoa wa Rukwa wamemuona na wameiona kazi yake nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ni lini tutajenga hospitali ya wilaya katika wilaya moja ambayo haijapata hospitali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kama alivyoeleza tumeanza hospitali 67 mwaka huu katika bajeti ziko hospitali 28 kwa hiyo, tuombe tu uvumilivu kwa wananchi ambao hawajapata hospitali moja ya wilaya, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya vitendo ni Serikali ya kutekeleza kwa hiyo tutajenga hospitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini naomba nitoe angalizo kwa sababu pia tunataka kujenga hospitali mpya ya Mkoa wa Rukwa. Kwa hiyo, ningeomba subira tukimaliza ujenzi wa mikoa mitano mipya kutekeleza ilani hii ya uchaguzi 2015/2020. Kwa hiyo, ile hospitali ya mkoa sasa tutaikabidhi kwa hospitali ya manispaa ya Sumbawanga kama tulivyofanya kwa Shinyanga na Singida ndio tutafanya hivyo, tukimaliza hospitali mpya hizi zilizokuwa zinatumika za mikao zitakabidhiwa katika manispaa. Sasa ni lini tutapeleka fedha ya ukarabati tumepata fedha takribani shilingi bilioni 14 kutoka mfuko wa Dunia wa kupambana na UKIMWI, TB na Malaria kwa hiyo tutapeleka Mkoa wa Rukwa kwa ajili ya kuboresha huduma za magonjwa ya dharura na ajali pia kuboresha huduma za ICU wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum pamoja na huduma za mama na mtoto.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa naipongeza Serikali kwa kutenga kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya barabara hiyo, lakini barabara hiyo imechukua muda mrefu sana, zaidi ya miaka mitano haijatengenezwa kabisa na madaraja yote yamekatika kabisa. Wananchi wa Kata ya Isaba, Kazovu, Bumanda, Korongwe, Katete wanapata tabu sana wakati wanapotaka kwenda kupata huduma za afya katika Kata ya Kirando. Swali la kwanza; nataka kujua, ni sababu zipi zimesababisha kusimama kwa ujenzi wa barabara hii?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana nami mguu kwa mguu kwenda kuona tatizo lililopo katika wilaya hiyo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo mawili ya Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tunakiri kabisa kwamba sababu kubwa ya kuchelewa ama kutokukamilika kwa wakati kwa barabara hii kwa muda mrefu ni kutokana na kuwa na bajeti finyu. Hivyo tumeendelea kufanya matengenezo ya kawaida kwa kipindi hiki cha miaka hii ambayo Mheshimiwa Mbunge alikuwa anaieleza. Hata hivyo, tunaahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali bado itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya barabara hii kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu ya kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Mbunge ya kuwapigania wananchi wa maeneo ya Nkasi pamoja na Mkoa mzima wa Rukwa na najua kila siku amekuwa akitukumbushia katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwenye barabara hizi, nimuahidi kabisa mara baada ya Bunge hili nitaongozana naye tukawasikilize wananchi na kupatia ufumbuzi barabara hizo. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwanza kabisa naishukuru Serikali imeweza kuingiza kiasi cha shilingi bilioni 1.3 kwenye mradi huu. Mradi huu ulifanya kazi miezi mitatu tu na watu wakaihujumu ile miundombinu kwa kuiba vifaa kama solar, betri na pampu. Sasa swali langu linakuja, ni lini sasa Serikali itarudisha vifaa hivi ili wananchi waweze kuendelea kupata maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wezi wapo wanajulikana kabisa kwenye Kata ile, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwachukulia hatua kazi za kinidhamu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake namba moja lini vifaa vile vitarudishiwa pale kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi na kadiri ambavyo tumekuwa tukiongea naye kuhusu suala hili na nimpongeze kwa namna ambavyo amekuwa mfuatiliaji mzuri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili hatutazingatia zaidi kwenye vile vifaa vya solar, tutazingatia kuleta umeme kwa kupitia REA ili tuwe na umeme wa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na wale wezi kuchukuliwa hatua, kwanza niombe ushirikiano Zaidi, tuendelee kuwasiliana, hawa wezi Mbunge akiwa kama mwakilishi wa akinamama wa eneo lile, aende akaripoti polisi, lakini tumekuwa tukimsikia mara nyingi Mheshimiwa Waziri wetu kwamba mwisho wa kuchezea miradi ya maji ni sasa. Kama una mambo ya kutaka kuchezea, kachezee kitambi chako. Kwa hiyo, tutaendelea kuhakikisha kwamba miradi ya maji mwisho kuchezewa. (Makofi)
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyogeza. Kwanza kabisa nipende kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa kutujengea hilo daraja liligharimu zaidi ya karibu bilioni 17. Tunashukuru sana. lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; Serikali sasa ina mpango gani wa kutujengea hata basi kuitengeneza hiyo barabara hata kwa kiwango cha changarawe ili wananchi waweze kupita katika barabara hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili ninaomba sasa commitment ya Serikali, kwa sababu barabara hiyo ni muhimu sana kwa uchumi wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Songwe. Ni lini sasa Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Bupe Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Rukwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ni kweli kwa mwaka jana na mwaka huu ilikuwa imeharibika sana. Nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hivi ninavyoongea madaraja yote yameshajengwa, bado madaraja mawili ambayo mkandarasi anakamilisha. Kwa sasa barabara hii inapitika vizuri kwa kiwango cha changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kwamba ni lini tutaanza ujenzi; kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi. Barabara hii tunatambua umuhimu wake ndiyo maana tayari tumeshakamilisha usanifu wa kina kwenye kilomita zote, na bado kilomita 27 ambazo wako tayari wanafanyia usanifu ili barabara yote ikamilike kwa usanifu na baada ya hapo ndipo ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwa niaba ya Wizara nimshukuru kwamba ameipongeza Serikali kwa kujenga Daraja la Mto Momba ambalo lilikuwa ni kikwazo kikubwa. Hiyo ndiyo adhma ya Serikali; na sasa mizigo yote kutoka Rukwa inapita daraja la Momba kwenye Mlowo. Ahsante.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, ahsante nashukuru sana, kwanza naipongeza Serikali kwa kazi inayoondelea, lakini pia nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maporomoko haya ya Kalambo Falls ni kivutio kikubwa sana kwa Mkoa wa Rukwa, sasa Serikali ina mpango gani wa kujenga lami kwa sababu wawekezaji na watalii wanapenda sana vitu vizuri kama lami, vitu vizuri kama umeme. Sasa Serikali ina mpango gani wa kutengeneza miundombinu kwenye maporomoko hayo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Bupe Nelson Mwakang’ata Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Rukwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba hili alilolileta Mheshimiwa Mbunge ni ombi kwa sababu ya umuhimu mkubwa wa maeneo haya ya maporomoko ya Kalambo Falls. Kwa hiyo na sisi tuseme tu kwamba tumelipokea tutafanya tathimini na tutaangalia mfuko wetu jinsi ulivyo kama fedha itapatikana basi tutailekeza Ofisi ya Rais kupitia TARURA Kalambo waweze kwenda kujenga huko. Lakini kwa sasa tutakwenda kufanya tathimini halafu tuone jinsi tutakavyopata fedha kwa ajili ya ujenzi wa lami katika eneo hilo. Ahsante sana.