Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Boniphace Mwita Getere (30 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita na kupata fursa ya kujiunga na vyuo mara tu wamalizapo masomo yao, huruhusiwa kutumia National Examination Results Slip kwa ajili ya taratibu za kujiunga na chuo.
Je, kwa nini wanafunzi wanaomaliza stashahada katika vyuo mbalimbali na kutaka kujiunga na elimu ya juu wasiruhusiwe kutumia academic transcripts badala ya kutakiwa kuwasilisha vyeti halisi ambavyo huchukua muda mrefu kutolewa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kiujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua kuwa vyeti vya kuhitimu stashahada huchelewa kutolewa, wanafunzi wanaomaliza stashahada katika vyuo mbalimbali na kutaka kujiunga na elimu ya juu wanaruhusiwa kutumia hati ya matokeo yaani academic transcripts ili kupata usajili wa muda yaani provisional registration mpaka hapo wanapopata vyeti vyao ili kupatiwa usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa udahili wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu hufanyika kupitia mfumo wa udahili wa pamoja yaani central admission system.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu unaratibiwa kwa pamoja kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu na hutumia matokeo ya mitihani ya ngazi ya stashahada yaliyohifadhiwa kwenye Hazina data ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi. Hivyo, waombaji udahili hawatumii vyeti kuomba udahili kwa kuwa baadhi ya taasisi zinazotoa mafunzo ya Stashahada huchukua muda mrefu kutoa vyeti hivyo katika jitihada za kudhibiti udanganyifu wa vyeti.
Kwa hiyo, wanafunzi hawa wanapo-report vyuoni hupewa usajili wa muda na baada ya kupata cheti ndipo huwasilisha taarifa hizo na kupata usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wanafunzi wanaopata tatizo la kutumia hati ya matokeo kusajiliwa vyuoni watoe taarifa ili Wizara yangu iweze kufanyia kazi ipasavyo suala hili.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Zao kuu la biashara katika Wilaya ya Bunda ni pamba lakini viwanda vya kusindika pamba vya Ushashi Ginnery na Kibara Ginnery vilivyokuwa vinamilikiwa na MCU (1984) havifanyi kazi tangu mwaka 1990:-
(a) Je, ni lini Serikali itafufua viwanda hivyo ili wakulima wa pamba wapate bei nzuri?
(b) Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika pamba ili kuongeza thamani ya zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphance Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba viwanda vya kuchambua pamba vya Ushashi na Kibara havifanyi kazi tangu mwaka 1990. Viwanda hivi kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge vinamilikiwa na kilichokuwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Musoma (MCU) ambacho kwa sasa kipo kwenye utaratibu wa mufilisi ulianza mwaka 1997. Utaratibu wa mufilisi umechukua muda mrefu kutokana na baadhi ya wanachama wa MCU kukata rufaa kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tatu kutaka viwanda hivi visifilisiwe na badala yake ikiwezekana viendeshwe kwa ubia kati ya sekta binafsi, wanaushirika na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya ushirika imeanza kushughulikia suala la mali za MCU ikiwemo viwanda hivyo ili vitafutiwe utaratibu wa kufufuliwa kwa ubia na vianze kazi ili kuwezesha ulipaji wa madeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bunda ina ginnery tatu zinazofanya kazi ya kuchambua pamba inayopatikana katika wilaya hiyo. Hivyo wakulima wa Bunda wanapata huduma za uchambuzi wa pamba kupitia ginneries hizo. Aidha, taarifa zilizopo zinaonesha kuwa ginneries zilizopo katika Wilaya ya Bunda bado hazipati pamba ya kutosha na hivyo kufanya kazi chini uwezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inahamasisha sekta binafsi na wadau wengine kuwekeza katika viwanda vidogo vidogo vya kusindika pamba ili kuongeza thamani ya zao la pamba na wakulima wapate faida zaidi. Nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wakulima wanajengewa uwezo wa kumiliki vinu vidogo vidogo vya kuchambulia pamba katika vikundi vya wakulima na Vyama vya Ushirika. Kwa kuwa tayari Serikali inasambaza umeme vijijini kwa nguvu kubwa kinachofuata sasa ni kujenga mazingira ya kuwawezesha wakulima kumiliki viwanda vya kusindika mazao yao ikiwepo pamba. Hii ndiyo nia na namna ya bora ya kuleta mapinduzi ya viwanda nchini katika Sekta ya Kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia inawashauri wamiliki wa vinu vikubwa vya kuchambua pamba wafikirie kuwekeza kwenye hatua zinazofuata za mnyonyoro wa thamani kama kusokota nyuzi katika maana ya spinning, kufuma vitambaa, weaving na kutengeneza nguo (textile).
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Malambo ya Kijiji cha Mikomahiro, Salamakati, Salama „A‟, Sanzati, Mgeta, Kihumu/Hunyari na Nyang‟aranga yamekuwa hayatumiki ipasavyo kutokana na magugu maji na hivyo kujaa matope:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha malambo haya ili yatoe huduma nzuri kwa watumiaji?
(b) Malambo haya yalichimbwa miaka ya nyuma na watumiaji kwa sasa wameongezeka; je, Serikali ina mpango wa kuyapanua malambo hayo ili kukidhi mahitaji ya watumiaji kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa malambo umewekwa katika Mpango wa Miaka Mitatu wa Halmashauri kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo tathmini iliyofanyika imebaini kuwa zinahitajika shilingi milioni 90 kwa kazi ya kuondoa magugu maji na matope. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kipaumbele kimewekwa katika ujenzi wa masoko mawili na mnada wa Mgeta kwa gharama za shilingi milioni 60. Aidha, malambo mengine matano ya kunyweshea mifugo yatajengwa katika Vijiji vya Hunyari, Manchimweru, Kyandege, Salama Kati na Kaloleni ambayo yatagharimu shilingi milioni 200 hadi kukamilika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) ya jibu hili, mpango wa Serikali ni kukarabati malambo sita na kujenga mengine matano ili kukidhi mahitaji yaliyopo. Aidha, mabirika ya kunyweshea mifugo yatajengwa katika Vijiji vya Hunyari, Kihumbu, Igundu, Salama Kati, Kaloleni, Mekomariro II, Manchimweru, Kyandege Nyang‟aranga, ambapo tathmini ilionesha zinahitajika shilingi 110 kukamilisha kazi hiyo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Eneo la Buhemba Holding Ground Farm (KABIMITA) linalomilikiwa na vijiji vitatu vya Magunga, Milwa (Wilaya ya Butiama) na Mekomarino (Wilaya ya Bunda) kwa ajili ya kilimo na ufugaji ambalo lilitolewa na Serikali tangu miaka 1970 na 1980 kama kituo cha kukusanyia mifugo (ng‟ombe) na kuwatibu kabla ya kupelekwa kwenye mnada wa ng‟ombe Bukoba; na sasa ni miaka 33 eneo hili linatumiwa na wakazi wa vijiji hivyo kwa ajili ya makazi, kilimo na ufugaji.
Je, ni lini Serikali itatoa tamko rasmi kwamba eneo hilo ni mali ya vijiji hivyo kisheria ili kuondoa dhana ya kuwa eneo hili ni mali ya Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Buhemba Holding Ground chenye ukubwa wa hekta 2,446 kilijengwa mwaka 1949 na Serikali ya kikoloni kwa ajili ya kukagua, kukarantini na kunenepesha ng‟ombe, mbuzi na kondoo waliokuwa wanauzwa nchi za jirani. Baada ya uhuru kituo hiki kilikabidhiwa kwa Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya mifugo hadi mwaka 1975 kilipokabidhiwa kwa Kampuni ya Biashara ya Mifugo Tanzania (KABIMITA) ili kitumike kwa karantini na kunenepesha mifugo kwa ajili ya kuchinjwa katika viwanda vilivyokuwa vinamilikiwa na Tanganyika Packers Limited vya Arusha na Kawe, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 1980 hadi mwaka 1982, kampuni ya KABIMITA ilikitumia kituo husika kukarantini mitamba ya ng‟ombe wa asili kwa ajili ya maandalizi ya kuisafirisha kwenda Uganda kupitia sehemu ya kupakilia mifugo ya Kituo cha Bweri Holding Ground cha Musoma Mjini. Mwaka 1984 Kampuni ya KABIMITA ilifutwa na kituo hicho kilihamishiwa kwenye Wizara yenye dhamana ya maendeleo ya mifugo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 1993, Wizara kwa kutumia fedha za mkopo kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ilianzisha mradi wa uendelezaji wa miundombinu ya masoko ya mifugo ya Tanzania (Tanzania Livestock Marketing Project). Mradi huo uliendeleza kituo hicho kwa kuweka alama za kudumu kwenye mipaka, kujenga ofisi za nyumba na nyumba ya Meneja wa Kituo, kukarabati nyumba za watumishi na kununua vitendea kazi kwa gharama ya shilingi milioni 104.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya karantini na Holding Ground nchini yanalindwa kwa mujibu wa Sheria Namba 17 ya Kuzuia Magonjwa ya Mifugo ya mwaka 2003 na Sheria ya Nyama Na. 10 ya mwaka 2006. Maeneo haya ni kwa ajili ya matumizi ya mifugo ya biashara ambayo ni lazima iwekwe chini ya karantini ili kufanya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo kabla ya kuchinja kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeruhusu wananchi kutumia eneo hilo kwa shughuli mbalimbali huku ikiendelea kuwa chini ya umiliki wa Wizara. Hata hivyo, Serikali inatoa rai kwa wananchi kutopanda mazao ya kudumu na kujenga makazi katika eneo hilo pamoja na vituo vingine vya karantini na Holding Ground nchini.
Aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge muwaelimishe wananchi juu ya umuhimu wa maeneo haya katika ukuaji wa tasnia ya nyama nchini ili mifugo na bidhaa zitokanazo na mifugo ziweze kukubalika katika masoko yenye ushindani kikanda na Kimataifa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kunusuru Taifa na janga la mabadiliko ya tabianchi?
(b) Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba Ofisi za Majiji, Manispaa, Miji na Halmashauri zinakuwa na Idara ya Usafi na Mazingira inayojitegemea kuliko kuitegemea Taasisi ya NEMC ambayo inaonekana kuzidiwa na majukumu ya kudhibiti na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi?
(c) Je, Serikali ilipata ushauri gani kuiondoa Idara ya Mazingira kutoka kwenye Kamati ya awali ya Mazingira, Ardhi, Maliasili na Utalii na badala yake kupelekwa kwa Viwanda na Mazingira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012. Mkakati huo umeainisha vipaumbele vya kisekta na hatua za kuchukua ili kunusuru Taifa na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baadhi ya hatua hizo ni ambazo Wizara za sekta zimekuwa zikitekeleza ni pamoja na kuhimiza kilimo kinachozingatia mabadiliko ya misimu ya mvua, ufugaji endelevu, kuhifadhi vyanzo vya maji na misitu, ujenzi wa mabwawa ya maji, upandaji miti, matumizi ya nishati mbadala, ujenzi wa miundombinu imara ya barabara, madaraja na mifereji ili kuhimili mafuriko na matumizi ya teknolojia rafiki wa mazingira viwandani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huu unazingatia Wizara zote za kisekta na Serikali za Mitaa kuhuisha suala la mabadiliko ya tabianchi katika mipango yao.
Aidha, Serikali imeendelea kutekeleza miradi ya kuhimili na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kama vile ujenzi wa kuta kwenye kingo za bahari, upandaji wa mikoko na kujenga uwezo wa wataalam kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI ilishatoa mwongozo wa uanzishwaji wa Idara ya Usafi na Mazingira katika Halmashauri zote nchini na Halmashauri nyingine zimeshaanzisha idara hiyo. Aidha, kutokana na changamoto za utekelezaji wa majukumu yake, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa mapendekezo ya kuboresha muundo huo.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la muundo wa Kamati za Kudumu za Bunge ni jukumu la Ofisi ya Spika wa Bunge na Wizara haihusiki katika uandaaji wa miundo ya Kamati.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Zao la pamba ndilo zao kuu katika Wilaya ya Bunda:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia zao mbadala wakulima wa zao la pamba, baada ya zao hili kuelekea kutokomea kutokana na matatizo ya bei ndogo isiyokidhi mahitaji ya uzalishaji wake?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza uzalishaji wa zao la pamba hasa ikizingatiwa kuwa Wilaya ya Bunda yenye majimbo matatu inategemea viwanda vya pamba katika mapato na ajira?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali bado inaona kuwa kuna tija katika zao la pamba kwa wakulima wa Bunda na maeneo mengine yanayolima pamba nchini kuliko mazao mengine kwa manufaa ya wakulima wenyewe na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, wakulima wanaweza kulima pamba
sambamba na mazao mengine kama vile mazao ya bustani ili kujiongezea kipato. Aidha, kuyumba kwa uzalishaji wa pamba hapa nchini kunasababishwa na changamoto nyingi ikiwemo mabadiliko ya mara kwa mara ya bei katika soko la dunia, kukosekana kwa mbegu bora, upatikanaji na matumizi sahihi ya viuatilifu na mbolea.
Mheshimiwa Spika, hali hii imefanya wakulima wengi wa pamba nchini kuzalisha wastani wa kilo 300 kwa ekari tofauti na kilo 800 zinazopaswa kuzalishwa kwa ekari. Ili mkulima aweze kuona faida ya kilimo cha pamba anayouza kulingana na bei inayopangwa na wadau wakiwemo wakulima, mkulima anatakiwa azalishe zaidi ya kilo 800 kwa ekari ya pamba nyuzi yenye ubora unaotakiwa na soko.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali imeandaa mpango maalum wa kuhakikisha kuwa kufikia msimu wa 2018/2019 wakulima wa pamba kote nchini wanatumia mbegu bora za pamba aina ya UKM08 zenye tija kubwa badala ya mbegu aina ya UK91 ambayo imepoteza ubora wake. Mbegu hiyo ya UKM08 inazalishwa katika maeneo ya Meatu, Nzega na Igunga ambayo hayana ugonjwa wa mnyauko. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia upatikanaji wa viuatilifu bora na matumizi sahihi ili kuhakikisha wakulima wanatumia na kupata pamba iliyo bora na kukidhi mahitaji ya soko.
Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine, Serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa Cotton To Clothing 2016 – 2020 wenye lengo la kuendeleza mnyororo wa thamani wa zao la pamba ambao utaondoa utegemezi wa bei ya soko la kimataifa kwa kuwekeza katika viwanda vitakavyonunua pamba ya wakulima na hivyo kupunguza uuzaji wa pamba ghafi nje ya nchi. Hatua hii inakwenda sambamba na malengo ya Kitaifa ya kuwa nchi ya viwanda.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Miradi ya maji ya Mugeta/Nyang’aranga na Nyamuswa ambayo inadhaminiwa na Benki ya Dunia imeshindwa kumalizika tangu mwaka 2013 hadi leo.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha miradi hii kwa ufanisi na kukabidhi kwa watumiaji?
(b) Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya ahadi ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Makala akiwa Bungeni ya ukaguzi wa miradi hii hususan mradi wa Mugeta ambao una bajeti mbili kwa mradi mmoja?
NAIBU WA WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji na Umwagiliaji inatekeleza miradi ya maji chini ya Programu ya Maendeleo ya Maji (WSDP) ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inatekeleza Miradi kwenye Vijiji 10 vikiwemo Vijiji vya Mugeta/Nyang’aranga na Nyamuswa. Jumla ya miradi mitano ya Karukekere, Mumagunga, Kung’ombe, Mugeta na Ligamba imekamilika. Miradi ya Nyamuswa, Nyamatoke, Kibara, Bulamba na Kinyambwiga ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mugeta umekamilika na hivi sasa wananchi wanapata huduma ya maji isipokuwa Kitongoji kimoja cha Manyangale ambacho kitapata maji kutoka chanzo kingine baada ya kufanyiwa usanifu mwezi Agosti, 2016. Ujenzi wa mradi wa maji katika Kijiji cha Nyang’aranga umekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa kuwa mradi huu ulikuwa unatumia bajeti mbili, tayari Mkoa wa Mara umechukua hatua kwa kuunda timu ya wataalam kukagua na kuchunguza jambo hilo. Pindi ripoti hiyo itakapotufikia, basi hatua stahiki zitachukuliwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kukarabati malambo ya Vijiji vya Makomariro 2, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Kihumbu, Kisangwa, Sanzete, Salama A, Salama Kati na Nyangaranga ambayo yamejaa magugu maji na mengine kina chake kimepungua?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilichimba malambo katika Vijiji vya Makomariro 2, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Kihumbu, Kisangwa, Sanzete, Salama A, Salama Kati na Nyangaranga kwa ajili ya kutatua matatizo ya ukosefu wa maji ya kunyweshea mifugo na kwa matumizi ya binadamu. Ni kweli malambo hayo kwa sasa yamejaa magugu maji na tope.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi wa vijiji husika kuyaweka malambo hayo katika mipango yao ya bajeti na kuiwasilisha Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ili yawekwe na kutengewa fedha kwenye mpango wa bajeti ya mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa malambo hayo, Halmashauri ya Bunda ilifanya tathmini ili kujua gharama halisi ya ukarabati unaohitajika kwa ajili ya kuweka kwenye bajeti ya mwaka 2018/2019. Ukarabati huo utagharimu jumla ya Sh.36,825,600 kwa mchanganuo ufuatao: Lambo la Kyandege litahitaji Sh.25,618,350, Mugeta Sh.97,870,400, Sanzete Sh.36,286,000, Salama A Sh.25,926,000, Salama Kati Sh.46,315,850, Makomariro Sh.25,926,000, na Kihumbu Sh.108,883,000. Ukarabati wa malambo haya umepangwa kufanywa katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili malambo yaliyochimbwa au kukarabatiwa yaweze kuwa endelevu, Serikali inatoa ushauri kwa vijiji husika kuunda Kamati za Uendelezaji wa Malambo ambazo zitahusika na utungaji wa Sheria ndogondogo za utunzaji wa malambo hayo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuza:-
Je, ni kwa nini mikakati ya dhati ya Serikali katika kunusuru na kuzuia uchafuzi wa mazingira ya Mto Rubana ambao unaingiza maji yake katika Ziwa Victoria na ni chanzo kikubwa cha maji katika Vijiji vya Tingirima, Kyandege, Mugeta, Mariwanda, Sarakwa, Kihumbu na Hunyari katika Jimbo la Bunda.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS – MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Rubana ulioko katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ni chanzo muhimu cha maji kwa wananchi wa vijiji vilivyoko maeneo unakopita mto na pia kwa shughuli za uhifadhi. Maji ya mto huu hutumiwa na wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kunyweshea mifugo, kilimo na uvuvi. Aidha, maji ya Mto Rubana hutumiwa na wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la akiba la Grumeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa Mto Rubana kama chanzo cha maji na shughuli za uhifadhi, Serikali imechukua hatu zifuatazo ili kunusuru na kuzuia uchafuzi na uharibifu wa mazingira katika mto huo:-
(i) Kuziagiza Halmashauri za Serengeti, Bunda na Bunda Mjini kuzingatia na kutekeleza kikamilifu Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji wa mwaka 2006 na Mkakati wa Hatua za Haraka za kuhifadhi Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa wa mwaka 2008 katika maeneo yao ili kuzuia uharibifu wa Mto Rubana.
(ii) Kuendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kwa viongozi wa Halmashauri za vijiji na wananchi wote wa Kata za Hunyari, na Mugeta kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002 inayozuia ukataji miti ovyo na Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009.
(iii) Kufanya doria za mara kwa mara na kukamata wanaokaidi na kukiuka sheria na kusababisha uharibifu wa mazingira ya mto kwa kukata miti ovyo na uchomaji wa mkaa.
(iv) Kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kunyweshea mifugo ili kuzuia wananchi kunyweshea mifugo kwenye mto.
Mheshimiwa Naibu Spika, natoa wito kwa wadau wote ikiwemo viongozi katika ngazi ya Halmashauri, Waheshimiwa Wabunge, viongozi wa Kata na Vijiji na wananchi wote katika maeneo hayo kushirikiana katika kutekeleza mikakati ya Serikali ili jitihada za kunusuru Mto Rubana na kuzuia uchafuzi zifanikiwe kikamilifu.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua au kumaliza kabisa tatizo la baadhi ya wakazi wanaoitwa Wahamiaji katika Vijiji vya Nyabuzume, Tiring’ati, Nyaburundi na Bigegu ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisumbuliwa na hoja hiyo bila kupewa ufumbuzi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama inavyofahamika nchi yetu, hususan maeneo ya mipakani, imekuwa na tatizo la wahamiaji ambao hufahamika kama walowezi walioingia na kuishi nchini kwa miaka mingi. Wahamiaj hawa waliingia nchini kwa sababu mbalimbali tangu wakati wa ukoloni, ikiwemo kufanya kazi katika mashamba na migodi ya wakoloni, vita vya kikabila na uhaba wa ardhi katika nchi zao na pia kuvutiwa na hali ya amani iliyopo katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura Namba 357, kama ilivyorejewa mwaka 2002 walowezi hawa hawatambuliwi kama raia wa Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa maeneo yenye tatizo hili. Hivyo, kwa kutambua changamoto za tatizo hili Serikali kupitia Idara ya Uhamiaji mwaka 2009 ilifanya sensa ya wahamiaji hao katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwa ni pamoja na vijiji tajwa ambapo, ilibaini kijiji cha Nyabuzume kuna walowezi 160, Tiring’ati 48, Nyaburundi 530 na Bigegu 72.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya sensa hiyo, Serikali imekuwa ikiwapatia wahamiaji hao vibali vya kuishi nchini baada ya kukidhi vigezo ili kuwatambua na kuhalalisha ukaazi wao.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha pamba yote iliyopo katika Jimbo la Bunda inanunuliwa kwa bei nzuri na kwa wakati muafaka?
(b) Katika Jimbo la Bunda kuna kilimo cha mkataba kwa kampuni moja na wakulima wana hofu kuwa huenda kampuni hiyo isifanye vizuri kwa wingi wa pamba iliyopo, je, Serikali inatoa kauli gani juu ya hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Bunda katika msimu huu imelima ekari 71,668 na inatarajia kuvuna pamba tani 21,000 za pamba mbegu. Kampuni mbili za Olam Tanzania Ltd. na S&C Ginning Company Ltd. ndizo zitakazonunua pamba katika Wilaya ya Bunda. Kutokana na uchunguzi uliofanywa na Bodi ya Pamba, kampuni hizi zina uwezo mkubwa wa kifedha na kwamba tayari zimekwishapata fedha kutoka vyombo vya fedha tayari kwa ajili ya kuanza kununua pamba baada ya msimu kuzinduliwa tarehe 1 Mei, 2018. Aidha, nichukue fursa hii kipekee kabisa kuwahakikishia wakulima wa pamba wa Wilaya ya Bunda na maeneo yote yanayolima pamba kwamba pamba yao yote itanunuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa kilimo wa 2017/2018 Wilaya ya Bunda na Wilaya nyingine 38 zimetekeleza kilimo cha mkataba baada ya kupewa idhini na Serikali ya kuingia mikataba na makampuni ya pamba. Katika Wilaya ya Bunda makampuni mawili ya Olam Tanzania Ltd. na S&C Ginning Company Ltd. ndiyo yaliyoingia mkataba na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Bunda Mji kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha mkataba. Makampuni hayo yamekopesha pembejeo wakulima ambapo fedha hizo inabidi zirejeshwe wakati wa kipindi cha mauzo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jumla ya wakulima 42,000 wamenufaika na mfumo huu wa kilimo katika Wilaya ya Bunda. Kwa kuwa makampuni haya yamewezesha wakulima kulima kwa tija na kwa ubora unaotakiwa na soko ni muhimu, mkataba katika maeneo haya lazima uheshimiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejiridhisha na uwezo wa makampuni haya na kwamba pamba yote katika Wilaya ya Bunda itanunuliwa kwa wakati na bei ya kuanzia itakuwa bei elekezi ya shilingi 1,100 kwa kilo na bei inaweza kupanda kulingana na hali ya soko.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Kampuni ya Olam Tanzania Ltd. ambayo itanunua pamba katika Jimbo la Mheshimiwa Boniphace Getere ni kampuni kubwa na imejipanga vizuri kuhakikisha itawahudumia wakulima wa pamba ipasavyo kama ilivyofanya katika ule msimu wa ununuzi wa 2017/2018. (Makofi)
MHE. DEO K. SANGA (K.n.y. MHE. BONIPHACE M. GETERE) aliuliza:-
Serikali imekuwa na mpango wa kufanya maboresho ya Vituo vya Afya nchini na Kituo cha Afya cha Ikizu ambacho kinahudumia kata zaidi ya 13, majengo yake licha ya kuwa hayatoshelezi hasa wodi ya akina mama wajawazito na watoto, lakini pia yamechakaa sana.
Je, Serikali inatoa tamko gani kuhusu maboresho ya kituo hicho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Ikizu ni kati ya vituo viwili vinavyotoa huduma za upasuaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kituo kingine ni Kasahunga. Katika kukiboresha Kituo cha Afya Ikizu ili kuweza kutoa huduma bora Serikali imeendelea kufanya maboresho ya miundombinu kwa awamu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilifanya ukarabati wa wodi ya wazazi kwa gharama ya shilingi milioni 20. Vilevile katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 33.5 fedha za ufadhili wa AGPAHI kwa ajili ya ukarabati wa jengo la kutolea huduma na tiba na jengo la stoo. Aidha, Halmashauri imetoa kiasi cha shilingi milioni 5.98 kwa ajili ya kusimika mfumo wa kukusanya mapato na takwimu za afya ili kukiwezesha kudhibiti upotevu wa mapato. Serikali inaendelea kutenga fedha kukikarabati kituo hiki ili kuboresha miundombinu na utoaji wa huduma kwa wananchi.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Kila mwaka wanyama waharibifu wamekuwa wanakula mazao ya wakulima katika Jimbo la Bunda na Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kulipa fidia ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakulima hao:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuzuia wanyama hao wakiwemo Tembo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua madhara yanayosababishwa na wanyamapori waharibifu na wakali, hususan tembo, kwa wananchi waishio kandokando ya maeneo ya hifadhi, ikiwemo Wilaya ya Bunda. Katika Wilaya ya Bunda Vijiji vinavyopata usumbufu wa mara kwa mara kutokana na wanyamapori waharibifu na wakali ni Kunzugu, Bukore, Nyatwali, Balili, Tamau, Serengeti, Nyamatoke, Kihumbu, Hunyari, Mariwanda, Mugeta, Guta, Kinyambwiga na Kinyangerere.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwanusuru wananchi kutokana na madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yote yanayopakana na maeneo ya hifadhi. Utekelezaji wa mikakati hiyo unaendelea ambapo katika Wilaya ya Bunda yafuatayo yamefanyika:-
a) Umeanzishwa ushirikiano wa kudhibiti wanyamapori waharibifu kati ya watumishi kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Ikorongo - Gurumeti, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Mwekezaji Gurumeti Reserve;
b) Kutafuta vitendea kazi kwa ajili ya doria za wanyamapori waharibifu;
c) Vikundi 83 vimeanzishwa kwenye vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuchukua hatua za awali za kudhibiti wanyamapori hao pindi kunapokuwa na matukio ya wanyamapori waharibifu, wakati wakisubiri msaada wa Askari Wanyamapori;
d) Wizara imetoa tochi 100 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Mwanga mkali husaidia kufukuza tembo usiku kwa vijiji vinavyounda vikundi hivyo vya kufukuza wanyamapori;
e) Mafunzo kwa wananchi juu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori waharibifu yametolewa kwa vijiji, sambamba na kuwashauri kuepuka kulima kwenye shoroba za wanyamapori;
f) Kuweka madungu (minara) ambayo Askari Wanyamapori wanaitumia kufuatilia mwenendo wa tembo;
g) Kutumia teknolojia ya mizinga ya nyuki ambayo imewekwa pembezoni mwa mashamba; na
h) Mpango wa kutumia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufukuza tembo unaendelea.
Mheshimiwa Spika, lengo la mikakati hii ni kuhakikisha kwamba, matukio ya uvamizi wa tembo yanashughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo. Sambamba na mikakati hiyo Wizara imekuwa ikitoa fedha za kifuta jasho au kifuta machozi pale ambapo mazao yameharibiwa au wananchi wamejeruhiwa au kuuawa na wanyamapori wakali, akiwemo tembo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Machi hadi mwezi Oktoba, 2017, Wizara imelipa kifuta jasho na kifuta machozi cha jumla ya Sh.249,741,250 kwa wahanga 1,284 na vijiji 14 katika Wilaya ya Bunda.
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa inayosababisha matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kuendelea kuwepo ni kuzibwa kwa shoroba na mapito ya wanyamapori. Kutokana na hali hiyo Serikali ina mpango wa kufufua shoroba za wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini kwa mujibu wa Kanuni za Shoroba, GN. 123 ya tarehe 16 Machi, 2018. (Makofi)
MHE. BONIPHANCE M. GETERE aliuliza:-
Mnamo tarehe 12 Januari, 2018 Jeshi la Polisi lilifanya msako mkali katika Kijiji cha Mekomario – Bunda na katika msako huo wananchi wa eneo hilo waliharibiwa mali zao kama ilivyothibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda na kutangazwa kwenye vyombo vya habari yaani Star TV tarehe 15 Februari, 2018:-
Je, ni lini Serikali itafanya tathmini ya kulipa fidia wananchi kutokana na uharibifu huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, ambaye anaongoza Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi na Usalama za Mkoa na Wilaya, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 12 Januari, 2018 zilienezwa tetesi katika Kijiji cha Mekomariro, Wilayani Bunda kwamba wezi kutoka katika Kijiji cha Remong’oroni, Wilayani Serengeti walikuwa wameiba mifugo ya wakazi wa Mekomariro. Badala ya kutoa taarifa Polisi ili wasaidiwe kitaalam kupitia uchunguzi wa Polisi kubaini walioibiwa na idadi ya mifugo iliyoibiwa, walijikusanya kwa utaratibu usiokubalika na kwenda katika Kijiji cha Remong’oroni, wakafanya vurugu zilizosababisha watu wawili wakazi wa Kijiji cha Remong’oroni kuuwawa kikatili na wakamteka mtoto mmoja wa kiume.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za ghasia hizo ziliporipotiwa Polisi, msako ulifanyika kuwabaini wahusika ambapo watuhumiwa nane wamefunguliwa mashtaka Mahakamani kwa kesi ya mauaji Na. RM 02/2018 ambayo bado inaendelea. Msako uliofanyika pamoja na ule wa watuhumiwa wengine waliojificha unaoendelea haujasababisha uharibifu wa mali za wananchi wa Mekomariro wala wa Remong’oroni. Kwa kuwa kesi inaendelea, nashauri tusubiri uamuzi wa Mahakama ili tupate ufumbuzi wa kisheria wa suala hilo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Kwa kuwa msimu wa pamba wa mwaka 2018/2019 ulikuwa na bei elekezi ndogo ya Sh.1,100 na kwa kuwa mara nyingi bei hizo elekezi zinapendekezwa kwa msukumo wa bei ya pamba duniani:-

(a) Je, Serikali katika msimu wa mwaka 2019/2020 ina mkakati gani wa kuinua bei ya wakulima kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500?

(b) Kwa kuwa kuna Vyama vya Ushirika na Benki ya Wakulima, je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la usambazaji wa mbegu za pamba katika Wilaya ya Bunda na hasa Jimbo la Bunda ambapo kila mwaka kunakuwa na uhaba wa mbegu na kutofika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, bei za mazao na bidhaa mbalimbali hutegemea nguvu ya soko kwa kuzingatia kiwango cha uzalishaji (supply), mahitaji (demand), ubora na viwango vinavyohitajika katika masoko ya ndani na nje na ushindani uliopo katika masoko husika.

Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa bei ya pamba kutoka Sh.1,100 hadi Sh.2,500 katika msimu wa ununuzi wa 2019/2020 kutategemea nguvu za soko hususani kupanda kwa bei ya pamba katika soko la dunia. Aidha, pamoja na kutegemea nguvu ya soko la dunia, Serikali inatekeleza mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo ili kuimarisha soko la ndani na ushindani.

(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imechukua hatua ya kuongeza upatikanaji wa mbegu za pamba nchini, ambapo katika msimu wa mwaka 2018/2019 jumla ya tani 27,851 zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima ikilinganishwa na tani 20,496 zilizozalishwa msimu wa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 36. Aidha, kati ya mbegu zilizozalishwa mwaka 2018/2019, tani 1,075 zimesambazwa katika Wilaya ya Bunda ikilinganishwa na tani 688 zilizotumika msimu wa kilimo wa mwaka 2017/2018 ikiwa ni ongezeko la asilimia 56.

Mheshimiwa Spika, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inahudumia sekta ya kilimo kwa ujumla wake kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu ukilinganisha na benki zingine. Aidha, Benki ya Kilimo inatarajia kushiriki katika ununuzi wa pamba sambaba na benki nyingine zilizopo nchini kwa kutoa mikopo kwa kampuni zitakazoshiriki katika ununuzi wa pamba kama ilivyofanyika msimu wa ununuzi wa mwaka 2018/2019.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Mapema mwaka 2016 Waziri wa Nishati alifanya uzinduzi wa Mradi wa Umeme wa REA na kuagiza Vijiji vya Sarakwa, Tingirima, Rakana, Nyang’aranga, Nyamakumbo, Saba–Osanza, Mmagunga, Nyabuzume, Bukama, Tiring’ati, Bigegu, Nyaburundu, Masaba, Nyansirori, Nyamuswa A, Saloka-Guta, Mahanga, Manchimweru, Nyangere, Makongoro A na B na Nyamuswa kupatiwa umeme:-

(a) Je, ni lini kifanyike ili miradi ya vijiji 21 ikamilike kwa wakati kama Serikali ilivyoahidi?

(b) Je, ni nani aliyepanga kijiji A kipate kilomita tatu, transfoma mbili au nguzo 20 na umeme upitie eneo bila kushirikisha vijiji na hata bila kujali wingi wa kaya?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendeelea kutekeleza mradi wa kupeleka umeme katika Vijiji vya Bunda vikiwemo vijiji 21 kupitia kampuni ya Derm Electric Company Limited. Hadi kufikia mwezi Aprili, 2019, mkandarasi alishawasha umeme katika Vijiji vya Nyangere, Bukama, Mugaja Centre, Marambeka, Bunere, Shule ya Msingi Mugaja pamoja na kuunganisha umeme wateja wa awali 289.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mkandarasi anaendelea na kazi ya kusimika nguzo, kuvuta nyaya na kufunga transfoma katika Vijiji vya Sarakwa, Tingirima, Rakana, Nyang’aranga, Nyabuzume, Tiring’ati, Bigegu, Nyaburundu, Guta B, Mahanga, Manchimweru na Makongoro A na B. Kazi za mradi wa kupeleka umeme katika vijiji hivyo inahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 74.8; njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 120; ufungaji wa transfoma 53 za KVA 50 na 100; pamoja na kuunganisha umeme kwa wateja wa awali 1,141. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 7.08 na kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivi itakamilika ifikapo mwezi Juni, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Vijiji vya Nyamakumbo, Saba – Osanza, Mmagunga, Masaba, Nyansirori na Nyamuswa vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III, mzunguko wa pili, unaotarajiwa kuanza Mwezi Julai, 2020 na kukamilika mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya upimaji hufanywa na Serikali kupitia TANESCO, REA na viongozi wa Serikali za Vijiji husika. Kipaumbele ni kupeleka umeme katika maeneo yasiyokuwa na miundombinu ya umeme na katika taasisi zinazotoa huduma za kijamii kama vile vituo vya afya, zahanati, shule na kadhalika. Hata hivyo, ukubwa wa wigo wa mradi wa usambazaji umeme katika mkoa, wilaya na kijiji husika hutegemea zaidi upatikanaji wa fedha.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Katika miaka ya hivi karibuni nchi yetu imekuwa na majina mengi katika Idara ya Ukaguzi toka Ofisi ya CAG kama vile Hati safi, Hati inayoridhisha na Hati chafu:-

(a) Je, Shirika au Halmashauri kupata hati safi ni ishara kwamba Shirika au Halmashauri husika halina ubadhirifu wa mali ya Umma kwa kuwa kuna kila dalili kuwa kutolewa kwa hati safi ni dalili ya wazi ya kuficha ubadhirifu katika baadhi ya Mashirika na Taasisi za Umma?

(b) Je, lini Serikali itafuta utaratibu huo ambao umekuwa kinga ya ubadhirifu wa mali ya Umma?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Boniphace Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya Mwaka 2008 inampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya kaguzi mbalimbali ambazo ni Ukaguzi wa Hesabu (Financial Audits), Ukaguzi wa Kiuchunguzi (Forensic Audits), Ukaguzi wa Ufanisi (Performance Audits) na Ukaguzi Maalum (Special Audits). Lengo Kuu la Ukaguzi wa Hesabu (Financial Audits) ni kutoa maoni kama Hesabu zinazokaguliwa zinaonyesha hali halisi ya mapato na matumizi ya Serikali kwa kuzingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Taarifa za Fedha. Maoni haya hutolewa kwa njia ya hati za ukaguzi ambazo zimegawanyika katika makundi manne ambayo ni hati inayoridhisha; hati yenye shaka hati isiyoridhisha na hati mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hati inayoridhisha hutolewa wakati taarifa za fedha zilizowasilishwa na kukaguliwa zinapokuwa zimezingatia Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Hesabu katika Sekta ya Umma na Sheria na Kanuni za Fedha za Umma. Hati hii huonesha taarifa za fedha zinatoa taswira ya kweli na hali halisi ya mapato, matumizi, mali na madeni ya taasisi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya kuwa ‘hati inayoridhisha’ inatoa tafsiri ya kutokuwepo kwa kila aina ya ubadhirifu siyo sahihi kwa sababu zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, maoni ya ukaguzi yanatolewa kwa malengo maalum ya kuwafahamisha watumiaji wa taarifa za fedha kama taarifa hizo zinaonyesha ukweli na hali halisi ya hesabu za mizania (financial positions) kwa tarehe husika, taarifa za mapato na matumizi (financial performance) pamoja na taarifa ya mtiririko wa fedha (cash flows) kwa kipindi kilichokaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, dhana ya ukaguzi wa hesabu inajikita katika masuala ambayo wakaguzi wanaamini kuwa ni mazito na yana athari kubwa kwenye taarifa za fedha za taasisi husika. Hii ina maana kuwa, mambo ambayo hayana athari kwenye taarifa za fedha yanashughulikwa na mifumo ya udhibiti wa ndani ya taasisi husika.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majibu haya ya sehemu (a), napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, utaratibu huu ndiyo unaotumika dunia nzima, hivyo Serikali haina mpango wa kufuta hati inayoridhisha yenye maoni ya kikaguzi wala kuingilia namna taaluma ya ukaguzi nchini inavyoendeshwa. Kutoa utaratibu mwingine itakuwa ni kukiuka Viwango vya Kimataifa vya Uandaaji wa Tarifa za Fedha katika Sekta ya Umma na pia Viwango vya Kimataifa vya Ukaguzi ambavyo Taifa na Serikali yetu imeviridhia vitumike.
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuliza:-

Idadi ya watu nchini inaongezeka kwa kasi sana na watu wanahitaji maendeleo; aidha ukuaji huu una matokeo hasi na chanya:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kutumia au kudhibiti kasi ya idadi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, utafiti wa idadi ya watu duniani unaonyesha kwamba idadi kubwa ya watu ni fursa kwa nchi iwapo baadhi ya mambo matano yatafanyika:-

(i) Kuboresha maisha ya watoto na kuboresha elimu na uwezeshaji kwa wanawake;

(ii) Kuimarisha uwekezaji katika afya ili kuwa na nguvukazi bora na yenye tija;

(iii) Kuimarisha uwekezaji katika elimu ya juu ili kuwa na nguvukazi yenye elimu, ujuzi na ubinifu;

(iv) Mageuzi ya kiuchumi yanayolenga kuharakisha ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa kazi kwa ajili ya nguvukazi iliyopo; na

(v) Mageuzi ya Sera ili kuvutia uwekezaji wa kigeni na kuhakikisha uwajibikaji hasa katika rasilimali za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya Mpango wetu wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 ni kujenga uchumi wa viwanda ili kufungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu. Mpango huu wa Pili umejikita zaidi katika uwekezaji wa kimkakati katika Sekta ya Viwanda kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji, kusambaza umeme mijini na vijijini, kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakati, kutatua changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa kujenga bwawa kubwa la kufua umeme katika Mto Rufiji na kuimarisha huduma za jamii kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji, hospitali na Vituo vya Afya vya Umma, shule pamoja na kutekeleza kwa ufanisi Sera ya Elimu Bila Malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kufungamanisha fursa za kiuchumi na ongezeko la idadi ya watu; na jitihada hizi zinalandana na mambo yaliyopendekezwa kwenye ripoti ya utafiti ya idadi ya watu duniani na athari zake. Hata hivyo, matokeo chanya yataonekana kama kila Mtanzania atashiriki kikamilifu katika uzalishaji mali na huduma za jamii kuanzia ngazi ya kaya hadi Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo jambo baya kudhibiti ongezeko la idadi ya watu kama familia au Taifa limefikia kiwango cha mwisho cha kutumia rasilimali (optimal utilization) ya rasilimali zake za asili pamoja na mikakati mingine mbadala. Hata hivyo, Taifa letu bado lina rasilimali asili za kutosha kama vile ardhi ya kulima, bahari, maziwa, mito na mabonde, madini, misitu, jiografia ya usafiri na usafirishaji pamoja na fursa za utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jukumu letu kama Taifa kuanzia ngazi ya kaya kuakisi jitihada zinazofanywa na Serikali yetu na hatimaye kutumia fursa hizi kwa ufanisi kwa lengo la kuongeza kasi ya uzalishaji mali pamoja na kuongeza kasi ya kupunguza umasikini badala ya kuogopa ongezeko la idadi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kwa sasa Serikali imejielekeza zaidi katika kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kufanya biashara na hivyo kutumia ongezeko la idadi ya watu kama fursa ya nguvukazi ya kuzalisha mali pamoja na soko la bidhaa na huduma.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Jimbo la Bunda hususan Kata saba za Mugeta, Mihinyo, Kitale, Nyamuswa, Nyamang’uta, Hunyari na Salama zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji ya kunywa; na Serikali ilishaliona hilo na kuwapeleka wataalam wake kufanya survey katika kata hizo:-

Je, baada ya survey hiyo nini kimeamuliwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutatua tatizo la uhaba wa maji katika kata saba zilizopo Jimbo la Bunda, wataalam kutoka Wizara ya Maji kwa kushirikiana na wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda walifanya upimaji (survey) katika vijiji 23 vilivyopo katika kata hizo. Matokeo ya upimaji yalionyesha ni maeneo 10 tu yenye uwezo wa kuhifadhi maji kati ya mita za ujazo 84,794 hadi 354,604. Maeneo hayo ni ya vijiji vya Tingirima, Salama A, Marembeka, Kambumbu, Bigegu, Mahanga, Mihingo, Nyaburundu, Rakana na Manchimweru.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020, Wizara imeweka mabwawa matano katika mpango ili kuanza utekelezaji wa mabwawa hayo ikiwemo Tingirima na Salama A. Aidha, kwa maeneo ambayo hayakufanikiwa kupata vyanzo hivyo vya mabwawa, Serikali itaendelea na tafiti za kuangalia uwezekano wa kupata maji chini ya ardhi au kutumia chanzo cha Ziwa Victoria.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

Ujenzi wa barabara ya Makutano-Nyamuswa- Sanzate.

(a) Je, ni lini barabara ya Makutano Juu - Sanzate itakamilika?

(b) Je, Serikali kupitia wataalam wake imeridhika na kiwango cha uwekaji lami katika barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa barabara ya Makutano Juu - Sanzate-Mgumu - Loliondo - Mto wa Mbu (kilometa 452) ulianza tarehe 5 Aprili, 2013 chini ya Mkandarsi M/S Mbutu Bridge JV akisimamiwa na Mhandisi Mshauri UWP Consulting Tanzania Limited ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na UWP Consulting Limited kutoka Afrika Kusini na hadi hivi sasa ujenzi umefikia asilimia 70.77 na mkandarasi ameomba nyongeza ya muda hadi mwezi Januari, 2020 ili kukamilisha mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, ninapenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa barabara ya Makutano Juu - Sanzate itakamilika ifikapo Januari, 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia wataalam wake, hususan Mhandisi Mshauri aliyeko eneo la mradi na wataalam wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ngazi ya Mkoa na Makao Makuu kuhakikisha kuwa kazi ya ujenzi inakuwa na ubora hivyo materials zote za ujenzi hupimwa ili kuhakikisha ubora wa viwango vinavyotakiwa katika mradi husika. Kwa kuzingatia utaratibu huu, ujenzi unatekelezwa kwa mujibu wa mkataba.
MHE. BONIFACE M. GETERE aliuliza:-

Je, Serikali inachukua hatua gani endelevu za kuondoa tatizo sugu la upungufu wa madawati kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kabla sijaanza kujibu swali namba moja la Mheshimiwa Mwita Getere, naomba kwa idhini yako nitoe shukrani kwanza kwa Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kushinda uchaguzi, lakini vilevile kuweza kuingia ndani ya Bunge. Pia kwa kipekee kabisa nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa imani kubwa ambayo amenionesha kwangu mpaka kuniteua kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI ambayo nahudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nikishukuru chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa imani yake kubwa ambayo wameionesha kwangu kwa kunipa nafasi ya kugombea na mwisho wa siku kunisaidia kampeni na kushinda kwa kishindo. Nakishukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kipekee kabisa niishukuru familia yangu. Mama yangu mzazi kwa kuwa nami katika kipindi chote mpaka kufikia hatua hii ambayo leo nimefikia…

SPIKA: Sasa majibu!

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, sasa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mwita Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniface Mwita Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, changamoto ya wanafunzi kukosa madawati katika shule za msingi na sekondari imetokana na mwitikio mkubwa wa wazazi kuandikisha wanafunzi shuleni baada ya Serikali kuanzisha mpango wa utoaji wa elimu bila malipo ambapo idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kwenye shule za msingi na sekondari umeongezeka maradufu.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati ambapo mpaka sasa mwaka 2015 kulikuwa na madawati 3,024,311 na mpaka sasa hivi kufikia mwezi Septemba 2020 Serikali imeongeza madawati kufikia madawati 8,095,207 ambapo kumekuwa na ongezeko la madawati 5,070,899.

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na upungufu wa madawati, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya utengenezaji wa madawati kwenye miradi yote inayotengewa fedha za ukamilishaji wa vyumba vya madarasa kwa shule za msingi na sekondari na kuhamasisha wananchi na kuwashirikisha wadau na asasi mbalimbali katika utengenezaji wa madawati pamoja na kuendelea kutenga fedha ya matengenezo ya madawati kwenye Halmashauri kupitia mapato ya ndani. Nashukuru sana.
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukamilisha dhana ya elimu bure kwa kutoa elimu bure kuanzia Shule ya Msingi hadi Kidato cha Tano na cha Sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dhana ya utoaji Elimu Msingi Bila Malipo inamaanisha kuwa mwanafunzi atasoma bila mzazi au mlezi kulipa ada wala michango ya fedha iliyokuwa inatozwa shuleni kabla ya kutolewa kwa Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka 2015. Gharama hizo zote ambazo mzazi au mlezi alitakiwa kutoa kwa sasa hulipwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, dhana ya Elimu Bila Malipo inalenga elimu msingi. Elimu hii inaanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Sekondari, Kidato cha Nne ili kuwajengea watoto wa Kitanzania misingi imara ya masomo ngazi zinazofuata na ustawi wa maisha yao kwa ujumla. Elimu ya kidato cha tano na sita nchini hutolewa kwa ushirikiano kati ya wazazi/ walezi na Serikali. Wazazi au walezi hutakiwa kuchangia ada ya shilingi 70,000 kwa wanafunzi wa shule za bweni na shilingi 20,000 kwa wanafunzi wa shule za kutwa kwa mwaka. Serikali hugharamia gharama nyingine zilizobaki kama vile mishahara ya walimu, vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa mfano vitabu na vifaa vya maabara pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE Aliuza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kufukia mashimo makubwa yaliyosababishwa na ulimaji wa barabara na uchimbaji wa madini hasa katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Mazingira Na. 20 ya Mwaka 2004 inaelekeza maeneo yaliyoharibiwa kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini kurejeshwa katika hali yake awali ikiwemo kufukia mashimo, kupanda miti na kudhibiti taka. Aidha, wamiliki wa migodi yote wanatakiwa kuweka Hati Fungani (Environmental Performance Bonds) kama dhamana ya Usimamizi wa Mazingira katika migodi husika.

Aidha, Sheria ya Madini, Sura ya 123 inawataka wamiliki wote wa leseni za uchimbaji madini kuhakikisha uzingatiaji wa utunzaji wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji wa madini ikiwemo ufukiaji wa mashimo yatokanayo na shughuli hizo.

Mheshimiwa Spika, Mikakati mbalimbali imewekwa ili kuzingatia utekelezwaji wa Sheria hizi ikiwemo:-

(i) Serikali kupitia Kamati ya Kitaifa ya Kufuatilia Utekelezaji wa Mipango ya Ufungaji Migodi inahakikisha hatua zote za urejeshwaji wa maeneo ya uchimbaji ikiwemo kufukia mashimo yaliyotokana na shughuli za uchimbaji zinazingatiwa ipasavyo; na

(ii) Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika migodi husika mara kwa mara imekuwa ikifanya ufuatiliaji na ukaguzi wa uzingatiaji wa matakwa haya ya kisheria.

Mheshimiwa Spika, mashimo makubwa yote yaliyotokana na uchimbaji wa madini katika Mikoa ya Mara, Geita na Shinyanga yanapaswa kufukiwa. Serikali inaendelea kufuatilia na kuhakikisha kuwa matakwa haya ya kisheria yanazingatiwa. Aidha, kwa upande wa mashimo makubwa yanayotokana na ulimaji wa barabara, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeendelea kuhimiza uzingatiaji wa masuala ya hifadhi ya mazingira wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-

(a) Je, ni nini kinasababisha Tanzania kutojitosheleza kwa mafuta ya kula?

(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mikoa yenye ardhi ya kutosha ya kuzalisha zao la alizeti hususan Mkoa wa Mara inatambuliwa rasmi na kupewa mahitaji yote ya mbegu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniface Mwita Getere, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya mafuta ya kula nchini yanakadiriwa kuwa wastani wa tani 570,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji wa mafuta ya kula nchini unakadiriwa kufika wastani wa tani 205,000 na kufanya upungufu wa wastani wa tani 365,000 kwa mwaka, ambapo husababisha nchi kutumia wastani wa Shilingi bilioni 474 kuagiza mafuta ya kula kutoka nje kwa mwaka.

Aidha, uhaba wa mafuta ya kula nchini umetokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya mbegu za mafuta yakiwemo alizeti, michikichi, pamba unachangiwa na matumizi hafifu ya teknolojia ikiwemo mbegu bora na usindikaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha mazao ya mafuta ikiwemo alizeti, michikichi na pamba katika mikoa yote yenye ardhi na hali ya hewa inayofaa kwa kilimo cha mazao hayo. Aidha, Serikali imeweka msukumo wa kuimarisha huduma za ugani nchini ambapo katika bajeti ya 2021/2022, Wizara imepanga kuwezesha Maafisa Ugani 680 wa Mikoa ya Singida, Dodoma na Simiyu pikipiki kwa ajili ya ufuatiliaji, kupatiwa mafunzo rejea na kuwezesha wagani hao kuanzisha mashamba ya mfano ya alizeti na pamba pamoja na kuanzisha mashamba ya (Block Farm) ambayo tunafanya pamoja na Wizara ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Lengo la uwezeshaji huo ni kuleta ufanisi katika kutoa huduma za ugani ili kuongeza tija na uzalishaji wa mazao ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2021/2022, Serikali itawekeza jumla ya bilioni 10 kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mbegu bora za mazao yakiwemo ya mbegu za mafuta kwa kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kupanua mashamba ya mbegu ya Wakala wa Serikali (ASA), mbegu hizo zitasambaza kwa wakulima kwa Mikoa yote itakayozalisha mazao hayo ikiwemo Mkoa wa Mara kupitia ASA na wasambazaji binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Serikali inaendelea kuhamasisha sekta binafsi kuingia kwenye uzalishaji wa mbegu na ipo tayari kufanya majadiliano na makampuni au watu wenye nia ya kuwekeza kwenye uzalishaji wa mbegu ili kuweka utaratibu wa kupunguza gharama za uzalishaji wa mbegu kwa tija.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, nini kinazuia kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya Makutano – Sanzate kwa kiwango cha lami ambayo ina miaka tisa sasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya barabara kutoka Makutano hadi Sanzate yenye urefu wa kilometa 50, ulianza mwezi Mei, 2013 na ulitarajiwa kukamilika Mei, 2015. Ujenzi wa sehemu hii ya barabara, unatekelezwa na Kampuni ya Mbutu Bridge JV Contractors ambayo ni Muungano wa makampuni ya kizalendo 11 kwa gharama ya shilingi bilioni 46.1. Mbutu Bridge JV Contractors walipata mradi huu kwa njia ya ushindani baada ya kumaliza mradi wa mafunzo kwa Makandarasi Wazalendo wa Ujenzi wa Daraja la Mbutu ambao ulifanyika kwa ufanisi mkubwa. Hivyo, Serikali iliona ni fursa nyingine kwa kampuni ya kizalendo kuongeza uzoefu katika ujenzi wa barabara za lami.

Mheshimiwa Spika, baada ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huu, kulijitokeza changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa changarawe kwa ajili ya tabaka la barabara (G45), kuongezeka kwa kiasi cha upasuaji miamba na kuongezeka kwa kiasi cha ukataji udongo. Hali hii ilisababisha kubadilishwa kwa usanifu wa barabara na kulazimu Mkandarasi kuongezewa muda wa utekelezaji wa mradi hadi Februari, 2021.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Mkandarasi hakuweza kukamilisha kazi hiyo kwa muda uliopangwa. Kwa sasa kazi iliyobaki ni asilimia 12 maana yake imefanyika asilimia 88. Kufuatana na mpango mpya wa ujenzi, Mkandarasi amepanga kukamilisha ujenzi ndani ya miezi minne kuanzia sasa. Mkandarasi ameshapeleka katika eneo la kazi vifaa muhimu vya ujenzi ikiwa ni pamoja na malori, kokoto na lami.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itahakikisha mapema iwezekanavyo baada ya kuhakiki madai ya mkandarasi shilingi bilioni 1.7 anazodai ili kumrahisishia kukamilisha kazi hii ndani ya muda nilioutaja. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kata Saba za Tarafa ya Chamriho watapatiwa maji kutoka mradi wa maji ya Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama ni endelevu. Kwa kata saba zilizopo Tarafa ya Chamriho, upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 61, ambapo vijiji vyote katika Kata tatu za Hunyari, Salama na Nyamuswa vinapata maji kutoka kwenye visima na chemchem.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Kata nne, vijiji ambavyo huduma ya maji siyo ya uhakika ni Mahanga na Mamicheru katika Kata ya Mihingo, Kiroeli, Kambumbu na Nyambuzume Kata ya Nyamanguta, Marambeka na Nyamburumbu Kata ya Ketere na kijiji cha Sanzate Kata ya Mgeta.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 mpango wa muda mfupi ni kuboresha huduma ya maji katika vijiji hivyo sita, kupitia utekelezaji wa miradi wa visima virefu ambao utaanza mwezi Oktoba, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkakati wa Serikali ni kutumia vyanzo vya maji vya uhakika hasa Maziwa makuu. Hivyo, mpango wa muda mrefu ni kufanya upanuzi kutoka miradi mikubwa ya maji inayotumia maji ya Ziwa Victoria.
MHE. CECIL D MWAMBE K.n.y. MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

(a) Je ni lini mikataba ya miradi mbalimbali ya migodi ya madini, ujenzi wa Bandari Bagamoyo, ujenzi wa Reli (SGR), ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Bomba la Mafuta na Mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam italetwa Bungeni ili kupata ufahamu wa miradi hiyo?

(b) Je, katika mikataba hii ni mingapi imewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za mikataba ya ujenzi wa Reli ya SGR, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, Migodi ya Madini, Bomba la Mafuta na Mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam kwa nyakati tofauti Taasisi na Mashirika yanayosimamia miradi hii yamekuwa yakiwasilisha kwenye Kamati za Kudumu za Bunge taarifa za mikataba ya miradi hiyo. Aidha, Kamati zina mamlaka kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge kupata taarifa zozote kuhusiana na mikataba ya miradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, miradi hii imekuwa ikikaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali yaani CAG. Kwa kuwa baadhi ya miradi Serikali inamiliki kwa asilimia 100 na mingine Serikali ni mbia, hivyo taarifa zake huwasilishwa katika Bunge lako tukufu kupitia Ripoti ya CAG. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, Sura ya Tano na Sita inabainisha kwa kina taarifa ya ukaguzi ya miradi ya ujenzi wa Reli SGR kwa Lot. 1 na Lot. 2 na Mradi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere. Aidha, mradi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umekuwa ukifanyiwa ukaguzi wa kawaida kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kumuarifu Mheshimiwa Mbunge na pia Bunge lako tukufu kuwa Bunge limekuwa likipokea taarifa za mikataba na Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kama nilivyoeleza hapo juu. Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, ni fursa zipi anazopata Askari anayeoa au kuolewa na Askari mwenzake?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kanuni, miongozo na taratibu za Majeshi ya Ulinzi, kila Afisa na Askari hupewa stahiki kulingana na cheo chake. Endapo Afisa au Askari ataoa au kuolewa na mwenzake, haitaathiri stahiki zake. Aidha, hakuna fursa za kipekee anazopata Afisa au Askari aliyeoa au kuolewa na mwenzake.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, Serikali ina kauli gani juu ya maeneo ya ardhi yanayotumika na Serikali au Taasisi zaidi ya miaka 12 yakiwa hayana hatimiliki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 62 lililoulizwa na Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa maeneo mengi yanayomilikiwa na Taasisi za Umma yana hatimiliki. Hata hivyo, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa maelekezo kwa Taasisi na Idara za Umma kuhakikisha maeneo yao yanapangwa, kupimwa na kupatiwa hatimiliki.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza: -

Je, mpango wa kupeleka maji ya Ziwa Victoria kutoka Bunda Mjini kwenda Vijiji 33 vya Tarafa ya Chamriho umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniface Mwita Getere, Mbunge wa Jimbo la Bunda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuboresha huduma ya maji katika Tarafa ya Chamriho ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 inatekeleza ujenzi wa miradi mipya mitatu ya KirolerI - Kambubu, Mariwanda na Sanzate pamoja na ukarabati wa mradi wa maji wa Nyang’aranga ambayo itatoa huduma ya maji kwa wananchi wapatao 12,648.

Mheshimiwa Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha Wananchi wa tarafa ya Chamriho wanapata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza. Katika kutimiza lengo hilo, taratibu za kumwajiri Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya usanifu wa mradi wa maji wa kutoka Ziwa Victoria zinaendelea. Matarajio ni kuanza ujenzi wa mradi katika robo ya pili ya mwaka wa fedha 2022/2023.