Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ritta Enespher Kabati (31 total)

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
(a) Je, ni lini askari wa Iringa watajengewa nyumba?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha wanachodai askari wa Mkoa wa Iringa posho na stahiki zao zingine?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la ukosefu wa nyumba za askari wa Jeshi la Polisi hapa nchini. Lengo la Serikali ni kujenga nyumba hizo kwa awamu kutegemea na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia ujenzi huo. Kwa nafasi hii nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wa suala hili na pia amekuwa akijitoa sana katika kuboresha mazingira ya askari katika eneo lake.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua madai ya askari ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa kama ilivyo kwa Mikoa mingine hapa nchini. Askari wa Mkoa wa Iringa wanaidai Serikali jumla ya shilingi 431,147,410 na uhakiki wake unaendelea chini ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani ili Serikali iweze kulipa baada ya ukaguzi huo.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Tatizo la kesi za ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo limekuwa likiongezeka siku hadi siku katika Mkoa wa Iringa.
(a) Je, nini mkakati wa Serikali kunusuru hawa watoto wasiendelee kufanyiwa matendo haya ya kikatili?
(b) Je, ni utaratibu gani unatumika kushughulikia watuhumiwa wa kesi hizi?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, ili kudhibiti vitendo hivi haramu dhidi ya watoto tumetunga sheria zenye adhabu kali kwa watuhumiwa wanaopatikana na hatia ya makosa ya ubakaji na ulawiti. Kifungu cha 136(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, kimeweka adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kubaka na kifungu cha 132(2) kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa yeyote anayekutwa na hatia ya kujaribu kubaka. Aidha, kifungu cha 154 kimeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 jela kwa kosa la kulawiti. Lengo la kutoa adhabu hizo kali lilikuwa kutoa fundisho na onyo kwa yeyote mwenye dhamira ya kutenda makosa hayo ya jinai.
Mheshimiwa Spika, matukio mengi ya aina hiyo Mkoani Iringa yanahusisha ndugu au jamaa wa familia moja au sehemu moja. Ushahidi wa msingi hufichwa unapohitajika na wahusika wa pande zote mbili huyamaliza masuala husika kwa maelewano kifamilia na hivyo kuchochea matendo hayo ya jinai kushamiri.
Napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi kuvisaidia vyombo vya dola wakati wa upelelezi na uendeshwaji wa mashauri haya mahakamani ili kukomesha kabisa matukio hayo. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge na wenzako Mkoani Iringa kuwa mstari wa mbele katika kampeni hii ya kuomba ushirikiano na wananchi.
Mhesimiwa Spika, aidha, ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi. Pindi, tukio la kubaka au kulawiti linaporipotiwa upelelezi hufanyika na mtuhumiwa hufunguliwa mashitaka mara moja.
(b) Mheshimiwa Spika, utaratibu unaotumika kushughulikia watuhumiwa wa kesi za kubaka na kulawiti umefafanuliwa katika Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 na Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Sheria hizi zimeainisha namna ya kushughulikia makosa hayo kuanzia wakati wa kupokea taarifa ya kutokea kitendo cha ubakaji na ulawiti mpaka hatua ya kutoa adhabu kwa wahusika wa vitendo hivyo.
Mheshimiwa Spika, pamoja na taratibu za kisheria zilizoainishwa katika sheria hizo, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa kesi za kubaka na kulawiti zinamalizika mapema na kuwa sheria zinasimamiwa ipasavyo.
Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa mashtaka kwa lengo la kujenga kesi na kuwa na ushahidi usiotia shaka ili kuiwezesha Mahakama kufikia maamuzi ya kuwatia hatiani watuhumiwa wa vitendo hivyo.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. MHE. RITTA E.
KABATI) aliuliza:-
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 imekuwa ya muda mrefu na hivyo kupitwa na wakati.
Je, ni lini sheria hii itafanyiwa marekebisho ili iendane na mahitaji na kuondoa upungufu uliopo?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 ni matokeo ya mjadala mpana na shirikishi kupitia Waraka wa Serikali Na.1 ya mwaka 1969. Lengo la mjadala huo lilikuwa kupata muafaka kuhusu maudhui ya sheria hiyo ambayo yaligusa imani, mila na desturi za Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya miaka zaidi ya 20 kupita tangu Sheria hiyo ya Ndoa itungwe, Serikali kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria iliifanyia mapitio sheria hiyo na kubaini maeneo kadhaa yenye udhaifu na hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa mwenyekiti, kutokana na maoni hayo ya tume, mwaka 2008 Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria iliandaa Waraka wa Baraza la Mawaziri uliokuwa na mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya M waka 1971.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, mnamo Desemba, 2010 kabla ya waraka huo kujadiliwa na kuridhiwa na Baraza la Mawaziri, mchakato wa mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukaanza na kulilazimu baraza kusitisha kwa muda mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Ndoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikuwa na matarajio kuwa wakati Tume ya Mabadiliko ya Katiba inakusanya maoni ya wananchi kuhusu mabadiliko ya Katiba, wananchi wangetoa maoni kuhusu Sheria ya Ndoa pamoja na sheria nyingine zinazofanana na hiyo. Hata hivyo, maoni yaliyotolewa wakati wa mchakato huo kuhusu Sheria ya Ndoa yalikuwa machache sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na muda kupita na mabadiliko kadhaa yaliyotokea kuhusu Sheria ya Ndoa, Wizara yangu imeendelea na mchakato wa ndani wa kuifanyia mapendekezo ya marekebisho sheria hiyo. Wakati muafaka utakapofika, tutawasilisha mapendekezo ya
marekebisho ya sheria hiyo Bungeni ili iweze kuendana na wakati kwa kuondoa upungufu uliopo kwa maslahi mapana ya nchi yetu na kuhuisha na kuimarisha maeneo yaliyo mazuri ndani ya sheria hiyo.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Zao la mbao linachangia pato la Taifa katika nchi yetu na zao hili linazalishwa kwa wingi katika Wilaya ya Mufindi katika Mkoa wa Iringa:- Je, zao hili linaingiza fedha kiasi gani kwa mwaka.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mbao ni miongoni mwa mazao yanayochangia pato la Taifa na pia kutoa ajira kwa wananchi. Zao hili linazalishwa kwa wingi katika Wilaya ya Mufindi kutoka katika shamba la miti la Serikali la Sao Hill. Aidha, kiasi cha fedha kinachopatikana kwa mwaka hutegemea kiasi cha meta za ujazo kilichopangwa kuvunwa ambacho nacho kutegemeana na kiasi kinachoruhusiwa kitaalam kuvunwa kwa mwaka kulingana na mpango wa uvunaji wa kila shamba (annual allowable cut).
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mdororo wa uchumi mwanzoni mwa miaka ya 1980, Serikali ilibinafsisha viwanda vyake vikiwemo viwanda vya bidhaa za misitu. Serikali ilibakia na jukumu la kuhifadhi misitu pamoja na kukuza miti katika mashamba yake. Hivyo, Serikali huuza miti iliyosimama kwa wawekezaji binafsi ambao huvuna na kuchakata magogo kwa ajili ya mbao, karatasi, nguzo na mazao mengine; shughuli za uchakataji zinabaki kuwa jukumu la sekta binafsi. Kwa kuwa Serikali haihusiki moja kwa moja na uchakataji, takwimu halisi zilizopo wizarani ni za ujazo wa miti inayouzwa kwa wadau mbalimbali na kiasi cha fedha kilichopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2015/2016, jumla ya meta za ujazo wa miti zipatazo 767,946.46 zilivunwa kutoka kwenye mashamba ya Serikali na kuiingizia Serikali jumla ya Sh.58,312,894,416.20. Aidha, kwa mwaka 2016/2017, mashamba ya Serikali yalivunwa na kuuza miti yenye meta za ujazo 754,931 kwa viwanda vya kuzalisha mbao na kuipatia Serikali fedha zipatazo Sh.55,102,043,000.00 ikiwa ni mrabaha na tozo, ushuru wa Halmashauri za Wilaya (CESS) na kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa misitu ya asili, mapato yanayotokana na zao la mbao, ni wastani wa shilingi bilioni 18.3 kwa mwaka.
RITTA E. KABATI aliuliza:-
Mwaka 2000 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini:-
Je, hali ya utekelezaji wa mpango huo wa TASAF ikoje?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mwaka 2000 ili kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umaskini. Mafanikio makubwa yamepatikana katika awamu zote za utekelezaji kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa awamu ya kwanza ambayo ilitekelezwa mwaka 2000 hadi mwaka 2005 iliwezesha jamii kutekeleza miradi 1,704 yenye thamani ya shilingi bilioni sabini na mbili katika halmashauri 40 za Tanzania bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Miradi hiyo iliibuliwa na wananchi na ilihusisha sekta zote muhimu za afya, elimu, maji pamoja na barabara vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa awamu ya pili, TASAF ilitekelezwa mwaka 2005 hadi mwezi Juni, 2013 ambapo miradi 12,347 yenye thamani ya shilingi bilioni 430 katika halmashauri 126 za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Miradi hii iliongeza upatikanaji wa huduma za maji, elimu, afya, pamoja na barabara vijijini na kuongeza upatikanaji wa chakula
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya tatu ilizinduliwa mwaka 2012 na utekelezaji wake ulianza mwezi Januari, 2013 na unaendelea kutekelezwa hadi mwaka 2022 katika halmashauri 159 za Tanzania Bara na wilaya zote za Tanzania Zanzibar. Madhumuni ya TASAF awamu ya tatu ni kuwezesha kaya maskini kuongeza kipato, fursa pamoja na uwezo wa kuwagharamia mahitaji muhimu. Kazi zilizofanyika katika awamu ya tatu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kaya maskini milioni 1.1 zenye jumla ya watu takribani milioni tano zimeandikishwa katika vijiji, mitaa na shehia 9,986. Hadi kufikia mwezi Agosti mwaka huu kaya hizi masikini zilishapokea ruzuku ya shilingi bilioni 521.9. Kaya hizo pia zimetekeleza miradi ya kutoa ajira za muda kwa kaya za walengwa 354,648 kutoka katika halmashauri 42 za Tanzania Bara pamoja na Tanzania Zanzibar. Hadi kufikia Agosti mwaka huu, jumla ya miradi 3,553 yenye thamani ya shilingi bilioni 51.1 kutoka katika vijiji 2,063, mitaa 329 na shehia 168 imeibuliwa na kutekelezwa. Hadi sasa miradi 2,952 imekamilika; lakini pia miradi 601 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa kukamilishwa katika mwaka huu wa fedha
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Agosti mwaka huu, miradi ya kuendeleza miundombinu ya huduma za jamii 192 yenye thamani ya shilingi bilioni nane imetekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. Aidha, mpango wa kuhamasisha kaya kuweka akiba na kuwekeza unatekelezwa na umewawezesha walengwa kushiriki katika kuweka akiba katika vikundi na kutekeleza miradi ya ujasiriamali ikiwa ni mkakati endelevu wa kaya kutoka kwenye umaskini. Jumla ya vikundi 5,136 vya kuweka akiba na kuwekeza vyenye wanachama 11,907 vimeundwa katika Halmashauri sita za Tanzania Bara ambazo ni Kibaha, Bagamoyo, Chamwino, Lindi, Mtwara pamoja na Manispaa ya Lindi, Unguja na Pemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je, ni lini Mahakama zote nchini zitaanza kuendesha kesi kwa lugha ya Kiswahili?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI NA MICHEZO (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 12 cha Sheria ya Mahakama Sura ya 11 yaani (Magistrates’ Courts Act CAP 11; S.12), lugha inayotumika kuendesha kesi katika Mahakama zote za Mwanzo ni Kiswahili. Aidha, kifungu hiki kinatamka kwamba kesi katika Mahakama za Wilaya na za Hakimu Mkazi zitaendeshwa kwa Kiswahili ama Kiingereza, isipokuwa hukumu inaandikwa kwa Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mahakama Kuu, Kanuni za Lugha za Mahakana ukisoma Kanuni ya (2) inasema kuwa Lugha ya Mahakama Kuu itakuwa Kiswahili au Kiingereza, isipokuwa kumbukumbu za maamuzi, ama hukumu itakuwa kwa lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni za Mahakama ya Rufani ya mwaka 2009, ukisoma Kanuni ya (5) lugha inayotumika katika kuendesha mashauri itakuwa ni Kiswahili au Kiingereza kulingana na maelekezo ya Jaji Mkuu au Jaji anayesikiliza shauri husika, isipokuwa hukumu inaandikwa kwa Kiingereza.
Mheshimiwa Spika, hivyo ninapenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba uendeshaji wa mashauri katika Mahakama zote nchini kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo unaruhusu kutumia lugha zote mbili, Kiswahili na Kiingereza na tumekuwa tukizingatia lugha hizo katika uendeshaji wa mashauri.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Serikali ya Tanzania ilisaini Mkataba Namba 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) tangu tarehe 16 Juni, 2011 na Rais Mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alishawahi kutamka kuwa, Tanzania haina tatizo na Mkataba huo.
Je, kuna kikwazo gani kinachokwamisha kuridhia Mkataba huo wa ILO Namba 189 wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani wakati Baraza la Wafanyakazi (LESCO) limeshapendekeza kuridhia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Tanzania kama nchi mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani ilishiriki kikamilifu katika majadiliano na upitishwaji wa Mkataba ya Kimataifa wa ILO wa Wafanyakazi wa Majumbani Namba 189 wa mwaka 2011 ambao unalenga kukuza kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani. Aidha, hadi kufikia tarehe 30/08/2017 mkataba huo umeridhiwa nan chi 24 kati ya nchi wanachama 187 ambapo nchi za Afrika zilizoridhia mkataba huu ni tatu ambazo ni Afrika Kusini, Mauritius na Guinea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha napenda nielezee kuwa Serikali inathamini mchango wa wafanyakazi wa majumbani katika kujenga uchumi wa nchi. Hii ndio maana Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004, ambayo inazitambua haki za wafanyakazi wa majumbani kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine. Vilevile kwa upande wa Zanzibar ipo Sheria ya Ajira, Namba 11 ya mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuridhia mikataba yote ya kimataifa ikiwemo ya Shirika la Kazi Duniani siku zote Serikali imekuwa ikizingatia maslahi mapana ya nchi na ustawi wa wananchi ikiwemo wafanyakazi kwa ujumla. Endapo Serikali itajiridhisha kuwa mazingira na ustawi wa wafanyakazi kwa sheria zilizopo hakuna ustahimilivu, Serikali itafanya maamuzi stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa kwa kushirikiana na wadau wote vikiwemo vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri, Serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi, ili kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani pamoja na kujenga uelewa wa wadau kuhusu matakwa ya mkataba na haki za sheria za wafanyakazi hao.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Kiwanja cha Ndege cha Nduli kipo katika mpango wa Serikali wa Ujenzi wa viwanja 11:-
(a) Je, ni lini kiwanja hicho kitajengwa?
(b) Mpaka sasa hakuna kituo cha kujaza mafuta katika kiwanja hicho; je, ni utaratibu gani unaotumika ili kiwepo kituo cha mafuta katika kiwanja hicho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS JOHN KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:
(a) Kiwanja cha Ndege cha Nduli kililichopo Mkoani Iringa ni miongoni mwa viwanja 11 vya ndege vilivyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina uliomalizika mwezi Mei mwaka 2017. Katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, Serikali ilitenga fedha za ndani kwa ajili ya maandalizi ya ujenzi wa kiwanja hicho ikiwa ni pamoja na kutangaza zabuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kutokana na Benki ya Dunia kuonesha nia ya kufadhili ujenzi wa uwanja huu, Serikali ilisitisha taratibu za ndani za manunuzi ili kusubiri manunuzi kufanyika kwa kuzingatia taratibu za Benki ya Dunia. Hivyo, uwanja huo utaanza kujengwa mara moja baada ya taratibu hizo kukamilika.
(b) Kwa sasa kiwanja hiki hakina ndege za kutosha zinazoweza kuvutia uwekezaji wa kituo cha mafuta. Ni vema ieleweke wazi kwamba sera ya uwekezaji katika viwanja vya ndege inatoa fursa ya kuuza mafuta ya ndege kwa makampuni binafsi yenye leseni ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga TCAA.
Mheshimiwa Naibu Spika, Makampuni yenye leseni hizo na yaliyoingia mikataba ya biashara ya mafuta ya ndege na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania TAA ni Puma, Oilcom, Total na Prime fuels. Kwa hiyo, ni utashi wa makampuni ya mafuta na nguvu ya soko inayosukuma uwekezaji wa biashara ya mafuta katika viwanja vya ndege. Ni matumaini yangu kwamba kiwanja hiki kitakapokamilika kujengwa kitawavutia wawekezaji na hatimaye kumaliza tatizo hili.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara uliopo Manispaa ya Iringa umekuwa ni wa muda mrefu sana toka umeanza.
Je, ni lini Serikali italeta fedha za kutosha ili kumaliza mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa machinjio ya kisasa wa Ngerewara unatekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kwa kushirikiana na wadau wengine. Mradi ulianza kutekelezwa mwaka 2008/2009 na ulikadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania 1,900,000,000. Aidha, mpaka sasa kiasi cha shilingi 928,000,000 zimetumika kugharamia mradi huu kupitia Serikali Kuu, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mradi wa ASDP na Shirika la Maendeleo la Viwanda la Umoja wa Mataifa ambalo lilisaidia kuweka vifaa vya machinjio vikiwemo mashine za kuchakata nyama na vyumba viwili vya kuhifadhi ubaridi (cold rooms).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa sehemu kubwa ya miundombinu inayohitajika kwa ajili ya machinjio imekamilika. Aidha, kiasi cha shilingi 1,090,000,000 zinahitajika kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa zizi, mabwawa matatu ya maji machafu na maji safi, uzio wa machinjio, tanuru la kuchomea taka kwa maana ya incinerator, jengo la ofisi za utawala, vyoo, jiko na kisima cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itashirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kuhakikisha fedha za kukamilisha machinjio ya Ngerewara zinapatikana ili Watanzania wapate ajira na bidhaa abora za mifugo na kuongeza pato la Halmashauri na Taifa kwa ujumla wake.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mradi wa umwagiliaji wa Mkoga Irrigation Scheme uliopo katika Manispaa ya Iringa Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ernest Kabati, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kutekeleza ujenzi wa scheme mbalimbali hapa nchini. Katika mwaka wa fedha 2014/2015 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kupitia mfuko wa Food Aid Counter Party ilitumia kiasi cha shilingi milioni 270 kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya mashambani na ujenzi wa mfereji mkuu katika scheme ya umwagiliaji ya Mkoga yaani Mkoga Irrigation Scheme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu wa scheme hiyo haujakamilika na bado unahitaji kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya umwagiliaji mashambani. Hivyo Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeingiza scheme ya umwagiliaji ya Mkoga kwenye awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango kabambe wa Taifa wa umwagiliaji utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019 hadi mwaka 2025/2026.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio vingi vya utalii kama vile Hifadhi za Taifa za Ruaha na Udzungwa, Makumbusho ya Mtwa Mkwawa ya Kalenga, Isimila, Eneo la Zana za Mwanzo za Mawe na Maumbile Asilia na Makumbusho ya Mkoa ambayo inaonesha utamaduni wa asili wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na mpango kabambe wa uendelezaji utalii, Serikali imekuwa ikitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Iringa. Mpango kabambe wa kuendeleza utalii nchini ulioandaliwa mwaka 1996 na kufanyiwa mapitio mwaka 2002 umeainisha Mkoa wa Iringa kama kitovu cha maendeleo ya utalii (tourism hub) kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuainisha vivutio katika Mkoa wa Iringa lilianza kufanyika mwaka 2007 ambapo mpaka sasa takribani maeneo 38 ambayo ni vivutio vya utalii yameainishwa katika Wilaya za Mufindi, Kilolo na Iringa. Kazi inayofuata sasa ni kuendeleza na kutangaza vivutio hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia taasisi zake ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania imeweka mikakati madhubuti ya kutangaza utalii. Mikakati hii ni pamoja na kujenga utambulisho wa Tanzania (Destination Tanzania Brand), kukuza maonesho ya utalii wa Kimataifa yanayofanyika ndani na nje ya nchi kama vile Karibu Kusini, kuanzisha channel ya utalii, kuanzisha Studio ya kutangaza utalii kwa njia ya TEHAMA, kuadhimisha Mwezi wa Urithi (Urithi Festival) na kuimarisha uhamasishaji kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanafunzi. Vivutio vya utalii katika Mkoa wa Iringa vimejumuishwa katika mikakati hii ya kutangaza utalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo hapo juu na ili utalii Mkoani Iringa, Serikali imeendesha mafunzo ya muda mfupi ya utalii na ukarimu kupitia mradi wa SPANEST kwa takribani watu 300, imefungua Ofisi ya Utalii ya Kanda ya Kusini iliyoko Iringa na imezindua mradi wa kukuza utalii Ukanda wa Kusini ujulikanao kama REGROW. Aidha, Iringa ni miongoni mwa mikoa iliyoajiri Maafisa Utalii kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Halmashauri za Wilaya.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Mheshimiwa Rais alitoa tamko kuwa Wazauni wote wanaoidai Serikali walipwe:-

Je, tokea tamko hilo litolewe ni Wazabuni wangapi wameshalipwa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Ernespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jumla ya wazabuni 2,048 wamelipwa madai yao tangu kutolewa kwa tamko na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 3 Januari, 2018 Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Kati ya wazabuni 2,048 waliolipwa, wazabuni 1,277 walihudumia sekretarieti za mikoa na 771 walihudumia Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali.

Aidha, jumla ya shilingi 199,064,014,966.64 zimetumika kulipa wazabuni hao, ambapo shilingi 3,729,605,175/= zimetumika kulipa wazabuni waliotoa huduma kwa sekretarieti za Mikoa na shilingi 195,334,409,791.64 zimetumika kulipa wazabuni wa Wizara, Taasisi na Wakala za Serikali. Aidha, madai haya yalilipwa baada ya uhakiki kufanyika.

Mheshimiwa Spika, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu na wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwamba, Serikali itaendelea kulipa madai mbalimbali ya wazabuni kulingana na upatikanaji wa fedha sambamba na uhakiki wa madai husika. Aidha, ili kukamilisha zoezi la uhakiki kwa wakati, wazabuni wote wanaombwa kutoa ushirikiano hususan kuwasilisha taarifa na vielelezo sahihi vya madai yao pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.
MHE. RITTA E. KABATI Aliuliza:-

Wananchi waliopisha ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Tumaini kuchepusha magari makubwa kupita katikati ya Mji wa Iringa walilipwa fidia zao baada ya muda mrefu sana kufanyiwa tathmini.

(a) Je, sheria inasemaje?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuwapatia nyongeza ya fidia zao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa mwongozo wa uthamini wa fidia wa mwaka 2016 na Kanuni ya Sheria ya Ardhi ya Mwaka 2001, malipo ya fidia yanapaswa kufanyika kwa wakati ndani ya muda wa miezi sita. Endapo hayatafanyika ndani ya muda huo, malipo hayo yanapaswa kulipwa pamoja na riba. Serikali inatambua kuwa waathirika 188 wa Kata ya Igumbilo na Kihesa na makaburi 43 yalihamishwa ili kupisha ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Tumaini – Iringa. Jumla ya shilingi 4,623,369,257.11 zimetumika kulipa fidia waathirika wa mradi huo. Aidha, shilingi 14,550,500 zimetumika kuhamisha makaburi kutoka katika eneo la mradi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itawalipa wananchi riba kwa mujibu wa sheria mara fedha itakapotolewa na Hazina.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Tangu Wilaya ya Kilolo ipate hadhi ya kuwa wilaya mwaka 2002 Serikali haijaweza kujenga ofisi za polisi na nyumba za kuishi yalipo Makao Makuu ya Wilaya:-

Je, ni lini Serikali itajenga ofisi na nyumba hizo za polisi Wilaya ya Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabatti, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Polisi lina jumla ya wilaya 168 za kipolisi na zile za Kiserikali, kati ya hizo 127 zina majengo kwa ajili Ofisi na vituo vya polisi na wilaya 41 zilizobaki hazina majengo kwa ajili ya ofisi na vituo vya polisi wilaya ikiwemo Wilaya ya Kilolo. Hii in atokana na ufinyu wa bajeti ya maendeleo kwa Jeshi la Polisi.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Jeshi la Polisi limejikita kukamilisha miradi iliyokwisha anzishwa huko nyuma, pindi miradi hiyo itakapokuwa imekamilika na hali ya kibajeti itakapokuwa imeimarika Jeshi la Polisi litajikita katika ujenzi wa vituo vya polisi vya wilaya pamoja na nyumba za askari katika wilaya ambzo hazina majengo hayo ikiwemo Wilaya ya Kilolo.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Hospitali ya Mkoa wa Iringa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya madaktari bingwa na hivyo kusababisha madaktari hao kuishi mbali na hospitali:-

Je, ni nini mkakati wa Serikali kutatua changamoto hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ina madaktari 26 kati ya hao, madaktari wanne ni madaktari bingwa. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, hospitali ilitenga kiasi cha Sh.40,000,000 kwa ajili ya kuwapa motisha madaktari wa kulipia gharama za nyumba kila mwezi kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ya ndani na fedha kutoka Serikali Kuu kwa maana ya OC. Hadi kufikia mwezi Mei, 2019 kiasi cha Sh.25,500,000 kimelipwa kwa ajili ya malipo ya kodi ya nyumba zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kutolea huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kutenga fedha kwa ajili ya motisha ya watumishi.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je Serikali inatumia sheria gani kuwahamisha wakulima kwenye maeneo ya mijini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji, Na.8 ya mwaka 2017 na Sheria ya Ardhi, Na.4 ya mwaka 1999, Serikali haihamishi wakulima kwenye maeneo ya mijini badala yake inazuia wananchi kujihusisha na shughuli za kilimo cha mazao marefu katika maeneo hayo. Aidha, mazao mafupi kama kilimo cha mazao ya mikunde yanaruhusiwa kulimwa maeneo ya mijini kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Mkoa wa Iringa mashine ya CT-Scan?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa huduma za kibingwa za vipimo vya mionzi kwa kutumia CT-Scan. Katika kuzingatia umuhimu huu tayari ilishakamilisha kufunga mashine hizi kwenye Hospitali za Kibingwa Taifa, kanda na Hospitali mbili za Rufaa za Mikoa zilipata mashine hizi mnamo Desemba, 2020 ambazo ni Mwananyamala na Sekou Toure.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, Serikali inaendelea kuziwezesha hospitali zingine zote za Rufaa za Mikoa ikiwemo Iringa kufunga mashine hizi kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha za utekelezaji wa mpango huu.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, ni lini utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) utaanza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum Iringa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Kuendeleza Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) tayari umeanza kutekelezwa tangu mwaka 2017. Mradi huu unatekelezwa kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia katika maeneo ya kipaumbele zikiwemo Hifadhi nne za Taifa ambazo ni Hifadhi ya Taifa Ruaha, Mikumi, Nyerere, Milima Udzungwa na maeneo yanayozunguka hifadhi hizo pamoja na eneo la chanzo cha maji cha Mto Great Ruaha. Mradi huu unatekelezwa kwa kipindi cha miaka sita kuanzia mwaka 2017 - 2023.

Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi 2021, mradi huu umeendelea kutekelezwa kwa ufanisi mkubwa ambapo kazi zifuatazo zimetekelezwa: ununuzi wa vifaa vya doria vimeshanunuliwa, magari 44 yameshanunuliwa, mitambo mikubwa mitatu kati ya 18 inayotarajiwa kununuliwa, pia mradi umeajiri kampuni sita ambazo zinaendelea na usanifu wa majengo, barabara na viwanja vya ndege.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kutokana na changamoto mbalimbali kama vile majadiliano ya utekelezaji wa mradi huu katika eneo la Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, mradi ulichelewa kuanza utekelezaji wake kwa takribani miezi 17.

Aidha, uwepo wa ugonjwa wa Covid – 19 umechangia kwa kiasi kikubwa kuendelea kuchelewesha utekelezaji wa mradi huu. Kutokana na kazi nyingi kusimama, mradi huu sasa umeshaanza kutekelezwa.

Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto zote ambazo zilijitokeza, mradi umefanyiwa mapitio ya kati ambapo miongoni mwa mambo mengine ni kuongeza muda wa utekelezaji wa mradi huu hadi mwaka 2025 ili kufidia muda uliopotea.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanaume, akina mama na watoto katika Hospitali ya Wilaya ya Frelimo katika Manispaa ya Iringa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Iringa (Frelimo) imeanza kufanya kazi kama Hospitali ya Halmashauri mwezi Februari, 2012 na kusajiliwa rasmi mwaka 2013. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Manispaa ya Iringa shilingi milioni 400 kwa ajili ya upanuzi wa hospitali ambapo jengo la maabara na jengo la mionzi yalijengwa na kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, miundombinu iliyopo katika Hospitali ya Frelimo ni pamoja na jengo la utawala, jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma za maabara, jengo la huduma za mionzi, jengo la kufualia na jengo la huduma za afya ya uzazi na mtoto. Miundombinu inayokosekana katika hospitali hii ni pamoja na jengo la upasuaji, wodi za kulaza wagonjwa, jengo la kuhifadhi maiti na jengo la kutunzia dawa. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya watoto, wodi ya wanaume na wodi ya wanawake magonjwa mchanganyiko (medical ward).
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je ni chombo gani kinasaidia abiria kupata haki yake pindi abiria anapopata ajali safarini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge Wa Viti Maalumu kutoka Iringa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu au watu wanaopata ajali au madhara kutokana na chombo cha moto ambacho fidia yake inasimamiwa na Sheria ya Bima wanapaswa kulipwa fidia ya madhara waliyoyapata ama kwa kuumia au kifo kutoka kwenye kampuni ya bima ambayo chombo hicho cha moto kimekatia bima yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ajali kutokea tukio hukaguliwa na Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani na wahanga wa ajali hupatiwa fomu ya matibabu. Taarifa ya ajali fomu hii hupelekwa ofisi za bima husika na kwa mmiliki wa chombo cha moto kilichopata ajali. Kisha shauri la ajali hupelekwa mahakamani na kesi ikimalizika fomu namba 115 hutolewa kuonyesha matokeo ya kesi (Final Case Report). Ndipo wahanga wa ajali au ndugu huchukua nyaraka za ramani ya tukio la ajali, fomu ya matibabu, fomu ya taarifa ya ajali, fomu ya matokeo ya kesi, fomu ya ukaguzi wa chombo kilichofanya ajali, taarifa ya uchunguzi wa marehemu, kama mhanga amefariki na nakala ya bima ya gari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyaraka zote hizo hupelekwa kwenye kampuni ya bima ambayo chombo cha moto kilichohusika na ajali kimekatia bima yake na wahanga hufidiwa kutokana na ukubwa wa madhara waliyoyapata. Kwa ufupi Jeshi la Polisi linathibitisha kutokea kwa ajali, Mahakama inatafsiri sheria kuhusu tukio, Daktari anathibitisha madhara waliyopata wahanga na kampuni ya bima inalipa fidia. Ninakushukuru.
MHE. DKT. RITHA E. KABATI aliuliza: -

(a) Je Serikali inayo database ya kutambua idadi ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi?

(b) Je nini mchango wa Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania katika kipindi cha miaka mitano?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitumia mifumo mbalimbali ya kutambua Watanzania wanaoishi nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na usajili wao kupitia Balozi zetu na Idara ya Uhamiaji kwa kutumia usajili wa hati za kusafiria za kielektroniki. Hadi kufikia Januari, 2021 idadi ya Watanzania wapatao Milioni moja na Laki Mbili (1,200,000) wanaishi nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania wamekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu. Kwa mfano katika kipindi cha miaka mitano iliyopita michango yao imehusisha sekta mbali mbali zikiwemo; Sekta ya Fedha, Sekta ya Afya na Sekta ya Nyumba. Mfano, takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonesha fedha za kigeni (remittance) ambazo zimetumwa kupitia mfumo rasmi kutoka kwa Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano ni takriban Dola za Kimarekani bilioni 2.3 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 5.3.

Mheshimiwa Spika, aidha, michango ya Watanzania wanaoishi nje ya nchi katika Sekta ya Afya kwa kipindi cha miaka mitano inahusisha utoaji wa vifaa tiba, madawa, vitabu vya masuala mbalimbali ya afya na mafunzo ya elimu ya afya bora kwa wauguzi na madaktari kwenye hospitali za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Sekta ya Nyumba Watanzania wanaoishi nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano wamenunua nyumba zaidi ya 135 zenye thamani ya shilingi za Tanzania bilioni 29.7 kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC). Ahsante sana.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuhamisha Gereza la Mkoa wa Iringa ili kuondoa muingiliano uliopo kati ya Gereza hilo na Hospitali ya Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali bado ina mpango wa kuhamisha Gereza hilo kwani eneo kwa ajili ya kuhamishia Gereza hilo, lilishapatikana maeneo ya Mlolo na Mbunge anafahamu jambo hilo. Kwa kuanzia Jeshi la Magereza lilishafungua kambi ijulikanayo kwa jina la Kambi ya Mlolo. Katika kambi hii zimejengwa nyumba 20 za watumishi na mabweni manne, kwa kutumia bajeti kidogo iliyokuwa inatengwa na Serikali kupitia vyanzo vya ndani vya Jeshi.

Mheshimiwa Spika, changamoto kubwa iliyokuwepo ni ufinyu wa bajeti hali inayopelekea kushindwa kutekeleza mpango huu. Aidha, kwa sasa gharama za ujenzi wa Gereza hilo zimeshaanza kupitiwa upya ili ziweze kuwekwa katika Mpango wa Maendeleo kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kutoa pongezi nyingi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kwa juhudi zake kupitia Mkuu wa Magereza wa Mkoa ambapo amekuwa mstari wa mbele kufuatilia maendeleo ya mpango huu. Aidha, natoa rai kwa wadau mbalimbali wa maendeleo waweze kujitokeza kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa mpango huu. Nashukuru. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni maeneo gani yametambuliwa kuwa na madini Mkoani Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati (Mbunge wa Viti Maalum) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia Taasisi yake ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), ilifanya utafiti wa awali na kuanisha madini yanayopatikana katika Mkoa wa Iringa. Miongoni mwa madini yanayopatikana katika Mkoa wa Iringa ni dhahabu katika Kata za Sadani, Ikweha, Malengamakali, Mlolo, Ifunda, Kalenga, Idodi na Pawaga; shaba katika kata za Mahenge, Kiwele, Pawaga, Nyang’oro, Malengamakali na Kihongota; madini viwanda aina ya chokaa katika Kata za Kiwele, Idodi, Inyigo, Ifunda na Kihongota; udongo wa mfinyanzi (ball clay) katika Kata za Ifunda na Rungemba; kaolin katika Kata za Mbalamaziwa, Nyanyembe, Nyololo na Ifunda; kyanite katika Kata ya Mlowa; bauxite katika Kata ya Rungemba; chuma katika Kata ya Mawindi; na vito katika Kata za Isimani, Idodi na Kiwele.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italeta sheria ya wamiliki wa vyombo vya usafiri kuwa na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Ritta Kabati, Mbunge wa viti maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2019, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) na kuweka kifungu katika Sheria hiyo kinachozingatia uwepo wa miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kifungu cha 6(e) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 413, kimeeleza kuwa moja ya Majukumu ya LATRA ni kuhakikisha uwepo wa huduma ya usafiri wa umma unaoweza kutumiwa na watu wote wakiwemo watu wenye vipato vya chini, waishio vijijini, na watu wenye mahitaji maalum ambayo inajumuisha watu wenye ulemavu. Aidha, Kifungu cha 5(c) (i) na (ii) kimeeleza kuwa moja ya Kazi za LATRA ni kuweka viwango vya bidhaa na huduma pamoja na vigezo na masharti ya utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, itakumbukwa kuwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, Kifungu cha 5(1) na (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini Sura ya 415 kilirekebishwa kwa kuiondolea LATRA jukumu la kuweka viwango vya bidhaa na huduma zinazodhibitiwa. Jukumu hilo kwa sasa linatekelezwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ambalo ndilo lenye dhamana ya kuweka viwango vya bidhaa na huduma mbalimbali nchini. LATRA imebaki na jukumu la kusimamia utekelezaji wa viwango na kuweka masharti na vigezo vya bidhaa na huduma zinazodhibitiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naielekeza LATRA ishirikiane na TBS katika kuweka na kusimamia utekelezaji wa viwango vya vyombo vya usafiri wa umma ili viwe na miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kutatua changamoto zinazokabili Miradi ya Umwagiliaji ya Mkoga na Kitwiru iliyopo Manispaa ya Iringa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Miradi ya umwagiliaji ya Cherehani Mkoga yenye hekta 750 na Kitwiru yenye hekta 100 iliyopo katika Manispaa ya Iringa inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uchakavu wa miundombinu ya umwagiliaji iliyojengwa muda mrefu; kutokamilika kwa miundombinu, pamoja na miundombinu kuharibiwa na mafuriko.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo kwa ajili ya kukamilisha miradi ya umwagiliaji mbalimbali ikiwemo miradi ya Mkoga na Kitwiru.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za madaktari wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imejenga nyumba 50 za watumishi zenye thamani ya shilingi bilioni 3.4 katika Hospitali za Kanda na Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwemo nyumba moja katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mashauriano yanaendelea ndani ya Serikali ili kukamilisha mchakato wa kuhamisha gereza la mkoa ili kutoa nafasi ambayo itawezesha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuendelea na upanuzi wa huduma mbalimbali ikiwemo ni pamoja na ujenzi wa nyumba za Madaktari.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kuzuia mmomonyoko wa barabara ya Dodoma – Iringa katika Mlima wa Nyang’oro?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa ujenzi na uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka 2022/2023, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 250 kwa ajili ya kazi ya kufanya uchunguzi wa miamba na udongo unaomomonyoka katika eneo la Nyang’oro katika Barabara ya Dodoma kwenda Iringa ili kujua tabia za miamba na udongo huo na kuja na mapendekezo ya kitaalam ya jinsi ya kuzuia kumomonyoka huo. Tathmini za zabuni ya kumpata mshauri (consultant) wa kufanya kazi hiyo iko hatua za mwisho na Mkataba utakuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2023. Baada ya taarifa ya kitaalam kutolewa, Serikali itatenga fedha za kutekeleza mapendekezo ya kuzuia mmomonyoko huo, ahsante.
MHE. MINZA S. MJIKA K.n.y. MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga kituo cha afya katika Kata ya Ihanu – Mufindi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni moja ambapo shilingi milioni 500 ni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Mgololo, shilingi milioni 150 ni kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha upasuaji kwenye Kituo cha Afya Mbalamaziwa na shilingi milioni 350 ujenzi wa Kituo cha Afya Mdabulo. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 halmashauri kupitia mapato ya ndani imetenga shilingi milioni 562 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la OPD Kituo cha Afya Ihalimba na shilingi milioni 120 ukamilishaji wa jengo la OPD Kituo cha Afya Mapanda.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya Afya kwenye kata za kimkakati kote nchini kikiwemo Kituo cha Afya Ihanu.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-

Je, lini Mradi wa Umwagiliaji wa Kata ya Ikweha uliopo Jimbo la Mufindi Kaskazini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagiliaji Ikweha ni miongoni mwa skimu zilizoko katika Wilaya ya Mufindi yenye ukubwa wa hekta 500. Skimu hii ina mchango mkubwa katika kuboresha Maisha ya wananchi katika Wilaya ya Mufindi.

Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kupata gharama za kukamilisha ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Ikweha.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, utaratibu gani unatumika kutangaza ajira nchini ili kuhakikisha Watanzania wote wanapata haki ya kupata taarifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, swali namba 722, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sera ya Menejimenti ya Ajira Toleo Na. 2 la mwaka 2008, Sura ya Nne, Aya ya 4(2) ikisomwa pamoja na ya Kanuni 12(1) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2022, nafasi za ajira katika Utumishi wa Umma ni za ushindani na zinazingatia sifa, taaluma, uwazi na usawa.

Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, matangazo ya ajira kwa ajili ya kujaza nafasi wazi ndani ya Utumishi wa Umma hutolewa kupitia tovuti za taasisi husika, mitandao ya jamii, magazeti na mbao za matangazo katika ofisi husika. Maombi ya nafasi hizi hudumu kwa muda wa siku kumi na nne 14 kwa kada za masharti ya kawaida na siku 21 kwa waombaji wa nafasi za Watendaji Wakuu na nafasi za Uongozi za Taasisi za Kimkakati.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -

Je, Serikali inawasaidiaje wakulima wa parachichi Iringa ili waweze kulima kilimo chenye tija?
WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwawezesha wakulima wa parachichi Mkoani Iringa na kwa nchi nzima, Serikali inachukua hatua zifuatazo: -

(i) Kuzalisha miche milioni 20 kwa kushirikiana na sekta binafsi na kuziuza kwa njia ya ruzuku;

(ii) Kufanya utaratibu wa usajili wa wazalishaji wa miche;

(iii) Kuandaa mwongozo wa kusimamia soko la parachichi na kuandaa mfumo wa madaraja;

(iv) Serikali kujenga vituo vya kuhifadhia parachichi la kuchakata na kuhifadhi (common use facility) katika mikoa mitatu kwa maana ya Dar es Salaam, Kilimanjaro - Wilaya ya Hai na Iringa - Wilaya ya Mufindi, Kijiji cha Nyororo).