Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Ritta Enespher Kabati (4 total)

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri Mkuu, hakuna Serikali yoyote duniani ambayo haitozi kodi. Ni lazima tulipe kodi ili tupate madawa, watoto wasome, tupate maji na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi kirefu sana, wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika kunyanyaswa na baadhi ya Maafisa wa Kodi na wengine wakikadiriwa kodi isiyostahili na mbaya zaidi kuna wazabuni ambao wanaidai Serikali yetu. Je, nini kauli ya Serikali kwa jambo hili?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabati, Mbunge wa Iringa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nikiri kwamba nimepata malalamiko na baadhi ya wafanyabiashara katika maeneo mbalimbali. Mimi nimekuwepo kwenye ziara ya kawaida Mkoani Mbeya na kwenye kikao changu na wafanyabiashara, wamewahi kueleza matatizo yanayowapata chini ya chombo chetu cha TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wao niliwahakikishia, naomba nirudie tena kwamba Serikali hii inaheshimu na kuwathamini wafanyabiashara wote, wawekezaji wote na wadau wote walipa kodi ndani ya nchi hii, kwa sababu maendeleo yetu katika nchi yataletwa na sekta ya wafanyabiashara na wawekezaji wakiwa ndio walipa kodi wakubwa, wazuri nchini na uchumi wetu unategemea sana kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo ndani ya chombo chetu cha TRA, tumeendelea kufanya vikao nao, kuwasisitiza na kuwataka wafuate kanuni na taratibu za ukusanyaji wa kodi na kuwasisitiza watumie lugha zenye busara pale wanapotakiwa kwenda kuonana na mfanyabiashara kuzungumzia jambo lolote au kukusanya kodi wanapofika kwenye duka lake au sehemu yake ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nataka niwasihi wafanyabiashara, popote ambako unadhani hutajendewa haki na mtumishi wa TRA; TRA yetu inacho chombo cha nidhamu na maadili cha TRA ambacho kinapokea malalamiko mbalimbali dhidi ya watumishi ambao hawafuati kanuni na hawana maadili katika kutekeleza jukumu lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, mfanyabiashara yeyote, mwekezaji yeyote, mlipa kodi yeyote ambaye pia atakuwa na malalamiko yoyote yale, bado anayo nafasi ya kwenda kwenye chombo chochote cha usalama kutoa taarifa ya jambo ambalo limemkwaza ili pia tuweze kutafuta dawa sahihi ya baadhi ya watumishi ambao hawafanyi kazi yao vizuri kwenye chombo chetu cha TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudie tena kuwahakikishia wafanyabiashara, wawekezaji na walipa kodi wote, Serikali hii itaendelea kuwapa ushirikiano wa dhati. Serikali hii ambayo sasa tunahitaji kupanua Sekta za Biashara itaendelea kuwaunga mkono kwenye jitihada zenu za kibiashara ili tuweze kupata mafanikio ya maendeleo na kuinua uchumi wetu katika Taifa letu. Ahsante sana.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Waziri Mkuu hivi karibuni Serikali imetoa tamko la kutosafirisha chakula nje ya nchi, lakini kuna baadhi ya mikoa ambayo imezalisha chakula cha kutosha cha ziada kinachoweza kusafirishwa hata nje ya nchi. Je, Serikali inatoa ufafanuzi gani kuhusiana na utekelezaji wa tamko hilo?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Iringa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, jambo hili nimelizungumza siku ya Idd Mosi nikiwa kwenye sherehe ya Idd kwenye Baraza la Idd kule Mjini Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Nilizungumza kwa msisitizo kwamba tumedhibiti na tumezuia usafirishaji wa chakula na hasa mahindi nje ya nchi kwa sababu historia yetu sisi kuanzia mwaka wa jana mwezi Novemba, 2016 mpaka Februari, 2017 nchi yetu ilikosa mvua za msimu unaotakiwa na tutapata usumbufu mkubwa ndani ya nchi kwa maeneo mengi kukosa chakula cha kutosha.

Mheshimiwa Spika, na chakula kikuu sasa nchi Tanzania naona utamaduni umebadilika, nilikuwa nazungumza pia na Mheshimiwa Mbatia hapa kwamba utamaduni umebadilika, Wachaga, Wahaya sasa badala ya kula ndizi wanakula ugali. Wamasai waliokuwa wanakula nyama tu pekee sasa wanakula ugali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo utakuta mahindi yanatumika sana kuwa ni chakula kikuu nchini na kwa hiyo lazima tuweke udhibiti wa utokaji wa mahindi ili yaendelee kutusaidia kama chakula kikuu hapa nchini kwetu.

Kwa hiyo tumeweka zuio, na hasa baada ya kuwa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa Kilimanjaro ilitoa taarifa kwamba kuna utokaji wa mahindi mengi kwenda nchi za nje kwenye mipaka yetu. Na siku ile nilipokuwa Kilimanjaro malori kumi yalikamatwa yakiwa na mahindi yakivushwa kwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo lazima tuweke utaratibu na ninyi wote ni mashahidi kwamba uzalishaji huu haukuwa wa uhakika sana kuanzia mwezi Machi mpaka mwezi Mei, kwa miezi mitatu. Maeneo machache yamezalisha sana kama ulivyosema Mheshimiwa Ritta Kabati lakini maeneo mengine hayana chakula. Juzi nilikuwa Mwanza nikiwa pale Usagara, Kigongo Ferry nilisimamishwa na wananchi, moja kati ya tatizo walilolieza ni upungufu wa chakula. Nimeona, hata Sengerema mahindi yote yamekauka, Geita mahindi yote yamelimwa yamekauka. Kwa hiyo, bado tuna tatizo la upungufu wa chakula. Pia bei za chakula chetu iko juu sana hatuna namna nyingine ni kudhibiti chakula chetu.

Mheshimiwa Spika, na nilieleza kwamba nchi nyingi za jirani hazina chakula. Sisi tuna barua hapa kutoka Congo, South Sudan tumepata kutoka Somalia na nchi za jirani wanaomba kupewa msaada wa chakula kutoka Tanzania wakati sisi wenyewe hatuna chakula cha kutosha. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa Serikali na wananchi mkatuunga mkono katika hili, kudhibiti utokaji wa chakula, na hasa mahindi yanayokwenda nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, nimeeleza kwamba sisi tulichofanya ni kudhibiti kutoa mahindi nje bila kibali. Na kama kuna umuhimu wa kupeleka mahindi nje basi tunataka yasagwe ndani ili yapelekwe, kwa sababu ukisaga tunafaida zake, pumba tunazipata, tunazitumia kwa chakula cha mifugo lakini pia mashine zetu ambako tuna msizitizo wa viwanda vitafanya kazi ya kusaga, tutakuwa na ajira, lakini tunapotoa mahindi maana yake tunatoa kila kitu huku ndani tunakuacha tupu. Kwa hiyo, lazima tuwe na mpango ambao utasaidia sasa, sisi wenyewe Watanzania kunufaika kupitia zao hili.

Mheshimiwa Spika, bado msimamo ni ule ule kwamba tumezuia mahindi kutoka nje ya nchi na kama ni lazima basi aende Wizara ya Kilimo akaombe kibali kama ni lazima Wizara ikiona inafaa utapata kibali, lakini kibali hicho ni cha kutoa unga na si mahindi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wote ni mashahidi, jana tumepata taarifa malori zaidi ya 103 kwa siku nne kutoka siku ya Idd mpaka leo hii, malori 103. Je, kwa mwezi mzima tutakuta na mahindi hapa ndani?

Mheshimiwa Spika, tunazo taarifa kupita Kamati za Ulinzi na Usalama kwamba wengi wanaofanya biashara kuja kuchukua mahindi Simanjiro, Kibaya kwa maana ya hapa katikati maeneo ya Kongwa ni watu kutoka nje ya nchi ndio wanaokuja kuchukua. Kwa hiyo hatuna faida sana hao kuingia zaidi ya kwamba wanatuachia fedha. Hivyo tunaitengeneza shida ambayo tutakuja kuanza kuuliza tutapateje chakula ndani ya nchi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Watanzania kwa jambo hili naomba mtuunge mkono kwa sababu tunachofanya ni kwa maslahi ya nchi, hatimaye bei zitapanda tutashindwa kununua mahindi na wote mnajua angalau sasa mahindi yamepungua kwenye masoko

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuendelee na hali hiyo ili chakula kiwe cha kutosha baada ya kuwa tumefanya tathimini tukijiridhisha kwamba chakula cha ndani cha kutosha kipo na tuna akiba kutoka kwenye maeneo yanayozalisha sana basi vibali hivyo vinavyotolewa kwa utaratibu vitaendelea kutoka, na wale ambao wanataka kufanya biashara nje ya nchi wataendelea kupata fursa ya kufanya biashara nje ya nchi. Lakini kwa sasa tumezuia; na ninataka nimpongeze sana Mkuu wa Mkoa ya Kilimanjaro mama Anna Mghwira na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama kwa kuendelea kusimamia.

Mheshimiwa Spika, tumeona malori yale agizo limebaki pale pale, mahindi yale ambayo yatakuwa yamaekamatwa; na tumejihisi kwamba yalikuwa yamekwenda nje ya nchi, yote yataingizwa kwenye hifadhi ya taifa, na hayo malori yanyofanya biashara hiyo yote yatabaki kituo cha polisi. Lakini pia kwa namna ambavyo wanaendelea na waendelee kwa utaratibu wote na maagizo yetu yatabaki vilevile ili tuweze kuwahudumia Watanzania ndani ya nchi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu imeendelea kutoa matumaini makubwa kabisa kwa wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini. Hivi karibuni tumeona mfanyabiashara mkubwa kama Dangote amejenga imani na kuahidi kuwekeza zaidi hapa nchini lakini kumekuwa na changamoto nyingi sana katika kuwekeza hapa nchini. Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa hivi inatengeneza sheria bora na kujenga mazingira mazuri kwa ajili ya kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza zaidi hapa nchini kwetu? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kabati, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge ameomba kujua mkakati wa Serikali na maboresho yake kwenye uwekezaji. Watanzania wote mtakiri kwamba Serikali yetu imeweka msisitizo wa kuhakikisha kwamba tunapanua wigo unaowawezesha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini kwa sababu fursa, malighafi na labor tunazo za kutosha. Sisi tunavutia uwekezaji kwa sababu maeneo mengi ya uwekezaji pia yanapunguza changamoto yetu ya ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo, mfanyabiashara Dangote aliyekuja ambaye amewekeza kwenye kiwanda cha saruji Mkoani Mtwara ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini ambao pia tumetoa fursa za kupanua wigo wa uwekezaji wake.

Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kupanua wigo wa uwekezaji? Kwanza tunafanya maboresho ya sheria na kanuni zetu kwenye uwekezaji ili kujenga mazingira mazuri wezeshi ya uwekezaji nchini ili kila mwekezaji anayekuja kuwekeza apate huduma hiyo kwa ukaribu. Tumeanzisha taasisi inaitwa Tanzania Investment Center ambapo mwekezaji atapata huduma zote kupitia taasisi hiyo tunaita One Stop Center na tunaweza kumpa ardhi na aina yoyote ya msaada ambao anauhitaji katika uwekezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Tanzania ya leo hatuna shida ya ardhi, ardhi tunayo, umeme upo wa kutosha, maji tunayo, barabara zetu nzuri na mazingira ya uwekezaji Tanzania sasa ni mazuri. Sheria hizi ambazo tunaendelea kuzirekebisha na kuzifanya kuwa sheria wekezi zitasaidia sana wawekezaji kuja nchini kama ambavyo tunaona sasa kasi ya wawekezaji kuja kwenye maeneo haya imeongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wawekezaji wote mliopo ndani ya nchi na walio nje ya nchi kuja Tanzania kuwekeza kwa sababu mazingira ya uwekezaji yanaendelea kuboreshwa. Sasa hivi tunakaribia kuweka ile sheria ambayo imekusanya changamoto nyingi ambazo zilikuwa zinawakwaza wawekezaji na mengine ni ya kisheria kwa hiyo tunafanya maboresho ya sheria ili kuondoa vikwazo vya uwekezaji Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tunataka tuainishe huduma ambazo sisi tunazitoa au fursa zilizopo Tanzania ili kuhakikisha kwamba tunafanya wawekezaji kuwa na imani nasi. Wiki iliyopita nilikuwa Mkoani Mara kwenye mkakati wa kutangaza vivutio vya uwekezaji. Huu ni mwendelezo wa kutangaza fursa za mikoa yote nchini ambapo mpaka sasa tumeshafika mikoa 24 kuhakikisha kwamba tunawaonesha wawekezaji nini kipo kwenye mkoa huo ili kila mmoja aamue kwenda mahali anapotaka. Tuna malighafi nyingi sana zinazogusa kwenye sekta ya kilimo, madini na maliasili, hizi zote pia zinasaidia uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunaendelea kufanya maboresho haya mara kwa mara ya kupitia changamoto tulizonazo na tunaziingiza kwenye sheria ili tuwe na sheria endelevu ambayo pia inaweza kutusaidia kuwekeza. Yale yote ambayo yanajitokeza kwa sasa tunayachukua, tunayafanyia utaratibu wa kuyaboresha hivyo na kurahisisha uwekezaji huo kwa yeyote anayetaka kuwekeza hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hili suala la vibali vya kazi tumeendelea kufanya maboresho ili wawekezaji sasa wawe na uhakika wa kuleta watu wao kuja kuwekeza hapa na mambo mengi ya uwekezaji ambayo yapo kwenye kile kitabu kinaitwa Blue Print ambacho kina maelekezo yote ya uwekezaji. Niendelee kuwahakikishia Watanzania fursa tulizonazo zitatusaidia pia sana kunufaisha Taifa letu.

Kwanza mwekezaji akija tutapata kodi lakini mbili ushiriki wa Watanzania, tatu ajira lakini nne malighafi na mazao tunayoyalima pia yanapata soko. Kwa hiyo, jambo hili kwa ujumla wake lina faida kubwa na sisi tunalisimamia kuwa linaleta tija kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kulijibu kwa upana huo ili wawekezaji wote wanaotaka kuja nchini waje kuwekeza na sisi tunawakaribisha. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mheshimiwa Waziri Mkuu, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki kutumia gesi asilia. Kwa sasa takwimu zinaonesha zaidi ya magari 2000 yameanza kutumia gesi hiyo.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kusambaza huduma hii nchi nzima ili wananchi waweze kufaidika na gesi yetu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge Mkoa wa Iringa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunayo gesi asilia nchini na ni kweli tumeanza kuitumia kwenye maeneo mbalimbali. Kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amesema tunatumia kwenye magari lakini gesi hii tunaipeleka viwandani na tunao mpango wa kupeleka gesi hii majumbani.

Mheshimiwa Spika, wizara yetu ya Nisjhati imeweka utaratibu mzuri wa kupanua wigo wa matumizi ya gesi hii. Sasa hivi tunakamilisha ujenzi wa kituo cha kukusanyia gesi hii kutoka kule Mtwara - Songosongo pale Jijini Dar es Salaam ili sasa tuweke utaratibu mzuri wa kusambaza gesi hiyo iende kwa matumizi hayo tuliyoyasema.

Mheshimiwa Spika, pia tumeshirikisha sekta binafsi baada ya kuona uwezo wetu Serikali peke yetu hatutamudu kuifikisha gesi hii kwa wananchi. Pamoja na uwezo tulio nao tukiunganisha nguvu na sekta binafsi tunaamini tutawafikia kwenye matumizi haya. Iwe ni kupeleka viwandani, majumbani hata kwenye matumizi mengineyo ikiwemo na hayo magari.

Mheshimiwa Spika, tayari zabuni zimekwisha tangazwa na watu wengi wameomba. Sasa hivi wako wachache ambao wameruhusiwa kutekeleza mfumo huo na wengine mchakato unaendelea na bado tumefungua fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika mchakato wa usambazaji wa gesi.

Mheshimiwa Spika, nchi yetu tumeigawa kwenye zone ambazo tutalaza mabomba kuelekea huko. Tutakwenda na bomba la kwenda Kaskazini kwa mikoa ya Kaskazini, tutakuwa na bomba linalopita Kanda ya Kati mpaka Magharibi ili kufikia mikoa ya hapa kati na tutaweka bomba kule kule Kusini ambako inatoka gesi hii kwa ajili ya mikoa ya Kusini. Lengo ni kuifikia kwa ukaribu na kwa haraka, mikoa, wilaya na kama uwezo utakuwa mzuri na sekta binafsi ikiingia ikiwekeza zaidi tunataka tufike vijijini ili wananchi walioko vijijini nao wanufaike na hii gesi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo basi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imejipanga vizuri kwenye eneo hili na ninaamini kupitia bajeti hii Wizara ya Nishati itakapokuja hapa itatoa ufafanuzi zaidi kwenye eneo hili. Pia nimwagize Mheshimiwa Waziri, sasa moja kati ya maelezo ambayo tutahitaji kwenye Bunge hili iwe ni namna ambavyo gesi itawafikia watanzania kwenye maeneo yao. Ahsante sana. (Makofi)