Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Anna Richard Lupembe (27 total)

MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Ujenzi wa barabara ya Sumbawanga hadi Mpanda bado haujakamilika.

Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utakamilika?
NAIBU WAZIRI UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Lupembe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya kutoka Sumbawanga hadi Mpanda umegawanyika katika sehemu nne ambazo ni Sumbawanga – Kanazi km 75, Kanazi – Kizi – Kibaoni km 76.6, Kibaoni – Sitalike km 72 na Sitalike – Mpanda km 36.

Mheshimiwa Spika, maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya Sumbawanga – Kanazi umefikia asilimia 68.6 na mpaka sasa km 43.47 za lami zimekamilika, maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya Kanazi hadi Kibaoni kupitia Kizi ujenzi umekamilika kwa asilimia 50.3 na mpaka sasa km 23.43 za lami zimekamilika. Maendeleo ya ujenzi wa sehemu ya barabara ya Sitalike – Mpanda ni asilimia 76 na mpaka sasa km 20 za lami zimekamilika. Ujenzi wa sehemu hizo tatu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki ya Kibaoni hadi Sitalike ambayo ni km 7.2 umekamilika na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Kata ya Katumba inakabiliwa na tatizo kubwa la maji linalosababisha akina mama wengi kwenda umbali mrefu kutafuta maji:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufikisha maji katika kata hiyo?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Katumba ilikuwa ni kambi ya wakimbizi chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) hadi mwaka 2014/2015. Huduma za kijamii zikiwemo maji zilikuwa zinatolewa na UNHCR. Ili kutatua tatizo la maji katika kata hii, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kwa kushirikiana na UNHCR imepanga kutekeleza mradi wa maji wa Nduwi Stesheni ili kukidhi mahitaji ya maji kwa wananchi.
Aidha, Halmashauri katika bajeti ya mwaka 2016/2017 imepanga kutenga shilingi milioni 345 ambazo zitatumika kwa ajili ya upanuzi wa mradi huo utakaonufaisha vijiji vya Nduwi Stesheni, Mnyaki A, Mnyaki B, Katumba na Sokoine ambavyo viko katika Kata ya Katumba.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Bandari ya Karema na ina mikakati gani na Bandari hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa awali wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ulikuwa wa kujenga gati dogo kwa ajili ya kuhudumia abiria wanaozunguka eneo la Karema. Hata hivyo, kutokana na mpango wa Serikali wa kuboresha Reli ya Kati ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kaliua – Mpanda – Karema yenye urefu wa kilometa 360 ambayo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea, TPA imelazimika kuboresha mpango wake kwa kujenga bandari badala ya gati ili kukidhi matarajio ya shehena ya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo itakayopitia Bandari hiyo ya Karema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mshauri Mwelekezi atakayefanya upembuzi yakinifu wa mradi huu ambaye anatarajiwa kuanza kazi ifikapo Juni, 2016 na kukamilika mwezi Desemba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongezee kusema kwamba, hiyo kazi imeshaanza. Aidha, baada ya kupokea taarifa ya upembuzi yakinifu, TPA itatangaza zabuni kwa ajili ya kuwapata wajenzi ambapo kazi ya ujenzi wa Bandari ya Karema unatarajiwa kuanza katika mwaka fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Karema wavute subira, kwani Serikali yao imedhamiria kujenga bandari hiyo ambayo itakuwa ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Karema na Taifa kwa ujumla.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE) aliuliza:-
Wanawake wengi wa vijijini hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii huko vijijini lakini pia hawana mafunzo maalum ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kufikia huduma hiyo ya kukopeshwa.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake wa huko waweze kupata mikopo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapa akina mama hao mafunzo maalum yatakayowasaidia katika kujipanga kukopa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mipango ya Serikali kupeleka huduma ya benki kwenye vijiji ili wanawake waweze kupata mikopo, napenda ikumbukwe kwamba kufuatana na mabadiliko ya mfumo wa kifedha nchini unaotekelezwa tangu mwaka 1991, Serikali imejitoa katika kuhusika moja kwa moja na uendeshaji wa shughuli za benki na badala yake Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya utoaji huduma za kibenki ili huduma hizi ziwafikie wananchi wengi. Kupitia Benki Kuu ya Tanzania, Serikali imefanya msukumo wa kuhakikisha kuwa huduma za kibenki zinawafikia wananchi ili kurahisisha shughuli zao mbalimbali za kiuchumi mijini na vijijini. Benki kadhaa zimeanzisha huduma za kibenki kupitia mawakala na huduma za kifedha kupitia simu za mkononi ambazo zimewasaidia sana wananchi sehemu ambako hakuna matawi ya benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Benki Kuu inaendelea kuweka mazingira wezeshi na taratibu rafiki ili kusaidia nguvu za wananchi na sekta binafsi kuanzisha benki au taasisi za fedha. Juhudi hizi zimesaidia wananchi kuanzisha benki za kijamii na taasisi ndogondogo za fedha katika maeneo yao. Ni matarajio ya Serikali kuwa wananchi watatumia fursa ya mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo hapa nchini kuwekeza wao wenyewe au kuzishawishi benki kuanzisha huduma za kibenki katika maeneo yao. Aidha, Serikali pia itaendelea kushawishi benki nchini kupanua shughuli zao ili ziwafikie wananchi wengi hasa wale wa vijijini wakiwemo akina mama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ikishirikiana na Benki Kuu ipo tayari kutoa mafunzo maalum ya elimu ya fedha kwa wananchi wote wakiwemo akina mama. Benki Kuu kupitia Kurugenzi yake ya Utafiti na Uchumi ina mpango wa kuelimisha umma (consumer literacy program) kuhusu utumiaji wa huduma za kifedha nchini ili kuleta uelewa mpana wa upatikanaji wa huduma za kifedha ikiwemo taratibu zinazohusu mikopo.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Wakazi wa Kichangani katika Wilaya ya Mpanda Mjini hawajawahi kupata hati kwa ardhi wanayomiliki:-
Je, ni lini wananchi wa maeneo hayo watapatiwa hati zao hasa ikizingatiwa kuwa zimechukua muda mrefu sana na haijulikani hatma yao ni nini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali Na. 416 la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, umilikishwaji wa viwanja katika eneo la Kichangani katika Wilaya ya Mpanda ulifanyika kwenye maeneo ambayo upimaji wake ulikuwa bado haujakamilika. Ili wananchi hao waweze kupewa hatimiliki taratibu za upimaji wa maeneo hayo zinapaswa kukamilishwa kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu umekuwa ukifanywa na Halmashauri nyingi hapa nchini na ulilenga kupunguza mfumuko wa makazi holela mijini. Hata hivyo, baada ya Wizara yangu kubaini kuwa kuna maeneo mengi nchini ambayo yamemilikishwa bila upimaji wake kukamilika hivyo kuwakosesha haki na fursa wananchi kupata hati kutokana na upimaji kutokamilika. Wizara yangu imeingilia kati na kuzitaka Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo yote ambayo yako katika demarcation ili upimaji wake ukamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Wizara yangu tayari imetangaza zabuni kwa ajili ya kukamilisha upimaji huo na wazabuni mbalimbali wameshawasilisha zabuni na kufanya kazi hiyo na taratibu za kumpata mzabuni mwenye sifa zinaendelea. Aidha, tunapenda kutoa wito kwa Halmashauri zote nchini ikiwemo Wilaya ya Mpanda kutenga fedha kwa ajili ya kukamilisha upimaji ambao haujakamilika katika maeneo yao yote ambayo yataguswa katika mpango huu wa Wizara.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Wananchi waliojenga nyumba katika maeneo ambayo hayajapimwa wanapopata kesi hasa kwenye Mahakama ya Wilaya wanatakiwa kutoa Hati au Ofa lakini kwa kukosa nyaraka hizo ndugu au jamaa wanakosa kudhaminiwa:-
Je, Serikali haioni kuwa iko haja ya kupandisha thamani ya makazi ya wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali namba 52 la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli maeneo mengi katika majiji na miji takribani asilimia 70 ya wakazi wake hayana miliki salama na kwa hali hiyo kukosa uhalali wa kutumika kama dhamana kuwadhamini ndugu zao pale wanapokuwa na mashauri katika Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa ardhi kama rasilimali inayoweza kuwasaidia wanyonge kujikwamua kiuchumi na kutumika kama dhamana katika mashauri ya Mahakama na shughuli nyingine za kiuchumi, Wizara yangu imefanya mambo yafuatayo:-
(i) Kuandaa program ya Kitaifa ya miaka mitano (2015 – 2020) ya kurasimisha makazi yaliyojengwa kiholela na kutoa hati miliki kwa wamiliki wake. Awamu ya kwanza ya urasimishaji wa makazi ambayo imeanza katika Kata za Kimara na Saranga katika Jiji la Dar es Salaam ambapo nyumba au viwanja 6,000 vitapimwa na kumilikishwa kwa wananchi katika kipindi cha miezi sita kuanzia Juni mpaka Disemba, 2016. Awamu ya pili itahusisha upimaji na umilikishaji wa nyumba au viwanja katika Manispaa tano za Jiji la Dar es Salaam za Kinondoni, Ilala, Temeke, Ubungo na Kigamboni) ambapo viwanja 299,000 vitapimwa.
(ii) Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri za Musoma, Tabora, Singida, Kigoma, Ujiji, Sumbawanga na Lindi mwezi Septemba 2016 imefanya tathmini ya maeneo ya urasimishaji ambapo jumla ya viwanja/nyumba 50,200 zimebainishwa kuweza kurasimishwa katika mwaka wa fedha 2016/2017. Kimsingi zoezi hili ni endelevu kwa nchi nzima na litaendelea pia kulingana na upatikanaji wa rasilimali utakavyokuwa unaruhusu.
(iii) Kuandaa progam ya miaka kumi (2015 – 2020) ya kupanga na kumilikisha kila kipande cha ardhi. Program hii ambayo itaratibiwa na Wizara yangu, itahusisha wadau wengine zikiwemo sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la urasimishaji makazi holela litaongeza thamani ya kila kipande cha ardhi kwa kuwapatia wakazi husika hati miliki baada ya kupanga maeneo yao. Aidha, litaongeza ulinzi wa ardhi na kupunguza migogoro ya ardhi na litarahisisha pia utoaji huduma muhimu za kijamii kwa kuainisha maeneo ya huduma na kuhakikisha huduma muhimu zilizokuwa zinakosekana zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa tumeshaanza kukabidhi hati katika Mkoa wa Morogoro, Mtaa wa Bingwa Kisiwani ambapo hati 28 zimetolewa na Mwanza eneo la Buhongwa hati 18 zimetolewa. Jumla ya hati miliki 46 zimetolewa kufikia tarehe 30/10/2016 ambazo imekuwa chachu kwa wananchi wengi katika maeneo mengine.
MHE. ANNA R. LUPEMBE Aliuliza:-
Wilaya ya Mlele haina Hospitali ya Wilaya. Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Mlele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ni miongoni mwa vipaumbele vinavyowekwa na Halmashauri yenyewe. Kwa sasa Halmashauri ya Wilaya ya Mlele imepanga kuboresha Kituo cha Afya cha Inyonga ili kiweze kutoa huduma zenye hadhi ya Hospitali ya Wilaya katika kipindi cha mpito kabla ya kujenga Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo hicho kwa sasa kina wodi nane zenye uwezo wa kulaza wagonjwa 98 kwa siku, jengo la wagonjwa wa nje, jengo la utawala lenye ofisi sita, stoo ya dawa, chumba cha maabara, chumba maalum cha upasuaji chenye vifaa vyote, mfumo wa maji safi na majitaka katika hospitali na matundu nane ya vyoo vya nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi zinazoendelea ni ujenzi wa jengo la upasuaji ambalo limefikia hatua ya lenta na jengo la kuhifadhia maiti (mortuary) ambalo limefikia hatua za umaliziaji. Ujenzi wa majengo hayo umeshagharimu shilingi milioni 418 na kazi inaendelea.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Kuna maeneo ambayo hayana kabisa mitandao ya mawasiliano huko Mpanda Vijijini hususan kata ya Katuma, Sibwesa, Mwese na maeneo ya Bujumbo, Kapanda pamoja na Wilaya ya Mlele kata ya Ilunde.
Je, ni lini Serikali itawapelekea mawasiliano wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote uliviainisha vijiji vya Kata za Katuma na Sibwesa na kuviingiza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mawasiliano vijijini.
Kata ya Katuma imekwishafikishiwa huduma ya mawasiliano na Kampuni ya Simu ya Vodacom ambapo shughuli za ujenzi wa mnara zilikamilika mwezi Septemba kwa ruzuku ya dola za Kimarekani 236,700.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kijiji cha Sibwesa katika kata ya Sibwesa tayari kimefikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia kampuni ya simu ya Vodacom kwa rukuzu ya dola za Kimarekani 90,411 ambapo utekelezaji wa mradi ulikamilika tarehe 23 Mei, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vijiji vya Ligonesi, Lwesa katika kata ya Mwese vimeshafikishiwa huduma ya mawasiliano kupitia mtandao wa Viettel (Halotel). Ujenzi wa mnara kwa ajili ya vijiji vya Nkungwi na Kabage vilivyoko katika kata ya Sibwesa uko katika hatua za mwisho kukamilika. Kata ya Ilunde yenye vijiji vya Ilunde na Isengenezya pamojana vijiji vya Kasekese vitaingizwa katika orodha ya utekelezaji wa mradi ya siku za usoni.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Kijiji cha Mtisi katika Kata ya Sitalike hakuna eneo la kilimo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa wananchi hao maeneo kwa ajili ya kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Mtisi kilichopo katika Kata Sitalike, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kina eneo la ardhi lenye jumla ya hekta 1,066.86. Kati ya hizo, hekta 1,043.86 ni sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Msaginya unaomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Maana yake ni kwamba, jumla ya kaya 589 zenye wakazi 3,416 wa kijiji hicho wamebakia na eneo la hekta 23 tu wanaloruhusiwa kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mahitaji ya ardhi ya kilimo katika kijiji hicho ni hekta 919.4, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, ifikapo mwishoni mwa Novemba, 2017, itakuwa imewapatia ardhi wakazi hao kutoka katika Kijiji cha Stalike (Makao Makuu ya Kata ya Sitalike) chenye ardhi ya ziada hekta 2,950.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejiwekea mpango mkakati wa kujenga Mahakama katika Mikoa na Wilaya zote nchini kwa awamu. Katika mpango huu, Mahakama ya Mkoa wa Katavi ambalo jengo lake litakuwa pia ni Mahakama ya Wilaya ya Mpanda lilipangwa kujengwa katka mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari ujenzi umekwishakuanza na unatarajia kukamilika kabla ya Juni 2018. Aidha, huu ni moja ya miradi ya ujenzi wa Mahakama inayotekelezwa nchini kwa kutumia teknolojia rahisi na ya kisasa ya moladi.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Polisi Wilaya ya Mlele?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uhitaji wa vituo vya polisi pamoja na nyumba za kuishi askari kote nchini ikiwemo Wilaya ya Mlele. Ili kutatua changamoto hii, Serikali kupitia Jeshi la Polisi inashirikisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wengine wa maendeleo ili kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga vituo vya polisi vya kisasa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ufinyu wa bajeti na uhitaji wa vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini kuwa mkubwa, namwomba Mheshimiwa Mbunge kushiriki katika jitihada hizi kwa kuhamasisha wananchi wake kushiriki katika mpango huu ili kuhakikisha huduma za Kipolisi zinaimarika karika eneo hilo. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA (K.n.y. MHE. MHE.ANNA R. LUPEMBE) aliuliza:-
Je, ni lini Redio Tanzania (TBC) itasikika katika Kata za Ilela na Ilunde Wilayani Mlele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TBC imeendelea na jitihada za kupanua usikivu katika Mikoa na Wilaya ambazo bado hazina usikivu au kuwa na usikivu hafifu wa redio. Katiba bajeti ya mwaka 2016/2017 TBC ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya tano za mpakani mwa nchi. Maeneo ambayo mitambo imefungwa na matangazo ya redio kuwashwa ni Rombo, Nyasa, Tarime, Kibondo na Namanga. Serikali inaendelea na utaratibu huo wa kuongeza usikivu kwenye maeneo yasiyo na usikivu mzuri katika Mikoa ya Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kujenga mitambo ya redio katika Mikoa hii katika bajeti ya mwaka 2019/2020 na katika bajeti ya mwaka 2018/2019 TBC imetengewa kiasi cha shilingi bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa studio za redio na television Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:- Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya Mwese?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 7 Mei, 2018, Serikali ilipeleka jumla ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga chumba cha mionzi (x-ray), nyumba ya mtumishi, maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya mama na mtoto na chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Kituo cha Afya cha Mwese katika Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda. Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2018.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Gereza la Wilaya ya Mlele?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa nchini kuna wilaya 51 ambazo hazina Magereza ya Mahabusu ya Wilaya ikiwemo Wilaya ya Mlele. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Wilaya nchini inakuwa na Gereza la kuhifadhi wahalifu wa wilaya husika. Vilevile ujenzi wa Magereza kwenye kila wilaya utapunguza gharama za kuwasafirisha wahalifu kutoka Wilaya moja kwenda nyingine kusikiliza kesi zao pamoja na kuhakikisha usikilizwaji wa kesi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa Magereza mapya kwa awamu kwenye wilaya zisizokuwa na Magereza. Hivyo, ni lengo la Serikali kuendelea na ujenzi huo kwenye Wilaya zote zisizokuwa na Magereza ikiwemo Wilaya ya Mlele kadri hali ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakarabati Shule ya Sekondari ya Mpanda Girls?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kufanya ukarabati wa Shule za Sekondari Kongwe nchini kwa awamu kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha. Katika Awamu ya kwanza, Serikali imekarabati shule za sekondari 53 kwa gharama ya shilingi bilioni 53.6 ikijumuisha ujenzi wa Shule za Sekondari za Nyakato na Ihungo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Awamu ya pili Serikali imepanga kukarabati shule 17 kongwe za Sekondari nchini ikiwemo Shule ya Sekondari ya Wasichana Mpanda. Jumla ya shilingi bilioni 16 zimetengwa kukarabati shule hizo. Miongoni mwa fedha hizo shilingi milioni 986 zimetengwa kwa ajili ya Shule ya Wasichana ya Mpanda. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa Gridi ya Taifa Mkoani Katavi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri na Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dada yangu Anna Richard Lupembe Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) inatekeleza Miradi mbalimbali ya kusafirisha umeme itakayohakikisha kuwa Mikoa yote nchini inaunganishwa katika gridi ya Taifa ikiwemo Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa kupitia shirika la umeme nchini (TANESCO) inatekeleza Mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi kupitia Ipole na Inyonga yenye urefu wa kilomita 381 ili kuunganisha Mkoa wa Katavi katika gridi ya Taifa. Kazi hiyo pia itahusisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme wa msongo wa kilovoti 132/33 vya Ipole, Inyonga na Mpanda Mkoani Katavi. Gharama za mradi huu ni Shilingi bilioni 135.3.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarehe 11 Oktoba, 2019 Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huu katika eneo la Orio Mjini Mpanda. Kazi zinazoendelea kwa sasa ni ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Mpanda, Ipole na Inyonga pamoja na upimaji wa njia ya kusafirisha umeme kwa ajili ya tathmini ya mali za wananchi watakaopisha mradi. Kazi za ujenzi wa mradi huu zinatekelezwa kwa kutumia wataalam wa TANESCO kupitia kampuni tanzu ya ETDCO. Mradi huu unatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Mei, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeanza kutekeleza Mradi mkubwa wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kV 400, Iringa - Mbeya – Tunduma - Sumbawanga – Mpanda - Kigoma – Nyakanazi (North West Grid) yenye urefu wa kilomita 1,384. Mradi huu upo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Shughuli za ujenzi wa mradi huu zitaanza mwezi Mei, 2020 na zinatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa Sayansi katika Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2016/2017 hadi 2018/2019, Serikali imeajiri jumla ya watumishi 7,515 katika shule za sekondari nchini. Kati yao, Walimu 7,218 na Fundi Sanifu Maabara 297. Kati ya walimu walioajiriwa walimu wenye mahitaji maalum walikuwa 29, walimu wenye elimu maalum ni 50 na walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ni 7,089 na walimu wa lugha (Literature in English) walikuwa 100.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2016/2017 hadi 2018/2019 Serikali ilipanga jumla ya Watumishi 121 katika shule za sekondari Mkoani Katavi. Kati yaoWalimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati walikuwa 115 na Fundi Sanifu Maabara walikuwa Sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo walimu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANNA R. LUPEMBE Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara za Kata ya Katumba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS - TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo ina mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 420.97 ambazo tayari zimeingizwa katika mfumo wa barabara za Wilaya (DROMAS). Aidha, Kata ya Katumba ina mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 185.88 ambazo ni sawa na asilimia 44 ya mtandao wote.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka wa fedha 2017/ 2018 hadi 2019/2020 Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Nsimbo umetumia kiasi cha shilingi milioni
246.08 kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Msaginya – Kanoge na Ikondamoyo – Kalungu. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 81.2 imetengwa kwa ajili ya matengenezo ya barabara za Msaginya – Kanoge na barabara ya Kituo cha Afya Katumba – Mto Kalungu.

MheshimiwaSpika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara kote nchini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kijiji cha Matandarani Kata ya Sitalike?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza mradi wa maji wa Magula ambao unahusisha ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa kilomita 14.9, ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 200,000 na nyumba ya mtambo wa kusukuma maji. Ujenzi wa mradi umeanza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2021 kwa gharama ya shilingi milioni 545.62. Mradi huo utanufaisha jumla ya vijiji vitatu ambavyo ni Mtisi (Magula), Matandarani na Ibindi.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini wananchi wa Kata ya Ugalla watapatiwa umeme wa REA III?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya kupeleka umeme vijijini kwa nchi nzima kwa kupeleka umeme katika vijiji ambavyo havijafikiwa na umeme.

Mheshimiwa Spika, vijiji tisa vya Jimbo la Nsimbo ambavyo havina umeme ikiwa ni pamoja na Vijiji vya Kata ya Ugalla vya Katambike, Mnyamasi na Kasisi vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu mzunguko wa pili unaoendelea. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Machi, 2021 na unatarajiwa kukamilika Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji hivyo inahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33, urefu wa kilomita 63.6; msongo wa kilovoti 0.4, urefu wa kilomita 3.0; na ufungwaji wa transfoma tatu, pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali zaidi ya 66. Gharama ya mradi ni Shilingi bilioni 2.46.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -

Barabara ya kutoka Ilembo hadi Itenka ni barabara muhimu kiuchumi.

Je, ni lini Serikali itaifanyia ukarabati barabara hii?

Je, ni lini sasa Serikali itaweka hela ya kutosha kuhakikisha barabara hii inakwisha kabisa kwa sasbabu ni barabara hii ya kiuchumi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa sababu kalvati kutokana na mvua nyingi zinazonyesha, makalvati haya yanachukuliwa hatimae inakuwa siyo barabara ya kalvati tena yanakuwa madaraja, na mpaka sasa hivi tunasema tumetengeneza makalvati matano, na najua si muda mrefu makalvati haya yatachukuliwa na mvua.

Je ni lini Serikali sasa itatenga pesa za kutengeneza madaraja, yapo makalvati matano sasa yatatengenezwa madaraja matano, ni lini Serikali itatoa pesa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge Jimbo la Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza alichokuwa anaomba kufahamu ni kwamba lini Serikali itatenga fedha za kutosha katika barabara hiyo ili kuhakikisha inakamilika?

Nimwambie tu kwamba Mheshimiwa Mbunge Serikali tutaendelea kuzingatia hilo ombi alilolisema lakini kwa kadri ya bajeti yetu inavyoendelea kuongezeka ndivyo tunavyoendelea kutenda fedha za kutosha kwa ajili ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ilikuwa lini badala ya kujenga makalavati anataka tujenge madaraja katika eneo husika. Nimwambie tu kwamba sisi tunajenga kulingana na tathmini ambayo inafanywa na wakandarasi wa maeneo husika. Kwa hiyo, kama kutakuwa na hitaji la msingi la kujenga madaraja tutafanya hivyo baada ya kufanya na kupata tathmini ya kina katika barabara hiyo kuhusu hayo makalavati anayoyazungumzia Mheshimwa Mbunge, ahsante sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, na nataka kumpongeza Mheshimiwa Anna Lupembe kwa swali lake zuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, mpango wetu Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa mwaka 2022/2023 ni kujenga madaraja na makalvati yote, kwa hiyo, sasa hivi tumeshaelekeza TARURA katika Halmashauri zote kufanya usanifu, kazi inayofanyika sasa hivi ni usanifu wa madaraja na makalvati ili tuweze kujua gharama halisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tumeona tunaweze kutoa hela tukajenga barabara, lakini kama madaraja na makalvati hayajajengwa hayapitiki maana yake tumefanya kazi bure. Kwa hiyo kipaombele chetu sasa tunataka mwakani tukaelekeze kwenye madaraja na makalvati, kwa hiyo, niwatoe hofu tu waheshimiwa wabunge hili swala tumelipa kipaumbele. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano ya simu katika Kata ya Litapunga?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kufatia mabadiliko aliyoyafanya katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na baadaye kuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kuniteua na kuniapisha kuendelea kuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Taknolojia ya Habari.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari sasa naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe Mbunge wa Nsimbo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Litapunga ina jumla ya vijiji nane ambavyo ni Kaburonge “A”, Kaburonge “B”, Kambuzi “A”, Kambuzi “B”, Kambuzi Halt, Bulembo, Lukama pamoja na Litapunga.

Mheshimiwa Spika, Kata hii imekuwa ikipokea huduma za mawasiliano kutoka kata Jirani za Katumba na Kanoge zenye huduma ya mawasiliano ya Mtandao wa Halotel na Vodacom.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itafanya tathmini ya kiufundi ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika Kata ya Litapunga ili kupata uelewa wa pamoja na ukubwa halisi wa changamoto ili kuelekeza ufumbuzi unaoendana na changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Spika, iwapo tathmini hiyo itabainisha kuwa utatuzi wa changamoto ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano iliyopo unahitaji kuwa na mnara katika kata hiyo, basi Serikali itaingiza kata hii katika zabuni zitakazotangazwa katika siku za karibuni kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaigawa Kata ya Katumba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe Mbunge wa Jimbo la Nsimbo kama ifuatavyo: -

Mheshimwa Spika, Serikali inatambua uhitaji wa kuigawa Kata ya Katumba kutokana na ukubwa wake na idadi kubwa ya watu.

Mheshimiwa Spika, kutokana na kuwepo kwa maeneo mengi ya utawala ambayo bado hayana miundombinu muhimu ya kiutawala na ya huduma za jamii, Serikali kwa sasa imeweka kipaumbele zaidi katika kujenga miundombinu hiyo ili kutoa huduma bora kwa wananchi badala ya kuanzisha maeneo mapya ya utawala.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo inashauriwa kukamilisha hatua za maombi na kuwa na subira katika kipindi hiki mpaka hapo Serikali itakapoona inaweza kuigawa Kata hiyo. Ahsante sana.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Kijiji cha Kanonge Kata ya Nsimbo kitapelekewa umeme wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kanoge kilichopo Kata ya Nsimbo kina jumla ya vitongoji vitano vya Kanoge A, Kanoge B, Tupindo, Kavikonge na Tulieni. Kijiji cha Kanoge tayari kimefikiwa na huduma ya umeme katika vitongoji vya Kanoge B na Tulieni. Vitongoji vitatu vilivyosalia vitafikishiwa umeme kupitia Mradi wa kusambaza umeme wa Kitongoji kwa Kitongoji (Hamlet Electrifiction Project) unaotajariwa kutekelezwa nchi nzima kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. RITHA E. KABATI K.n.y. MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -


Je, ni lini Serikali itajenga daraja la Ugalla lililopo katika Kata ya Ugalla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa Daraja la Ugalla lenye urefu wa mita 150, ikiwa ni maandalizi ya kuanza kwa ujenzi. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha ili kuanza ujenzi wa daraja hilo. Ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza: -

Je, ni lini wananchi wa Kata ya Sitalike waliopisha ujenzi wa barabara ya Sitalike hadi Mpanda Hotel watalipwa fidia?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wananchi wa Kata ya Sitalike hadi Mpanda wanaodai fidia ni wale walio kwenye eneo la nyongeza la upana wa hifadhi ya barabara la kutoka mita
22.5 kwenda mita 30.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuwalipa fidia wananchi hawa, ahsante.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa mradi wa lambo Kata ya Nsimbo, Kijiji cha Mwenge, Halmashauri ya Nsimbo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Jimbo la Nsimbo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo hapa nchini, Serikali ilianza ujenzi wa mabwawa manne ya maji kwa mifugo likiwemo bwawa la Isulamilomo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo. Aidha, ujenzi wa Bwawa la Isulamilomo haukukamilika katika muda uliopangwa kutokana na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi, ikiwemo kukosekana kwa barabara ya kusafirisha mitambo kwenda eneo la mradi na kipindi kirefu cha mvua nyingi katika eneo la mradi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto hizo, Mkandarasi aliomba kuongezewa muda wa kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambapo ujenzi unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2023. Kwa sasa, Mkandarasi yupo katika eneo la mradi akiendelea na kazi ya ujenzi wa tuta na njia ya utoro wa maji. Naomba kuwasilisha.