Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Angelina Adam Malembeka (19 total)

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA aliuliza:-
Matukio ya kubakwa na ulawiti kwa watoto nchini yamekuwa yakijirudia mara kwa mara na watuhumiwa walio wengi huachiwa au humalizana na wazazi wa waathirika kifamilia:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kesi hizo hazimalizwi kifamilia?
(b) Je, ni mkakati gani umewekwa ili kuhakikisha kuwa watuhumiwa hao wanapopatikana na hatia wapewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia mbaya?
(c) Je, watoto waliopatwa na matukio hayo wamewekewa mazingira gani ili kuwaondoshea msongo wa mawazo na kuendelea na elimu bila kubughudhiwa na wenzao.
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Agelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b), na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli matukio ya kubakwa na kulawitiwa, watoto yamekuwa yakitokea na kuripotiwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Pia ni kweli kuwa baadhi ya kesi za aina hiyo zimekuwa zikimalizwa kifamilia kwa maridhiano kati ya mtuhumiwa na wazazi wa mtoto muathirika. Hivyo kuwapa shida sana Wapelelezi wa kesi hizo kupata ushahidi.
(a) Tatizo la kuficha ushahidi na kuzimaliza kesi hizo kifamillia haliwezi kumalizwa na Vyombo vya Dola vinavyofanya uchunguzi peke yake bila ushirikiano na wananchi wanaoishi na watuhumiwa. Hivyo, Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kwa kuficha ushahidi na kuyamaliza matukio hayo ati kifamilia siyo kosa la jinai peke yake, bali vile vile, utaratibu huo unachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya Polisi yanayopokea taarifa kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi. Pindi tukio la kubaka au kulawiti linaporipotiwa upelelezi hufanyika na mtuhumiwa hufunguliwa mashtaka mara moja. Kwa utaratibu huu Serikali inahakikisha kuwa matukio haya hayamalizwi nje ya utaratibu wa haki jinai.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Bunge lako Tukufu tumetunga sheria zenye adhabu kali kwa watuhumiwa wa makosa hayo, wanapopatikana na hatia. Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kumbaka msichana, hicho ni Kifungu cha 136(1) au miaka 14 kwa anayekutwa na hatia ya kujaribu kumbaka msichana, Kifungu cha 136(2). Pia sheria imeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14, kwa kosa la kulawiti Kifungu cha 154.
Mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kuwa, sheria hizi zinasimamiwa ipasavyo na kuendelea kuimarisha upelelezi na uendeshaji wa mashauri ya ubakaji na ulawiti ili kuiwezesha Mahakama kutoa adhabu stahiki pindi mtuhumiwa anapopatika na hatia.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, waathirika wa vitendo hivi viovu, hupata msongo wa mawazo na kujisikia vibaya mbele ya wenzao, hali ambayo ina athari mbaya kwenye masomo yao na makuzi ya watoto hao. Serikali imeanza utekelezaji wa mwongozo wa mwaka 2015 wa kuzuia ukatili dhidi ya watoto, mwongozo ambao unataka Walimu Washauri, wateuliwe kila shule ya Msingi na Sekondari na kupatiwa mafunzo ya ushauri nasaha.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Serikali imepanua wigo wa uandishi na usomaji wa vitabu vya ziada na kiada mashuleni na kuna wakati tunapokea vitabu mbalimbali kutoka kwa wahisani.
(a) Je, ni utaratibu gani uliopo wa kudhibiti vitabu visivyo na maadili mema kwa watoto?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Kitengo cha Udhibiti na Usimamizi wa Vitabu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliandaa Waraka wa Elimu Na. 4 wa mwaka 2014 unaoipa Mamlaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuandika vitabu vyote vya kiada kwa ngazi ya elimu msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Wizara kupitia TET imeandaa na kutoa mwongozo wa kutathmini maandiko ya kutekeleza mitaala ikiwa ni pamoja na vitabu vinavyoandikwa na waandishi binafsi, vinavyotolewa na wahisani pamoja na vitabu vya kiada vinavyoandaliwa na TET unasisitiza masuala ya maudhui yanayotakiwa kwa kuzingatia muhtasari wa ngazi ya elimu husika pamoja na utamaduni na maadili ya Kitanzania.
Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia TET imeanzisha somo la uraia na maadili kuanzia darasa la tatu mpaka la sita ili kuwajengea uwezo watoto wa Kitanzania wa kuyafahamu ipasavyo maadili na utamaduni wetu mapema. Pia TET hutoa mafunzo kwa walimu ili kusisitiza suala la maadili kwao wenyewe na kwa watoto wanaowafundisha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha Kitengo cha Tathmini na Udhibiti wa Ubora wa Maandiko yanayotumika kutekeleza mitaala, Wizara kupitia TET imeanzisha kitengo maalum chini ya Idara ya Utafiti, Habari na Machapisho, ambacho moja wapo ya majukumu yake ni kuratibu na kusimamia shughuli za kutathmini vitabu na maandiko ya kutekeleza mitaala ikiwa ni pamoja na vitabu vilivyoandikwa na waandishi binafsi pamoja na vitabu vilivyoandikwa na TET.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya maandiko ya kielimu hufanywa na wataalam kutoka vyuo vikuu, vyuo vya ualimu, shule za sekondari, shule ya msingi pamoja na makampuni mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu na makala za kielimu. Aidha, hadi sasa TET imeshatathmini jumla ya miswada ya vitabu 160 vilivyochapishwa na wachapishwaji binafsi.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA aliuliza:-
Uwezeshwaji wa wananchi ni suala muhimu sana ili kuweza kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo hususani vijana na wanawake na Mifuko iliyopita kama ule wa Mabilioni ya Kikwete, Mfuko wa Wanawake na Vijana na kadhalika haikuwafikia walengwa:-
(a) Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mkakati gani wa kuboresha Mifuko hii na kuibua mingine?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kilichorejeshwa na wananchi kwenye Mifuko hiyo ili na wengine waweze kufaidika nayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inakusudia kufanya tathmini ya Mifuko yote ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inayosimamiwa na Serikali ili kutambua ni kwa kiasi gani Mifuko hiyo inafikia malengo yake ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na pia kufanya maboresho kwenye utendaji wa Mifuko. Tathmini hiyo ndiyo itakayotoa uelekeo wa namna bora ya kuratibu utendaji wa Mifuko hiyo kwa kuzingatia tija katika kila Mfuko. Kwa maana hiyo, suala la kuanzisha au kupunguza Mifuko mingine litategemeana na matokeo ya tathmini itakayofanyika.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotumika kukopesha wananchi mikopo hii ni wa mzunguko (revolving fund), hivyo bado fedha hizo zinaendelea kuzunguka miongoni mwa wananchi na hivyo kutoa fursa kwa wengi kunufaika nayo. Kwa mfano, Mfuko wa Mabilioni ya JK ulikopesha shilingi bilioni 50.6 na zilirejeshwa shilingi bilioni 41.533 sawa na asilimia 82; Mfuko wa Wajasiriliamali wa Wananchi (NEDF) ulikopesha shilingi bilioni 36.387 na zimerejeshwa shilingi bilioni 32.748 sawa na asilimia 90; na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ulikopesha shilingi bilioni 5.789 na kurejesha shilingi bilioni 3.473 sawa na asilimia 60.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Ofisi nyingi za Balozi zetu katika nchi mbalimbali zimekodishwa. Aidha, ofisi nyingine ujenzi haujakamilika au hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu sasa na ofisi nyingine zina madeni makubwa.
(a) Je, ni lini ujenzi wa baadhi ya ofisi za Ubalozi zitakamilika ikiwemo ya Msumbiji?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati ofisi chache za Ubalozi zilizopo pamoja na kununua samani mpya?
(c) Je, kwa nini Serikali isilipe madeni ya Balozi zetu kwa wakati ili kuepusha aibu kwa Taifa?
NAIBU WAZIRI KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi zetu umekuwa ukitekelezwa kwa awamu kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha za bajeti ya maendeleo. Mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ilipanga kutekeleza miradi ya ujenzi katika Balozi zake ikiwemo Maputo, Nairobi na Stockholm na uboreshaji wa mifumo ya mawasiliano kati ya Balozi na Makao Makuu wa Wizara. Mradi wa Maputo umepangiwa shilingi 1,316,435,000. Tunategemea utekelezaji wa mradi huu ufanyike pale Wizara itakapopokea fedha kutoka Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua kuwa fedha za bajeti ya maendeleo hazikidhi mahitaji, Wizara inaendelea kushirikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kama vile Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Taasisi ya Miradi ya Maendeleo ya Miundombinu katika ujenzi wa majengo ya ofisi na vitega uchumi katika Balozi zetu. Wizara inaamini uamuzi wa kuishirikisha mifuko hiyo itaongeza kasi ya ujenzi wa majengo ya ofisi katika Balozi zetu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Wizara uliopo hizi sasa katika kukarabati majengo ya ofisi yaliyopo kwenye Balozi zetu ni kuendelea kuiomba Serikali kutenga fedha za bajeti ya maendeleo; pili, kuelekeza Balozi zetu kutumia utaratibu wa karadha (mortgage finance) ili kuwezesha Balozi kupata fedha za ukarabati, kununua na kujenga majengo ya ofisi na vitega uchumi; na tatu, kuishirikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iliyopo nchini kutekeleza miradi ya Wizara Balozini kwa Wizara kuingia makubaliano na vyombo hivyo. Aidha, Wizara itaendelea na utaratibu wa kununua kwa awamu samani mpya za ofisi kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kulipa madeni ya Balozi zake nje. Serikali ilitoa kiasi cha shilingi 7,315,720,301.84 kulipa madeni ya Wizara yaliyohakikiwa na Wakaguzi wa Hesabu. Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016 deni lililobaki ni shilingi 15,540,603,526. Madeni haya yameanza kukaguliwa na Hazina, hivyo ni matarajio yetu kuwa baada ya kukamilika kwa ukaguzi huo, Hazina itatoa fedha za kulipa madeni hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Hazina imetoa mwongozo unaoelekeza kuandaa mpango wa bajeti ambao unaelekeza madeni yote ya Wizara, Wakala na Taasisi za Serikali kulipwa moja kwa moja na Hazina.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Kuna vijana zaidi ya 300 Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wanajihusisha na kazi mbalimbali za kujitolea kama vile usafi, upandaji miti, kilimo cha mboga mboga na matunda na wapo tayari kijiunga na Jeshi la Ulinzi kama wakifikiriwa:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwachukua vijana hao kujiunga na Jeshi hasa ikizingatiwa kuwa wana maadili mema na wameweza kujitolea?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa sasa wa wananchi wa Tanzania kuajiriwa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania unataka waombaji kuwa wamepitia Jeshi la Kujenga Taifa. Jeshi la Kujenga Taifa hutoa nafasi kwa kila mkoa. Vijana wanaopenda kujiunga na Jeshi hujadiliwa na kupitishwa na Kamati za Ulinzi na Usalama ngazi ya wilaya na mkoa husika. Kwa upande wa Zanzibar nafasi hizo hutolewa kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na idara maalum za SMZ. Ofisi hiyo ndiyo yenye wajibu wa kupeleka mgao huo katika mikoa husika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu vijana zaidi ya 300 wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao wanajihusisha na kazi mbalimbali za kujitolea na ambao wako tayari kujiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, vijana hao wanashauriwa kuomba kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa mara nafasi zitakapotangazwa. Endapo watakuwa na sifa za kuajiriwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania naamini watapewa fursa hiyo kwa kadri ya nafasi zitakavyopatikana.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Kutokana na uvamizi wa ardhi katika maeneo ya mashule, masoko na zahanati.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha upimaji wa maeneo hayo?
(b) Je, kutokana na ukubwa wa gharama za upimaji, kwa nini zoezi la upimaji lisitolewe bure kwa taasisi za umma kupitia Halmashauri hizo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya shule, soko, zahanati, vituo vya afya, hospitali, vyuo, ofisi za Serikali, vituo vya polisi, mahakama, maeneo ya majeshi, hifadhi za misitu na wanyama na maeneo ya makumbusho hutengwa maalum kwa ajili ya matumizi ya umma na shughuli mbalimbali za Serikali. Maeneo yote haya yapo chini ya usimamizi na uangalizi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa au Serikali Kuu. Hata hivyo, maeneo mengi kati ya hayo yamekuwa yakisimamiwa na taasisi za Serikali bila kupimwa wala kuwa na hatimiliki badala yake yamekuwa yakimilikishwa kwa utaratibu wa kupewa government allocation.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu pamoja na kwamba umekuwa ukifanywa kwa nia njema, umetoa mwanya kwa wananchi wenye nia ovu kuyavamia, kuyamega na kuyaendeleza maeneo ya Serikali kinyume na utaratibu. Ili kuhakikisha kuwa changamoto ya uvamizi wa maeneo ya umma unakomeshwa, Serikali kupitia Wizara yangu iliagiza kuwa maeneo yote ya umma, yapimwe na yamilikishwe kwa taasisi husika kupitia barua yenye Kumb. Na. AB225/30/305/01 ya tarehe 7 Septemba, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuitikia wito huu baadhi ya taasisi za Serikali ikiwemo TBA, Hazina na TANROADS zinaendelea kuyatambua maeneo yake na kuyamilikisha maeneo wanayoyasimamia. Nitoe rai kwa Wakuu wote wa taasisi za umma kuhakikisha wanakamilisha zoezi hili mapema na kwa maeneo ambayo yamevamiwa ni vema wavamizi wakaondoka kwa hiari yao na wasisubiri mkondo wa sheria uwakumbe. Aidha, nampongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Tabora na timu yake kwa kutekeleza agizo la Waziri kwa vitendo na ni vema Wakuu wote wa Mikoa wengine wakachukua hatua ili kuondoa wavamizi kwenye maeneo yote ya umma.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama elekezi za huduma za upimaji ambazo kwa mara ya mwisho zilifanyiwa mapitio mwaka 2016 siyo kubwa kama inavyodhaniwa kwa kuwa upimaji wa ardhi hufanywa kwa misingi ya kurejesha gharama pakee. Gharama hizo hujumuisha vifaa vya upimaji, shajara, usafiri, matengenezo ya vifaa na mawasiliano ya kitaalam. Aidha, kukamilika kwa mtandao wa upimaji (Taref 11) tutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za upimaji nchini.
Mheshimia Mwenyekiti, natoa rai kwa taasisi zote za Serikali nchini kuhakikisha zinapima na kumilikishwa maeneo yao ili kuwa na miliki salama kwa kuwa ulinzi wa ardhi wanayomilikishwa ni jukumu la taasisi husika. Aidha, taasisi zote za umma nchini zinahimizwa kutenga fedha katika bajeti zao kwa ajili ya kuharakisha upimaji wa maeneo yote wanayoyasimamia.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga viwanda kwa ajili ya malighafi ya karafuu?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kujenga viwanda hivyo hapa nchini itapunguza kusafirisha karafuu nje ya nchi kinyume na utaratibu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kwama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la karafuu huzalishwa kwa wingi Zanzibar kwa wastani wa tani 5,500 kwa mwaka na Tanzania Bara kwa Mikoa ya Morogoro na Tanga kwa wastani wa tani 364.4 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya zao hili huuzwa nje ya nchi hasa nchini India, Singapore, Indonesia, Umoja wa Nchi za Kiarabu na Ulaya. Kwa sasa kuna kiwanda kimoja cha kuzalisha mafuta ya makonyo kwa kutumia malighafi zitokanazo na karafuu ambacho kipo Kisiwani Pemba. Kwa mwaka 2016/2017 kiwanda hicho kiliweza kuzalisha mafuta ya makonyo jumla ya tani 974.714 yenye thamani ya shilingi milioni 974.714 yaliyouzwa ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanda ni jukumu la sekta binafsi Serikali inabaki na jukumu la uhamasishaji na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Kutokana na fursa iliyopo kwenye zao la karafuu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda tutaongeza jitihada ya kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuongeza thamani zao la karafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikubaliane na Mheshimiwa Angelina Malembeka kuwa kwa kujenga viwanda nchini kutapunguza kusafirisha karafuu nje ya nchi kinyume na taratibu. Pia ujenzi wa viwanda nchini utatengeneza ajira kwa wananchi wetu na kuongeza thamani ya karafuu hali itakayowezesha wazalishaji kupata bei nzuri na kutokana na kuwa shuguli hizi zinafanyika kwa utaratibu rasmi tutaongeza wigo wa walipa kodi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Mitihani ya Taifa kidato cha nne na sita hufanyika kwa pamoja kwa wanafunzi wa Tanzania Bara na Visiwani.
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kutumia mitaala na vitabu vya aina moja ili kuwapa wanafunzi wa Zanzibar fursa ya kujisomea na kufanya vizuri katika mitihani yao?
• Kwa kuwa mitaala na vitabu vya elimu ya awali na ya msingi kwa upande wa Zanzibar ni tofauti na Tanzania Bara, je, kwa nini Zanzibar wasiruhusiwe kutunga mitihani ya Taifa tofauti na Bara kwa kidato cha nne na sita, na mitihani hiyo ikapata hadhi sawa na ile inayotungwa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala na vitabu vinavyotumika kufundishia na kujifunzia kwenye ngazi ya elimu ya sekondari (kidato cha kwanza hadi cha sita) kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni vya aina moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mitaala na vitabu vinavyotumika katika ngazi ya elimu ya sekondari kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ni vya aina moja, Sheria ya Bunge namba 21 ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 inalipa mamlaka Baraza la Mitihani la Tanzania ya kuendesha mitihani ya Taifa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kwa kuzingatia kuwa mitaala na vitabu vya elimu ya awali na msingi vinavyotumika kwa upande wa Zanzibar ni tofauti na vinavyotumika Tanzania Bara, mitihani ya elimu ya awali na msingi kwa upande huo huendeshwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.
MHE. SAADA MKUYA SALUM (K.n.y. ANGELINA ADAM MALEMBEKA) aliuliza:-
Baadhi ya Wabunge wa Majimbo walihama Vyama vyao na kujiunga na vyama vingine hivyo Chaguzi Ndogo zikafanyika na Chama cha Mapinduzi kikashinda Majimbo hayo:-
(a) Je, ni nini hatma ya Wabunge wa Viti Maalum walioingia Bungeni kupitia asilimia za Majimbo yao ya Uchaguzi?
(b) Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kimeongeza idadi ya Majimbo zaidi, je, ni lini Wabunge wa Viti Maalum wapya wa CCM kupitia Viti Maalum wataingia Bungeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 78(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeainisha bayana kuwa vyama vya siasa vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu na kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za Wabunge vitapendekeza kwa Tume ya Uchaguzi majina ya wanawake kwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa Wabunge ili Tume iweze kuteua miongoni mwao Wabunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa msingi wa sheria hii, idadi ya Wabunge wa Viti Maalum kwa kila chama inapatikana wakati wa Uchaguzi Mkuu ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano. Hivyo, mabadiliko yoyote yanayotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo hayaathiri idadi ya Viti Maalum vya chama husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kupokea maoni na ushauri kuhusu jambo hili hivyo kutokana na hali ilivyo hivi sasa, Katiba na Sheria za Nchi vitaendelea kuwa msingi mkuu wa ufafanuzi na mgawanyo wa Viti Maalum Bungeni.
MHE. SALMA R. KIKWETE (K.n.y MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA) aliuliza:-
Kwa kuwa Serikali ina mkakati madhubuti wa kupunguza vifo vya akina mama na watoto:-
(a) Je, ni lini Zahanati ya Kiboga katika Kata ya Msongola itafunguliwa ili wananchi wapate huduma ya afya?
(b) Kwa kuwa wananchi wa Mtaa wa Mbondole katika Kata ya Msongola walitoa ardhi kwa ajili ya ujenzi wa zahanati, je, ni lini zahanati hiyo itakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiboga na Luhanga ni mitaa miwili inayopakana ambayo hapo awali ilikuwa miongoni mwa vitongoji katika Kijiji cha Mvuti, Kata ya Msongola. Wananchi wa Mtaa wa Luhanga kwa nguvu zao wenyewe walianza ujenzi wa zahanati na Serikali ikawaunga mkono na sasa jengo la zahanati ya Luhanga lipo katika hatua za upakaji rangi, kuweka madirisha na milango. Mtaa wa Kiboga bado hauna zahanati hivyo halmashauri inatakiwa kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa zahanati. Hata hivyo, wakazi wa Kiboga wanapata huduma za afya katika Zahanati ya Mvuti ambayo ipo ndani ya kilometa tano ambayo ni matakwa ya utekelezaji wa Mpango Maalum wa Uimarishaji Afya ya Msingi 2009 - 2017.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Zahanati ya Mbondole imebaki kupigwa rangi na kuwekewa milango ili ikamilike na kuanza kutoa huduma. Halmashauri ya Wilaya ya Ilala imetenga shilingi milioni 70 katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambayo inaweza kukamilisha ujenzi huo.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

Serikali ilikuwa na nia kuanzisha Ranchi za Taifa katika maeneo mbalimbali.

(a) Je, kuna ranchi ngapi na kati ya hizo ngapi zimebinafsishwa na ngapi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa?

(b) Kwa siku za nyuma Ranchi ya Kongwa na Ranchi ya Ruvu, mifugo ilikuwa inaonekana hata ukipita barabarani hali hiyo sasa haipo, je, kuna tatizo gani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kampuni ya Ranchi za Taifa ilianzishwa mwaka 1968 kwa Sheria ya Makampuni (Cap 212) kwa lengo la kuendeleza ufugaji wa mifugo bora ya nyama ili kitosheleze mahitaji ya nyama ndani na ziada ya kuuza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NARCO inamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100 ikiwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Aidha, NARCO inamilikiwa jumla ya ranchi 14 zenye ukubwa wa hekta 544,207 zilizotawanyika sehemu mbalimbali nchini ambazo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa siku za nyuma Ranchi za Ruvu na Kongwa zilikuwa na idadi kubwa ya mifugo ambayo ilionekana hata ukiwa barabarani. Hata hivyo, Kampuni ya Ranchi za Taifa impitia changamoto mbalimbali ikiwemo mwaka 1992 kupendekezwa kubinafsishwa na kuwa nchini ya uangalizi wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashiriki ya Umaa (PSRC) kwa miaka 14. Katika kipindi hicho kampuni haikutekeleza shughuli za maendeleo na hivyo kupelekea uchakavu wa miundombinu na mashamba kuvamiwa, vichaka na mifugo kupungua. Aidha, kampuni inafanya jitihada za kuboresha miundombinu na malisho katika ranchi hizi ili kuirejesha hali ya kuwa na mifugo mingi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

Baadhi ya wanawake huingia gerezani wakiwa na ujauzito na hivyo kujifungulia gerezani.

(a) Je, ni huduma gani wanazopata ili kuhakikisha wanajifungua salama?

(b) Je, ni jitihada gani zinafanywa ili kuwapatia akina mama hao vyakula vinavyopendwa na wajawazito?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza limekuwa likihifadhi wafungwa wa aina zote wakiwemo wafungwa wa kike wajawazito. Katika kuhakikisha kwamba wafungwa wajawazito wanajifungua salama, Jeshi la Magereza limekuwa likitoa huduma za afya, chanjo na kuhakikisha wanahudhuria kliniki za mama wajawazito katika vituo vya afya vya magereza na pale inapobidi kuwapeleka hospitali za Serikali.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Magereza limekuwa likiwapatia wafungwa wajawazito vyakula wanavyovihitaji kiafya kwa kuzingatia maelekezo na ushauri wa Daktari wa gereza ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto inalindwa. Aidha, Serikali inazidi kuboresha bajeti ya huduma hizo ili kuhakisha kwamba wafungwa wajawazito wanapata huduma hizo inavyostahili.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

Majanga ya moto yamekuwa yakitokea mara kwa mara hasa Viwandani, Majumbani na katika majengo ya Serikali:-

(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa mafunzo kwa Wafanyakazi na wananchi juu ya mbinu za kujihami na kujiokoa katika majanga ya moto?

(b) Je, Serikali imejipangaje katika kutoa mafunzo katika maeneo ya kazi na wananchi juu ya matumizi ya mitungi ya kuzima moto (Fire Extinguishers)?

(c) Je, Serikali ina mpango gani wa kukagua mitungi hiyo kama bado inafaa kwa matumizi au imeshapita muda wake wa kutumika?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kaskazini Unguja, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linaendelea kutoa mafunzo ya mbinu za kujihami na jinsi ya kujiokoa katika majanga ya moto kwenye maeneo ya kazi na wananchi kwa ujumla. Elimu dhidi ya kinga na tahadhari ya moto imeendelea kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo maeneo yenye mikusanyiko ya watu kama vile masoko, Shule za Sekondari na Msingi, Vyuo, Makanisani na Misikitini kupitia vyombo mbalimbali vya habari vikiwemo magazeti, radio na televisheni.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limejipanga vyema kutoa mafunzo kwenye maeneo ya kazi na wananchi juu ya matumizi ya mitungi ya kuzimia moto kwa kuanzisha kampeni mbalimbali kama vile “Ninacho, Ninajua Kukitumia,” “Mlango kwa Mlango” na “Nyumba Salama” zenye lengo la kuhamasisha watu kuwa na vizimia moto na kujua kuvitumia katika maeneo ya makazi, viwanda, maeneo ya vyombo vya usafiri na usafirishaji, majumbani, maeneo ya biashara na katika mikusanyiko mikubwa ya watu. Aidha, wananchi wanaendelea kupatiwa elimu na mafunzo juu ya mifumo yote ya kuzima kuzima katika majengo na maeneo mbalimbali ili kuepusha majanga ya moto.

(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Ukaguzi wa tahadhari na kinga dhidi ya moto kwa mujibu wa Kanuni za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji umeendelea kufanyika sambasamba na ukaguzi wa mitungi ya kuzima moto na kumshauri mtumiaji juu ya ubora wa mtungi na kumshauri mmiliki ipasavyo.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

(a) Je, ni vijana wangapi kutoka Wilaya ya Kaskazini A na Wilaya ya Kaskazini B wamepata nafasi ya kujiunga na Jeshi kuanzia mwaka 2015?

(b) Je, mgawanyo wa idadi ya vijana wanaojiunga na Jeshi kwa kila wilaya nchini upoje?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita yaani kuanzia mwaka 2015 hadi 2018 vijana walijiunga na JKT kutoka Zanzibar kwa kujitolea ni kama ifuatavyo:-

(i) Mwaka 2015/2016 vijana 300;
(ii) Mwaka 2016/2017 vijana 300;
(iii) Mwaka 2017/2018 vijana 400 kwa hivyo jumla katika miaka hiyo mitatu ni vijana 1000.

Jukumu la kugawa nafasi hizo kwa wilaya liko chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kwa mwaka 2019/20 Zanzibar imetengewa nafasi 500.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa idadi ya vijana wanaojiunga na JKT kwa kujitolea kwa kila mkoa huzingatia uwiano wa idadi ya watu kulingana na takwimu za sensa ya Taifa ya watu na makazi, elimu, jinsia na sifa nyingine zinazokuwa zimeainishwa na mkuu wa JKT. Zoezi hili ikiwa ni pamoja na mgawanyo wa vijana hadi ngazi ya wilaya huratibiwa na wakuu wa mikoa husika baada ya Makao Makuu ya JKT kuainisha idadi ya vijana kwa kila mkoa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA Aliuliza: -

Kuna mpango wa kujenga bandari kubwa ya uvuvi inayotegemewa kutoa ajira zipatazo 30,000.

Je, ajira kwa upande wa Zanzibar zitakuwa ngapi kati ya hizo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mpango wa kujenga bandari ya uvuvi nchini ambapo inaendelea kufanya upembuzi yakinifu, uchambuzi wa awali umetoa mapendekezo ya kujengwa kwa bandari ya uvuvi katika eneo la Mbegani, Bagamoyo. Aidha, uamuzi wa kujenga bandari ya uvuvi ni miongoni mwa vipaumbele vya Taifa, lakini katika sera ya uvuvi ya 2015 lakini Mpango wa Maendeleo Miaka Mitano wa Awamu ya III 2021 hadi 2026.

Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa ujenzi wa bandari kunakadiriwa kutoa ajira zaidi ya 30,000 wakiwemo wananchi kutoka Zanzibar, aidha, Serikali itahakikisha kuwa Watanzania kutoka pande zote nchini wananufaika na fursa za ajira, biashara ya mazao ya uvuvi na uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

Je, ni gharama kiasi gani na taratibu gani hutumika ili kupata huduma za ulinzi za SUMA JKT?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, huduma ya Ulinzi toka SUMA JKT Guard inapatikana kupitia njia kuu nne, ikiwemo:-

(1) Idara ya masoko kutembelea wadau wa huduma ili kutangaza shughuli za kampuni;

(2) Mteja mwenyewe kuwasilisha barua za maombi ya kupatiwa huduma ya ulinzi;

(3) Kampuni imesajiliwa katika mfumo wa manunuzi ya Serikali ya TANEPS ambapo wadau, hasa Taasisi za Serikali hutumia kutangaza zabuni.

(4) Ushiriki katika mchakato wa zabuni shindanishi zinazotangazwa kupitia magazeti na vyombo vya habari.

Mheshimiwa Spika, naomba nifafanue zaidi kuwa gharama ya kupata huduma za ulinzi za SUMA JKT Guard kwa mlinzi mmoja bila silaha ni shilingi 590,000 kwa mwezi ikijumuisha VAT, lakini silaha moja ni shilingi 129,800 hivyo mlinzi akiwa na silaha, gharama yake ni shilingi 719,800 kwa mwezi. Huduma ya mlinzi mmoja kwa maeneo ya migodini ni shilingi 944,000/= ikiwa ni pamoja na VAT kwa mwezi.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-

Jeshi la Polisi linao uwezo wa kukomesha tatizo sugu la ubakaji na ulawiti kwa watoto wadogo nchini:-

Je, ni kwa nini Serikali isiunde Kikosi Maalum cha kuwashughulikia watu wanaojihusisha na vitendo vya ubakaji na ulawiti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kupambana na tatizo sugu la ubakaji na ulawiti Jeshi la Polisi limejiwekea mikakati thabiti inayohusisha ufuatiliaji wa vyanzo vya makosa na kuyatafutia ufumbuzi. Moja miongoni mwa mikakati hiyo ni kutoa elimu kwa kushirikisha jamii kupitia madawati ya unyanyasaji wa jinsia yaliyopo kwenye vituo vya polisi. Aidha, hutoa elimu ya mapambano dhidi ya makosa ya aina hii katika shule za msingi na sekondari, maadhimisho pia ya kitaifa na matamasha mbalimbali. Aidha, wale wote wanaobainika kutenda makosa hayo huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Mheshimwa Spika, kwa sasa mikakakati ya jeshi la polisi inatosheleza kukabiliana na tatizo hilo bila ya kuhitaji kuanzishwa kwa kikosi maalum kwani yote ya jinai ikiwemo udhalilishaji yana adhabu zake kisheria. Aidha, makosa haya yanatendeka miongoni mwa jamii hivyo, ni lazima jamii nzima ishirikiane kuyapinga na kuyakataa kwa kutoa taarifa vituo vya polisi na kuwa tayari kwenda kutoa ushahidi mahakamani, ili adhabu stahiki zitolewe kwa wahalifu hao, ahsante.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

(a) Je, ni asilimia ngapi ya mapato yatokanayo na Uvuvi wa Bahari Kuu yanaenda upande wa Zanzibar?

(b) Je, kwa miaka mitano iliyopita Zanzibar imepata kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Spika, mgawanyo wa mapato yatokanayo na uvuvi wa Bahari Kuu unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu Na. 5 ya mwaka 2020, Kifungu cha 79, ambayo inaelekeza mgawanyo wa mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu kwa utaratibu ufuatao, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar asilimia 20; Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania asilimia 30; na Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi Bahari Kuu asilimia 50.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu ilikusanya jumla ya Dola za Kimarekani 1,352,107.50 sawa na Sh.3,091,837,178.10. Kutokana na makusanyo hayo na kwa kuzingatia maelezo yangu katika kipengele (a), Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufikia mwezi Machi, 2021 imepata mgao wa Sh.618,367,435.62.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Benki ya Wavuvi nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) tayari ipo kwa ajili ya kutoa huduma za kifedha kwa wadau wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi. Benki hii ilianzishwa mnamo mwezi Septemba, 2012 chini ya Sheria ya Makampuni (Sura ya 212).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilianzisha Benki hiyo ili kusaidia kuongoza mageuzi ya kuleta maendeleo kwenye sekta ya kilimo sambamba na kujenga uwezo wa wadau kutekeleza programu mbalimbali za kuongeza thamani mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Benki hii inatoa mikopo ya muda mfupi, wa kati na mrefu kwa watu binafsi na vikundi vinavyojishughulisha na sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumshauri Mheshimiwa Mbunge awahamasishe wavuvi kuchangamkia fursa mbalimbali za mikopo na huduma nyinginezo za kifedha zinazotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo. Ahsante.