Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Cecilia Daniel Paresso (35 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyoko mezani. Nianze kwa kusema Serikali nyingi duniani huongozwa kwa Katiba iliyojiwekea, Sheria zilizopo, Kanuni zilizopo, Taratibu zilizopo au Dira
ambayo imejiwekea kama nchi, lakini katika Serikali ya Awamu ya Tano tunaona mnaongozwa
kwa kauli mbiu ya hapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mtanielewa tu! Nasema mnaongozwa kwa hapa kazi, bila kufuata Sheria zilizopo, Kanuni zilizopo, utaratibu uliopo na Katiba mliyojiwekea. Nasema haya kwa mifano nitakayoitoa; Rais anafukuza watumishi wa umma! Ni kweli kwamba kuna baadhi ya watumishi wa umma sio waaminifu na wana upungufu. Pia, ni kweli kwamba kuna baadhi ya watumishi wako kwenye mamlaka ya Rais, wale aliowateuwa anaweza kuwaondoa, lakini kuna wale ambao wameajiriwa, ni sharti taratibu na sheria za kiutumishi zifuatwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine; mmesema mnatoa elimu bure, mtapeleka takribani shilingi bilioni 18 kwa Halmashauri! Mnapeleka kwa bajeti ipi ambayo hatujapitisha ndani ya Bunge? Bunge la Kumi, tulipitisha Bajeti, ni lini mmeleta Supplementary Budget ndani
ya Bunge, ili mtekeleze hili? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano mwingine, Rais alifuta sherehe za Uhuru! Ni kweli kwamba katika Bunge la Kumi kati ya mambo ambayo Upinzani tulikuwa tunapigia kelele, ni kufuta sherehe mbalimbali ambazo hazina tija, ni jambo jema. Amefuta sherehe za Uhuru akatoa agizo fedha zipelekwe kwenye ujenzi wa barabara ya Morocco; amefanya fedha hizo zimekwenda, taratibu za manunuzi, kutangaza tender, Sheria mliyojiwekea ya Manunuzi, mmefuata au mnasema tu hapa kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, kupitia vyombo vya habari, jana au juzi, Afisa mmoja wa Serikali amesema watapeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji! Nawauliza kwa Bajeti ipi? Kwa Sheria ipi? Kwa Supplemantary Budget ipi mliyojiwekea? Au mnaongozwa tu kwa hapa
kazi, bila kufuata sheria zilizopo? Mtakuwa ni Serikali ya ajabu duniani kuongozwa na kauli mbiu badala ya sheria mlizojiwekea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Hotuba ya Rais ameelezea kwa upana suala la amani na utulivu na mmekuwa mkijivunia amani na utulivu. Mnawaambia Watanzania kuna amani na utulivu, wakati hakuna demokrasia ndani ya nchi hii, demokrasia zinaminywa zinakanyagwa.
Kuna migogoro ya ardhi, wakulima na wafugaji, halafu mnasema amani na utulivu! Hakuna ajira kwa vijana, halafu mnasema amani na utulivu! Mahakama hazitoi haki kwa wakati, halafu mnasema amani na utulivu! Hospitalini hakuna dawa, kinamama wakienda kupata huduma
zipo mbali au wakati mwingine hazipatikani, mnasema amani na utulivu! Tumeona utumiaji wa nguvu za kidola wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi, halafu mnasema amani na utulivu!
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itafika mahali Watanzania hawatathubutu tena kuvumilia amani na utulivu wakati wana shida lukuki! Hakuna haki, watu wanakandamizwa, watu wananyanyaswa, halafu mnang‟ang‟ania kusema amani na utulivu! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie machache kwa kusema katika Hotuba ya Mheshimiwa Rais, ameelezea hali ya kisiasa Zanzibar. Hili tunamwambia nalo ni jipu alitumbue, alifanyie kazi! Mshindi atangazwe! Si mmesema ninyi hapa kazi! Fuateni basi Sheria, Katiba na Taratibu mlizojiwekea. Mtangazeni mshindi wa Zanzibar, kwa nini mnaogopa? Mkiambiwa hili mnaogopaogopa na mnaanza kupiga-piga kelele, kuna nini kimejificha hapa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka suala la mgogoro wa kisiasa, kama amesema yeye atakuwa ni Rais wa kutumbua majibu basi atumbue na hili, Wazanzibari wapate haki yao waliyemchagua aweze kutangazwa. Ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Mfuko wa TASAF; Fedha hizi ni mkopo toka World Bank kiasi cha dola za Kimarekani 220,000,000 ili kusaidia kaya maskini nchini. Kaya hizo kulingana na utofauti wa mahitaji, hupewa kati ya sh. 20,000 hadi sh. 62,000 kila baada ya miezi miwili.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huu ni wa miaka mitano, je, Serikali imejipangaje kufanya mradi huu uwe endelevu? Je, Serikali itaweza kugharamia mradi huu pindi muda wa mradi kwisha ukifika?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, Serikali imekuwa na mwenendo wa kuanzisha miradi na Mifuko mingi bila kuwa endelevu na kutoleta tija inayotakiwa. Mfano wa Mifuko iliyoanzishwa ni pamoja na Mabilion ya JK, Mfuko wa Wanawake na Vijana (Halmashauri za Wilaya), TASAF, Mfuko wa Dhamana ya Mikopo, Mfuko wa Amana ya Ubinafsishaji na sasa shilingi milioni 50 kila kijiji. Kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kubadili mtindo huu wa kutoa fedha mikononi mwa wananchi kwani kwa kufanya hivyo haiwezi kuondoa umaskini au kuboresha maisha yao, umuhimu ungewekwa kwanza kuboresha huduma muhimu za kijamii kwa kiwango cha juu na ndipo tuwaze mpango huo wa kutoa fedha kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika Mifuko hiyo tathmini ya kina imefanywa ili kupima matokeo yaliyotarajiwa? Ni kwa kiwango gani Mifuko hiyo imekuwa endelevu? Serikali haioni umuhimu wa kuachia sekta binafsi ifanye na kutekeleza mpango huu na Serikali ibaki kama mdhibiti? Nashauri Serikali ijipime upya na kuacha kufanya mambo au maamuzi kwa mazoea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. CECILIA D. PARESO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika bajeti hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Kwanza naunga mkono maoni yaliyotolewa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani hapa Bungeni na nafikiri Serikali ni vizuri mkayapitia, mkasoma na mkayachukua kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliingia kwa mbwembwe nyingi ikijiita ni Serikali ya ‘Hapa Kazi tu.’ Lakini Serikali hii ya ‘Hapa Kazi Tu’ pia kupitia hotuba ya Waziri Mkuu ukurasa wa 11 inasema ili kuboresha demokrasia hapa nchini hatuna budi kujenga jamii inayoheshimu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu. Wameandika hivi kwenye vitabu lakini sisi Wabunge na wananchi ni mashahidi kwamba hii Serikali ya hapa kazi ndio Serikali ambayo inavunja katiba, inavunja sheria, haifuati taratibu na haifuati misingi ya utawala bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini nasema hivi? Sababu zipo nyingi lakini kutaja tu kwa uchache hoja mojawapo tu, leo tunawadhibiti na kuwanyamazisha wananchi na vijana mbalimbali ambao wanatoa maoni yao kwa namna yoyote katika nchi hii. Tunajenga vijana wawe waoga kwenye nchi yao, tunawaziba midomo vijana na wananchi wasitoe maoni yao wakati katiba ya nchi imetoa uhuru huu kwa wananchi kutoa maoni yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavinyima vyama vya siasa visifanye mikutano wakati katiba na sheria zinaruhusu; na uhai wa vyama vya siasa, chama chochote cha siasa ni kufanya mikutano ya hadhara, ni kukutana na wanachama wake. Uhai wa wa vyama vya siasa ni kuongeza wanachama kwa sababu hawa wanachama; ni kama ilivyo makanisa kwenye vyama vya siasa, leo mtu yupo chama hiki na kesho
yupo chama hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kuendelea kuimarisha vyama vyetu kwa kuongeza wanachama, tunaongeza wanachama kwa kupitia mikutano ya hadhara; lakini Serikali leo inapiga marufuku mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, inavunja katiba ya nchi iliyojiwekea, inavunja sheria. Sasa ndio tunajiuliza hii ndio hapa kazi kweli ya kuvunja katiba na kuvunja sheria? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo watu wanatekwa, wananchi hawana amani; kwenye mitandao sasa hivi ukisoma wananchi wanasema hata nikienda mahali naaga naenda sehemu fulani kwa sababu sijui kama nitarudi salama au nitatekwa. Tumeshuhudia hapa kuna watu wametekwa wamepotea, hawajulikani walipo, hakuna kauli ya Serikali; hatujasikia kauli nzito inatolewa na Serikali, tunajiuliza kama Serikali imekaa kimya je, ndiyo inayohusika na hili jambo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kama na ninyi mngekuwa mnaliona jambo hili kweli linatishia amani ya wananchi mngetoa kauli, hamtoi kauli watu wanatekwa, watu hawajui wanapotelea wapi; hatujui kama kina Ben Sanane haijulikani kama ni wazima au wameshauwawa, haijulikani walipo. Hamuwezi mkajiita hapa kazi tu kwa kufanya hivi vitu; au inawezekana mnajiita hapa kazi kwa kufanya hivyo vitu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali hii kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa ilitakiwa ilee hivi vyama vya siasa. Leo mnashabikia ugomvi wa ndani ya Chama cha wananchi (CUF); Serikali imechukua upande ina-support upande mmoja na kuacha upande mwingine. Wakati wanachama wa chama hicho wanawatambua viongozi ikiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF kama ndio Katibu Mkuu wao,
lakini Msajili wa Vyama vya Siasa badala ya kulea chama hiki na kuhakikisha mgogoro uliopo unatatulika wamechukua upande na wanashabikia upande ule ambao wanaharibu Chama cha Wananchi CUF. Sasa hii ndio hiyo inayoitwa ‘Hapa Kazi Tu’. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Devotha ameeleza hapa asubuhi, hakuna tena ile hadhi ya Ubunge; Mbunge unaonekana si kitu na hasa upande wa upinzani wakati wowote unaweza kuvamiwa nyumbani kwako. Yaani Mbunge ni mtu ambaye anaweza akapotea kwenye nchi hii? Mbunge kama anatakiwa polisi akipewa taarifa ya kwenda kituoni hivi atapotea? Kwa nini tunamchulia Mbunge kama ni mtu ambaye anaweza kupotea? Kwa nini polisi wanatumia madaraka yao vibaya kuwaita Wabunge na kuwataka wakati wowote na kutumia silaha nzito utafikiri Mbunge ni jambazi sugu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima Wabunge tutetee hadhi yetu na ni lazima Wabunge tusimame tutetee hadhi ya mhimili wa Bunge; tukisimama hata mhimili wa Serikali nao utaweza kuona kwamba Bunge lina hadhi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya katiba mpya nadhani yapo pale pale, tunahitaji katiba mpya. Rasimu ya katiba mpya ilitengenezwa kwa fedha nyingi za walipa kodi, mmeiweka kapuni, mmeificha na hatusikii tena Serikali ya Awamu ya Tano mkizungumzia suala la katiba mpya.
Watanzania wanahitaji katiba mpya; tunahitaji katiba mpya na tunaitaka katiba mpya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mifuko ya Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi. Kumekuwa na mifuko mingi sana, kuna hizo asilimia kumi ambazo zinatengwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri. Kumekuwa kuna mifuko mingine kupitia Wizara mbalimbali, ya Vijana, ya Fedha na vitu kama hivyo. Kwa nini isifike mahali sasa mifuko hii ikaunganishwa kuliko kuwa na mifuko mingi ambayo inatoa fedha kidogo ambayo mwisho wa siku hata ukipima ufanisi wa hizo fedha haupo kabisa? Kwa nini tusiwe na mfuko mmoja wa pamoja ambao utatoa mikopo kwa vijana, akinamama na makundi mbalimbali ili kuwawezesha kiuchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu ni kuunganisha hii mifuko na kuufanya mfuko mmoja ili iweze kwenda kutoa mikopo kwa wananchi wetu na kuwaimarisha kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/2017 ambayo tunaimalizia mwezi Juni. Bajeti tuliyoipitisha ilikuwa ni ya shilingi trilioni 29.5 lakini mpaka kufikia Februari fedha za maendeleo zilizotolewa kwa Halmashauri na Wizara ni asilimia 35 tu. Sasa asilimia 35 tumebakiza miezi kama miwili kwenda kumaliza mwaka wa fedha; kutakuwa na muujiza gani wa kwenda kukamilisha hizi fedha za maendeleo?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sababu ambazo zinaelezwa na Serikali, kwamba kwa nini wameshindwa kufikisha hiyo wanasema kuna fedha za wafadhili nyingine zimechelewa na nyingine hazijatolewa. Wakati tunapitisha bajeti hapa mwaka jana tulieleza athari ya MCC na wafadhili wengine kujitoa, mkasimama mkatetea sana hoja hii mkasema nyie mnaweza kujitegemea, mapato yenu ni mazuri na leo hizi ndio athari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kingine tulikuwa tunaona hizi taarifa Serikali ya Awamu ya Tano mnasema mnakusanya karibu Shilingi trilioni 1.2 kila mwezi. Serikali ya Awamu ya Nne iliyopita ilikuwa inakusanya kati ya bilioni 800 mpaka 900 kila mwezi. Kwa hiyo, ninyi mmejigamba kwamba mnakusanya mapato zaidi kila mwezi halafu siku hizi hata hatuoni hizo taarifa za TRA tena; mnajigamba kwamba mnakusanya vizuri kuliko Serikali iliyopita, lakini mnakusanya zinakwenda wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri zetu zipo taabani hakuna fedha za maendeleo; wenyewe mnasema mpaka Februari fedha zilizokwenda ni asilimia tano tu, zingine zinaenda wapi? Mnakusanya zinakwenda wapi? Mtafikiaje kutekeleza bajeti hii ya Shilingi trilioni 29 wakati fedha zenyewe hazijakwenda?
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inayotolewa kwamba wananchi hawana uelewa wa walipa kodi, mashine za EFD; ni hoja dhaifu sana ambazo zinatolewa na Serikali. Nadhani mnapaswa kutafakari na kutumia taarifa za wataalam ili muweze kufikia haya malengo ambayo
yanatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti inayokuja ya mwaka 2017/2018, mnasema mna bajeti ya Shilingi trilioni 31.6; mimi naomba Watanzania muwashangae kama ambavyo mimi naishangaa hii Serikali. Hii ambayo tunamaliza sasa hivi ni trilioni 29 wakati fedha za maendeleo imefika asilimia 35 halafu hiyo projection ya 2017/2018 ni Shilingi trilioni 31, hivi kuna muujiza? Kuna Yesu atashuka awaletee fedha nyie mkatekeleze hii bajeti? Kwa kweli inashangaza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka Serikali ituambie mnaenda kufanya mabadiliko gani katika ukusanyaji wa kodi au katika kuimarisha kodi ili hiyo bajeti ya trilioni 31 iweze kufikiwa? Mtupe majibu sahihi. Hata hivyo, kama haifikiwi kama ambavyo hii ya sasa hivi tunamaliza
haitafikiwa kwa nini msije na bajeti halisi hata kama itakuwa na kiwango kidogo ambayo inaweza kutekelezeka? Kwa nini mnawafurahisha Watanzania kwa namba kubwa wakati utekelezaji wake unakuwa ni sifuri? Kwa hiyo, tunaomba tuambiwe ni kwa namna gani mnaenda kufanikiwa na bajeti hii. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hoja ambayo imewasilishwa na Serikali hapa Bungeni. Kwanza naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani ambayo yamechambua na kutoa mapendekezo mengi. Hapa ndani ya Bunge upande wa pili mmekuwa na mtazamo wa kuona kwamba hatushauri lakini kuna ushauri mwingi sana umetolewa na mapendekezo mengi, naamini Serikali mtaichukua na kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kutoa maoni yangu kuhusu utekelezaji wa bajeti ambayo tunaimalizia. Bajeti ya mwaka 2016/2017 tulipitisha shilingi trilioni 29 kama bajeti ya jumla lakini katika hizo shilingi trilioni 29 mpaka tunapoongea ni takribani asilimia 38 tu ya fedha zote ndiyo imeenda kwenye miradi ya maendeleo. Katika fedha hizi za miradi ya maendeleo ambayo Serikali mmepeleka ni kama ifuatavyo kwa ufupi kwa mujibu wa kitabu cha Waziri. Ujenzi na ukarabati wa barabara imepelekwa shilingi bilioni 675, miradi ya uzalishaji wa umeme shilingi bilioni 441, malipo ya awali ya ujenzi wa reli shilingi bilioni 300, usambazaji wa maji vijijini shilingi bilioni 186 na huduma za afya ni shilingi bilioni 170.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunajiuliza hata hizi fedha tu za miradi ya maendeleo ambayo imepelekwa kwa asilimia chache kiasi hiki, zile ambazo ni muhimu kwa afya za Watanzania ikiwemo afya, maji imepelekwa kidogo ukilinganisha na hizo nyingine za ujenzi na ukarabati wa barabara. Kwa hiyo, unaona kabisa hata umuhimu wa kuwapa Watanzania hizi huduma muhimu za maji na afya haupo na wala hazipewi kipaumbele.

Kwa hiyo, Waziri sasa hivi tunaposema hata hii pia hamtaweza kutekeleza tunamaanisha kwa sababu ya maneno yenu ambayo mmeyaandika humu kwenye hivi vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ya 2017/2018 ambayo sasa tunaitarajia kuanza, mnakisia maoteo ya bajeti itakuwa shilingi trilioni 31.7. Kama hii tunayoimaliza ya shilingi trilioni 29 haijatekelezwa hata kwa asilimia hiyo, je, hii tunayoiendea itatekelezwa? Mnawahadaa Watanzania kwa kuwaambia kwamba hii bajeti haijawahi kutokea, ni bajeti ya karne, mimi naamini ni kweli itakuja kuwaumiza Watanznaia kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini wakati mnafanya bajeti hii kufikia shilingi trilioni 31 maana yake bajeti hii ni shirikishi kuanzia Serikali za Mitaa, watu wamepanga kwa mfumo wa O&OD, wakaibua, wakapanga, tukapitisha kwenye Halmashauri zetu, zikapita kwenye process nzima za kibajeti mpaka Serikali mkaja Bungeni mkasema kwamba bajeti ni shilingi trilioni 31. Sasa muone mnavyojikanganya, hii shilingi trilioni 31 ni pamoja na mapato ya ndani ya Serikali za Mitaa kwa sababu bajeti imeanzia kule chini. Halmashauri zetu zimesema zitakusanya ushuru mbalimbali kama mapato ya ndani baadaye mkafanya compilation mkatuletea bajeti ya shilingi trilioni 31 lakini mnatuletea bajeti ya shilingi trilioni 31 huku nyuma mnafuta vyanzo vingi vya Serikali za Mitaa ambavyo tayari mmeshaweka kwenye bajeti yenu. Mheshimiwa Waziri hiki unachokisema shilingi trilioni 31 hautakaa utekeleze kwa sababu umesahau vyanzo vingine umevifuta wakati viko kwenye bajeti ya Halmashauri zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unatuambia bajeti zimefutwa, kwanza kuanzia miaka ya 2000-2010 Serikali mlifanya maboresho ya Serikali za Mitaa kwa kuziboresha kwa kuweka mfumo ya O&OD, mkasema mnagatua madaraka, mnaziachia Serikali za Mitaa ziwe na madaraka kamili, zikusanye mapato yake, zijiendeshe, leo mmegeuka baadhi ya mapato mnayachukua, mengine mnayafuta bila kuzishirikisha Serikali za Mitaa, hamtambui umuhimu wa Serikali za Mitaa? Mheshimiwa Waziri Serikali za Mitaa ziko kwa mujibu wa Katiba ya nchi kwanza mnavunja hata hii Katiba ya nchi. Leo umekuja unatuambia umefuta ushuru wa huduma (service levy), Halmashauri zetu nyingi jamani zinategemea ushuru wa hizi guest house na zimeshaweka kwenye bajeti yake. Leo unafuta ada ya machinjio, Halmashauri zetu ndiyo zinategemea ipate hizo ada, umefuta ada ya makanyagio minadani Halmashauri nyingi za vijijini ndiyo zinategema hii ada, umeondoa kodi ya mabango umeichukua umepeleka TRA halafu unasema utazirudisha, hamrudishagi mnatudanganya kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnasema mmepunguza ushuru wa mazao kutoka asilimia tano mpaka asilimia mbili kama ni mazao ya chakula na biashara lakini Mheshimiwa Waziri unasahau kwamba Halmashauri zetu tayari zilishaweka fedha hizi kwenye bajeti yao kwa nini mnawadanganya Watanzania? Halafu nitashangaa sana Waheshimiwa Wabunge wa CCM mkiendelea kusema mnaunga mkono hoja, Halmashauri zenu mtaona tukianza mwaka wa fedha hazitakuwa na fedha kwa sababu vyanzo vingi vimefutwa na Serikali Kuu na tayari walishaweka kwenye bajeti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mnaenda kuua Serikali za Mitaa au basi mseme kwamba Serikali za Mitaa hazipo tena, mfanye vitu vyote. Mmekuwa mkiahidi mara zote kwamba mtarudisha hizo fedha na hamjawahi kurudisha. Mheshimiwa Susan Lyimo amesema hapa Kodi ya Majengo tu, mliahidi mtarudisha hamrudishi hata senti tano. Sasa Serikali za Mitaa zitawezaje kwenda kujitegemea na kufanya shughuli zake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie Kodi ya Majengo. Serikali ya Awamu ya Tano mlichukua kodi hii ya majengo mkasema TRA inakusanya. Juzi niliuliza swali la nyongeza hapa Bungeni kwa Mheshimiwa Waziri Simbachawene, nikataka kujua kauli ya Serikali ni majengo yapi hasa ambayo yanatozwa kodi hii kwa sababu kwenye Wilaya zetu mpaka nyumba za tembe, nyumba za udongo zinatozwa kodi hii. Mheshimiwa Simbachawene akanijibu hapa akasema majengo yatakayotozwa kodi ni yale yanayotengeneza faida kwa maana ya nyumba zinazofanya biashara. Mheshimiwa Waziri wa Fedha ukasimama ukaniambia kuwa subiri bajeti yangu tutasoma, sasa hii bajeti yako ukurasa wa 48 inasema hivi; “Serikali itatoza Kodi ya Majengo kwa nyumba zote kwa viwango vitakavyopangwa na Waziri na Fedha na Mipango. Nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini zitatozwa kwa kiwango maalum (flat rate) cha shilingi 10,000 kwa nyumba na shilingi 50,000 kwa nyumba za ghorofa kwa kila ghorofa.” (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi ni zile ambazo hazijafanyiwa uthamini, kati ya shilingi 10,000 mpaka shilingi 50,000, acha zile zingine ambazo zitafanyiwa uthamini. Mheshimiwa Waziri hamuoni ninyi wenyewe mnajikangaya kwenye kauli zetu? Mheshimiwa Simbachawene amesema ni zile ambazo zinaingiza faida, akasema unaweza kwenda vijijini ukakuta mtu ana guest house na kadhalika huyo sawa atozwe kodi lakini wewe unasema nyumba zote, maana yake unasema hata za tembe nazo zitozwe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu mnasema hii ni bajeti ya kuwakomboa Watanzania au kuwanyonya Watanzania? Mnathubutu kusema kwamba hii bajeti haijawahi kutokea ni bajeti ya karne, hii haiwezekani hata kidogo. Nitawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wa CCM mkasome tena upya hii bajeti yenu ambayo mnasema eti inaenda kumkomboa Mtanzania wakati siyo kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la Road License. Wamepongeza sana hapa Wabunge wenzetu wa upande wa pili lakini tunajiuliza hivi ni Watanzania wangapi kati ya Watanzania milioni 40 ambao wana own magari? Inawezekana ni asilimia tano ya Watanzania wote, sasa asilimia tano ya Watanzania wote hawa leo mmewaondolea Road License ambayo watalipa kwa mwaka, mnasema mnapeleka kodi hii kwenda kutozwa kwa shilingi 40 kwa kila lita moja ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunafahamu ukiweka ongezeko lolote kidogo kwenye kila lita ya mafuta nchi hii, kila kitu kinapanda bei. Kwa sababu mafuta yanahusiana moja kwa moja na masuala mengine, utakuta bidhaa zinapanda sokoni, ukisafirisha mazao bei inapanda na kila kitu. Sasa kwa nini tuwaadhibu Watanzania wengine walio wengi ambao hawamiliki vyombo vya moto kwa sababu hawalipii Road License halafu tunawaacha hawa asilimia 5 tu tunawapa msamaha huu wakati itawagharibu Watanzania walio wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Serikali ya Awamu ya Nne ya JK...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu iliyowasilishwa na Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua Tanzania ni nchi ambayo imeingia katika Mfumo wa Vyama Vingi na hayo yametamkwa na yapo katika Katiba yetu. Kama tunatambua Mfumo wa Vyama Vingi, maana yake tunaamini kwamba Serikali inatambua vyama vilivyopo ambavyo vinaunda huo Mfumo wa Vyama Vingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri Mkuu ameeleza kwamba tuko kwenye Mfumo wa Vyama Vingi takriban miaka 23 leo; na vyama hivi vimeendelea kukua kadri miaka inavyoendelea. Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani inaonesha jitihada kubwa sana za kuua vyama hivi kwa kuvinyima haki yake ya msingi ambayo inapaswa kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Uwepo wa vyama hivi unatambuliwa na sheria, ufanyaji wa kazi wa vyama hivi umetamkwa katika sheria. Maana yake Vyama vya Siasa vinatakiwa viendelee kufanya kazi ya siasa kwa kuhakikisha vinaendelea kupata wanachama kadri inavyowezekana na kadri ambavyo miaka inazidi kwenda. Haya yamesemwa na Waziri Mkuu katika hotuba yake ukurasa wa 10, amesema:

“Katika kipindi hiki tumeona ushiriki wa Watanzania katika siasa ukiendelea kuongezeka na uhuru wa kujiunga na vyama vya siasa umeendelea.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unajiuliza, kama Vyama vya Siasa ili viendelee kupata wanachama, maana yake ni lazima vifanye mikutano ya hadhara kunadi na kueleza sera zake, ndivyo ambavyo mwananchi ataamua sasa ajiunge na chama hiki au aende chama hiki au asiwe na chama mpaka pale ambapo ataweza kuridhika kuamua kujiunga na chama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naeleza kwamba ili Mheshimiwa Waziri Mkuu tukuelewe kwenye kauli hii kwamba vyama hivi vinaendelea kufanya kazi yake, halafu huku mmebana uwepo wa mikutano ya hadhara, ni kwa uhakika mnalidanganya Taifa hili na mnawadanganya Watanzania. Utaendeleaje kupima kwamba Chama cha Siasa kinakua kama hakifanyi mikutano ya hadhara ikaongeza wanachama? Vyama vya siasa ni kama Makanisa leo mtu anajiunga, kesho anatoka. Ndivyo hivyo.

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu wanisikilize vizuri, naongelea Vyama vya Siasa. Siongelei Mbunge wala Diwani. Kwa hiyo Mheshimiwa Vuma naomba unisikilize vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama mnakataza Vyama vya Siasa visifanye mikutano ya hadhara, hamwezi leo kuja hapa Bungeni na kutuambia kwamba vyama hivi vimeendelea kufanya vizuri miaka 26 iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma, waasisi wa nchi hii walituaminisha Watanzania kwamba tuna maadui watatu wa nchi hii; umasikini, ujinga na maradhi. Kwa yanayoendelea leo, jambo lingine limeongezeka kwa Serikali iliyopo madarakani, adui mwingine ni Vyama vya Siasa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema haya? Kwa sababu leo tunashuhudia Waheshimiwa Wabunge mbalimbali na Madiwani mbalimbali kila siku ama wanaripoti Polisi au wanakamatwa wanaingia Polisi, wanakaa ndani, waliowaweka ndani wakiridhika kwamba sasa wamekaa ndani kwa muda, wanaachiliwa wanaendelea. Kila leo, ama kuripoti Polisi au kwenda Mahakamani. Hapa tuna Wabunge wengi wana kesi kila kukicha, wanahudhuria Mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba Vyama vya Siasa vya Upinzani ni adui mwingine ambaye mmemwongeza. Kwa nini nasema haya? Tumeshuhudia pia kwenye chaguzi ndogo zilizofanyika za marudio, kwanza tumefanya Uchaguzi Mkuu 2015, wananchi wameamua kwa ridhaa yao kuchagua mwakilishi wa chama chochote ambacho walikipenda kwa wakati huo na wakawaweka madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, humu ndani tuna Wabunge wanaotokana na CCM, tuna Wabunge waaotokana na CHADEMA, tuna Wabunge wanaotokana na CUF, tuna Wabunge pia wa NCCR na ACT. Ni ridhaa ya wananchi kwenye maeneo yao wakawachagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kiongozi mmojawapo wa CCM anazunguka kuwarubuni na kuwanunua baadhi ya viongozi na Wawakilishi hao ambao wamechaguliwa na wananchi, wanasema wanaunga jitihada wanaingia upande wa pili labda inawezekana ikawa ni haki yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba hawa ambao wanarudi upande wa pili inatulazimu kurudi kwenye uchaguzi. Hapa Bungeni tulipitisha shilingi bilioni 4.7 kwa ajili ya Tume ya Taifa Uchaguzi kwa uchaguzi wa dharura endapo itatokea Mwakilishi yeyote amefariki au kwa namna yoyote ameacha nafasi ile. Leo baada ya hizi chaguzi ndogo, tumetumia shilingi bilioni 6.9.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajiuliza, hivi tunafanya kazi ya kurubuni na kununua wahame upande wa pili; tunarudi tena kutumia fedha za walipa kodi kwenda tena kufanya uchaguzi, huku kuna Watanzania wengi ambao hawana huduma muhimu za kimsingi za kijami! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajiuliza…

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachozungumzia hapa ni bajeti tunayoitumia bila ulazima wowote. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ulinde muda wangu, naomba unilinde ninapochangia. Kama kuna Mbunge anataka kunijibu, asubiri akipata nafasi na yeye ajibu ninayoyasema. Halafu najiuliza, haya ninayochangia hapa, kama hamjayafanya kwa nini mnahangaika, si msubiri niseme? Kwa nini mnahangaika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu hapa ni utumiaji mbovu wa fedha za wananchi. Kama tulitenga fedha za dharura endapo kutatokea chaguzi, shilingi bilioni nne, leo tumetumia shiligi bilioni 6.9, kwa nini tusingefikiria kuendelea ku-save hizi hela na kuzielekeza kuliko kurudisha wananchi kufanya chaguzi tena kwa sababu watu wameamua kununua watu na warudi upande wa pili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata chaguzi za marudio zilipofanyika, tumeshuhudia ukiukwaji mkubwa wa taratibu nzima za uchaguzi. Uchaguzi huu tulipofanya tumeshuhudia ilikuwa ni uchaguzi kati ya chama kilichosimamisha mgombea; mfano mimi nilienda Siha, nilienda uchaguzi mdogo wa marudio Jimbo la Arumeru Magharibi, tumeona ni uchaguzi kati ya CHADEMA na Jeshi la Polisi. Nilishuhudia Wakala anatekwa Kituoni, Polisi yupo, hakemei, hasemi kitu; hakuna anayezungumza, maana yake tumeingia kwenye uchaguzi kati ya Vyama vya Upinzani na Jeshi la Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu inaonekana mmeongeza adui mwingine ambaye hamtaki kumsikia wala hamtaki kuona Vyama vya Siasa hasa vya upinzani vikifanya kazi yao, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa Serikali yako, ni kuleta marekebisho ya Katiba hapa Bungeni tufute Vyama Vingi ulimwengu ujue, dunia ijue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitaki kabisa Mfumo wa Vyama Vingi, turudi kwenye mfumo wa chama kimoja. Nadhani hiyo ndiyo itakuwa njia sahihi na mtaendelea kufanya mnayoyafanya kwa kadri ambavyo mtataka.

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba tu kumwambia Mheshimiwa Mwigulu kwa sababu unaingia kwenye Cabinet, naomba upokee ushauri wangu kumwambia Mheshimiwa Rais Magufuli, tufute Vyama vya Upinzani nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, waasisi wa nchi hii walituachia tunu za Taifa zikijikita katika umoja, amani na haki, lakini leo tunashuhudia katika nchi hii hakuna umoja. Umoja ule ambao umejengwa na hawa viongozi ambao walitutoa nchi kwenye utumwa na kwenye ukoloni wakatufikisha hapa tulipo, umoja ule haupo. Kwa nini haupo? Kwa sababu tunashuhudia matamko mbalimbali ya viongozi wakiligawa Taifa. Wakiona wananchi hawa wamevamia ardhi, wanasema hawa msiwabomolee kwa sababu walinipa kura; lakini wengine wanabomolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwalimu Nyerere alituachia tunu ya umoja, lakini leo tunu hii inavunjwa, tuliachiwa amani na mmeendelea kuimba kwamba amani ipo, hakuna amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wana hofu. Leo tunashuhudia wananchi wanaopotea, wapo wanaouawa na wako wanaotekwa. Amani ambayo ni tunu ya nchi hii, haipo tena. Kumekuwa na vitisho vingi. Naona leo tunalijenga Taifa kwenye hofu. Watanzania wana hofu. Tunu ambayo tumeachiwa na Waasisi wetu leo inavunjwa na viongozi na Serikali iliyoko madarakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeachiwa tunu ya haki. Haki hii inatiliwa msisitizo kwenye Katiba ambayo ni sheria mama. Katiba inatoa msisitizo wa haki ya Mtanzania kuongea kuonesha hisia zake ama kwa kuandamana ama kwa kuandika kwenye mitandao au kwa kusema chochote ilimradi asivunje sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo watu wanatishiwa, wanakamatwa, wanakuwa na hofu ambazo zimejengwa na watu walioko madarakani, wanachukuliwa hatua kinyume na taratibu, hakuna utawala wa sheria, hatuheshimu wala hatulindi tunu tulizoachiwa na Waasisi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoko mbele yetu kuhusu Mpango wa Maendeleo ya Taifa na nashukuru kwa kuwa mchangiaji wa kwanza jioni hii. Dhima ya Mpango wetu wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano ni kuangalia suala zima la uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchumi huu wa viwanda utaendana na ukuaji wa uchumi lakini na maendeleo ya watu. Tunajadili Mpango huo mwisho wa miaka mitano, ni mwaka wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilidhani ingekuwa ni vema sana Serikali ikajitathmini katika miaka minne ya utekelezaji wa Mpango; je, tumetekeleza kwa kiwango kipi, tumekwama wapi na tunafikiri nini turekebishe ili yale malengo tuliyojiwekea kwa miaka mitano sasa tuuweke kwenye Mpango huu ambao umebaki wa mwaka mmoja ili kufidia kuziba mapungufu yaliyojitokeza katika Mpango uliopita. Nilidhani wangefanya hivi ingeweza kusaidia sana kujipima kwamba, katika miaka mitano mipango yetu ya miaka mitano ni kiwango gani tupo na tunaendelea vipi, hali yetu ya uchumi ikoje, maendeleo ya watu wetu kwa ujumla yakoje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni dai la muda mrefu hasa Kambi ya Upinzani, tumekuwa tukidai sana kuwepo na sheria ya kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Taifa. Tumedai muda mrefu na hii sheria itasaidi mfano tukifanya tathmini tukaona kuna upungufu fulani na upungufu kama unahitajika kuzibwa na sheria, basi ni muhimu sasa tukawa na sheria ya utekelezaji wa Mpango huu. Tukiwa na sheria hii maana yake pia tutakuwa na uwajibikaji wa kutosha kwa watekelezaji wa Mpango huu lakini tutasaidia kufanya reallocation mbalimbali za bajeti ambazo ziko nje ya mpango. Maana yake mpango ule ambao utakuwa umepitishwa Bungeni kama tutakuwa tuna sheria kwa kiwango kikubwa itaziba hii mianya mingine ya kuibua miradi mingine au mipango mingine mingi mingi ambayo kwa kweli kwa kiasi kikubwa inaenda kuathiri bajeti ambayo tumejiwekea au bajeti ambayo imepitishwa hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kama nilivyosema tukiwa na sheria kutakuwa na uwajibikaji wa kutosha, Serikali itawajibika kwa kuhakikisha kwa kweli mipango inatekelezwa kwa kiwango kikubwa na kwa asilimia hata mia moja ikiwezekana inaweza kufikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kutokutekelezwa kwa miradi ya maendeleo. Tumeona, tunashindwa kutekeleza baadhi ya miradi ya maendeleo kwa sababu tunakuwa na mipango mingi ambayo haiendani na bajeti, haiendani na makusanyo yetu ya ndani, lakini tunakuwa na mipango mingi na miradi mingine mikubwa ambayo kwa kweli kwa kiwango kikubwa hatutaweza kutokana na fedha zetu kutekeleza. Ndiyo maana nikatoa rai hapa mwanzo kwamba ni lazima tufanye kwanza tathmini tuone tumejikwaa wapi, tumeshindwa nini ili tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona pia Bunge limekuwa likiidhinisha bajeti hapa lakini utekelezaji wa bajeti hiyo hasa kwenye miradi ya maendeleo kwa kweli ni kiwango cha chini sana. Ukirejea hotuba ya Kambi yetu ya Upinzani inaeleza mfano, kwenye Wizara ya Kilimo na Sekta nzima ya kilimo. Tukielewa umuhimu wa Sekta ya Kilimo hapa nchini tunajua ndiyo watanzania wengi wanategemea kilimo lakini kilimo hiki ndiyo tunategemea. Kama tunataka viwanda maana yake tunategemea kilimo tupate malighafi, viwanda viweze kuendelea na hatimaye hicho tunachokisema kwamba tunataka uchumi wa viwanda ili kuchochea maendeleo ya watu na hali ya uchumi kwa ujumla tuweze kufikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutakuwa hatutekelezi miradi ya maendeleo, kama tutakuwa Bunge lako linaidhinisha bajeti hapa halafu hazifiki kwenye wizara husika maana yake tutakuwa hatupigi hatua tunarudi nyuma. Kwa hiyo, ni muhimu sana sana tukaangalia kuwa na miradi michache ambayo tunajua tunaweza kutekeleza na miradi hiyo ikapitishiwa fedha hapa Bungeni na kwa kweli ikatoka kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, ukienda kwenye Wizara ya Kilimo, ukienda kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ukienda kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara, wizara zote ambazo zinafungamana na hicho ambacho tunakitaka, uchumi wa viwanda zote fedha zake za miradi ya maendeleo kwa kweli hazijafika hata asilimia 60, 70 au asilimia 100. Kwa hiyo, ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine, Serikali sasa hivi inatekeleza miradi mikubwa mitatu, kuna Stiegler’s Gorge, kuna SGR na ununuzi wa ndege, hii yote ni miradi mikubwa ambayo inahitaji fedha nyingi. Sasa tunakuwa na miradi mikubwa kwa mara moja ambayo inahitaji fedha nyingi maana yake ni kwamba fedha zozote zinazopatikana zinaenda kwenye miradi mikubwa. Halafu huku kwingine kwenye miradi midogo midogo ambayo kwa kiwango kikubwa ina mgusa mwananchi wa kawaida haifikiwi na hatuwafikii watu wa kawaida. Kwa hiyo, rai yangu kwa Serikali kwamba mnapokuwa na miradi mikubwa mje na mkakati wa ziada wa kuonesha ni namna gani miradi mikubwa inaweza ikatekelezwa, ni namna gani itakuwa financed ili miradi hii iweze kutekelezwa. Ni muhimu sana ili tusiweze kuathiri mambo mengine, utekelezaji wa miradi mingine ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali ndani ya nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirudi kwenye Serikali zetu za Mitaa kuna hali mbaya sana. Tuligemea kwamba, na tunategemea kwamba Serikali za Mitaa ndiyo kwa kiwango kikubwa ndiyo wananchi wako kule, ndiyo kwa kiwango kikubwa tunategemea miradi muhimu ambayo inamgusa mwananchi mmoja mmoja; maji, barabara, kilimo, masoko, kwa kiwango kikubwa mwananchi kule kwenye Serikali za Mitaa ndiyo inamgusa. Serikali za Mitaa hizi sasa hivi zimekuwa hoi bin taabani, hakuna kitu, fedha zote za makusanyo zimebebwa. (Makofi)

T A A R I F A

MWENYEKITI: Mheshimiwa Keissy taarifa nimekuona.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba anasema Serikali yetu haipeleki miradi katika wilaya. Tangu uhuru haijajengwa hospitali za wilaya 67, tumejenga zahanati hazina hesabu, sasa nashangaa anasema hatupeleki wakati miaka yote 45 sijui hakuna… kama Namanyere tulikuwa hatuna hospitali ya wilaya acha kwake. Juzi ametoa hospitali ya wilaya pale Ubungo tena kwa mpinzani, sasa anasema wapi hatupeleki miradi midogo midogo!

MWENYEKITI: Amesahau kidogo unajua tena hayo mambo, Mheshimiwa Cecilia si unajua alikuwa kwenye utaratibu maalum! Mheshimiwa Cecilia. (Kicheko)

Tunatumaini mjukuu hajambo! Endelea Mheshimiwa Cecilia. (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante taarifa ya Mheshimiwa Keissy siipokei na siipokei kwanini! Ukifanya tathmini kwa sababu si toka tumepata uhuru nchi hii inaongozwa na Chama cha Mapinduzi, nchi hii ndiyo inakusanya kodi. Ukifanya tathmini toka tumepata uhuru mpaka leo yaani tulipaswa Tanzania hii kuwa ulaya, kama kwingine maana yake ni tumechelewa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unapoongelea Namanyere ndiyo wamepata hospitali ya wilaya wamechelewa sana, walipaswa wapate kwenye miaka labda ya 80 huko, 70, miaka ya 90 mnaongelea habari za hospitali za rufaa kwenye maeneo yenu sasa namna gani ya kuboresha. Kwa hiyo, kwa mtazamo wa kwamba ipo inafanyika, imechelewa kufanyika, ilipaswa ifanyike mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niendelee kwenye Serikali zetu za Mitaa nadhani ni rai sasa kwa Serikali kuzitazama upya Serikali zetu za Mitaa, vile vyanzo vingi ambavyo mmevinyang’anya mvirudishie ili viweze kujiendesha. Namna gani itaendesha, namna gani itatumikia wananchi, leo kuna baadhi ya halmashauri hata Vikao vya Baraza la Madiwani kwa mujibu wa sheria havifanyiki kwa sababu hakuna fedha, havifanyiki kwa sababu mapato ni madogo, yale yanayopatikana kidogo yanachuliwa. Siyo tu kuchukuliwa wakati mwingine maagizo yanayokuja kwa kiwango kikubwa kinaenda kufanya nini, kuharibu bajeti ambayo imewekwa kwenye Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, bado Serikali zetu za mitaa zina hali mbaya zinapaswa kwa kweli kwa kiwango kikubwa kubebwa na kusaidiwa na kurudishiwa fedha zile ambazo zitakusanywa na Serikali Kuu, zinazotakiwa kurudi kwa mujibu wa sheria zikarudi zikatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo machache, nashukuru sana kwa nafasi ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo wa malipo wa maji wa pre-paid ukisimamiwa vizuri utaleta tija kubwa na uendelevu wa Mamlaka na Bodi mbalimbali za Maji hapa nchini. Wilaya ya Karatu ni miongoni mwa Wilaya za kwanza kuwa na mfumo huu na mafanikio yameonekana. Je, ni kwa nini Serikali isihakikishe Mamlaka za Maji kwenye miji mikubwa zinaanzisha mifumo hii ambayo itasaidia kufanya mamlaka hizi kuwa endelevu? Nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa ni migogoro ya muda mrefu hapa nchini. Serikali haijaonesha mikakati ya dhati ya kumaliza migogoro hii. Mara nyingi Wabunge wameitaka Serikali imalize migogoro hii iliyodumu kwa muda mrefu, kuwepo na mipango sahihi ya ardhi, hakika kutapunguza migogoro hii. Naishauri Serikali kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali pamoja na Halmashauri za Wilaya ziweke bajeti inayotosheleza na inayotekelezeka ili zoezi la upangaji wa matumizi bora ya ardhi liweze kufanyika au kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pembejeo za kilimo na mbolea; kumekuwa na tatizo la ucheleweshaji wa mbolea kwa wakulima hasa msimu unapoanza. Ucheleweshaji ni jambo moja ila hata mbolea halisi inayohitajika na wakulima kulingana na ardhi zao ni tatizo lingine. Tatizo hili ni kubwa sana na linaleta athari kubwa kwa wakulima.
Kwa kuwa Viwanda vya Mbolea ni vichache na kwa kuwa kilimo ni jambo endelevu na hitaji katika maisha ya kila siku ya wananchi wetu, nashauri Serikali iwe na mpango wa muda mrefu wa kuwa na viwanda vya mbolea ambavyo vitaendeshwa na Serikali ili kuondoa na kupunguza kabisa urasimu na upatikanaji wa mbolea hapa nchini.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa kuwasilisha hotuba yake nzuri inayoonesha mwelekeo mzuri wa kuletea maendeleo Taifa letu. Pia nimpe changamoto kwamba ajitahidi kwa sababu Wizara hii ndiyo Wizara ambayo iko kwenye kioo cha kila mtu. Kwa hiyo, akifanya kweli ataonekana na asipofanya ataonekana hata kabla ya kuja hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kuchangia kuhusu hali ya anga la Tanzania. Kwa uono wangu kimataifa tunajulikana Tanzania tuna anga la Tanzania, hakuna anga la Zanzibar wala anga la Tanzania Bara. Hivyo basi, ni muhimu tunavyotoa huduma za anga tuzijenge kulenga kufanikisha kwa sifa ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kirefu sasa kumekuwa na mawasiliano ya muda mrefu kati ya TCAA na Mamlaka ya Kiwanja cha Ndege cha Zanzibar. Kiwanja hiki kwa muda mrefu hakijafungwa kifaa cha Instrument Landing System (ILS) ambacho kilikuwa kifungwe kipindi cha miaka minne, mitano iliyopita, kila siku ahadi inakuwa kitakufungwa. Kweli huduma za ndege zinaendelea lakini hiki ni kifaa muhimu kinachowasaidia marubani kutua wakati wa usiku, mawingu na mvua kwa uhakika na usalama zaidi.
Niombe basi Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atuambie kama hili jukumu si la TCAA, ni bora watoe kauli dhahiri inayosema kwamba hiki kifaa hawatakifunga na hakiwahusu ili sasa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iweze kuchukua jukumu la kutafuta hicho kifaa na kukifunga kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri vitu kama hivi vikawa vinatupwa kama mpira. Ni bora kuambizana ukweli ili kila mtu afahamu jukumu lake, lakini litekelezwe ili kuleta ufanisi wa kazi tunazozifanya za kila siku. Tukipata sifa ya anga, nasema mara ya pili, ni sifa ya Tanzania na likitokea tatizo bado mamlaka hizi zitahusika na kutakiwa kujibu maswali ambayo kwa kweli nahisi hayatakuwa muhimu na ya msingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nichangie hilo lakini nimkumbushe Mheshimiwa Waziri akisaidie kiwanja hiki cha ndege cha Zanzibar. Nakumbuka lilitolewa jibu lakini nimsisitize tu awasaidie kulipwa lile deni lao la shilingi milioni 230 na ATC. Tunasikia au tumeambiwa madeni yatahamishiwa Hazina, lakini nimuombe tu alipe uzito ili kuwasaidia wenzetu hawa kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliomba dakika tano na nahisi zimenitosha kwa kuchangia jambo hili muhimu sana. Na mimi naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini kuna mabonde yenye mchanga ambapo siku za awali (nyuma) umiliki huo ulikuwa chini ya vijiji husika na kuwezesha vijiji hivyo kupata mapato.
Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, Wizara ya Nishati na Madini imebadili utaratibu huo na kukabidhi mabonde hayo kwa mawakala mbalimbali ambao wamekuwa wakitoza tozo tofauti kwa kila eneo na wakati mwingine mawakala hawa hutoza tozo hizi katika barabara kuu kwa kuweka road blocks kwa kushirikiana na askari wa barabarani. Kwa kuwa utaratibu wa tozo hizo ni chanzo cha mapato ya Halmashauri za Vijiji na wameweka katika by laws zao; na kwa kuwa utaratibu huo mpya haujawashirikisha vijiji husika, je, Serikali haioni upo umuhimu wa kupitia upya utaratibu huu kwa manufaa ya Serikali za Vijiji hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Karatu ni mji wa utalii kwa kuwa ni lango kuu la kuingilia Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro. Tukitambua mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika nchi yetu lakini baadhi ya vijiji katika Wilaya ya Karatu havina umeme. Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Vijiji vya Buger, Gongali, Endamanghang, Kansay na baadhi ya vijiji katika Mji wa Karatu?
Mheshimiwa Naibu Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyowasilishwa na Waziri Mkuu hapa Bungeni. Na mimi nitaanza mchango wangu kwa kujielekeza katika ugonjwa huu wa Corona.

Mheshimiwa Spika, watu wamekuwa na mitizamo kwamba ugonjwa huu siyo wa kutisha sana ukilinganisha na ugonjwa mwingine kama UKIMWI, kansa na magonjwa mengine. Hata hivyo, ni ukweli kwamba ugonjwa huu wa Corona unatisha sana kuliko magonjwa mengine kwa sababu ya njia ya uambukizaji wa ugonjwa wenyewe na unatishia uhai wa binadamu na umesababisha vifo vingi katika mataifa mbalimbali ulimwenguni tena kwa muda mfupi sana.

Mheshimiwa Spika, bado hatujaona jitihada za dhati za Serikali za kuhakikisha ugonjwa huu unadhibitiwa. Tumeambiwa na wataalamu na tumeona kwamba tunawe mikono, kwa kweli tunajitahidi kunawa mikono hata Watanzania wananawa sana mikono popote walipo. Tumeona shule na vyuo vimefungwa na mambo mbalimbali ikiwemo makongamano, semina, michezo mbalimbali vyote zimeahirishwa ili wasipate maambukizi haya ya Corona.

Mheshimiwa Spika, hiyo ni hatua moja lakini bado hatujaona hatua nyingine katika maeneo yenye misongamano mikubwa mfano stand za mabasi, mabasi yanayotoka mikoani yanaingia kwenye miji mikubwa, kwenye mabasi kuna misongamano na tumeambiwa ugonjwa huu unaambukizwa kwa njia ya hewa. Sokoni tunakoenda bado kuna misongamano mikubwa sana. Kwenye magereza yetu kuna misongamano, magereza yetu yamejaa kupitiliza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukumbuke pia tuna cell zetu polisi ambazo wahaalifu kila siku wanaingizwa. Cell za polisi kwa utamaduni uliopo zinajaza wahalifu kupitiliza na hawapimwi. Mfano muhalifu akipatikana leo wala yeye hatawekwa kwenye chumba kingine cha karantini kwa siku 14 halafu achanganywe na wahalifu wengine kwa sababu hatuna hata hivyo vyumba vya kuwahifadhi katika vituo vyetu vya polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika,ndiyo maana nikasema hatua za awali zilizochukuliwa kukabiliana na ugonjwa huu bado hazitoshi, tunahitaji jitihada kubwa sana za kukabiliana na ugonjwa huu kwa sababu ya namna ambavyo unaambukizwa na jinsi ambavyo tumeona katika nchi za Ulaya, Marekani na China watu walivyokufa. Siyo huko tu, tujiangalie hata katika block ya Afrika Mashariki jinsi ambavyo ugonjwa huu umeweza kuuwa watu wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa nini bado nasema Serikali inahitaji kujipanga sana kwenye ugonjwa huu wa Corona? Tuna maabara moja tu ambayo ndiyo inapima na kutoa majawabu ya watu walioathirika na virusi hivi vya Corona. Maabara hii ipo Dar es Salaam tu, hata hapa Makao Makuu ya nchi haipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tunajiuliza, kama mfano ikitokea kuna mgonjwa katika Wilaya ya Tanganyika labda kule Katavi au Kigoma mpaka sampuli iletwe Dar es Salaam itolewe majawabu, kama mtu huyu hajawekwa karantini huko aliko, kwa kweli tutakuwa tunajiweka kwenye wakati mgumu kama nchi. Serikali iliyopo madarakani nyie mmejipambanua kama ni Serikali wanyonge lakini tutawaonaje mkiwatetea wanyonge hawa wa Tanzania katika janga hili kubwa la Corona ambalo linauwa watu kwa upana mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, lakini bado tunahitaji kupata majibu na Serikali ituambie. Binafsi nilitegemea tulipoanza Bunge hili Serikali ingetuletea mkakati wa kina na wa dhati wa namna gani wanaenda kupambana na ugonjwa huu wa Corona. Tunajiuliza kama nchi hivi ongezeko likiwa kubwa, mpaka jana tumeona wagonjwa wamefika 20, tulikuwa na wagonjwa 13 leo wamefika 20. Tunajiuliza kama idadi hii ya maambukizi itaendelea kuongezeka, hivi tuna vitanda vya kutosha vya kulaza wagonjwa hawa? Tuna madawa ya kutosha kusaidia kama ambavyo wanafanya kwenye nchi nyingine, tunajua dawa haijapatikana lakini angalau kutibu katika zile hatua za awali? Je, tuna mashine za kutosha za kusaidia kupumua kwa wagonjwa hao? Kwa sababu tumeambiwa ugonjwa huu unashambulia mfumo wa upumuaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunajiuliza hivi tuna madaktari na manesi wa kutosha wa kuhudumia kama janga hili likiongezeka? Leo tuna upungufu wa asilimia 52 ya watumishi wa afya hapa nchini. Je, idadi hii ikiongezeka, hatuombi iongezeke kila mtu hapa anatishika kwa sababu ugonjwa huu ukija haijali wewe ni CCM, CHADEMA, CUF, Muislam au Mkristo, yeyote yule unaweza kumpata. Ugonjwa huu hauchagui mtu lakini tunajiuliza ni kwa namna gani Serikali mmejipanga tuone jambo hili linadhibitiwa kama ambavyo nchi zingine wameweza kudhibiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi na sijui kama Serikali mnakiri kwamba ugonjwa huu ukiendelea hapa nchini ni kwa hakika uchumi unakwenda kuanguka. Hili siyo la kubisha, uchumi wa nchi na wa mtu moja moja unaenda kuporomoka.

Mheshimiwa Spika,nitoe mfano, sekta ya utalii, mimi natoka Wilaya ya Karatu, tuna hoteli za kitalii 58, leo hoteli zinafungwa, wafanyakazi wanarudi majumbani, wengine wanarudishwa hakuna kazi tena mpaka pale ambapo hali itatengamaa. Hoteli hizo zinategemea watalii wengi kuja na watalii wetu wengi wanatoka nchi za nje na hawaji kwa sababu huko kwao tayari hali ni mbaya. Je, hapa hatujagusa uchumi wa mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa?

Mheshimiwa Spika,lakini leo tunapoanza tu kujadili bajeti ya nchi kwenye sekta ya utalii tu Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika mwaka 2018/2019 inaingiza shilingi bilioni 143, kwa hali hii ya Corona hizi fedha tunaenda kuzipata? Hatuwezi kuzipata. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, hapa hatujagusa uchumi wa mmoja mmoja na uchumi wa taifa? Leo tunapoanza hata kujadili bajeti ya nchi, kwenye Sekta ya Utalii tu, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika mwaka 2018/2019 inaingiza shilingi bilioni 143. Kwa hali hii ya Corona hizi fedha tunaenda kuzipata? hatuwezi kuzipata.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, naishauri Serikali kupitia Waziri wa Fedha, lazima atuletee mpango wa haraka hapa Bungeni wa namna gani ya kukabiliana na suala la uchumi wa nchi na uchumi wa mtu mmoja mmoja hasa kutokana na janga hili la Corona. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tusijifunze tu, tuangalie katika nchi za karibu tu hapa, kwa sababu kuna watu wanaosema kwamba tusitazame nchi zilizoendelea; Italy, Marekani na kadhalika. Hapana, hebu tutazame wenzetu wa jirani; Kenya na Uganda kwa hatua ambazo tayari wameshazichukua. Mfano tu mmoja, leo benki za Kenya zimetoa unafuu wa mikopo kwa siku karibia 90 kwa watu wao. Serikali ya Kenya imewataka wenye nyumba wawape nafuu wapangaji wasilipe kodi kwa kipindi fulani. Hii ni kwenda kumsaidia mtu mmoja mmoja kutokana na hali iliyoko. Sasa sisi kama Serikali ya hapa, watuambie wamejipangaje na jambo hili? Hili jambo halihitaji mzaha wowote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hapo hapo kwenye kuwasaidia wapangaji, tunashangaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam; kwanza mnakataza msongamano, yeye anaenda Mwenge, anaenda Ubungo, anakusanya watu, anaongea, anasema sijui naye anaanza kuongea na wenye nyumba wasamehe wapangaji. Hivi kweli tuko serious? Tumesema tufute misongamano yote kila mahali, kiongozi unaenda unakusanya watu.

Mheshimiwa Spika, halafu tunajiuliza, yeye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salam ndio amekuwa msemaji wa nchi hii? Suala la kuangalia namna gani wenye nyumba wanatoa unafuu kwa wapangaji, mimi nadhani lichukuliwe na Serikali lifanyiwe na…

SPIKA: Mheshimiwa Cecilia, nilidhani sisi Wabunge tungekuja na mapendekezo kwa Serikali badala ya kuitegemea Serikali peke yake ndiyo ifikirie halafu ije na mpango fulani. Pamoja na Serikali kutakiwa ikifirie, ije na mpango, lakini nasi tuwe tunapendekeza.

Nilikuwa nawaza tu, hili la kusema kwamba Serikali itoe amri, mwenye kajumba kake basi apangishe bure, sijui kama una nyumba yako halafu ipangishwe bure kwa sababu Serikali imesema, sijui kama… hebu weka sawa kidogo hili, maana yake, nilikuwa namwona Mheshimiwa Lema, maana yeye ni tajiri wa nyumba nyingi, sasa anasita hapo. Itakuaje hapo?

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nadhani hujanisikia vizuri, sijasema hivyo na nimeshauri kwamba Serikali ijifunze kwa majirani zetu katika bloc ya Afrika Mashariki jinsi wanavyofanya na tuangalie na sisi hali ya kwetu ikoje. Ndiyo maana nikashauri kwamba Waziri wa Fedha naye atuletee mpango wake kwa jinsi gani tunaenda kuangalia uchumi wa nchi utakavyoporomoka na hatua gani zitachukuliwa kwa uchumi wa nchi na kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja. Ndicho nilichosema. (Makofi)

SPIKA: Ndiyo ukatoa mfano kwamba Kenya imesema nyumba sijui imefanyaje.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. (Kicheko)

SPIKA: Si unaona lilivyo gumu. Haya endelea Mheshimiwa Cecilia. (Kicheko)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, kingine ambacho Serikali inapaswa kukifanyia kazi na kuchukua ushauri huu, kama tatizo litaendelea, ni kwa kiasi gani kama nchi tuna hifadhi ya chakula? Huo nao utakuwa ni mtihani mkubwa sana kwa sababu tunaelewa hali ya watu wetu. Watu wetu ni wa kwenda asubuhi…

SPIKA: Mwaka huu chakula kingi sana. Hata kabla Serikali haijasema, kingi kweli kweli! Hata Dodoma hatuombi chakula mwaka huu.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama unasema kingi, basi Serikali ituletee taarifa hapa Bungeni kwamba ni namna gani inaweza kukabiliana na hali ya upungufu wa chakula kama hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Corona itaendelea na ugonjwa wagonjwa wataendelea wengi? Sasa hilo litakuwa la msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimesema hayo kwa sababu tunaelewa watu wetu ni wa kwenda sokoni leo akanunue kitu kidogo apate riziki, siku iende kesho hivyo hivyo. Sasa kama ikifikia hatua wagonjwa wataongezeka, maana yake lazima tutaenda lockdown. Kama tutaenda kwenye lockdown, namna gani watu hawa tunahakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha?

Mheshimiwa Spika, Serikali yoyote duniani panapotokea majanga na milipuko, jamani kitu cha kwanza ni mwananchi. Uhai na afya ya mwananchi, mengine ndiyo yanafuata. (Makofi)

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Naambiwa tayari. Malizia hiyo sentensi yako ya mwisho.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali, bado Watanzania wanahitaji majibu na mikakati ya dhati, Serikali iwaambie Watanzania kwamba namna gani inaenda kukabiliana na ugonjwa huu wa Corona?

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya TAMISEMI na Utawala Bora na Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kueleza kwamba ni ukweli usiopingika hali za Halmashauri zetu nchini kwa ujumla wake ni mbaya sana. Halmashauri hizi zina hali mbaya kwa sababu nyingi zimekuwa tegemezi na kwa asilimia kubwa zinategemea fedha kutoka Serikali Kuu. Halmashauri zetu hizi pia vyanzo vile muhimu ambavyo vingewezesha mapato ya Halmashauri zetu kuongezeka, kwa kiwango kikubwa vimechukuliwa pia na Serikali Kuu. Kwa hiyo, tumeziacha Serikali zetu za Mitaa katika hali ngumu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine kuna uhaba mkubwa wa watumishi katika Serikali za Mitaa kwa maana ya rasilimali watu. Takwimu zinaonesha tuna uhaba wa watumishi 43,560 katika idara 470 za Halmashauri zetu nchini, huu ni upungufu mkubwa sana. Kama kuna upungufu huu mwisho wa siku hata ufanisi wa fedha zinazopelekwa unakuwa hauonekani au haupo kabisa au ufanisi unakuwa kwa kiwango kidogo sana.
Kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali ikaangalia ni namna gani wanakwenda kupunguza uhaba wa watumishi walioko katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine unapoongelea suala la Serikali za Mitaa huwezi kuwaacha Madiwani pembeni. Ni kwa muda mrefu Serikali mmewatelekeza Madiwani si kwenye maslahi, si kwenye kujengewa uwezo, Madiwani maslahi yao yanaboreshwa kwa kiwango kidogo sana. Ukiangalia sisi Wabunge hatuna utofauti sana na Madiwani lakini tunawaacha Madiwani na sisi tukiwa Bungeni muda mrefu wanaotufanyia kazi kwa kiwango kikubwa na kutusaidia ni Madiwani. Ni muhimu sana Serikali ikaangalia namna gani maslahi ya Madiwani yanaboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si maslahi tu, wakati wa awamu iliyopita walifuta mafunzo (capacity building) kwa Madiwani. Hivi unampeleka Diwani akamsimamie Mkurugenzi na watendaji wake ambao wao ni wataalam wa mambo fulani fulani halafu Madiwani wetu wamechaguliwa tu kwa kigezo cha kusoma na kuandika, hana ujuzi wowote, baadhi lakini wako wengine ambao wana ujuzi lakini walio wengi hawana ujuzi huo, hivi kwa nini Serikali isiirudishe ile programu ya kuwajengea uwezo Madiwani kwa kuwapatia mafunzo. Mimi nilikuwa Diwani, nakumbuka kulikuwa kuna programu ya kuboresha Serikali za Mitaa, tulikuwa tunapelekwa mafunzo ya miezi sita lakini inakwenda kwa awamu, ilitusaidia kutujenga na kusimamia zile fedha zinazopelekwa. Kwa hiyo, ni muhimu pia mkalitazama hili muone namna gani Madiwani wanarudishiwa hizo programu za kujengewa uwezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuchangia kuhusu TAMISEMI ni udhaifu mkubwa ulioko katika usimamiaji wa Bajeti na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa. Kuna udhaifu mkubwa sana, udhaifu huu unaendana na bajeti zilizoidhinishwa kutokufuatwa na hizi bajeti wakati mwingine hazifuatwi kwa sababu ya matamko ya viongozi mlioko ngazi za juu na mlioko katika Serikali Kuu. Mfano, Halmashauri 34 zimetumia kiasi cha shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Hakuna mtu anayepinga au anakataa umuhimu wa maabara, umuhimu wa maabara unajulikana lakini ujenzi huu na fedha hizi zimetokana na tamko lililotolewa na Rais bila kuangalia wakati huo anatoa tamko kwenye bajeti za Halmashauri za Wilaya fedha hizi zipo? Kwa hiyo, inaonesha kuna shilingi bilioni 33 zimetumika kinyume na bajeti eti kujenga maabara katika shule zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, kuna takriban upotevu wa shilingi bilioni nane kwa ajili ya malipo yaliyofanywa na Serikali za Mitaa bila kuwepo na nyaraka za malipo. Pia kuna Halmashauri 62 zimefanya malipo ya shilingi bilioni 1.4 kinyume na vifungu vilivyopitishwa katika bajeti. Sasa kama Serikali hizi za Mitaa hazifuati bajeti ambayo imejiwekea hakuna sababu ya kupitisha bajeti au kama kuna matamko yanayotolewa bila kuangalia uhalisia wa Serikali zetu za Mitaa hakuna sababu ya kuwa na Serikali za Mitaa kama hatutambui na kuthamini yale ambayo yanayopitishwa katika bajeti zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti ya CAG anasema watekelezaji wa miradi 76 walifanya matumizi nje ya bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 4.6. Yote ni kukiuka bajeti waliyojiwekea, yote ni kukiuka Sheria ya Fedha ambayo ipo. Wanasema matumizi mengine yalifanywa nje ya bajeti na yameongezeka, CAG anasema matumizi nje ya bajeti yameongezeka kwa asilimia 224. Kwa hiyo, haya ni mambo ya kuyaangalia na kuyasimamia kuona yanaondoka katika Serikali zetu za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie eneo lingine la elimu bure. Mmesema mnatoa elimu bure, lakini nilidhani mngepaswa kujiridhisha na kuangalia hivi ni kweli mnaweza kutoa elimu bure au mlikurupuka tu mkachukua Ilani yetu na yenyewe mkaweka kwenye Ilani yenu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nasema hivyo, kuna watu wamefanya tafiti, wanasema ili uweze kutekeleza elimu bure unahitaji takriban shilingi bilioni 715 kwa mwaka mmoja wa fedha. Ili uweze kutekeleza elimu bure maana yake unahitaji mambo makuu manne; jambo la kwanza ni kutoa ile ruzuku ambayo ilikuwa inatolewa ya shilingi 10,000 kwa shule za msingi na shilingi 25,000 kwa shule za sekondari. Kama ile ruzuku mmeamua kuitoa kwa sababu mnasema ni elimu bure maana yake Serikali inahitaji karibia shilingi bilioni 130 kwa shule za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kama mnaondoa ada ya shilingi 20,000 kwa watoto wa sekondari, Serikali inahitaji kuwa na shilingi bilioni 31.5 ili kufidia ada hiyo. Hivi hizi fedha hizi mnazo? Si huwa mnasema kasungura kadogo? Safari hii kamenenepa? Nadhani mnapaswa kuangalia haya mliyoyasema ya elimu bure hivi mnakwenda kutekeleza? Halafu mmetoa Waraka mwingine Na. 5 wa elimu mnasema kama wanataka wapate kibali kwa Mkuu wa Mkoa, sasa kwa nini hizi contradiction, si mmesema elimu bure? Basi acheni bure mbebe huo mzigo, mtafute fedha hizi mwende kutekeleza elimu bure ambayo mnataka kuitekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa haraka ni kuhusu Mfuko wa Vijana na Wanawake. Waheshimiwa Wabunge wengi tunachangia kwamba tuhakikishe Serikali za Mitaa zinatenga ile 10 percent kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake lakini lazima kidogo twende mbali ya hapa. Mifuko hii ukiangalia mwongozo wake na mwongozo huu ulipitishwa na Bunge hili mwaka 1991, ni mwongozo wa zamani ambao hauendani na uhalisia wa leo.
Katika Bunge la Kumi niliuliza Swali Na. 379 kuitaka Serikali i-review ule mwongozo wa kuanzisha Mifuko ya Vijana na Wanawake, ni mwongozo wa zamani sana kwa sababu unasema kikundi cha watu watano watapewa mkopo wa shilingi 500,000. Hivi unawapa mkopo wa shilingi 500,000 kwa watu watano, shilingi laki moja moja inasaidia nini, haisaidii kitu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri ni vizuri mkaangalia tena kwa upya namna gani ya kuu-review mfuko huu uendane na hali halisi iliyoko katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kwenye Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, kuna Mfuko wa TASAF. Mfuko wa TASAF ni mkopo kutoka World Bank ambao ni dola za Kimarekani milioni 200 lakini fedha hizi zinakwenda kupewa watu kwenye kaya, wanasema kaya maskini na kwenye kaya maskini wanaangalia vigezo mbalimbali kama kuna wategemezi na vitu kama hivyo na kwenye kila kaya range ya fedha hizi ni kati shilingi 20,000 mpaka shilingi 62,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuwakwamua watu wetu kutoka kwenye hali mbaya ya umaskini hivi ni kuwapa fedha mkononi? Kwa sababu ukimpa fedha mkononi itamsaidia nini? Kwa sababu hizo hizo Kaya maskini wakati mwingine hata mlo kwa siku ni taabu, ukimpa shilingi 20,000/= unamwendelezaje aondokane na huo umaskini? Kwa hiyo, ni muhimu mkaangalia hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kumekuwa na mifuko mingi ambayo mwisho wa siku hatuoni manufaa yake.
MWENYEKITI: Mheshimiwa muda wako umeisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2016/2017, Wizara imeeleza kwamba inafanyia mapitio ya Sera ya Ardhi ya mwaka 1995. Mapitio haya yatakuwa hayana maana kama Wizara haitajikita kuimarisha mfumo wa utendaji wa vyombo vya usimamizi wa ardhi katika nchi hii. Hapa tunaongelea Serikali za Vijiji, pamoja na mabaraza yake ya ardhi maana yake hata kama ukiwa na sera lakini hujaviwezesha vyombo hivi ukavipa rasilimali fedha, ukavipa rasilimali watu, sera yao wanayokwenda kurekebisha itakuwa haina maana.
mamlaka hizi za usimamizi wa ardhi katika nchi yetu na kuimarisha mfumo mzima wa utendaji wa Wizara katika maeneo mbalimbali. Pamoja na marekebisho hayo ni muhimu tukaangalia masuala mazima ya wawekezaji au baadhi ya wawekezaji na viongozi na wanasiasa kuhodhi maeneo makubwa kinyume na taratibu au kuihodhi kwa kufuata utaratibu lakini wameya-damp na hawayaendelezi ni muhimu sana hili likatazamwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wawekezaji wengi baadhi yao wana-forge muhtasari wanalaghai Serikali zetu za Vijiji, wanahodhi maeneo na wanayatumia maeneo hayo kwenda kukopea benki na kudanganya au kudanganya kwamba wana mitaji lakini hawana mitaji, wanatumia ardhi hiyo kwenda kukopa benki wanafanya biashara nyingine wanatelekeza zile ardhi. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara ikatazama kwa ujumla wake suala zima la hawa wawekezaji, baadhi yao wamekuwa ni wadanganyifu wakubwa wakitumia ardhi zetu vibaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna baadhi ya wawekezaji wanabadilisha matumizi ya ardhi kinyume na hati miliki zao zinavyoeleza, kuna wawekezaji wanapewa kwa ajili ya kilimo, anakwenda kubadilisha. Nimpe mfano Mheshimiwa Waziri, Wilaya ya Karatu, kwa taarifa ambayo tumeletewa kwenye Baraza la Madiwani kuna mashamba ambayo yanamilikiwa na wawekezaji, yametembelewa mashamba 18 ambayo yana jumla ya hekari 13,985 wengi wao mashamba haya wamepewa kwa ajili ya kilimo cha kahawa, lakini wako baadhi wamebadilisha matumizi wamejenga hoteli kubwa za kitalii, hatuna uhakika kama wamefuata taratibu za sheria za kuomba kubadili matumizi ya ardhi ile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya ardhi ile inaonekana ni kilimo, lakini wako wengine wamejenga hoteli za kitalii maana yake ni nini? Maana yake ni pia wanaikosesha Serikali mapato, anakwenda kulipa tu kwa sababu inaonekana hati yake ni ya kilimo lakini amejenga hoteli kubwa ya kitalii analaza wageni, anapata fedha za kutosha. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara ikafanya uhakiki kutembelea mashamba, ambayo jumla yako mashamba 32 ndani ya Wilaya ya Karatu yakabaini ni watu gani ambao wamekiuka taratibu za kisheria katika umiliki wao wa ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia katika hao wawekezaji wenye mashamba 32, wako wengine wameyatelekeza mashamba, wako wengine wameyaacha, wamehifadhi halafu kuna wananchi wengi pembezoni pale hawana hata maeneo ya kuzika. Mheshimiwa Waziri ningetamani aje karatu aone. Yako mashamba yanamilikiwa na Wahindi, wananyanyasa watu, wanadiriki kuwaambia hata kaya zinazokaa pale, ni marufuku kuzaana eti kwa sababu wataongeza idadi, huu ni unyanyasaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa sana Mheshimiwa Waziri afike, aone jinsi gani wananchi hawa, hawana hata maeneo ya kuzikana sasa wananchi wanakuwa watumwa katika nchi yao, haiwezekani! Hatuwezi kuthamini wawekezaji, hatuwezi kuthamini watu hao tukawapuuza wananchi wetu ambao ni damu zetu. Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, suala hili liondoke na wananchi hawa wapate haki yao, wapate maeneo angalau hata kuweza kuzikana katika nchi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka niongelee ni kuhusu migogoro ya ardhi. Migogoro hii ya ardhi imekuwepo kwa muda mrefu na migogoro hii mara nyingi ni kati ya wakulima na wafugaji, hifadhi na wananchi, vijiji na vijiji na kadha wa kadha kama ambavyo imeoneshwa katika hotuba yetu ya Kambi ya Upinzani. Pamoja na kwamba bado tuna migogoro lakini imepungua sana, lakini inawezekana ikaendelea kuibuka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro hii pamoja na sheria tulizonazo, lakini ni lazima Serikali ijikite katika kuimarisha vyombo vya utatuzi wa migogoro ya ardhi na lazima Serikali iangalie namna bora ya kumaliza migogoro hii ya ardhi kwa njia shirikishi na kutumia mila na desturi za maeneo mbalimbali. Hatuwezi tu kusema wakati mwingine tunafuata sheria kama ilivyo, kwa sababu mkisema mnafuata sheria kama ilivyo, ndiyo mnaua watu, mnajeruhi watu, mnafukuza watu, wakati mwingine busara itumike kwa kutumia mbinu shirikishi ya kuondoa migogoro hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano migogoro ya wakulima na wafugaji inaweza wakati mwingine kusuluhishwa kwa kutumia, mila na desturi na njia shirikishi siyo unakwenda kusuluhisha migogoro hii kwa kuchimba sijui mitaro, sijui kwa kusema wasivuke huku, haiwezekani ni lazima mtumie njia shirikishi ambayo itaweza kuondoa migogoro ya ardhi katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala moja la umiliki wa ardhi. Wapo Watanzania wengi ambao hawana hati miliki na wako wachache ambao wana hati miliki. Sababu ambazo zinapelekea hili, wakati mwingine ni urasimu na mlolongo mzima wa kupata hati hizi, kuanzia kwenye Halmashauri zetu mpaka hizo Ofisi za Kanda ambazo zinatoa hati miliki. Pia, wakati mwingine kuna rushwa kwenye halmashauri zetu, Halmashauri kule kuna shida sana kwa hao Maafisa Ardhi. Hizi rushwa zinawanyima wananchi haki ya kupata ardhi yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali muandae programu maalum ya kuhakikisha mnakopesha wananchi, yaani kuliko mwananchi atafute fedha ya kuingia gharama ya hatua hizi mpaka apate hati, mnaonaje mkiwa na programu maalum, Serikali ikagharamia, mkawakopesha wananchi wakawa na hati zao, wakalipa kidogo kidogo mpaka akamilishe deni lile, ili tuhakikishe wananchi walio wengi wanapata hati, maana yake hati hizi wakipata mwisho wa siku wanalipa mapato, inakuwa ni sehemu ya mapato ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie jambo la mwisho, kuhusu ulipaji wa fidia pale ardhi inapotwaliwa. Jambo hili mmeeleza kwamba mmeanzisha Mfuko huu wa kutoa fidia ambayo itaanzia na bilioni tano. Ni muhimu sana Serikali ikawalipa wananchi fidia kwa wakati, ikawashirikisha wananchi katika…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia katika bajeti hii ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Mchango wangu wa kwanza utajikita katika suala zima la misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeendelea kushuhudia misitu yetu ikizidi kutoweka kwa kasi kubwa sana na hatujaona mikakati ya dhati ya Serikali kuhakikisha kunakuwa na misitu endelevu. Kuna takwimu ambazo zinaonesha national annual deforestation ni kati ya 0.8% mpaka 1.1%. Kwa kiwango kikubwa misitu hii inatoweka kwa shughuli mbalimbali ikiwemo shughuli za kilimo, uvunaji wa miti, moto na pia biashara kubwa ya mkaa. Ni vizuri Serikali ikatambua misitu hii leo tunaipoteza miaka 20, 30 ijayo nchi hii inaenda kuwa jangwa na hatujaona mkakati wa dhati kabisa wa Serikali kuhakikisha tunakuwa na misitu endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu kwamba tuna hiyo TFS ambapo jukumu lake kubwa ni kuhakikisha inasimamia na kutunza hiyo misitu ya asili. Hata hivyo, hii TFS imejikita katika kukusanya mapato zaidi bila kuwa na mipango endelevu ya misitu hii. Mheshimiwa Mbunge mmoja jana alichangia hapa akahoji hata mapato yenyewe yanakusanywaje na haya mapato yanayokusanywa kweli yana uhalisia? Ukichukua mfano, kuna tafiti zimefanywa, kwa Mkoa wa Tabora peke yake kwa mwaka wanazalisha magunia ya mkaa 2,244,050 wanapata shilingi bilioni karibu 21 kwa mwaka kwa shughuli za mkaa peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa za TFS wao wanasema makusanyo ya mkaa tu kwa mwaka ni shilingi bilioni saba, lakini Mkoa tu wa Tabora ni bilioni 21, kitaifa wanasema ni shilingi bilioni saba. Kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Waziri anapaswa ku-deal na hawa watu wa TFS, kuna tatizo hapa. Kuna watafiti wamefanya utafiti wanaonesha hizi takwimu mkoa mmoja wanaingiza fedha nyingi, lakini Kitaifa TFS wanasema ni shilingi bilioni saba tu. Wizara inatakiwa kuhakikisha wanaitazama vizuri hiyo TFS kwa sababu wao nadhani ama ni rushwa ama kuna watendaji ambao si sahihi wanakwamisha shughuli hizi za kukusanya mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishauri Serikali kwamba pia wasiitazame TFS katika kuhakikisha inawaletea mapato tu au kutoa vibali vya misitu na vitu kama hivyo. Ni muhimu TFS ikatekeleza majukumu yake kama dhamira ya uanzishwaji wa TFS ilivyokuwa katika taratibu zake za uanzishwaji. Ni muhimu sana Serikali mkatazama hawa TFS wanapotoa leseni, watoe leseni lakini hao wanaopewa leseni walete mpango mbadala au mkakati mbadala wa kuendeleza misitu yetu ili tuweze kuondokana na kutoweka kwa misitu kwa kiwango kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la migogoro ya mifugo inayoingia hifadhini. Waheshimiwa Wabunge sisi kama viongozi pia wakati mwingine ni lazima tuangalie kauli zetu zisije zikalibomoa Taifa. Ni kweli kwamba tunawahitaji wafugaji, ni kweli tunawahitaji wakulima, ni kweli kwamba tunahitaji hifadhi au misitu. Ni muhimu tukafahamu kuwa mifugo inaongezeka na mahitaji ya kilimo kwa maana ya wakulima wanaendelea kuhitaji ardhi lakini ardhi ni ile ile tu haiongezeki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri sana Serikali wakakaa na Wizara zote ambazo zinaingiliana katika masuala haya ya mifugo, kilimo na wa maliasili kuhakikisha wanaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha wafugaji wanapata maeneo yao, wanatengewa kabisa, hifadhi nayo inakuwa na maeneo yasiingiliwe na wafugaji, vivyo hivyo kwa wakulima pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kusema pia wakati mwingine unaruhusu moja kwa moja mifugo inaingia hifadhini lakini kama hawa watu wangetengewa maeneo yao hakika tusingekuwa na hii migogoro ambayo inaendelea. Serikali lazima ipime, ukipima kati ya suala la maliasili na utalii na kati ya sekta ya mifugo utaona kwa takwimu kwa sasa kwamba maliasili inaiingizia Serikali pato zaidi kuliko mifugo. Inawezekana pia mifugo ingeweza kuliingizia Taifa pato zaidi kuliko maliasili lakini kama wangekuwa na ufugaji wa kisasa, wakapangiwa maeneo yao, wasiingiliane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu sana Serikali wakayapima haya, wakahakikisha migogoro hii ya wakulima na wafugaji inakwisha. Niwasihi Waheshimiwa viongozi wenzangu Wabunge, ni muhimu sana tukachunga kauli zetu, tuangalie tunawahitaji watu wote. Tunawahitaji wakulima, tunawahitaji wafugaji, tunahitaji pia na misitu yetu na uhifadhi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la utalii. Wizara imetoa takwimu hapa kwamba kwa mwaka nchi yetu inaingiza watalii karibu 1,200,000 na kuna Mheshimiwa Mbunge wa Arusha jana alichangia vizuri sana akafanya comparison na nchi nyingine ambazo zinakuwa na idadi kubwa ya watalii. Nchi yetu mtalii kuja hapa anakumbana na tozo kibao. Anaanzia kwanza kwenye viza, akienda kama ni Ngorongoro getini kuna fees, akilala kwenye hoteli kitanda kina fees, kila mahali Mzungu huyu au mtani huyu anatozwa tozo na hizi tozo zimekuwa ni fixed mwaka mzima na watalii ni wale wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishauri Serikali kwa nini msiwe na promotion package kwa kipindi fulani ili muongeze idadi ya watalii halafu baadaye mkifika kwenye pick fulani mtaendelea na hizi tozo zenu ambazo ziko fixed ili tuhakikishe tunaongeza idadi ya watalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni muhimu sana pia wakahakikisha wanakuza utalii wa ndani. Kuna baadhi ya maeneo, mimi natoka Wilaya ya Karatu, Wilaya ya Karatu ina hoteli za kitalii 54, wako Watanzania ambao hawajui. Mtanzania yuko Dar es Salaam anafikiria kwenda kupumzika South Africa lakini kumbe angekuja kupumzika Karatu kuna hoteli nzuri, zile ambazo wanazifuata nje ya nchi pia ziko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti,una hoteli nzuri sana ambazo wageni wengi wanapenda kulala pale halafu wanakwenda kutembea Ngorongoro. Wilaya kama hizi ambazo ziko pembezoni mwa Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni sehemu ya lango la kuingilia Ngorongoro tayari kuna hizi hoteli za wawekezaji na wazawa pia wamejitahidi kujenga hoteli za standard mbalimbali, unakuta kuna hoteli ya mpaka kulala siku moja ni karibu dola 700, hoteli yenye standard na quality ya juu kuliko labda hizo mnazofuata South Africa na kwingine, ziko Karatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni muhimu pia Wizara wakaangalia Wilaya kama hizi ambazo tayari kuna hoteli kama hizi wakazitangaza, wakafanya utalii wa ndani pia wakawa na target ya kukuza utalii wa ndani na si tu kuangalia target ya kukuza utalii wa wageni kutoka nje. Kwa hiyo, ni muhimu sana wakalitazama hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu TANAPA. TANAPA ina jukumu la msingi la kusimamia hifadhi za Taifa, uhifadhi wa wanyamapori na shughuli za utalii. Leo TANAPA mapato yake yote yanapelekwa kwenya pool moja kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, lakini hawa baadaye wakitaka kutekeleza shughuli zao maana yake waje tena waombe huko, kwa maana ya Hazina au Mfuko Mkuu wa Serikali waweze kwenda kutekeleza majukumu yale. Mfano, leo pale Ziwa Manyara liko chini ya hifadhi ya TANAPA linapotea kwa sababu limejaa tope hakuna kinachofanyika. TANAPA wanakusanya fedha badala nyingine zirudi kwenda kutekeleza zile shughuli zinapelekwa Mfuko Mkuu wa Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo wanaipa TANAPA kazi ya kutengeneza madawati nchi nzima halafu Waheshimiwa Wabunge wanapongeza wakati TANAPA ina kazi ya kudhibiti ujangili, ina kazi ya kudhibiti na kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu, ina kazi ya kuhakikisha mfano Ziwa Manyara linaendelea kuwepo? Mheshimiwa Waziri baada ya miaka 10 au 20 Ziwa Manyara linapotea kwa sababu limejaa tope maji yale yanakuwepo tu msimu wa masika baada ya muda ni tope linajaa pale. Kwa hiyo, ni muhimu sana Wizara wakaangalia shughuli za TANAPA zisiweze kusimama. Haiwezekani wao wanakusanya fedha wanawapelekea halafu mwisho wa siku yale majukumu yao ambayo wanapaswa kuyafanya hawawezi kuyatekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu Operesheni Tokomeza. Kwa kuwa kulikuwa na Azimio la Bunge kwa wananchi walioathirika na Operesheni Tokomeza ni muhimu sana Serikali ikahakikisha inalipa fidia kwa wakati kwa wananchi hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili ni kuhusu leseni ya biashara ya Nyara, kuna baadhi ya kampuni zilizopewa leseni hizo na baada ya muda leseni zikafutwa na tayari kampuni hizo zilishakuwa na nyara hizo na baada ya muda wahusika kukamatwa ilhali wakati wanatekeleza jukumu hilo walikuwa na leseni halali. Serikali itueleze kwa nini kumekuwa na mkanganyiko huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Wilaya ya Karatu inapakana na TANAPA (upande mmoja) na Hifadhi ya Ngorongoro (kwa upande mwingine). Wilaya imekuwa haina makubaliano ya kimkataba wa namna gani Wilaya hiyo inafaidika na utalii ili kujenga ujirani mwema. Misaada hiyo imekuwa inatolewa bila ya kuwa na uhakika wa kuipata (hisani). Ni kwa nini mamlaka hizi zisiingie makubaliano rasmi ya kimkataba ili Halmashauri iwe na uhakika kwa mwaka ni miradi ipi, kwa gharama ipi itatekelezwa na mamlaka hizo? Ni muhimu mambo haya yakawekwa wazi ili kujenga ujirani mwema.
Taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo; na Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) pamoja na Maoni na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hiyo
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia katika hizi taarifa zilizowasilishwa mbele yetu, taarifa ya Kamati ya PAC na LAAC. Mchango wangu wa kwanza utajielekeza katika suala zima la Deni la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi Juni, 2016 Deni la Taifa limeongezeka kwa asilimia 9.76 maana yake linakimbilia shilingi trilioni 40. Madeni haya kwa mujibu wa taarifa ya CAG ameeleza kabisa hakuna mkakati wa namna gani yanaweza kwenda kulipika. Kulikuwa kuna rasimu ya mkakati huu ya mwaka 2002, ikatengenezwa rasimu nyingine ya mwaka 2004, ikatengenezwa nyingine ya 2014 lakini zote ni rasimu bado haijakamilika kuwa mkakati wa kuona namna tuta-control Deni la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tusipoangalia, itafikia mahali fedha zote za makusanyo ya nchi hii zinaenda kulipa madeni. Kama ambavyo ilivyo leo kila kinachokusanywa karibu shilingi bilioni 900 inaenda kulipa madeni. Kwa hiyo, ni lazima Serikali ifike mahali iandee mkakati. Ripoti ya CAG imesema kabisa hii rasimu ambayo ipo tena imeandaliwa kizamani haiendani na hali halisi ya uchumi wa nchi. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaona umuhimu wa kuwa na mkakati huu ambao utaendana na hali halisi ya uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee kuhusu Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Tuna Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo kwa kiwango kikubwa fedha zake zinakopwa na zinaenda kuwekezwa katika miradi mikubwa. Hatukatai kufanyia shughuli hizo, lakini unapoenda kukopa halafu hurejeshi inakuwa ni tatizo. Mfuko mmojawapo tu kwa mujibu wa taarifa ya CAG ni PSPF una hali mbaya ambapo unakaribia kufilisika kabisa kwa sababu Serikali hairejeshi fedha ilizozikopa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima ifike mahali muache kabisa kukopa hizi fedha za wanachama. Ni fedha za wanachama wanaweka kule wakijua wanajiwekea akiba lakini Serikali mnaenda kuzichukua na ku-invest kwenye miradi mikubwa ambayo tunaona kabisa siyo rahisi muweze kurudisha kwa sababu mmejaa madeni, mnadaiwa ndani na nje, mnakopa tena kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, mnadaiwa kila kona, mwisho wa siku mtaenda kuua hii akiba ya wafanyakazi ambao wanatarajia waipate siku wakistaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaongelea sana suala la kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, tumesema sana kwenye Bunge la Kumi. Leo mnajiita wazee wa hapa kazi tu, wazee wa kubana matumizi, si ndivyo mnavyojiita? Kama kweli mnataka kubana matumizi ni lazima muangalie suala la kuunganisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii iko takribani tano au sita yote ina Wakurugenzi, ofisi, inaendeshwa kwa gharama na kwa fedha za wanachama. Kama mnasema mnabana matumizi muende muunganishe hii Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwepo na ama mifuko miwili au mitatu ili hicho mnachokiita cha kubana matumizi mkifanye kwa vitendo siyo mnatuambia tu halafu hakuna mnachokifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya mwisho nitajielekeza katika Serikali za Mitaa. Katika Awamu hii ya Tano mnaenda kuua kabisa Serikali za Mitaa. Mnaenda kuzimaliza wakati Serikali za Mitaa zipo kwa mjibu wa Katiba ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uteuzi tu mliofanya, Mheshimiwa Rais alifanya uteuzi wa hawa ma-DC, ma-DED, ma-DAS, kwa kweli ni watu ambao hawajapitia kwenye mifumo ya local government, wengine wametolewa mnakojua, wamepewa nafasi ambazo hawana experience hata nukta moja. Hivi wanaendaje kufanya kazi? Ma-DED wengine hawajui hata vote ni nini, anauliza vote ni nini? Wanauliza hawajui. Hivi mnategemea kutakuwa na ufanisi? Ndiyo maana tunawaambia mnaenda kuua Serikali za Mitaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali miaka yote imeonesha suala la Serikali Kuu kutokupeleka fedha za maendeleo katika Halmashauri za Wilaya. Hivi tunavyoongea leo, fedha zilizoenda katika local government ni fedha za mishahara tu. Mfano mzuri ni Halmashauri yangu ya Karatu. Fedha kidogo tu iliyoenda ni ya barabara shilingi milioni 50 lakini hakuna fedha za miradi ya maendeleo zilizoenda yaani mpaka leo tunaingia robo ya pili ya bajeti ya Serikali fedha hazijaenda katika Serikali za Mitaa. Mnatarajia nini si mnaenda kuziua Serikali za Mitaa.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Naomba nitoe mchango wangu mfupi hasa kuhusiana na suala zima la hali ya uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukipitia taarifa ya tathmini ya MDG kwa nchi yetu kuanzia mwaka 2000 hadi 2015, taarifa inaonyesha kwamba uchumi wetu umekua kwa asilimia saba kwa kipindi cha miaka 15. Lakini taarifa hiyo inaonesha kwamba kama uchumi utakuwa mfululizo kwa asilimia saba kwa miaka 15 maana yake inategemewa suala la umaskini utapungua kwa kiwango cha asilimia 50. Lakini taarifa hiyo inaonyesha kwa Tanzania imepungua kwa asilimia kumi tu, kwamba bado tuna safari ndefu ya kufikia hicho kinachoitwa uchumi wa kati ambayo ni dira ya Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukisema suala la ukuaji wa uchumi lazima pia tuangalie sekta zingine ambazo zinaweza kuchochea suala zima la ukuaji wa uchumi, bado tuna safari ndefu. Ukiangalia kwenye sekta tu ya kilimo uchumi unakua kwa asilimia mbili tu na tunajua kabisa suala la kilimo ni tegemeo kwa Watanzania wengi, wanategemea ili kuondokana na umaskini.
Lakini sekta hiyo imekua kwa asilimia mbili tu kama ambavyo taarifa hiyo inaonyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la ukuaji wa uchumi Serikali mkija hapa na figures na kujigamba mkisema kwa ujumla wake inakuwa kwa asilimia saba bila shaka mtakuwa mna wahadaa wananchi lakini kwa uhalisia ukienda kwenye sekta moja moja ambazo zinachochea uchumi huo bado tupo nyuma na tuna hali ngumu. kwa hiyo, ni vizuri sana mnaposema suala hili la uchumi muangalie uhalisia wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisema pia suala la uchumi tukiangalia hali ilivyo sasa kuna mdororo mkubwa wa uchumi, hakuna mzunguko wa fedha, hakuna fedha katika hata bajeti tuliyopitisha ukiangalia sasa tunaingia kwenye quarter ya pili hata asilimia 26 ya utekelezaji wa bajeti bado hamjafikia na kama mmefikia ni hiyo asilimia 26 tu. Kwenye Serikali za Mitaa hakuna fedha, kwenye taasisi za umma hakuna fedha, Wizarani tumeona taarifa mbalimbali Wizara zikiwasilisha kwenye Kamati hakuna fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya, hakuna fedha, nini kipaumbele? Mna mpango gani wa kufikia hiyo bajeti ambayo tumeipitisha kwa shilingi trilioni 29 katika mwaka huu. Lakini mnafanya projection ya bajeti ya shilingi trilioni 33 kwenye bajeti ijayo. Napata mashaka sana kama hii tu ya sasa utekelezaji wake tunaingia kwenye quarter ya pili bado hali ni mbaya halafu unafanya projection ya shilingi trilioni 33 kwenye bajeti ijayo tafsiri yake ni kwamba mnajifurahisha ninyi kama Serikali kwa namba hizi kubwa kubwa, lakini mnawaongezea wananchi mzigo wa kuendelea kulipa kodi.
Kwa hiyo, unaona kabisa ni bajeti ambayo kwa kweli mwisho wa siku haitaweza kutekelezeka ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeeleza katika mpango huu kumekuwa na changamoto mbalimbali za kuweza kufikia mipango hiyo. Mojawapo mmesema ushiriki mdogo wa sekta binafsi lakini pia kuna suala la upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji. Hivi hizi sekta binafsi kama hazijatengenezewa mazingira rafiki, kama hizi sekta binafsi hazijawa na imani na Serikali iliyopo madarakani kwa sababu tumeona wakati mwingine mna ndimi mbili mbili sekta binafsi ataogopa ku-invest hela zake kwasababu hajui Serikali kesho inatamka nini? Inafanya nini? Kesho inakuja na kodi gani? Kama msipoweka haya mazingira mazuri hakuna sekta binafsi atakayeweza kuja kuwekeza katika nchi hii kama ambavyo nyie wenyewe mmekiri hapa ni changamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, bado tunahitaji kuwepo na sera na mazingira rafiki ya kuweza kuhakikisha hizi sekta binafsi kwa kweli zinakuwa na wao ni sehemu ya uchumi wa nchi hii. Mmeeleza pia changamoto nyingine ni upatikanaji wa mitaji ya uwekezaji, hili pia ni changamoto kweli kwa sababu kama sasa hivi mabenki hali ni mbaya, mabenki mengine yameshakua chini ya usimamizi wa BOT, mabenki hayana mzunguko wa fedha, fedha ambazo zilikuwa za Serikali kwenye commercial banks zote zimehamishiwa BOT, obviously hakuna uwekezaji unaweza kufanyika. Kwa hiyo, bado tuna changamoto kubwa sana ambayo kwa kweli itakuwa ni ngumu sana kuweza kufikia hicho kinachoitwa uchumi wa kati ambayo ni dira ya Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona hali ilivyo sasa hivi, lakini wakati mwingine unajiuliza hivi kuna haja gani ya kujadili pia mpango au kujiwekea mpango wakati mpango wenyewe ukienda kwenye utekelezaji hauwezi kufanyiwa tathmini na kuona matokeo. Lakini kuna vitu vingine ambavyo vinaenda kutekelezwa ambayo hayapo kwenye mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ambao tunaumalizia 2016/2017 suala la kuhamia Dodoma halikuwepo lakini Rais amelitamka limetekelezeka, halikuwepo kwenye mpango na kuhama Dodoma sio kazi ndogo, inahitaji fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini angalau sasa hivi mmeiweka kwenye mpango unaokuja; sasa unaona wakati mwingine kama tunaendeshwa kwa matamko ya namna hii ambayo hayapo kwenye mipango maana yake unaenda kuharibu bajeti ambayo imepitishwa hapo. Kwa hiyo, pia wakati mwingine ni lazima haya ambayo mnayatamka ni lazima yaendane na bajeti ambayo tumeipitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuulize Waziri wa Fedha na anisaidie majibu atakapohitimisha. TRA wamesema wanakusanya 1.3 trillion kila mwezi, hiyo ni projection. Mishahara inayolipwa nchi hii ni shilingi bilioni 540, madeni ya ndani ama ya nje inalipwa shilingi bilioni 900, ukifanya hapo mahesabu ni kama one point four trillion na makusanyo ni 1.3 trillion kila mwezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza hizo ndege zilizonunuliwa kwa fedha cash hii hela mliipata wapi? Wakati mnachokikusanya TRA kila mwezi ni 1.3 trillion, ukilipa madeni, ukilipa mishahara ni 1.4 trillion; fedha za kununua ndege kwa hela cash mmeipata wapi? Naomba Mheshimiwa Waziri unijibu ama ni hizo fedha zilizopo BOT ambazo zimekusanywa na taasisi zikawekwa kule mkaenda mkazichukua mkanunua ndege cash? Naomba nipate majibu ya suala hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala lingine ni kuhusu suala zima la elimu. Wakati nimechangia kwenye bajeti ya elimu hapa mnajivunia leo suala la elimu bure, lakini elimu bure hii ni bure tu kwa sababu hawalipi kile ambacho kinatakiwa. Ukienda kwenye uhalisia wa shule zetu hali ni mbaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kibaya zaidi mmesema mwanzoni wakati wa awamu ya JK mliagiza kujengwe maabara nchi nzima; wananchi wakajichanga, mkaita wadau mbalimbali wakachanga maabara ikajengwa, yamebaki majengo yameachwa. Mmeyaacha yale majengo hayana vifaa, maabara hayafanyi kazi ni majengo tu yaliyosimama mkahamia kwenye madawati mmetangaza madawati nchi nzima watu wametengeneza madawati mengine hayana standard, hayana quality inayotakiwa leo mnataka kukimbilia kujenga madarasa kwa mfumo ule ule wa kulipuka. Kule mmeshasahau maabara, madawati mengine hayana kiwango, leo mnakurupuka mnaenda kujenga…
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema muache kukurupuka, mkianzisha jambo moja likamilike, liwe na manufaa, lianze kufanya kazi muende kwenye jambo lingine, ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na namshukuru Mheshimiwa Mwakajoka kwa kunipa dakika tano. Nami nianze kuchangia kwenye suala zima la mamlaka makubwa ambayo nafikiri RC na DC na DAS wanazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi sana kuona leo kwa sababu mwaka jana hapa wakati sisi Wabunge wa Kambi ya Upinzani tunajaribu kuonesha matatizo na changamoto na udhaifu ambao baadhi ya RC na DC wanayo katika maeneo yetu, tulibezwa hapa, hatukusikilizwa lakini leo humu baadhi ya Wabunge wa CCM nao wameona hiyo shida na wameanza kusema. Nafikiri huu utakuwa ni mwanzo mzuri ili tuendelee kuelewana sawasawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema kwamba hawa RC na DC wamekuwa Miungu watu, wameona kwamba wana mamlaka makubwa kuliko mtu yeyote, hawatambui nafasi za Wabunge, wanaweza ku-revoke maamuzi ya Baraza na kuyaingilia, hata pale ambapo hayastahili. Ifike mahali hizo semina elekezi ambazo mlizisema zimefutwa nadhani iko haja ya kurudisha na kukaa na hao watu na kuwaambia. Siyo semina tu, hata akili nyingine tu ya kawaida ya busara ya RC au DC kujua mipaka yake, kujua namna ya kushirikisha hawa watu hawana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni lazima muangalie mfumo mwingine, sijui wateuliwe wengine au wafanye nini hawa wameshindwa kazi, wamekuwa Miungu watu. RC anakaa kwenye kikao anaongea anasema, nadhani mnaelewa hapa kuna Waziri naweza kuwa na maamuzi makubwa kuliko Waziri hata Waziri mwenyewe anaelewa, anasema kwenye kikao na Waziri yupo, huyu ni RC. Sasa kama wanasema vitu kama hivi mbele ya Mawaziri unategemea nini kwa Wabunge?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, RC anakuja kwenye eneo lako, Wabunge mnaomba kuonana nae hana muda na Wabunge. Haya ni masikitiko, lakini sasa angalau tunaanza kuelewana humu ndani na angalau haya machungu na ninyi Wabunge wa CCM mmeanza kuyapata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utawala wa sheria; sioni sasa kama kuna utawala wa sheria. Kuna Mbunge mmoja ameongelea kuhusu mlundikano wa kesi au mlundikano wa wafungwa Magerezani, lakini leo kama kuna kesi ya uchochezi ya mwana CHADEMA haichukui miezi mitatu hukumu tayari na inasikilizwa haraka sana, lakini kuna watu wamekaa gerezani kwa kesi ama za kusingiziwa au ambazo siyo za kisingiziwa miaka tisa, miaka 10, miaka mitano, miaka miwili wanasema upelelezi bado, lakini mwana-CHADEMA akisema jambo tena anaambiwa mchochezi na hii tafsiri ya uchochezi itabidi mtuambie uchochezi ni nini maana yake neno uchochezi linatumika vibaya, anaambiwa ni mchochezi, anapelekwa Mahakamani haraka hukumu miezi sita, miezi nane, miezi mitatu jela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sidhani kama kuna utawala wa sheria, ni lazima mjitafakari upya, muangalie kama tuna Katiba, kama tuna sheria, kama kweli kuna kutenda haki kwa nini haki inatendeka kwa watu wachache na watu wengine wananyanyaswa kwa sababu ni washabiki wa upande fulani au wa Chama fulani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie suala la mwisho kuhusu Madiwani; Madiwani wamekuwa ni Wasaidizi wetu hata sisi Wabunge kwa maana kama tukiwa hapa Bungeni kwenye vipindi virefu vya Vikao vya Bunge, wao ndiyo wamekuwa wakikaa na wananchi na wakiwasikiliza kero zao, lakini Madiwani wamesahaulika. Madiwani leo wanapewa posho ya sh. 350,000 basi na hizo posho za vikao, tena wako Wakuu wa Wilaya wengine wanafuta posho za Madiwani ambazo zingine ziko kwa mujibu wa taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wakuu wa Wilaya wengine wanasema posho hii haitakiwi, hii haitakiwi, kweli kuna zile ambazo haziko kwa mujibu wa taratibu, lakini zile zilizoko kwa mujibu wa taratibu DC wanaingilia, wanazifuta. Tumewasahau Madiwani, hatufikirii kuwaongezea posho zao, tumewaacha Madiwani hawapewi mafunzo, capacity building haipo tena, angalau kwenye awamu zilizopita walikuwa wanapewa. Sasa unampeleka Diwani asimamie mradi wa mabilioni, yuko kwenye Kamati ya Fedha lakini hajajengewa uwezo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2017/2018 unaonyesha kwa kiwango kikubwa Serikali inategemea kukopa fedha katika mifuko hii ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, kukopa sio dhambi, lakini mikopo ambayo inazidi uwezo na kupelekea hatari ya kuua/kufifisha uwezo na kupeleka hatari na lazima Serikali ituambie imejipanga vipi kuhakikisha mifuko hii haifi/kupunguza uwezo wake?
(a) Je, return on investment kwa miradi ya namna hii ambayo inachukua muda mrefu kurudisha faida imetazamwa kwa kiwango gani?
(b) Je, foreseeable risk kwenye operation za viwanda na miradi inayowekezwa imefanyika assessment kina?
(c) SSRA ambaye ni mdhibiti na msimamizi wa mifuko hii inaweka ukomo/kiwango kwa mifuko kutokopa zaidi ya 20%. Hata hivyo kwa taarifa ya Benki Kuu ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa proportion ya mifuko kwenye deni la ndani ni 26% kutoka 16% na imechukua nafasi ya mabenki ya biashara. Uhai wa mifuko hii upoje? Kwa nini Serikali iendelee kukopa zaidi kinyume na sheria zilizopo?
(d) Kumekuwa na hoja ya muda mrefu wa kuunganisha mifuko hii ya hifadhi ya jamii. Je, lini Serikali itaanza machako wa kuunganisha mifuko?
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Katiba na Sheria
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, usikilizaji wa mashauri mahakamani; pamoja na Serikali kueleza 80% ya mashauri yameweza kusikilizwa, kasi hii bado inahitaji kuwekewa nguvu zaidi ili kuendelea kupunguza mrundikano wa kesi zilizopo mahakamani. Serikali lazima itie nguvu na mkazo katika Mahakama za Mwanzo na Mahakama za Wilaya kwani huko ndiko kwenye mrundikano wa kesi nyingi, jambo ambalo linawafanya wananchi wenye kesi mbalimbali kuendelea kutumia muda mwingi mahakamani. Hata hivyo, haki inayocheleweshwa ni sawa na haki iliyonyimwa. Nashauri Serikali iendelee kujipanga kuhakikisha mrundikano wa kesi katika mahakama za chini zinakwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo; pamoja na umuhimu wa Taasisi hii ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo, ipo haja ya kuongeza chuo hiki katika kanda nyingine za nchi hii. Ni ukweli kuwa nchi hii ni kubwa na wanafunzi wanaohitaji kupata mafunzo haya ni wengi. Hivyo basi, ni muhimu kwa Serikali kuongeza vituo vya mafunzo hayo kwa angalau Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kusini na Magharibi. Kwa kuongeza vituo hivyo itasaidia wanafunzi kumudu gharama za mafunzo na hivyo kuongeza wanafunzi zaidi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa dawa nchini; kumekuwa na upungufu wa muda mrefu wa dawa hapa nchini, tatizo hili limekuwa la kudumu na kwa kuwa chanzo kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununua dawa inategemewa na mapato ya makusanyo ya kodi mbalimbali hapa nchini. Hata hivyo, kumekuwa na mifuko ambayo inaanzishwa na chanzo cha mapato kwa ajili ya mfuko huo unakuwa wa uhakika na kuleta ufanisi unaokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano ni Mfuko wa Barabara, Miradi ya REA ambayo chanzo cha mapato inatokana na fedha za mafuta na mfuko huo fedha zake haziguswi (ring fenced). Kwa kuwa dawa ni suala muhimu sana kwa ajili ya maisha ya Watanzania, hivyo ni wakati muafaka sasa Serikali ianzishe mfuko maalum wa dawa na fedha zake zitokane na chanzo cha uhakika ili kupunguza na kuondoa kabisa tatizo la ukosefu wa dawa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Taifa ya Mount Meru; Hospitali hii ndiyo hospitali inayotegemewa katika Mkoa wa Arusha, hata hivyo kuna changamoto katika utoaji wa huduma kwa vifaa muhimu kama x-ray machine kuharibika mara kwa mara. Serikali ione umuhimu wa kuiwezesha kwa kiasi kikubwa hospitali hii ambayo ni muhimu kwa Mkoa wa Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni motisha kwa watumshi wa afya. Watumishi wa afya nchini ni kada muhimu sana ambayo wameamua kufanya kazi kubwa ya kutoa huduma kwa Watanzania wote. Hata hivyo, suala la afya ni muhimu sana kwa ustawi wa nchi yetu. Serikali lazima itazame kwa upya maslahi ya watumishi wa afya hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wazee; kumekuwa na ahadi ya muda mrefu ya Serikali kuwa itaboresha makazi ya wazee, jambo hili limekuwa linaandikwa kwenye vitabu bila utekelezaji. Wazee ni hazina ya nchi, tunapaswa kuwaenzi na kuwahudumia. Serikali ijipange vizuri ili kuhakikisha makazi ya wazee yanaboreshwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia kuhusu fidia kwa wananchi. Katika maeneo mbalimbali ya nchi ambapo Hifadhi za Taifa zimepakana na vijiji ambavyo wananchi wanaendesha shughuli za kilimo kumekuwa na changamoto za wanayama kuharibu mazao ya wananchi na wananchi hawapewi fidia kutokana na uharibifu huo. Kilio hiki cha wananchi kimekuwa cha muda mrefu na wakati mwingine hata kama fidia inatolewa kwa kuchelewa sana na kuleta usumbufu mkubwa kwa wananchi. Hivyo basi naishauri Serikali ifanye yafuatayo:-

(a) Kulipa fidia kwa wakati; na

(b) Malipo ya fidia yalipwe na mamlaka husika ambapo uharibifu umetokea kwani kwa kufanya malipo ya fidia kuwa central kwa maana ya kulipwa na Wizara imekuwa na usumbufu mkubwa na kuchelewesha malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu migogoro ya vijiji na hifadhi za wanyamapori; migogoro ya wananchi na mipaka au hifadhi za wanyamapori imekuwa ya muda mrefu bila kupatiwa ufumbuzi, matokeo yake Serikali imekuwa ikikimbilia kuunda tume ya kufuatilia migogoro bila mafanikio. Nashauri ije na mkakati wa namna gani inamaliza migogoro hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu sekta ya misitu, natambua umuhimu wa misitu na tunaunga mkono juhudi na jitihada za kulinda misitu. Miongoni mwa mazao ya misitu ni mkaa ambayo ni nishati muhimu sana kwa wananchi kwa ajili ya matumizi ya kupikia. Wizara imetoa katazo kuwa mkaa usitoke nje ya Wilaya. Katazo hili limekuja bila kuwepo na nishati mbadala kwa wananchi hao. Miji ambayo haina sasa watakosa nishati ya mkaa na wananchi hawawezi kumudu gharama za gesi. Nashauri Serikali ifute katazo hili huku tukiwandaa wananchi kutumia nishati mbadala ambayo wataiweza na kuimudu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Nianze mchango wangu kwa sekta nzima ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta ya utalii imekuwa ikichangia asilimia 17 ya Pato la Taifa ukilinganisha na sekta zingine. Kwa tafsiri nyingine unaweza ukasema Pato la Taifa chanzo chake kikuu ni sekta ya utalii. Sekta hii ya utalii imekuwa na changamoto nyingi ambazo zinazidi kuongezeka. Kama changamoto ni nyingi na zinazidi kuongezeka maana yake sekta hii haiwezi kukua na kuendelea kuongeza Pato la Taifa kwa maana ya kutoka kwenye hiyo asimilia 17 kwenda hata angalau asilimia 20.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa changamoto zilizopo kwenye sekta hii, imekuwa haitiliwi mkazo kutangazwa ipasavyo. Mikakati ipo lakini inawezekana fedha zinakosekana ya kutangaza kwa upana sekta ya utalii ndani na nje ya nchi, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu ndio maana tunabaki palepale hatuwezi kwenda mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine Serikali haina ubunifu wa kuongeza vivutio vingine vipya. Tumekuwa na vivutio vya zamani na hivyo vingine vimetelekezwa, lakini hakuna ubunifu wa kuwa na vivutio vipya ambavyo vitawashawishi watalii waweze kuja kuangalia kwa wingi hapa nchini. Kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali kuangalia namna gani vivutio vilivyopo mnaviendeleza, lakini mnabuni vivutio vingine ambavyo vitaweza kuhahakisha kwamba watalii wanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linaifanya sekta hii ya utalii iwe na changamoto kubwa ni masharti magumu kwa wawekezaji ikiwemo suala la kodi. Katika Awamu ya Nne kodi ambazo zilikuwa zinalipwa na wawekezaji katika sekta ya utalii ilikuwa ni kodi kati ya 14 mpaka 16. Leo Serikali ya Awamu ya Tano mmeingia madarakani mmepandisha kodi ambazo wanalipa wawekezaji katika sekta ya utalii zimetoka 14 mpaka 36 na sasa hivi ninasikia tena mnataka kupandisha nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto hizi au namna gani kama mnaongeza kodi hakuna mwekezaji ambaye atakuja ku-invest kwenye sekta ya utalii na tukaona inakuwa atakuwa anazikimbia hizi kodi. Kwa hiyo, tunatarajia kwamba muende mkae, mpunguze kodi muweze ku- encourage wawekezaji wengi ili sekta ya utalii iweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine katika haya haya masharti magumu, leo mtu akitaka kupata TALA licence unalipa dola 2000 kwa magari kuanzia matatu. Tunajua huko huko nyuma ilikuwa ni magari matano unalipa dola 2000, mkapunguza mkafanya magari matatu kwa dola 2000, lakini kwa wale vijana wa Arusha ambao maeneo yenye utalii atapambana atapata magari matatu atalipa dola 2000, huyu anashindana na mwekezaji mkubwa mwenye magari 100 naye analipa dola 2000. Kwa mfano, Leopard Tours wana magari kibao, naye analipa TALA licence ya dola 2000. Halafu kijana wa Arusha anajitahidi amepata magari matatu naye analipa dola 2000. Kwa nini Wizara msifikirie kupunguza hii TALA licence mkalipa TALA licence kwa gari ambayo itaiingizia Serikali mapato zaidi; yule mwenye magari 100 atalipa kulingana na idadi yake ya magari na yule mwenye magari matatu naye atalipa kulingana na idadi yake.

Mheshimiwa Waziri hii limekuwa ni kelele ya muda mrefu lakini hatupati majibu ya kuwasaidia hawa. Pia itawasaidia na ninyi kuongeza mapato, kwa hiyo, ni vizuri mkalifikiria hilo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine katika sekta ya utalii ni ushiriki mdogo wa maonesho ya utalii na kutokupewa kipaumbele. Masuala mazima ya maonyesho ya utalii na vivutio vya utalii inaoneka imeachiwa sekta binafsi na Serikali imekaa pembeni, imekuwa ni changamoto ya muda mrefu. Sasa kama ninyi mkaa pembeni mnaziachia sekta binafsi ziende zenyewe zijitangaze, zijipambanue na kuonesha wana vitu gani, ni kwa namna gani sekta hii itaweza kukua. Haiwezi kukua obviously kutakuwa kunaendelea kuwa na changamoto hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ni vyuo vichache vya utalii vinavyotoa mafunzo ya utalii na imekuwa ikitoa mafunzo duni haiendani na kasi ya ukuaji wa utalii. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali mkafikiria namna gani kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha kwamba vyuo vya utalii vinakuwa na ubunifu zaidi, lakini inaendana na kasi ya ukuaji wa utalii duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la migogoro ya vijiji na hifadhi za wanyamapori. Migogoro hii imekuwa ni migogoro ya muda mrefu, ni migogoro ambayo ndani ya Bunge tumekuwa tukisema lakini unachokiona tukipiga kelele kuhusu migogoro, Serikali mnakimbilia kuunda Tume. Mnakimbilia kuunda Tume, mnatuahidi kwamba Tume zikifika maeneo hayo mtashirikisha wadau mbalimbali, wanafanya kazi hizo wanamaliza hatujawahi kusikia ripoti ya Tume hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2009 Bodi ya TANAPA iliunda Tume ya kuchunguza migogoro ikatoa mapendekezo, sijui yamefanyiwa kazi kwa kiasi gani. Mheshimiwa Waziri Mkuu wa zamani Mheshimiwa Mizengo Kayanza Pinda aliunda Tume, Mheshimiwa Kagasheki akiwa Waziri aliunda Tume, Mheshimiwa Lukuvi aliunda Tume na sasa hivi nasikia mmeunda tena Tume inayohusisha sekta zote lakini hakuna majibu. Serikali mkisikia migogoro ya wananchi na hifadhi badala ya kutuletea majibu mnakimbilia kuunda Tume zinazotumia fedha nyingi za walipakodi, taarifa ya Tume mnaweka kapuni hamtuambii. Leo hapa msimame mtuambie angalau ni mgogoro gani ambao mmeumaliza? Hamna na migogoro inaendelea! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kila siku kuona wananchi wanashughulikia tu migogoro wanaacha shughuli zingine, Serikali mnakimbilia kuunda tume ambazo hatupati majibu yake. Kwa hiyo, nafikiri ni wakati muafaka sasa Serikali mtuambie kwanza hizi Tume zote ambazo mmeziunda majibu yake yako wapi? Ripoti yake iko wapi? Utekelezaji wa matokeo ya Tume hizo umefanyika kwa kiwango gani? Kwa nini kama ambazo hazijafanyika ni kwa nini imeshindikana kufanyika mpaka sasa hivi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la mgogoro wa Loliondo. Mgogoro wa Loliondo pia ni kati ya migogoro ambayo imekuwa ni ya muda mrefu. Leo Serikali inataka kuondoa wananchi takribani 54,000 katika vijiji 14 waondoke kwenye eneo la kilometa za mraba 1,500, hivi unawaondoa watu 54,000 unawapeleka wapi? Huko unakowapeleka si ndiyo unaenda kuendeleza mgogoro mwingine wa ardhi? Serikali mtuambie mna maslahi gani na suala la Loliondo, kwa nini mmeshindwa kulipatia ufumbuzi wa muda mrefu? Kwa sababu umekuwa ni mgogoro wa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala mtuletee ufumbuzi wa tatizo la Loliondo, mnakimbilia mnasema NGO’s zilizoko Ngorongoro zinachochea wananchi kuendeleza migogoro hii. Kwanza hizi NGO’s zilizo nyingi zimesaidia kujenga uelewa wa wananchi wa kule, lakini kama kweli kuna NGO’s ambazo zinafanya ushawishi na uchochezi it is okay zichukuliwe hatua lakini siyo kuzihukumu NGO’s zote labda kwa sababu ya baadhi ya NGO’s ambazo zinafanya ndivyo sivyo.

Kwa hiyo, Serikali mtuambie hivi mna maslahi gani na huyu Mwekezaji wa Loliondo huyo OBC huyu Mwarabu mtuambie? Huu mgogoro umekuwa wa muda mrefu, mnaenda mnaunda Tume, sijui Waziri Mkuu ameunda Tume, sijui Waziri umeenda, Mkuu wa Mkoa Gambo ameenda, sijui ataenda na nani labda aje na malaika naye aende, lakini hamtupatii ufumbuzi, kwa nini wananchi wa Loliondo wanateseka kwa muda mrefu? Mtuambie Mheshimiwa Waziri kwanza mna maslahi gani na huyu Mwarabu na kwa nini mgogoro huu haumaliziki?(Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwa dakika tano hizo katika Wizara hiyo ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na Watanzania wote kutoa pole nyingi sana kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha kufuatia ajali ambayo imechukua maisha ya watoto wetu, walimu pamoja na dereva iliyotokea Wilaya ya Karatu Wilaya ambayo ninatokea, Mkoa wa Arusha ambao ninauwakilisha. Poleni sana na Mwenyezi Mungu azidi kuwapa nguvu familia. Pia nitoe pole kwa wazee wetu hawa ambao wametangulia mbele ya haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mchango mfupi kuhusiana na Wizara hii kwa sababu pia ya muda. Taifa lolote ambalo linachezea elimu ni Taifa ambalo linaenda kuangamia na Taifa ambalo linaenda kupotea. Nasema hivi kwa sababu kumekuwa na utamaduni kila Waziri anayekuja kwenye Wizara hii anakuja na style yake ambayo ama anafikiri inaenda kuboresha elimu au inaenda kuangamiza elimu kabisa.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mama Ndalichako umeingia hapa wewe, wewe ni mtaalam, hujawahi kuwa mwanasiasa, tunaamini utaenda kuweka mifumo thabiti, mifumo itakayoboresha elimu kwa watoto wetu, mifumo ambayo itawaandaa watoto wetu kuwa na Taifa ambalo litaendelea kuwa Taifa kama ambavyo nchi nyingine tumeona. Tunategemea utaenda kuweka mifumo ambayo hata wewe ukiondoka kesho, Waziri yeyote atakayekuja hataenda tena kucheza na elimu ya watoto na hataweza kwenda kucheza na elimu ya Watanzania. Kwa hiyo, Mheshimiwa Ndalichako tunategemea utaenda kuweka hiyo mifumo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie kuhusu mfumo wa mpango wa elimu bure. Serikali imekuwa ikitamba sana kuhusu suala la elimu bure na imesema imefanikiwa. Ukweli sio sahihi. Huwezi kuangalia mafanikio ya elimu bure kwa kuangalia idadi ya watoto waliojiandikisha, ndiyo mmekuwa mkisema hivyo. Idadi ya watoto waliojiandikisha kuanza darasa la kwanza kweli inaongeza, lakini hiyo sababu pekee ya kutamba ya kujigamba na kusema eti elimu bure imekuwa na matokeo chanya kwa Watanzania siyo kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kuna changamoto nyingi, kuna changamoto nyingi sana katika suala zima la elimu katika nchi hii, ambapo pia taarifa ya Kamati imeonesha. Kwa hiyo, tunategemea ama mje na mfumo mwingine wa kusema kabisa, ama mmeshindwa hiyo elimu bure kutoa, ambayo mnaita elimu bure kwa sababu hizo changamoto au muondoe hilo neno au muwaambie sasa Watanzania kwamba tulisema elimu bure, lakini kuna changamoto, tunahitaji kuwa-engage Watanzania na wao katika suala zima la kuondoa changamoto za elimu hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuhusu wanafunzi waliopata mimba na kurudishwa mashuleni. Hatuelewi ni kwa nini kuna kigugumizi kuhusiana na watoto wa kike waliopata mimba wananyimwa kurudi shuleni. Mheshimiwa Kakunda amechangia hapa asubuhi, yeye ni mtaalamu mzuri sana, amekaa kwenye system muda mrefu anapinga hili jambo. Hivi, watoto wanapata mimba, hawarudi shuleni, hivi tunazidi kuondoa ujinga au tunazidi kuzalisha ujinga? Kwa sababu hawa watoto wanapata mimba wapo wanaobakwa, wapo ambao kweli inawezekana mazingira yanawalazimisha, wako wengine ambao tu ni watundu wanakuwa kwenye hiyo hali wanapata mimba. Hivi kupata mimba na kuzaa ni dhambi? Wavulana walowapa mimba wanaendelea, hawa watoto wa kike waliopata mimba wanarudi majumbani. Tunaendelea kuzalisha ujinga kwa Watanzania, na hatujui ni kwa nini Serikali mnapata kigugumizi. Mbona wenzetu wa Zanzibar wanaendelea hawa watoto wakipata mimba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bunge la Kumi nilikuwa na Kamati ya Huduma za Jamii tulikuwa tunasimamia Wizara ya Elimu tulienda Zambia, wanarudi mashuleni watoto hawa. Kwa nini kwa Tanzania? Kwa nini mnapata kigugumizi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wewe ni mama, wewe ni mwanamke mwenzetu, tuwaonee huruma watoto wetu wa kike ambao wako kule vijijini wanapata mimba, wanarudishwa majumbani, hawawezi kuendelea na shule, halafu watoto wa kiume waliowapa mimba wao wanaendelea na shule.

Waheshimiwa Wabunge wanawake, Waheshimiwa Wabunge, Wajumbe wa TWPG, Wizara hii bajeti yao isipite mpaka tupate kauli ya Serikali ni lini wataruhusu watoto waliopata mimba waweze kurudi mashuleni. Kwa hiyo, tunategemea Mheshimiwa Waziri utakuja na majibu siku unahitimisha hoja yako na ujiandae kwa hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee Mabaraza ya Ardhi; mojawapo ya malengo ya kuanzisha mabaraza haya ni kupunguza migogoro ya ardhi katika maeneo mbalimbali hapa nchini na pia kuharakisha usuluhishi wa kesi za ardhi. Pamoja na malengo haya mazuri mabaraza haya haiwezekani kutekeleza majukumu yake, ufanisi umekuwa mdogo kwa kukosa vitendea kazi, watumishi wachache wenye maslahi duni na kutopelekewa fedha za kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa zaidi ipo katika Mabaraza ya Kata ambapo ndipo kuna kesi nyingi na hawapatiwi fedha za kuendesha shughuli zao. Serikali kuwaachia Halmashauri wawezeshe mabaraza haya ni kuzidi kuyadumaza mabaraza haya kwani Halmashauri zenyewe vyanzo vyake ni vya kusuasua na wakati mwingine hazina fedha kabisa kwani mahitaji ni mengi zaidi ya fedha hizo za own source katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ifanye yafuatayo:-

Kwanza, kuyawezesha mabaraza ya Ardhi ya Wilaya ikiwa ni pamoja na kuongeza watumishi ili mabaraza haya yatimize majukumu yao kwa mujibu wa sheria; na

Pili, Wizara ichukue jukumu la kuyawezesha Mabaraza ya Kata kuliko kuziachia Halmashauri, kwani mapato ya Halmashauri hayatoshelezi. Sehemu ya fedha za kodi ya ardhi katika Wilaya husika kiasi fulani zibaki ili kuyawezesha Mabaraza ya Kata katika Wilaya husika.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika mpango huu uliowasilishwa na Serikali hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, napenda kushauri Serikali inapoleta mipango hasa kwenye miradi mikubwa, isiwe na miradi mikubwa mingi ambayo itagharimu fedha nyingi tena za mkopo, lakini matokeo yake inachukua muda mrefu. Ni vizuri mkawa na miradi michache, hata kama mtakopa lakini angalau iwe michache mwisho wa siku iweze kuwa na ufanisi. Kama ambavyo mmefanya hapa, kuna miradi mingi lakini ukiangalia hata mipango ya miaka miwili nyuma iliyopiata hivyo vivyo, mmekuwa na miradi mingi sana ambayo hata leo ukifanyia tathmini nafikiri hakuna hata mmoja ambao tayari umeshaanza kuonesha matokeo, lakini tena mmekopa maana yake mnaendelea kuendeleza Deni la Taifa.

Kwa hiyo, ushauri wangu ni bora muwe na miradi michache yenye matokeo ya haraka lakini itakayotumia fedha kidogo au hata kama ni nyingi lakini kwa ukopaji ambao utakuwa si wa kiwango kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nichangie katika Sekta ya Utalii. Pato la Taifa asilimia 17.2 inachangiwa na Sekta ya Utalii. Maana yake ni kwamba asilimia 25 ya fedha za kigeni inatokana na utalii. Lakini ukiangalia hapo kwenye mpango ambao umewasilishwa na Serikali hamjatilia mkazo wa kutosha wa namna gani sekta hii ya utalii ambayo inaingiza kiwango kikubwa cha Pato la Taifa inawezeshwa ili kuhakikisha utalii huu ambao unaingizia fedha za kigeni nchi hii uweze kuendelea kwa kiwango kikubwa. Mfano, umesema hapa Mheshimiwa Waziri, kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato yanayotokana na utalii. Maana yake ni kwamba mmekuwa mkizoea kuendeleza kuongeza kodi kwenye sekta ya utalii au kwa watu ambao wanafanya biashara ya utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tuliwashauri hapa wakati tunapitisha bajeti kwamba mfute baadhi ya kodi zilizopo kwenye utalii, hamkufuta, wenzetu wa Kenya wakafuta, sisi hapa tukaongeza. Maana yake ni kwamba unaendelea kufanya sekta ya utalii ni ghali sana hapa nchini, mwisho wa siku mzungu au mtalii yeyote atachagua kwenda kwenye eneo ambalo ni rahisi na ataona vile vitu ambavyo anavitaka, kwa hiyo mkiwa mnashauriwa, Waziri mpokee ushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mtu anayewekeza kwenye hoteli za kitalii analipa kodi 46. Mheshimiwa Waziri ni vizuri sana muwe na kodi chache ili watu wengi waingie kwenye kuwekeza kwenye utalii ili tuendelee kupata wageni maana yake utalii utakuwa ni rahisi. Tulimshauri sana Mheshimiwa Profesa Maghembe kipindi hicho lakini hakusikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi nyingine ni ya TALA license, unalipa dola 2,000 kwa magari matatu. Uwe na magari 100 unalipa dola 2,000. Ni kwa nini msifanye kodi hii ikalipwa kwa gari? Ukilipa kwa gari maana yake utawa- encourage watu wengi wawe na magari, utalii utakua, ushindani utakuwa mkubwa, biashara itakua. Unalipa dola 2,000, magari 100; wale Leopard Tours Arusha, makampuni makubwa wana magari 100 mpaka 200 lakini analipa dola 2,000. Kijana wa Kitanzania aliyepambana amepata hela ana magari matatu analipa dola 2,000, hii ni nini Mheshimiwa Waziri?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeishauri Serikali, tulimshauri sana Mheshimiwa Maghembe hapa hakusikia akaendelea kushukilia msimamo huo, nafikiri ni vizuri muangalie hilo. Lakini sekta hii ya utalii pia imeajiri vijana wengi ambao walikosa ajira lakini wameji-engage huku. Kwa hiyo, tunategemea kwamba jinsi ambavyo utalii utaongeza Pato la Taifa ndivyo ambavyo wawekezaji wataingia kwenye sekta hii, ndivyo ambavyo pia vijana wetu wengi watapata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda, Serikali ya Awamu ya Tano mliingia kwa nguvu kubwa sana mkasema nchi hii ni nchi ya viwanda, Tanzania ya viwanda. Lakini siku hizi wimbo huu umeanza kupotea, sijui mnaendeleaje, hausemwi kwa nguvu ile ambayo mlianza nayo mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matamko ya kutafuta kiki za kisiasa. Mheshimiwa Waziri jana wamezindua, wanasema kila mkoa utajenga viwanda 100, maana yake mikoa 26 tunategemea kuwa na viwanda 2,600. Sasa hivi viwanda mnavyotamka, kwanza mtupe tafsiri yake, kwa sababu akija Waziri wa Viwanda anasema vyerehani vitatu kiwanda, akija mwingine anasema viwanda ni viwanda, mtupe tafsiri sahihi ya viwanda ni nini ili siku tunapowafanyia tathmini ya hivyo viwanda ambavyo mmekuwa mkiwaambia Watanzania tujue ni viwanda kweli au si viwanda. Kwa hiyo msitafute kutafuta cheap kiki za kisiasa kuwanufaisha Watanzania wakati sio sawasawa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika Wizara hii, kwa sababu ya muda nitaenda haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ya kilimo inaajiri asilimia 65 ya nguvu kazi ya Taifa; inachangia asilimia 9.9 ya pato la Taifa; inachangia asilimia 65 ya malighafi viwandani na inachangia asilimia 100 ya chakula kinachopatikana hapa nchini. Sekta hii ya kilimo kama ikiwekezwa vizuri itatoa ajira ya kutosha; itaondoa umaskini; tutafikia hicho mnachokitaka kinaitwa Serikali ya viwanda na tutaweza kufikia uchumi wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, sekta hii imekuwa haipewi fedha kama inavyotakiwa. Fedha tunazozitenga hapa Bungeni hazifiki kwenye Wizara na kwenda kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa miaka 10 fedha ambayo imepitishwa na Bunge lako ambayo imefika kwenye Wizara hiyo ni asilimia 2 tu. Mwaka huu fedha hizo za miradi ya maendeleo ambazo zinaombwa imekuwa ni pungufu ya asilimia 23 ya bajeti ambayo tulipitisha mwaka 2017/2018. Maana yake ni kwamba sekta hii ya kilimo imeendelea kupuuzwa, kuachwa nyuma na haipewi msisitizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukuaji wa sekta ya kilimo kwa mujibu wa Ripoti ya Benki Kuu ni kama ifuatavyo: Mwaka 2011 ilikua kwa asilimia 1.9; 2012 ilikua kwa asilimia 3.2; 2013 ilikua kwa asilimia 4; 2014 ilikua kwa asilimia 3.4; 2015 ilikua kwa asilimia 3.2; 2016 ilikua kwa asilimia 1.9; 2017 ilikua kwa asilimia 1.3. Serikali ya Awamu ya Nne wakati inaondoka madarakani iliacha sekta ya kilimo ikikua kwa asilimia 3.2.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mmeingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano mmejiita Serikali ya Hapa Kazi, Serikali ya Viwanda, mmeweka mikakati ya kufikia uchumi wa kati lakini sekta ya kilimo ambayo inategemewa na asilimia 65 ya Watanzania, ambayo inachangia pato la Taifa imeendelea kushuka na kufikia kiasi cha asilimia 1.3. Kwa wastani maana yake ni kwamba sekta ya kilimo imekua asilimia 1.9 tu. Kila siku mnatuambia uchumi unakua kwa asilimia 7, Watanzania asilimia 65 wanategemea kilimo, halafu uchumi huu wa sekta ya kilimo tu unakua kwa asilimia 1.9 halafu mnataka miujiza mfikie kitu kinachoitwa uchumi wa kati? Haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wa nchi hii ni lazima wajue adui yao ni Serikali hii ambayo ina mipango mibovu ya kutoweza kuiwezesha sekta ya kilimo. Asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo lakini uwekezaji unaofanywa kwenye sekta hii ni kiasi cha asilimia 0.52 ya bajeti kuu ya Taifa lakini asilimia 5 ya Watanzania ambao wanategemea usafiri wa ndege inapewa kipaumbele ndege unawaacha asilimia 65 ya Watanzania ambao wanategemea kilimo. Huku ni kuwahadaa Watanzania, ni kuwahadaa wakulima, ni kuwadanganya wakulima wa Tanzania. Wakulima wa nchi hii adui yenu ni Serikali hii ya CCM iliyoko madarakani. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikia hapa michango ya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wakilalamikia suala la mahindi kutokuuzwa. Nimeona leo mzigo anashushiwa Mheshimiwa Tizeba pale, hivi tumesahau ni nani alikataza mahindi yasiuzwe. Kauli zikatolewa hapa kwamba mahindi yasiuzwe na Mheshimiwa Waziri Mkuu alisimama hapa akasema hakuna kuuza mazao nje ya nchi. Sasa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanasimama wanampongeza Waziri Mkuu, wanampongeza Rais, wanamshushia mzigo Mheshimiwa Tizeba pale na Mheshimiwa Tizeba ataubeba tu mzigo huu kwa sababu kama huwashauri tunafanyaje.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, uhifadhi wa Ziwa Manyara; ziwa hili ni miongoni mwa maeneo ya utalii hapa nchini kwa watalii wengi kutembelea. Hata hivyo, ziwa hili lipo kwenye hatari ya kupotea/kutoweka kutokana na tope lililojaa ziwani kunakosababishwa na shughuli za kilimo katika maeneo yanayozunguka ziwa. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka kuokoa Ziwa Manyara ambalo ni kivutio cha utalii hapa nchini?

Mheshimiwa Spika, kuhusu tozo nyingi katika hoteli za kitalii; tunapohitaji sekta ya utalii iendelee kukua na kuongeza pato la Taifa ni muhimu na ni lazima kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri na rafiki kwa wawekezaji katika sekta hii ya utalii. Hoteli za kitalii zimekuwa zikilipa tozo nyingi sana hivyo kufanya hoteli hizi kuwa na mazingira magumu kuendesha biashara.

Ushauri, Serikali itazame kwa upya tozo hizi ili kuendelea kuwajengea mazingira mazuri wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, TALA ni leseni inayotolewa kwa makampuni ili waweze kuendesha shughuli za utalii. Hata hivyo leseni hii imekuwa ikilipwa na/au kutolewa kwa mtu akiwa na magari matatu kwa kulipa dola 2,000. Hata hivyo, mtu akiwa na magari zaidi ya matatu analazimika kulipa sawa na mwenye magari matatu (kwa kuwa ni takwa la kisheria). Hivyo basi, mtu akiwa na magari 50 au 100 atalipa sawa na mwenye magari matatu. Hapa hakuna usawa na ni unyonyaji kwa watu na kuendelea kuweka mazingira magumu kwa vijana wanaotaka kujiajiri.

Mheshimiwa Spika, ushauri, Serikali itoze leseni hii kwa kila gari, kwa kufanya hivi Serikali itaongeza mapato na kutawapa vijana nafasi/fursa ya kuingia katika sekta ya utalii na kujiajiri.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika hoja iliyoletwa mezani kuhusu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/ 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeeleza vipaumbele vitatu ikiwemo kilimo, viwanda, huduma za jamii kwa maana ya maji, elimu na afya. Mimi nitachangia katika suala la kilimo na elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya CCM toka tumepata uhuru wananchi hii imekuwa na kaulimbiu na mikakati mingi kuhusiana na sekta ya kilimo. Tulikuwa na kaulimbiu na mikakati mingi ikiwemo, Siasa ni Kilimo ya mwaka 1974, Azimio la Arusha la mwaka 1967, Azimio la Iringa mwaka 1974 lakini hata mwaka 2009 tulikuja na Kilimo Kwanza na Serikali ya Awamu ya Nne pia katika Big Results Now, sekta ya kilimo na yenyewe iliongezewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna ambaye anapinga umuhimu wa sekta ya kilimo kwa Watanzania. Nilipochangia Wizara ya Kilimo hapa nilieleza umuhimu wa sekta ya kilimo kwamba inaajiri nguvu kazi asilimia 65 ya Watanzania, inachangia asilimia 30 kwenye pato la Taifa, malighafi viwandani asilimia 65 inatoka sekta ya kilimo na asilimia 100 ya chakula hapa nchini inatoka kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika malengo ya MKUKUTA ya miaka 10, ilijiwekea mkakati wa ukuaji wa sekta ya kilimo angalau kwa asilimia 6 mpaka asilimia 8. Ukuaji wa sekta ya kilimo kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2011 mpaka 2015 umekua kwa asilimia 3.4 tu. Hata hivyo, toka Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, Serikali ya Hapa Kazi, Serikali ambayo inataka kutupeleka kwenye uchumi wa Kati, Serikali inayojiita ya viwanda, ukuaji wa sekta ya kilimo pamoja na umuhimu wake wote umeshuka ukilinganisha na Serikali ya Awamu ya Nne ilivyokuwa madarakani. Ukuaji wa sekta ya kilimo umekua kwa asilimia 1.9 tu toka mwaka 2016 mpaka 2017. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, bajeti ambazo tumekuwa tukizipitisha hapa Bungeni kwenye sekta ya kilimo imekuwa haifiki kwenye Wizara, hazitolewi kwa wakati. Mwaka 2016/2017 tulipitisha Bungeni hapa shilingi bilioni 100 zilizotolewa ni shilingi bilioni 2 tu fedha za maendeleo ni sawasawa na asilimia 2.2. Mwaka 2017/2018 sekta ya kilimo ilitengewa shilingi bilioni 150 zilizotolewa ni shilingi bilioni 16.5 sawasawa na asilimia 11 na mwaka huu fedha zilizoombwa kwenye sekta ya kilimo kwa maana ya Wizara ya Kilimo zitakazotekeleza miradi ya maendeleo ni shilingi bilioni 98.1. Tunawashangaa sana kila siku Serikali iliyoko madarakani, pamoja na kaulimbiu zenu na mikakati yenu mnayosema kwenye vitabu lakini sekta ya kilimo ambayo tunaitegemea sisi Watanzania tulio wengi, mmeendelea kutoipa kipaumbele na kutoona umuhimu wa sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukifanya uwiano kati ya bajeti kuu ya Serikali na sekta ya kilimo, mwaka 2016/2017 uwiano kati ya bajeti kuu na sekta ya kilimo kama ambavyo mmesaini Maazimio mbalimbali ya Kimataifa ni asilimia 0.93, mwaka 2017/2018 ni asilimia 0.85, mwaka 2018/2019 ni asilimia 0.52 na mwaka huu imeshuka zaidi ukilinganisha na miaka mingine. Sasa tunajiuliza mmesema mtaweka kipaumbele chenu cha kwanza ni sekta ya kilimo lakini sekta hiyo hiyo ya kilimo hamuipi fedha, mmewasahau Watanzania wakulima walio wengi, tutawaaminije? Mbona mmetudanganya miaka mingi sana? Mmekuwa wazuri kwenye maandishi, kwenye vitabu lakini kuja kwenye utekelezaji mmekuwa tofauti kabisa. Kwa kweli nirudie kusema, wakulima wa nchi hii adui yenu namba moja ni Serikai iliyopo madarakani kwa mikakati na sera mbovu ambazo hazitekelezeki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutuambia kwamba kwenye bajeti hii kipaumbele ni kilimo lakini miaka iliyopita, mavuno ya mwaka juzi, wakulima mbaazi tu imewasumbua mpaka leo, kupata masoko ya wakulima wetu mbaazi ni mtihani, korosho ni mtihani, pamba ni mtihani yaani hakuna ambako afadhali, tumbaku ni mtihani, mahindi imewasumbua mwaka mzima yanawahangaisha mnakataza vibali, mnageuka kwa nyuma mnaruhusu vibali. Kahawa imewasumbua, pamba, mkonge, mazao mchanganyiko hakuna mkulima wa nchi anayelima zao lolote ambaye ana uhakika wa soko. Sasa mnasema kipaumbele ni kilimo mnawahakikishiaje Watanzania wakulima kuwa na uhakika wa masoko? Nini mkakati kwenye bajeti hii kuhakikisha wakulima wana masoko ya kutosha? Tunaomba majibu Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu sekta ya elimu. Serikali ya Awamu ya Tano mmesema mnatoa elimu bure na Serikali ya Awamu ya Nne iliona kutoa elimu bure ni changamoto, ikaona namna bora ni kusaidiana na wazazi kuhakikisha wanakabiliana na upungufu mbalimbali kwenye sekta ya elimu ikiwemo miundombinu na changamoto nyingi katika shule zetu za msingi na sekondari hapa nchini. Ninyi mmekuja, mmefuta michango, mnasema elimu ni bure, Mheshimiwa Waziri kwenye mambo yako 10 uliyoyataja hapa ya kumsifia Rais Magufuli umeelezea suala la elimu bure, nataka nikwambie elimu bure imekuwa na changamoto kubwa, mnaua sekta ya elimu kuliko hata Serikali ya Awamu ya Nne ilivyokuwa madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe takwimu, upungufu wa walimu, shule za msingi, mwaka 2016 upungufu ulikuwa 191,772 mwaka 2017 upungufu umeongezeka umefika 179,291; shule za awali, upungufu wa walimu umekuwa 1,948; shule za sekondari masomo ya hisabati upungufu wa walimu ni 7,000, baiolojia 5,000, kemia 5,000, na fizikia 6,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa miundombinu; upungufu wa maktaba…

T A A R I F A . . .

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, siipokei hiyo taarifa na kitu ambacho nafikiri Serikali mnakosea sana, mnapima mafanikio ya elimu bora na idadi ya uandikishwaji siyo quality na hiki kitu mmekuwa mnakisema siku nyingi. Pia idadi ya wanafunzi wanaondikishwa inawezekana ikaongezeka kwa sababu ya uzao, birth rate nayo inawezekana ikawa inaongezeka, population inaongezeka, sasa mnapimaje hayo? Mheshimiwa Naibu Waziri utapata nafasi baadaye na wewe utasema ya kwako.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upungufu wa maktaba; mwaka 2016 upungufu ulikuwa ni asilimia 88, mwaka 2017 upungufu umekuwa ni asilimia 91. Maana yake badala ya kwenda mbele kupunguza changamoto mbalimbali za kimiundombinu tunarudi nyuma hatua kadhaa haya matatizo yanazidi kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maabara; upungufu wa maabara ya baiolojia ni asilimia 51, fizikia 54 na kemia 53. Upungufu wa madawati ni milioni 1,170,000 na upungufu wa walimu ni 186,000. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajiuliza, mnatuambia elimu bure, elimu hii siyo bure, mnakwenda kuua Taifa la kesho. Badala tuliandae Taifa la kesho, mnajua umuhimu wa elimu ni kuandaa rasilimali watu, kuliandaa Taifa, tuwe na wataalam na wajuzi wa kutosha, tuandae mazingira ya kufikia haya, tunatengeneza mazingira mabovu ya kuwa na elimu mbovu ya kuiangamiza nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia ripoti ya LAAC na mimi pia ni mjumbe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 1998 na mwaka 2008 ilifanyika reforms kubwa sana kwenye Local Government na ilitumia fedha nyingi. Reforms hizo zilielekeza kuwajengea uwezo watumishi kwa maana ya Mkurugenzi na timu yake na menejimenti kwa ujumla lakini pia reformshizo ziliwajengea uwezo Madiwani katika kusimamia fedha za Halmashauri zinazoletwa katika Halmashauri zao na reforms hizi zilitumia fedha nyingi kama nilivyoeleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani kwa kweli imeonesha kabisa kutokuzithamini Local Government kwanza kwa uteuzi tu uliofanyika wa ma- DED tumeona ma-DED walioteuliwa kwa kiwango kikubwa wengi hawana uwezo, hawakutoka kwenye mfumo wa Local Government. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma utaratibu uliokuwa unatumika kutokana na hizo reformszilizofanyika, Mkurugenzi alikuwa anateuliwa ni mtumishi wa Serikali za Mitaa ambaye amehudumu kwa kipindi kisichozidi miaka mitano anaenda kuteuliwa kushika hiyo nafasi. Hii maana yake ni kwamba alitakiwa awe anazielewa Serikali za Mitaa, ajue kusimamia fedha vizuri, aielewe Serikali za Mitaa kwa ufanisi zaidi, lakini sasa hivi watendaji walioteuliwa kwa kweli hawana uwezo wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndiyo yanayosababisha tunaona Local Government leo hata miradi kwanza miradi yenyewe inayotekelezwa vipaumbele vinavyowekwa havifikiwi na wala havifanyiki kwa sababu ya upungufu huo. Pia reforms zile zilijenga uwezo kwa Madiwani, leo Madiwani wetu kwanza hata baadhi ya Halmashauri vikao havikai, hakuna fedha. vikao havifanyiki, Kamati za Fedha hazisimamii ipasavyo hata hizo fedha kidogo zinazopelekwa kwenye Local Government. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani tufike mahali kama nchi kama utawala wa awamu fulani unafanya mambo wa kadha wa kadha. Mfano, kama tulifanya reforms kwenye tawala zilizopita huko nyuma, utawala unaokuja hauna budi kurithi na kuhakikisha inaendeleza yale ambayo yaliendelezwa na utawala uliopita na sio kupindisha. Nadhani uzalendo wa nchi hii ni pamoja na kuyaenzi na kuyatekeleza yalifanyika kwenye awamu zilizopita na kuendeleza na si kuharibu ama kufanya ambavyo haitakiwi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeongea toka tunaanza Bunge hili na sasa tunaelekea ukomo wa Bunge hili. Tumeeleza jinsi ambavyo Serikali za Mitaa zimenyang’anywa mapato ya uhakika ambayo kwa kiwango kikubwa ndio yalikuwa yanasaidia kuwepo na uhai wa Serikali za Mitaa.

Leo wamenyang’anya vyanzo vya uhakika, mambo hayaendi kwenye Serikali za Mitaa, tutaendelea kuwataka Serikali kuhakikisha kwanza vyanzo vya uhakika kwenye Local Government vinarudishwa, waziachie Halmashauri zikusanye mapato/hizo fedha ili iweze kuendeleza miradi katika maeneo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni hiki kitu kinachoitwa force account; Serikali inaisemea sana na kuipigia chapuo, lakini mimi naona kutakuwa kuna shida kubwa sana mbeleni. Hizi force account miradi inayotekelezwa kwaforce account inaenda kutekelezwa kwa kiwango kikubwa na hao mafundi ambao watateuliwa kwa utaratibu unaokuwepo lakini hatuangalii ubora wa majengo yanayojengwa kwa force account. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunawataka wasimamizi kwa maana ya Mainjinia wa Wilaya wakasimamie lakini tuna mainjinia wangapi kwenye wilaya moja wakasimamie miradi hii kuangalia ubora wa majengo yanayojengwa? Mainjinia wenyewe hawatoshi, utakuta kwenye wilaya moja labda kuna miradi minne ama mitano inayojengwa kwa force account halafu unataka injinia mmoja kwenye Halmashauri kwa sababu pia tuna upungufu mkubwa sana kwenye Halmashauri, unataka injinia huyohuyo mmoja akasimamie, hivi ufanisi wa miradi hii uko wapi?.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokwenda mbele watakuja kuona miradi ya force account majengo yanaanguka tu hovyo hovyo kwa sababu hayajajengwa kitaalam, hayana usimamizi wa kila siku, tunawaachia hao mafundi sanifu ambao kwa kweli hawakidhi vigezo wanaenda wanazitazama hatuwaachii mainjinia, kwanza hatuna lakini haipati usimamizi wa kutosha kuhakikisha kwamba miradi hii kwa kweli inasimamiwa inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la miradi ya mikakati. Kuna fedha nyingi sana zinakopwa kwa ajili ya miradi ya mkakati. Mfano hapa Dodoma…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Muda wako umeisha Mheshimiwa, zilikuwa dakika tano, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea kuhusu Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Majukumu ya jeshi hili ni kupambana na majanga ya moto pamoja na kufanya uokoaji pale inapotokea majanga. Jeshi hili umuhimu wake unaonekana zaidi pale panapotokea majanga, hata hivyo umuhimu wake haupewi uzito kutokana na kutopewa fedha za kutosha na vitendea kazi ili waweze kufanikisha majukumu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ihakikishe inalisaidia au inalipatia Jeshi la Zimamoto na Ukoaji fedha za kutosha na vitendea kazi vya kisasa ili utekelezaji wa majukumu uwe na ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, vituo vya polisi nchini. Vituo vya polisi nchini vingi vina uchakavu wa kutisha. Vituo hivi vimekuwa vikihifadhi wahalifu pamoja na uchakavu huo jambo ambalo ni hatarishi kwa usalama. Umuhimu wa kukarabati vituo hivi ni jambo ambalo haliepukiki. Jeshi lipange kimkakati wa ukarabati wa vituo hivi kwa awamu ili kuwa na vitu bora na vinavyokidhi haja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Jeshi la Magereza. Jeshi hili lina jukumu la kuwahifadhi wafungwa na kutazama mahitaji yao kwa ujumla, lakini majukumu haya hayatekelezwi ipasavyo kwa ufinyu wa bajeti na vitendea kazi ili kufanikisha majukumu yake. Msongamano ni mkubwa katika magereza yetu, magari ya kupeleka wafungwa mahakamani ni machache na mabovu sana. Nashauri Serikali itenge fedha za kutosha ili kukabiliana na upungufu mkubwa uliopo katika hili Jeshi la Magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, vitambulisho vya uraia. Vitambulisho vya uraia ni haki ya kila Mtanzania kwa kuwa ndicho kinachomtambulisha. Zoezi hili licha ya kushushwa kwenye wilaya zetu limekuwa la kusuasua na kuleta usumbufu na urasimu usiokuwa na ulazima. Wananchi wametakiwa kuchangia fedha ili kupata vitambulisho hivyo. Kwa nini Serikali inachangisha wananchi wakati ni haki ya wananchi kupatiwa vitambulisho. Serikali inawajibika kuwapatia vitambulisho bila vikwazo kwa kuwa Serikali inakusanya kodi ambazo zinapaswa kuwahudumia wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, upelekaji wa fedha za maendeleo katika Hospitali za Mikoa imekuwa wa kusua jambo ambalo linakwamisha shughuliza za utoaji wa huduma katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuwa mahitaji ya fedha za maendeleo ni mkubwa katika sekta na maeneo mbalimbali, hivyo basi naishauri Serikali kuliko kugawa fedha za miradi ya maendeleo kwa mtawanyiko wa nchi nzima bila kuonesha matokeo ya haraka na miradi kubaki viporo. Nashauri fedha za miradi ya maendeleo kila mwaka ipelekwe kikanda kwa kuangalia na kutanguliza maeneo yenye mahitaji makubwa zaidi. Hata hivyo ugawaji huu uendane na takwimu zinaonesha uhitaji upo kwa kiwango gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu upungufu wa watumishi katika sekta ya afya, sekta hii inakabiliana na upungufu wa asilimia 49 ya watumishi wa afya katika mwaka a fedha 2016/2017; changamoto hii imekuwa ya muda mrefu hasa maeneo ya vijijini jambo ambalo linapelekea wananchi kukosa huduma na hasa tukilinganisha idadi ya ongezeko la watu nchini. Naishauri Serikali kuhakikisha inaweka mkakati wa haraka wa kuhakikisha inakabiliana na changamoto hii kwani idadi ya watu nayo inaongezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu chakula na lishe, tatizo la udumavu nchini ni kubwa kutokana na lishe duni kwa watoto na wajawazito, udumavu huu kwa watoto ambao ndiyo Taifa la kesho maana yake tutatengeneza Taifa la udumavu. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na REPOA takribani watoto milioni 2.4 wana udumavu; takwimu hii ni kubwa na watoto hawa wengi ni wale walio katika kaya maskini za vijijini. Hivyo basi, Serikali ituambie ina mkakati gani wa kuiwezesha Taasisi ya Chakula na Lishe kifedha na kuweka mikakati ya haraka ya kukabiliana na hali hii ya lishe duni unaosababisha udumavu kwa watoto hapa chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uzazi wa mpango, uwekezaji wa Serikali katika mpango wa uzazi ni jambo la muhimu sana kwani jambo hili limekuwa haliwekewi fedha za kutosha, umuhimu na uhusiano wa mpango wa uzazi na mkakati wa kupunguza vifo vya wanawake wajawazito; uzazi vina mahusiano ya karibu, hata hivyo kukiwepo na uzazi wa mpango ndivyo ambavyo tunaweza kupanga mipango bora ya maendeleo. Nashauri Serikali ihakikishe upatikanaji wa madawa, vifaa vya uzazi wa mpango katika maeneo yote ya utoaji wa huduma ya afya nchini. Serikali iongeze bajeti na kutoa fedha zilizoainishwa za fungu hili. Pia kuwa na huduma na vituo vya afya ya uzazi kwa vijana nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu pensheni kwa wazee; wazee wa nchi hii wamekuwa wakipewa matumaini ya kupatiwa pensheni bila mafanikio yoyote. Je Serikali ina mpango kati wa haraka wa kutoa pensheni kwa wazee nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, uwakilishi na usawa wa kijinsia, kwa mujibu wa takwimu za Employments and Earns Report ya mwaka 2015 nafasi za wanawake walioshika nyadhifa mbalimbali ni asilimia 15 tu ya idadi ya waajiri, wateuliwa na wachaguliwa wote nchini. Idadi hii ni ndogo sana. Hivyo basi Wizara iwajibike kuona ongezeko la usawa wa kijinsia katika nafasi mbalimbali unaongezeka zaidi, nawasilisha
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi nichangie katika hoja iliyoko mbele yetu kuhusiana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imekuwa ni kama desturi au taratibu zinatutaka tupitishe Mipango hii na mara nyingi imekuwa ni Mipango mizuri sana kwenye maandishi na imekuwa ni Mipango mingi kwa mara moja lakini ukija kwenye utekelezaji ndipo ambapo kunakuwa na changamoto kubwa. Utekelezaji umekuwa ni hafifu kwa sababu kwanza tumekuwa na mipango mingi ndani ya mwaka mmoja wakati tunaambiwa hako kasungura tunakokakusanya nako ni kadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni bora tuwe na Mipango michache ambayo inahusiana moja kwa moja na maisha ya mwananchi wa kawaida, tukaitekeleza kwa ufanisi, tukamsaidia yule mwananchi wa chini kabisa maskini. Tukipitisha mipango tukaenda kupitisha na bajeti maana yake fedha zitolewe na bajeti hiyo iweze kutekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, tunapitisha mipango mbalimbali kwenye sekta zote muhimu zinazomgusa Mtanzania mfano ya kilimo, maji, viwanda, afya, yote kwa namna moja au nyingine inamgusa mtanania wa chini kabisa. Hata hivyo, tukipitisha Mipango hii ukija kwenye kuangalia namna gani bajeti zinapitishwa kwenye Wizara hizi haiendani kabisa na kile ambacho tumekipitisha. Fedha hazitolewi kwa wakati, wakati mwingine hata kikitolewa hicho kidogo kinafika kwa kuchelewa maana yake kile tulichokipitisha basi kinakuwa ni kama hakuna kwa sababu hakuna matokeo ambayo yanafikiwa kulingana na kile ambacho tumekipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala la mfumuko wa bei, ukisoma Mpango hapa unaeleza kabisa kwamba mfumuko wa bei Serikali imeendelea kudhibiti. Uhalisia sidhani kama iko hivyo, inawezekana imedhibitiwa kwenye makaratasi lakini tukitoka nje ya jengo hili huo mfumuko wa bei unaosemwa haujadhibitiwa kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Desemba mwaka jana mpaka leo hii January tunapoongea kuna mfumuko mkubwa sana wa bei ya bidhaa. Mfano, unga wa ngano wa kilo 50 ilikuwa inanunuliwa kwa Sh.60,000 leo unanunuliwa kwa shilingi 69,000. Unaenda kwenye mafuta ya kula ya lita 20, yalikuwa yananunuliwa kwa shilingi 52,000 leo yananunuliwa kwa shilingi 82,000. Ukienda kwenye bidhaa za ujenzi, vivyo hivyo, bati zimepanda bei, saruji ndiyo usiseme. Saruji sio tu kupanda bei, yaani saruji imekuwa bidhaa adimu ndani ya nchi hii na tuna viwanda. Saruji ilikuwa inanunuliwa kati ya shilingi 13,000 au shilingi 14,000 leo unaitafuta kwa shilingi 17,000 mpaka shilingi 28,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisoma Mpango, Hali ya Uchumi wanakwambia mambo ni mazuri, Serikali ya wanyonge inasema hakuna mfumuko wa bei mambo yako sawasawa. Sasa, mambo kweli yako sawasawa kwenye makaratasi lakini hayako sawasawa tukitoka nje ya hapa. Bati za geji 8 zilikuwa zinanunuliwa kwa Sh.62,000 leo zinafika Sh.70,000 na zaidi. Nadhani yale mnayoyanena kwenye makaratasi basi yanenwe kwa vitendo huko nje tunakotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la mfumuko wa bei nadhani lipatiwe ufumbuzi sasa hivi halisubiri bajeti. Mtuambie, Watanzania huko nje wanataabika, mambo ni magumu, kila kitu kimepanda bei hatuelewi ni kwa nini kimepanda bei na bidhaa nyingine hazipatikani kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo napenda kuichangia ni kuhusu wafanyabiashara. Wafanyabiashara wa nchi hii imekuwa kama ni ule mchezo wa paka na panya. Ni mchezo wa kuviziana, wa kutafutana. Leo wafanyabiashara wa nchi hii wako wengine ambao wanaamua kufunga biashara kwa sababu mazingira ya ufanyaji wa biashara siyo rafiki hata kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa Dodoma hivi tunavyoongea kuna wafanyabiashara wengi tu wameshaandikiwa barua na TRA; wengine wanataka kufungiwa akaunti na wengine wanaanza kufikiriwa kupelekewa hiyo task force ya kuangaliwa kodi ya miaka mitatu nyuma. Kuna wafanyabiashara kule Karatu wamepelekewa hizo task force zinawachunguza eti wanachunguzwa mapato yao kwa miaka mitatu nyuma yalikuwaje wakati huyu mtu analipa kodi yake kila mwaka hajawahi kukwepesha kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tunaambiwa mashamba hayatozwi kodi, Karatu kule kuna wafanyabishara kwenye Bonde la Eyasi wanalima vitunguu, wote wameambiwa wanapelekewa hiyo task force inachunguza kwa miaka mitatu namna gani wanalima, mapato yao ni nini, wana wafanyakazi kiasi gani, wanatakiwa kulipa nini na kwa nini hawajalipa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Cecilia Paresso.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, wote wanalima mashamba ya vitunguu, lini tumeanza tena kutoza kodi mpaka mashamba? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ushauri wangu kwa Serikali.

SPIKA: Muda wako umeisha.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani kidogo tu nimalizie, ili uweze kuongeza mapato ni kuwatengenezea wafanyabiashara mazingira rafiki na unapunguza kodi, ndivyo ambavyo utapata kodi nyingi. Ukiongeza kodi unafukuza na kufunga biashara. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Miswada iliyoko mbele yetu, mchango wangu utajikita katika Muswada wa kuanzisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni takriban asilimia 73 ya Watanzania hutegemea kilimo na ni muhimu sana ili kilimo hiki kimnufaishe Mtanzania au Watanzania hawa wa asilimia 73 ni lazima hiki kilimo kiwe na manufaa, kiwe na tija lakini ni lazima kiwe ni kilimo ambacho tafiti zitafanywa zitaweza kuwasaidia kuboresha kilimo chao ili kiweze kuwasaidia kwa maana ya uchumi, mahitaji ya familia na mahitaji ya nchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba tumekuwa tukianzisha hizi taasisi. Hii ni moja tu ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo lakini tunakuwa na taasisi nyingi na Muswada huu unapendekeza kuanzisha taasisi hii ambayo itakuwa ina Bodi, Menejimenti na Itakuwa na Baraza la Taifa la Utafiti. Kikwazo kikubwa ambacho mara nyingi tunakiona ni uwezeshwaji wa hizi Taasisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna changamoto kubwa sana, Taasisi zinaundwa, zinaachwa, fedha inapewa „kiduchu‟, inapewa OC, zile za other charges lakini fedha kwa ajili ya maendeleo na fedha kwa ajili ya shughuli maalum hasa ya utafiti inakuwa ni mtihani na mara nyingi hili tumeliona. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Wizara na Serikali kwa ujumla kwamba ni muhimu sana mtakapokamilisha mchakato huu kuhakikisha hii taasisi inapatiwa fedha ya kutosha kuhakikisha inaendesha shughuli zake, inafanya utafiti ili iweze kuwasaidia wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na fedha, wanahitaji pia kupata fedha au wanahitaji kupata fedha za uwezeshwaji wa kununua hivyo vitu ambavyo watafanyia utafiti au ambavyo vitaendana na teknolojia ya kisasa zaidi ili kuwasaidia na kurahisisha ufanyaji wao wa kazi. Kwa hiyo, ni muhimu sana, pamoja na kwamba tunapitisha hii Miswada, tunaunda hizi Taasisi ambazo ziko nyingi lakini bila kuwezeshwa kwa bajeti ya uhakika ya maendeleo mwisho wa siku hizi taasisi zitabaki tu kwenye makaratasi itakuwa hakuna kazi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi hii itakuwa ina kazi ya kuratibu utafiti, ufuatiliaji na tathmini, kwa hiyo, ni muhimu sana inapofanya tathmini yake, inapofanya tafiti yake, haya matokeo yanayopatikana ni lazima yawe-shared yaweze kushirikisha na mrejesho uweze kuwafikia wadau husika kwa maana ya wakulima au wale wote ambao wananufaika kwa namna moja ama nyingine. Kwa hiyo, haya ni masuala ya msingi sana kuyazingatia kuona tathmini hii inayofanyika ni lazima wadau washirikishwe, ni lazima wadau waweze kunufaika nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii taasisi sasa ni lazima iangalie namna ambavyo itaungana au itaunganisha nguvu za pamoja na vyuo vyetu vikuu ambavyo vimekuwa vikifanya tafiti mbalimbali. Kwa hiyo, tusiwaache pembeni pia wataalam wetu, kwamba leo tunaanzisha hii Taasisi lazima pia tuangalie namna gani tutaendelea kushirikisha na kuunganisha nguvu za pamoja na hivi vyuo vikuu ambavyo vimekuwa vikifanya tafiti miaka yote kabla ya kuanzisha chombo hiki. Kwa hiyo, haya ni mambo ya msingi ya kuzingatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kuanzisha Taasisi hii, tunatarajia kwamba ni lazima Serikali sasa itumie takwimu hizi, itumie matokeo ya tafiti hizi katika upangaji wa mipango yake, katika upangaji wa bajeti, katika kukifanya kilimo kiwe na tija kwa wakulima. Kwa hiyo, ni lazima hili likazingatiwa kuona tunaanzisha taasisi inakuwa na matokeo fulani, inakuwa na mitazamo fulani, inakuwa ina ushauri fulani kuhusiana na masuala haya ya kilimo, ni vyema Serikali ikayafuata, ikayachukua, ikawa ni dira yake ya kupangia bajeti na mipango mbalimbali ya sekta ya kilimo hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie sasa kwa kuchambua kidogo Muswada na kutoa mapendekezo. Ukisoma Muswada huu wa Kiswahili, kwenye heading pale inahitaji kufanyiwa marekebishao kwa sababu kule juu inasomeka Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, lakini content zote ni Taasisi ya Kilimo na mwanzo kabisa wa heading hapa kwenye Kiswahili, ya Kiingereza iko sawa, lakini kwenye Kiswahili imeanza, ukurasa wa kwanza iko sawa, kwamba ni Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, lakini ukiendelea page ya pili mpaka ya mwisho inasomeka Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi na siyo Mifugo. Kwa hiyo, nadhani inahitaji kufanyiwa marekebisho ili iweze kuleta maana sahihi kama ilivyokusudiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kifungu cha 5(2)(a) kinasema, Mwenyekiti wa Bodi atateuliwa na Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 8(1) pia kinaeleza, Mkurugenzi atateuliwa na Rais. Kama ambavyo Kambi ya Upinzani imependekeza ni lazima tuondoke kwenye huu mfumo wa uteuzi, tuingie kwenye mfumo wa ushindani, tushindanishe watu wenye sifa, tutangaze hizi kazi, ni kazi ambazo kwa kweli zinahitaji utaalam na watu ambao wako tayari. Kwa hiyo, ni lazima tuondokane na huu mfumo wa uteuzi ambao umekuwa ni mwingi mno wa kubebana. Ni lazima tutoke huku tushindanishe hizi kazi, watu wenye sifa waombe, wachujwe kwa vigezo ili mwisho wa siku waweze kupata hizi nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukienda Kifungu cha 8(2)(d) wanasema katika uteuzi wa huyu Mkurugenzi anasema awe mbunifu, najiuliza hivi utapimaje ubunifu wake wakati ndiyo uko kwenye uteuzi? Sina hakika kama unaweza ukapimika ubunifu wa mtu kabla hujampa task fulani aifanye. Kwa hiyo, nadhani hapa inahitaji kurekebishwa labda ibaki tu yale maneno mengine kwamba awe na uzoefu na uadilifu, lakini ubunifu sina uhakika kutakuwa na kigezo gani cha kumpima ubunifu wake. Kwa hiyo, nadhani inahitaji kufanyiwa marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Kifungu cha 21(1)(c) kinazungumzia kuanzisha Kamati ya Kitaifa za kuratibu tafiti za mazao. Mwanzoni kwenye vifungu vingine inaeleza mfumo wa taasisi, kutakuwa kuna Bodi, kutakuwa kuna Menejimenti, kutakuwa kuna Baraza la Ushauri la Utafiti la Kitaifa, lakini huku tena mnasema kutakuwa kuna Kamati za Kitaifa za kuratibu utafiti wa mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani tunaweza tukawa na Kamati na Mabaraza mengi ambayo mwisho wa siku ukiyapima au pamoja kuyapima yatakuwa na gharama kubwa za uendeshaji lakini ukipima hata matokeo yake yanaweza mengine yanaingiliana kazi zake au majukumu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani ama Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi wakati anahitimisha ama hili liweze kufanyiwa marekebisho na kuona namna gani linaondolewa ili kupunguza hizi Kamati na haya Mabaraza ambayo yamekuwa mengi, mwisho wa siku inagharimu fedha nyingi ikiwa na matokeo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie tu kwa kusema kwamba ni lazima Serikali iangalie umuhimu wa kuwezesha hizi taasisi ambazo zimekuwa zikianzishwa, siyo tu kuwapa fedha za mishahara, fedha nyingine za OC, lakini fedha za maendeleo hamuwapi. Kwa hiyo, ni lazima Serikali muwajibike kuwapa fedha ili hiki kinachokusudiwa katika Muswada huu na kuwalenga Watanzania asilimia 73 ambao wao wanategemea kilimo, basi kiweze kuwa na tija na manufaa, kwao binafsi, jamii zao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Muswada huu ambao umewasilishwa mbele yetu siku ya leo, na naunga mkono maoni ya Kambi ya Upinzani ambayo yamewasilishwa hapa. Ni vizuri sana Serikali mkatupa majibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuongezea mchango wangu, napenda kwanza watuambie ni kwa nini leo wanatuletea mapendekezo haya ya kutoka kuwa Kampuni ya Simu na kwenda kuwa Shirika la Mawasiliano. Mheshimiwa Waziri hapa ameeleza kwamba Muswada huu sasa unaitoa TTCL kutoka kampuni kwenda shirika kwa mambo ambayo ameeleza hapo; moja likiwa ni kulinda usalama wa nchi. Tunajiuliza, ilipokuwa kampuni ilikuwa haiwezi kulinda usalama wa nchi? Jambo la pili, amesema kukuza uchumi; ilipokuwa Kampuni ya TTCL ilikuwa haikuzi uchumi, leo tunapobadilisha kwenda shirika ndiyo itakuza uchumi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kutoa huduma za mawasiliano kwa jamii; ilipokuwa kampuni ilikuwa haitoi huduma, leo tunapofikiria kuwa na Muswada wa kwenda kuwa shirika, je, ndiyo itaweza kutoa huduma hizo za mawasiliano kwa jamii? Nadhani kinachokosekana sio ubadilishaji wa sheria kutoka kampuni kwenda shirika, kinachokosekana ni Serikali kutokuziwezesha hizi kampuni ambazo zimeanzishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, TTCL imekufa kwa sababu ilikuwa haiwezeshwi na Serikali, haipewi ruzuku kwa wakati, haiboreshwi, haiendani na ushindani uliopo. Kwa hiyo,leo wakituletea tu kusema wanabadilisha, kama hawatahakikisha hilo shirika ambalo leo tunataka kulipitisha hapa litapatiwa ruzuku ya kutosha, maana yake litaendea kuwa kama ambavyo leo liko katika hali mbaya sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo hotuba yetu ya Kambi imesema, tunahitaji pia kuhakikisha namna gani Serikali inatoa ruzuku kwa wakati na kuwepo na vyanzo vya uhakika vya kuwezesha hili Shirika la Mawasiliano la Taifa. Kwa hiyo,ni muhimu sana, pamoja na kuwa na sheria nyingi au sheria tu kwenye vitabu, lakini bila uwezeshaji bila shaka hakuna kitu kitakachofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunapofikiria wananchi wetu waweze kupata mawasiliano kama ambavyo Mheshimiwa Waziri amesema, ni mawasiliano ya namna gani, yanaweza kuwa affordable na wananchi wa level ipi na kwa kiwango gani. Kwa hiyo, pamoja na kwamba tunaona tunaanzisha shirika, lakini lazima kuwepo na urahisi wa upatikanaji wa mawasiliano kwa wananchi kule vijijini kuhakikisha mawasiliano yanapatikana kwa wakati na yanaweza kuwa affordable kwa kila mwananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nitoe mapendekezo katika Muswada kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha saba (7) kimeelezea Board of Directors; napendekeza pale kwenye uwakilishi wa members wa Board of Directors wameleta mapendekezo kwamba upande wa Zanzibar awepo mwakilishi mmoja kati ya five members watakaokuwa kwenye bodi. Kama kweli tunaitambua Zanzibar kama sehemu ya nchi hii, kuwapa nafasi moja sio kuwatendea haki, nafikiri kuwatendea haki ni kuwaongezea nafasi, mbili zitoke Zanzibar na nafasi tatu zitoke Tanzania Bara. Kwa hiyo, napendekeza pale katika kifungu cha saba (7) waweze kuongeza idadi ya wajumbe kutoka Zanzibar kwenye hiyo Board of Directors; wawe wawili badala ya mmoja kama ambavyo wameweza kuandika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vivyo hivyo, katika ibara hiyohiyo ya 7(7), wamesema pale napenda kuongeza maneno kwamba The Minister in consultation with the Board anaweza ku-publish mambo yote ambayo yanaweza kufanyiwa marekebisho. Tusimwachie tu Waziri mwenyewe abebe hili jukumu, lakini Waziri afanye mawasiliano na bodi yake. Sasa kutakuwa hakuna maana ya kuwa na bodi kama Waziri anaweza tu akawa anaamua kila kitu. Kwa hiyo,ni vizuri Waziri anapofanya mambo yoyote yale, ni lazima afanye consultaion na bodi yake aliyounda ili kuwepo na ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika ibara ya tisa (9), wanapendekeza kwamba Waziri anaweza kuzi-direct bodies; ni sawa, anaweza kutoa maelekezo, lakini sheria inasema maelekezo yote yatakayotolewa na Waziri ni lazima bodi ifuate na itimize. Nadhani tusiweke kipengele hiki cha kuilazimisha bodi; Waziri ni mtu, ni binadamu, leo anaweza akatoa maelekezo akiwa kwenye hali ya hasira au ana frustration au anatoa maelekezo ambayo mwisho wa siku hayawezi kuleta ufanisi wa shirika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri tuache kipengele kiseme kwamba kama Waziri atatoa mapendekezo kwa bodi, basi iwe ni bodi kuamua kuyafuata, kusiwepo na ulazima wa kisheria au uhitaji wa kisheria kwamba lazima yale ambayo yatatolewa na Waziri yaweze kufuatwa. Kwa hiyo, napendekeza kwamba kifungu cha tisa (9) kuondoa maneno ya mwisho pale baada ya neno act kwamba and the Board shall give effect to any direction given to it. Kwa hiyo, ibaki tu maneno ambayo yatasomeka hapo haya mengine yaondoke.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema haya kwa sababu nimepeleka schedule of amendment, naambiwa nimechelewa muda hautoshi wakati kuna mambo mengine ambayo tunaweza kuyapendekeza kwa ajili ya Muswada huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, natoa pia mapendekezo katika kifungu cha 15; uzoefu katika appointments hizi za Director wa shirika, kama ilivyosema hotuba ya Kambi ya Upinzani, unaposema miaka nane ni mingi sana,
napendekeza iwe experience ya miaka mitano. Tunaangalia experience, ndiyo ni jambo moja, lakini kuna uadilifu, kuna mambo mengine mengi sana ya kuweza kuona mtu gani anafaa katika nafasi fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza kusema awe na experience ya miaka nane wakati mtu mwenyewe ni mbovu, hana uadilifu wowote ana upungufu mwingi. Kwa hiyo, tusiweke kwamba ni lazima awe na experience ya miaka nane, napendekeza kuwe na experience ya miaka mitano kwa huyo ambaye atateuliwa kuwa Director wa shirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie mchango wangu kwa kuendelea kuisisitizia Serikali kwamba, hatuwezi tu kusema tunabadilisha sheria kila kukicha, leo tunabadilisha sheria hii kutoka Kampuni ya TTCL kwenda Shirika la TTCL halafu bado tunakuja na sheria nyingine nyingi ikiwemo hizo ambazo tumeshapitisha kwenye Bunge hili ya kuzuia mawasiliano, kudhibiti mawasiliano ya watu, kuzuia watu kutoa maoni yao na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Serikali ni vizuri ikawa consistency na mambo inayoyafanya katika utungaji wa sheria. Kama tunatunga sheria hiyo tukilenga kumaanisha wananchi wote waweze kupata mawasiliano kwa kadri inavyowezekana, basi tusije na sheria nyingine ambazo zinaweza kuwa zinanyima uhuru wa watu kupata mawasiliano au kutumia mawasiliano kwa kadri ambavyo yataweza kupatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.