Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Zaynab Matitu Vulu (22 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema. Kwa sababu hii ni mara yangu ya kwanza kwa ruksa yako, niwashukuru wapiga kura wote wa Mkoa wa Pwani wakiongozwa na wanawake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Mheshimiwa Rais wewe endelea na kuchapa kazi kama kaulimbiu yako ulioitoa ya “Hapa Kazi Tu” haya maneno ya humu ndani ni sawa na wimbi la baharini, Waswahili sisi kule baharini tunasema wimbi la nyuma halimsumbui wala halimkeri mvuvi, kwa hiyo ya nyuma yamepita sisi tusonge mbele, tuchape kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nijikite kwenye mpango ambao tunao mbele yetu. Mpango huu unauzungumzia ujenzi wa uchumi. Nianze kwa kuipongeza Serikali kuwa na uamuzi wa kufanya elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na chekechea yake lakini nitoe msisitizo tunaposema elimu bure tusaidie kutengeneza mazingira bora. Kwenye Mpango haikugusa maeneo ambayo yatamfanya Mwalimu, yatamsaidia Mwalimu kuweza kufanya kazi zake kwa amani zaidi ya hivi sasa anavyofanya. Majengo, Nyumba za Walimu, miundombinu na mambo mengine yale muhimu kwa ajili ya kuendeleza elimu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ndiyo itakayotusaidia kuinua uchumi wetu na hasa huo uchumi wa viwanda tunaouzungumzia. Kuna masomo ya sanaa na masomo ya sayansi, tunapozungumzia masomo ya sayansi ndipo tutakapopata wataalam wa viwanda, sasa hivi tujikite katika kujenga vyuo vya VETA, kupeleka wanafunzi wengi, ili waweze kuajiriwa maeneo mbalimbali katika viwanda vyetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ni vipi Mpango umemuangalia mwanamke katika kuinua uchumi wa viwanda, ni vipi mwanamke atashirikishwa, ni vipi umeme utaweza kusaidia kwenda kijijini ili mwanamke au gesi itakavyoweza kusaidia inayotoka Mtwara ifike mpaka kijijini ili mwanamke yule apungukiwe na mzigo wa kutafuta kuni, apungukiwe na mzigo wa kuhangaika na mambo mengine, aweze kwenda kushiriki katika kazi za kuinua uchumi katika, katika kuajiriwa kwenye viwanda, hata kuweza kuwa na viwanda vyao wenyewe wanawake kama Serikali ilivyotuwezesha kuwa na Benki yetu ya Wanawake kuwa na Benki ya Kilimo. Hayo ndiyo mambo ninayoomba mimi, huu Mpango uangalie na uende ukarekebishe tuone hayo yatafanywaje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapotaka kumkomboa mwanamke aweze kushiriki katika ujenzi wa uchumi, tuangalie na mazingira ya mtoto wa kike toka anasoma chekechea. Watu wamegusia suala la maji humu ndani, maji ni msingi unaoweza kuleta maendeleo katika nyanja zote, lakini maji hayo kama hayatofika kila mahali na kwa wakati, kuna udumazi wa maendeleo utakaotokea na kuwanyima wengine haki ya kuweza kwenda kujiendeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa maana kwamba tunahitaji uvunaji wa maji mashuleni, uwezo wa kuchimba visima kama water table iko chini sana basi itengenezwe miundombinu ya kuvuna maji ya mvua. Mahitaji ya maji ya mtoto wa kike au ya mwanamke ni makubwa zaidi ya wanaume, tunahitaji watoto wa kike wawekewe utaratibu, wanapewa pesa za kuwasaidia lakini wawekewe na utaratibu wa kupewa mataulo ya kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa wa Jimbo la Ludewa Mjini aliyeguswa na maendeleo na mahitaji makubwa ya mtoto wa kike. Nakushukuru sana na nakupongeza, wanawake wote tunasema tuko pamoja na wewe na tumekutaja leo kwenye vikao vyetu tutakushirikisha ili uone tutasaidiaje watoto wa kike katika kuleta maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kutoa misaada. Mtoto wa kike anaweza asiende siku saba shule, yuko nyumbani, mama anahitaji maji zaidi ya baba, anahitaji ndoo tatu, nne kwa siku. Leo hii kama mama hapati maji ya kutosha hawezi kwenda kushiriki kwenye uchumi, kwa hiyo suala la maji ni suala la kuwekea msisitizo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuja kwenye suala la gesi. Naipongeza Serikali kwa juhudi iliyofanya, gesi inatoka Mtwara imefika Dar es Salaam mpango haukueleza, katika Mkoa wetu wa Pwani inapoanzia Rufiji watu watanufaika vipi! Tunahitaji gesi ile ipate manufaa Wilaya ya Rufiji, Wilaya ya Mkuranga, Wilaya ya Kisarawe, Wilaya za Kibaha, Bagamoyo, ambako pia nako kuna uwezekano pamoja na Mkuranga kupata gesi tuone tutafaidika vipi, viwanda vingapi tumeandaliwa kuletewa, gesi imekuja, tunawaambia watu wasikate mkaa, watu wamezoea kukata mkaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam yote inalishwa mkaa unaotoka Pwani, sasa Mpango huu unaelezaje, gesi hii imeandaliwa vipi na Serikali ili wale wakataji wa mkaa waweze kunufaika na biashara yao wakaacha, misitu yetu ikarudi pale pale. Sasa hivi misitu imekuwa kama vipara, eeh unakwenda unakuta pembeni kuna miti lakini ukienda katikati miti hakuna. Mama anahangaika kutafuta kuni asubuhi mpaka jioni. Watani zangu kule Usukumani miti yote imekwisha matokeo yake wanatumia mavi ya ng‟ombe. Kwa hiyo, niwaombe, ufanywe utaratibu Serikali ihakikishe gesi na umeme inafika kwa watu wote ili kuleta maendeleo ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wangu mniwie radhi nasema ukweli wa maisha. Niseme kwamba suala la maendeleo katika Wilaya ya Mkoa wa Pwani, naomba tuliangalie sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Rufiji. Rufiji watu wameanza ujasiriamali, wanachonga vitanda lakini ushuru wa kitanda ni laki moja na ishirini. Huyo muuzaji atanunua hicho kitanda kiasi gani? Ushuru wa mkaa umepanda asilimia moja na kumi na nne, huyo mwananchi anayekata miti na mbao anafanya biashara ya kujisaidia ataendelea vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Nyamwage mpaka Utete na Utete ndiyo kuna hospitali ya Wilaya, tunatarajia watu watolewe Utete wapelekwe kwenye hospitali ya Wilaya Kibaha, barabara mbaya, Wilaya ile ni miongoni mwa Wilaya kongwe katika nchi hii, mpaka leo hii hatujaiona lami. Tunaomba suala hilo liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika twende Mafia. Kuna barabara inaanza Kilindoni hadi Bweni haina lami, lakini pia Mafia kuna utalii, naomba Serikali kupitia Wizara ya Utalii, hebu ijaribu kuangalia ni vipi watainua wilaya ile na kuifanya wilaya ya kiutalii. Watalii wengi sana wanakwenda, tunashukuru, gati limejengwa tunangoja tishari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuu uwanja wa ndege umejengwa tunasubiri taa ziwekwe, watalii waingie asubuhi na jioni hali kadhalika na wananchi waingie asubuhi na jioni. Hata hivyo, bado tuna tatizo la hospitali zetu, Wilaya zetu za Mkoa wa Pwani, zimepakana na Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwenye vituo vya afya na zahanati na hospitali za Wilaya...
MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge muda wako umekwisha!
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MH. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma aliyenijalia kusimama hapa na nichukue pia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa kwetu, pia wala sitaki kusema neno baya kwa upande wa pili niwapongeze kwa sababu wametupa nafasi na sisi tuweze kuongea, wananchi wajue Serikali yao chini ya Chama cha Mapinduzi imefanya nini na itaendelea kufanya nini. Niseme kwa niaba yenu, niwaambie wale ahsanteni sana, acheni tujimwage kwa raha zetu ndani ya Ukumbi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuzungumzia suala la afya. Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake ameligusia vizuri sana suala la afya, ukiangalia bila afya bora hakuna ambaye anaweza akafanya kitu chochote, hata humu ndani kama afya zetu zisingekuwa bora tusingeweza kuja humu ndani, hivyo ninampongeza sana kwa kuliona hilo na kwa kulizungumzia lakini naiomba Serikali tusaidiane, tumeambiwa tuhamasishe suala la mfuko wa afya CHF wananchi wamepokea wito kwa nguvu zao zote, tatizo linakuja kwenye utoaji wa dawa. Wanafika kwenye dirisha hawapati dawa, sasa ni wakati muafaka, MSD (Medical Store Department) iwezeshwe vya kutosha, nimpongeze Waziri wa Afya na Naibu wake, kwa kazi nzuri wanayoifanya lakini MSD isimamie suala la upelekaji dawa ili watu wapate dawa afya zao ziweze kuimarika na waweze kufanya kazi vizuri. Mtu hawezi kwenda shambani kama afya yake siyo nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kilimo. Kilimo ndiyo uti wa mgongo. Bila pembejeo, bila mbegu nzuri hakuna kilimo kitakachoweza kuwa kizuri. Ufunguaji wa milango ya biashara, ukimwezesha Mkulima kuna uhakika wa kutosha, akipata pembejeo, akipata mbegu bora, atalima yeye na atalima kwa ajili ya kuuza nje hata ndani ya nchi, hilo naomba tuliangalie na tulipe kipaumbele chake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka Mkoa wa Pwani. Mkoa wa Pwani tuna mabonde na mito mingi sana, tuna Mto Ruaha, tuna Mto Wami, tuna Mto Rufiji, tuna Mto Ruvu, tuna mambonde mengi sana, tunaomba kilimo cha umwagiliaji kiwekewe mkazo katika mabonde hayo ili wananchi waweze kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wakiwezeshwa, wakipewa teknolojia ya umwagiliaji hatutaweza kuwaona tena wanakwenda kucheza pool, tuwawezeshe vijana walime zao ambalo ni jepesi kulima kwenye mabonde, zao la mpunga, zao la nyanya, zao la vitunguu, zao la bamia, mbogamboga hata mahindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo, naiomba Serikali iweke utaratibu mzuri katika kilimo, pia kutumia maji katika mito yetu na kuweza kufanya zoezi la umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, maji ya mito niliyoitaja mitatu, naiomba Serikali ifikie wakati sasa ule mradi wa Kisemvule uanze kazi mara moja. Mradi ule uko Wilaya ya Mkuranga lakini utakapowezeshwa utawanufaisha hata watu wa Dar es Salaam kama mradi wenyewe unavyosema. Lakini mpaka sasa hivi katika maeneo ya Wilaya ya Kisarawe, Wilaya ya Mkuranga, hata Wilaya ya Kibaha Vijijini na Mjini bado tuna matatizo ya maji, naomba sana Serikali ione umuhimu wa kuwezesha upatinaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha mradi huo wa Kisemvule tuone Serikali imechukua hatua zipi sasa za kuweza kuuwezesha mto Rufiji ufike kwenye maeneo jirani, ufike kwenye Wilaya Mkuranga, ufike Wilaya ya Kisarawe hata Dar es Salaam, maji ya Rufiji yanaweza yakasaidia badala ya kuyaacha maji yale yanakwenda yanaingia baharini hatuoni faida kwa watu wengine. Naiomba Serikali iangalie uwezekano wa kutusaidia katika upatikanaji wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nimpongee Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kauli mbiu yake aliyoitoa ya kwamba Tanzania sasa iwe nchi ya uchumi na viwanda. Kweli huu ndiyo wakati muafaka umefika, Serikali ina wajibu wa kufanya hilo na sisi tunaunga mkono. Kwa kuanzia katika Mkoa wetu wa Pwani pamoja na maeneo mengine viwanda vipo lakini Wilaya ya Mkuranga tayari inaongoza kwa kuwa na viwanda vingi, ninaiomba Serikali iangalie umuhimu wa kuwasaidia Watanzania kwanza, tuweke mikataba ambayo itakuwa endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iwaangalie Watanzania wenye elimu ya kutosha, waweze kupata nafasi kusimamia shughuli za viwanda isiwe vijana wa ajira ndogo ndogo ndiyo waajiriwe katika viwanda vile. Kweli tunasema viwanda ni mkombozi, nimuombe kaka yangu na ndugu Mheshimiwa Mwijage ahakikishe kwamba wale Wawekezaji nazungumzia kwa upande wa Mkuranga sasa hivi ambapo ndiyo tunapokea malalamiko, wanalipwa shilingi 5000 kwa siku, anaingia saa mbili asubuhi, anatoka saa 2 usiku, shilingi 5,000 ukipiga hesabu elfu tano kwa mwezi ni shilingi 150,000, hapa tumemsaidia au tunatumia nguvu zake tu kuwasaidia wale wenye viwanda?
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaiomba sana Serikali iangalie hasa Wizara husika ya ajira ipite kwenye viwanda, ikibidi hata tufuatane naye Waziri husika akaangalie ili aweze kuona hata usalama wa wale wafanyakazi, tunachohitaji viwanda kwa ajili ya ajira, lakini pia vitakavyozalishwa vije kwa Watanzania waweze kununua na pato la nchi liongezeke, lakini tuangalie na maslahi ya Watanzania watakaouwa wameajiriwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la mikopo. Suala la mikopo kwa wakulima limeoneka vizuri, lakini naomba kujua je, wavuvi wao wamefikiriwaje? Watajiendelezaje katika uvuvi mdogo mdogo? Tunao wavuvi wa baharini, tuna wavuvi wa kwenye maziwa, pia kuna wavuvi wengine wapo kwenye mito yetu ambayo inatuzunguka katika nchi yetu ya Tanzania.
Ninaiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwawezesha wavuvi na kuangalia zile sheria, sheria zinamlindaje mvuvi mdogomdogo pamoja na hata yule mvuvi mkubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kuipongeza Serikali yangu ya Awamu ya Tano kwa kuleta mkopo kuwawezesha wananchi milioni 50 kila kijiji, milioni 50 kila mtaa, ni wazo jema, tulipangie utaratibu mzuri, tuwawezeshe wanawake, tuwawezeshe vijana wetu bila kuwasahau wananume, wako ambao na wao wanahitaji kusaidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba nichukue nafsi hii kusema kwamba naunga mkono hoja ya Waziri Mkuu na tuko tayari Watanzania kufanya kazi kwa kuijenga nchi yetu na kukijenga Chama chetu ahsante sana.(
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha siku ya leo kujadili hotuba ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nampongeza Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuunga mkono hoja, naomba nipate maelezo ya kina juu ya juhudi za Serikali kuhusiana na zao la nazi maana ni zaidi ya miaka 10 sasa zao hili limekuwa linapotea kwa kushambuliwa na wadudu mwishowe hufa. Mimi natoka Mkoa wa Pwani ambako sehemu kubwa tunalima zao hili na ndilo linaendesha maisha ya Wanapwani. Zao hilo halihitaji mvua na wala halina matatizo kipindi cha jua. Zao hili huvunwa mara nne kwa mwaka. Kwa taarifa tu, maeneo mengi kwa sasa watu wananunua nazi zinazotoka Mombasa. Kwenye mnazi tunapata samani, mafuta ya kula, kujengea nyumba na maji (madafu) ni kiburudisho na pia hutumika kama tiba mbadala inapobidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na kituo cha utafiti wa zao la nazi pale Mikocheni. Kwa masikitiko sijaona juhudi zozote za kusaidia tiba ya mdudu huyu mharibifu. Pia naomba Serikali iwe na mpango wa kuwasaidia waathirika wa minazi hiyo ama kwa kuwapa zao mbadala au miche mipya ya minazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina hakika Mheshimiwa Waziri na Naibu wake mtalipa Kipaumbele ombi langu na kunipatia majibu stahiki, kwani nimekuwa nauliza jambo hili katika kila bajeti sijapata jibu. Pia naomba mfikirie kuanzisha bodi ya zao hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie suala la wavuvi hasa wadogo wadogo ambao wanatozwa leseni ambao kipato chao ni kidogo. Naomba Serikali ijiwekeze kwenye viwanda vya samaki ili kuwasaidia wavuvi wadogo wadogo ambao wanauza samaki kwa wenye viwanda. Wavuvi hawa hupata hasara maana wenye viwanda hushusha bei kila baada ya masaa na mvuvi anapoingia baharini au ziwani hana uhakika wa wingi wa samaki na hao anaowapata huuza kwa bei ndogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria za wavuvi wadogo na wakubwa ni vyema zikaagaliwa tena hasa ile ya uvaaji wa vifaa vya kuokolea kwenye kina kirefu cha maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, uchomaji wa nyavu za wavuvi nao uangaliwe upya. Ni vema kuzuia uingizaji wa nyavu hizo ili wasiweze kuzipata. Naomba msimamo wa Serikali juu ya suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake wa hotuba ya bajeti. Viwanda vidogovidogo vilivyokuwepo kwa tathmini ya mwaka 2012 imeonesha kulitolewa ajira milioni 5.2 na kuchangia Pato la Taifa (GDP) ambapo ajira hizo zilisaidia kuwezesha familia kujiendesha na kupunguza uzururaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema kwamba, kiasi cha shilingi bilioni 81, kilichoombwa kwa mwaka 2016/2017 kinashabihiana na kasi ya Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli cha kutaka kujenga Tanzania ya viwanda kwa sababu asilimia 49.3 ya pesa zote zinaenda kwenye shughuli za maendeleo na asilimia 50.7 iende kwenye matumizi ya kawaida. Ili tuwe na viwanda ambavyo vitazalisha kwa uhakika, suala la miundombinu ya umeme, barabara na reli iwe imeimarika zaidi tuweze kusonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuwepo leo na kuchangia hotuba ya Wizara yako.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mheshimiwa Profesa Jumanne Maghembe, Naibu Waziri Mheshimiwa Ramo Makani na watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu kubwa na ombi langu kwa Wizara hii ni kwamba naomba Wizara inipe majibu ni lini itaweka utaratibu wa kuzuia wananchi ambao hupata kipato chao kupitia uvuvi kwenye bwawa/mabwawa yaliyopo Selous, lakini Serikali imezuia na hata kufikia kuwaua. Hili ni tatizo naomba ufafanuzi.
Pia Mkoa wa Pwani kumezungukwa na misitu hivyo kwa wale ambao wanafanya biashara ya mbao (kutengeneza samani) hutozwa ushuru mkubwa wa shilingi 120,000 hata kama kitanda au samani ishatumika zaidi ya miaka 20. Naomba kauli ya Serikali lini itapunguza ushuru huo wa samani na mkaa? Naomba majibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, misitu iliyopo Mkoa wa Pwani mingi imebaki vichaka kwa kuwa hakuna usimamizi mzuri na kupelekea ukataji hovyo wa miti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Mkuranga eneo la Mwandege kuna msitu ambao kwa neno msitu kwa sasa si sahihi kwani ni kichaka na kuficha wahalifu wengi, naiomba Serikali itoe maelekezo au kubadili matumizi ya eneo hilo ili kupendezesha eneo hilo, laa kama hiyo haiwezekani basi uwepo upandaji upya wa miti na ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba maelezo ya Serikali na naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote nami nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyenzi Mungu, mwingi wa rehema, ametujalia na leo tumeiona siku yetu ya Ijumaa, basi azidi kutupa heri na baraka na atuongoze kwa kila jambo lilokuwa na heri na sisi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbele yetu kuna hoja inayohusu viwanda. Viwanda tunavyovizungumzia tunataka vituletee mabadiliko ambayo tayari Watanzania tulianza kuwanayo katika miaka ya nyuma. Kwenye miaka ya 1970 tulikuwa na viwanda vingi kwenye maeneo mbalimbali. Msimamizi mkuu katika shughuli hizo za viwanda ilikuwa ni NDC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapozungumzia uchumi wa viwanda, nasi Watanzania tuko tayari, tumesema tutaupokea uchumi wa viwanda. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri aliyotuwasilishia; ameyataja maeneo mbalimbali ya Tanzania kwamba tutapata viwanda ikiwemo Mkoa wa Pwani ninakotoka mimi. Ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kwanza atufufulie viwanda ambavyo vilikuwepo na vimekufa. Viliuzwa kwa watu, iweje mpaka leo hakuna kitu chochote ambacho kimeendelezwa au kimefanyika katika viwanda hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika hotuba yake ameelezea kwamba kutakuwa na utaratibu wa viwanda ambapo wenye viwanda watashirikiana na wananchi waliokuwepo katika maeneo yale kwa maana ya kuwa wakulima watakaotumia maeneo yale kwa kilimo na vile viwanda vitatumia mazao yale kuzalisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai au ushauri kwake, sasa hivi tumeona kuna viwanda vingi nchini, ikiwemo Mkuranga na Bagamoyo, lakini kwa nini jambo hili la kuchukua wakulima wadogo wadogo wanaozalisha mazao yao wasianze sasa hivi tukaona mfano? Hata sisi Wabunge tutakapokuwa tunazungumzia suala la kuhimiza na kushawishi watu kuja kutengeneza viwanda kwa maeneo yetu, tuwe na mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano Arusha kuna maeneo wanazalisha maua, lakini pia kuna wakulima wadogo wadogo ambao wanazalisha yale maua, yanauzwa kwenye viwanda, wao wanasaidia zile mbegu na dawa za kuzuia uharibifu wa mazao kwa maana ya maua. Kwa hiyo, naomba na huku kwetu uwezekano wa wakulima wadogo wadogo waweze kununuliwa mazao yao kwa sababu Mkoa wa Pwani, mfano, tuna machungwa mengi, maembe mengi, na matunda ya aina mbalimbali. (Makofi)
Mhshimiwa Mwenyekiti, ukitaka kuthibitisha hilo, msimu wa matunda pita katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani uone mazao yanavyoharibika kwa sababu hakuna pa kuyapeleka. Mkulima hasa mwanamke; asilimia 80 ya wanawake ni wakulima wadogo wadogo. Naomba basi uwezekano Serikali kufikiria ni vipi watakwenda kununua mazao hayo kwa wakulima kuwawezesha na wao wainue kipato chao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunapozungumzia viwanda, nilizungunguzia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Kwenye viwanda vyetu vilivyokuwepo sasa hivi nchini, vijana wetu wanatumika vibaya sana. Wao wanaajiriwa kwa mshahara mdogo sana, wakati sisi tunatarajia waajiriwe wapate fedha zitakazowaendesha katika maisha yao, lakini kinyume chake wanapewa mshahara wa shilingi 150,000 kwa mwezi. Shilingi 150,000 kwa mwezi anaifanyia nini kijana yule, mama yule, dada yule, kaka yule? Naomba kama tunakwenda kwenye mtindo wa kuwa na viwanda vingi, basi hata mshahara uwekwe kabisa, aambiwe mwekezaji kwamba mshahara wa kima cha chini isiwe shilingi 5,000 kwa siku.
Mhehimiwa Mwenyekiti, naomba sana, kama kutakuwa na uwezekano kwa Serikali yetu ichukue hata vile viwanda ambavyo vilikufa, vikawezeshwa na wakachukuliwa akina mama wakapewa kiwanda kile waendeshe wao. Wako ma-engineer, wako wataalam wa aina mbalimbali, iwe mfano wa kiwanda kile tuone uzalishaji utakotoka pale. Akina mama ni wachapakazi! Sisemi kama wanaume hawafanyi kazi, lakini nasema uchumi wa viwanda umkomboe na mwanamke katika viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema viwanda, tuangalie na mazao tunayoyalima katika maeneo yetu. Mkoa wa Pwani tunalima nyanya nyingi sana, lakini mwisho wa siku tunanunua nyanya za kopo, zinazotoka nje ya nchi, haipendezi! Tuwe na viwanda vyetu, tuwe na nyanya tunazotengeneza wenyewe, tuwe na matunda ya aina mbalimbali ambayo akina mama wanaweza wakatengeneza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimalizie na hotuba ya Wapinzani kwenye ukurasa kama sikukosea ni wa 16, waligusia ahadi ya Mheshimiwa Rais, kwamba aliahidi atajenga kiwanda cha Korosho, Mkuranga na Rufiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie neno moja tu, Waswahili wana msemo wao wanasema hivi, tena hata waimbaji waliimba, “mtoto acha kupiga mayowe, waache watu waje waone wenyewe.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi toka imetolewa hata miezi sita haijakamilika. Subirini muone kazi itakavyokwenda. Nawaomba himizeni wapiga kura wenu, wananchi wetu, wasimamie uzalishaji wa korosho, wasimamie uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali ili tuweze kuhakikisha viwanda vyetu vitakuwa na malighafi, inayotoka ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, nasema ahsante sana. Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na tunamuunga mkono Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli, kwa ajenda yake ya uchumi wa viwanda. Watanzania na hasa akina mama, tumesimama imara, tutaifanya kazi katika viwanda vitakavyoletwa. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake na kuendelea kutupatia amani kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali yangu kwa juhudi zake katika kuboresha miundombinu, huduma muhimu kwa wananchi wake, vyote hivyo vikiwa chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu na Waziri Mkuu Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa. Kutokana na juhudi zote hizo tunaona jinsi gani Pato la Taifa lilipo ambapo ni asilimia saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Mkoa wa Pwani, tunashukuru kwa mkoa wetu ambao tumebahatika kuwa na viwanda ambavyo tayari vinazalisha na vingine viko kwenye hatua za ujenzi au taratibu za kuanzishwa. Pamoja na manufaa hayo kwa mkoa wetu kuna mambo
muhimu ambayo tunapaswa yapewe vipaumbele ili viwanda hivyo viweze kuwa na uzalishaji ambao hautakuwa na vikwazo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Pwani tuna tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali pamoja na neema tuliyopewa ya kuwa na mito mingi tena mikubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya barabara zetu sio nzuri, Wilaya ya Kisarawe imetenga eneo mahususi kwa ajili ya viwanda, lakini tatizo ni barabara. Hivyo basi naiomba Serikali inipe majibu ni vipi tutatokana na matatizo hayo ili kuweza kuvutia wawekezaji ambao wako tayari kuja
kuwekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua ni kwa kiasi gani Serikali imejipanga kwa kuhakikisha ajira za vijana hasa kwenye viwanda vinazalisha na vinatarajiwa kuwa kuna baadhi wanatoa ajira lakini mshahara ni mdogo sana (shilingi 5,000) kwa siku. Hii nilishawahi kuuliza hapa Bungeni kwenye kipindi cha maswali na majibu. Mipango mizuri ndio faida ya Watanzania ambapo ni Serikali yetu inavyofanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa gesi utasaidia sana kupunguza gharama za uzalishaji viwandani, lakini pia utaratibu wa kupeleka umeme huo majumbani uongezewe speed.
Mheshimwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na pongezi kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama na Naibu wake Mheshimiwa Antony Mavunde.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuwa miongoni mwa wanaochangia hoja hii kwa bajeti hii ya 2017/ 2018. Naanza kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa jinsi inavyotenga fedha na kuendeleza miundombinu mbalimbali ya barabara, madaraja na mawasiliano. Pia pongezi kwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Mbarawa kwa umakini na ufuatiliaji wa karibu sana katika miradi yote na bila ya kuchoka, yeye na wasaidizi wake hatimaye kuona kila lililopangwa linakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa Mbunge toka Mkoa wa Pwani na kuona jinsi ambavyo nachangia kuomba kujengewa barabara za lami katika wilaya zilizozopo Mkoa wa Pwani, ikiwemo barabara ya Kisarawe – Vikumburu – Mlandizi – Maneromango. Hii imekuwa adha kubwa sana kwa wananchi wa huko hasa nyakati za mvua. Awamu zote katika ilani yetu imekuwa ikiahidi lakini hadi leo haijafika kokote. Naomba sana, barabara hii ipatiwe fungu la kutosha na kuweza kujenga. Je, ni lini ujenzi huo utaanza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, pia naomba ahadi za Marais wetu zitimizwe, kwani barabara ya Nyamwage – Utete - Mkuranga – Kisiju – Bungu – Nyamisati, hizi barabara ni muhimu sana kwa wananchi wa maeneo hayo na hata kwa wasafiri wengine na kukuza biashara na kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa ujenzi wa reli (standard gauge) ambayo Mkoa wa Pwani tutasaidiwa kwa maana mbili; ajira, usafiri na uuzaji wa vyakula na hiyo itainua kipato cha wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mkiwa maeneo hayo ya ujenzi, kipaumbele cha ajira kianze kwa wananchi walioko jirani na ujenzi wa hiyo reli.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutoa kipaumbele kwa Wizara ya Afya. Hivyo basi, pongezi pia ziende kwa Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile pongezi nyingi kwa Waziri husika Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Dkt. Hamis Kigwangalla na Watendaji wote, kwa kusimamia vyema Wizara hii na matunda tunayaona, pamoja na ufinyu wa bajeti. Waswahili husema, ng’ombe haelemewi na nunduye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ipandishe hadhi baadhi ya Vituo vya Afya vilivyopo Mkoa wa Pwani. Hii ni kutokana na umuhimu wa kuongeza/kupanua huduma kwa jamii. Vituo hivyo ni Kibiti, Muhoro (Rufiji), Mlandizi (Kibaha Vijijini), Ubena (Chalinze), Mzenga (Kisarawe) na Kibaha Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuwa kutaimarisha huduma hizo, pia vituo hivi viko barabara kuu za mkoa ambapo usafiri wa aina mbalimbali hupita hivyo, endapo kukitokea ajali kunakuwa hakuna uwezo wa kutoa huduma na hivyo kulazimika kusafiri kwenye Hospitali za Wilaya au kupelekwa Hospitali za Mkoa jirani, Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chonde chonde, pamoja na matatizo ya kiufundi (kama yapo) tusaidiwe X-Ray ya Mafia ipate ufumbuzi wa kufungiwa, ukizingatia Mafia ni kisiwa na hawana pa kukimbilia endapo imetokea dharura. Nimalizie kwa kuomba suala la maji kwa zahanati na vituo vya afya. Ni muhimu, kuwe na elimu ya uvunaji maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami jioni hii ya leo niweze kutoa mchango wangu katika hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili wana msemo wao, wanasema hivi, “ng’ombe hashindwi na nunduye.” Nina hakika pamoja na uchache wa pesa ambazo zimetolewa, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli haitashindwa kutekeleza miradi ya maji ambayo tunaitarajia katika maeneo yetu. Nawatoa hofu wenzangu, hilo walijue kwamba hakuna nundu yoyote ambayo ng’ombe imemshinda akasema mimi leo, siwezi kutembea, nundu hii imezidi ukubwa, nakaa chini. Hata siku moja! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumzia suala la maji, lazima tutazungumzia suala la fedha; na tunapozungumzia suala la fedha, maana yake tunataka miradi hii ifike kwa walengwa na kwa wakati. Tumeona baadhi ya maeneo yamepata maji.

Mhshimiwa Naibu Spika, nimesoma kitabu cha hotuba, mimi natoka Mkoa wa Pwani; Mwenyezi Mungu ametupa neema, tuna Mto Rufiji, tuna Mto Ruvu, tuna Mto Wami, lakini pamoja na uzuri wa wananchi wale kulinda vyanzo vya maji katika mito ile, kwenye kitabu hiki yametajwa mabomba yaliyowekwa kutoka Ruvu, mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu chini kwenda Dar es Salaam na baadhi ya maeneo kwa Wilaya ya Kibaha, Bagamoyo na Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka kumtua ndoo mwanamke kichwani. Wanawake wa Pwani ndoo wao kwao siyo shida, maji siyo shida, lakini wao wanachotaka miundombinu ya maji kutoka kwenye mito iweze kufika kwenye maeneo yao. Unakuwa na mti wa matunda unatarajia mti ule ukupe kivuli na ule yale matunda, lakini kule baadhi ya maeneo wanatunza maji, wanajitahidi, lakini maji yale yakiwekwa mabomba moja kwa moja yanakwenda Dar es Salaam. Siwaonei wivu ila nasi tunahitaji hayo maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, imetenga fedha, lakini bado fedha zile hazitoshelezi. Kwa mfano, Shule za Sekondari za Rufiji, wako karibu na Mto Rufiji, lakini shule zile kama Utete, Ngorongo, Kibiti na maeneo mengine hawana maji. Kuna visima vimechimbwa lakini tunaomba yawekwe mabomba ambayo yatafika kwenye shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama imeshindikana, kuna DAWASA na DAWASCO waweke miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ya kuweka matenki. Maji yale siyo kwa watoto wa kike tu na akinamama wanaoyahitaji, hata watoto wa kiume wanahitaji maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado katika vyanzo hivyo hivyo vya maji, kuna wakulima wadogo na wakubwa. Naomba Wizara husika na Taasisi husika ziangalie utaratibu gani utatumika kuzuia zile dawa ambazo zinatumika kwenye kilimo zisiende zikaharibu afya katika yale maji, kwa sababu baadhi ya watu hawana mabomba, wanakunywa maji yale yale ambayo kwa sasa hivi kwa mfano mvua zimekuwa nyingi, yametiririka maeneo mengi, dawa nyingine ni sumu. Matokeo yake watu wanakunywa maji, maradhi ya aina mbalimbali yanapatikana. Mwishowe tunajiuliza, kunani? Mbona magonjwa yamekuwa mengi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba uwekwe utaratibu, wakulima wadogo wadogo wapate elimu, wapewe namna ya kuweza kuhifadhi vyanzo vyao vya maji ili zile dawa wanazomwagilia kwenye mazao zisiweze kuharibu yale maji wanayoyatumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali kadhalika, katika huo Mradi wa Ruvu Juu ambao umeanzia Mlandizi; mto umeanzia Morogoro umekwenda Dar es Salaam; watu wanaokaa maeneo ya Kisarawe, kuna eneo la Kimaramisale, Kigogo, Mzenga na Kurui. Hao wote hawana maji safi na salama yanayotoka kwenye mabomba ambapo wao ndiyo wanatunza vile vyanzo vya maji vya Mto Ruvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali, pamoja na kutenga hizo fedha, lakini bado kuna utaratibu wa kufuatwa, tunaomba tusaidiane, tushirikiane nao, inapobidi hata kutoa elimu wananchi wa Kisarawe tutakuwa tayari hata kujitolea katika uchimbaji wa mitaro, watuletee mabomba tu. Sisi shida yetu ni mabomba na dawa za kuhakikisha maji yale hayataharibu afya za watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona mvua hizi jinsi gani maji mengi yamepotea yamekwenda baharini na jinsi gani maji yameharibu kilimo chetu, lakini bado kungeweza kukafanywa utaratibu wa kuvuna maji ya mvua, elimu ikatolewa majumbani. Siyo mara ya kwanza nasema neno hili. Elimu ikatolewa mashuleni, pesa zikatengwa na Halmashauri zetu na Serikali Kuu ili kuhakikisha maji ya mvua yanavunwa, wananchi wanatumia maji ya mvua kwa wakati fulani, yakiisha wanajua sasa maji yamekwisha. Tunaachia maji yanakwenda bila kuwa na utaratibu wa kuyavuna. Kwa kweli hilo ni tatizo kubwa sana! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo cha umwagiliaji, tuongeze scheme za umwagiliaji katika maeneo yetu. Nchi yetu haiwezi kuwa na shida ya njaa; iwe mchele au sukari lakini scheme za umwagiliaji zikiongezwa tutakuwa tumevuka hatua kubwa sana especially akinamama wanaolima mpunga. Wale akinamama wakiwezeshwa, wakajengewa scheme nzuri za umwagiliaji, watalima mpunga wa kutosha, watalima miwa ya kutosha, tutaondokana na njaa, watu watajiwezesha, wataendeleza maendeleo katika nchi yetu. Naomba sana, hilo pia liangaliwe na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la adha ya mfumo wa majitaka. Mji wa Dar es Salaam umekua vibaya sana, kwa maana ya kwamba kwanza ongezeko la watu limekuwa kubwa, miundombinu ya nyumba zile za kwetu tulizozaliwa nazo za vyumba sita banda la uani, hazipo! Kumejengwa nyumba za ghorofa, lakini miundombinu ya kuchukulia maji machafu bado haijakaa sawa. Naomba sana hilo nalo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naelekea Kisiwa cha Mafia. Sote tunaifahamu Mafia. Mafia ni kisiwa ambacho kina visiwa vingine zaidi ya vitatu, lakini kuna kisiwa kimoja kinaitwa Jibondo. Kisiwa hicho kina watu zaidi ya 3,000, lakini watu wale hawayajui maji matamu mpaka wavune maji ya mvua kwa sababu wako juu ya jabali. Juhudi zimeanza kuoneshwa za kutaka kupelekewa maji; ni kilometa tisa tu kutoka kisiwa kikuu kwenda kwenye Kisiwa cha Jibondo na usafiri wake ni boti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Serikali iangalie utaratibu wa kuwajengea miundombinu ya kuvuna maji ya mvua au kuweka utaratibu wa mabomba kutoka kisiwa kikuu cha Mafia kupita chini ya bahari ili waweze kupatiwa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niwe miongoni mwa wale wanaochangia hotuba hii ya bajeti ya awamu ya pili katika kipindi hiki cha Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Rais Dokta John Pombe Magufuli, bajeti ambayo imeonesha dira na msisimko wa hali ya juu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa juhudi anazozifanya kwa Watanzania kwa maendeleo ambayo anayaona yakiweza kufanikiwa basi Watanzania watakuwa wamegomboka na wamepiga hatua kuondokana na umaskini. Mheshimiwa Rais amelenga kuhakikisha pale palipokuwa na mianya ya mchwa anatia dawa wale mchwa wote waweze kufa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi sote ni mashahidi na sio tu humu ndani tu tunaompongeza Mheshimiwa Rais, Dokta John Pombe Magufuli hata Rais wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Ali Hassan Mwinyi amesema hadharani kazi anayoifanya Rais Magufuli ni kazi ambayo imefanywa na wao kwa miaka 30 iliyopita. Kwa hiyo, sisi sote tuna kila sababu ya kuunga mkono juhudi zake.

Mheshimiwa Spika, nikupongeze na wewe, jana umetuwakilisha vizuri sana, sisi tuko na wewe bega kwa bega, mguu kwa mguu, mbele kwa mbele hadi tujue mwisho wa wale ambao wanataka kuharibu na kudhulumu uchumi wa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake wametuletea bajeti. Bajeti hii sisi tunaifurahia, wengine wanafurahia ndani ya mioyo lakini usoni hawataki kusema ukweli na huo ni ugonjwa. Kama wamekasirika waweke magari yao pembeni, kama wamekasirika yale yote ambayo yamependekezwa wayakatae hadharani kwa vitendo sio kwa maneno ya siasa ya humu ndani.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amesema yeye tumpe ushirikiano na tumwombee dua, sisi wengine tuko kwenye Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, dua zetu, sala zetu, ibada zetu tumemwongezea yeye na tunamuombea na tunawaombea Watanzania wote kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye kulipia mafuta nyongeza ile ya Sh.40/=, wataalam wa masuala ya uendeshaji wamesema hakuna hasara yoyote inayopatikana, ni faida tupu. Kwa hiyo, hii itasaidia pesa hizo zikipatikana si vibaya kama zitapelekwa zikatumike kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya maji, umeme na mambo mengine. Pia hii imeondoa mzigo, si kwamba kutakuwa na nauli kubwa, mbona petroli inapopunguzwa wamesema hapa wanaofanya hizo biashara, hakuna hasara yoyote, tusitie maneno chumvi kabla mchuzi haujaiva. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la utalii. Utalii ni sehemu ambayo ina nafasi kubwa sana. Kuna aina nyingi za utalii, niombe wanaohusika Kijiji cha Makumbusho kiboreshwe tuweze kupata pesa zaidi na tuangalie maeneo mengine ambayo yatatuletea tija kwa maana ya kuingiza pesa. Utalii utoke Kaskazini uweze kwenda Kusini, uje Pwani, Mafia tuna utalii wa kutosha, Kisarawe tuna utalii wa kutosha kuna mapango wanakaa popo mule ndani kinyesi cha popo kikichukuliwa kinaweza kikatoa nishati ya aina fulani, niombe hilo nalo lizingatiwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukija kwenye kitabu cha bajeti, nimefarijika sana na si mimi tu nina jirani yangu Mbunge mmoja yeye pale Dar es Salaam maeneo yake mengi wanakaa watu wanaofuga kuku, sasa akiwa analipinga hili nitamshangaa sana tena nitakwenda hata kuwaambia hao watu wa huko. Sitaki kumtaja yeye mwenyewe ameshajijua. Ufugaji sasa hivi umepunguzwa tozo, kwenye mayai ya kutotolea vifaranga, kwenye vifaranga vyenyewe, kwenye bei ya vyakula, sasa unataka nini binadamu wewe zaidi ya hayo? Huoni kwamba hiyo ni tija kwa wapigakura wako? Jirani yangu, nikisema jirani yangu anajijua, hebu simama ulipongeze basi hata hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongeze lingine kwenye ushuru wa mazao, hili jambo limetusaidia sana hasa sisi ambao maeneo makubwa sana ya majimbo yetu ni sehemu za wakulima. Mkulima mdogo ndiye aliyekuwa anaumia sana, anatozwa ushuru wa mazao lakini leo akipakia gari lake halizidi tani moja, hadaiwi senti tano. Hii inatoa unafuu wa maisha, inampa nafasi mkulima aweze kuuza alichonacho, apate pesa ajiongezee katika kujiendeleza yeye, watoto wake, familia yake hali kadhalika na kujijenga katika mazingira ya kuondokana na umaskini. Sasa leo basi hata hilo ndugu zangu mnalikataa, mbona inakuwa mushkeli kidogo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi sitaki kusema hawana jipya, wanayo mapya lakini wajipange, wazungumze yale ya uhalisia wa maisha. Hakuna eneo katika jimbo ambalo halina wajasiriamali, leo wajasiriamali watapewa vitambulisho, watatafutiwa maeneo ya kufanyia biashara zao na sisi ndiyo wasemaji wao, leo hii wewe hata hilo ukilipinga, wewe mtu wa aina gani? Kilimo ukikatae, ushuru wa mazao uukatae, license ukatae!

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dokta Magufuli katuletea neema, anataka kumtua mzigo mwananchi wa kijijini. Hii Sh.40/= ikienda kijijini wanawake watapunguziwa mzigo wa kubeba maji kichwani, watapunguziwa muda wa kufanya kazi za kutafuta maji watarudi watafanya kazi zao za kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze Waziri na niombe Wabunge tusimame kwa pamoja tuhakikishe kwamba bajeti hii inapita, mambo mazuri yanayoletwa na Mheshimiwa Rais yetu yanatimizwa, asilimia inayotakiwa kwa kila eneo ipelekwe lakini maendeleo yabaki palepale kwamba Watanzania tupate faraja, tuondokane na ukubwa wa matatizo ya kujiendesha kimaisha.

Mheshimiwa Spika, sisi tutaungana na wewe kwa yale yote ambayo umeyaahidi jana mbele ya Rais, Mheshimiwa Dokta John Pombe Magufuli kuhusu makinikia na mazagazaga mengine yote ambayo yamezungumzwa tutakuwa pamoja na wewe, tutashirikiana na wewe. Nina
uhakika kwenye suala la tozo ya maji, wewe na Wabunge wenzangu tutasimama pamoja kuhakikisha tunatua ndoo ya mwanamke kichwani, tunahakikisha kwamba mwanamke atakuwa na nafasi ya kutosha katika kufanya kazi zake badala ya kwenda kukaa saa sita, saba anasubiri maji ayafikishe nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa dakika ulizonipa ni chache, lakini kwa kutumia taaluma yangu nitahakikisha nazitumia vizuri na naomba ridhaa yako nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutuwezesha kuwa hapa leo na kupata nafasi hii ya kuchangia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kikubwa zaidi, naomba ridhaa yako niweze kuishukuru Serikali yangu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisimamiwa na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kitendo alichokifanya Waziri Mkuu leo humu ndani ni cha kihistoria cha kuhakikisha mafuta yanapatikana, sisi wengine ni wananchi tunaotokana na wazazi wenye kipato cha chini ambao tunatumia mafuta katika biashara ndogo ndogo na kutuwezesha kuishi katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri Mkuu kila la kheri, Mawaziri wote kila la kheri pamoja na watendaji na Watanzania wote sasa


ambao tunakaribia kufunga mwezi wa Ramadhani na wale ambao hawatahitaji kuyatumia mwezi wa Ramadhani kwa kweli hii ndiyo nafasi yao.

KUHUSU UTARATIBU . . .

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba unilindie dakika zangu. La pili, nadhani Mchungaji hajui lugha ya Kiswahili vizuri amezoea lugha ya Kichungaji, nimesema naomba nipongeze, sijasema naomba nichangie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia bajeti ya Wizara ya Maji. Nchi yetu awamu hii tunakwenda kwenye awamu ya viwanda, lakini pamoja na hayo tunahitaji maji ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu. Naomba Serikali iangalie uwezekano wa kutuletea maji maeneo mengi, Wabunge wengi humu ndani wamesimama wakielezea tatizo la maji kwenye maeneo yetu. Kwanza naomba wataalam wafike hadi kwenye miradi ya vijiji vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, mradi wa Wilaya ya Kisarawe ambao umepata baraka za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwamba maji kutoka Ruvu Juu yafanyiwe utaratibu yaweze kwenda hadi Kisarawe. Mradi huo tayari taratibu zote zimeshakamilika, ni nini na ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa mradi huo na kitu gani ambacho kinakwamisha mradi huo mpaka leo usiweze kufanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la maji kwa Mkoa wa Pwani kwa kweli tukisema kwamba kuna maeneo maji hayapatikani inasikitisha sana kwa sababu mkoa wetu umezungukwa na mito mingi sana. Kwa mfano, Mto wa Rufiji maji yake yanamwagika hovyo, kwa nini usitengenezwe utaratibu wa kuutumia? Toka nimeingia ndani ya jengo hili nimekuwa nikiomba maji ya Rufiji yaweze kutumika maeneo mengine, haijawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna Mto Wami nao una maji mengi sana. Tatizo linakuja wakati wa mvua yale maji yanakuwa machafu kwa maana yanakuwa na tope nyingi. Je, ni lini Serikali itaona umuhimu au itatengeneza utaratibu wa kuhakikisha maji yale yanasafishwa na kuweza kutumika kwa maeneo yaliyo jirani? Hakuna sababu sasa hivi maji ya kwenda Chalinze yatoke Ruvu Juu wakati Mto Wami uko jirani na Chalinze. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kero ya maji ni kubwa sana kwenye shule zetu za msingi na maeneo ya huduma muhimu kama zahanati, vituo vya afya na hospitali. Kwa nini haya mashirika na idara za maji zilizopo zisipewe jukumu la kusimamia uvunaji wa maji ya mvua wakawezesha kuwapatia maji watoto wa shule, vituo vyetu vya afya na kwenye huduma muhimu? Maji ya mvua yakivunwa yanaweza kutumika kwa ajili ya wananchi na kuondoa kero ya maji na tumeahidi kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani japokuwa wanaume wakibeba maji wanauza, lakini shida ni ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikija kwenye suala la maji taka, mfumo wa maji taka Dar es Salaam siyo mzuri. Tunajua maji taka, mniwie radhi kwa kutumia hili neno, ni maji ya kinyesi au ya uchafu mwingine, lakini sasa hivi Dar es Salaam imefurika maji taka kweli. Machupa machafu yamo humo, mifuko ya rambo imo humo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara ikiongozwa na Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi wanayofanya na kuweza kutekeleza zaidi ya asilimia 50. Lini mradi wa maji toka Ruvu Juu kwenda Kisarawe utaanza ukizingatia kazi zote muhimu za uzalishaji mradi huo umeanza, wananchi wanahitaji maji na viwanda pia vinahitaji maji. Mradi wa Kimbiji na Mpera lini utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mto Wami una maji mengi sana lakini wakati wa mvua maji hayo huwa machafu, nini mpango wa Serikali wa kuweza kuyasafisha yatumike wakati wote na kuweza kuondoa kero za wananchi Mkoa wa Pwani. Nini mkakati wa Serikali kwenye matumizi ya maji ya Mto Rufiji? DAWASA wapewe jukumu la kuvuna maji ya mvua maeneo ya shule na hospitali. Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa na kuipongeza Serikali yangu kwa kutimiza miaka mitatu katika utekelezaji wa shughuli zake. Pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, pongezi nyingi kwa Baraza la Mawaziri, pongezi nyingi kwa viongozi wote waliokuwa maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Mpango wa Maendeleo. Naomba kwanza nianze kupongeza kwa yale ambayo yemetekelezwa kwa wakati na yakakamilika. Hapo hapo, naipongeza Serikali kwa kuthubutu kutengeneza reli ya Standard Gauge kwa kutumia fedha za ndani kitu ambacho siyo cha kawaida. Kwa kutumia fedha za ndani, Mheshimiwa Rais amethubutu na ameweza kuanza kuijenga reli hiyo. Ujenzi wa reli hiyo utatusaidia kukuza uchumi wetu kwa sababu itarahisisha suala la usafiri iwe wa abiria, iwe wa mizigo kwa Tanzania na hata kwa nchi jirani na kwa muda mfupi sana. Ujenzi wa reli unakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ambazo zinaunganisha Mikoa yote nchini Tanzania hata zile za kwenye Halmashauri zetu tunakotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ufufuaji wa reli ya kutoka Ruvu – Tanga – Moshi. Hili ni jambo jema. Reli hii ilisahaulika kwa muda mrefu sana. Ukichukulia hii awamu ya uchumi wa viwanda, reli hii itakuwa kiunganishi cha usafiri hasa kwa wale ambao mikoa yao imepakana na reli hii, wanaofanya biashara ikiwemo Mkoa wetu wa Pwani, ambako kuna viwanda vingi, imevunja record, viwanda vingi vinazalisha na malighafi zinatoka ndani na nje ya nchi yetu. Kwa hiyo, hili litakuwa litasaidia sana na sisi wote hapa ni mashuhuda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, napongeza Serikali kwa juhudi ambazo zimeanza upya za ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Hii ni bandari ambayo inatakiwa ijengwe kwa wakati kwani itasaidia katika kukuza uchumi wetu na wa nchi nyingine. Kuna kikwazo kidogo, sina mashaka, nina uhakika Serikali italifanyia kazi kwa maana ya kulipa fidia wale wananchi waliokaa katika maeneo yale ili ujenzi uanze na uende kwa wakati na watu wa kujenga hiyo bandari tunawajua ni watu wa kutoka Oman na Wachina wako pale wanasubiri. Kwa hiyo, ulipaji wa fidia ni jambo la msingi na juhudi tunaziona. Juzi tulikuwa na Makamu wa Rais katika Mkoa wetu wa Pwani, aliweka juhudi ya kwenda kuona jinsi bandari ile ilivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya kama tutaweka utaratibu wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi. Nchi yetu ina eneo kubwa sana la ukanda wa bahari lakini hatuna bandari mahsusi kwa ajili ya uvuvi. Ni wakati muafaka sasa tukaweka Bandari ya Uvuvi ikaweza kuwasaidia wavuvi wakubwa na hata wadogo wadogo. Bandari zetu za uvuvi ziwepo lakini yale maeneo ya fukwe (beach) ambapo wanachi wanaweza kwenda wakapumzika, ijulikane hili ni eneo la kupumzika na hili ni eneo la biashara ya uvuvi kuliko sasa hivi maeneo mengi ya ufukwe yamechanganyika kati ya wavuvi na watu wanaotaka kwenda kupumzika jioni. Mfano mzuri, miaka ya nyuma, pale Posta ya zamani ule ufukwe ulitengenezwa vizuri na wananchi wengi jioni walikuwa wanakwenda kupumzika, wanapata upepo wa bahari na kupata afya nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tupo kwenye awamu ya uchumi wa viwanda ambao unakwenda sambamba na nguvu kazi ya wananchi ambayo inatokana na afya bora, naipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na Hospitali za Wilaya. Kwenye maeneo ambayo majengo hayajakamilika, yalijengwa kwa nguvu za wananchi, ni vyema sasa Serikali ikaongeza juhudi zake, ikatenga fedha, ikashirikiana na wale wananchi kwenye yale maboma, wakajenga na kuhakikisha majengo yale yanakamilika ili wananchi wetu waweze kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya ujenzi ndiyo hiyo tunaiona na magari ya wagonjwa tumeona yamepelekwa, tunaomba maeneo mengine ambako hamna magari ya wagonjwa yapelekwe. Kwenye maeneo ambayo majengo yamejengwa na vyumba vya upasuaji vimeshajengwa, nashauri na kuiomba Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka vifaa tiba na miundombinu ya kuweza kufanya kazi vizuri katika hayo maeneo, kwa maana ya Madaktari wa Upasuaji, Madaktari wa Macho na wa magonjwa mbalimbali ili iweze kukidhi standard ya kile kituo ambacho kimejengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta maeneo mengi hawana hata vifaa vya kupimia sukari kwa wagonjwa wasukari na vya kupimia pressure. Ni vizuri sasa tukapeleka zaidi hivyo vifaa kule chini vitasidia wananchi wasiweze kuhamishwa kutoka hospitali hiyo kwenda kwenye ngazi ya Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika naipongeza Serikali yangu kupitia Wizara ya Afya kwa hatua ilizofikia kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaimarika. Inahakikisha idadi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua inapungua, hali kadhalika na matatizo mengine yanayomkuta mwana mama. Hili ni jambo jema lakini bado kampeni hii naomba iendelee. Pia naomba ikiwezekana vile vifaa vya kujifungulia mama kwa sababu mama naye ana haki ya kuzaa salama na mtoto hana kosa lolote, anahitajika azaliwe, aishi maisha salama, ni vyema basi vile vifaa tiba ikaangaliwa uwezekano, bei iliyokuwepo siyo kubwa sana, lakini bado siyo vibaya kama itapungua zaidi ya hapo, ikibidi hata wakipewa bure nao ni haki yao ya msingi. Kwa hiyo, ni vizuri tukaliangalia hilo ili kuweza kumlinda mama mjamzito, mama anayejifungua halikadhalika na yule mtoto anayezaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu inavyosaidia watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa. Mungu azidi kuwasaidia hao watoto lakini juhudi tumeziona. Maagizo na maelekezo kwenye Halmashauri zetu tunayasikia yakitolewa. Haya ni mambo mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie suala la maji. Maji ni muhimu sana. Tunalenga kumtua mama ndoo kichwani lakini pia tunalenga kumtua na baba ndoo kichwani kwa sababu naye kama hajaoa lazima akajitafutie mwenyewe maji. Juhudi ya Serikali iliyofanyika kusogeza huduma ya maji tunaipongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mikubwa ya maji tuliyoiona, tumeona Mradi wa Maji wa Kisarawe, nashukuru Serikali na imefanya vizuri lakini naomba speed isilegee, iendelee, speed iwe nzuri, watu waweze kupata maji, hasa wale ambao hawajapata maji ya bomba kwa muda mrefu hasa Wilaya ya Kisarawe. Vilevile kuna Mradi wa Maji Mkuranga na Chalinze na naipongeza Serikali kwa Mradi wa Maji wa Mafia Jibondo. Hicho kisiwa kilikuwa hakijawahi kusikia hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Awali ya yote kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia kusimama hapa leo na namuomba Mwenyezi Mungu alijalie Bunge hili tuendelee kujadiliana kwa salama na amani katika Kamati hizi mbili ambazo zinalenga kubeba uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwatoe hofu Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri, inapotokea Mbunge yeyote anapochangia, anapotoka nje ya mstari msisite kusimama kwa mujibu wa kanuni na kufafanua yale ambayo yanapaswa yafafanuliwe. Maana kuna wengine hapa wanataka kutulisha matango pori na sisi hatutaki kula matango pori, tumeona bundi na bundi wameshindwa. Kwa hiyo, endeleeni kuchapa kazi na fanyeni kazi yenu kwa uadilifu kama ilivyo. Ninyi mnaisimamia Serikali na tunapaswa na wananchi wanapaswa kujua Serikali yetu inafanya nini, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia suala la uwekezaji. tunapozungumzia suala la uwekezaji Serikali inaweka mkono wake ili kuhakikisha uchumi na mapato ya nchi yetu yanaendelea. Niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuifufua ATCL, imenunua ndege sita hadi sasa na inahakikisha uchumi unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimsaidie mwanangu, mwanafunzi wangu Ester Bulaya, unapojua kuendesha gari ya Volkswagen hushindwi kuendesha V8 na unapotoka kuendesha V8 huwezi kushindwa kuja kuendesha beetle, IT au corolla kama unavyosema mwenyewe. Kwa hiyo, mwanafunzi wangu naomba hilo ulizingatie usisahau ulipotoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, anapozungumzia kwamba marubani wanakosea kukosea ndege, anataka kuupotosha umma. Mimi nasema Serikali imefanya jambo zuri na la uhakika kufufua uchumi wa ndege na kuendelea kujenga reli ya SGR. Ndege na reli zikiwa pamoja uchumi utaimarika.

Tunaomba tu Serikali ihakikishe na suala la bandari linawekwa katika moja ya ajenda zake ili wafanyabiashara badala ya kutumia magari kutoa hapa kupeleka maeneo mengine kwa kutumia barabara sasa wanaweza wakatumia hiyo reli na ikapokelewa bandarini na uchumi ukaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kusema kwamba tunahitaji kuyasimamia na kuyaboresha mashirika yetu ya umma. Iangalie uwezekano, wa pale panapohitaji kupeleka mtaji basi ipeleke mtaji kwa wakati, wakati huo huo kuangalia rasilimali watu. Rasilimali watu katika mashirika yetu ni muhimu sana, wao ndio watasaidia kuhakikisha kazi zinakwenda vizuri na kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la bodi za Wakurugenzi na Wenyeviti, mashirika yahakikishe kwamba bodi za Wakurugenzi na Wenyeviti wanateuliwa kwa wakati ili waweze kusimamia shirika alilopangiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Shirika la SUMA JKT, hili shirika lina vitengo vingi vya kufanyia kazi, lakini nishauri kama Kamati ilivyoshauri, wale vijana wanaokwenda JKT iwe kwa mujibu wa sheria au kujitolea kuwekwe na sera ambayo itawasaidia na kusaidia shirika na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wanaokwenda kufanya kazi za kujitolea, wafanye mafunzo ya kijeshi ambayo ni nidhamu, lakini baada ya hapo, waende kwenye Shirika la SUMA JKT ambako kule watafundishwa kushona, kulima, kutengeneza maji kwa ajili ya biashara; na mbinu za ujenzi na ujenzi ambao hauna gharama kubwa. Nao wakitoka hapo, wanakwenda kujiajiri wenyewe ama wanaweza wakaajiriwa kwenye Taasisi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hili shirika likiwezeshwa vizuri, linaweza likasaidia, kwa mfano, tukisema shirika hili lipewe kazi ya kushona uniforms za Jeshi zote, kwa sababu tayari wana kiwanda cha nguo. Pia tunaweza tukasema washone viatu vya majeshi yote, kwa sababu tayari wana kiwanda cha kushona viatu na ngozi. Kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaona ni jinsi gani tunaweza tukaisaidia SUMA JKT ikawa kiwanda cha kuzalisha bidhaa lakini vilevile ikawa kiwanda cha kuzalisha rasilimali watu, wakitoka hapo wakaenda kufanya kazi maeneo mengine ama wajiajiri wenyewe. Kwa sababu sehemu kubwa ya vijana wetu wako mitaani wamezagaa, wengine hawana utaalam lakini wana elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, elimu wanayoipata shuleni na elimu watakayokuwa wameipata vyuoni, wakienda huko wanaweza wakapata utaalam wa kuja kufanya kazi za kujipatia kipato; na vilevile kipato watakachopata kitakatwa kodi na hiyo kodi itaingia kwenye sehemu ya kipato cha Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tukaona ni jinsi gani tunaweza kuisaidia Serikali kwa kuzalisha vijana ambao watakwenda kufanya kazi na kujiajiri, wakati huo huo SUMA JKT na yenyewe ikafanya kazi ya kuwafundisha hata maeneo mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo, SUMA JKT wamekopesha matrekta, tunaiomba Serikali isimamie upatikanaji wa fedha ambazo zinatokana na malipo ya matrekta waliokopa watu. Matrekta hayo, mengine Wabunge tumo humo tunaodaiwa. Tunaomba Bunge lisimamie kama wamo Wabunge waliokopa, basi Serikali ilete barua huku ili hela zilizokopwa zirudishwe kwa wanaohusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Mimi ni miongoni mwa Wajumbe wa Kamati ya PIC.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kupata nafasi hii. Nianze kwanza kwa kumshukuru mwenyezi mungu kwa kutujaalia leo kuweza kujadili bajeti hii ya Wizara ya Afya. Lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli, halikadhalika nimpongeze Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na Naibu wake Mheshimiwa Faustine Ndungulile, Katibu wa Wizara wajina wangu Zainab Chaula pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Afya kwa kazi nzuri wanayoifanya na wala haina kificho kwa sababu tunaona na tunashuhudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza ambalo tunaliona katika awamu hii ambayo limefanywa kwa juhudi kubwa ni Taasisi ya Moyo ambayo wameweza kupeleka vifaa vingi vya kisasa wameleta wataalam kutoka nje pamoja na wataalam wa ndani wakisimamiwa na Prof. Jannabi tunawapa pongezi nyingi sana kinachobakia hapo ni kuhakikisha wale wagonjwa ambao wako nje ya mji wa Dar es Salaam, wako nje ya mikoa wako vijijini wengi wapo wanaopata matatizo ya moyo elimu ipelekwe na utaratibu uelekezwe jinsi gani tunaweza tukawatoa kule wakaja kupata huduma hapo kwenye Taasisi ya Moyo Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo limedhihirisha kwamba Wizara yetu pamoja na Serikali imesimama kidete kuweka madaktari wengi, kuweka vifaa tiba vingi matokeo yake idadi ya wagonjwa ambao ilikuwa wanakwenda kutibiwa nje imepungua kutoka 683 2014/2015 hadi wagonjwa 62 kwa mwaka huu tunaongea leo hii inabidi tuwapongeze na ningekuwa kwenye mkutano wa nje ningesema watu wote wawapigie makofi Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, twende kwenye suala la matibabu lakini kupitia bima ya afya, bima ya afya ni suala ambalo ni muhimu kwa Taifa letu bado Serikali ina jukumu la kuhakikisha Watanzania wote wanapata elimu na kujua faida na umuhimu wa bima ya afya. Baadhi ya Wabunge humu ndani wamezungumza jinsi mgonjwa anavyoenda kutibiwa anakutwa na deni kubwa anashindwa kulipa maiti zinashindwa kutolewa kwa sababu ya deni lakini elimu ya bima ya afya ikitolewa vya kutosha yule mtu hatodaiwa na niseme tu kwa maiti za kiislamu lazima itangazwe anadaiwa au hadaiwi? Sasa kama anadaiwa tunamtwisha mzigo ambao haustahili nishauri tu suala la bima ya afya liendelee kutolewa elimu na ikiwezekana uwekwe utaratibu wa kuwa na bima ya afya ambayo kila mtu ataimudu, kila mtanzania atamudu na kila mtanzania ataitumia hiyo bima ya afya kokote kule isiwe tu kama mimi natoka Mkoa wa Pwani basi bima ile iishie Pwani hapana siku nikipelekwa Muhimbili nitatibiwa na tiba gani kwa hiyo naomba hilo nalo litizamwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Sera ya tiba ya wazee hili lifanyiwe bidii wakati ndiyo huu unakuta wazee wengi ukienda huko kwa watani zangu Shinyanga wengi wanapigwa wanauwawa hawana mahala pa kukimbilia mpaka wapate hifadhi kwa hiyo kuna haja ya kutengeneza sera si tu matibabu waangaliwe na mambo mengine muhimu wazee wote watarajiwa ndiyo sisi na wengine wanakuja weze kupata utaratibu mzuri wa sera ya wazee kwa ajili ya maisha yao na tiba halikadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kuhakikisha elimu ya afya ya mama mzazi mtarajiwa ilivyoboreshwa lakini bado kuna haja na kuna kila sababu hawa akinamama huko chini zahanati zetu tumeziboresha, vituo vya afya tumeboresha tuhakikishe basi wanakwenda hospitali. Nimeona takwimu kwenye jedwali humu kwamba wanatakiwa waende mara nne katika kipindi cha ujauzito lakini wengi wamekwenda mara moja wengine mara mbili bado kuna haja ya kuboresha zahanati zetu na vituo vya afya ili mama mjamzito ashawishike kwenda kwa sababu kwingine huduma hazipo zipo mbali kwa hiyo inamuwia vigumu kuna haja ya kuongeza miundombinu ya vifaa tiba na hata watumishi katika zahanati zetu katika vituo vya afya ili waweze kwenda sambamba na mahitaji ya jamii wanayowazunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nagusa kidogo kidogo kwa sababu muda hautoshi.

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.

MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa miongoni mwa washiriki katika mjadala wa bajeti 2018/2019. Naipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa kufanya kazi vizuri chini ya uongozi wa Mheshimiwa Waziri na Manaibu wake pamoja na watendaji wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona juhudi za Serikali katika suala la afya na kuongeza juhudi katika ujenzi wa zahanati. Naiomba Serikali iendelee kutoa mchango wake katika zahanati na maeneo ya visiwani. Naomba nielezee zilizopo Mkoa wa Pwani Wilaya ya Rufiji, Kibiti, Mkuranga na Mafia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jamii inayoishi kwenye visiwa inahitaji huduma zote muhimu katika maeneo yao ikiwemo afya na usafiri wa uhakika ambao ni haki yao kwa kuwa maeneo mengine kuna aina mbliambali za usafiri. Naomba Serikali iongeze nguvu au kupeleka usafiri wa boti la wagonjwa kwa wananchi wa Kisiwa cha Koma na Kwale vilivyopo Wilaya ya Mkuranga ili kuokoa na kurahisisha usafiri kwa wagonjwa hususani kwa wajawazito, watoto na wengine wanapougua ukizingatia mama mjamzito anapotoka kujifungua hajui muda gani wala siku. Kusipokuwa na huduma sahihi na za haraka hupelekea kupoteza maisha na hivyo inatokea sana kwenye visiwa vyetu vya Mkoa wa Pwani. Chondechonde naiomba Serikali itupatie huduma hiyo au kupeleka vifaa vyote muhimu vya tiba na wahudumu muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara ya TAMISEMI izielekeze Halmashauri zote ziweze kutenga fedha kwa ajili ya taulo za wasichana mashuleni ili kuwawezesha wale wasio na uwezo wa kuzipata na kushindwa kuhudumia masomo pia kuwa na ufaulu usioridhisha kwa watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linawezekana kwani Halmashauri ya Kisarawe imeanza kutenga fedha hizo kwa mantiki hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe na nyingine ambazo zimekuwa zinatenga fedha. Nimelisema hilo kwa kuwa ni tatizo kubwa sana kwa baadhi ya wanafunzi wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutoa fedha na kukarabati shule Kongwe nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali katika juhudi zake za kusogeza maendeleo jamii na kuziwezesha. Suala la kupunguza riba kwenye mikopo ni jambo jema sana, hivyo basi mchakato wake ukamilike kwa haraka ili ulete unafuu kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA; iwezeshwe ili iweze kufanya kazi zake kwa wepesi. Mkoa wa Pwani unahitaji barabara zake ziwe za kupitika mwaka mzima kwani zitarahisisha maendeleo na pia kuwezesha kusafirisha malighafi na bidhaa zinazotoka kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu kwa usimamizi mzuri wa kazi za Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuchangia kwa maandishi na nianze kwenye michezo. Pamoja na juhudi za kusimamia michezo, kuna haja ya kuongeza bidii kwenye michezo mingine ikiwa ni pamoja na riadha, mpira wa pete, gofu na mengineyo badala ya kuweka jicho letu kwenye mpira wa miguu ambako bado tunahitaji kuweka juhudi na mikakati madhubuti ili vijana wetu waweze kucheza vizuri na pia miongoni mwao watokee makocha badala ya kutegemea makocha kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuwe na utaratibu wa kuimarisha viwanja vya michezo badala ya kuwa na viwanja vingi vya mpira wa miguu wakati kuna vipaji vya aina mbalimbali vya michezo nchini.

Mheshimiwa Spika, Serikali iangalie au chombo maalum kiwepo kwa ajili ya kufuatilia watangazaji, kwanza katika maslahi yao, vifaa vya uhakika vya utangazaji na mwisho kuangalia au kuchuja waandishi/watangazaji ambao hawana maudhui ya utangazaji na matamshi sahihi na fasaha ya Kiswahili.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe J. Magufuli, Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe, Naibu Waziri Mheshimiwa Kwandikwa, Naibu Waziri Mheshimiwa Mhandisi Nditiye, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara husika. Mheshimiwa Waziri ameacha historia Pwani kwenye maji, nina hakika na barabara atazitendea haki, hongera sana.

Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa usimamizi mzuri na kufuata ilani kwani miradi mingi imeweza kuvuka na kupiga hatua na kuleta sura nyingine nchini. Hii ni kwa sababu Mheshimiwa Rais Magufuli ameamua kuleta maendeleo nchini. Kwani tumeona ununuzi wa ndege, ukarabati vya viwanja vya ndege na hata Wilaya yetu ya Mafia imepata fedha kwa ajili ya matengenezo ya Mafia.

Mheshimiwa Spika, sambamba na ukarabati wa Bandari ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga pia tunaishukuru Serikali kwa ujenzi wa Bandari ya Nyamisati na ukarabati, tunaomba ukarabati Gati la Kilindoni, Mafia uende sambamba kwani ndiyo itakuwa mwanzo/mwisho wa safari zote za wananchi wa Mafia na kuinua uchumi na kuendeleza Kisiwa cha Mafia na hata idadi ya watalii itaongezeka. Naomba kupata maelezo lini kazi hiyo itaanza.

Mheshimiwa Spika, jiografia ya Mkoa wa Pwani iko katika hali ya kutegemeana na mikoa mingine nchini na pia kiungo cha safari zote za mikoani. Napenda kujua ujenzi wa barabara ambazo ni kiungo kikuu kwa wilaya nyingine na hata mikoa utaanza lini. Mfano, barabara ya Kisarawe – Maneromango – Vikumburu - Mloka, hii barabara ni muhimu sana na hasa kwa sasa ambapo kuna ujenzi wa mradi wa umeme Rufiji.

Mheshimiwa Spika, mkoa una visiwa vidogo vidogo vingi katika Wilaya ya Kibiti, Mafia, Mkuranga na Rufiji, tunaomba bajeti zinazokuja wafikirie kupeleka boti za uhakika ili wananchi wa maeneo hayo nao wawe na uhakika wa safari na kupata huduma muhimu.

Mheshimiwa Spika, kuna tatizo kubwa la mawasiliano kwenye Mkoa wa Pwani kwenye baadhi ya maeneo, kwingine mawasiliano ya simu na maeneo mengine mawasiliano ya redia hasa Radio TBC. Mfano, Wilaya ya Kisarawe ambako kuna minara yote/baadhi ya TV/Radio lakini bado kuna maeneo hawapati/kusikia chombo hicho cha Taifa, ikiwemo Wilaya ya Mafia na baadhi ya maeneo na hata mawasiliano ya simu. Hili suala linaeleweka kwenye ofisi ya Mheshimiwa Waziri, hivyo napenda kupata majibu ya ufumbuzi wa matatizo hayo.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kupata taarifa rasmi ya lini Kisiwa cha Mafia kitapata chombo/meli/boti/feri ya uhakika kwa ajili ya wananchi wa Mafia.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha leo hii kuweza kuijadili bajeti ya nne kwa Awamu hii ya Tano – 2019, chini ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Mpango; Naibu wake, Mheshimiwa Ashatu Kijaji pamoja na watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa umakini wao kwenye kutekeleza majukumu yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka huu imegusa kila sekta katika nchi yetu na kuelekea kwamba hali ya uchumi itazidi kuwa nzuri kwa wananchi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa umeme wa Maji, Bonde la Rufiji (Stiegler’s Gorge), ni mradi ambao umeleta sura mpya kwa Taifa letu na uhakika na wepesi wa maisha kwani bei ya umeme itashuka, viwanda vingi vitajengwa, wananchi watapata ajira, kutakuwa na utunzaji na uboreshaji wa mazingira na kilimo cha umwagiliaji kitaongezeka. Haya yote ni matarajio makubwa sana kwa Taifa na pia kwa mikoa inayozunguka eneo husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli ya SGR lazima kuwe na umeme wa bei nafuu ili treni ziweze kufanya safari zake, hivyo mradi wa Stiegler’s Gorge ni sahihi kabisa. Ni vyema, Serikali ikaanza utaratibu wa ujenzi wa skimu za umwagiliaji kwa ajili ya kilimo kwani maeneo mengi yapo kwenye bonde. Hii itasaidia uzalishaji wa chakula na ajira pia kuwa na viwanda vya kukoboa na kusaga nafaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa barabara toka Ubena Zomozi hadi eneo la mradi na kutoka eneo la mradi hadi Utete – Nyamwage kwa kiwango cha lami itafungua uchumi wa nchi na matumizi ya Bandari ya Mtwara na nchi jirani. Pia utalii uliopo Kusini mwa Tanzania ikiwemo na Mafia. Pia barabara ya Kibiti – Mkoka itakapokuwa kwa kiwango cha lami itainua uchumi wetu. Ujenzi wa bwawa hilo sio kitu kigeni duniani kwani hata Ethiopia, Egypt na kwingineko wanajenga. Nimalizie hoja hii kwa kusema kelele za mlango hazizuii mtu kulala.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kodi kwenye viwanda vya taulo za kike ni zuri, hii itasaidia wanawake na watoto wa kike (wasichana) kuweza kumudu kupata kununua hizo taulo. Ni vyema Serikali ikaweka utaratibu wa bei maalum pia utaratibu wa kuhakikisha maeneo mengi vijijini, zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizo pembezoni zinapata taulo hizo kwa urahisi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza kodi kwenye mawigi, hii haina faida yoyote kwa jamii uzuri au kupendeza kwa mtu ni vile unavyojiremba.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nachukua nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi kwenye bajeti hii ya mwisho kwa kipindi hiki cha Bunge la Kumi na Moja la Awamu hii ya Tano chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph Magufuli. Pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa juhudi zake katika kuongoza Taifa letu kwa kushirikiana na Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Baraza la Mawaziri.

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa kwa hotuba nzuri ya bajeti ya 2020/2021 ambayo imegusa kila eneo na kuelekea mafanikio yalipatika nchi.

Mheshimiwa Spika, naipongeza Serikali kwa juhudi ambazo inazifanya katika kutoa elimu na kupambana na virusi vya Corona ambavyo ni tishio kwa nchi yetu na dunia kwa ujumla. Pamoja na juhudi hizo je, ni kwa kiwango gani nchi yetu tumeweka mpango wa elimu, vifaa tiba kwa maeneo ya pembezoni na maeneo ambayo yana mkusanyiko wa watu wengi?

Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa na mafuriko maeneo mbalimbali ambapo kumepelekea uharibifu wa miundombinu ya barabara, nyumbani na maeneo mbalimbali ya majengo ya huduma kwa jamii, mifugo pamoja na mazao na mashamba. Kwa kuwa jambo hili la mafuriko limekuja kidharura na mvua bado zinaendelea kunyesha, je, Serikali imejipangaje kurudisha hali ya miundombinu ya barabara kwa haraka ili kuleta urahisi wa mawasiliano kwa jamii?

Mheshimiwa Spika, miradi mingi imekumbwa na kadhia hiyo hivyo kuna uwezekano wa miradi mingi kuchelewa kukamilika kwa wakati mfano mradi wa kufua umeme wa Mwalimu Nyerere ambao uko Rufiji ambako barabara imeharibika na safari ya kupeleka vifaa kuchelewa. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa fedha kwa TANROADS na TARURA ili kuboresha miundombinu ya barabara?

Mheshimiwa Spika, natoa pongezi kwa Waziri Mkuu katika suala la mafuriko alilisimamia vyema kwa kufika maeneo mbalimbali yaliyopata kadhia hiyo na kuwafariji na kutoa misaada. Pamoja na hilo Mheshimiwa Waziri Mkuu hongera kwa usimamizi wa Ilani na utekelzaji wake kama ulivyoeleza kwenye hotuba yako kwa “mmeahidi na mmetekeleza.” Miradi mbalimbali iliyoanzishwa imeweza kuongeza kipato cha uendeshaji maisha kwani tumetoa ajira hasa kwa vijana na kuweza kukuza uchumi wetu. Pia kutoa mafunzo mbalimbali kwa vijana ambayo yanawasaidia kujiendesha.

Mheshimiwa Spika, kuna kundi la vijana ambao waliathirika kwa kutumia madawa ya kulevya na Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuhakikisha wanaacha na wengi wanaingia kwenye mfumo wa kutumia dawa ambazo zimewawezesha kurudi kwenye hali yao ya kawaida. Ni vyema Serikali ikawawekea utaratibu wa kuwapa mafunzo ya ujasiriamali. Mfano mzuri wa vijana kama hao ni Kituo cha Kutolea Dawa kilichopo Mkoa wa Dodoma.

Mheshimiwa Spika, nalipongeza Bunge Mtandao limeanza kwa wakati muafaka kwani kutokana na tatizo hili la Corona sijui Bunge letu lingeendeshwaje. Pongezi kwako na Serikali yetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba kuwasilisha.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. ZAYNABU M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Niwe miongoni mwa wale ambao watachangia katika jambo lililo mbele yetu ambalo ni Muswada. Muswada huu ni muhimu sana, kwa waandishi wa habari, lakini pia Muswada huu ni muhimu sana, kwa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri ameweka historia. Sote tunajua, waandishi wa habari walikuwa wanalitaka jambo hili kwa muda mrefu sana, kiasi ambacho kulianzishwa taasisi zisizo za kiserikali kwa maana ya NGO’s za wanahabari wanawake, za wanahabari wa michezo, za wanahabari wa mazingira, wote hawa walikuwa na lengo moja la kutaka kupata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Muswada umeletwa, niombe Muswada huu uharakishwe kama Mheshimiwa Rais alivyosema na bahati nzuri tunaumaliza leo Jumamosi, kesho unasafirishwa, Jumatatu anaweka saini kazi mbele kwa mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamesemwa, lakini niombe katika yaliyozungumzwa mle niweke msisitizo kwa mambo machache. La kwanza, bodi iwe na uwiano, wanawake watazamwe, kanuni ziharakishwe, kwa sababu ndiyo zitakazosaidia mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa umuhimu wa Muswada huu, ndugu yangu Kubenea hayupa a.k.a Yuda Iskarioti, amezoea kuajiri watu kuwalipa kwa posho ya stori anauogopa Muswada huu. Uharakishwe, wanaonyanyasika na wanaodhalilika, waandishi wa habari ambao hawajawahi kupata mshahara kwa wakati, basi hii sheria itakwenda kuwasismamia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi ni suala la bima. Tumeshuhudia waandishi wa habari, wanapita katika maeneo mbalimbali hawana bima wanahitaji kupatiwa bima kwa sababu hayo waajiri walikuwa hawayaangalii. Kwa hiyo, nina hakika hili litawasaidia na litawapeleka kwenda kufanya kazi zao vizuri na kwa uadilifu na kwa uangalifu. Napata kigugumizi wanaposema watu wasipatiwe leseni, hivi dereva gani atakayepita na gari barabarani asiwe na leseni, traffic akamwacha, Daktari gani atakayemtibu mgonjwa hana cheti, tumeshuhudia Madaktari feki wangapi wanaokamatwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumelalamika sana kwenye tasnia ya habari, kwamba ilikuwa inaachwa nyuma haiangaliwi. Niombe wenzangu mliokuwa humu ndani tuhakikishe tunaupitisha na nawashukuru wale waliotoa historia ndugu yangu Tundu Lissu ametoa historia nzuri sana, wengine tumejifunza mengi, tulikuwa hatuyajui. Baada ya kuchangia yeye akaona atoe historia mdogo wangu na Devota Minja na yeye hali kadhalika. Kwa hiyo, nasema Muswada huu umekuja kwa wakati tuupitishe uweze kufanya kazi kwa urahisi kwa ajili ya Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.