Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Taska Restituta Mbogo (13 total)

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa mradi wa maji wa Ikorongo umeshindwa kutosheleza mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Mpanda; Kuna vijiji 20 vilivyoko Wilaya ya Nsimbo havina maji; kuna vijiji 13 na vitongoji viwili vilivyoko pale Mpanda Mjini havina maji; kuna vijiji tisa vilivyoko Wilaya ya Tanganyika, havina maji. Je, Serikali ni lini itachimba visima kwenye vijiji hivi na Kata hizi ili imtue ndoo mwanamke wa Mkoa wa Katavi?
Swali la pili; Mradi wa kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika ni programu ya muda mrefu ambayo haiwezi ikatekelezwa leo au kesho na wananchi na akinamama wa Mkoa wa Katavi wanaendelea kuteseka: Je, Waziri anaweza akatueleza hiyo programu ya kuvuta maji kutoka Ziwa Tanganyika itaanza lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kwamba mradi wa Ikorongo haujitoshelezi, ni kweli. Mradi wa Ikorongo unatoa lita milioni 3.5 kwa siku wakati mahitaji ya Mji wa Mpanda pekee ni lita milioni 11 kwa siku. Kwa hiyo, kuna upungufu mkubwa. Wakati tunasubiri huu mpango wa muda mrefu, tumeendelea na uchimbaji wa visima katika maeneo mbalimbali ya vijiji ambavyo amevitaja. Kwa mfano, tayari tumeshachimba visima katika Halmashauri ya Nsimbo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunaendelea kuchimba visima katika Halmashauri ya Mpimbwe na tayari tumechimba visima katika Halmashauri ya Mlele na Halmashauri ya Tanganyika, sasa hivi tunaendelea kufanya mazungumzo nao ili tuweze kupeleka fedha kwa ajili ya kuchimba visima ikiwa ni hatua ya muda mfupi.
Swali la pili; Mpango huu wa muda mrefu unaanza lini? Mpango huu unaanza katika mwaka wa fedha 2017/2018. Tumeshapokea maandiko tayari, kwa hiyo, katika bajeti inayokuja, tuombe tu Mheshimiwa Mbunge na wewe upitishe hiyo bajeti ili tuweze kuweka Mhandisi mshauri aweze kusanifu ili kuandaa Makabrasha ya Zabuni ya kutoa maji kutoka Karema katika Ziwa Tanganyika kuleta Mji wa Mpanda na kutoa maji upande wa Sumbawanga kuleta Mji wa Sumbawanga kutoka kule Kasanga.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ajili ya mahusiano ya ujirani mwema TANAPA Mkoani Katavi wamejitolea kuchimba visima kwenye vijiji vitatu ambavyo ni Kijiji cha Matandarani, Igongwe na Stalike lakini condition yao ni wanakijiji wachangie 30%. Gharama ya hivyo visima ni milioni 21, asilimia 30 itakuwa kama kwenye shilingi milioni saba, wanakijiji watatakiwa wachangie ili waweze kuchimbiwa hivyo visima vitatu. Je, TANAPA ili kudumisha mahusiano mema na Mkoa wa Katavi na ukizingatia kwamba kule mkoani kwetu vipato viko chini, wananchi hawana uwezo wa kuchangia hiyo shilingi milioni saba, inaonaje ikachukua hiyo gharama ikachimba bila kuwachangisha wananchi?Hilo swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, ni lini TANAPA itajenga hoteli ya nyota tatu katika Mkoa wangu wa Katavi ili tuweze kupata watalii kutoka nje na ndani ya nchi? Nauliza hivyo kwa sababu mkoa hauna hoteli ya nyota tatu ambayo inaweza kuwawezesha wageni kutoka nje kuja kutalii mkoa wetu na kuangalia huyo twiga mweupe ambaye hapatikani duniani kokote isipokuwa Mkoa wa Katavi?Ukizingatia kwamba sasa hivi uwanja wetu ni mzuri…
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza la uchangiaji kwenye utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema na nafikiri niweke vizuri tu hapa kwamba, TANAPA hawajitolei bali wanatekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu kwamba pale ambapo kuna wananchi wanaishi jirani na maeneo ya hifadhi, mahali ambako utalii unafanyika tunao wajibu wa kuweza kutekeleza miradi mbalimbali chini ya utaratibu wa ujirani mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango tulioweka wa kuchangia unawafanya wananchi waweze kwanza kushiriki moja kwa moja kwenye shughuli za uhifadhi lakini pia kujisikia kwamba na wenyewe ni sehemu ya uhifadhi lakini sehemu pia ya kufanya shughuli za maendeleo. Kwa hiyo, kwa kuwa utaratibu huu uko kwa mujibu wa kanuni, ikiwa Mheshimiwa Mbunge ana maoni bora zaidi ya haya aliyotuambia au ana namna bora zaidi ya kueleza kwa kirefu maoni hayo, basi anaweza kuyaleta Wizarani tukapitia utaratibu mzima wa utekelezaji wa miradi ya ujirani mwema.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, je, ni lini TANAPA itajenga hoteli ya nyota tatu Mkoani Katavi na kwa kweli anauliza kwamba kwa nini TANAPA wasijenge hoteli ya nyota tatu ili kuweza kuboresha shughuli za utalii Mkoani Katavi. Kwa ufupi tu ni kwamba, Serikali haijengi hoteli kwa ajili ya matumizi ya watalii au kwa ajili ya matumizi mengine yoyote kwenye sekta ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, jukumu la Serikali ni kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wawekezaji ambao wanatoka private sector kuweza kuwekeza kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, nimshauri tu Mheshimiwa Mbunge aungane na Serikali kuwashawishi wadau kutoka mahali popote pale waweze kuja kwenye Mkoa wa Katavi kuwekeza na kujenga hoteli si ya nyota tatu tu, hata kama wanaweza ya nyota nne, nyota tano, ili mradi kuwe na mazingira ambayo yatawawezesha watalii kuvutiwa na kuja kutalii wakiwa katika hali ambayo ni bora zaidi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa ajili ya usalama wa nchi kwa kawaida viwanja vya ndege vinatakiwa viendeshwe na Agency za Serikali ambazo ni TCAA na TAA pamoja na Taasisi ya Meteorological . Taasisi hii ya KADCO ni kampuni, sasa swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, Kampuni ya KADCO itaunganishwaje na TAA kama alivyoeleza kwenye majibu yake?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni lini ndege za Bombardier zitashuka Wilayani Mpanda, Mkoani Katavi maana tunazihitaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, katika jibu langu la msingi nimeeleza tu kwamba, KADCO ni Shirika la Umma ambalo linamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, siyo kitu cha ajabu kuunganisha KADCO na TAA kwa sababu zote zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, zote ni taasisi za Serikali na zikiunganishwa tutapata uongozi wa aina moja na bodi ya aina moja ambayo itarahisisha sana menejimenti ya viwanja vya ndege kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, tuko kwenye harakati za kupanua uwanja wa ndege wa eneo hilo. Kwa hiyo, tutakapopanua uwanja wa ndege wa eneo hilo Mheshimiwa Mbunge, ndege za Bombardier zitaanza kushuka. Tuna lengo la kuhakikisha kwamba viwanja vyetu vyote vya ndege vinaongezwa ubora wake na ukubwa ili ndege zote ambazo zina ukubwa wa kutosha ziweze kutua kwa ajili ya kuhudumia Watanzania. Ahsante.
MHE. TASKA R MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante naomba kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa matatizo ya Mkoa wa Geita yanafanana na matizo ya Mkoa wa Katavi. Mkoa wetu wa Katavi hauna Hospitali ya Mkoa na hauna pia Hospitali ya Rufaa.
Je, ni lini sasa Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi na kuleta Madaktari Bingwa wa magonjwa mbalimbali kama upasuaji wa macho, meno kwa sababu siku nyingine watu wanavimba ufizi wanashindwa kupasua? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mkoa wa Katavi nimeutembelea ikiwa ni sehemu ya Mikoa 12 ambayo nimetembelea ndani ya miezi minne tangu nimeteuliwa kuwa Naibu Waziri. Nimeiona changamoto hiyo katika Mkoa wa Katavi, lakini kama nilivyojibu katika swala langu la msingi ni kwamba sasa hivi Serikali imechukua majukumu ya kuendesha Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachokuomba Mheshimiwa Taska Mbogo na Wabunge wengine wa Mkoa wa Katavi ni kuendelea kuihimiza Serikali yetu ya Mkoa kuhakikisha kwamba wanatenga eneo na kuanza maandalizi ya awali na sisi kama Serikali tutaendelea kujipanga kuhakikisha kwamba tunajenga Hospitali ya Rufaa ya Katavi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninaomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa umeme wa gridi mpaka kufika Mkoa wa Katavi utachukua muda mrefu; na kwa kuwa umeme hautoshi Mkoani Katavi, lakini pia napenda kuishukuru Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uholanzi kwa ujenzi wa jenereta mbili na jenereta hizo zimeanza kufanya kazi kutoka tarehe 27 Mei, 2017 , lakini jenereta hizo hazitoshi.
Mheshimiwa Spika, umeme unaotakiwa Mkoa wa Katavi ni megawati tano, jenereta zinazalisha megawati 2.2. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza jenereta nyingine mbili kwa Mkoa wa Katavi? Kwa sababu mahali pa kuzifunga jenereta hizo tayaripameshajengwa, maana eneo la hizo jenereta limejengwa sehemu za kufunga jenereta nne, lakini Serikali pamoja na Serikali ya Uholanzi imefunga jenereta mbili, eneo hilo lipo. (Makofi)
Meshimiwa Spika, je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza jenereta mbili?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa jenereta hizi zinatumia mafuta ya dizeli na ni gharama zaidi, je, Serikali haioni kwamba matumizi ya jenereta kwa Mkoa wa Katavi ni gharama zaidi kuliko kufunga umeme wa gridi? Naomba kuwasilisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA NISHATI NA MADINI): Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa, maswali yake ni mazuri na kwa faida ya Mkoa wa Katavi ambao na mimi mwenyewe natoka kule siwezi kuahidi lakini niseme kwamba nitalifikisha hili ili waweze kuongeza jenereta nyingine mpya kuongeza umeme. Lakini pia haya masuala ni ya kiuchumi. Ipo historia kwamba matumizi ya umeme katika mkoa wetu, hasa katika masuala ya viwanda bado hatujawa na viwanda vingi, kwa hiyo umeme sehemu kubwa unatumika majumbani tu na taarifa iliyopo ni kwamba TANESCO imekuwa inatoa gharama kubwa zaidi kuliko makusanyo yanayofanywa kutokana na matumizi ya umeme, lakini suala hili tutalifikisha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili linalozungumzia dizeli. Ni kweli kabisa kwamba kutumia dizeli ni gharama kubwa kabisa na ndiyo maana sasa hivi Serikali nzima inataka kwenda kwa kutumia umeme ama wa gesi au wa maji, na ndiyo maana sasa Serikali imeshalitambua hili, inaleta umeme wa msongo mkubwa ambao sehemu kubwa utatumia uzalishaji kwa kutumia maji badala ya kutumia dizeli. Kwa hiyo, mawazo yako Mheshimiwa Mbunge ni mazuri na tayari Serikali imeshaanza kuyatekeleza.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Wabunge wa Viti Maalum ni Wabunge sawa na Wabunge wa Majimbo, hivyo basi, Serikali haioni kwamba kuwanyima Wabunge wa Viti Maalum kuhudhuria kwenye Kamati za Fedha inawasababisha wasielewe mipango ya fedha kwenye Halmashauri zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini basi hii sheria isiletwe humu Bungeni ikabadilishwa ili kuweka usawa na kuondoa ubaguzi wa jinsia kwa sababu kutomruhusu Mbunge wa Viti Maalum kuingia kwenye Kamati za Fedha ni ubaguzi wa jinsia ya mwanamke na mwanaume ambayo inaanzia kwenye sheria zetu za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, ni kweli kama alivyosema ni vigumu sana kujua kwa kina yale ambayo yamejadiliwa na kikao husika kama wewe siyo Mjumbe. Hiyo ni kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu kwa nini Serikali isilete Bungeni marekebisho ya sheria ili kusudi Wabunge wa Viti Maalum wawe Wajumbe, naomba tu nilipokee hili sasa kwa niaba ya Serikali ili tukalizungumze ndani ya Serikali kwa kuwa Vyama vya Siasa ambavyo viliwateua Wabunge wa Viti Maalum na kila Mbunge wa Viti Maalum amepangiwa Halmashauri fulani ya kuhudhuria vikao na kupiga kura. Basi nadhani hiyo inaweza ikawa ni mwanzo mzuri wa kuangalia ni namna gani tuweze kuleta marekebisho ya hiyo sheria. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kwa kuwa wapo watoto ambao wanamaliza elimu ya msingi hawajui kuandika wala kusoma. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kila mtoto wa Tanzania anapomaliza elimu ya msingi ambayo ni darasa la saba anajua kusoma na kuandika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa wapo watu wazima wenye umri na wazee labda umri kama wangu pia hawajui kusoma kutokana na mazingira labda waliyokuwa labda maeneo yao yalikuwa hayana shule. Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha elimu ya watu wazima iliyokuwepo hapo zamani miaka 1973 ili watu hawa waweze kusoma na kuandika?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbogo kwa maswali yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nisisitize tu kwamba Serikali imeendelea kutoa hamasa na kuwafuatilia walimu, lakini vilevile kuhakikisha kuwa watoto waweze kusoma na kuandika pale wanapokuwa hasa elimu ya msingi na hivyo kwa sasa mtoto inapofikia darasa la tatu ikigundulika hajui kusoma na kuandika imekuwa akipewa mpango maalum wa kumsaidia na kumuwezesha kuweza kumudu masomo yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya watu wazima nikubaliane naye kwamba kweli Tanzania bado tunalo kundi kubwa takribani 20% ambao hawajui kusoma na kuandika. Kuna programu mbalimbali ambazo zimekuwa zikiendelea kupitia elimu ya watu wazima ambapo wanapewa baadhi ya mafunzo ya kujitegemea, lakini vilevile nipende kusisitiza kwamba kila Mtanzania ambaye hajui kusoma na kuandika awe na kiu ya kuweza kujifunza kusoma na kuandika kwa sababu sasa elimu imeshakuwa karibu kila mahali hasa katika maeneo yetu tunayoishi.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mila na desturi za makabila yetu ya Tanzania zinaendelea kupotea kwa kasi kubwa; na kwa kuwa vijana wetu wameingia kwenye utandawazi wa kuiga mila za kigeni mpaka wanaiga mambo ambayo sio utamaduni wetu. Kwa mfano, kumekuwa na wimbi la vijana wa Tanzania kutaka mabadiliko ya ndoa za jinsia moja, mwanaume kwa mwanaume au mwanamke kwa mwanamke ambazo siyo desturi na mila zetu za Tanzania kama jinsi tunavyoishi na makabila yetu yalivyo. Je, ni lini Serikali itawatambua rasmi Machifu na Watemi ili waweze kutoa mchango wao kwenye jamii kurekebisha na kufundisha mila na desturi zetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa mikoa mingi ya Tanzania haina nyumba za makumbusho za kuhifadhi hizo kanzidata za mila na desturi za makabila tofauti. Je, ni lini Serikali itajenga nyumba za makumbusho kwenye mikoa yote ya Tanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Restituta Mbogo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ametaka kujua ni lini Serikali itawatambua rasmi Machifu pamoja na Watemi. Niseme kwamba si kwamba Serikali haiwatambui Machifu pamoja na Watemi ambao tunao na ndiyo maana katika shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali watu hawa wameendelea kualikwa ikiwepo shughuli ya Mwenge. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali inawatambua na itazidi kuwatambua Machifu na Watemi kwa sababu ni njia mojawapo ya kuendelea kuenzi na kudumisha mila pamoja na tamaduni zetu.
Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kujua kwamba ni lini Serikali itajenga maeneo ya makumbusho kwa ajili ya kuhifadhi mila na tamaduni. Kama ambavyo nimejibu katika swali langu la msingi kwamba sisi kama Serikali ni waratibu pamoja na wasimamizi wa sera na sheria zinazohusiana na masuala mazima ya utamaduni, wamiliki wakubwa wa utamaduni ni jamii kwa maana ya wananchi. Kwa hiyo, ni jukumu letu sisi sote kuhakikisha kwamba tunashirikiana pamoja na Serikali kujenga na kudumisha mila na tamaduni za Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pia kama ambavyo nimejibu kwenye jibu langu la msingi, nitoe wito kwa mashirika yote ya umma na ya kiserikali na watu binafsi kuhakikisha kwamba tunashirikiana kwa pamoja kudumisha mila pamoja na tamaduni ikiwepo suala ambalo ni muhimu sana la kujenga makumbusho kwa ajili ya kuhifadhi mila pamoja tamaduni zetu. Ahsante.

WAZIRI HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO:
Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kunipa fursa hii. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda tu niongeze kwamba wiki iliyopita nilipata bahati kubwa ya kuhudhuria Maadhimisho ya Kituo cha Kumbukumbu ya Utamaduni wa Kabila la Wasukuma huko Bujora, Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kilichonifurahisha sana ni ushiriki mkubwa wa Machifu wa Kisukuma, wote walikusanyika pale. Wana Umoja wao unaitwa Bubobatemi-Babusukuma. Waliweza hata kunipa cheo pale kuwa Manji Mkuu wa ngoma moja pale na ni cheo kikubwa sana hicho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka tu kusisitiza kwamba nafasi ya Machifu katika kudumisha utamaduni wa Tanzania tunaiona. Nadhani hili suala tutaendelea kuliangalia kwa umakini na kulileta lipate mjadala mpana tuweze kuiona nafasi yao kabisa ambayo itaweza kujikita hata kisheria.
Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kusema kwamba Waheshimiwa Wabunge wametoa mchango mkubwa sana katika hili eneo hasa tukizingatia ukuzaji wa utamaduni Mkoa wa Songea, Mheshimiwa Eng. Stella Manyanya, Tamasha la Utalii Nyasa; Mheshimiwa Dkt. Ndumbaro, Majimaji Selebuka; Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson ambaye kila mwaka naye anaazimisha ngoma za kiutamaduni Mkoa wa Mbeya. Ningeoomba Waheshimiwa Wabunge wote tuingie katika kuhamasisha utamaduni katika maeneo yetu. (Makofi)
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Kilimo, ninayo maswali maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mfumo wa Uagizaji wa Mbolea kwa pamoja unatumika tu kwa mbolea za DAP na UREA. Je, ni kwa nini sasa Serikali isitumie mfumo huu kwa kuagiza mbolea nyingine za NPK, CAN, SA na pembejeo nyingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Katavi ni umbali wa kama kilimita 1,500 kutoka Dar es Salaam, kwa hiyo, mbolea inaposafirishwa na magari inakuwa na bei juu zaidi.

Ni kwa nini sasa Serikali isiweke utaratibu wa kusafirisha mbolea hiyo kwa njia ya treni ili mkulima wa Mkoa wa Katavi apate bei nafuu ya mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Taska Mbogo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Taska Mbogo alitaka kujua kwa nini Serikali tusitumie Mfumo huu wa Uagizaji wa Mbolea kwa Pamoja (BPS) kwa mbolea zingine kama NPK, CAN na SA. Kwanza, mfumo huu tumeanza kuutumia mwaka jana na umeonyesha matokeo mazuri. Tusingeweza kuingiza mbolea zote kwa wakati mmoja lakini baada ya mafanikio tuliyoyaona katika mfumo huu, mwaka huu tumeshaanza kuutumia mfumo huu kwa ajili ya mbolea ya NPK kwa wakulima wa tumbaku na sasa tutaendelea na utaratibu ili kuingiza mbolea tajwa, viuatilifu na pembejeo zingine katika mfumo wa BPS ili kurahisisha upatikanaji wa mbolea kwa haraka na bei nafuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, anasema kwa sababu Mkoa wa Katavi uko mbali na Dar es Salaam, ni vizuri tungesafirisha mbolea hizi kwa njia ya treni ili kupunguza gharama za usafiri. Tunachukua mawazo haya na tulishayafanyia kazi, tangu mwaka jana kama nilivyosema hii mbolea ya NPK tuliisafirisha kwa kutumia treni na gharama za usafiri zilishuka na mbolea hii kufika kwa wakulima kwa wakati. Mawazo yake tunayachukua ili tuyahamishie katika mazao mengine. Kama nilivyojibu kwenye swali langu la msingi, tayari tumeshalielekeza Shirika letu la Reli Tanzania ili kutoa kipaumbele kwenye kusafirisha bidhaa ya mbolea ili kushusha gharama za usafiri.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba wapo Watanzania zaidi ya milioni moja wanaishi nje ya Tanzania kama diaspora. Sheria ya Citizenship ya Tanzania inakataza uraia pacha. Je, ni lini Serikali ya Tanzania itabadilisha sheria hiyo na kuruhusu uraia pacha? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2014 Serikali ya Tanzania ilitoa uraia kwa wageni waliokuwa wanaishi kama wakimbizi 150,000 nchini Tanzania. Je, Serikali haioni kwamba kutoruhusu uraia pacha tunawanyima haki Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuja kushiriki na kujenga nchi yao na kukaa na ndugu zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo kwa swali lake zuri la msingi lakini na maswali yake mazuri mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza linahusu kubadilisha sheria ili kuruhusu uraia pacha. Suala la uraia pacha ni la Kikatiba, kwa hiyo kabla hatujaongelea sheria tunapaswa kwanza tukaongelee Katiba. Mchakato wa kubadilisha Katiba bado unaendelea, pale Katiba itakapobadilika na kuruhusu uraia pacha ndipo tutakwenda kurekebisha Sheria ya Uraia Na.6 ya mwaka 1995 ili kuongeza kipengele cha kuruhusu uraia pacha.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anasema kwamba hatuoni kwamba kuzuia uraia pacha tunanyima haki. Watanzania hawa ambao wako nje tunaowaita diaspora, bado wanaendelea kufurahia haki nyingine ambazo zimetolewa hapa Tanzania ikiwemo haki ya kuwekeza kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya mwaka 1997 na haki nyingine ambazo wangeweza kuzipata.

Kwa hiyo, tunashauri kwamba Watanzania hawa kwa hivi sasa na ambao wamefanya kazi nzuri sana kama ambavyo nimeeleza, ikiwemo kuleta misaada mingi sana katika huduma za afya na baadhi ya Majimbo kama Chakechake, Kondoa, Makunduchi, Kivungwe pamoja na Namanyere yamefaidika, bado tunaendelea kushirikiana nao na wanaendelea kufurahia haki zao kama diaspora.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili y nyongeza, swali la kwanza natambua juhudi za Serikali zinazofanywa kuitangaza Kiswahili ili kiweze kutumika duniani mpaka kufikia kwamba Kiswahili sasa ni lugha rasmi inayotumiwa SADC, hatua hizo zinazofanya Serikali ni nzuri lakini ninalo swali moja.

Je, kwa kipindi hiki TBC kama TBC ina mkakati gani wa kuwa na translate kwenye vipindi vyake anaye translate Kiswahili kwenda kingereza, na kingerez akwenda Kiswahili wakati anatangaza taarifa zake za habari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni ukweli usiopingika kwamba kuna television na redio za TBC. Je, TBC kama TBC ina mkakati gani wa kukuza lugha hii duniani kwa kuongeza masafa yake nikiwa na maana frequency ziweze kusikika kwenye nchin mbalimbali duniani?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa maswali mazuri ya nyongeza, lakini nikianza na swali lake la kwanza ametaka kujua kwamba TBC tuna mkakati gani kwa kuwa na mtafusiri kutoka kwenye lugha ya Kiswahili kwenda kwenye lugha ya kingereza. Kama ambavyo nimejibu kwenye jibu kangu la msingi kwamba kwa sasa hivi tunavyo vipindi mbalimbali ambavyo vinatangazwa kwa lugha. Kwa hiyo, naamini kwamba kupitia hivyo vipindi watu wa mataifa mengine kwa maana ya nchi za nje wanaweza kupata kila kitu ambacho kinaendelea ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija pia kwenye swali lake la pili anataka kujua kwamba tuna mkakati gani wa kukuza lugha ya ksiwahili duniani. Mimi niseme kwamba Mheshimiwa Taska Mbogo anatambua namna gani ambavyo Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa mstari wa mbele katika kukuza Kiswahili, vilevile tunamshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa sababu ndiye ambaye amewezesha sasa hivi kiswahili kinatumika kwenye mikutano ya SADC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme kwamba sisi kama Shirika la Utangazaji la Taifa mkakati wetu kuhakikisha ya kwamba tunakuza kiswahili na ndiyo maana tumekipa kiswahili kipaumbele katika vipindi vyetu, vilevile tumetengeneza apps mbalimbali ambazo zinapatikana ndani pamoja na nje ya nchi. Kwa hiyo, vipindi vyote ambavyo vinatangazwa ndani ya Tanzania, vilevile kwa kupitia app mbalimbali kwa maana ya mtandao wanapata taarifa mbalimbali ambazo zinatokea katika nchi yetu ya Tanzania, ahsante.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa ugonjwa wa sickle cell unatokana na mtoto kurithi cells kutoka kwa baba na mama yake, wazazi wake wote wawili wanakuwa na cells ambazo ziko half. Sasa mtoto anapozaliwa anakuwa amerithi zile cells ndiyo maana anazaliwa na huo ugonjwa.

Je, ili kuzuia hili tatizo Serikali ina mkakati gani wa kuwapima watoto wanapozaliwa kwenye vituo vya afya na katika hospitalini mara tu wanapozaliwa iwapime ili wagundulike kwamba wana ugonjwa wa sickle cell ili kuepusha vifo vya watoto kwa sababu mara nyingi wanapogundulika wanakuwa wameshakuwa watu wazima na wengi huwa wanapoteza maisha, hasa vijijini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa commitment kwamba Serikali inaandaa mwongozo wa kutoa msamaha wa matibabu bure kwa familia ambazo hazijiwezi kupitia kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii, sasa basi, yako magonjwa kama UKIMWI na TB watu hawahakikiwi, wanapata matibabu bure.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa bure matibabu ya sickle cell bila kuhakikiwa kama ilivyo magonjwa ya UKIMWI na TB?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge Restituta Mbogo kwa kuwa ni mfuatiliaji wa karibu wa magonjwa haya yasiyoambukiza na hususani ugonjwa huu wa seli mundu.

Mheshimiwa Spika, hoja yake inahusiana na suala la upimaji wa watoto wanapozaliwa. Ni kweli ugonjwa huu huja kwa njia ya pale wazazi wanapokuwa na vinasaba ambavyo vinahamishwa katika kipindi cha ujauzito kuja kwa watoto pale wazazi wanapokuwa na vinasaba hivi vya ugonjwa huu wa seli mundu, genetic transfer. Kwa hiyo, katika nchi ambazo zimeendelea, watoto ambao wana Ugonjwa huu wa seli mundu wanaweza wakabainika kwa njia mbili; njia ya kwanza ni kupima ujauzito wakati mtoto akiwa bado tumboni kwa kupitia katika maji yaliyopo katika mfuko wa uzazi, unaweza ukabaini kwamba mtoto anaweza akazaliwa na ugonjwa wa seli mundu. Lakini njia ya pili, baada ya mtoto kuzaliwa akipimwa anaweza akabainika kama ana ugonjwa huu wa seli mundu.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi; Tanzania na nchi nyingi za Afrika ugonjwa huu ni mkubwa na wako wagonjwa wengi na sisi kama Serikali, pamoja na kazi nzuri ambayo imefanyika pale Hospitali ya Muhimbili kupitia programu ile ambayo inaongozwa na madaktari mahiri ya Profesa Julie Makani, wamekuwa wanatoa msaada mkubwa sana kwa wagonjwa hawa wa seli mundu. Sasa sisi kama Serikali tumeamua sasa tunataka tuje na mpango wa kitaifa ambao utasimamia matibabu haya ya seli mundu na ndiyo maana tumesema kwamba ifikapo Novemba programu hii tutakuwa tumeianzisha rasmi na mkakati wa upimaji unaweza ukawa ni moja ya mkakati huo ambao tutaweza kuufanya kuhakikisha kwamba tunaubaini ugonjwa huu katika hatua za awali na kuweza kuwatibu hawa wagonjwa vizuri zaidi na kwa ufasaha zaidi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili linahusiana na suala la uhakiki wa wagonjwa. Ili uweze kumbaini mgonjwa wa seli mundu ni lazima kwanza apimwe na kuthibitishwa. Katika utaratibu ambao tunao sasa hivi hizo njia ambazo nimezisema hapo awali hatuzifanyi, kwa hiyo, mara nyingi unakuta mgonjwa anakwenda akiwa na tatizo la upungufu wa damu au akiwa na zile crisses, maumivu makali ambayo anayapata kutokana na ugonjwa huu, na akishathibitika kwamba ni mgonjwa wa sickle cell anapata matibabu.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa hatuna mfumo wa matibabu bure kwa wagonjwa wa seli mundu na hili niseme tu kwamba pale anapobainika mgonjwa kwamba hawezi kugharamia matibabu, kwa utaratibu wa sasa tuna utaratibu wa misamaha na utaratibu ni ule ambao nimeusema katika jibu langu la msingi, wanatakiwa kupita katika Serikali zao za Mtaa au Serikali za Vijiji kupata barua, wakija kwa Maafisa Ustawi wa Jamii katika ngazi ya hospitali watapata matibabu bure. Lakini katika mpango ambao tunataka kuanzisha mwezi Novemba tutaweka utaratibu mzuri zaidi wa matibabu kwa wagonjwa hawa wa seli mundu.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mkoa wa Katavi unaongoza kwa vifo vya watoto wachanga. Takwimu tu za mwaka 2018 zinaonesha kwamba Mkoa wa Katavi ulipoteza watoto wachanga 581. Hii ilisababishwa na ukosefu wa vifaa bora wakati akina mama wakijifungua lakini hata vifaa hivyo vikiwepo kwenye vituo hivyo vya afya haviwezi kufanya kazi kwa sababu havina umeme. Je, Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini pamoja na WIzara ya Afya ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba vituo vile vya afya ambavyo havina umeme Mkoani Katavi vinapata umeme ili viweze kutumia vifaa vya kisasa kuokoa vifo vya mama na motto? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wauguzi wengi Mkoani Katavi hawana mafunzo, Serikali kupitia Wizara ya Afya ina mkakati gani wa kutafuta wadau wa afya ya mama na mtoto ili tuweze kutokomeza vifo hivi Mkoani Katavi? (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya katika majibu ya swali lake la msingi. Pia niendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali kuhusu upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Katavi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Mkoa wa Katavi baadhi ya vijiji havijaanza kufikiwa na mkandarasi. Nimpe taarifa tu Mheshimiwa Mbunge maeneo yote ambayo ameyauliza Mheshimiwa Mbunge mkandarasi ameshaanza kwenda site. Katika Mkoa wa Katavi kuna vijiji 149 vitapelekewa umeme. Sasa hivi mkandarasi ameshawasha Mchakamchaka lakini anaendelea na Kaparara na katika vijiji vingine saba atawasha kuanzia wiki inayokuja. Kwa hiyo, wananchi wa Katavi wategemee kupata umeme katika maeneo yote. Kesho kutwa watawasha kwenye Mgodi wa Society kwa Mheshimiwa Kapufi. Kwa hiyo, mkandarasi yuko site vijiji vyote vitapatiwa umeme kwenye kipindi hiki cha Julai mpaka Desemba mwaka huu. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili madogo ya nyongeza ambapo sehemu ya swali la kwanza ameshalijibu Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Niendelee na kipengele kingine ambacho kilikuwa kimebaki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba idadi ya vifo vya watoto katika Mkoa wa Katavi ni vingi sana na hili ni kweli lakini halitokani na ukosefu wa huduma za afya kwa watoto wachanga. Mkoa wa Katavi una changamoto kubwa sana ya mimba za utotoni. Wastani wa Kitaifa sasa hivi tuna asilimia 27 ya watoto kati ya miaka 15 mpaka 19 aidha wana watoto au wana mimba. Katika mikoa ambayo inaongoza ndani ya nchi yetu ni pamoja na Katavi, umri wa kupata ujauzito bado ni mdogo sana na kwa kuwa bado hawajafikia ukomavu uliotosha, hili nalo linachangia sana katika vifo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na masuala ya mafunzo, Serikali inaendelea kujipanga na imekuwa inaweka utaratibu wa mafunzo endelevu kwa watoa huduma wake wa afya katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na mafunzo kwa ajili ya huduma ya mama na motto. Katika Mkoa wa Katavi, Serikali imekuwa inashirikiana kwa karibu sana na wadau.