Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Najma Murtaza Giga (14 total)

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na
majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, bado nina swali moja la nyongeza
ambalo linahusiana na hawa watoto wadogo chini ya umri wa miaka 18 kutumia
huu ulevi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile nilisema sheria hii ya mwaka 1969 ni ya
muda mrefu sasa ni lini Serikali itaweza kujipanga na kuleta ili tuweze kufanyia
marekebisho sheria hii ili tuwabane na hawa watoto wadogo walio chini ya umri
wa miaka 18 kutumia ulevi?
NAIBUWAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli. Sasa hivi kuna tabia kwenye baadhi ya Mikoa,
utakuta watoto wadogo asubuhi au wakati wa weekend wananyweshwa pombe. Jambo hili kwanza kimsingi ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu kwanza
na haki za watoto ambapo mtoto mdogo anatakiwa kuendelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuchukue huu ushauri kwa
sababu sheria hii ni ya muda mrefu sana na kutokana na maoni ya wadau
mbalimbali tutaangalia jinsi gani tutafanya turekebishe, lengo kubwa ni
kuhakikisha kwamba Taifa letu linakuwa Taifa imara kwa sababu lazima tuwalee
hawa watoto kwa kizazi kijacho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba tuchukue ushauri.
Itakapoonekana pale ina haja, basi wadau mbalimbali wataleta maoni yao na
sisi Wabunge ni miongoni mwa wadau wa kutengeneza hizo sheria. Kwa hiyo, hili
nadhani tutalifanyia kazi vema tuweze kulifanikisha.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa vile suala la elimu ya juu ni suala la Muungano na kuna watu kama sisi yaani kama mimi, wazazi, hasa wa kike tulio majumbani, huwa hatuwezi kwenda directly kusoma kwenye vyuo vikuu kwa kujiendeleza. Kwa mfano kama mimi mwenyewe nimesoma distance learning kwenye Chuo cha ICM cha Uingereza.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa hili si tatizo kwa upande wa Jamhuri ya Muungano, wenzetu hawa ambao wamesoma distance learning wanaajiriwa kwenye taasisi za muungano na Serikali kwa ujumla lakini tatizo lipo kwa upande wa Zanzibar; sisi ambao tumesoma distance learning, hasa wanawake tunaoishi majumbani tunakuwa hatuwezi kwenda vyuoni, tunaonekana kwamba vile vyeti vyetu vya distance learning si chochote isipokuwa wale ambao wamekwenda direct kusoma wanakubaliwa.
Sasa je, kwa nini Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hazikai pamoja zikakubaliana mfumo ulio bora ili na sisi wazazi hasa wa kike wa Zanzibar tuweze kujiendeleza kimasomo kupitia distance learning?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Niseme tu kwamba, ni kweli suala la elimu ya juu ni suala la muungano na taratibu za kujiunga na vyuo na kuhakiki watu wanaosoma nje zinafanywa na TCU. Lakini pia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina taratibu zake za ajira na ndiyo maana kabla ya kuajiri wana taratibu zao za kuhakiki vyeti. Kwa hiyo, niseme kwamba na mimi nilipokee ili kama sehemu ya masuala ambayo ni ya muungano tunakaa tunayajadili na lenyewe tuangalie kwa pamoja na Waziri mwenzangu wa Elimu wa Zanzibar ili tuangalie namna ya kulipatia ufumbuzi. Nashukuru sana.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu aliyoyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Waziri bado nina swali moja la nyongeza. Je, kwa nini Serikali haioni umuhimu wa kutuletea taarifa zote pale ambapo changamoto za Muungano zinapopatiwa ufumbuzi ndani ya Bunge hili ili sisi Wawakilishi wa Wananchi tuweze kumsaidia Mheshimiwa Waziri kuzifikisha kwa wananchi kwa wepesi zaidi? (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais(Muungano na Mazingira) napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga ambaye ni nyara ya CCM na tegemeo kubwa la CCM kule Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hilo ni zuri kwamba iko haja ya kuleta taarifa zote kwa namna ambavyo Ofisi ya Makamu wa Rais wanavyoweza kupitia Kamati yetu ya pamoja ya kero za Muungano hapa Bungeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali yetu imekuwa ikitoa taarifa hizi kila wakati kama nilivyosema kwenye majibu yetu ya msingi. Zile taarifa ambazo zinatolewa kwenye maeneo hayo ya siku ya Muungano kwenye televisheni Mheshimiwa Waziri wetu tunatekeleza amekuwa akiongelea mambo haya, hata hapa Bungeni ambapo anasema ni vema tukazileta. Naomba nimhakikishie hizi Hansard hizi zimesheheni taarifa mbalimbali kuhusu namna ambavyo Serikali imekuwa ikitatua kero za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapa, Mheshimiwa Najma nitakupatia hizi Hansard hizi na tayari nimeonesha maeneo yale ili usipate usumbufu ili uweze kuona namna ambavyo Serikali yeu inavyotoa taarifa hiyo. (Makofi)
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa vile tafiti zimeonesha moja kwa moja kwamba zinakinzana, kuna zinazokubali na zinazokataa na kuonesha na sababu zake.

Sasa je, kwanini Serikali haijikiti zaidi katika kutafuta adhabu mbadala yenye tija zaidi na kuliacha suala la viboko mikononi mwa wazazi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kama wewe mwenyewe ulivyosema, suala la viboko ni suala vilevile la mila. Hata sisi Serikali tukisema leo hatutaruhusu viboko, nina hakika wazazi wengi wataendelea kuwachapa wanafunzi na hapa Bungeni nina hakika tukiwauliza wazazi walioko huku kwamba ni wangapi wanachapa viboko, inawezekana wote tukakuta wanafanya hivyo.

Sasa Serikali kama nilivyosema, kwa sababu adhabu inayotumika mashuleni sio viboko peke yake, hata hivyo kama nilivyosema tutaendelea kutumia viboko kwa njia ambayo haina madhara. Tukifuata ule waraka kwa kweli adhabu ya viboko wala hata isingetolewa kwa kiasi kikubwa.
MHE. NAJMA M. GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa vile spices yaani viungo vya vyakula mbalimbali ni vinaonesha kwamba vina afya zaidi katika miili ya binadamu. Sasa kwa nini Serikali haitumi wataalam wake wakaja Zanzibar kujifunza faida za viungo hizo ili Watanzania wengine walioko Bara ambao hawajui kama vile Wasukuma, Wamasai na makabila mengine waweze kujua na kutumia na kupata afya njema? (Makofi)
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wake tumeupokea, ni kweli hizi spices zina faida nyingi ikiwemo faida kwa upande afya kwa akinababa na akinamama. Ni ushauri mzuri kwa sababu tunatafuta masoko ya nje, lakini pia masoko ya ndani lazima nayo tuyatumie.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe wito kwa wanaume wenzangu, ukiangalia spices kuna faida nyingi sana kwa upande wa wanaume na ni namna mzuri ya kukuza soko la ndani. Kwa hiyo, ushauri wa Mheshimiwa Najma tumeuchukua.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na nashukuru Serikali kwa kukubali na kuelewa kwamba suala hili linatambulika na lipo.

Mheshimiwa Spika, kabla sijauliza maswali yangu mawili ya nyongeza, nataka ieleweke kwamba suala hili kama ilivyo ushoga yaani Lesbianism ni masuala ya usiri sana, kwa hiyo, kuyajua kwake siyo rahisi sana. Kwa hiyo, kwanza ningeomba Serikali isicheleweshe jambo hili la utafiti ili tuweze kujua kiwango cha athari hizo.

Mheshimiwa Spika, pia nataka ieleweke na itambulike kwamba kunyamaza kwetu kimya sasa hivi na kuogopa mambo haya miaka 50 ijayo ndani ya Bunge hili badala ya kujadili maandeleo na maadili mema ya Kitanzania watakuja kujadili namna gani ya kupitisha ndoa ya jinsia moja.

Mheshimiwa Spika, sasa narudi kwenye maswali yangu ya nyongeza. Swali la kwanza, nashukuru Serikali imeona umuhimu wa kutoa elimu pamoja na kwamba kuna sheria ambazo zinadhibiti suala hilo na baada ya utafiti wamesema pia watafanya marekebisho ya sheria. Swali langu lipo hapa, je, wakati tunaendelea kufanya utafiti huo, kwa nini sasa Serikali isishirikiane Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya kuona namna gani bora wanaweka mitaala katika shule zetu na kuonyesha madhara na athari ya mambo haya ambayo ni kinyume cha maadili ya Tanzania ili wanafunzi wetu ambao wanasoma waanze kujengeka na misingi ya maadali na kuachana na mambo haya popote watakapoyaona?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba tuna wanazuoni wengi sana katika Taifa hili wa dini mbalimbali, kwa nini Serikali sasa hakai nao na ikawataka watoe mahubiri ya kukataza masuala hayo ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza badala ya mambo mengine ambapo haya hawajayatilia mkazo? Maswali yangu ni hayo.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Najma Giga ambaye ameongea kwa uchungu sana.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ameuliza kwa nini Wizara ya Afya isikae pamoja na Wizara ya Elimu kuangalia mitaala ili masuala haya ya maadili yaweze kufundishwa katika shule mbalimbali. Tunapokea ushauri wake na sisi kama Serikali tutaenda kuufanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameuliza kwa nini tusiwatake wanazuoni nao wakatoa mahubiri kuhusiana na suala hili. Moja ya taasisi ambayo imekuwa inatujenga katika maadili mema ni pamoja na taasisi zetu za kidini. Kwa hiyo, naamini nao wanatusikiliza kupitia Bunge lako hili Tukufu na wao tuwaombe wachukue majukumu yao ya msingi kuhakikisha kwamba wanahubiri maadili mema ya kitaifa vilevile wanawajenga waumini wao katika maadili mema yanayozingatia misingi yetu ya maadili ya kitaifa. Kwa hiyo, sisi kama Serikali hatuwezi kusema taasisi za dini zifanye lakini taasisi za kidini nazo zina wajibu kuhakikisha kwamba zinajenga waumini wao na Watanzania katika msingi ya maadili mema.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nishukuru na kuipongeza sana Serikali kwa jitihada inazozichukua katika kulipoteza hili suala baya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza, la kwanza, mwaka jana nilizungumza hapa kwamba iwapo elimu tosha itatolewa basi ripoti hizi zitazidi. Kweli Mheshimiwa Waziri amethibitisha, hivyo nawapongeza sana kwa hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nachotaka kujua hii idadi kubwa ambayo imeongezeka baada ya wananchi kuhamasika na kutoa ripoti, je, ni wangapi kati ya hao wameweza kufikishwa kwenye vyombo vya sheria na wangapi wametiwa hatiani na kuchukuliwa hatua zinazostahiki? Siyo lazima mnijibu sasa hivi lakini majibu nayataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunajua kabisa vitendo hivi vinafanywa miongoni mwa jamii tunazoishi, ni miongoni mwa wanaume tunaoishi nao wakiwemo babu zetu, baba zetu, waume zetu, wajomba zetu na wengine wanaofanana na hao. Kwa nini Serikali haiji na mpango mbadala wa kutoa ruhusa kwenye jamii ili kuwatambua hawa watu ambao wanajulikana wana vitendo hivi kama ambavyo wanatambuliwa wabakaji, wezi, wavuta unga na wavuta bangi; ili jamii yetu sasa iweze kuwajua na wazazi pamoja na watoto wetu waweze kujitenga na watu hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, matukio haya ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa yanafanywa na watu ambao wako karibu na familia na mara nyingi inakuwa ndani ya familia. Sisi kama Wizara tumeendelea kuelimisha jamii na tunawashukuru sana wenzetu wa Jeshi la Polisi pamoja na Idara ya Mahakama, wamekuwa wanatoa ushirikiano mkubwa sana. Matukio mengi yanashindwa kufika mbali kwa sababu ushirikiano umekuwa ni mdogo ndani ya familia kwenda kutoa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hapa sina takwimu ambazo zinaonesha matukio ni mangapi na kiasi gani yamehukumiwa, lakini kwa taarifa chache ambazo ninazo, ni matuko machache sana ambayo yanafika mwisho kwa sababu tu familia zimekuwa hazitoi ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na Idara ya Mahakama ili matukio haya yaweze kufika mwisho. Kwa hiyo, nitoe rai kwa jamii kutomalizana na haya matukio ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto majumbani na badala yake waruhusu mkondo wa sheria uweze kufika mwisho.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili, katika nchi ambazo zimeendelea, kuna kitu kinaitwa Sexual Offender Register. Wale watu ambao wamehukumiwa kutokana na makosa haya ya ukatili wa kijinsia wanatambulika wapi wanakaa, wapi wanafanya kazi na akihamia sehemu mpya watu wote wanaweza wakamfahamu. Kwa hiyo, kwa sasa Serikali hatuna utaratibu huo, lakini ni wazo ambalo tunaweza tukalipokea na kuweza kuliangalia ni jinsi gani ya kulifanyia kazi.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi kwa vile suala la elimu kwa ujumla wake siyo suala la muungano na kwamba Baraza la Taifa la Mitihani pamoja na elimu ya juu ndiyo vya muungano. Sasa swali langu liko hapa Sera za elimu pamoja na mitaala kwa vyovyote itakuwa ni tofauti baina ya Zanzibar na Tanzania Bara.

Sasa kwa nini Serikali zetu mbili kwa lengo la kuimarisha elimu Tanzania zisikae pamoja zikatengeneza sera ya elimu na mitaala inayofanana ili kuinusuru Zanzibar kila mara kutokea kumi za mwisho? Ahsante; dhamira ni kuimarisha muungano.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anashauri kwamba Serikali zetu mbili zikutane na kujaribu kukaa ili kuangalia uwezekano wa mitaala yetu iweze kufanana. Ni wazo ametoa sio wazo baya kwa sababu ni nchi moja tutaenda kuliangalia sio kitu ambacho hakiwezekani.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwanza niipongeze Serikali kwa jitihada inazochukua katika kupiga vita ukatili wa watoto kwa suala la ubakaji. Hata hivyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza litalenga kwenye majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na tafiti ambyao amefanya na kututaka sisi sasa Wabunge pamoja na wananchi kwa ujumla kuweza kusaidia katika kutatua changamoto hizi.

Swali langu liko kwamba, je, ninyi kama Serikali mmejipangaje kuhakikisha kwamba vitengo vyote vinavyoshughulikia masuala ya sheria na kutoa haki vinashirikiana kikamilifu ili kuweza kutokomeza masuala haya ambayo mmeyatafiti?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusiana na Sheria Namba 21 ya Mtoto ya mwaka 2009. Sheria hii imeweka wajibu na jukumu la wazazi ama walezi kuweza kuwalinda watoto dhidi ya ukatili ikiwemo hili la ubakaji.

Je, mmekwama wapi katika kutekeleza sheria hii kiasi kwamba tunaona hakuna mzazi au mlezi anayeweza kuchukuliwa hatua pale ambapo mtoto anapatikana na makosa haya tukizingatia ndoa zinavunjika kwa wingi na watoto wanatelekezwa na inasababisha kufanyiwa vitendo hivyo vya ukatili, lakini pia wale wazazi ambao wanabaki, akina baba wanaweza kufanya vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto wao wenyewe. Je, Serikali inasemaje kuhusiana na hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mbunge, Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza lilikuwa linasema kwamba, je, Serikali ina mpango gani au je, kuna jitihada gani nyingine ambazo zimechukuliwa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba, tunatokomeza vitendo hivi. Kama Serikali tumechukua jitihada nyingi na tumechukua jitihada mbalimbali, lakini bado tunaendelea kuchukua jitihada ya kwanza ikiwemo ya kuendeleza kutoa elimu kwa jamii kwa sababu, tunaamini jamii ikipata elimu ya kutosha kwenye masuala haya maana yake masuala haya yanapungua au yatamalizika moja kwa moja. kwa hiyo, kama Serikali tumeanza kutoa taaluma kwanza kupitia kwenye madawati ya kijinsia ambayo mara nyingi yapo katika Jeshi la Polisi, tunayatumia yale kutoa taaluma hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tunao hawa para legals, wasaidizi wetu wa sheria ambao wako huko, wanatusaidia kuipa jamii taaluma. Pia tunavitumia vyombo vya habari kuhakikisha kwamba, taaluma inafika kwa jamii, lakini kizuri zaidi tunaenda kutengeneza mazingira ya kuipa nguvu sheria hii Namba 21 ya mwaka 2009 ili kuhakikisha kwamba, sheria inafuatwa na wananchi kwa kiasi kikubwa jamii inapungukiwa na matendo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine la pili ameuliza kwamba, sheria hii inakwama wapi? Naomba pia kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati tunaipitia sheria hii tumegundua kwamba, sheria hii ipo kimadai zaidi rather than kijinai. Sasa ukitazama unakuta kwamba, watu wanaweza wakafanya vitendo hivi wakitegemea kwamba, wao watafunguliwa kesi zaidi za madai na kwa sababu, madai si analipa. Kwa hiyo, sasa unakuta haiko kijinai zaidi. Kwa hiyo, unakuta sheria ndio maana unafika wakati utendaji wake wa kazi unakuwa haupo vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine ni ugumu wa wananchi kwenda kutoa ushahidi, ugumu wa mashahidi. Ukimchukua mtu akitoa ushahidi huko nyumbani ukikaa naye atatoa ushahidi vizuri tu, tena atatoa ushahidi maana yake ambao uko evident, lakini kesho twende mahakamani ndio inakuwa ngumu. Sasa na mahakama nayo ikiwa siku mbili, tatu, mara nne tano umeitwa hujaenda kutoa ushahidi maana yake mahakama inatoa uamuzi kwa upande mmoja. Kwa hiyo, upo ugumu kwenye utoaji wa ushahidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine sasa wanafamilia, wanamalizana tu kienyeji. Jambo limetokea kwa sababu, baba mkubwa, baba mdogo wanamalizana huko mwisho wa siku huku sheria inakuwa haipewi nguvu. Nakushukuru.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nashukuru Serikali kwa hatua iliyofikia katika kurekebisha masuala ya sera na mitaala kwa pande mbilli za Muungano, hata hivyo na maswali mawili madogo sana ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, muda mrefu sana Baraza la Mitihani lilikuwa likiwasiliana moja kwa moja na vituo vya mitihani vya Zanzibar na mara nyingi Wizara ya Elimu bila kuwa na taarifa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunda chombo maalumu cha kisheria ambacho kinatambulika ili kuweza kuunganisha Wizara ya Elimu ya Muungano na Wizara ya Elimu ya Zanzibar?

Mheshimiwa Spika swali langu la pili ni kuhusu elimu ya juu, katika Bunge la Kumi na Moja niliuliza na nikaambiwa linafanyiwa kazi kuhusu vyuo vikuu huria ambapo vilevile vyuo ambavyo vinatumika hapa na kutambulika na NACTE wale watu ambao wamefanya mitihani kupitia vyuo hivyo wanakubalika kufanya kazi Tanzania Bara na pia
wanatambulika kwamba wamesoma na vyeti vyao vinatambulika lakini kwa Zanzibar havitambuliki. Je, suala hili limefikia wapi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Giga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ni Taasisi ya Muungano ambayo inaendesha mitihani hapa nchini. Baraza la Mitihani lina muundo wa namna ya kuendesha shughuli zake; tunakuwa na Kamati za Mitihani ngazi ya Taifa, Mikoa na Wilaya. Kamati hizi ndizo ambazo zinafanya ule mtiririko wa mawasiliano na mahusiano katika uendeshaji wa shughuli za Baraza la Mitihani. Kwa hiyo, kimsingi vyombo vipo, kwa kutumia Kamati hizi; ndizo ambazo zinaratibu pamoja na kuendesha mitihani kote nchini ikiwemo Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.

Mheshimiwa Spika, Baraza la Mitihani lina watumishi kule Zanzibar na vilevile tuna ofisi pale Zanzibar katika jengo lile la Shirika la Bima Zanzibar. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Baraza la Mitihani limejipanga vizuri na namna bora ya mawasiliano pamoja na co-ordination ni kama hivyo nilivyoeleza.

Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili, kwamba kuna vyuo ambavyo havitambuliwi na NACTE; naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vyuo vyote vya elimu ya kati ambavyo vinahusika na masuala haya ya NACTE vimesajiliwa na NACTE na orodha ya vyuo hivyo ipo kwenye website.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namqomba tu Mheshimiwa Mbunge labda tuweze kukaa na kuangalia kuna changamoto zipi kule Zanzibar ambapo labda kuna vyuo ambavyo havijapata usajili ili tuweze kujua kitu gani cha kufanya. Nakushukuru sana.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naishukuru Serikali kupitia kwa Naibu Waziri wa Mambo ya Muungano kwa niaba ya Waziri wa Fedha kwa majibu mazuri ambayo nafikiri sasa yataielekeza nchi yetu kuwa shirika hili ni la Serikali kwa mujibu wa sheria.

Swali langu ni moja tu kwamba kwa vile Serikali imeelekeza taasisi za Muungano na taasisi zote za Serikali kutumia Shirika la Bima la Taifa sasa kwa nini Serikali hairudi na kuelekeza wananchi wake ili waelewe kwamba Shirika la Bima la Zanzibar ni Shirika la Kiserikali na wana wajibu pia wa kutumia kulingana na huduma zao wanakavyoona ni nzuri na mimi nikiwathibitishia wabunge kwamba huduma hizo ni nzuri? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Najma kwa juhudi yake ya ufuatiliaji wa kero za wananchi na kwa namna anavyopambana kwa wananchi wote, kwa kweli naomba hili tulichukue kama ni wazo, ni ushauri na tutalifanyia kazi. Tutashauriana na Serikali kulifanyia kazi jambo hili, ahsante.

MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nitakuwa na maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; pamoja na kutoa elimu hii katika shule zetu bado suala la mimba za utotoni ni changamoto katika jamii. Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utafiti tunakosea wapi na wakati masomo yote tunatoa kwa watoto wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; ni kuhusu Uraia. Tuna Somo la Uraia kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha sita, lakini suala la uzalendo limeondoka miongoni mwa wananchi wetu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka mada maalum ya uzalendo kwenye Somo la Uraia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Najma Murtaza Giga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kufanya utafiti na kutilia mkazo juu ya masuala haya ya maadili. Kwa kuliona hilo katika miaka ya nyuma wanafunzi wetu wa shule za msingi walikuwa wanafanya mitihani katika masomo matano, lakini katika mwaka huu katika mitihani ambayo imeanza leo kwa kuona umuhimu wa somo hili la maadili tumeanza sasa kulifanyia mitihani ili kulijengea uwezo na kulitilia msisitizo zaidi. Kwa hiyo nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafanya utafiti na kwa umuhimu wa masomo haya imeonekana ni vyema vilevile nayo yakawa sehemu ya mitihani ya wanafunzi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili, nitoe wito tu kwa ndugu wazazi na walezi; jukumu la malezi ya watoto ni la jamii nzima, siyo la shule wala Walimu peke yake. Hivi sasa imetokea tabia na mtindo kwamba majukumu sasa ya malezi ya watoto wetu yamekuwa ya shule peke yake. Kwa hiyo tutoe wito kwamba, majukumu haya ni ya kwetu kuhakikisha kwamba maadili ya watoto wetu pamoja na mienendo ya taaluma zao tunafuatilia kwa karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili, kwamba Serikali sasa tuna mpango gani? Nimtoe wasiwasi vilevile Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, mchakato tunaoendelea nao sasa wa kuboresha mitaala yetu, mambo haya yote tutayatilia mkazo. Waheshimiwa Wabunge mna nafasi nzuri ya kutoa mawazo yenu ili kuweza kuangalia namna gani tunaweza tukatengeneza maadili, lakini tukaweka taaluma vizuri kwa vijana wetu kuhakikisha kwamba tunahitaji kizazi gani chenye maadili gani cha huko mbele tunakokwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri na naipongeza sana Serikali kwa kupokea mashauri mengi ya Waheshimiwa na kuyafanyia kazi. Hata hivyo, nina maswali mafupi mawili ya nyongeza. Swali langu la kwanza, ni lini Serikali sasa itaweza kukamilisha mapitio hayo na kazi hii kuwa nzuri zaidi kwa manufaa ya vijana wetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa vile Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) pamoja na Elimu ya Juu ni masuala ya Muungano: Je, Serikali haioni umuhimu wa kushirikiana na Wizara ya Elimu Zanzibar ili manufaa ambayo watayapata vijana wetu wa Tanzania Bara na Zanzibar waweze kupata? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba sasa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Giga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la uratibu au upitiaji upya wa mitaala yetu ni agizo la Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akihutubia Bunge tarehe 22 Aprili, 2021. Nasi kama Wizara, baada ya maagizo yale, tulianza kuyafanyia kazi kwa haraka. Nimhakikishie Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba kazi ile inaendelea vizuri na tumeanza kukusanya hayo maoni; tulianzia pale Dar es Salaam, baadaye tukaenda Zanzibar na baadaye tulifanyia hapa Dodoma na kazi hiyo bado inaendelea. Kazi hii inatarajiwa kukamilika baada ya miaka mitatu na miezi tisa. Tunatarajia mtaala huu mpya utaanza kutumika ifikapo Januari, 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika eneo la pili ambalo amezungumzia namna gani Wizara hizi mbili katika maeneo haya, namna gani yanaweza kufaidika? Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, eneo ambalo tupo tofauti na wenzetu wa Tanzania Visiwani ni katika eneo la elimu ya msingi; lakini upande wa sekondari tunatumia mtaala wa aina moja na upande wa Vyuo Vikuu tunatumia mtaala wa aina moja.

Mheshimiwa Spika, nimwondoe wasiwasi, wakati tunafanya mapitio ya mitaala yetu hii, tunashirikiana kwa karibu sana na Taasisi ya Elimu ya Zanzibar, nayo vilevile inafanya mapitio ya mitaala hiyo ili basi ile Tanzania tunayoihitaji iweze kufikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushuruku sana.
MHE. NAJMA MURTAZA GIGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, na nimpongeze sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kulipa kipaumbele suala la jinsia katika ajira katika kipindi chake.

Mheshimiwa Spika, swali langu ni kwamba, kwa mujibu wa Ibara ya 22 na 23 ya katibu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haki ya usawa wa ajira na ujira ni ya raia wote wa nchi yetu kwa shughuli yoyote inayosimamiwa na mamlaka yetu ya nchi.

Sasa, je, Mheshimiwa Waziri kwa nini hamuoni jambo la busara kwenda kumshauri Mheshimiwa Rais ili sasa Serikali ije ilete sheria ili hizo kanuni zenu na miongozo iingie humo iwe sheria, ili yoyote yule ambaye atakiuka sheria hiyo aweze kuadhibiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA. Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Najma Murtaza Giga kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, wote humu ni mashahidi, Mheshimiwa Rais wetu wa awamu ya sita Mama yetu Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya dhati ya kuweza kuleta uwiano sawa katika nafasi za uteuzi. Lakini vilevile sisi kama Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kama nilivyosema awali kwenye majibu yangu ya msingi, tumeanza kuweka miongozo, tunaandaa namna ya kuweza kupata usawa katika utumishi wa umma.

Mheshimiwa Spika, nitoe mfano, miongozo ya Sekretarieti ya Ajira inasema wazi pale endapo candidate wawili watagongana maksi na mmoja ni mwanamke, basi atachuliwa yule mwanamke katika kuingia katika ajira ya Utumishi wa Umma. Miongozo hii ipo na tutaendelea kuisimamia na kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini niwatoe mashaka, Mheshimiwa Rais ameweza kutafuta fedha kutoka European Union, Serikali ya Finland na Serikali yetu ya Tanzania vilevile imewekeza fedha katika Chuo kile cha Uongozi Institute; ambapo sasa tunaenda kutoa mafunzo ya uongozi kwa wanawake zaidi ya 500. Na hivi ninavyozungumza tayari kuna wanawake 50 ambao wapo katika mafunzo ya uongozi kwenye Taasisi yetu ya Uongozi Institute. Watakapo maliza wao wanakuja tena wanawake mia 100 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuweza kupata mafunzo ya uongozi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imejipanga vyema katika kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa katika uteuzi na ajira nchini. Naomba kuwasilisha.