Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Leah Jeremiah Komanya (16 total)

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Ujenzi wa bwawa la Mwanjoro lililopo Wilaya ya Meatu ulianza mwaka 2009 lakini hadi sasa ujenzi wa bwawa hilo haujakamilika:-
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa bwawa hilo ili liweze kutumika kwa ajili ya wananchi na mifugo katika Vijiji vya Jinamo, Mwanjoro, Itaba, Nkoma na Paji?
(b) Je, ni lini Serikali italeta fedha za miradi ya aina hii kwenye Halmashauri ili Halmashauri ziweze kutafuta Mkandarasi kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa karibu na hatimaye kuondoa usumbufu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bwawa la Mwanjoro ulisimama baada ya Mkandarasi kuondoka eneo la mradi bila ridhaa ya mtaalam mshauri wala mwajiri. Hadi wakati shughuli za ujenzi zinasimama utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 78. Serikali itafanya tathmini ya bwawa hilo mwezi Mei, 2016, baada ya mvua zinazonyesha hivi sasa kupungua ili kujua ubora wa tuta lililojengwa, viwango vya kazi zilizobaki, kazi zinazohitajika kuboreshwa, kuandaa michoro ya kuendeleza ujenzi na kuandaa kabrasha la zabuni kwa ajili ya kutafuta Mkandarasi mwingine. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kufanyika mwaka wa fedha 2016/2017
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa usumbufu wa huduma ya maji kwa wananchi, Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo ya kujenga mabwawa na kutenga bajeti ya ujenzi wa bwawa angalau moja kila mwaka. Aidha, Serikali itaendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K. n. y. MHE. LEAH J. KOMANYA) aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu hauna Chuo cha Ufundi (VETA) na kuwa vijana wengi waliohitimu elimu ya msingi na sekondari:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga chuo cha ufundi ili vijana hao waweze kupata elimu ya ufundi na kuweza kujiajiri?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mkoa wa Simiyu tayari imeshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Simiyu, katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge waliipitisha ya Wizara yangu, kiasi cha fedha cha shilingi 4,045,000,000 kimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi huo. Maandalizi ya awali ikiwemo kumpata mshauri elekezi, uandaaji wa michoro pamoja na makadirio ya ujenzi yaani Bills of Quantities (BOQ) na kumpata Mkandarasi yanatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2016 na ujenzi unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Simiyu ni kutoa mafunzo ya ufundi stadi na huduma kwa vijana wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ili waweze kupata elimu ya ufundi na hivyo kuwawezesha kujiajiri.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Jeshi la Polisi nchini linafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini linakabiliwa na upungufu mkubwa wa makazi kwa Askari wake:-
(a) Je, Serikali imepanga kujenga majengo mangapi katika Wilaya Mpya ya Itimila na Busega kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuyakamilisha makazi ya Askari Polisi yaliyomo Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka huu wa Fedha 2016/2017, Wilaya Mpya za Itilima na Busega hazikutengewa fedha za ujenzi. Hata hivyo, kwa kuwa Wilaya ya Itilima na Busega ni mpya hivyo kuwa na mahitaji makubwa. Katika mradi wa nyumba 4,136 unaotarajiwa kuanza punde taratibu za mkopo wa ujenzi wa nyumba hizi utakapokamilika kipaumbele ni kwa mikoa mipya ukiwemo Mkoa wa Simiyu wenye Wilaya za Itilima na Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kukamilisha miradi yote ya Makazi ya Askari nchi nzima ambayo ujenzi wake umesimama kutokana na
ukosefu wa fedha. Azma hii nzuri itategemea upatikanaji wa Fedha za Maendeleo katika Bajeti ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Wizara itaendelea na juhudi mbadala zikiwemo kuhamasisha Waheshimiwa Wabunge, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuchangia na kushiriki katika kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza tatizo kubwa la makazi ya Askari nchini pamoja na ofisi.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Kumekuwa na mauaji ya Watanzania wenye ulemavu wa ngozi kwa muda mrefu sasa ambapo hali hiyo imesababisha wananchi wasamaria wema kuanzisha makazi maalum kwa ajili ya kuwahifadhi.
Je, Serikali inashiriki vipi katika kutoa huduma muhimu ikiwemo kuhakikisha wanapata elimu, matibabu pamoja na lotion?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha takriban miaka kumi, kumekuwa na matukio ya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino ambavyo vimesababisha baadhi ya wasamaria wema kuanzisha makazi maalum ya kuwahifadhi watu wenye ualbino. Licha ya matukio hayo kupungua, bado kuna makazi yanayotumika kuwatunza watu wenye ualbino kwa sababu mbalimbali zikiwemo sababu za unyanyapaa na taarifa za baadhi ya matukio ya mashambulio japo si mara kwa mara kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita. Makazi hayo yanajumuisha yale yaliyoanzishwa na Serikali na yale yaliyoanzishwa na wasamaria wema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makazi haya, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inawajibika kuhakikisha kuwa watoto wenye ualbino wanapata elimu katika mazingira salama na kadri inavyowezekana kwa kuzingatia hali halisi Serikali itahakikisha watoto hawa wanapata elimu katika mazingira shirikishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matibabu na mafuta maalum ya ngozi, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Tiba za Ocean Road, KCMC, Bugando na wadau wengine imekuwa ikitoa matibabu na mafuta maalum ya kuzuia athari za mionzi ya jua katika ngozi, yaani sun screen lotion, kwa watu wenye ualbino. Aidha, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Madawa (MSD) imeandaa mkakati wa kusambaza mafuta maalum katika hospitali zote za Wilaya ili kuwasaidia watu wenye ualbino ambapo mafuta hayo yameingizwa katika kundi la dawa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali ikishirikiana na wadau wengine imeandaa utaratibu wa kuwapima macho na ngozi watu wenye ualbino na kuwapatia tiba pamoja na ushauri ili wasiathirike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaamini kuwa suluhisho la kudumu la kuondoa vitendo vya ukatili na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino nchini ni kutoa elimu ili kubadili fikra potofu kwa jamiii kuliko kunzisha makazi na vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hii, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana mamlaka ya Serikali za Mitaa na wadau wengine imeanzisha kampeni ya kupinga unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa lengo la kutoa uelewa na kutokomeza imani potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuhusu watu wenye ualbino.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali imeweka kipaumbele kwenye sekta ya kilimo na kuainisha kwamba mazao ya kilimo yatakuwa moja ya malighafi kwenye viwanda nchini:-
(a) Je, Serikali imeweka mkazo gani kwenye vyanzo vya kilimo ambavyo ndivyo vitakuwa malighafi na kusababisha uzalishaji ukue?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani juu ya uhakika wa wakulima wengi zaidi kuingia kwenye kilimo cha umwagiliaji?
(c) Je, Serikali imewekeza kwa kiasi gani kwenye zana za kilimo za kisasa kwa wakulima wadogo na hasa wanawake waishio vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mchango wa Serikali kwenye sekta ya kilimo ni pamoja na:-
(i) Kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija.
(ii) Kutoa elimu ya kilimo bora kwa kutumia mashamba darasa 16,786 na mashamba darasa 44 ya vijana yaliyoanzishwa.
(iii) Kutumia Vituo vya Rasilimali vya Kata 587.
(iv) Kuanzishwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ili kuimarisha soko la mazao ya kilimo.
(v) Kukarabati maghala ya kuhifadhia mazao katika Halmashauri ambapo hadi sasa maghala 33 yamekamilika na maghala haya yatanufaisha wakulima wadogo 13,800 kwa kuhifadhi mazao yao.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili wakulima wengi zaidi waingie kwenye kilimo cha umwagiliaji. Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na:-
(i) Kukarabati na kuziboresha skimu za umwagiliaji 37 zenye ukubwa wa hekta 28,612.
(ii) Kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone.
(iii) Kuanzisha na kuimarisha vyama vya wamwagiliaji 442 katika skimu za wakulima wadogo.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza mikakati mbalimbali kwenye zana za kilimo kwa wakulima wadogo na hasa wanawake waishio vijijini ili kuwarahisishia kazi shambani. Kwa mfano, hadi sasa kuna matrekta makubwa 10,283 na matrekta madogo ya mkono 7,350.
Wizara kupitia Mradi wa Sera na Maendeleo ya Rasilimali Watu (Policy and Human Resource Development) imesambaza mashine za kuvuna mpunga 64, kukata mpunga 16 na mashine za kukoboa mpunga 14 katika skimu 14 za umwagiliaji. Mashine hizo zilizosambazwa zitasaidia kuongeza tija na kurahisisha kazi mashambani hususani kwa wanawake.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali hutumia gharama kubwa katika utafiti wa maji na ujenzi wa miundombinu ya maji, lakini baadhi ya miradi inayokabidhiwa kwa mamlaka za maji za mji na jumuiya ya watumia maji (COWUSA) zinasuasua na kutonufaisha jamii kama ilivyokusudiwa:-
Je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha miradi ya maji inanufaisha jamii kama iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiaha Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini. Katika kuhakikisha miradi hiyo inanufaisha jamii kama ilivyokusudiwa Wizara imeandaa na inatekeleza uundaji, usajili wa vyombo vya watumia maji na kuvijengea uwezo kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi. Katika kuhakikisha mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira zinatoa huduma endelevu mamlaka hizo zinasimamiwa na bodi ambazo zinajumuisha wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utekelezaji huo kumekuwa na changamoto mbalimbali katika miradi hiyo ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya maji, wizi wa vifaa vya maji pamoja na watumiaji maji kutolipia huduma hiyo zikiwemo taasisi za Serikali. Hali hiyo ya baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa madeni yao kumepelekea mamlaka nyingi kushindwa kugharamia matengenezo ya miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na wizi wa maji pamoja na uchakavu wa miundombinu Wizara inaendelea kurekebisha Sheria za Maji ili ziweze kutoa adhabu kali kwa wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji. Vilevile mamlaka za maji na usafi wa mazingira mijini zinaendelea kukarabati miundombinu ya maji iliyochakaa, kufunga dira za maji kwa wateja wote ili kubaini matumizi yao halisi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji. Aidha, Wizara imeanza kuchukua hatua za kutumia nishati ya jua kwenye mitambo ya maji hususani vijijini kwa ajili ya kupunguza gharama za uendeshaji.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road pamoja na gharama kwa ndugu wa wagonjwa ya kuwaleta na kuwauguza ndugu zao.
Je, Serikali haioni haja ya kuanza kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza leo nasimama hapa toka niteuliwe na Mheshimiwa Rais, naomba na mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kunipa majukumu zaidi kwenye Serikali yake, pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Nzega Vijijini, Wilaya ya Nzega na Mkoa wetu wa Tabora kwa ujumla kwa ushirikiano ambao wameendelea kunipa. Napenda kusema tu kwa wote kwamba kwa hakika sitowaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye Saratani ili kusogeza huduma hizi karibu zaidi na wananchi na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Ocean Road, pia kupunguza gharama kwa wagonjwa na ndugu. Kwa sasa Serikali inakamilisha maandalizi ya kuanzisha matibabu ya saratani kwa mionzi katika Hospitali ya Bugando ambapo baadhi ya majengo kwa ajili ya huduma husika yamekamilika, yakiwemo jengo maalum ambalo ni kwa ajili ya kudhibiti mionzi, ambapo ukuta wake umejengwa kwa zege nene la mita moja (bunkers), jengo la kutolea huduma za mionzi, baadhi ya wataalam wapo na baadhi ya mashine za matibabu kwa mionzi zimeshanunuliwa zikiwemo Cobalt 60 na CT Simulator.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha brachytherapy na immobilization devices zinatarajiwa kuwasili mwezi Disemba, 2017. Kwa sasa huduma za tiba ya saratani zinazopatikana Bungando ni zile za matibabu yasiyo ya mionzi (chemotherapy) na zilianza mwezi Januari mwaka 2009, kufuatia sera ya Serikali ya kutoa huduma hizo kikanda. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa kipindi cha mwaka 2009 - 2017 hospitali imetoa matibabu kwa wagonjwa 39,300 kati yao 12,200 wakiwa ni wapya, sawa na wastani wa waginjwa 1,500 kwa mwaka.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu ambao ni mkoa mpya hauna Hospitali ya Rufaa, hivyo wagonjwa wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 140 kufuata huduma hiyo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Shinyanga na Mwanza; mwaka 2015/2016 Mkoa wa Simiyu ulipokea fedha kidogo ya kuanzisha jengo la OPD.
• Je, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa?
• Je, ni lini Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukukaribisha tena katika Bunge letu tukufu. Tumefurahi sana kukuona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, Wizara inapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kwa kutambua jitihada ambazo Serikali imefanya katika kuendeleza mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ukiwa ni mmoja wa mikoa mipya ulioanzishwa mwaka 2012. Kutokana na uhitaji wa huduma za afya ngazi ya rufaa katika ngazi ya mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu iliandaa na kupeleka andiko Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa kwa kuzingatia mahitaji ya kitabibu kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, niongeze hapa tu kwamba, pamoja na andiko hili hospitali hii sasa kwa agizo la Mheshimiwa Rais, zimeletwa tena katika Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha na hadi sasa jumla ya shilingi 2,087,268,672 zimeshatolewa. Kati ya fedha hizo, shilingi 299,896,185 zilitumika kununua ardhi yenye ukubwa wa ekari
(a) Shilingi milioni 595,650,815 zilitumika katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na utawala katika awamu ya kwanza na shilingi 1,191,721,672 zilitumika kuendeleza ujenzi wa jengo la OPD katika awamu ya pili.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za tiba katika Hospitali za Rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Simiyu. Hii inaenda sambamba vilevile na kupatiwa ahadi ya fedha ya shilingi bilioni 10 ambayo zilitolewa na Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu tarehe 11 Januari, 2017.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali hupeleka katika Halmashauri zilizopo katika Hifadhi ya Wanyamapori asilimia 25 ya fedha zitokanazo na mapato ya uwindaji wa kitalii na upigaji picha pasipo Halmashauri husika kujua msingi wa tozo hizo.
• Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki zake?
• Je, ni kiasi gani cha mapato kimepatikana kutokana na Maswa Game Reserve na Hifadhi ya Makao na kiasi gani kilipelekwa katika Wilaya ya Meatu kila mwaka kuanzia mwaka 2015 hadi 2017?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa mgao wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada za wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya Wilaya husika. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 Wilaya ya Meatu ilipata mgao wa shilingi 40,017,158 na shilingi 41,696,616.43 sawia ikiwa ni asilimia 25 ya mapato yatokanayo na wanyamapori waliowindwa katika vitalu vya Mbono na Kimali katika Pori la Akiba la Maswa na Makao WMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha katika vitalu vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na kutolewa taarifa mbalimbali. Aidha, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama MNRT Portal ambapo taarifa zinazohusu Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana humo. Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 1 Julai, 2018. Aidha, nakala ngumu zitatumwa kwenda Wilaya husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa Halmashauri nchini zinazopata mgao huu kutumia asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali kama ilivyokubalika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Pamoja na nia nzuri ya Serikali kudhibiti ulimbikizaji wa madeni lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kila siku katika Idara za Halmashauri za Wilaya zinazopokea ruzuku ya matumizi ya kawaida toka Serikalini:-
Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka fedha za ruzuku katika Halmashauri za Wilaya kama zilivyopitishwa na Bunge?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi. Kinachoidhinishwa na Bunge lako Tukufu ni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka husika. Pili, utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa sasa unafanyika kwa mfumo wa cash budget. Hivyo basi, ruzuku kutoka Serikali Kuu hupelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya kulingana na makusanyo halisi ya mapato ya mwezi husika. Serikali yetu kwa mtindo huo itaendelea kupeleka fedha za ruzuku kwenye Halmashauri zetu kutokana na makusanyo halisi kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Moja ya mkakati wa EQUIP – Tanzania ni kuinua ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa kike ili waweze kuhitimu Shule ya Msingi na kuendelea na Sekondari, lakini mtoto wa kike ana vikwazo vinavyoweza kukatiza ndoto hii:-

(a) Je, mpango huu umejikita vipi katika kutokomeza mimba na ndoto za utotoni, udhalilishaji kingono, ukeketaji na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto?

(b) Je, ni upi usaidizi wa mpango wa wanafunzi walio katika hatari zaidi kwa makundi kama vile waliotelekezwa, walio katika umasikini wa kupindukia, yatima na walionusurika kutokana na unyanyasaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, udhalilishaji kongono na ukeketaji, Serikali kupitia programu ya EQIP Tanzania imeanzisha clubs za wanafunzi ziitwazo Jiamini Uwezo Unao (JUU) kwenye Shule za Msingi 4,476. Malengo ya clubs hizo ni kuwajengea wanafunzi hasa wa kike uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujitambua. Kupitia clubs hizo, wanafunzi wanajifunza masuala mbalimbali ikiwemo hedhi salama na athari za kupata mimba katika umri mdogo.

Aidha, ili kuboresha mazingira ya watoto wa kike, mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kwa kupitia programu hii ilitoa ruzuku ya jumla ya shilingi bilioni 2.46 kwenye shule 4,476 ambazo kila shule ilipewa shilingi 550,000/=. Kupitia ruzuku hiyo, elimu ilitolewa kwa wanafunzi wa kike na wazazi kupitia ushirikiano wa Wazazi na Waalimu (UWAWA), kuhusu namna ya kutengeneza taulo salama za kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali kupitia programu ya EQUIP Tanzania imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii wakiwemo wanafunzi, wazazi na Walimu kupiga vita vitendo vya ukatili kwa watoto na kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia kwa makundi maalum wakiwemo watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia programu ya EQUIP Tanzania, Serikali imeongeza fursa ya kujifunza kwa watoto wa kike sawa na wa kiume na kuwakinga na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto. Jumla ya shilingi bilioni 6.8 zimetumika kuwajengea uwezo Walimu 50,446 kuhusu mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo matumizi ya mbinu zinazojali jinsia na ujenzi wa mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huo umeboresha mbinu rafiki na zinazozingatia jinsia katika ufundishaji na ujifunzaji kutoka asilimia 54 mwaka 2014 hadi aslimia 65 mwaka 2016 katika shule zilizo katika Mikoa iliyotekeleza programu hiyo ya EQUIP Tanzania. Tathimini inaonesha kuwa wasichana waliopata wastani wa juu katika kumudu stadi za kusoma na kuandika, walifikia asilimia 26.7 ikilinganishwa na wavulana asilimia 18 katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Moja kati ya vigezo vya “Capital Development Grant Assessment”ni namna Halmashauri inavyoweza kutoa taarifa kwa wananchi juu ya mtiririko wa fedha ambazo Serikali imepeleka katika Halmashauri na miradi iliyokusudiwa kutekelezwa:-

(a) Je, kwa nini mchakato huo ulisitishwa?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kurejesha mchakato huo ambao utakuwa ukiongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa wa viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa Halmashauri ulikuwa ni kigezo cha kuziwezesha Halmashauri kupata ruzuku ya maendeleo isiyo na masharti (Local Government Development Grant) kuanzia mwaka 2005. Miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa ni kuwepo kwa uwazi katika mapokezi na matumizi ya fedha kwenye ngazi ya Vijiji, Kata na Mitaa kwa kuhakikisha mapato na matumizi yanabandikwa kwenye mbao za matangazo. Mradi huo ulitekelezwa kupitia fedha za wafadhili ambapo Serikali pia ilikuwa na mchango katika fedha hizo. Mradi huo ulifikia ukomo mwaka 2013, baada ya wafadhali kujitoa na Serikali kuendelea kutekeleza mradi huo kuanzia mwaka 2014/2015 na 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuziwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo afya na elimu. Wananchi wanachangia nguvu kazi na vifaa mbalimbali kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hiyo. Serikali inakubaliana na wazo la kuzipima Halmashauri katika matumizi ya ruzuku hiyo inayotolewa na Serikali kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo liko kwenye mjadala ndani ya Serikali ili kuona namna bora ya kulitekeleza katika kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenye Halmashauri hadi ngazi ya vijiji.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni vigezo vipi vinatumika kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kumjibu Mheshimiwa Leah Komanya swali lake, kama ifuatavyo:-

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika anapaswa kuwa na sifa kuu mbili ambazo ni kuwa mwanachama wa Chama cha Ushirika; na awe na sifa ya kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushirika. Aidha, sifa nyingine ni sawa na zile za utaratibu wa uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Ushirika ambazo zimeelezwa katika Kanuni za Maadili, kifungu 134(3) na Jedwali la Pili la Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pamoja na maelezo hayo, Wizara imebaini upo upungufu katika sheria kuhusu taratibu na sifa za kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika. Wizara inakamilisha mabadiliko ya Sheria ya Ushirika ili pamoja na mambo mengine kuiboresha na kupata viongozi bora. Mabadiliko hayo yatazingatia kuweka mfumo wa kupata viongozi wenye uaminifu na uadilifu, uwezo wa usimamizi, kiwango cha elimu na teknolojia. Aidha, sheria iliyopo ilikidhi mahitaji na mazingira ya wakati huo ambayo inafanyiwa maboresho ili kuendana na mazingira ya sasa. Mwanachama wa Chama cha Ushirika hatapaswa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika endapo atakuwa na mgongano wa maslahi na Chama cha Ushirika katika kufanya shughuli za biashara zinazofanywa na Chama cha Ushirika husika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 kinatekelezwa ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hiki kinahusu utoaji wa nafasi ya ajira kwa watu wenye ulemavu waliokidhi vigezo vya msingi vya nafasi zilizo wazi. Sharti hili la sheria ni kwa waajiri wote yaani Serikali na waajiri binafsi. Sharti hili la sheria ni kwa sababu Serikali inatambua kwamba kazi ni muhimu katika maendeleo ya watu wenye ulemavu inayowawezesha kujitegemea na kuondokana na hali ya kuombaomba. Pia inaleta heshima na hali ya kujiamini katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kifungu hiki kinatekelezwa ipasavyo ni kama ifuatvyo:-

i. Serikali imeanzisha kanzidata ya wahitimu wenye ulemavu wenye fani mbalimbali ambao wanazo sifa za kupatiwa ajira kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

ii. Lakini pia tumekuwa tukifanya kaguzi za kazi kupitia Sheria ya Taasisi za Kazi kifungu cha 45A kinachompa fursa Afisa Kazi kutoa adhabu za papo kwa papo.

iii. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kufanya uhamasishaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu kwa njia mbalimbali zikiwemo warsha, mikutano, makongamano, vipindi vya redio pamoja na runinga.

iv. Kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania tumekuwa tukitoa tuzo kwa mwajiri bora ambaye ameajiri watu wenye ulemavu na kuwawekea mazingira wezeshi ya kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

v. Tumekuwa tukitumia programu ya ukuzaji ujuzi kwa kukuza ajira kwa kutoa mafunzo ya kitalu nyumba kwa vijana wakiwemo wenye ulemavu katika Halmashauri mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri wao wenyewe lakini pia kuajiri wenzao na pia kuweza kuajiriwa.

vi. La mwisho tumekuwa tukitoa mafunzo kupitia vyuo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu vya Yombo - Dar es Salaam na Sabasaba -Singida ambavyo mafunzo haya ambayo yamekuwa yanawawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Serikali ina Mkakati gani wa kuhakikisha kuwa watumishi hewa hawapo katika payroll ya Serikali:-

Je, Serikali inadhibiti vipi mishahara ya watumishi wasiostahili kulipwa kama wastaafu, waliofariki, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHESHIMIWA JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 kumekuwepo na mkakati madhubuti wa kudhibiti uwepo wa watumishi hewa katika Mfumo wa Malipo ya Mishahara kwa Watumishi wa Umma nchini. Utekelezaji wa mkakati huo ulifanyika kuanzia mwaka 2016 kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi wote waliopo kwenye taasisi zote za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika uhakiki huo, watumishi wote ambao hawakuwa na sifa ya kulipwa mishahara waliondolewa mara moja katika Orodha ya Malipo ya Mishahara (Payroll).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti malipo ya mishahara kwa watumishi wasiostahili kulipwa kama vile wastaafu, waliofariki na waliofukuzwa kazi, Serikali imekuwa ikisitisha mara moja malipo ya mishahara ya watumishi wa aina hiyo kupitia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (Human Capital Management Information System) na Mfumo wa Malipo ya Mishahara (Government Salary Payment Platform) pindi tu wanapokosa sifa ya kuendelea na Utumishi wa Umma. Mifumo hii inatumika katika Taasisi zote za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna udhibiti ulivyo hivi sasa na ufuatiliaji unavyofanyika, hakuna mtumishi anayeweza kulipwa mshahara bila kustahili. Aidha, naomba kutoa wito kwa Maafisa Masuuli katika Taasisi zote za Umma kuendelea kusimamia kikamilifu udhibiti wa malipo ya mishahara kupitia mifumo iliyopo.
MHE. LEAH J. KOMANYA Aliuliza: -

Mji wa Mwanhuzi unakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji safi na salama kutokana na chanzo chake cha maji cha bwawa la Mwanyahina kujaa tope: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wa Mji wa Mwanhuzi na vitongoji vyake wanapata maji safi na salama ya kutosha kwa mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mwanhuzi, Wilayani Meatu unategemea chanzo kimoja cha Maji ambacho ni Bwawa la Maji la Mwanyahina. Bwawa hilo lilijengwa mwaka 1999 lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo millioni 1.6. Bwawa hili kwa sasa limejaa tope jingi na kusababisha kupungua kina cha kuhifadhi maji kutoka kina cha mita 9 hadi mita 5 zinazohifadhi maji kwa matumizi ya wakazi wa Mji wa Mwanhuzi na vijiji jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika mji wa Mwanhuzi na vitongoji vyake, Serikali imekamilisha utafiti, usanifu na kuanza kutekeleza ujenzi wa chanzo mbadala cha ukusanyaji na usafirishaji wa maji kutoka bonde la Mto Semu hadi kwenye matanki yanayotumika kusambaza maji katika Mji wa Mwanhuzi. Gharama za mradi huo shilingi milioni 742. Tayari Serikali imetuma kiasi cha shilingi milioni 276.6 kwa ajili ya kazi hizo za ujenzi wa mradi mbadala wa kutoa maji katika bonde la Mto Semu na kuyapeleka mjini Mwanhuzi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kutatua tatizo la muda mrefu katika mji wa Mwanhuzi na vitongoji vyake, Serikali ipo katika hatua za awali za kutekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria unaolenga kumaliza changamoto za huduma za maji katika mkoa wa Simiyu zikiwemo Wilaya za Busega, Bariadi, Maswa, Itilima na Meatu.