Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Nape Moses Nnauye (38 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mimi ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (HUSM). Ahsante sana kwa nafasi hii uliyonipa. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imegusa kila kona, bahati mbaya imekuwa dozi kubwa imewafanya wenzetu wapate kiwewe na kukimbia humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na michango ya Waheshimiwa Wabunge kuna hoja zimeguswa. Baadhi ya hoja tutazishughulikia kwenye bajeti ya Wizara tutakapoileta, lakini nimesimama nishughulike na hoja moja ambayo kwa kweli inapotoshwa sana. Ni vizuri tukaweka kumbukumbu na rekodi sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya kurusha Bunge moja kwa moja; la kwanza, yanazungumzwa mengi lakini kuna mambo hayasemwi. Jambo la kwanza, mpango wa kuanzisha Studio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulipitishwa na Bunge hili na pesa zake zikatengwa. Hili jambo wenzetu hawataki kuwaambia Watanzania! Wanasema ni mpango ambao umebuniwa, unapitishwa kinyemela kwa lengo la kutaka kuwanyima Watanzania kuona Bunge lao. Huu ni uongo, tena uongo wa mchana peupe, kwa sababu mpango huo ulipitishwa hapa, Mheshimiwa Freeman Mbowe na wenzake walikuwepo na mpango huu waliupitisha. Hili la kwanza, ni vizuri tukaweka rekodi sawasawa.
Mheshimwa Mwenyekiti, la pili, kunasemwa hapa kama vile Bunge hili limezuiwa lisionekane kabisa, kwamba pana total blackout ya kuoneshwa Bunge hili. Nadhani either ni kutoelewa, uelewa mdogo au wanafanya makusudi baada ya kukosa hoja za msingi za kuja kuzijadili hapa, sasa wanaanza vioja ili ionekane liko tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichofanyika, pengine nitafute lugha rahisi wenzetu watuelewe; utaratibu umebadilishwa wa kulionesha Bunge letu, kama ambavyo utaratibu mwingine wowote unaweza ukabadilishwa. Dar es Salaam pale, barabara ya Samora ilikuwa ni barabara inapitisha gari kwenda na kurudi. Kwa sababu ya tatizo la foleni, ule utaratibu ukabadilishwa. Sasa utaratibu ukibadilishwa, anakuja mtu anazira kwenda barabarani kwa sababu utaratibu umebadilishwa kupunguza foleni. Nadhani hapa pana shida ya kuelewa au pana makusudi au pana kushindwa kazi kwa sababu ya kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kupitisha mpango wa kuanzisha Studio ya Bunge utaratibu wa kurusha Bunge hili ukabadilishwa na umebadilishwa kwa makusudi yafuatayo:-
Moja; Bunge hili wakati linarushwa mchana, wananchi waliokuwa wanapata fursa ya kuliona Bunge letu, idadi yake ukilinganisha na idadi ya watakaoliona Bunge usiku, kwa takwimu, siyo kwa maneno ya kelele, kwa takwimu, idadi yake inaongezeka. Maana yake ni nini? Maana yake tunatoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kuliona Bunge, kushuhudia kazi za Bunge kuliko ilivyokuwa inatokea mwanzo. Kwa watu ambao wamezoea kupiga kelele, wala hili siyo tatizo, jambo jema, Watanzania wametuelewa na tunasonga mbele bila matatizo. (Makofi/ Kelele)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ambalo hawasemi, Waziri wa Habari, tena Waziri wako, hawasemi na hii ni tabia yao; nami naomba Watanzania wawasamehe na wala sina mashaka, Jumatano watarudi hapa tutaendelea na mjadala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nalo ni kubwa Watanzania hawaambiwi, utaratibu wa kuweka Studio hapa Bungeni unarahisisha urushaji wa matangazo ya Bunge bila kulazimisha Vituo vya Habari vya Utangazaji kuja Dodoma na kuleta mitambo yao na gharama za Watumishi kuwaleta Dodoma. Kazi hiyo inafanywa na Studio ya Bunge. Uelewa mdogo!
Kazi hiyo inafanywa na Studio za Bunge, inapelekwa kwenye satellite, chombo chochote kila uwezo wa ku-link na kuchukua matangazo haya na kuyarusha kwa gharama nafuu na hivyo inaongeza idadi ya watazamaji, inapunguza gharama na inafanya kazi ya Bunge hapa ionekane zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, uongo wa kusema utaratibu huu…
MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba mtulizane, tumsikilize Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, uongo wa kusema kwamba utaratibu huu unawanyima haki wananchi, pengine tukubaliane, wenzetu wanaposema tafsiri ya mwananchi wanamaanisha mwananchi yupi? Huyu mama ntilie! Huyu mpiga debe! Huyu Machinga! Au wanamzungumza mwananchi yupi?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Sisi tunamzungumza mwananchi ambaye anaamka asubuhi, anakwenda kufanya kazi zake, jioni anarudi nyumbani kwenda kupumzika, anapata muda wa kutosha wa kuliangalia Bunge na kushuhudia kinachoendelea hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua wenzetu wana agenda nyuma ya hili, lakini Watanzania wametuelewa, dhana ya Hapa Kazi Tu imeiweka Serikali hii madarakani, tuendelee bila kurudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie pia Watanzania hili, jambo ambalo hawaambiwi; inaonekana kama vile utaratibu huu ni wa ajabu sana, lakini Tanzania siyo nchi ya kwanza kwa Bunge lake kuwa na Studio yake na kufanya kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mabunge yote ya Jumuiya ya Madola yameweka Studio za Bunge, yanafanya utaratibu huu tunaoufanya, tena sisi tumeenda mbali tumetoa uhuru kuliko ule uliotolewa na Mabunge mengine. Vile vile Serikali na Bunge tumezungumza na Wanahabari na kuwahakikishia kwamba utaratibu huu kwa Bunge letu ni mpya. Kama mpya, unaweza ukawa na upungufu wake katika utekelezaji wake. Serikali na Bunge tuko tayari kukaa na Wanahabari tukaangalia upungufu uliopo katika utekelezaji wa mpango huu, tukauboresha, tukautekeleza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwahiyo, tunaomba watuunge mkono. Wameendelea kutuunga mkono na tutaendelea kufanya hivi; Watanzania wanatuelewa, dunia inatuelewa na wasiotuelewa leo watatuelewa kesho, wala siyo mara ya kwanza wao kutoelewa kwa mara ya kwanza. Tutaendelea namna hiyo, tutafanya na tutasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kwa kuwapongeza na kuwashukuru sana, Wabunge wa Chama cha Mapinduzi kwa uzalendo wao na kuamua kubaki hapa kujadili na kutimiza wajibu wao wa Kikatiba, tofauti na wenzetu ambao wanalalamika Katiba inavunjwa, lakini wao wanatoka na kuivunja zaidi Katiba hii wanayodhani wanaitetea. Naomba niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge wa CCM na nimalizie kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nachukua fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka 2016/2017 kwa kauli na maandishi. Namshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya KUdumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mheshimiwa Peter Serukamba, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Vijijini, kwa maoni na ushauri wa Kamati yake katika hotuba ya bajeti ya Wizara yangu ya mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, namshukuru sana rafiki yangu, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu), kwa mchango wake katika hotuba yangu. Mheshimiwa Mbilinyi ni mdau mkubwa na muhimu katika tasnia ya sanaa ya muziki, hivyo kuimarika kwa tasnia hii kunamgusa moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba michango yote ya Waheshimiwa Wabunge inalenga kuimarisha na kuendeleza sekta ya habari, utamaduni, sanaa na michezo ili iweze kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa letu, kuzalisha ajira hususani kwa vijana, vilevile kuendeleza utamaduni, mila na desturi za Mtanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba yangu imechangiwa na jumla ya Waheshimiwa Wabunge 41 ambapo waliochangia kwa maandishi ni Waheshimiwa Wabunge 22 na kwa kauli ni Waheshimiwa Wabunge 19. Majibu na ufafanuzi nitakaoutoa umezingatia hoja zilizotolewa na Kamati ya Kudumu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni na hoja za Waheshimiwa Wabunge zilizotolewa kwa kauli na maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hoja ya mwisho, mwisho. Kuna baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanasema, Mheshimiwa Nape ni katika wanasiasa wachache vijana wanaochukiwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mafisadi wananichukia sana, ni kweli wasiopenda ukweli wananichukia sana, lakini wapo Watanzania wengi wakiongozwa na wananchi wangu wa Jimbo la Mtama, wananipenda sana na wananiamini kwa msimamo wangu wa kuwa mkweli hata pale ambapo ukweli unauma. Kwa hiyo, katika majibu nitakayoyatoa hapa, yako majibu mengine yanauma kwa baadhi ya watu lakini nitaomba tuvumiliane. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, imekuwepo hoja hapa ya kuhoji wadau wa Wizara hii wamekujaje Dodoma? Nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwa dhati wadau waliokuja kutuunga mkono kwenye hotuba hii kwa sababu wadau hawa wamejitolea kwa pesa zao mfukoni, kwa uzalendo wao na mapenzi yao kwetu, wakajitolea kuja Dodoma. Hakuna senti tano ya Wizara iliyotumika kuwaleta Dodoma. Nawashukuru sana wadau wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichofanya ni jambo rahisi sana. Hawa wadau wako Dodoma, akina Mzee King Kiki wako Dodoma, tukawaomba kwa uzalendo huo huo wapate muda wa saa chache kuja kutoa burudani hapa Bungeni. Hakuna dhambi ya wao kufanya hivyo. Wamejitolea wenyewe, badala ya kuwasema, badala ya kuwakashifu, badala ya kuwasemea maneno mabaya ya kuwavunja moyo nilidhani tuwapongeze kwa uzalendo wao na moyo wao. Kwa hiyo, Mzee King Kiki na wenzako nawashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwatangazia Waheshimiwa Wabunge kwamba baada ya kumaliza kazi hii nzuri twendeni pale tukacheze muziki vizuri, tufurahi pamoja. Hili haliwezi kuwa rushwa, hii ni Wizara ya Sanaa; Wizara ya Burudani. Baada ya kazi tunaburudika. Kazi na dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la pili ambalo nalo limezungumzwa sana. Nadhani ni vizuri nikazungumza mambo machache. Tumelizungumza kwa muda mrefu ndani ya Bunge letu, nalo ni suala la uhuru wa vyombo vya habari na hasa hili suala la Bunge live. Nadhani nigusie kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, uamuzi wa kuanzisha studio ya Bunge siyo uamuzi wa Mheshimiwa Nape kama Waziri, siyo uamuzi wa Serikali, ni uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Serikali haina mkono wake. Wanaonyoosha mikono, vidole na kusema Serikali, Serikali, nataka nirudie, huu ni uamuzi wa Bunge, ulipitishwa Bungeni hapa, ukatengewa pesa wakati Serikali ya Awamu ya Tano na Mheshimiwa Nape akiwemo, tulikuwa bado hatujawa wala Wabunge hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo kunyoosha kidole kwa Serikali kwa uamuzi uliopitishwa na Bunge hili, siyo sawasawa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, mara kadhaa nimekuwa nikisimama hapa Bungeni kulifafanua jambo hili, siyo kwa sababu jambo hili ni la Serikali, lakini kwa sababu Wizara yangu ndiyo yenye dhamana ya kusimamia Sera ya Habari; kwa hiyo, inapofikia mahali mambo yanapotoshwa kwa makusudi tunadhani tuna umuhimu wa kusimama na kufafanua. Leo nitazungumza ambayo sijawahi kuyazungumza, niyatolee ufafanuzi kwa uchache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, kuna watu wanasema uamuzi huu umevunja Katiba na kwa kweli maana yake umevunja sheria. Wizara hii inasimamia Sheria na Kanuni za Utangazaji hapa nchini na nitawasomeeni. Kanuni ya Utangazaji Namba 13(1) nitainukuu kama inavyosema na inasema hivi, ni ya kiingereza: “A licensee shall be free to cover Parliamentary sessions subject to laid down Parliamentary rules, regulations, procedures and on Parliamentary broadcasting.” Hii ndiyo Kanuni ya Utangazaji ambayo Wizara yangu inaisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa tafsiri rahisi inasema; “Chombo cha utangazaji kitatangaza matangazo ya Bunge kwa kuzingatia taratibu, sheria na kanuni zitakazowekwa na Bunge.” Siyo la Serikali; na Bunge lenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama kuna lolote linafanyika, halijapangwa na Serikali, Kanuni inalitaka Bunge ndiyo lipange namna gani vikao vyake vitarushwa na vyombo vya habari. Hii Serikali kuingizwa kwenye hili tunatoka wapi? Mimi nadhani tukae upya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, kama wasimamizi wa Sera ya Habari, tuliposikia kelele zinakuwa nyingi, mimi kama Waziri nilikwenda Mwanza kuhudhuria shughuli ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani. Nikiwa Mwanza nikasema hadharani, wanahabari ziko kelele juu ya jambo hili, sisi kama Serikali wasimamizi tuko tayari kusimama katikati ya Bunge na wadau tuzungumze upungufu wowote uliopo kwenye huu mfumo wa utangazaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea, wako wadau zaidi ya ishirini na kitu wakiongozwa na Jukwaa la Wahariri, wako hapa Dodoma leo siku ya tano, wanazungushwa kwenye studio ya Bunge, wanaongea na uongozi wa Bunge na mimi niliwashauri; ongeeni na uongozi wa Bunge, piteni kwenye studio ya Bunge, zungumzeni na wadau, wekeni mezani upungufu mnaouona halafu sisi Serikali tutakaa katikati yenu na Bunge tuzungumze upungufu uliopo. Hiyo ndiyo kazi yangu, huo ndiyo wajibu wangu na huo nautimiza na ndiyo maana wadau wako hapa. Juzi nilikutana nao, tumekaa nao mpaka saa 9.00 usiku, leo watu wananinyooshea vidole, Nape, Nape, Nape, Nape! Eeh!
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI SANAA NA MICHEZO: No, no, no! Lazima tuambiane ukweli, maana hili jambo mnalipigia kelele sana. Ni vizuri tukaambiana ukweli. Mliamua wenyewe, mmepitisha wenyewe, mmetenga pesa wenyewe; kama yako matatizo, kaeni chini yatatueni. Kanuni inataka Bunge hili ndilo lipange namna ya kurusha hiyo studio yenu. Studio hiyo siyo mali ya Serikali, studio hiyo ni mali ya Bunge. Tafadhali twendeni taratibu. (Makofi)
La nne, naona yako mengi katika hili, lakini labda la nne nizungumze. Ni vizuri, maana wakati mwingine tunabebeshana mizigo isiyokuwa na sababu. Kuna maneno yanazungumzwa na shemeji yangu na bahati nzuri wako shemeji zangu wengi Wakurya huku; shemeji yangu Mheshimiwa Mwita alisema kwamba unajua hili Bunge lenyewe linaonyeshwa mpaka saa 9.00 usiku. Mimi nawashauri Waheshimiwa Wabunge, studio ziko hapa nyuma; chukueni muda mchache nendeni mkatembelee pale, muwaulize namna gani studio inafanya kazi? Wanaoonyesha mpaka usiku, wameamua wenyewe; kituo kimeamua na hao ni TBC wameamua waonyeshe kila kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini viko vituo ambavyo vinaonyesha mwisho saa 3.00 na saa 3.00 ndiyo mwisho wa studio hii kurusha matangazo yake. Sasa kwa sababu ume-concentrate na kituo kimoja kinaitwa TBC ambacho pia bahati mbaya baadhi ya Waheshimiwa Wabunge humu humu huwa wanasema TBC bwana, Mbunge mmoja alikuwa anasema wala sikumbuki mara ya mwisho nimeiona lini, lakini akisimama hapa, kwa nini umeifungia?
Sasa namwambia wewe hukumbuki mara ya mwisho umeiona lini, lakini unapigia kelele kwa nini imefungiwa! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema pateni muda, nendeni pale mkaangalie inavyofanya kazi. Inarusha matangazo yake studio hii mwisho saa tatu. Ina delay ya saa moja. Dada yangu Mheshimiwa Minja, hii ni practice ya Mabunge ya Commonwealth.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda Mabunge ya Commonwealth, na mimi mifano ninayo ya kutosha. Sitaki kuwa msemaji wa studio hiyo, lakini nadhani ni vizuri Waheshimiwa Wabunge, studio si ziko hapa, nendeni mkaangalie. Dunia ya leo iko mikononi, just google Commonwealth practice ikoje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye uhuru wa vyombo vya habari, la pili kutoka mwisho, kuna hoja imezungumzwa na rafiki yangu Mheshimiwa Sugu, kama vile hii nchi inaongoza kwa kuvunja haki za vyombo vya habari na kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari. This is not right! Hebu tufike mahali tuwe fair, kama kuna mahali pa ku-improve semeni, ongezeni hapa na hapa, badala ya ku- condemn kama vile hakuna kinachofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Sugu anatoa taarifa hapa, akieleza kwamba sisi tumekubuhu kwa kuvunja haki za uhuru wa vyombo vya habari, waandishi wa habari, Shirika la Waandishi wa Habari wasiokuwa na Mipaka, wametoa ripoti yao mwezi wa nne wanasema hivi, wamefanya utafiti kwa nchi 180, katika nchi 180 duniani, Tanzania ni nchi ya 71 duniani; tumewazidi wakubwa wengi sana. Kwa Afrika, Tanzania ni nchi ya 11, lakini Afrika Mashariki Tanzania ni ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ripoti imetolewa juzi mwezi wa nne na ni ripoti imefanywa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka na vyombo vya habari vya Tanzania vimenukuu ripoti hii. Nilipokwenda kwenye Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, wenyewe waandishi wa habari walikuwa wakizungumza ripoti hii. Utafiti umefanyika, ripoti imetolewa na huo ndiyo ukweli. Kwa hiyo, tunapoangalia upande mmoja, twendeni na upande wa pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni upande wa habari. Kuna hoja hapa zinatolewa, kwamba sisi tumeleta hotuba hapa Bungeni ambayo haijali kabisa waandishi wa habari, maslahi yao, haki zao na kila kitu, tumepuuza. Dada yangu Mheshimiwa Minja, mimi ni mwandishi wa habari. Degree yangu ya kwanza ni ya uandishi wa habari na nimeisotea miaka mitatu, sikupewa, nimesoma! Kwa hiyo, tasnia ya habari iko ndani ya damu yangu, sijakurupuka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hii kwenye hotuba tumesema, katika mipango, mpango wa kwanza tutakaofanya mwaka wa fedha 2016/2017 ni kuboresha mazingira ya tasnia ya habari kwa kukamilisha mchakato wa utungaji wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari. Ndani ya muswada ule, haki zote zinazozungumzwa tumeziweka mle.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada ule uliletwa, ukapigiwa kelele, ukatolewa, tumerekebisha, tunatengeneza mchakato, ukikamilika tumeahidi mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 tutauleta Bungeni. Wenye uchungu mzuri tupitisheni huo Muswada. Ukipita, una majibu ya changamoto nyingi sana ikiwemo nani mwandishi wa habari. Maana yake leo kila mmoja anasema ni mwandishi wa habari, mpaka makanjanja wanasema ni waandishi wa habari. Matokeo yake tasnia inafika mahali inakosa heshima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweke heshima lazima tutafsiri nani mwandishi wa habariwa kweli. Mmezungumza kuhusu habari ya elimu; dunia ya leo huwezi ukapuuza elimu. Mbona madaktari wameweka viwango? Mbona wanasheria wameweka viwango? Kwa nini leo waandishi wa habari tusiweke viwango?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kazi zetu ziwe na weledi, ni lazima tuweke viwango vya elimu ili tufike mahali tulipane vizuri. Kwa hiyo, Muswada ule ukija uta-take care haya yote yaliyozungumzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ndiyo nilikuwa juu kidogo, sasa twende taratibu, kuna hoja ya maudhui, kuna hoja ya haki, mkwe wangu ananiambia ninywe maji.
Tutulie kidogo eeh! Nakushukuru Mheshimiwa Sugu. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya kujali muziki wa ndani, upande wa sanaa. Tunayo sheria inayosimamiwa na TCRA, inazungumzia habari ya asilimia 60 ya maudhui ya ndani (local content). Bahati mbaya kanuni hii imejumlisha maudhui yote yakiwemo habari, vipindi, muziki na vitu vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utekelezaji wake umekuwa na matatizo. Matatizo yake nini? Uzalishaji wa vipindi vya ndani, vile vya kawaida ambavyo siyo vya muziki una gharama kubwa. Practice inaonyesha hili jambo limekuwa gumu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunapitia upya kanuni hizo na mwenye dhamana hiyo ni mimi. Tunapitia kanuni hizo na moja ya jambo tulilolipendekeza kwenye kanuni ni kutenganisha maudhui ya vipindi vingine na maudhui ya muziki ambapo uzalishaji wake haufanywi na kituo cha utangazaji. Ukishafanya hivyo, hata ukiwawekea asilimia 80 hawana ujanja wa kukwepa kwa sababu cost of production siyo yao ni ya mzalishaji wa ile kazi ya sanaa. Kazi hiyo inaendelea, tunakamilisha na kwa kuwa iko mikononi mwangu, tutamalizana nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwahakikishie wasanii wa nchi hii, haki zenu ziko salama mikononi hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko tatizo limezungumzwa pia la kulinda haki zao. Bahati mbaya tunayo sheria ambayo kwa kweli imeweka adhabu ndogo sana, kwa hiyo, ukimkamata mtu ameivunja, ana uwezo wa kulipa na akaendelea na usaliti wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili tutalileta, tutabadilisha, tuwe na sheria ambayo ukimkamata mtu anaiba kazi ya msanii, adhabu yake iwe kubwa kiasi kwamba kila mmoja a-feel kwamba ni adhabu kubwa na hivyo akwepe kwenda kufanya kosa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushiriki wa wasanii, namshukuru sana Mheshimiwa January amelizungumzia.
Niende kwenye michezo, muda wangu unakimbia sana. La kwanza, Kamati ya Kudumu ya Bunge wameeleza masikitiko yao juu ya makusanyo kidogo kwenye sekta ya michezo, na sisi tunakiri kwamba kwa kweli makusanyo yako chini sana. Moja ya tatizo kubwa ilikuwa ni mifumo ya ukusanyaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako kwamba sasa Wizara imekamilisha utaratibu wa uwekaji wa mfumo kwenye uwanja wetu wa Taifa wa kulipa kielektroniki tiketi za kuingilia kwenye uwanja ule. Jambo hili likifanyika, litaongeza sana mapato na hivyo tutaondokana na hili tatizo la mapato kidogo kwenye sekta ya michezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, tunapitia upya Sheria ya Baraza la Michezo lakini pia tunapitia upya Sera ya Michezo katika nchi yetu. Wako watu wamezungumza maoni yao juu ya hili, Waheshimiwa Wabunge, nataka niwahakikishieni, mwaka huu wa fedha tutakamilisha hili. Kwenye Sheria ya Baraza la Michezo, moja ya jambo ambalo tutalizingatia ni kuhakikisha tunaangalia kwenye sheria na sera vyanzo vingine ambavyo vitaisaidia Baraza hili kupata pesa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie kwa haraka haraka, suala la mshahara wa kocha. Ni kweli Serikali ya Awamu ya Nne ilikuwa ikilipa mshahara wa kocha wa mpira wa miguu. Hili nililitangaza hadharani kwamba uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano ni kutolipa mshahara huo, kwa nini? Kwa sababu michezo iko mingi katika nchi yetu na sisi hatukuona busara ya kumlipa Kocha mmoja na ukaacha michezo mingine.
Kwa hiyo, uamuzi huu ulishapita, ni kazi ya vyama vya michezo, Serikali tutawawezesha kuwatengenezea mazingira mazuri vyama vya michezo vipate uwezo wa kulipa makocha wake badala ya Serikali kubagua na kulipa makocha wachache na michezo mingine ikaachwa nje ya wigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwepo hoja hapa ya unaoitwa mgogoro kati ya TFF na TRA hasa lile sakata la kufungiana akaunti. Hili nalo tulilieleza lakini labda nilieleze tena.
Mheshimiwa Mwenyekiit, ni kweli kwamba kimsingi ukisikiliza kesi hii, tatizo siyo la TFF, tatizo ni la Serikali. Kwa nini? Mshahara huu ulikuwa unalipwa na Hazina, bahati mbaya wote wawili (Hazina na TFF) walitegeana kwamba ile kodi inayotokana na mshahara inalipwa na mwenzake. TRA mteja wao wanaomjua ni TFF ndiyo maana wanakwenda kumkamata TFF na kukamata mali zake. Hivyo hivyo kwenye mechi ile ya Brazil na Taifa Stars, Ndugu yangu Mheshimiwa Nkamia amelieleza vizuri kwamba kwa kweli TFF hawakushiriki, lakini kwa kuwa mteja wa TRA ni TFF, TRA wanambana TFF. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliambie Bunge lako, tumekaa pamoja Serikali, TFF na TRA tukakubaliana kimsingi anayetakiwa kuilipa kodi hii ailipe na ndiyo maana hali imetulia. Na sisi kama Serikali tutajitahidi kufuatilia na kusukuma jambo hili liishe. Bahati mbaya limekuwa ni jambo ambalo limekuwa linaisha, linarudi, linaisha na kurudi. Safari hii tunaamini tutalisimamia na kuhakikisha kwamba jambo hili linakwisha.
Mheshimia Mwenyekiti, nadhani kwenye michezo, pia niwapongeze watani zangu Yanga, Mheshimiwa Zitto alisema timu yako imeshinda; mimi ni Waziri wa Michezo. Nilivaa jezi ya Yanga kuwatia moyo na Simba mkifanya vizuri nitakuja kuvaa jezi yenu msipate shida, mimi Taifa Stars. Ila nawatakia kila la kheri Yanga kwenye mchezo wao na kuhakikisha kwa kweli tunawaombea wafanye vizuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia hoja hii, naomba mashabiki wa timu zetu hasa Simba na Yanga, inapotokea timu moja inakwenda kucheza mchezo wa Kimataifa, kwa kweli ni nchi yetu inacheza na Taifa hilo lingine. Tutangulize uzalendo mbele. Tumeona timu hizi wakati mwingine zikizomeana, lakini aibu siyo ya timu, ni aibu nchi. Ushauri wetu kama Wizara, tunaomba inapofikia mechi za Kimataifa, basi tupunguze kidogo ushabiki, tuweke uzalendo wa nchi yetu na nadhani litakuwa ni jambo zuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumze kidogo juu ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC). Kuna hoja hapa kubwa, nadhani ni vizuri nikaigusa, hoja ya mkataba kati ya Startimes na TBC kupitia Star Media. Wengi waliochangia wanasema jambo hili halina tija, lakini siyo kweli kwamba hakuna tija kabisa. Ngoja niziseme baadhi ya faida zilizopatikana kwenye mkataba huu na kabla ya kuzisema, niseme kwamba tulipopata Bodi mpya ya TBC moja ya kazi tuliyowapa kama Wizara ni kuupitia upya mkataba huu na kuangalia maeneo ambayo yanalalamikiwa kwamba ni maeneo yanye matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nataka niliarifu Bunge lako, maeneo hayo yamepitiwa na Bodi imefanya kazi nzuri, taarifa yao wameikabidhi kwangu, na sisi kama Wizara tunaifanyia kazi kuona upungufu wowote ambao umebainisha tukae mezani tuone namna ya kushughulika nayo. Pamoja na upungufu mkataba huu umeiwezesha Tanzania imekuwa mojawapo ya nchi za kwanza Afrika ikiwemo Rwanda na Visiwa vya Shelisheli kuhama kutoka mfumo wa utangazaji wa analojia kwenda dijitali mwaka 2012, ni kupitia huu mkataba nchi yetu imepata sifa na heshima ya kuwa nchi ya kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya pili, mwaka 2015 Startimes walishinda tuzo ya Kimataifa ya World Quality Commitment ijulikanayo kama Golden Quality Award ambayo ni heshima kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya tatu, mwaka 2016 Startimes imeshinda tena tuzo ya European Society Quality Research, ambayo watakabidhiwa Juni mwaka huu wa 2016, jijini Brussels, Ubelgiji. Tunadhani hii bado ni faida kwetu. Startimes imeajiri zaidi ya Watanzania 400 katika nafasi mbalimbali. Startimes imesajili wateja takribani milioni 1.2 lakini Startimes walikarabati jengo la ghorofa tano ambapo kwa sasa wanailipa TBC pango lake, kwa sababu kuna watu wanasema kama vile TBC hawapati chochote kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo waliyojenga vituo vya kurushia matangazo wamekodi kutoka TBC kwa sababu wao hawakuwa na maeneo, maeneo mengi waliyojenga ni maeneo ya TBC, kwa hiyo, wanailipa TBC na ziko faida nyingine nyingi, lakini nataka nikiri kwamba yako maeneo yanayolalamikiwa, nasi kama Serikali tuliagiza Bodi, Bodi imepitia mkataba na kwa kweli wameleta ripoti nzuri na tunaifanyia kazi na baada ya muda tutachukua hatua za kuboresha baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwisho pengine kwa sababu muda umeisha, kuna hoja nzuri ilitolewa na Kambi ya Upinzani, hoja ya kuangalia namna ambavyo tutahifadhi historia yetu. Niseme, kwa awamu sasa tumekuwa na mradi wa kuweka kumbukumbu ya ukombozi Kusini mwa Bara la Afrika na Tanzania imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa mradi huo. Katika bajeti tunaomba mpitishe hapa, kuna pesa tumeomba kwa ajili ya kuweka kwenye mradi huo. Mradi huu ni mkubwa, unahusisha nchi za Kusini mwa Bara la Afrika na kwa sababu Tanzania ilishiriki katika harakati za ukombozi wa hizo nchi, tukapewa heshima hiyo, tunasaidiwa na wenzetu wale lakini pia kuna mashirika ya Kimataifa ambayo nayo yanaingiza mkono wake kusaidia kuhakikisha mradi huu unatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kupitia mradi huu tumeanza mazungumzo ya kuona namna ambavyo tutaufanya huu mradi pia u- trickle-down kwenye nchi yetu ili tuwe na uwekaji mzuri wa kumbukumbu na hasa kumbukumbu za ukombozi na nyingine ambazo zitalisaidia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie, kwa kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, niwahakikishie hoja zenu ambazo sikuzigusa zitaletwa kwenu kwa maandishi na kila Mbunge atazipata. Tutazifanyia kazi na ninaamini mtapitisha bajeti yangu. Safari ijayo tukija, tutaripoti namna tulivyofanya vizuri. Kwa vyovyote vile, safari ni hatua, turuhusuni tupige hatua katika safari hii njema tunayoianza na ninaamini mtaturuhusu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa muda wako, ahsanteni sana, naomba kutoa hoja.
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ikiongozwa na Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba. Namshukuru sana Mheshimiwa Juma Nkamia kwa kuwasilisha maoni ya Kamati na nashukuru kwa ushauri wao na kwa kweli ushiriki wao katika kuhakikisha Azimio hili linafika hapa lilipofika, nawashukuru sana!
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa masikitiko pengine, kwa kutopata mawazo ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa uwasilishaji wa kutosha ukiacha kuleta hotuba yao hapa kwa uamuzi ambao pengine wanadhani unawasaidia wao, lakini nadhani utaratibu huu mbovu wa kuwa wanakuja wanasaini, wanachukua posho na kuondoka haufai!
Mheshimiwa Naibu Spika, michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge, inaonesha namna ambavyo ni muhimu sasa kwa Tanzania kuridhia mkataba huu ili Taifa letu liweze kunufaika na fursa zitokanazo na mkataba huu ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa ushindani uliosawa michezoni na pia kulinda afya na ustawi wa michezo na wanamichezo wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, sasa nitoe ufafanuzi wa hoja chache. Niwashukuru Wabunge wote waliochangia, natambua mchango wa Mheshimiwa Hafidh Tahir Ali, Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mheshimiwa Joseph Kakunda, Mheshimiwa Esther Mahawe, Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile, Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mheshimiwa Seleman Jafo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, mchango pia wa Dkt. Mwakyembe, Waziri wa Katiba na Sheria. Pia namshukuru sana Naibu Waziri wa Wizara hii kwa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizowasilishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nilihakikishie Bunge lako, utayari wa Serikali katika kutekeleza mkataba huu. Kuna mashaka yameoneshwa hasa kwenye maneno ya Kambi ya Upinzani Bungeni kwamba wakati mwingine mikataba hii inaridhiwa halafu utekelezaji wake unakuwa na mashaka. Nataka nilithibitishie Bunge lako, kwanza, kitendo cha kuleta mkataba huu uridhiwe Bungeni ni uthibitisho kwamba, Serikali iko tayari kuutekeleza ndiyo maana tumeuleta hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tayari kama alivyosema Naibu Waziri, tumeshaanzisha ofisi pale Uwanja wa Taifa. Uanzishwaji wa ofisi hii ambayo itashughulikia jambo hili pia ni uthibitisho wa utayari wa Serikali kutekeleza mkataba huu. Kwa hiyo, sioni sababu ya kuwa na mashaka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumeshapeleka wataalam wetu kwenda kufanya mafunzo ya awali. Watumishi kadhaa wamekwenda wamefanya mafunzo ya awali juu ya utafiti, elimu na mafunzo katika kutekeleza jambo hili, tuna hakika wataalam wetu wamefanya vizuri kwenye mafunzo yale na wako tayari kwa kazi hii. Kwa hiyo, walichokuwa wanasuburi ni kuridhiwa tu kwa mkataba huu ili waanze utekelezaji. Hivyo, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba, Serikali iko tayari kutekeleza mkataba huu. Sasa hivi tuko katika mchakato wa kupitia upya sera ya michezo na sheria zinazoongoza Baraza la Michezo katika nchi yetu. Katika mapitio haya tutazingatia uwepo wa sheria, ambazo zitasaidia sana utekelezaji wa Mkataba huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Bunge katika maoni yao ya Kamati wameeleza kwa umuhimu sana na hata baadhi ya Wabunge waliochangia, suala la kuelimisha wadau juu ya jambo hili. Jambo hili ni kubwa, lina madhara makubwa lisipotekelezwa vizuri na inawezekana kwa kutokuwa na elimu ya kutosha, utekelezaji wake ukawa na tabu!
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imejipanga vizuri kuhakikisha pamoja na wadau ambao kwa kweli hata mwanzo wakati tukijadili mkataba huu, tulikuwa tukizungumza jambo la kutoa elimu ya kutosha kwa wanamichezo wetu na wadau wetu kwa pamoja ili walielewe vizuri jambo hili ili utekelezaji wake uwe na mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua mchango wa Dkt. Mwakyembe, alikuwa anazungumza hapa wakati mwingine, kwetu huku unaweza ukawa na vitu, ambavyo huvioni kama vina madhara kwenye kuongeza nguvu kwenye mwili, lakini baada ya kuvitumia vinaoneka ni vya kawaida vikawa na madhara.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo haya yote tutayazingatia kwa pamoja kuhakikisha elimu inayotolewa inasaidia na kwa kuwa naamini Bunge lako litaridhia, sisi tutakuwa moja ya wanachama halali kwenye harakati hizi. Kwa hiyo, baadhi ya maoni na ushauri wa namna ya kuboresha hata mkataba wenyewe, tutakuwa na fursa ya kutoa maoni yetu kama wanachama halali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati ya Kudumu ya Bunge imependekeza na mengi kwa kweli ni mapendekezo kwamba mkataba usainiwe mapema. Wanasema ni rai ya Kamati kuwa, maazimio ambayo ni mazuri na yenye faida kwa nchi yetu, Serikali iwe inaridhia mapema ili kuweza kunufaika nayo kama inavyokusudiwa. Ni kweli ushauri ni mzuri, lakini pia nadhani ni vizuri kuchukua tahadhari kutosaini kwa haraka baadhi ya mikataba, ni vizuri tukajiridhisha kama ina manufaa kwa nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia inaishauri Serikali kuangalia sheria mbalimbali zilizopo na kuona zinaweza kukidhi mahitaji ya Azimio hili. Kama nilivyosema kwamba, tunapitia upya sasa Sheria ya Baraza la Michezo na Sera zake, kuona namna gani tutaziboresha ziendane na wakati na moja ya jambo kubwa tutakalolizingatia ni namna ambavyo sheria hizi zitasaidia utekelezaji wa Azimio hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati imetushauri pia kwamba, utekelezaji wa mkataba huu uzingatie kundi la wakufunzi. Zimekuwepo hizi hoja hapa kwamba, siyo wanamichezo tu pengine na wakufunzi nao, tutazingatia ushauri huo. Ilikuwepo hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kwamba pamoja na mkataba huu lakini bado michezo yetu inakabiliwa na changamoto nyingi likiwemo tatizo kubwa la rushwa kwenye michezo, ambalo linachangia sana uporomoshaji wa michezo katika nchi yetu na hasa kwenye eneo la upangaji wa matokeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wa hotuba ya bajeti ya Wizara yangu, nilizungumza hili kwamba, ni changamoto kubwa katika michezo yetu. Sisi tumejipanga kuanza na vita dhidi ya rushwa kwenye Vyama vya Michezo. Kwa sababu kule ndiko ambako pasipotengenezwa vizuri tunapata viongozi ambao wanatokana na rushwa, wakiingia kwenye michezo, maslahi yao siyo kuendeleza michezo, maslahi yao ni kurudisha pesa walizozitumia kuingia madarakani. Kwa kuwa, ziko chaguzi mbalimbali zinaendelea, nitoe wito kwa vyombo vyetu hasa TAKUKURU kutusaidia kupambana kiukweli na tatizo hili kubwa la rushwa kwenye hasa chaguzi za Vyama vyetu vya Michezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati pia imeshauri lishe bora kwa wanamichezo kama sehemu mojawapo ya kuangalia kwamba wanamichezo wetu, basi hawakumbwi na maswahibu haya, lakini pia wanafanya vizuri michezoni. Nadhani ni ushauri mzuri na Wizara tunauchukua na tutaufanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue nafasi hii kuwashukuru Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Hawa wanasaidiana na sisi na kwa kweli wao ndiyo waratibu wa michezo kwenye shule zetu kwa commitment yao, kwa sababu kama elimu hii ya utekelezaji wa Azimio hili itaanza kutolewa vizuri kwa vijana wetu na mwezi huu mwishoni wanaanza mashindano pale Mwanza, naamini tukitumia fursa hii tutajenga vijana wanaojiamini, wanaotumia uwezo waliojaliwa na Mwenyezi Mungu kuonesha vipaji vyao, tutapata wachezaji wazuri. Nadhani huku ni mwanzo mzuri na tutatumia fursa hiyo kila michezo hii inapofanyika, ikiwezekana mpaka mashuleni, elimu hii itolewe ili vijana wetu wajiamini, waachane na vishawishi vya kutumia madawa kuongeza nguvu michezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tunaamini hili likifanyika, samaki ukimkunja angali mbichi inawezekana mambo yakawa mazuri. Kwa hiyo, uamuzi wa kupitisha Mkataba huu kwa Bunge lako kutasaidia sana kuliletea heshima Taifa letu. Mwezi wa Nane tunakwenda kwenye michezo ya Olympic, safari hii tutakwenda kifua mbele kwa sababu tumeridhia na tumesaini mkataba huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa ufafanuzi huo, sasa naliomba Bunge lako Tukufu, liridhie Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Katika Michezo, yaani International Conversion Against Doping in Sport wa Mwaka 2005.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa 2018/ 2019. Pamoja na kazi nzuri na jitihada kubwa ambayo inafanywa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo katika nchi yetu. nimepongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji kwa wizara kwa kazi mnayofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu umeletwa hapa ili tuuboreshe, tutoe mawazo yetu ambayo yanaweza kutumika kuboresha ili tufikie lengo la kuleta maendeleo katika nchi yetu. Na mimi nina amini Waziri na wenzake watatusikiliza na watachukua mawazo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma haya mapendekezo ya Mpango, utagundua humu ndani imeorodheshwa miradi mikubwa ya aina mbili; unaweza uka- group unavyoweza lakini iko ya aina mbili. Iko miradi ambayo ni ya kihuduma, miradi ambayo inahusiana na maji, afya, elimu, utawala na maeneo mengine. Miradi ambayo kwa asili yake haiendeshwi kibiashara, lakini upande wa pili kuna miradi ambayo kwa asili yake inaweza kuwekezwa na kuendeshwa kibiashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa huu mgawanyo wa aina hizi mbili za miradi, niliposoma nilishtuka kidogo kuona Serikali inapendekeza kuwekeza pesa za Serikali kwenye miradi ambayo inaweza kuendeshwa kibiashara. Nilitegemea miradi hii tungeruhusu sekta binafsi, tukatengeneza mazingira mazuri ya sekta binafsi kuwekeza kwenye miradi hii badala ya kuchukua pesa za Serikali na kuipeleka kule kwa sababu madhara yake ni makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mpango huu utatekelezwa kama ulivyo, miradi hii inakwenda kuua uchumi wa nchi yetu. Nitatoa mfano, miradi hii mikubwa ambayo ninaizungumzia ni miradi kama ya uzalishaji wa umeme na hapa imekuwa ikizungumzwa Stiegler’s Gorge kwa mfano, miradi ya ujenzi wa reli, uboreshaji wa Shirika la Ndege, mradi wa bandari na baadhi ya barabara ni miradi ambayo kwa asili yake inaweza kuwekezwa kibiashara, kuendeshwa kibiashara na ikajilipa kibiashara. Sababu ya kuchukua hela za Serikali kupeleka kwenye miradi hii kwa kweli sijaiona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sifa ya miradi hii kwanza ni miradi mikubwa sana, lakini ya pili kwa ukubwa wake ni miradi ambayo ina gharama kubwa; ukiingalia ni mabilioni kadhaa ya dola kwa asili yake, lakini sifa ya tatu miradi hii niliyoitolea mfano hapa ni miradi ambayo uwekezaji wake utachukua muda mrefu na hivyo payback period yake ni ya muda mrefu sana. Sio miradi ya kulipa kesho, ni miradi ambayo itachukua muda mrefu kwa vyovyote vile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi siipingi miradi hii naomba niweke rekodi vizuri isipokuwa ninapingana na mapendekezo ya Serikali ya namna ya kuiwekeza na kuiendesha miradi hii kwa kutumia pesa za Serikali. Tafsiri ya uamuzi wa kutumia pesa za Serikali kwenye miradi hii ni hii ifuatayo:-

Moja, itailazimisha Serikali kukopa hela nyingi kwa vyovyote vile kwa sababu ni miradi mikubwa, gharama yake ni kubwa, kwa hiyo ni lazima Serikali iende ikakope. Serikali ikienda kukopa na kwa sababu miradi hii inachukua muda mrefu, maana yake ni moja tutaanza kulipa deni hilo lililokopwa kabla ya miradi hii haijaanza kulipa faida kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tafsiri yake ni kwamba tutachukua hela kwenye maeneo mengine tuilipie deni miradi hii. Hapo maana yake ni kwamba tutaendelea kufunga mikanda muda mrefu, sasa tunafunga mkanda kwa nini? Ndio maana nahoji kwa nini Serikali inafikiri kwamba kuwekeza pesa za Serikali kwenye miradi ambayo ingeweza kuwekezwa kibiashara na sekta binafsi ni jambo la tija kwa uchumi wa nchi yetu, mimi nadhani hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vyovyote vile ukichukua pesa za maeneo mengine maana yake utaathiri maeneo hayo, maana yake utaathiri miradi ile ya huduma kama maji, afya, elimu na utawala na mtafika mahali hata malimbikizo ya wafanyakazi itashindikana kulipa kwa sababu tunachukua pesa za Serikali kuzipeleka kwenye miradi ambayo ingeweza kujiendesha kibiashara. Kwa hiyo, mimi nadhani hili la kwanza sio sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuna madhara makubwa kwa Deni la Taifa kuchukua hela za Serikali ambazo nyingi kama nilivyosema itabidi tuzikope kuziwekeza kwenye miradi hii. Na hapa Waheshimiwa Wabunge nataka twende kwa takwimu vizuri kwa mahesabu na ndipo hapa ninapohoji uzalendo wa wachumi wetu kuishauri Serikali na Mheshimiwa Rais kuwekeza hela za Serikali kwenye miradi hii, hapa mimi napata taabu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa ripoti uliyotupa hapa Mheshimiwa Waziri, deni letu la taifa limefikia dola bilioni 26 ambayo ni sawa na asilimia 32 ya ustahimilivu wa deni la taifa. Ukomo ni asilimia 56, sasa kama 26 imetupeleka kwenye 32 unahitaji dola bilioni 45 kufikia ukomo wa asilimia 56 ambayo ni mwisho wa kukopesheka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa twende tuchukue mfano wa miradi mitatu, acha miradi mingine yote kwamba hatukukopa, hatukukopa maji ambayo tunachukua hela za wahindi, hatukukopa kwenye barabara, elimu na wala kwenye umeme na maeneo mengine yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu chukua miradi mitatu; mradi wa kwanza ni mradi wa ujenzi wa reli ya kati ambao kwa tathmini yake unaweza ukagharimu approximately dola bilioni 15, ziweke dola bilioni 15, chukua mradi wa Stiegler’s Gorge wa uzalishaji wa umeme ambao kama ninavyosema leo ukikohoa wawekezaji wanakuja, tunataka kuweka hela za Serikali, dola bilioni tano, jumla 15 na tano unapata dola bilioni 20. Halafu chukua uboreshaji wa Shirika la Ndege, kwa ujumla wake mpaka umalize karibu dola bilioni moja kwa hiyo unazungumzia dola bilioni 21.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama una dola bilioni 26 deni la taifa ukijumlisha dola bilioni 21 maana yake unazungumzia dola bilioni 47 na ukomo wetu ni dola bilioni 45, kwa vyovyote vile hii ime-burst. (Makofi)

Sasa kama inakwenda ku-burst maana yake tunakwenda kutokopesheka, kama tusipokopesheka ina maana gani kwa uchumi wetu? Kwa nini tunataka kung’ang’aniza kuchukua hela ya Serikali na tumeanza kwenye reli na ndege tumeweka na kwenye Stiegler’s na kwenyewe tunakwenda, mwisho wake uitakuwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani hebu tufikirie upya, hii thinking ya kwamba sekta binafsi tunaiandika kwenye makaratasi kwamba ndio itakayotekeleza mpango huu, lakini kimsingi kwa matendo yetu tumeiweka pambeni, kwa nini tusiitumie? Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi walianza kuiruhusu sekta binafsi na akatengeneza mazingira, inawezekana kuna mapungufu yake lakini sekta binafsi ilianza kupata mwanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Awamu ya Nne Mheshimiwa Waziri Mheshimiwa Rais wa sasa Magufuli alikuwa Waziri wa Ujenzi. Wakati wake waliruhusu wakandarasi kutoka sekta binafsi wakachukua mikopo ya benki, wakaanzisha makampuni, leo hii tunavyoongea hawa watu mortgage zao zinauzwa. Na zinauzwa kwa kuwa wana madeni wanaidai Serikali, lakini Serikali imeamua kuanza kuchukua mkondo wa shughuli zake za ujenzi kutekelezwa na Serikali yenyewe. Kwa hiyo, hawa tuliowatengeneza kwa miaka yote tunawakosesha hela sasa, they are starving and they are dying.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu mpango wako mzuri ndio lakini hebu rudini kwenye thinking ya kuruhusu sekta binafsi kufanya kote, duniani kote mambo yanakwenda hivyo. Jana mmesikia mifano hapa na Mheshimiwa Spika alitoa mfano, Warusi ambao walikuwa waumini wakubwa wa ujamaa wameruhusu sekta binafsi mpaka viwanja vya ndege; sisi leo kiwanja chetu cha ndege pale karibu dola bilioni 560 hivi, hela nyingi kweli. Hivi tungeruhusu watu binafsi wakawekeza nani asingekuja pale, kwa vyovyote inalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mradi kama Stiegler’s gorge pamoja na kwamba nauunga mkono, sina hakika kama tumefanya tathmini ya madhara yake ambayo yanatokana na shughuli za kibinadamu zinazoendelea kuuzunguka mradi wenyewe. Tuna miradi mingine ya maji hapa nchini ambayoo yote ina-prove failure; tumechukua tahadhari gani katika mradi huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu wa kuamini kwamba Serikali itafanya kazi ya kuzalisha umeme yenyewe, ndio utaratibu unaotesa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Tumevunja Mkataba wa Symbion tunasema tutawekeza mitambo wenyewe pale, leo Lindi na Mtwara tunakaa mpaka siku tatu au nne umeme hakuna, maisha yanasimama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kama hali hiyo ingekuwa inatokea Dar es Salaam kwamba mnakaa siku tatu/nne umeme hakuna Serikali mngevumilia? Hawa watu wanavumilia hali mbaya lakini kwa sababu gani, tunataka kuwekeza wenyewe kwa kutumia pesa za Serikali kwenye suala la kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Serikali ibaki kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji badala ya sisi wenyewe kwenda, tunatumia hela hii kidogo kwa uchumi huu mchanga tunataka tuwekeze kwenye miradi mikubwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mahesabu ya kawaida kabisa Mheshimiwa Waziri, mipango hii inakwenda kuua uchumi wa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nilitegemea hebu tufikirie upya pesa kidogo tuliyonayo twendeni tukaboreshe maslahi ya wafanyakazi, twendeni tukawekeze kwenye maji, afya na maeneo mengine ya huduma badala ya kuichukua na kupeleka kwenda kuwekeza kwenye miradi ambayo inaweza ikajiendesha kibiashara. Kila siku sisi tunapeleka sura mbaya, tunaanza kuonekana kama vile hatutaki sekta binafsi ifanye kazi katika nchi yetu. Utaratibu huu mbaya utaua uchumi wa nchi yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie hotuba hii ya Wizara ya Maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nianze kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri sana ambayo Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na watendaji Wizarani wanafanya. Tunawaona wanajitahidi, wanakimbia, wanafanya kazi, wanabeba maji vichwani, wanafanya kazi nzuri, nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuongelea eneo la uboreshaji wa Mamlaka mbalimbali za Usimamizi wa Maji. Imefanyika kazi kubwa sana na mfano mzuri ni pale Dar es Salaam (DAWASCO), nadhani kuna maboresho na uimarishaji mkubwa wa Mamlaka ile kiasi kwamba kelele ambazo tulikuwa tukizisikia sana Dar es Salaam zimepungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri tupongeze na kutambua kazi ya Bodi inayoongozwa na Gen. Mwamnyange pia na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hii Ndugu Luhemeja. Nadhani wanafanya kazi nzuri sana. Kwa muda sasa zile kelele ambazo tulikuwa tukizisikia zimepungua, wanajituma, tunawaona mtaani wanafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya maboresho na marekebisho yaliyofanyika kwa Mamlaka ya Dar es Salaam yafanyike na mikoani na kasi iende hiyohiyo kwa Mamlaka zingine. Nadhani itatusaidia sana kwa sababu moja ya eneo kubwa lenye changamoto ni usimamizi. Kwa hiyo, Mamlaka hizi zikiboreshwa wakaiga mfano wa hii Bodi ya Gen. Mwamnyange na mwenzake Ndugu Luhemeja nadhani watakuwa wamefanya kazi nzuri na tutayaona mabadiliko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa kweli napongeza kazi nzuri iliyofanyika Dar es Salaam na sasa ihamishiwe mikoani. Nadhani ni vizuri uimarishaji huu ukaenda pia kwenye Mamlaka zile ndogo za kule chini kabisa na zile Jumuiya za Usimamizi tusiwaachie wananchi peke yake. Usimamizi uwe wa wananchi lakini pengine tupeleke utaalam fulani pale ili kusaidia usimamizi uwe bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka ni Mfuko wa Maji. Mwaka 2018/2019 takwimu za upelekaji wa fedha kwenye miradi ya maji kutoka kwenye Mfuko wa Maji zimepelekwa asilimia 67, napongeza, lakini kutoka kwenye vyanzo vya ndani vingine tumepeleka asilimia 17. Maana yake nini? Maana yake ni kwamba kama isingekuwa Mfuko Wizara hii mngekuwa hamjafanya chochote kwa sababu ingekuwa asilimia 17 peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitatu mfululizo hoja ya kuongeza fedha ili zikaongezeke kwenye Mfuko huu zimekuwa zikija hapa Bungeni. Hoja yangu hapa nachoshangaa huku kutoona kwa Serikali kunakuja kwa sababu gani? Ni kwamba ninyi mkishawaza ndiyo final, hapa tunakuja kufanya nini kama kwa miaka mitatu tunasema hela iongezwe na haiongezwi na Serikali inaendelea na msimamo wake? Tunaletwa kufanya nini hapa, shilingi 50 tu inashindakana kuongezwa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo kwetu sisi umeme ni bora kuliko maji kwa sababu REA tunapeleka shilingi 100 na mambo yanakwenda vizuri na tunaipongeza sana Serikali lakini kwenye jambo ambalo linagusa maisha ya kila mtu hata maskini wa mwisho, hivi tunachoogopa ni nini? Tunachong’ang’ana nacho ni nini? Kwa nini tunataka tulifanye Bunge lionekane halina maana kwa miaka mitatu mfululizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani safari hii Waheshimiwa Wabunge tusikubali. Tumesema na tumebembeleza vya kutosha, safari hii tuweke mguu chini fedha iongezwe, si sawa hivi tunavyoenda. Mimi nimeona hapa tunabembelezana inakuja tunajibishana ooh sijui inflation sijui nini si sawa. Kwa sababu tatizo hili ni kubwa na takwimu zimeonesha bila huu Mfuko miradi yote ingesimama, sasa tusiendelee na kiburi hiki maana kinaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona humu kuna miradi kwa mfano kuna fedha zile wa Wahindi dola milioni 500, hizi fedha zina miradi specific sisi wananchi wa vijijini hizi fedha hazitafika kwa baadhi ya maeneo yetu. Ukombozi wetu peke yake ni huu Mfuko wa Maji.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa Serikali na kwa Bunge…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nape, tusikilize taarifa kidogo.

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokisema kaka yangu Mheshimiwa Nape Nnauye naungana naye kwa silimia 100 siyo tu lazima tupate fedha kutoka kwenye chanzo anachokisema cha mafuta lakini ku- compliment anachokisema Mheshimiwa kaka Nape tunaweza tukapata fedha za kuwasaidia Watanzania hata kutoka kwenye mawasiliano ya simu. Mheshimiwa kaka Nape unachokisema nina ku-compliment safari hii bila kuongeza fedha Wabunge hatutokubali kwa lengo la kuwasaidia watu wetu kwenye sekta ya maji. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nape.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa yake na namshukuru kwa kuniunga mkono. Ni kweli Serikali tukibaki na kisingizo kwamba kwenye mafuta kutaleta inflation hivi chanzo ni mafuta peke yake, je, kwenye simu au data? Hoja yetu hapa ni kwamba huu Mfuko uongezewe chanzo cha fedha, basi. Mnatoa wapi msiende kujificha kwenye mafuta peke yake, Serikali inaweza kufikiria nje ya boksi tukaenda kwenye vyanzo vingine. (Makofi)

Hoja yetu ni kwamba bajeti ya maji safari hii tunaipitisha hapa kama mnakuja na mpango wa kuongeza fedha vinginevyo mtatuona Waheshimiwa Wabunge wabaya. Kwa hiyo, zile siku za mashauriano zikatumike vizuri na Serikali wekeni commitment hapa kwamba mnakwenda kushauriana, nendeni mkabane kwenye vyanzo vingine huu Mfuko tuuongezee fedha tuone maji yanatiririka vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, tatizo kubwa hili la maji linahitaji mikono ya wadau wengi tulete nguvu ya pamoja. Tulitunga sheria hapa ya Kudhibiti Rasilimali ya Maji ya mwaka 2009. Sheria hii ilianzisha pia mabonde, yako mabonde ya usimamizi wa maji ni kama tisa (9) kama sikosei. Huku kuna kanuni zimetungwa za kusimamia, lengo ni jema lakini zimeweka tozo mbalimbali za watumiaji wa maji haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wanatumia maji kwa domestic use, mtu anachimba kisima nyumbani kwake kwanza anatakiwa apewe kibali na anatakiwa akilipie halafu kila mwaka anatakiwa alipe tozo kwa ajili ya kutumia kile kisima. Mimi nasema tukiwatoza watumiaji wa maji ambao wanakwenda kutumia kibiashara sina matatizo nalo lakini hawa ambao ni mtu binafsi ameamua kusaidia watu kwenye eneo lake amechimba kisima kwa fedha zake, ameweka infrastructure kwa fedha zake halafu bado tunaenda kumtoza, actually, nilidhani Serikali badala ya kumtoza ilitakiwa kumlipa kwa sababu anaisadia kusambaza huduma ya maji kwenye eneo lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana mnasimamia na kutekeleza kwa sababu ni suala la kisheria. Ushauri wangu kama ni sheria leteni hapa tufute kwa sababu ni sheria ambayo haina maana badala ya ku-encourage watu wachimbe visima zaidi, kwangu pale Mtama Makao Makuu ya Jimbo kuna watu zaidi ya 50 wamechimba visima halafu unajua kilichotokea nyuma pale walikuwa wanafumbia macho kidogo hivi kwa hiyo watu wanachimba wanaendelea, sasa hivi kwa sababu ya hii dhana ya kukusanya zaidi wameenda kukusanya mpaka madeni ya nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unamkuta mtu ana kisima anaambiwa alipe Sh.700,000 leo, mwanakijiji wa kawaida amechimba kisima kwa hela zake, unachofanya ni kumwambia huyu afunge na akifunga hasara ya nani? Kwa sababu maji yakikosekana hapa mwisho wa siku Serikali itabidi mpeleke fedha za kutibu watu waliougua kwa sababu ya kupata maji machafu, sasa mnachokipata ni kipi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu Serikali kwanza wekeni commitment halafu jipangeni leteni kama ni sheria hiyo tubadilishe, kama ni kanuni nendeni mkakae mzibadilishe. Mimi nashauri wale wanaofanya biashara tena siyo ile biashara ya kuuziana mtaani pale, mtu amechimba kisima anawauzia wenzake pale shilingi tano na yeye mnafanya ni mfanyabiashara, huyu ni mtoa huduma tu. Kuna watu wanafanya biashara, wanaotaka kuzalisha umeme tozeni kodi mnayotaka, wanaozalisha maji yale ya kuuza ya chupa tozeni kodi mnayotaka, wale wanaofanya umwagiliaji mkubwa tozeni lakini watumiaji wa kawaida, nimechimba kisima nyumbani kwangu nataka nijihudumie mwenyewe na majirani zangu, nadhani tukiendelea kutoza si sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mapendekezo yangu Serikali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, Mheshimiwa malizia.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja nikiamini kwamba Serikali itakuja na commitment ya kutosha juu ya hoja nilizoziweka hapa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais (TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora) kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuwapongeza Waziri wa TAMISEMI na Waziri wa Utumishi kutoka Ofisi ya Rais kwa hotuba zao nzuri na jinsi wanavyochapa kazi. Pia nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri wa TAMISEMI, ndugu yangu Mheshimiwa Jafo anafanya kazi nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kuchangia maeneo mawili. La kwanza upande wa michezo kwenye ngazi za chini kwa maana ya wilaya. Ilitokea hoja hapa ya namna ambavyo Wizara ya Michezo inaweza kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI katika kuimarisha michezo kwenye ngazi za chini. Tumeanza mazungumzo na wenzetu wa TAMISEMI tuone namna ambavyo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zinavyoweza kushirikiana na wenzetu wa local government katika kuhakikisha tunaboresha michezo katika ngazi hizo. Mfano mzuri wenzetu wa TFF sasa watashiriki katika mchezo wa mpira wa miguu kwenye UMITASHUMTA na UMISETA na hili liko mahali pazuri na tunakwenda vizuri. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba safari hii michezo hii imeboreshwa sana. Tunaomba ushiriki wao katika kuhakikisha vijana wetu wanashiriki michezo hii vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili, ulifanyika utafiti hivi karibuni na ulifanywa na Waandishi wa Habari Wasiokuwa na Mipaka katika nchi 180 kuangalia uhuru wa vyombo vya habari katika nchi hizo. Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kwamba katika hizo nchi 180 Tanzania ni nchi ya 71. Kwa hiyo, tunafanya vizuri sana duniani katika kuangalia na kutunza uhuru wa vyombo vya habari. Katika Afrika Tanzania ni nchi ya 11 kwa kutunza uhuru wa vyombo vya habari. Kwa Afrika Mashariki Tanzania ni nchi ya kwanza kwa uhuru wa vyombo vya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa matokeo ya utafiti huu ni kwamba tunafanya vizuri. Utafiti huu inafuta dhana inayojaribu kujengwa kwamba nchi yetu inabinya na kuua uhuru wa vyombo vya habari. Hii ni taarifa ambayo imetokana na utafiti si suala la kubuni, ni utafiti umefanyika na taarifa hii imetolewa na iko hadharani na baadhi ya vyombo vya habari katika nchi yetu vimeripoti hii taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, imetokea dhana hapa…
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Na inajengwa kuonyesha kwamba…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waitara naomba ukae, Mheshimiwa Nape endelea.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuonesha kwamba kuna mwingiliano mkubwa kati ya Serikali na mhimili wa Bunge. Baadhi ya wachangiaji wamefikia mahali pa kutoa hoja wakisema studio ya Bunge inaendeshwa na TBC.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Na kwamba TBC wamevaa koti la Bunge na ndiyo wanaoendesha studio.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni huu ufuatao. Studio ya Bunge inaendeshwa na Bunge na inasimamiwa na Bunge lenyewe. Walichofanya studio ya Bunge wameomba msaada wa kitaalamu (technical support) kutoka TBC.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Na sisi Serikali kupitia TBC tumewasaidia kuwapa wataalam hao mpaka hapo watakapofika mahali wakaajiri wataalamu wao.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Kusimama hapa Bungeni na kujaribu kuudanganya umma kwamba studio hii inaendeshwa na TBC maana yake Serikali imeingiza mikono ndani ya Bunge ni uongo wa mchana kweupe. Tunao wafanyakazi wa TBC ndiyo lakini pia wako wafanyakazi waliotoka taasisi zingine ambao Bunge kama taasisi huru inao uwezo wa kuazima wafanyakazi kutoka taasisi zingine kusaidia kutimiza wajibu wake. Hili siyo jambo baya wala siyo jambo geni, nilidhani hili niliweke sawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu na la mwisho. Iko hoja inazungumzwa kwamba matangazo yanayorushwa kutokea hapa…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nape sekunde tatu…
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Sekunde tatu, basi naomba niunge mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi zangu kwa Serikali kwa hatua kadhaa zinazochukuliwa kuboresha sekta ya maji na umwagiliaji nchini, nina mapendekezo yafuatayo:-

(i) Serikali iongeze bajeti kutoka bilioni mia sita hadi at least bilioni mia tisa iliyokuwepo.

(ii) Serikali iangalie uwezekano wa kuanzisha Wakala wa Maji kama ilivyo REA.

(iii) Tozo ya Sh.50/= kwa lita ya dizeli na petroli iongezwe kufikia Sh.100/= kwa lita.

(iv) Suala la majengo nchini kuwekewa miundombinu ya kuvuna maji ya mvua lisiwe la hiari bali liwe la kisheria ili kupata maji ya kutumia lakini pia kuzuia mafuriko nchini.

(v) Suala la sekta binafsi kujengewa mazingira ya kushiriki kikamilifu kwenye sekta ya maji hasa umwagiliaji, kupitia ubia wa Serikali na sekta binafsi (PPP)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ambapo imeeleza mambo mengi kwa kweli ambayo yamefanyika na mengi ameyachukua yaliyofanyika katika kipindi cha miaka mitano ambayo amepewa dhamana na Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Spika, nitoe pole kwa tatizo la Corona linalotukabili Watanzania. Naamini Mwenyezi Mungu atatuepusha pamoja na kuchukua tahadhari mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2015, Chama cha Mapinduzi tulitengeneza Ilani ya Uchaguzi. Wakati tunaitengeneza Ilani tuliweka kazi zitakazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano. Tulipoikamilisha tukaanza kumtafuta mtu atakayefanya kazi tuliyoiweka kwenye Ilani. Wakati ule walijitokeza watu wengi walioomba kazi hiyo na Chama cha Mapinduzi mwishoni tukamteua Mheshimiwa John Pombe Magufuli kufanya kazi ya kutekeleza Ilani. Hakuteuliwa kwa bahati mbaya, tuliona ana uwezo wa kuifanya kazi tunayompa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haikuwa bahati mbaya, chama hiki ni kikubwa sana. Tulitengeneza kazi, tukamtafuta mtu mwenye uwezo, jasiri, mzalendo ambaye atakwenda kutekeleza kazi tuliyompa. Sina mashaka chama hiki kikifanya tathmini leo tuliyempa kazi ameifanya vizuri na hivyo anastahili kupewa tena miaka mingine mitano ya kukamilisha kazi tuliyompa lakini pia tumpe nafasi nyingine kwa sababu amefanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitapitia maeneo machache. Eneo la kwanza, Ilani ya Uchaguzi ilimtaka huyu tutakayempa kazi yeye na Serikali yake, wafanye kazi ya kutafsiri ukuaji wowote wa uchumi kwenye maisha ya kawaida ya Watanzania. Kazi hii imefanyika vizuri sana kwa takwimu ambazo zimo ndani ya hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza lilikuwa ni kwenye afya. Kwenye afya tulitaka tusogeze hizi huduma za afya na kuziboresha. Katika kipindi cha miaka mitano Serikali ya Awamu ya Tano imejenga vituo vya afya 352. Kama uchumi usingekuwa una-perfom isingewezekana kufanya kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki cha miaka mitano zimejengwa hospitali 67 za Wilaya. Hata Jimbo langu la Mtama siyo Wilaya lakini tuna Hospitali ya Wilaya. Kazi hii imefanyika vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna mikoa mipya ambayo ilikuwa haina Hospitali za Rufaa. Mikoa ya Njombe, Songwe, Katavi, Geita na Simiyu zimejengwa Hospitali za Rufaa na kazi inaendelea vizuri. Pia zimejengwa Hospitali tatu za Kanda: Kanda ya Kusini tuna Hospitali Mtwara; Kanda ya Magharibi tuna Hospitali Tabora; na Kanda ya Ziwa inajengwa hospitali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kazi hii, sina mashaka chama changu kitampa fursa tena Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli awe mpeperusha bendera mwaka huu. Sina mashaka kwamba Watanzania wameona tafsiri ya kukua kwa uchumi kwenye huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa umeme, nilikuwa naangalia takwimu mpaka asubuhi tayari tumeshakwenda kwenye vijiji zaidi ya 9,000. Vijijini kabisa umeme unawaka. Kama uchumi ungekuwa hauendi sawa kazi hii isingewezekana. Kazi hii imefanyika vizuri tafsiri yake ni kwamba maisha ya watu yanabadilika, inaonesha kwamba kuna kazi nzuri ya uchumi inakua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, elimu, kila mwezi zinatolewa zaidi ya shilingi bilioni 24 kwenda kwenye elimu bure. Tulisema kwenye Ilani ya Uchaguzi tutatoa elimu bila ada shilingi bilioni 24 kila mwezi zisingewezekana kama siyo kazi nzuri ya kutafsiri ukuaji wa uchumi kwenye maisha ya kawaida ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye maji kuna takwimu nyingi nzuri. Kwenye maji kuna ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miradi mbalimbali ya maji, Arusha, Babati, Dodoma, Kigoma, Iringa, Lindi, Musoma, Morogoro, Moshi, Mtwara, Mwanza, Sumbawanga, Shinyanga na mingine mingi. Kama isingekuwa uchumi umekwenda ndiyo maana fedha zikapatikana kupelekwa huko, kazi hii isingewezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili la kwanza tulimpa Mheshimiwa Dkt. Magufuli alifanye. Mimi kama Mwenezi Mstaafu wa Chama ambaye nilisimamia utengenezaji wa Ilani ya Uchaguzi nataka niseme kazi imefanyika vizuri na tuna sababu ya kumpa tena fursa Mheshimiwa John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, huu ni wakati mzuri wa kufanya tathmini. Kazi ya pili, kwenye Ilani ya Uchaguzi tulimpa Mheshimiwa Magufuli kazi ya kubadilisha utamaduni wa namna tunavyofanya mambo kwenye nchi yetu. Ndiyo maana tukawa na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu, wapo watu wengi pengine hawajui. Tuliiweka kwa makusudi kwa sababu ulianza kujengeka utamaduni, mtu unaweza ukawa unafanya kazi unapata kipato kikubwa hakilingani na kazi unayoifanya. Wakati mwingine biashara hewa au kazi hewa, tukasema lazima tubadilishe utamaduni huu ili nchi yetu iende.

Mheshimiwa Spika, kwenye uchumi ndiyo vyuma vinakaza lakini vinakaza kwa sababu wakati mwingine tulizoea dili, dili zikifungwa kwa vyovyote vile vitakaza. Kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ukisikia kelele maana yake kazi hii imefanyika vizuri. Ndiyo maana itabidi tumpe fursa tena kwa miaka mingine mitano amalizie kazi ambayo alikuwa ameshaianza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye siasa, siasa na yenyewe ilishazoea hivyo hivyo, kuna kelele ndio lakini leo ukiangalia namna tunavyofanya tumekuwa more serious. Nimeona watani zangu CHADEMA wamefanya Uchaguzi, angalia uchaguzi walivyofanya, angalia walivyofanya ACT kwa vyovyote vile kuna mabadiliko hata kwenye namna ya kuendesha siasa zetu ambayo naamini ni kazi nzuri ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina-recommend kwamba kwa kweli Mheshimiwa Magufuli na Serikali yake wamefanya vizuri. Nimpongeze Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Mawaziri, Watendaji wa Serikali, Vyombo vya Ulinzi na Usalama wameitendea haki Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata mtaani hali imebadilika, watu kidogo wako serious, hii ndiyo kazi tuliyomtuma Mheshimiwa Magufuli. Mwalimu alituambia ukiwa unasafisha nyumba unaweza ukafagia shilingi, kufagia shilingi hakufanyi nyumba isisafishwe. Mimi naamini upungufu wa hapa na pale katika kutengeneza mambo haya tukakanyagana vidole yatumike vizuri kutusaidia turekebishe mambo siku za usoni ili Tanzania iendeleee kuwa nchi njema ya fursa ya kila mmoja. Kwa hiyo, kwa kweli niipongeze sana Serikali kwa kazi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu nikupongeze Bunge la Kumi na Moja limefanya mabadiliko makubwa sana ya namna ya kuendesha mambo kutoka Bunge la analojia kwenda Bunge la digitali na mengine mengi ambayo umeyafanya. Utakumbuka Bunge hili la Kumi la Moja ulifanya uamuzi wa kijasiri hapa wa kuamua kuanzisha studio ya Bunge ambayo ni uamuzi ulifanywa na Bunge la Kumi, ukaamua sasa twende tutekeleze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni katika mambo matatu. La kwanza, nimeangalia kwenye randama ya Bunge, nilidhani ni vizuri tukaitengea fedha studio ya Bunge ili ifanye kazi vizuri zaidi. Kwa sababu huyu ni mtoto wako, umemsimamia wewe ndani ya Bunge hili, tusipomtengea fedha ya kutosha bado mambo hayatakwenda sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, tusimuache nyuma kwenye mabadiliko haya ya teknolojia unayoenda nayo na wao tuwape vifaa vya kisasa ili waweze kufanya kazi vizuri. Hii kazi umeisimamia wewe na mimi naamini wananchi wa Kongwa watakuchagua tena urudi uje ukamilishe kazi hii uliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu kwenye studio ya Bunge, nimeona tumeanza kupitia Kanuni za Kudumu za Bunge, si vibaya tukazungumzia Kanuni ya kuendesha hii studio ya Bunge nayo ikawa sehemu ya Kanuni za Kudumu za Bunge ili mambo yakaenda vizuri zaidi. Tupanue wigo ikiwezekana tukafanye coverage hata kwenye Kamati za Bunge na kwenye shughuli mbalimbali za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 na naipongeza Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya. Ni matumaini yangu Chama cha Mapinduzi kitasimama tena na Mheshimiwa Magufuli, ni matumaini yangu Watanzania watamchagua tena turudi kufanya kazi ambayo tulimpa mwaka 2015. Ameifanya vizuri kwa miaka mitano, tumuongezee miaka mingine mitano akamilishe kazi tuliyomtuma. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nachukua fursa hii kuwashukuru kwa dhati wachangiaji wote wa hoja niliyoiwasilisha jana kuhusu Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua michango yao na ninashukuru sana kwa hoja mbalimbali zilizotolewa, hoja ambazo kwa namna moja ama nyingine zimesaidia katika kuboresha muswada tuliouwasilisha hapa. Pia nyingine naamini zitatumika wakati wa kuandaa kanuni zitakazosaidia utekelezaji wa sheria tutakayoipitisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikufahamishe kuwa tumepokea michango kwa njia ya maandishi na kwa njia ya uchangiaji wa kuongea moja kwa moja wakati wa kuijadili hoja niliyoiwasilisha hapa jana. Naomba kutambua maoni na mapendekezo mazuri yaliyotolewa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii; maoni ambayo yalisomwa hapa na Mwenyekiti wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kuiongoza Kamati yake na kupata maoni aliyoyawasilisha hapa. Nampa pole kwa kunyooshewa vidole sana na wengine mpaka wakampa majina mabaya, wakamwita jipu. Ukweli ni kwamba kama kuna jipu, basi jipu lilikuwa huu muswada usioisha na leo tunautumbua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kutambua maoni yaliyotolewa na Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo ndani yake yako mawazo mazuri ambapo kama Serikali tumeyaona na yale ambayo yatahitaji kuzingatiwa kwenye kanuni, tutayazingatia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iko michango ya Waheshimiwa Wabunge mbalimbali. Tumepokea michango na hoja zaidi ya 94 ikiwa ni michango ya maandishi kama nilivyosema pamoja na wale waliozungumza. Kamati ya Bunge imetoa hoja karibu 30, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni hoja 28; Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa njia ya maandishi walikuwa kumi; waliochangia kwa njia ya mjadala ni Wabunge 26.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kupitia hoja moja baada ya nyingine, nitajibu hoja chache kwa ujumla. Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kauli yake ya kutia moyo sana aliyoitoa jana kwamba yuko tayari kui-sign sheria hii tukiipitisha hapa siku yoyote ikifika mezani kwake. (Makofi)
Namshukuru kwa moyo huu na ni uthibitisho kwamba ana mapenzi mema na tasnia hii na ndiyo maana yuko tayari kutia sign sheria hii tukiipitisha. Na mimi natoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuipitisha sheria hii, tumpelekee Mheshimiwa Rais akai-sign. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiona marekebisho tuliyoyawasilisha Bungeni, yako mengi, ni ushaidi na uthibitisho tosha kwamba Serikali ya Awamu ya Tano licha ya maneno mengi ya washindani wetu, ni Serikali sikivu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulileta muswada, umejadiliwa; maoni yametolewa. Namshukuru Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hata jana hapa wakati Waheshimiwa Wabunge wanachangia, katika michango yao akaona haja ya kuendelea kufanya marekebisho. Huu ni ushahidi kwamba hii ni Serikali sikivu sana, tofauti na maneno yanayosemwa kwamba siyo sikivu. Ingekuwa siyo sikivu tungeweka mguu chini na muswada tuliouleta hapa, lakini mapendekezo haya ya marekebisho tunayoyaleta yanathibitisha kwamba tumesikiliza ushauri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipitie hoja chache. Nawashukuru wenzangu, wachangiaji wote ambao pamoja na kuchangia, lakini walijitahidi kujibu baadhi ya hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge wenzetu. Nawashukuru sana Mawaziri wenzangu, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, Mheshimiwa January Makamba, Mheshimiwa Possi na Naibu Waziri, kwa kazi nzuri ya kujibu baadhi ya hoja. Sasa ziko hoja chache nitazigusia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni hoja ya ushiriki wa wadau; imekuwa ni hoja inazungumzwa ndani ya Bunge lako, lakini pia imezungumza hata nje ya Bunge. Pengine labda ni suala la kukumbushana. Ushiriki wa wadau katika utungaji wa sheria ya namna hii, uko wa awamu mbili. Awamu ya kwanza ni awamu ya ushiriki wa wadau wakati Serikali inafanya maandalizi ya muswada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakati inafanya maandalizi ya muswada inao wajibu wa kuwashirikisha wadau kuhakikisha inapata maoni yao kabla hata ule muswada haujapitishwa kwenye Baraza la Mawaziri. Utaratibu huo tuliufuata, wadau wakateta maoni yao na maoni yao yapo kwa maandishi kwa ushahidi, yapo. Walishirikishwa vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata pale ambapo Serikali kwenye vikao vya juu waliona ushiriki bado hautoshi, Wizara iliagizwa kuongeza wadau wa kutoa maoni na tulifanya hivyo na ndiyo maana Baraza la Mawaziri likaridhia kwamba muswada huu uletwe hapa ndani ya Bunge lako. Hii ni awamu ya kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili, ni baada ya muswada kusomwa kwa mara ya kwanza ndani ya Bunge, ambapo ukishasomwa, inakuwa sasa ni wajibu wa Kamati ya Bunge kuwataka wadau kuja kutoa maoni yao na kwa kweli wadau ni hawa hawa ambao Serikali ilikutana nao, wakatoa maoni yao. Hii awamu ya pili wanaitumia kuja kuangalia ni kwa namna gani maoni yao walioyatoa kwa Serikali yamezingatiwa kwenye muswada uliosomwa kwa mara ya kwanza ndani ya Bunge. Huo ndiyo utaratibu ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii awamu ya pili walipokuja, ndiyo hapo pakawa na mgawanyiko; wakatokea ambao waliamua kutoa maoni yao, lakini wakatokea ambao waliamua kutotoa maoni yao. Na mimi naamini pamoja na maneno mengi yaliyosemwa, wale walioamua kutotoa maoni yao, pengine kwa namna moja ama nyingine waliridhika sana na namna tulivyozingatia maoni yao kwenye muswada na ndiyo maana hawakuona sababu ya kutoa maoni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nilihakikishie Bunge lako kwamba muswada huu tunaoujadili na tutakaoupitisha leo ninaamini ni muswada ambao umezingatia sana maoni ya wadau na hivyo hatuna sababu ya kuwa na mashaka kwamba muswada huu haukuzingatia maoni ya wadau.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ambayo umeguswa na watu wengi kidogo, lakini inagusa hisia, ni hoja ya tofauti ya muswada tuliouleta na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976. Ni hoja ambayo imezungumzwa kwa hisia kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inanishangaza, unless tunataka kufanya siasa za uchochoroni; lakini kama nia yetu ni kujadili kwa ukweli, mtu anayesema muswada huu hauna tofauti na sheria ya mwaka 1976 ninapata shida sana kumuelewa kwamba hata lile ambalo halihitaji kwenda kusoma sana kujua yako mambo yana utofauti, nalo hili linapigiwa kelele hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 ilikuwa inampa Waziri mamlaka makubwa mno ukilinganisha na mamlaka ambayo Waziri anapewa kwenye muswada tuliyouwasilisha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulichofanya kwenye muswada huu; na hii ni nia ya dhati ambayo nimeieleza hadharani, siyo mara moja, siyo mara mbili; ni kwamba tunataka tupunguze control ya Serikali kwenye uendeshaji wa vyombo vya habari, badala yake tuchukue jukumu hilo kulipeleka kwenye Baraza Huru la Wanahabari ambalo linaundwa na wanahabari wenyewe na ndiyo msingi wa kuwa na Baraza Huru la Habari katika nchi yetu. Maana yeke ni moja tu kwamba tunapunguza mamlaka ya Waziri; na yamepunguzwa kwa kiasi kikubwa mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukisoma Muswada vizuri, Baraza Huru la Habari, moja ya kazi waliyopewa ni kuunda Kamati ya Malalamiko. Kamati hii itashughulikia malalamiko yanayotokana na uendeshaji wa magazeti na vyombo vya habari katika nchi yetu, ambapo Kamati hii pia iko kwenye TCRA upande wa utangazaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilichofanyika ni nini? Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kila kosa likifanyika, likishtakiwa linakuja Idara ya Habari - Maelezo, linakwenda kwa Waziri na Waziri ana discretion ya kusema kwa kosa hili nakufungia miezi mitatu, ninakupiga mwaka au nakufuta kabisa. Mamlaka hayo yalikuwa yako kwa Waziri kwa makosa yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada huu tuliouwasilisha, tumemwachia Waziri makosa mawili tu; usalama wa taifa na afya ya jamii. Haya ndiyo ambayo tumemwachia Waziri ashughulike nayo. Makosa mengine yote tumewapelekea Baraza la Habari washughulike nayo. Kweli tunasema huu muswada unafanana na sheria ya mwaka 1976? Siyo sawa sawa hata kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu umepunguza sana mamlaka ya Waziri, sana. Sheria ya mwaka 1976; chombo cha habari wakiandika story, chombo kizima cha habari kinabeba dhamana, chombo kizima, ndiyo maana iko mifano. Gazeti la Mawio nililifuta kwa kutumia sheria ya mwaka 1976. Pale walikuwa wana wafanyakazi ambao kwa namna moja ama nyingine hawahusiki kabisa na ile story, lakini unafuta gazeti zima, unaadhibu hata wasiohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii ambayo tunataka kuipitisha hapa, inashughulika na taaluma ya mtu mmoja mmoja. Kwa sheria hii, tutashughulika na mwandishi na taaluma yake badala ya kufungia chombo kizima. Bado tunaona inafanana tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi hata hili kweli hatulioni? Tumezungumza hapa, kwa sababu inawezekana ndani ya chombo cha habari kukawa na mtu mmoja au wawili wakorofi, ndio wanapitisha story za ovyo. Sasa kupitisha kwao story kusimwathiri mhasibu, mhudumu, mfuagiaji au mwanasheria mwingine; hii sheria inakwenda kutatua tatizo hilo. Bado tunasema inafanana na sheria ya mwaka 1976. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya mwaka 1976 imeingiza mchapishaji (printers) kwenye kosa. Ndiyo maana yako makosa kwa mfano yale waliyoshtakiwa kina Kibanda na wenzake, iliwaingiza kina Makunga kwenye kesi kwa sababu wana mtambo wa kuchapisha. Sheria tuliyoileta hapa imezingatia mabadiliko ya teknolojia duniani kwamba leo unaweza ukatengeza gazeti lako Dodoma ukalituma Mwanza, likaingia mtamboni lisikutane na mtu, likachapishwa, likatengezwa, likachukuliwa, likapelekwa mtaani. Tukasema kwa mabadiliko haya ya teknolojia, tukiendelea na sheria ya mwaka 1976 tunakuwa hatumtendei haki huyu ambaye ana mtambo kwa sababu hana room ile ya kwenda kuliona gazeti. Tukaweka tu exceptional mahali ambapo, huyu mwenye mtambo ataamua kufanya makusudi; gazeti limefungiwa, yeye anafanya makusudi ya kuchapa; huyu tutamkamata. Sasa unasemaje sheria inafanana na ya mwaka 1976? Ya mwaka 1976 imemweka printer; ya mwaka 2016 imemuondoa printer; na bado tunaona ni vitu vinavyofanana, unless tunacheza siasa. Kama tunataka kuambiana ukweli, hizi ndiyo facts. Huu ndiyo ukweli. Hata siasa zenyewe basi, siasa gani za majitaka?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya mwaka 1976 haina Baraza Huru la Habari, haina! Sheria hii tunaweka Baraza Huru la Habari ambalo linajiendesha lenyewe. Hata hili linahitaji shule kujua kwamba sheria hizi hazifanani? Acha mambo mengine, sheria ya mwaka 1976, hapa pana hoja zilikuwa zikizungumzwa; hoja ya namna ya kuwalinda waandishi wa habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya mwaka 1976 ilikuwa haiwalindi waandishi wa habari, ndiyo maana leo yuko mwandishi wa habari mmoja anitwa Athuman Khamis nadhani, alipata ajali wakati wa kazi, ame-paralyze mwili mzima, yuko ombaomba kabisa. Ukiangalia anavyoishi, anaishi kwa shida, kwa taabu, lakini ametumikia sekta hii. Hapa tunasema, tumwekee bima ya mazingira ya kazi yake ili hata kama ikitokea amepata majanga ya namna hiyo, bado aendelee kuishi kwa sababu amechangia kwenye maendeleo ya nchi yetu. Tunasema kweli bado haifanani. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kutakuwa na bima ya mazingira magumu, ukiacha bima za afya, lakini inasema pia sheria hii ya mwaka 2016 tukiitunga, inataka tuweke masharti ya umiliki wa chombo cha habari ambapo kule ndani tutatunga kanuni zitakazombana mmiliki wa chombo cha habari kuhakikisha anampa mkataba mwandishi wa habari. Leo tuna waandishi wa mabari ma-day worker wanalipwa shilingi 50, 000 kwa mwezi. Matokeo yake, huyu akipewa pesa ndogo akapewa story atakwenda akakupige tu, halafu mtajuana huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya mwaka 1976 haikuwa na mfuko wa kuwaendeleza wanahabari, wanajiendeleza wenyewe kama kuku wa kienyeji. Sheria hii tunatunga mfuko wa kuwaendeleza wanahabari. Hapa kuna jambo tunataka kutibu. Leo hili la shule sitaligusa, limegusiwa sana, lakini niwaambieni ndiyo maana magazeti mengi leo, nenda kaangalieni lead story ya magazeti yote wana-lead story na story za siasa. Kwa nini hawaendi kwenye kilimo au uchumi? Kwa nini hawaendi huko? Elimu. Ni rahisi kuandika habari za siasa, Nape kamtukana huyu, kamtukana yule; lakini tukiwabana kwenye elimu, watu wakawa wachumi hapa, watu wakajua kilimo chetu, wataandika vizuri na wananchi wanataka wapewe taarifa hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku moja, Katibu Mkuu Kiongozi (Chief Secretary) alitoa taarifa, ameiandika. Taarifa ya idadi ya Wakuu wa Wilaya walioteuliwa na walioachwa. Alipoitoa ile taarifa, magazeti manne yalitoa takwimu nne tofauti na zote zilikuwa kwenye lead story.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtoa taarifa huyu, mmoja, kaisema, kaiandika, lakini waandishi walipoenda kuitafasiri, wakatoa takwimu nne tofauti. Tunataka kumlisha Mtanzania kitu gani? Kuna kitu kinapikwa na vyombo vya habari kwenda kuwalisha Watanzania; tunataka kitu hiki kipikwe kikiwa kizuri. Namna ya kuwa kizuri, lazima tumpe elimu ya kutosha ili atoe jambo zuri mbele ya safari, unless tunataka kuiua hii tasnia. Kama lengo letu ni kuifanya iwe tasnia bora, hii ndiyo njia ya kuifanya kuwa tasnia bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mabadiliko na marekebisho hayo, bado kama lipo jambo zuri kwenye sheria ya mwaka 1976 halitufanyi tusilichukue tukaendelea nalo. Zipo sheria ngapi tumeendelea nazo hata kama zilitungwa miaka ya 1800? Nyingi tu, ili mradi lipo jambo zuri, unaifuta sheria ya msingi, lakini unabeba vitu vichache ndani ya sheria hiyo kama vitakusaidia katika mazingira uliyonayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tunataka tuwaaminishe watu kwamba kwa kuwa sheria ya mwaka 1976 imepigiwa kelele, basi sheria nzima ifutwe? Hii siyo sawa. Nadhani tusifike huko, tutendee haki nafasi tulizopewa, tushauri, tutunge sheria nzuri itakayofaa kuendesha tasnia yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ambalo nilidhani niligusie ni suala la uhusiano wa Bodi ya Ithibati na Baraza Huru la Habari. Kumekuwa na mkanganyiko mwingi sana hapa kuhusu nani ni nani; nani anafanya nini na mpaka wengine wanakwenda mbali wanasema Waziri amejipa madaraka makubwa mno kwenye hivi vyombo. Unless tumesoma hatukuelewa; au tumeamua kupotosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muswada unazungumza wazi, vizuri, kwamba tutakuwa na Baraza Huru la Habari ambalo litaundwa na wanahabari wenyewe. Baraza hili Huru la Habari litaundwa na kila mwanahabari ambaye amekuwa accredited. Hakuna mkono wa Waziri kwenye Baraza hili. Ni Baraza ambalo tumelitofautisha na Baraza lililopo sasa hivi (MCT) ambalo kwa kweli kimsingi ni NGO. Nenda kasome sheria vizuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia kimsingi tumelifanya liwe Baraza huru ambalo wajumbe wake ni wanahabari ambao wamekuwa accredited; watajichagua wenyewe, wataunda kamati wenyewe na tena ni kadri wanavyotaka, wataziunda na watatunga kanuni za kujiendesha wenyewe. Hawapewi hela na Serikali, hivi Serikali inali-control vipi hili Baraza mpaka inasemekana kwamba kuna mkono mkubwa wa Serikali humu ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hapa yapo maslahi na leo nataka niyaseme. NGO inayoitwa MCT walikuwa wanapata pesa nyingi sana kutoka nje, mabilioni ya pesa, nyingi tu kutoka nje. Sasa hapa tuna tatizo; kuna watu wanatetea ulaji wao. Wanatetea ulaji at the expense ya maisha ya waandishi wetu katika nchi hii. Mimi nitakuwa Waziri wa ovyo sana nikikubali utetezi wa namna hiyo. Mnatetea ulaji, tuache kuanzisha Baraza lenye tija kwa waandishi wa habari tuendelee kuhangaika na MCT ambayo kazi yake ilikuwa ni kupokea pesa kutoka nje? Hapana, si sawasawa. Tutendee haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Baraza hili liko huru, wanajitungia kanuni zao wenyewe. Tena kuna watu wanahusisha, sana sana nasikia vijembe wanatupa, kwamba wanasema bodi. Bodi ni chombo kilichotengenezwa ku-enforce, kutekeleza maamuzi yatakayofanywa na Baraza. Ni jambo la kawaida kabisa katika utungaji wa sheria wa aina yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tulichofanya, Baraza Huru la Habari tumesema watatengeneza mpaka code of ethics za kuendesha taaluma ya habari. Wakishazitengeneza, kipo chombo hapa pembeni kinaitwa bodi na kinatengenezwa na Serikali; kazi yao moja tu, kutekeleza yale yaliyoamuliwa na Baraza kule. Tatizo linatoka wapi hapa? Tunabishana nini katika hili? Sasa mahusiano yake ni hayo tu. Bado hata bodi yenyewe, uundaji wake ina wajumbe saba, katika Wajumbe saba, wanne ni wanahabari, wametokana na Baraza lenyewe; lakini bado aah, unajua, unajua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachodhani, hapa pana shida ya kutoaminiana. Mjumbe mmoja leo amethibitisha, anasema hatuamini kama Mheshimiwa Nape ataleta jambo jema ndani ya Bunge hili. Nadhani sasa hii ni perception yake na hii hainihusu wala haitusumbui.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakachofanya, naamini Waheshimiwa Wabunge mtatuunga mkono, mtaunga mkono marekebisho tuliyoyaleta na tutapitisha Muswada huu kuwa sheria na tutampelekea Mheshimiwa Rais kama alivyoaihidi, atakwenda kusaini na itakuwa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa muda, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa maoni yenu. Ahsanteni sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.
Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na nichangie kwa kifupi sana. Nianze kwa kumpongeza sana Waziri wa Ulinzi, Mheshimiwa Dkt. Mwinyi kwa kazi nzuri anayofanya. Kazi hii anaifanya kwa unyenyekevu na uadilifu mkubwa tunakupongeza sana Dokta. Pia nilipongeze jeshi letu kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya. Nchi yetu inaendelea kusifiwa kuwa na amani na utulivu kwa sababu ya kazi yao nzuri wanayoifanya, ahsanteni sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kuweka rekodi sawa, kwenye hotuba ya Kambi ya Upinzani, ukurasa wa 11, wamenukuu Katiba ya CCM, Ibara ya 80(1)(c) na 94(1)(c). Bahati mbaya sana na nadhani ni kwa makusudi, wamenukuu nusu ya Ibara hizo na wakaamua kwa makusudi kupotosha ukweli. Sasa nimesimama kuuweka ukweli sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wao wamenukuu Ibara ya 80(1)(c) lakini (d) inasema hivi, Mkuu wa Wilaya ambaye anatokana na CCM. Ukienda Ibara ya 94(1)(c) inasema, Mkuu wa Mkoa ambaye anatokana na CCM. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya nafasi hizi zinateuliwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika Katiba na sheria zote zinazosimamia uteuzi huu sifa ya kuwa mwanachama wa chama cha siasa haipo. Kwa hiyo, mtu yeyote anaweza kuteuliwa kwenye nafasi hizi bila kujali chama chake cha siasa
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Sikilizeni, kwa utaratibu huo ndiyo maana katiba ya CCM imeeleza Wajumbe wa Kamati za Siasa ambao wao wanalalamikia kwamba hawa ni wajumbe imeeleza wajumbe hao ambao ni Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa ambao wanatokana na CCM, siyo kila Mkuu wa Wilaya ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya CCM na siyo kila Mkuu wa Mkoa ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na ushahidi upo. Tunao Wanajeshi ambao wameteuliwa kuwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya na kadri tunavyoongea sasa hakuna hata mmoja ambaye amehudhuria kikao cha Kamati ya Siasa ya Wilaya wala ya Mkoa na ushahidi upo. (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri ni vizuri tusitumie Bunge hili kujaribu kupotosha ukweli na kujaribu kulipaka matope jeshi letu…
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Jeshi letu linafanya kazi nzuri, tuache unafiki, tunasimama tunawapongeza tunasema wanafanya kazi nzuri wakati huo huo tunatumia mlango wa nyuma …
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe mfano wa wazi kabisa kwa sababu bahati mbaya sana Bunge hili linataka kutumika kucheza siasa za hovyo. Alikuwepo Brigedia Jenerali Balele, aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga akiwa amestaafu. Alipofika Shinyanga akaenda Ofisi ya CCM, alipofika Katibu wa Mkoa alikuwa anaitwa Agusta Muba akamuuliza Jenerali wewe una kadi ya CCM? Huwezi kuingia kwenye vikao vya CCM kama wewe siyo mwanachama wa CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana, mimi hapa sizungumzi kama Katibu Mwenezi, uenezi nilishaacha huko, wenzetu wamekuwa na utamaduni wa kutoheshimu Katiba za vyama vyao. Katiba ya CCM inasema Ukuu wako wa Wilaya, Ukuu wako wa Mkoa haukuingizi kwenye vikao hivi. Katiba ndivyo inavyosema na tunaisimamia. Isipokuwa uanachama wako plus Ukuu wa Wilaya na Ukuu wa Mkoa wako, kama siyo mwanachama huingii na hapa ninapozungumza tunao Wakuu wa Mikoa ambao ni Wanajeshi hawajastaafu na hawaingii kwenye vikao vya CCM. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vizuri tukaweka rekodi sawa; ukizoea vya kunyonga vya kuchinja vinakua tabu. Acheni uwongo na kutaka kuwadanganya Watanzania kwa mlango wa nyuma. Liheshimuni jeshi kwa maneno na matendo yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru, ahsante kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye hoja. Kwanza nimpongeze sana Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya. Najua, yako maneno mengi watawasema lakini sisi wenzako tunajua unafanya kazi nzuri na tunakuunga mkono endelea kufanya kazi hiyo.
Pili, nilipongeze sana Jeshi letu la Polisi kwa kazi nzuri waliyofanya na hasa wakati wa uchaguzi mwaka jana. Uchaguzi ule umekwisha kwa amani na utulivu kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa na Jeshi la Polisi. Jeshi la Polisi endeleeni kufanya kazi hiyo, msisikilize kejeli zinazoelekezwa kwenu, Watanzania wanajua mnafanya kazi nzuri pamoja na mazingira magumu endeleeni kufanya kazi hiyo nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ambalo nilidhani ni vizuri tukaliweka sawa. Hapa pamefanyika utaratibu ambao ulifikia uamuzi wa Kamati ya Kanuni kwenda kushughulika na hotuba ya Kambi ya Upinzani Bungeni. Bahati mbaya sana ninachokiona hapa, kunatengenezwa upotoshaji kama vile kulikuwa na hoja ngumu, nyingi Serikali imeziona, ikaona tabu kuzijibu, kwa hiyo ikatengeneza utaratibu wa kukimbia. Utaratibu huu wa kupotosha mambo, unaendelea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo liko wazi, kila mahali na hapa Bungeni pana utaratibu wake, wenzetu wamezoea kunyonga, wanapoambiwa kuchinja wanapata tabu. Mimi wala sipati tabu na kelele zao kwa sababu ndivyo walivyofundishwa, wasipoipenda hoja wanatakiwa wazomee, endeleeni kuzomea. Hata hivyo, nataka tuweke jambo hili sawa, kilichofanyika hapa ni utaratibu wa kawaida wa Kibunge, kuna kanuni zake, wamekwenda wamekaa wameshauriwa, hawataki walichoshauriwa wameamua wenyewe kuweka mpira kwapani na kuondoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni vizuri Watanzania wakaujua ukweli huu kwamba wenzetu hawapendi kufuata kanuni na taratibu ndiyo maana wanafanya walichofanya na ndiyo maana hata humu ndani wataendelea kuzomea kwa sababu ndiyo taratibu zao.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hili lilikuwa la kwanza na nadhani limeeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, imetolewa hoja hapa kwamba, Serikali hii haina uwezo wa kuongoza nchi, lakini nataka nimwambie Mchungaji wangu Msigwa, Watanzania ndiyo wametupigia kura, wakatuamini, wakatuleta hapa na kwa muda mrefu siyo jana wala juzi, mmekuwa mkiwaomba wawaamini wamekataa kuwaamini. Wameendelea kutuamini siye na wanatuamini kwa sababu wanaamini tunaweza, tunajua na ndiyo maana wameendelea kutupa na wataendelea kutuamini kuturudisha hapa.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mmeendelea kutoaminiwa kwa sababu ya ukigeu geu mnaoendelea nao mpaka leo, kwa hiyo tupo hapa kwa sababu Watanzania wanataka tuwe hapa, wanatuamini na wataendelea kutuamini na kwa kazi nzuri tunayoifanya, wataendelea kutuamini, kwahiyo hili halina mjadala.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya mwisho. Imetolewa hoja hapa pia, inatuhumu kwamba Jeshi la Polisi limekuwa likitumiwa na Chama cha Mapinduzi hasa kwenye uchaguzi. Nadhani hili nalo si suala la kuliacha liendelee kuzungumzwa, kama Jeshi la Polisi na hapa maneno haya ni ya kulidharau na kulidhalilisha Jeshi la Polisi na ndiyo maana Mheshimiwa Lwakatare anasema, hawa jamaa laini sana maana yake Jeshi la Polisi laini sana. Hivi kama kweli…
MWENYEKITI: Order. Ahsante Mheshimiwa Nape.
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, WASANII NA MICHEZO: Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie na nianze kwa kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano hasa katika eneo hili la maliasili na utalii, ziko juhudi kadhaa zimefanyika na kwa kweli zinaonekana kwamba zinaweza kuzaa matunda mazuri. Ninaamini kwamba yako mambo yakiboreshwa tutapata matokeo mazuri zaidi, na nimefurahi leo nimemsikia rafiki yangu Musukuma akichangia hapa kwa ukali kidogo na nadhani ukali ule alioutumia ndio ukali tulikuwa tukiutumia hapa kuchangia kwenye maji na maeneo mengine na bahati mbaya wakati mwingine ukichangia kwa kueleza hisia za wapigakura wako unaonekana kama unashambulia Serikali hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa tupo kuboresha, kinacholetwa hapa kinaletwa mapendekezo ya Serikali, tunapochangia lengo ni kuboresha ili tutoke na kitu kizuri zaidi kwa faida ya Watanzania, bila kujali mitazamo mbalimbali iliyoko hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni suala hili la migogoro ya hifadhi na wananchi wanaozunguka maeneo hayo. Hili limekuwa tatizo la muda mrefu sana na limekuwa likizungumzwa sana na kunaonyeshwa nia ya Serikali ya kulimaliza, lakini likiendelea kutolea kwa ahadi kama ambavyo limekuwa likitolewa halitakwisha.

Ushauri wangu Mheshimiwa Waziri hebu njooni na time frame ya kushughulika na tatizo hili kwa sababu liko mahali kwingi na limeumiza watu sana. Na ukisoma kwenye hotuba humu wanazungumza habari ya kuweka zile beacons, mimi nadhani badala ya kuendelea na utaratibu huo na kwa sababu hifadhi nyingi hizi ziliwekwa miaka ya 1974 wakati population yetu ilikuwa ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda leo ene la Mkoa kama Tabora karibu eneo zima ni hifadhi, watu wameongezeka sana, sasa mkiendelea kuweka mipaka kwa kufuata uamuzi huo huo wa mwaka 1974 nadhani tutakuwa hatutendi haki kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ushauri wangu mimi nilidhani sitisheni utaratibu wa kuweka mipaka fanyeni tathimini kama kweli bado tunahitaji kutunza eneo kubwa kiasi hicho katika mazingira ambayo population imeongezeka sana, halafu tukishafikia uamuzi ndio tuweke mipaka ambayo itatupeleka kwa miaka mingine mingi zaidi mbele na katika hili pamoja na time frame mmekuwa mnaweka utaratibu wa task forces mbalimbali za kushughulikia matatizo kama haya. Mimi nilidhani katika hili kama nia ya dhati ya Serikali ni kulimaliza kwanza tuweke time frame lakini tutengeneze task force ipewe muda maalumu iende ikalimalize tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala la biashara la kusafirisha viumbe hai. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ambaye nakiri anafanya kazi nzuri amesema wazi kwamba walisitisha biashara hii kwa miaka mitatu. Naanakiri kwamba baada ya kusitisha imefanyika tathimini kwenye mazizi ya wale ambao walishakusanya hawa viumbe hai na mwishoni anazungumza kwamba tathimini hiyo lengo lake ni kutoa kifuta jasho kwa wafanyabiashara walioathirika na katazo hilo. Sasa kwanza kitendo cha Serikali kukiri kwamba wamefanya tathimini na wana nia ya kutoa kifuta jasho maana yake ni kukiri kwamba yako makosa katika uamauzi huu, ambao mimi nadhani ni jambo la kiungwana kwamba kuna watu wameathirika hawakustahili kuathirika lakini wameathirika na uamuzi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu mimi nilidhani la kwanza hawa watu wasisubiri hiyo miaka mitatu iishe, Serikali iruhusu hawa watu wasafirishe viumbe hai hawa ambao walishawakamata na waliwakamata wakawaweka kwenye mazizi yao kwa kufuata utaratibu, wamepata lesini, wamelipia kodi na wengine wamechukua mikopo kwenye mabenki na wengine walishalipwa pesa za utangulizi kabla ya kupeleka hawa viumbe kule nje. Kwa hiyo, mimi nilidhani badala ya kuzungumza habari ya kivuta jasho hapa izungumzwe habari ya fidia. Kwa sababu hawa watu wamepata hasara kutokana na uamuzi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili uamuzi huu utenguliwe na Mheshimiwa Waziri mimi niko tayari kukamata shilingi yako leo hapa utengue huu uamuzi, hawa watu ambao kwa kweli hawakustahili kuadhibiwa nilikuwa naangalia zinapokiukwa sheria, kulikuwa na matatizo hapa katika uwindaji, kuna baadhi ya makampuni yalikiuka sheria hatukuwaadhibu wote walioshughulika na uwindaji, tuliwaadhibu wale waliokiuka sheria. Kwa hiyo, hata katika hili mimi sikuona sababu ya kuwaadhibu wote waliokuwa wanafanya biashara hii. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba walioathirika wapate fidia, lakini uamuzi huu sasa ufutwe na waruhusiwe kupeleka wanyama wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Waziri kwanza tumepoteza masoko, tumepoteza imani ya wale ambao walikuwa wanaamini kwamba biashara hii ingeendelea lakini kwa takwimu inaonekana hata wanyama wanaopelekwa ni kidogo sana, lakini mwisho wa yote Mheshimiwa Waziri nyuma ya jambo hili kuna harufu ya rushwa. Pengine inawezekana wasaidizi wako hawakwambii lakini kunahalufu ya rushwa na inazungumzwa wazi wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo la kwanza nilidhani uamuzi huu tusizungumze habari ya kifuta jasho, tuzungumze habari ya kufidia, la pili, tusiendelee na uamuzi huu hasa kwa wale ambao kwa kweli hatuna shida nao wale ambao tayari walishakamata wanyama, wamekopa mikopo, wanawafanyakazi wao, lakini walishachukua advance payment za kusafirisha hawa viumbe kuwapeleka nje. Tubadilishe kwenye hili na tukifanya hivi tutakuwa tumewaokoa na kwa sababu sheria ilishabadilishwa biashara hii ifanywa na wazawa. Kuna mikono ya wageni, lakini biashara hii inafanywa na wazawa, mimi nilidhani tuisimamie na tuwasaidie Watanzania hawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nchi yetu ina utajiri mkubwa wa utamaduni tuna makabila karibu 126 mimi nadhani umefika wakati sasa kwa kushirikiana na Wizara ya Utamaduni tuende tukawekeze kwenye utalii wa utamaduni wetu. Na mimi nadhani tukiwekeza huko tutapata faida kubwa, huu utamaduni usipowekezwa kitalii ukaanza kutuingizia pesa utaanza kupotea taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nenda kaangalie leo tamaduni kama za Wamasai, Wamakonde, Wasukuma, Waha ni tamaduni ambazo zinaweza kuvutia utalii na uwekezaji wake sio mkubwa sana, uwekezaji wake mdogo sana ni kuutengeneza tu utamaduni ule ukae katika mazingira ambayo mtu akija anaweza akajifunza, anaweza akafanya utalii wake na wapo ambao watafanya tafiti mbalimbali katika utamaduni wetu. (Makofi)

Sasa mimi nazani tukiwaachia Wizara ya Utamaduni peke yake hawataweza, lakini sisi Wizara ya Maliasili na Utalii tunaweza tukawekeza katika utajiri huo wa utamaduni ambao tunao wenzetu wakaja wakajifunza. Mimi nimekwenda Bujora pale, pana mkusanyiko wa utamaduni mkubwa sana wa Wasukuma, lakini nenda Kusini Wayao, Wamakonde...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye Wizara hii ya Viwanda, Uwekezaji na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa juhudi ambazo zimeanza kuonekana za kufufua viwanda na hasa kwa kweli viwanda vya korosho. Jimboni kwangu kuna kiwanda wamefufua, lakini na maeneo mengine tumeanza kuona juhudi hizi zinakwenda na nadhani hatua walizochukua zinakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba naunga mkono, vile viwanda vilivyobinafsishwa na havikufanya vizuri, kwa sababu mikataba ipo na wengi hawakufanya sawasawa na mikataba na ukisoma ripoti zote zinaonyesha kwamba, wengi walipobinafsishiwa viwanda hivyo, wakavitumia wakaenda wakakopa na pesa zile zikaenda maeneo mengine. Mheshimiwa Mwijage aache upole, achukue hatua tuwadhibiti watu waliofanya kinyume na tulichokubaliana. Pamoja na kazi nzuri ambayo mmeanza kufanya, ningeshauri maeneo machache yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza Mheshimiwa Mwijage tuna shida kubwa ya tafsiri tuliyonayo juu ya nini tunakiita ni kiwanda. Ukiangalia maeneo mengi ukitaja idadi ya viwanda ambavyo vimeanza kujengwa watu wanaangaliana usoni, kwa nini? Kwa sababu tunalo tatizo la tafsiri ya pamoja ya kukubaliana hivi kiwanda hasa ni nini? Ni lile dubwashika kubwa au hata nikiwa na karanda kangu bado tunakaita viwanda, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri akitoa idadi ya viwanda hapa aasema elfu tano, elfu kumi, elfu ngapi, wakati mwingine watu wanaangaliana wanapata mashaka na tunachokisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani Mheshimiwa Mwijage kwenye hitimisho lake hebu tuzungumze tunaposema viwanda tunamaanisha nini, tukikubaliana hapa, tutakwenda vizuri. Niliwahi kukutana na wanahabari nikiwahamasisha wazungumze juu ya viwanda. Wakaniambia lakini Nape hata ninyi wenyewe hamna tafsiri moja, sasa tukizungumza tunazungumza nini hasa. Nadhani hili la kwanza kubwa litatuweka mahali pazuri, tunaposema kiwanda tunamaanisha nini, tukikubaliana hapa sasa tutasonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Mwijage viwanda ni ukombozi na hasa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara kwa sababu bado maskini sana. Ukombozi wowote una vita na una vita hasa kwa wale ambao wanafaidika na mfumo wa kutokuwepo kwa viwanda. Hapa nitatoa mfano, tumekuwa tukizungumza juu ya ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea Lindi, pale Kilwa. Taarifa tulizonazo, Mataifa makubwa yenye interest na mbolea katika nchi hii yanapambana kuhakikisha kiwanda hicho hakijengwi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo ambalo hatutakubaliana nalo Mheshimiwa Mwijage ni pamoja na kuruhusu vita hii iendelee kutuumiza; Wanakusini wanapigana kwa maslahi yao na kama Serikali mtayumba kwenye hili, Wanakusini hatutakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulishalizungumza, mlishakubaliana, mwekezaji alishapatikana na utaratibu uko wazi, sasa vita hii ya wakubwa isituumize, wakapiganie nje ya Lindi lakini tunakitaka kiwanda cha mbolea Lindi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine, moja ya jambo linalopigiwa kelele na wawekezaji ni vitu vinavyoitwa vivutio (incentives), vinavyowavutia kuja kuwekeza kwenye nchi yetu. Mjadala katika nini vitumike kama vivutio vya kuwekeza inachukua muda mrefu sana na hata katika ranking za urahisi wa uwekezaji katika nchi yetu, katika jambo linaloturudisha nyuma ni pamoja na mjadala juu ya vivutio.

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua mjadala uliokuwepo juu ya bomba la mafuta, mjadala juu ya viwanda vya uunganishaji wa vipuri mbalimbali katika nchi yetu, suala la vivutio nadhani ni tatizo kubwa. Sasa umefika wakati Mheshimiwa Waziri na Serikali ya Awamu ya Tano fikirieni kutengeneza vivutio ambavyo tunakubaliana navyo, kwamba wanaokwenda kwenye mjadala waende wakiwa wanajua, huu ndio msimamo wa nchi katika kutoa vivutio katika uwekezaji ili tupunguze muda wa mjadala; kwa sababu wapo wawekezaji wengi wana pesa zao; anakuja akiona mjadala unachukua muda mrefu anaondoka, kwa sababu hatujaweka vipaumbele katika vivutio tunavyotaka kuviweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo,ushauri wangu kwa Serikali; umefika wakati kaeni kubalianeni; hivi ndivyo vivutio tutakavyovitoa, vikitokea vya ziada hivyo ndivyo viingie kwenye mjadala, vinginevyo tutashindwa kushindana. Kama mtu anakwenda Rwanda anatumia masaa machache anapata mkataba yuko tayari kuwekeza, halafu akija kwetu anachukua miaka miwili au mitatu, watatukimbia; na wakitukimbia maana yake nchi kinachozungumzwa hakitatekelezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la mchango wa sekta binafsi na kuna watu wamezungumza hapa. Nataka kushauri Serikali yangu, hebu tusiingie kwenye mtego wa kuiingiza Serikali kwenye uwekezaji wa viwanda, tuwaachie sekta binafsi. Kazi yetu iwe ni kuwatengenezea mazingira mazuri ya kuwekeza. Dunia ya leo tukitaka kwenda wenyewe tutakwama, lakini tukiwatengenezea mazingira mazuri inawezekana, mchango wao ni mkubwa, tutengeneze mazingira ikiwemo vivutio, lakini pia waone kwamba hili ni eneo sahihi la kuwekeza. Mtaji wa mwanzo wa amani na utulivu tunao, lakini haya maeneo mengine lazima tuyawekee kipaumbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, ni suala kubwa sana la kuhusisha maendeleo ya viwanda na maendeleo ya watu, ni suala la msingi sana. Tusipolihusisha tutawaacha watu wetu nyuma na haya maendeleo hayatakuwa na maana kabisa, kwa hiyo, ni lazima tuhusishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo moja la kuhusisha ambalo nadhani tushauriane, Serikali, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Elimu pengine na TAMISEMI kupitia VETA, tuangalie tunawatengeneza akina nani kwenda kufanya kazi kwenye hivi viwanda? Vinginevyo tutajikuta tunaanzisha viwanda na mwisho wa siku wanaokuja kufanya kazi si vijana wetu hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna mtaala wa VETA ambapo nchi nzima mtaala ni huo mmoja, lakini mazingira yanatofautiana. Ukienda Lindi na Mtwara mahitaji yetu ni kuwatengeneza vijana wetu wakafanye kazi kwenye mafuta na gesi, lakini mtaala wa kwao ni sawasawa na mtaala wa Bukoba, mazingira ni tofauti. Wa Bukoba wafundishwe kuchonga mtumbwi na kuvua samaki, lakini wa Mtwara na Lindi wafundishwe namna atakavyofanya kazi kwenye mafuta na gesi. Sasa nadhani tufikirie namna ya kutengeneza mtaala kwa mujibu wa mahitaji ya ukanda na shughuli za kiuchumi zilizoko kwenye eneo husika badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa hivi wa mtaala mmoja kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani tukienda hivi maendeleo ya viwanda pamoja na kuongeza thamani ya mazao yetu, lakini pia utakidhi haja ya wale wanaokwenda kufanya kazi. Ukienda leo pale Mtwara kwenye utafiti wa gesi na mafuta pana shida, mpaka walinzi wanaajiriwa kutoka Kenya, wanaajiriwa kutoka Uganda. Hivi hatuna vijana wetu pale tukawafundisha Kiingereza kidogo na kuwafundisha discipline ya kufanya kazi pale?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nadhani VETA inaweza kuboreshwa zaidi kutoka hapa ilipo ikawaandaa vijana wetu wakakidhi haja ya soko la huko tunakokwenda. Tukifanya hivyo tunaambatanisha maendeleo ya viwanda pamoja na maendeleo ya wananchi wetu na tukifanya hivyo naamini hatutakuwa na matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua iko nia njema ya Rais wangu, najua iko nia njema ya Serikali ya Awamu ya Tano, lakini hebu tuhusianishe basi haya tunayoyafanya yapate tafsiri sahihi, tuweke vigezo sahihi, vile vile tuyahusianishe na maendeleo ya watu wetu. Tukifanya hivi mambo yetu yatakwenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, namuunga mkono Mheshimiwa Waziri kwenye bajeti yake na kwa kweli mambo yake nadhani yatakwenda vizuri.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie bajeti hii ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwa niaba ya wananchi wangu wa Mtama nitoe pole kwa wenzetu wa Arusha kwa msiba mkubwa walioupata kutokana na ajali na kufiwa na wanafunzi karibu 32, tunaamini Serikali itachukua hatua kuzuia hizi ajali ambazo zimeendelea kutokea siku hadi siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani ilianza kuchukua hatua kadhaa za kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kubana mianya ya wakwepa kodi. Pia kupunguza matumizi ikiwepo kupunguza safari, kupunguza sherehe na matumizi ambayo kwa kweli pengine kwa namna moja au nyingine hayakuwa ya lazima; ikiwemo kushughulika na wafanyakazi hewa na hatua mbalimbali ambazo zilichukuliwa na Serikali katika kipindi ambacho Serikali imekuwepo madarakani. Pia kwa takwimu tunaambiwa uchumi unakua kwa asilimia 7.2. Haya yote hayatakuwa na maana kama hayatatafsiriwa kwenye maboresho kwenye huduma za jamii na hasa maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hizi lengo lake lilikuwa ni kuongeza uwezo wa Serikali. Sasa kama hatua hizi zimechukuliwa na matokeo yake ni chanya tunapaswa tuyaone kwenye ongezeko la huduma za jamii, na hapa tuanze na suala la maji ambalo linagusa kila mtu. Tusipofanya
hivi hatua tulizochukua hazitakuwa na maana hata kidogo.
(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti iliyopita tumetenga bilioni mia tisa. Bajeti hii tukiwa tumesimamia hatua tulizozichukua ambazo kwa kweli zingeongeza uwezo wa Serikali; tunatoka 900 kwenda 600, hatujatafsiri mafanikio ya hatua tulizozichukua, kwa vyovyote vile Watanzania hawawezi wakatuelewa. Ukuaji wa uchumi wetu hauwezi ukabaki kwenye makaratasi peke yake, hatuna tunayemfurahisha, tunataka tuwafurahishe wananchi wetu na hivyo, lazima tutafsiri ukuaji huu kwenye huduma za jamii na hapa kwenye sekta ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu wa kwanza, naamini Serikali ni sikivu. Watu wamepiga kelele juu ya jambo hili lakini lazima pia tuone matokeo yake, wananchi hawataelewa hatua tunazozichukua kama haziwezi kwenda kubadilisha maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Ilani ya Uchaguzi ya CCM, ambayo bahati nzuri kwa mujibu wa Katiba ya CCM ilani hii inatengenezwa na kusimamiwa na Idara ya Itikadi na Uenezi, ambapo wakati ikitengenezwa mimi nilikuwa mkuu wa idara hiyo.

Vile vile nilibahatika kuzunguka nchi nzima, jimbo kwa jimbo na kwa kila jimbo nimelala siku moja. Tatizo la maji liko kila jimbo katika nchi hii, hakuna mahali ambako hakuna tatizo hili. Tunapishana ukubwa wa tatizo lakini umegusa kila mahali na mimi nimeshuhudia kwa macho yangu. Ndiyo maana tulipokuwa tunatengeneza ilani ya uchaguzi moja ya jambo kubwa ambalo tumelizungumza kwa kina ni suala la maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani hii ya Uchaguzi, iliyotengenezwa na Chama cha Mapinduzi ndio mkataba wetu kati ya CCM na wananchi. Tusipoitekeleza wananchi hawataturudisha na huu ndio ukweli, kwa sababu tuliwaahidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya tatizo la maji pamoja na kuathiri watu wote lakini akinamama ambao ndio wapiga kura wakubwa wa CCM ndio waathirika wakubwa wa tatizo hili. Ndiyo maana sina mashaka kwamba Serikali itasikiliza iende ikaongeze pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ilani hii tumeahidi kwamba tutatoa kiwango cha upatikanaji wa maji vijini kutoka asilimia 67 kwenda 85. Dar es Salaam pale ambapo DAWASCO na Luhemeja wanajitahidi kufanya vizuri lakini kama hakuna hela mambo yatakwama; tunataka kutoa 68 kwenda 95. Kwenye miji na makao makuu ya mikoa kutoka 86 kwenda 95, miji midogomidogo kutoka 57 kwenda 90. Hili halitafanikiwa tukienda na bajeti hii. Ndiyo maana naunga mkono hoja Serikali wasione aibu wala wasijisikie vibaya kurudi kwenda kuongeza pesa hapa. (Makofi)

Mwishoni nitatoa mapendekezo. Eneo la pili ni kwenye umwagiliaji. Umwagiliaji ukiangalia hapa hela iliyotengwa ilikuwa kidogo, hela iliyopelekwa asilimia 8.4 lakini hela yenyewe sijui kama wanajua kwamba sehemu kubwa imekwenda kuliwa. Tunayo miradi ya umwagiliaji; jimboni kwangu nina miradi mitatu ya umwagiliaji mradi mmoja umetumia miaka nane haujakwisha, mingine ipo kisingizio kikubwa ni kwamba ilibuniwa vibaya .

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya sana pale jimboni kwangu wakamfukuza Mkurugenzi ambaye hakuwepo, ambaye siye aliyebuni, waliobuni miradi na pesa zikazama wapo na wanaendelea kula nchi hawaguswi kwa lolote. Leo mafuriko tunayoyaona ni kwa sababu tumeshindwa ku-manage maji yanayotokana na mvua ambayo yanatiririka kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama tunaendelea kuona umwagiliaji kama kasehemu kadogo sana kwenye Wizara, nadhani pengine either it is wrong placed, tuipeleke mahali sahihi ili umwagiliaji ufanye kazi iliyokusudiwa, tukienda hivi hili eneo hatutafika. Sasa napenda nitoe mapendekezo yafuatayo:-

La kwanza, hili…

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.
Hali ya Uchumi wa Taifa Kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri waliyofanya. Kwa kiasi kikubwa Mheshimiwa Waziri mmejitahidi kusikiliza kelele za Wabunge hapa na ambao ndio wawakilishi wa wananchi na kwa kweli bajeti hii kwa kiasi fulani na kwa kiasi kikubwa ime-reflect ambacho tulikuwa tukikipigia kelele. Kwa hiyo, nadhani ni mfano mzuri wa Serikali kuwa sikivu kwa wale ambao inawasimamia hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya na hasa kwenye usimamizi wa rasilimali za nchi yetu. Nadhani ameonyesha mfano mzuri na kwa mjadala unavyoenda nadhani watu wengi wanamuunga mkono, wanaweza kupatikana wachache ambao pengine wana mawazo tofauti, lakini hiyo haitufanyi tusisonge mbele na msimamo wa kulinda rasilimali za nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ambalo ningelipenda kulisema katika hili nadhani ni vizuri ukweli huu ukasemwa kwamba hizi juhudi za kulinda rasimali za nchi yetu hazijaanzwa na Awamu ya Tano, zimeaanzwa kutoka Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere kuna mambo aliyafanya katika kuhakikisha rasilimali za nchi yetu zinalindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo aliyafanya hata kama kunaweza kuwa na mapungufu. Awamu ya Pili ya Mzee Mwinyi yako mambo aliyafanya, Awamu ya Tatu ya Mzee Mkapa yako mambo aliyafanya, Awamu ya Nne ya Mheshimiwa Kikwete yako mambo aliyafanya mazuri. Kwa hiyo, hakuna namna ambayo tutapuuza juhudi zilizofanywa na watangulizi wa Mheshimiwa Magufuli, kwa sababu nao wana mchango hata kama leo yataonekana yalikuwepo mapungufu lakini kwa nafasi yao walitimiza wajibu wao. Na ni vizuri tukatambua mchango wao na kuuheshimu mchango wao badala ya kubaki tunawanyooshea vidole kama vile hawakufanya lolote kabisa katika juhudi za kulinda rasilimali za nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukisoma Ilani zote za Uchaguzi za Chama cha Mapinduzi, tumezungumza habari ya ulindaji wa rasilimali zetu. Kwa hiyo, hiki anachokifanya Rais anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndio mkataba wa CCM na wananchi tukiunda Serikali. Hapa nitanukuu Ilani ya Uchaguzi inasema hivi; “kubuni na kutekeleza mikakati mahsusi itakayowezesha kupunguza au kukomesha kabisa vitendo vya utoroshaji wa madini kwenda nje ya nchi na biashara haramu ya madini nchi.” Kwa hiyo, iko kwenye Ilani ukisoma mwongozo, ukisoma muelekeo wa sera kote tumezungumza. Alilolifanya Rais Magufuli ambalo ndilo tunalomuunga nalo mkono
ametupeleka kwenye hatua kubwa zaidi ukilinganisha na hatua tulizozichua mwanzoni. Lakini anajenga kwenye msingi ambao ulishaanzwa na wenzake, kwa hiyo, kwa kweli tusitenganishe na kufanya kama vile waliopita ni waharifu hivi, hapana. Naamini walitimiza wajibu wao Magufuli anatimiza wajibu wake tumuunge mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na katika hili tunaweza tukagawanyika katika mitazamo, wapo wale wanaunga mkono asilimia 100, wapo wale wanaopinga kwa namna wanavyowaza wao. Sasa kelele zisiturudishe nyuma lazima tusonge mbele kwa sababu vita hii ni takatifu, lakini tusipuuze katika kelele nyingi kunaweza kuwa na ushauri mzuri ndani yake. Tusifike mahali tukapuuza kabisa nadhani sio jambo jema, hii vita ni yakwetu wote nchi hii ikifaidika na jambo hii ni faida kwetu wote bila kujali itikadi zetu za vyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusitoboane macho, tusitupiane vijembe visivyokuwa na sababu ni wakati wa kuileta nchi yetu pamoja twende tukapigane hii vita tuishinde. Kwa hiyo, wapinzani na CCM na watu wengine wote kwa ujumla wetu bila kujali tofauti zetu nadhani ni vizuri tukaungana katika hili, tuondoe tofauti zetu tusitafute mchawi kati yetu wenyewe sisi tuungane. Kama vita yoyote safari yoyote inaweza kuwa na mashimo na mabonde kunaweza kuwa na ghrama za vita hii, tukubali kuzilipa faida yake ni kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Rais kwa kazi hii na nadhani sasa ni wakati mzuri tumuunge mkono kama yako maeneo ya kurekebisha, kushauri tushauriane ili vita iishe salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili, ambalo nilitaka nilizungumzie Mhehimiwa Waziri uchumi wa gesi na mafuta. Sisi Kusini, Mikoa ya Lindi na Mtwara gesi na mafuta ndio ilikuwa inazungumzwa kuwa ni ukombozi. Bahati mbaya ugunduzi ulipopatikana habari zilizotolewa ni kama vile ndio tunageuza siku moja kule kuwa nchi ya asali na maziwa. Na ninyi mnajua habari ilipotoka kukatokea vurugu kubwa sana Lindi na Mtwara, kwa sababu habari iliyopelekwa kwa wananchi ilijaa chumvi nyingi badala ya kupeleka ukweli kwamba faida ya gesi yenyewe iliyogunduliwa na mafuta inaweza ikatuchukua zaidi ya miaka 20, 30 kabla hatujaanza kuifaidi. (Makofi)

Kwa hiyo, wako wananchi waliokata mikorosho yao wakiaamini biashara imeisha, wako watu waliokaa na kubweteka wakadhani mambo yameisha. Sasa nadhani hili lilikuwa kosa moja kubwa sana ndio maana ikatokea vurugu ya Lindi na Mtwara juu ya gesi na bomba lake na mambo yote yaliyoendana na hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sisi tulidhani kwamba mchakato kuelekea huko kwenye kufaidika ungeenda vizuri na kwa wakati. Na hapa nataka nizungumzie ujenzi wa mtambo wa kuchakata gesi (LNG plant) pale Lindi. Kwetu sisi huu ndio ungekuwa ukombozi wa mwanzo wa kuanza kuyaona matunda ya ule ugunduzi, bahati mbaya hali ilivyo ni kama vile hili jambo linasuasua sana na linawezekana kabisa sijui lisiwezekane linatupa tabu. Kwa sababu leo makampuni yote matano ambayo ndio yangeshirikiana katika ujenzi kinu hiki, ukichukua British gas, orfil energy, start oil, Exon Mobil na hata Petrobrass tulidhani ofisi zao zingekuwepo Lindi na Mtwara na ziwe active, tulidhani vifaa vyao mahelkopta yao yale, meli zao zile leo hazionekani? (Makofi)

Sasa tunataka Serikali ituambie kinachoendelea ni nini huu mradi bado upo? Ukisoma kwenye hotuba ya Nishati na Madini unaona imezungumzwa ka-para kamoja lakini kweli mradi mkubwa wa zaidi ya dola bilioni 33 kitu unazungumzwa kwa para ndogo kama vile hakuna kinachoendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Serikali hapa kuweni serious tuambieni ukweli huu mradi upo au haupo?

Na kama haupo tujue namna ya kufanya na kama upo unaanza lini tulijua mwanzoni tatizo lilikuwa ni ardhi. Rais amefuta hati hili jambo lilitakiwa liwe limekwisha kwanini bado inaendelea hivi na ziko habari kwamba hawa jamaa sasa wanahamia Msumbiji, tuambieni ukweli hali ikoje, mradi upo au haupo? Na tungedhani kwa sababu mradi huu ungeanza uchumi wa Lindi ungebadilika, pesa zingeingia nyingi hata katika ile process yenyewe tu ya kuujenga huu mradi ambao ungechukua zaidi ya miaka nane, lakini zaidi ya dola bilioni nne zingiingia Lindi zingebadilisha maisha ya watu wetu pale. Lakini kwa hali tunavyoenda nayo tunapata mashaka. Sasa ni vizuri Serikali tukawa wa kweli, kauli ya Serikali itolewe katika jambo hili, tukowapi, tunaenda wapi, nini matumaini ya mradi huu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo nilitaka nilizungumzie la mwisho nadhani kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri pamoja na uzuri wa hotuba hii, lakini kuna mahali umezungumzia sera za mapato. Hapa ukisoma umeweka mipango karibu saba, lakini Mheshimiwa Waziri mipango yote inalenga kubana na kukamua wakwepa kodi na kukamua ukusanyaji wa kodi. Sijaona mpango straight unaozungumza namna ya ku-stimulate growth ya economy ya nchi yetu. Sasa kama hata…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kusema naunga mkono taarifa zote mbili na maazimio yake. Pia nawapongeza Wenyeviti wa Kamati hizi kwa kazi nzuri waliyofanya pamoja na Wajumbe wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, niende moja kwa moja. Nilitaka nichangie kwenye eneo moja la mahusiano yaliyopo kati ya wafugaji na hifadhi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu zilizopo, kwa nchi za Ukanda wa Kusini huku na Afrika Mashariki, Tanzania ni nchi inayoongoza kwa kuwa na mifugo mingi. Inasemekana tuna zaidi ya ng’ombe 28,000,000 na pointi zake, lakini pia kuna mbuzi, kondoo na mifugo mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu, sekta hii ya mifugo inasemekana inahudumia zaidi ya kaya 4,000,000 ambazo zinajumlisha zaidi ya watu 25,000,000 ambao ni karibia zaidi ya asilimia 50 ya population ya nchi yetu. Kwa takwimu hizo hizo, sekta hii ya mifugo inachangia zaidi ya 4% kwenye pato la Taifa ambalo inashindana karibu sawa na madini katika nchi yetu. Kwa hiyo, ni sekta kubwa na inagusa eneo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali inayoendelea kwenye sekta hii ya mifugo ni mbaya sana. Bahati mbaya kwa miaka sasa hili jambo limekuwa linakuja, linazungumzwa hapa Bungeni, moto unawaka, halafu zinachukuliwa hatua za kuufunika ule moto, watu wananyamaza, halafu dhuluma na hujuma inaendelea pale pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013/2015 moja ya kazi nilizofanya ni pamoja na kupita kwa wafugaji nchi nzima, kuwasikiliza na kusikia manung’uniko yao. Nilitegema baada ya uchaguzi wa mwaka 2015 hali itabadilika. Bahati mbaya sana, juzi nikiwa Mjumbe wa Kamati hiiya Ardhi, Maliasili na Utalii, tumekutana na wafugaji walikuja hapa Dodoma, hali ni mbaya kuliko ilivyokuwa mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutaendelea na hatua hizi za kuzima moto kila unapowaka, maana yake ni moja, tunatoa kafara asilimia 50 ya population ya nchi yetu ambayo inahudumiwa na sekta ya mifugo na kuacha hali yao ikiwa mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyoongea na hapa nataka niijenge hii hoja tuuunge mkono pendekezo la Kamati la kuunda Kamati Teule ya Bunge kwenda kusaidia kumaliza tatizo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kwa hatua za kawaida za Serikali, tukubali imeshindikana. Njia peke yake iliyobaki, tuunde Kamati Teule ya Bunge ikaisaidie Serikali kwa nia njema ya kuokoa zaidi ya asilimia 50 a population ya nchi yetu ambayo inahudumiwa na sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyoongea mifugo ambayo imeshikiliwa kwenye hifadhi kwa takwimu hizi kama ni za kweli, basi hali mbaya sana. Meatu kuna ng’ombe 948; Kakonko ng’ombe 700; Bukombe ng’ombe 716; Bariadi 158; Kasulu 90; Morogoro 401; Chemba 411; Mlele 640 na Kaliua ng’ombe 1,129; hawa wameshikiliwa kwenye hifadhi. Wapo wanaoendelea kufa kwa sababu hawana huduma za kutosha, wapo wanaouzwa kinyemela na wapo wanaouawa kwa risasi. Hali hii ikiendelea tunakokwenda ni kubaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa takwimu nilizonazo mwaka 2015 - 2018 ng’ombe ambao wameshauawa kwa kupigwa risasi na wengine kwa kunyimwa huduma, kwa sababu wako wengi ambao wamekamatwa, namna ya kuwahudumia ni ngumu, Katavi ng’ombe 6,503; Morogoro Vijijini ng’ombe 200; Bunda ng’ombe 150; Meatu ng’ombe 48; Chemba ng’ombe 196; hii ni mifano ya maeneo machache. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa…

(Hapa kengele ililila kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2017
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie. Kwanza niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote mbili kwa kazi nzuri wanayofanya, naomba nijikite kwenye ripoti ya Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania inatekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa sasa na tumeshuhudia Rais Magufuli akitangaza kuongeza nguvu ya vita ya kiuchumi kwa nchi yetu ambayo ni jambo zuri sana, litaisaidia nchi yetu kutoka hapa ilipo, kwa sababu tumeshapata uhuru wa kisiasa ni vizuri tukapata uhuru wa kiuchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vita hii na Diplomasia hii haiwezi kutekelezwa vizuri kama Taasisi yetu ya Usalama wa Taifa itaendelea kusimamiwa na sheria tuliyonayo inayoisimamia Taasisi hii ya Usalama wa Taifa. Kwa muda mrefu, Taasisi hii imekuwa inashughulika na usalama wa Viongozi zaidi, kuliko kushughulikia usalama wa nchi kwa ujumla na hasa masuala yanayohusu uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko scandal mbalimbali ambazo zimekuwa zikitokea katika nchi yetu, ukianzia kwenye EPA, ESCROW, RICHMOND, kwenye Madini na Mikataba mbalimbali mibovu ambayo nchi yetu imekuwa ikiingia. Kwa muda mrefu mambo haya yakitokea tumekuwa tukishuhudia Wanasiasa wakiadhibiwa na Watendaji ndani ya Serikali wengine wakiadhibiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taasisi hii ingekuwa inatimiza wajibu wake kwa mlengo wa kulinda uchumi wa nchi yetu, maana yake ingefanya kazi ya kuzuia nchi yetu isiingie kwenye mikataba hiyo mibovu. Kwamba watu wanakwenda wanafanya utaratibu, wanachukua hela za EPA wanagawana, inakwenda kwa muda mrefu unnoticed halafu baadaye tunakuja kuambiwa unajua kuna watu walipiga hela mahali, halafu wanachukuliwa hatua hawa watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, chombo hiki hakinyooshewi kidole, hawaulizwi, hawasemi chochote, nadhani inawezekana sheria tuliyonayo inawafunga mikono kwa namna moja ama nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitegemea kwamba Kamati yetu ingeleta mapendekezo, tupitie upya Sheria ya Usalama wa Taifa ili mikono yao iende mbali, wakumbuke jukumu lao la kuhakikisha wanalinda uchumi wa nchi yetu, katika kipindi hichi ambacho tunahama kutoka kwenye Diplomasia ile ya Siasa kwenda kwenye Diplomasia ya Uchumi muda mwingi wautumie huku, badala ya hivi sasa wanavyofanya kubaki tunasikiliza simu za watu, tunafanya mambo ambayo kimsingi nadhani hayalindi uchumi wetu na mwisho wake gharama yake inakuwa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilidhani twende huko, sheria ile iletwe hapa, tuipitie tuone kama yapo mapungufu yanayowafanya tupelekwe huko tunakoenda, mwishowe tutabaki tunalaumiana kila siku, nchi yetu inaingia kwenye mikataba ya hovyo kila siku na wanaoumia na kuathirika wanakuwa ni wale waliopewa dhamana kwa maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanaopaswa kushauri tusiingie huko ni akina nani? Maeneo yetu ya bandari, airport na maeneo mengine, nilidhani eneo la kwanza nishauri umefika wakati tupitie upya Sheria ya Usalama wa Taifa...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, tunakukaribisha tena nyumbani namshukuru Mungu aliye kukurudisha salama, karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa uamuzi ambao umewasilishwa hapa na Mheshimiwa Waziri wa Utumishi Baba yangu Mzee Mkuchika. Nadhani mmefanya jambo jema kuona hali halisi na kuchukua hatua. Kwa hiyo, naipongeza sana Serikali kwa uamuzi waliouchukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulipopiga kura mwaka 2015 Mikoa ya Lindi na Mtwara, moja ya sababu tuliamini sana kwamba uchumi wa gesi wa Mikoa ya Lindi na Mtwara ni ukombozi mkubwa na uko salama mikononi mwa Rais Magufuli na Serikali ya Awamu ya Tano. Tulipopiga kura ndiyo ulikuwa mkataba wetu siyo, kwa maneno lakini iliwekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Spika, ukurasa wa 76 na 77 inaanzia ukurasa wa 75, eneo kubwa sana limezungumzwa uchumi wa gesi, suala la gesi na imeandikwa mafuta na gesi asilia. Kwa hiyo, kura nyingi alizozipata Magufuli ni kwa sababu ya makubaliano haya yaliyoko kwenye hii Ilani ya Uchaguzi kwamba atakwenda kuyaendeleza.

Mheshimiwa Spika, kwa summary, moja ilikuwa ni kuendela miundombinu ambayo ita-facilitate huu uchumi wa gesi wa Lindi na Mtwara. Pili, ilikuwa ni kuwandaa wananchi wanufaike na kufaidika kwa gesi na mafuta kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara. Lipo jambo specific la ujenzi wa mradi wa LNG plant kwa Mikoa ya Lindi, kwa hiyo hili limo kweye ilani ya uchaguzi. Pili, kwenye mpango wa miaka mitano na mpango ambao umekuwa ukiwasilishwa hapa mwaka hadi mwaka.

Mheshimiwa Spika, nasikitika sana nilipoangalia hotuba ya Waziri Mkuu kuanzia ukurasa wa kwanza mpaka wa mwisho hakuna neno gesi kabisa. Inaonekana ukienda hata site kwenyewe, shughuli mbalimblai zinazoendana na gesi kwa Lindi na Mtwara ni kama vile zimeanza kufungwa na zimesimama kabisa.

Swali langu la kwanza, hivi ni bahati mbaya hotuba ya Waziri Mkuu imeshindwa kuliona jambo hili kuwa ni kubwa na ikaamua kuliacha au Serikali imeamua kuachana nalo? Kwa sababu naona jitihada kubwa zinaanza kwenda kwenye Stieglers (umeme wa maji) mimi sina matatizo nalo inawezekana ndiyo maamuzi lakini Stieglers kwenye Ilani haimo. Ilani tumezungumza nishati ya gesi tena kwa sehemu kubwa sana na hii ndiyo ilikuwa imani ya wananchi wa Lindi na Mtwara kwa Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zilikuwepo jitihada zilifanywa na Mzee Mwinyi mpaka tukapata Songosongo, jitihada zikafanywa na Mzee Mkapa, Awamu ya Nne ikaja kwenye jitihada hizi za huu uchumi ambao tulianza kupata matumaini nao.

Mheshimiwa Spika, wakati jitihada zinafanyika watu watakumbuka, kuna watu walipoteza maisha Lindi na Mtwara, kuna watu walipata majeraha na vilema Lindi na Mtwara, kuna mali za watu lakini tukaamini kuna neema kesho. Kwa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na bahati mbaya tulimkabidhi Mheshimiwa Magufuli tukaamini liko salama, alipotupa Mheshimiwa Majaliwa tukaamini tuko salama zaidi, kwa sababu Waziri Mkuu ametoka kwetu. Sasa ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani hakuna kabisa, maana yake ni kwamba hili jambo pengine limeanza kuachwa sasa twende kwenye Stieglers. Je, hatusaliti Ilani ya Uchaguzi ya CCM? Je, hatuwasaliti wananchi wa Lindi na Mtwara waliotupa kura na kutuamini kwamba gesi yao na uchumi wao uko salama? Hili ni bomu kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati wa mchakato hali ya kisiasa, hali ya kijamii Lindi na Mtwara kulikuwa na taabu, sasa imetulia tukiamini neema ipo, kiuchumi baada ya harakati za gesi na mafuta Kusini watu walianza kuja kuwekeza uchumi wa Lindi na Mtwara ukaanza kukua, watu wakaanza kuwekeza. Hali ilivyo sasa hivi watu wameanza kuondoka, uchumi wa Lindi na Mtwara unadorora, hali yetu ni ngumu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa unyenyekevu sana asikubali suala la gesi lifie mikononi mwake akiwa Waziri Mkuu wa Tanzani, siyo sawa. Nimeuliza maswali hapa mara moja, mara mbili Serikai imeendelea kusisitiza, mchakato unaendelea lakini huo mchakato ambao hauwi reflected kwenye hotuba nzima ya Waziri Mkuu, mimi nadhani tuambieni ukweli, kama limeshindikana hili hebu tujue ukweli, tusiwasaliti wananchi wa Lindi na Mtwara siyo sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ukiacha gesi na mafuta, Lindi na Mtwara ni korosho. Mwaka jana kuna jitihada zimefanyika mambo yameenda vizuri, lakini Serikali ikafanya uamuzi, ikachukua kazi iliyokuwa inafanywa na Mfuko wa Pembejeo na Waziri anajua, wakasema ipelekwe kwenye Bodi ya Korosho na pembejeo hasa sulphur itagawanywa bure. Kulikuwa na mapungufu yalitokea lakini tukafumba macho kwa sababu ndiyo mara ya kwanza tukasema fanyeni uchunguzi, mlikokosea mrekebishe. Hali inavyoenda sasa hivi mwaka huu hali itakuwa mbaya kuliko tunavyodhani, kwa sababu mpaka mwezi huu wa nne wakulima hawajui chochote. Mheshimiwa Waziri, Jimbo langu mwezi huu watu wanaanza kupuliza dawa leo hawajaambiwa chochote.

Mheshimiwa Spika, wakati mnachukua mfuko ulikuwa na zaidi ya shilingi bilioni 49, walikuwa na uwezo wangeendelea nao, mkatuaminisha na tukawaamini, lakini hali inavyoendelea mbaya sana, kwa hiyo, tumaini peke yake lililokuwa limebaki Kusini ilikuwa korosho. Mnajua mbaazi imekwenda kutoka shilingi 200 mpaka shilingi 100, kuna wakulima wameacha mbaazi shambani wamesema bora zifie huko, sasa na korosho mnatupeleka huko, siyo sawa jamani! Ukiacha Lindi na Mtwara twende wapi, tuishi vipi sasa? Hili ni kutusaliti. Tulipotoa kura tuliwekeza tukaamini mtatusaidia, mkiendelea kufanya hivi mnatusaliti Mheshimiwa Waziri Mkuu na siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama imeshindikana rudisheni kwenye mfuko wa pembejeo tulikuwa tunakwenda vizuri. Kuna dhana ya kudhani kila mtu mwizi, siyo sawa, Mfuko wa Pembejeo ulienda vizuri sana. Mmebeba tumewaachieni bado mnakwenda vibaya kuliko hata mlivyochukua, hapa ni kutunyonga na siyo sawa sawa mtakuwa mnatusaliti sana watu wa Lindi na Mtwara (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anajua kuna watu bado wanadia mpaka leo malipo ya korosho. Kuna wakati fulani tulizungumza hapa, Ushirika ndiyo mkono wenu wa kusaidia kushirikiana na wakulima kuhakikisha wanapata soko, bei na mfumo mzima wa mazao yao. Hali ilivyo kule tumeweka watu, bahati mbaya elimu yao ndogo, sasa kuna mahali walikuja watu wamepata hasara ya zaidi shilingi milioni 400 na hawajui imepatikanaje, kwa nini? Wako watu wamechaguliwa uwezo hawana, sasa kwa nini tusibadilishe mfumo kwenye wale wa kuchanguliwa haya tusijali elimu yao, lakini tupate watu wa kusimamia, haya ni mabilioni ya hela yanasimamiwa na darasa la saba anashindwa kupiga hesabu, anakuja analia anatakiwa akamatwe, apelekwe Mahakamani, ukimuuliza umepotezaje hajui! Sasa kama tunashindwa hata hili la kuimarisha ushirika kwa sababau mapesa yapo, kwa nini tusiajiri watu wenye uwezo, waliosoma wakasimamia hela zetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda mpaka leo loss ni kubwa matokeo yake ni nini? Wakulima wanaambiwa wakubaliane wachangie loss inayopatikana, lakini hii loss inasababishwa na nani? Inasababishwa na wakubwa kwenye mabenki na wakubwa kwenye Ushirika ngazi ya juu, siyo hawa wa chini, hawa wa chini hawajui chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu kwa Serikali, la kwanza, tupitie upya mfumo wa ushirika. Pamoja na kuchaguana demokrasia safi, lakini ni vizuri tupate watu wa kuajiriwa wenye elimu ya utunzaji wa mahesabu wakashirikiane kusaidia.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kwenye mapendekezo haya ya bajeti ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpa pole Kaka yangu Engineer Dkt. Tizeba nadhani hii kazi ni ngumu kidogo na pengine yako mambo yapo nje ya uwezo wake, naona toka jana shughuli imekuwa ngumu kidogo hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza mjadala huu toka jana kwa mara ya kwanza kuna dalili kwamba watu wengi hawaungi mkono haya mapendekezo, bila ya kujali pande zote na bahati nzuri kwa mfumo wetu wa bajeti tulionao iko room ya Serikali kwenda kuangalia upya, kwa sababu tunaanza na bajeti ndogo ndogo halafu tunakwenda kwenye bajeti kubwa. Kwa hiyo, ushauri wangu wa kwanza Mheshimiwa Waziri na Serikali tusione shida kukubali hali halisi kwamba ni vizuri tuende tukaangalie upya bajeti hii wala tusione taabu, ni jambo la kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira tuliyonayo kama trend yenyewe ndiyo hii, nataka kusema huu ni mtihani mkubwa sana kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwenye hii bajeti. Kwa sababu ni hapa ambapo tutatakiwa kujipambanua tunajikita kwenye maendeleao ya vitu au maendeleo ya watu. Kama ni maendeleo ya watu bajeti hii ndiyo inagusa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kelele unazozisikia Mheshimiwa Waziri kwenye pamba, kahawa, korosho na mbaazi ambayo mmetuambia tukale na maeneo mengine yote ni kwa sababu inagusa maisha ya watu. Sasa Serikali tunayo choice ya message tunayotaka kuipeleka kwenye umma. Message kwamba tunajali maendeleo ya vitu au tunajali maendeleo ya watu ambao ndiyo waliotuweka madarakani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia trend mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga asilimia 0.93 ya bajeti kwenye Wizara ya Kilimo, mwaka 2017/2018 ikashuka ikaenda asilimia 0.85, mwaka 2018/2019 haya mapendekezo ya sasa hivi tumeshuka tena tumekwenda asilimia 0.52 ya bajeti. Maana yake moja tu ni kwamba kila mwaka tunashusha bajeti tunayoitenga kwenye sekta ambayo ndiyo inagusa watu wengi kuliko wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakumbukwa hapa tuliwahi kupendekeza wakati fulani na tukashambuliwa kama vile siyo wazalendo, kama vile tuna chuki hivi, tulisema Serikali ni vizuri ikakwepa kuwekeza fedha za ndani nyingi kwenye miradi mikubwa ambayo inaweza kujiendesha kibiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kuendelea kushuka kwa bajeti muhimu kama ya kilimo ni kwa sababu tumeamua kupeleka fedha zetu za ndani kwenye kuwekeza kwenye miradi mikubwa ambayo ingeweza kujiendesha kibiashara, kwa hiyo madhara yake tutayaona tu. Inawezekana kweli tukaonekana siyo wazalendo lakini hivi ukweli huu unahitaji elimu gani kujua kwamba tunaendelea kushuka na mimi naamini hili kaka yangu Mheshimiwa Tizeba siyo lako, tutakubebesha mzigo ambao siyo wako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jana nimemsikia shemeji yangu Mbunge wa Ruvuma mpaka analia hapa, watu wanadai, watauziwa mali zao kwa sababu bajeti unayopewa ndogo huna namna. Hela inaenda wapi kama tumebana matumizi, hela inaenda wapi kama tunakusanya? Bahati mbaya rafiki zangu ushabiki unakuwa mwingi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu wa kwanza Serikali isione aibu kuipitia upya bajeti hii kwa sababu bajeti hii tukiipitisha kama ilivyo message kwa Watanzania ni mbaya sana kwa Serikali ya Awamu ya Tano kwamba tunataka kuwekeza zaidi kwenye vitu badala ya watu! (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda ukaangalia hali halisi thamani ya mazao ambayo wananchi wetu wanazalisha imeshuka sana. Nilikuwa naambiwa jana mahindi Ruvuma yamefika shilingi 15,000 kwa gunia, nenda kwenye maeneo yote kwenye mbaazi huko hata sitaki kusema, lakini bidhaa ambazo wananchi wanatakiwa kuuza bidhaa zao wakanunue bidhaa kama sukari, mafuta ya kula na vitu vingine vyote vimepanda sana, sasa uhalisia unakataa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukikubali ni wananchi wangu nikikubali wakulima wa korosho watanishangaa, nikikubali wakulima wa mbaazi, ufuta na wakulima wengine wote katika nchi hii watanishangaa, wakulima wa pamba ambao tumewahasisha wamelima pamba kiasi kile watanishanagaa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mazingira haya Mheshimiwa Waziri sijui, lakini nilikuwa naangalia Ilani ya Uchaguzi ambayo wengi hawataki tuinukuu, lakini ndiyo tuliyoiombea kura, ndiyo mkataba wetu na wananchi, bajeti hii ukipitia Ilani ya Uchaguzi zinakataana. Sasa kama zinakataana simple logic ndogo tu, tuishauri Serikali irudi mezani, muda upo bajeti kubwa tutakuja kuipitisha baadae, muda upo tuende tukaangalie upya tuweke vipaumbele ndicho tulichokubaliana na wananchi, humu tumekubaliana kwamba wananchi wetu Serikali tutakayoiunda itawasaidia kupata masoko ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kelele unazozisikia za mahindi na mazao mengine mgogoro wake uko hapo, kelele unazozisikia za mbaazi mgogoro wake upo hapo, ukimwambia mtu akale magunia 20 ya mbaazi si unamtukana huyu! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Tanzania iliingia mkataba na Serikali ya China tupeleke muhogo, mkataba mmesaini mwezi Mei, 2017 tangazo kutoka Wizarani kwako ya kupeleka imetolewa Aprili. (Makofi)
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie. Kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii nichukue nafasi hii kwa niaba ya Kamati kuwashukuru Waziri na Naibu Waziri na Katibu Mkuu wake pamoja na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara hii kwa ushirikiano mkubwa ambao walitupa wakati wa kutekeleza kazi zetu kama Kamati. Kwa kweli wametupa ushirikiano mkubwa, kwa hiyo, nimshukuru sana Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na watendaji chini ya Wizara hii kwa ushirikiano wao.

Mheshimiwa Spika, nilisema nichangie jambo moja hapa kubwa. Wakati tunakamilisha Taarifa ya Kamati, tarehe 25 Aprili, 2018 Tanzania Forest Services walitangaza tender ya kukata miti kwenye Pori la Akiba la Hifadhi la Selous. Tender hii inahusisha ukataji wa miti zaidi ya cubic meter 3,495,362, na point fulani. Maelezo, ukisikiliza tafsiri ya idadi ya miti itakayokatwa wanasema ni karibia ukubwa wa Mkoa mzima wa Dar es Salaam na zaidi yake na wapo wengine wanasema ni ukubwa wa Unguja nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa eneo hili ni kubwa sana kukatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa ambayo inaliletea heshima nchi yetu hifadhi hii, ni kubwa sana kiasi kwamba imenishtua sana.

Mheshimiwa Spika, lakini itakumbukwa Bunge hili lilitunga sheria mwaka 2004, Sheria Na. 20 ya mwaka 2004 ya Usimamizi wa Mazingira. Katika sheria ile sehemu ya saba ya sheria ile inazungumza tathmini ya mazingira kimkakati. Naomba niinukuu, inasema hivi:-

“Iwapo rasilimali ya madini au mafuta itagundulika kabla ya mpango wowote au kabla ya kuwa na mpango wa kujenga kituo cha nishati ya umeme wa maji haujafanyika Waziri mwenye dhamana ya masuala ya madini, nishati au maji atafanya tathmini ya mazingira ya kimkakati.” (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunavyoongea, tathmini hii haijakamilika, tathmini hii bado inaendelea, TFS wametangaza tender ya kukata miti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sehemu ya pili ya sheria hii inasema hivi:-

“Tathmini ya mazingira kimkakati iliyotajwa chini ya kifungu cha kwanza itatathmini eneo lililotengwa kwa ajili ya shughuli husika pamoja na mambo yafuatayo; la kwanza; hali halisi ya mazingira na ya maliasili, utambuzi wa maeneo nyeti kiikolojia yanayolindwa, utambuzi na maelezo kuhusu jamii zinazolizunguka eneo husika, hali halisi ya kiuchumi, ya jamii iliyopo, shughuli za kiuchumi na miundombinu…”

Mheshimiwa Spika, na yako mengine muda hautoshi kusoma. (Makofi)

Sasa nataka nimuombe AG aisaidie Serikali kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria zilizopitishwa na Bunge. Kwa unyenyekevu sana, Serikali naiomba isitishe zoezi hili, isubiri tathmini ya kimkakati ya mazingira ikamilike. Hifadhi hii ya Selous inahusisha mikoa mitano, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Haiwezekani tukapuuza maisha ya watu, wanyama, mimea na viumbe mbalimbali katika mikoa mitano ya nchi, tunaamua kwenda kukata miti yote hii; napata taabu, inaingiaje akilini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nilidhani tungesubiri tathmini hii ikafanyika, ikija hata kama tunataka kuendelea na mradi, tathmini itatuambia wapi tukanyage, wapi tusikanyage, tutaokoa maisha ya watu hawa. Maisha ya kwetu sisi kule baada ya gesi kuyumba ni korosho, ufuta, mbaazi na mazao mengine.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hizi taarifa za Kamati mbili.

Mheshimiwa Spika, wakati ukimuagiza Mheshimiwa Lusinde apeleke invoice kwa Waziri wa Maliasili na mimi kwangu tembo wameingia lakini kwangu wamekula maembe. Kwa hiyo, nami nitapeleka invoice. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimepitia ripoti ya Kamati hii inayoshughulika na kilimo na naunga mkono mapendekezo yao mengi sana. Nitaomba tufanye maboresho maeneo machache lakini kwa kweli wamefanya kazi nzuri ya kuchambua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi yetu ina mazao mengi, yako mazao yale ya biashara lakini yako mazao mchanganyiko. Hapa nataka nizungumzie suala la Bodi ya Nafaka ya Mazao Mchanganyiko. Tunazo Bodi kwenye mazao mengine mengi lakini hii ya mazao mchanganyiko ambayo of course sasa hivi inafanya kazi ya kusimamia ununuaji wa zao la korosho, kwa mujibu wa sheria imeandikwa hapa kwamba hii ni taasisi ya Serikali ambayo inajiendesha kibiashara.

Mheshimiwa Spika, mwaka jana na mwaka juzi sisi ambao tuna wakulima wanalima mazao mchanganyiko na hasa sisi wa mbaazi tulipata matatizo kwa sababu tunadhani hii bodi haikutimiza wajibu wake sawasawa na ni kwa sababu ya ukosefu wa fedha kwamba hawakupewa fedha za kutosha. Kazi yao moja ni pamoja na kuyanunua haya mazao mchanganyiko kwa bei ya soko lakini kuyatafutia soko na hasa nje ya nchi.

Mheshimiwa Spika, Kamati imeonesha hapa moja ya changamoto kubwa ambayo imewapata wenzetu wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko ni kutopewa fedha. Ushauri wangu nadhani kwa kuwa, ni Bodi ambayo inaweza kujiendesha kibiashara badala ya kuendelea kutengewa fedha na Serikali kutoka kwenye Mfuko Mkuu, kwa nini Serikali isitengeneze utaratibu wa kuwadhamini Bodi ya Mazao Mchanganyiko wapate fedha kutoka kwenye taasisi za kifedha kwa maana ya kwamba wafanye kibiashara, wakakope, wanunue, wauze, Serikali iwe ni guarantor tu badala ya kupeleka fedha kule. Tuwa-guarantee, wapewe fedha na vyombo vya fedha wakanunue haya mazao wakatafute soko, wakulima wetu wangekuwa wako sawasawa kabisa na leo tungekuwa hatuzungumzi kabisa tatizo la mbaazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, habari nilizonazo waliomba fedha hawakupata, wakaomba kwenda kukopa kwa kupewa guarantee na Serikali nayo wakanyimwa, matokeo yake sasa wakabaki wako tu. Sasa wamebaki wako loose, tumeenda kuwachukua kuwapeleka kununua korosho, mimi nadhani siyo sawasawa. Tuwawezeshe, tuwadhamini, wakachukue fedha kwenye vyombo vya fedha kibiashara wafanye biashara kwa kuwa sheria inasema hivyo na mapendekezo ya Kamati hapa yanaonesha wakipewa fedha watafanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili ni mapendekezo juu ya korosho. Kamati imechambua vizuri sana suala zima la korosho. Nami naamini tumejifunza mengi namna korosho ilivyoenda na bila shaka mafunzo yake yatatusaidia kuboresha namna ya kuendesha mazao yetu ya kibiashara nchini. Tumevuna tulichopanda lakini sasa tujifunze badala ya kuendelea kulaumiana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la utata wa takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa na wenzetu wa Serikali. Kila mara Serikali imekuwa ikitoa takwimu mbalimbali juu ya zoezi zima la ununuzi wa korosho. Mimi nataka niwatahadharishe, takwimu nyingi mnazozisema Serikali ukienda kule chini ukweli unakataana. Mnachokisema mmelipa na hali halisi ilivyo, ukweli unapingana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sijui kama kuna sababu ya kuendelea kutoa takwimu. Takwimu hizi kila siku zinakua, nikienda Jimboni kwangu hali ya malipo bado mbaya lakini takwimu zinaonesha mambo yanakwenda, nadhani hili tulirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna mambo yametokea kwenye zoezi zima na hili nadhani kwa sababu ya kuchanganya. Tumei-suspend Bodi ya Korosho, tumeweka Bodi ya Mazao Mchanganyiko na Jeshi, kuna matendo ya dhuluma yamefanyika kwenye maeneo haya. Nashauri Serikali tufumbue macho, twende tuchunguze na tuchukue hatua, dhuluma haitakufa kama hatutachukua hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu katika korosho, zoezi la uhakiki bahati mbaya sana limeanza kutumika kama kichaka cha kulinda uzembe wa kupunguza kasi ya kulipa wakulima. Bahati mbaya limeanza muda mrefu siyo korosho tu kila mahali tukitaka kuchelewa kulipa tunasema tunafanya uhakiki ambao unachukua muda mrefu watu wanaumiaa inafika mwisho basi inapotea hewani hivi. Wasiwasi wangu uhakiki kwenye zao la korosho isipotelee hewani, uhakiki utupe matokeo, kama kuna korosho tumeamua kuitaifisha tuseme kiasi gani tumetaifisha na kwa nini tumetaifisha. Suala hili la uhakiki tukiweka wazi kila mtu atatuelewa na tutasonga mbele pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtama nataka kuchukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Rais na hapa nataka tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno hasa tunaposhutumiana bila sababu. Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi sisi Jimbo la Mtama tulipeleka maombi ya kufuta baadhi ya mashamba makubwa yaliyotelekezwa. Namshukuru Rais na Waziri wa Ardhi, moja ya shamba lililofutwa ni shamba Na. 37 lipo Maumbika – Mtama, Mkoa wa Lindi. Aliyelipeleka kuomba lifutwe ni mimi Mbunge, nilimpelekea Waziri, Waziri akapeleka kwa Rais, Rais akafuta. Nataka niwaombe wenzangu kwanza kwa niaba ya wakulima nimshukuru Waziri na Rais kwa kulifuta shamba hili kwa sababu sasa tutaenda kugawana vizuri. Kwa hiyo, wakati mwingine tunapolishwa maneno tukaanza kusema, tuweke akiba ya maneno juu ya nani anapinga nini, anasema nini, itatusaidia sana kama wanasiasa tukiwaweka akiba ya maneno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye mapendekezo haya ya Bajeti ya Kilimo. Bahati mbaya sana ni dakika tano na mambo ni mengi kidogo, lakini niwapongeze Wizara kwa kazi nzuri wanayofanya, Waziri na Manaibu wake, wanafanya kazi nzuri. Ninaamini kwamba mazonge yaliyopo kwenye Wizara ya Kilimo mengi wameyakuta kwa hiyo pengine hayawahusu sana isipokuwa wanao wajibu sasa wa kurekebisha tunapotokea hapa kwenda mbele pengine wafanye kazi ile ambayo inakusudiwa. Mengi kwa kweli siyo ya kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la kwanza ambalo ninataka kushauri Sekta hii ya Kilimo inachukua watu wengi sana lakini bahati mbaya sana ukiangalia mtiririko wa utengaji wa fedha ukilinganisha na Makubaliano kwa mfano ya Malabo ya asilimia kumi, sisi bado tuko kwenye average ya asilimia 1.2. Nadhani kama lengo letu ni kupambana na umaskini wa watu wengi kwa wakati mmoja, basi lazima tuongeze bajeti kwenye Wizara ya Kilimo, vinginevyo kasi ya kupambana na umaskini itakuwa shida. Kama tunataka kushughulika na umaskini wa watu wetu lazima tuongeze bajeti maana mtiririko wake kwa kweli ni mbaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mwaka jana hapa tulifanya mabadiliko madogo kwenye Sheria ya Korosho. Matokeo ya tulichokifanya watu wote tunajua, haihitaji kwenda shule kujua kwamba hali ya tasnia ya korosho sasa hivi ni mbaya sana, ni almost iko ICU, matatizo ni mengi, mambo ni mengi. Kulikuwa na nia njema ya Serikali, Rais akaweka nia njema, waliokwenda kuitekeleza nia njema ya Rais wamekwenda kugoroga na kuua Sekta ya Korosho.

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea,bahati mbaya zoezi lilikumbwa na dhuluma, lilikumbwa na rushwa, lilikumbwa na ubabaishaji mwingi sana na uongo mwingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea Jimbo la Mtama peke yake kwenye vyama vya msingi 11 wakulima ambao wana korosho chini ya tani 1,500 ambao wamehakikiwa mashamba yao zaidi ya 1,281 kwa miezi nane toka korosho yao ichukuliwe hawajapata senti tano, 1,281, lakini korosho yao imechukuliwa. Msimu umeanza hawana fedha za kutengeneza mashamba yao, hali ni mbaya.

Mheshimiwa Spika, sasa mapendekezo yangu; la kwanza; napendekeza tuilete Sheria ya Korosho hapa Bungeni, yote tuipitie upya ili tuokoe zao la korosho. Kile kipengele tulichokinyofoa kimesumbua sheria nzima, sasa ileteni sheria yote tupitie.

Mheshimiwa Spika, la pili, zoezi hili kwa kuwa lilikumbwa na maneno mengi, mengine ni ya uongo, ninapendekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aende kukagua atuletee ripoti hapa ndani ya namna zoezi lilivyokwenda ili tuchukue hatua ya kuziba mashimo kwenye yale maeneo ambayo yana shida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pendekezo la tatu, kama nilivyosema watekelezaji wa nia njema ya Mheshimiwa Rais wengi wamekwenda kukoroga mambo. Sasa ni vizuri waliokoroga wawajibike kwa matendo ya kuvuruga tasnia ya korosho. Na hapo ni vizuri tukawa specific, si sahihi kuingiza Serikali yote kwenye mambo yaliyofanyika hovyo, watu waliofanya hovyo wanajulikana na kama wasipochukua hatua wenyewe… (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Nape Nnauye, dakina moja ya kumalizia.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nasema hivi; waliokoroga kwenye jambo la korosho wachukue hatua wenyewe, wasipofanya tutaleta kusudio la kusema jinsi walivyoshiriki mmojammoja na jinsi ambavyo wanapaswa kuchukua hatua kwa sababu waliyoyafanya ni kuhujumu korosho, wananchi, lakini pia wamehujumu uchumi wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tukiulizana korosho yetu iko wapi, korosho haiwezi kukaa zaidi ya miezi sita hapa nchini ikabaki salama. Mkituambia bado mna korosho sahihi, korosho inayoweza kutumika, huu ni uongo, tukiendelea kusema uongo huu na bado hatuoni aibu tunaendelea kubaki, sio sawa. Ndiyo maana wito wangu, leteni sheria tuipitie upya, CAG aende akakague lakini waliotukoroga wawajibike na msipowajibika tutaleta hoja hapa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye mapendekezo ya bajeti hii ya Wizara ya Nishati. Nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri wanayofanya, wanafanya kazi nzuri sana na wasaidizi wao. Kwa kweli katika Mawaziri wasikivu na wanyenyekevu nadhani Mheshimiwa Kalemani na msaidizi wake wanafanya kazi nzuri sana. Na hii haimaanishi kwamba, hakuna changamoto, lakini usikivu wao na unyenyekevu wao unapunguza sana machungu ambayo yangekuwepo kwenye Wizara hii kwa hiyo, kwa kweli nawapongeza na nadhani waendelee hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nataka niipongeze sana Serikali kwa kuhuisha, kwa kufufua na kuendeleza mazungumzo juu ya mradi wa uwekezaji pale Lindi wa LNG. Tulipiga kelele hapa, nadhani bajeti mbili zilizopita, lakini Serikali imesikiliza na imehuisha na Mheshimiwa Waziri juzi umekuja Lindi kwa mazungumzo yale tunayo matumaini sasa kwamba, mradi huu ambao kwa kweli kwanza ni mkubwa kuliko miradi yote mikubwa katika nchi yetu na hata ukijumlisha ukichukua reli, ukachukua ATC, ukachukua Stiegler’s, ukijumlisha kwa pamoja Mradi wa LNG bado una thamani kubwa kuliko miradi yote kwa pamoja. Kwa hiyo, naamini uamuzi huu ni uamuzi wa busara, uamuzi mzuri, nimesimama kuipongeza kwa dhati Serikali yangu kwa kazi nzuri mnayofanya kwenye mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi huu pamoja na kwamba, ni mkubwa lakini mradi huu ni ushahidi wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza miradi mikubwa ya namna hii kwa sababu, hela za Serikali zitakazoingizwa ni kidogo sana. Sehemu kubwa ya fedha hizi karibu dola bilioni 30 ni fedha ambazo zinaletwa na sekta binafsi kwa hiyo, ni mfano mzuri wa ushiriki wa sekta binafsi katika uendelezaji wa miradi mikubwa. Ninaipongeza Serikali kwa uamuzi huu, sasa ninayo mapendekezo mawili yafuatayo:-

Mheshimiwa Spika, la kwanza tukamilishe mazungumzo yamechukua muda mrefu na wenzetu wanaotuzunguka wata-take advantage ya kuchelewa kwetu na halitakuwa jambo zuri. La pili, ushiriki wa wazawa, local contents kwenye huu mradi, Serikali haiwezi kukwepa wajibu wake, tukiwaachia wazawa peke yake ushiriki wao utakuwa mdogo; wito wangu kwa Serikali vizuri Serikali ikajihusisha kwenye maeneo mawili, moja kuzionesha fursa na kuwapa elimu wazawa ili washiriki vizuri, lakini ya pili kuwawezesha hawa wazawa washiriki.

Mheshimiwa Spika, nchi za wenzetu huwaachi wananchi wako wakaenda wenyewe. Ukiwaacha wataenda kushiriki kuuza nyanya, lakini kama tunataka washiriki kwa ukweli kwenye Wizara yako, lakini Wizara ya Uwekezaji, vizuri tukaanzisha room ambayo itawachukua wazawa na kuwawezesha kiuchumi ili washiriki, ili local content yetu iwe nzuri. Kwa hiyo, pamoja na pongezi, lakini malizeni mazungumzo ya huu mradi, lakini pia Serikali ijipange kuwawezesha wazawa kushiriki kwenye huu uchumi mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili nataka nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya kwenye REA yeye na Naibu wake. Wanafanya kazi nzuri sana, wanakimbizana sana, najua wakandarasi kwenye maeneo mengi wanawaangusha kwa sababu kasi yao ndogo, lakini kwa kweli mnyonge mnyongeni, Waziri Kalemani na Naibu wake wanafanya kazi nzuri, wanakimbizana, wanajituma. Ninaamini kama kuna Wizara Mheshimiwa Rais ameweka Mawaziri wazuri, hii Wizara amefanya kazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo mapendekezo mawili; la kwanza nadhani ni vizuri tukaligawa Shirika letu la TANESCO, mapendekezo haya yamekuwa yakizungumzwa. Hebu fikirieni kwa miaka mingi inazungumzwa tugawe uzalishaji, usambazaji na uuzaji yawe ni maeneo tofauti yanayojitegemea, itasaidia sana kuboresha utendaji wa Shirika letu la TANESCO. Na kwenye upande sasa wa uzalishaji kwa sababu tunakwenda kwenye kuzalisha umeme kwa kutumia vyanzo tofauti, vizuri tukavutia wawekezaji binafsi kutoka kwenye private sector watusaidie kwenye kazi ya kuzalisha umeme halafu kazi ya kusambaza iendelee. (Makofi)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ninaunga mkono hoja na mapendekezo ya Wizara hii, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie kwenye hoja iliyoko mezani ambayo imetokana na taarifa za Kamati zetu na nitakwenda kujikita kwenye taarifa iliyotokana na Kamati ya Miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia kidogo, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais Samia kwa kuniamini na kuniteua kuwa Waziri kwenye kusimamia sekta hizi za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Ahadi yangu kwake na kwa Watanzania kwamba sitamwangusha, nitatimiza wajibu wangu kama inavyotakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kuipongeza Kamati ya Miundombinu chini ya Mwenyekiti wetu Mheshimiwa Kakoso na Wajumbe wote wa Kamati hii kwa kazi nzuri sana na ripoti nzuri waliyoiwasilisha mezani leo, wanafanya kazi nzuri sana. (makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie mambo mawili makubwa. La kwanza, kumekuwa na malalamiko ya muda juu ya namna ambavyo bundles zetu zinatumika kwenye simu zetu. Kuna uwekezaji mkubwa sana umefanyika kwenye Taasisi yetu ya Kudhibiti Mawasiliano ya TCRA. Awamu ya Tano imefanya uwekezaji mkubwa, lakini Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa sana, kiasi kwamba uwezo wao wa kufuatilia miamala hii mbalimbali umeongezeka sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaendelea kuchambua malalamiko ya matumizi ya hizi bundle kwenye simu zetu. Hoja hii kwamba kuna bundle ambazo zinawekwa kwenye simu, zinatumika bila mtumiaji kuzitumia yamekuwepo haya malalamiko, yamefikishwa kwenye mamlaka husika na uchambuzi umefanyika. Matokeo ya uchambuzi yanaonesha, matokeo ya uchambuzi ambayo yamefanyika mpaka sasa yanaonesha hakuna wizi uliotokea, isipokuwa kuna tatizo la matumizi ya simu za kisasa na matatizo hayo yamejikita kwenye maeneo mawili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja hizi simu za kisasa wakati mwingine hata ukiwa huitumii kuna baadhi ya applications zinaendelea kufanya kazi nyuma ya simu na zinatumia bundles ambazo umeziweka. Matokeo yake ukija ukiangalia unakuta bundle imetumika, wewe unaona hujaiutumia, lakini kuna applications zimeendelea na kwa sababu sasa ni simu za kisasa, wakati mwingine ujuzi wa kujua kwamba kuna applications zinaendelea imekuwa shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu ya pili; simu hizi za kisasa unaweza ukaweka bundle lako, ukawasha kuna kitu kinaitwa hotspot, kinachoruhusu mtu mwingine kutumia data uliyonayo bila kufunga, ukiweka password ni lazima umruhusu, usipoweka wapo watu wamelalamika simu zao zilipochunguzwa ikakutwa kuna watu wametumia kwa kujiunga wakatumia wifi wakatumia bundle zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa suluhisho ni nini? Tunayo mamlaka ya watumiaji ni Baraza la Watumiaji wa Huduma za Simu, wametengeneza application ambayo ipo kwenye majaribio ambayo ikianza kutumika itamsaidia mtumiaji wa simu awe anafuatilia matumizi ya bundle aliyoiweka na atakuwa na option sasa ya kuzima baadhi ya applications ambazo zinatumia mtandao wake. Kwa hiyo, kwa hapa tulipofika tunafanya majaribio ya application hiyo na ikishakuwa tayari watumiaji watapewa, wanatafuatilia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hili, tumejikita kwenye kutoa elimu ya matumizi ya hizi simu za kisasa ili watu wasijikute wanaingia kwenye gharama ambazo hazina sababu kwa kutokujua. Utafiti umeonesha shida kubwa ni kwenye matumizi badala ya wizi, mpaka sasa hatujakamata wizi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, muda umekwisha?

MWENYEKITI: Muda umekwisha, lakini kwa sababu unaongelea bundle nakuongezea dakika moja. (Makofi)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Jambo hili limekuwa kubwa na kwa sababu limekuwa linazungumzwa kwa muda mrefu ni rahisi kudhani kuna wizi na tukawahukumu operators kwamba wanaiba, lakini Mamlaka ya Mawasiliano malalamiko yote ambayo mpaka sasa yamefikishwa kwenye mamlaka, hakuna lalamiko ambalo limethibitisha kuna wizi. Bado yanaendelea kupokelewa, lakini tunadhani njia mbili kubwa za kutumia; moja tutoe elimu ya matumizi ya simu za kisasa; lakini ya pili kubwa kuliko yote tutengeneze application ambayo imeshatengenezwa inafanyiwa majaribio. Huu utakuwa ni muarobaini kwa sababu itakwambia umetumiaje data yako, ni application gani umetumia zaidi na umetumia kwa wigo gani. Tunadhani hili litaondoa haya maneno.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru Sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo. Kwanza nimpongeze Waziri wa Fedha kwa mpango mzuri aliouleta, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujipambanua kusukuma maendeleo ya watu. Nishukuru sana kwenye mpango huu kuna mawazo mazuri na uamuzi wa busara wa Serikali kutumia TEHAMA katika kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa ujumla wake hatufurahishi sana na mahusiano yaliopo kati ya watoa huduma za mawasiliano na watumiaji wa huduma za mawasiliano, hakuna mahusiano mazuri. Kumekuwa na mashaka makubwa na kutuhumiana kukubwa sana. Sasa Serikali inachukua hatua zifua tazo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; tunadhani kuna mapungufu kwenye kanuni zinazosimamia huduma zinazowasimamia watoa huduma na watumiaji wa huduma katika kuzipata hizi huduma, na hasa kwenye maeneo ya wajibu wa watoa huduma na wajibu wa watumia huduma. Serikali tumefanya uamuzi wa kuzipitia upya kanuni hizi ili tuone mashimo yako wapi ili mahusiano haya yarekebishwe, huduma za mawasiliano nchini ziboreshwe. Hapa niwathibitishie Waheshimiwa Wabunge mawazo yenu tumeyachukua na mawazo ya wananchi katika hili tumechukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, wananchi wanasema tunapobadilisha bei ya bando kwa nini tunapeleka matangazo kwenye vyombo vya habari badala ya kumpelekea mtumiaji moja kwa moja? Tunadhani hii ni hoja ya msingi kwamba siku moja kabla ya mabadiliko mwananchi apelekewe taarifa moja kwa moja kwenye simu yake afanye uamuzi anaendelea na matumizi ya bando hilo au anabadilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili tunalolifanyia kazi, tunao utaratibu, kila baada ya miaka mitano, kunafanyika tathmini ya gharama halisi za usafirishaji wa data katika huduma ya mawasiliano. Gharama ya mwisho ilifanyika mwaka 2018, tathmini ikatupa range ya shilingi mbili mpaka shilingi tisa. Sasa ni miaka mitano tunafanya tathmini hiyo, mwezi wa 12 mwaka huu, tathmini hiyo itakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwelekeo unavyoenda, kwa sababu kuna uwekezaji mkubwa umefanyika, kuna hatua zinachukuliwa za kikodi, lakini pia kuna taratibu zinaendelea, kwa hiyo, mwelekeo unavyotupeleka, tunadhani matokeo ya tathmini yatashusha gharama za usafirishaji wa data nchini. Kwa hiyo, hayo mambo mawili ya msingi tunayafanyia kazi.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Nape, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mheshimiwa Waziri anafanya kazi nzuri, lakini wakati anaendelea, nataka kujua jambo moja; huwa inanisikitisha sana na nimelisema muda mrefu pole pole naona haliendi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina shilingi 3,000,000 kwenye benki, mimi ni mchungaji, niko porini kule nachunga; salio limeniishia kwenye simu, nataka kutoa fedha kwenye benki kwa kutumia sim banking, wananiambia niweke salio nami sina uwezo wa ku-access hili salio, sina, nimeishiwa; kwa nini benki au hii mitandao wasifanye mawasiliano na mimi ili hela yangu inapokuwa nimeichukua bure, ikatwe kwenye benki? Yaani mimi nina hela kwenye simu, halafu inafia porini! Siwezi kutoa hela kwa sababu sina tu vocha ndani? (Makofi)

MWENYEKITI: Sasa Waheshimiwa Wabunge, hiyo ni taarifa au unachangia na wewe una hoja yako mpya kabisa umeileta ambayo haikuwa umeizungumza? Mheshimiwa Waziri naomba utiririke na yale maelezo yako, hii taarifa iweke kando kwanza, kwa sababu inaleta jambo jipya. Ni la msingi, lakini ni jambo jipya. (Kicheko/Makofi)

WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Hoja ya pili ambayo nilitaka kuichangia hapa, kumekuwa na mjadala kwamba kulikuwa na mtoa huduma ambaye aliamua kubadilisha bei ya bundle lake kabla hajabadilisha taarifa kwenye bango lake. Asubuhi nilitoa taarifa hapa kwamba Serikali tumechukua hatua, tumemwita TCRA, bahati nzuri, huyu mtoa huduma amekiri uzembe katika kutekeleza wajibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tumechukua hatua zifuatazo: Moja, tathmini iliyofanyika imeonesha walioathirika na jambo hili ni watu 22,107 walitumia huduma wakati zile taarifa hazijabadilishwa. Baada ya kuling’amua hili, Serikali imemwagiza mtoa huduma: kwanza, awarudishie hawa walioathirika MB zao 200 ambazo walitakiwa wazipate kutokana na bango lake lilivyokuwa; pili, awape MB 300 kila mwathirika kama fidia ya usumbufu alioupata kwa sababu ya uzembe uliofanywa na mtoa huduma; na tatu, tumemtaka mtoa huduma awaombe radhi watumiaji wa huduma hiyo walioathirika kwa kuwatumia ujumbe kwenye simu zao kueleza uzembe alioufanya. Hii itakuwa ni hatua za mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali tunatamani tuone kuna mahusiano mazuri kati ya watoa huduma na wapokeaji wa huduma. Sasa mahusiano haya, moja ya eneo kubwa ambalo ni muhimu tukalipitia na hli ndilo ambalo tumeanza nalo kazi, ni kutengeneza hizi kanuni. Zilizopo tuzipitie, lakini kama iko haja, tutengeneze kanuni nyingine mpya, zi-regulate mahusiano haya ili mtoa huduma ajue wajibu wake na mpokea huduma ajue wajibu wake. Tunaamini hili likifanyika, mawasiliano nchini yataboreka na matumizi ya TEHAMA yatakuwa bora na uchumi wetu utaimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo taarifa zilizowekwa mbele ya Bunge lako leo. Nichukue nafasi hii kulipongeza Bunge kwa kazi nzuri ya kuisimamia Serikali kupitia Kamati hizi mbili; Kamati ya miundombinu na Kamati ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, specific kwa Kamati ya Miundombinu, kwa Taarifa yake, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Kamati hii kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wanaifanya katika kipindi cha Taarifa hii chini ya Mwenyekiti Ndugu Kakoso ,Makamu Mwenyekiti Mama Anna Kilango na Wajumbe wake, wanafanya kazi nzuri sana ya kuisimamia Serikali na kushauri. Mafanikio tunayoyaona ni matokeo ya ushauri mzuri na kazi nzuri inayofanywa na Kamati hii kwa niaba ya Bunge. Kwahiyo tunawashukuru sana Kamati kwa kazi nzuri waliyofanya.

Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwanza kwa msukumo wa kipekee aliyouweka kuhakikisha Sheria ya Taarifa Binafsi inatungwa na kuletwa Bungeni; na nalishukuru Bunge lako kwa kuipitisha Sheria ile. Pia namshukuru kipekee Rais kwa kuisaini kwa wakati na sasa iko tayari kuanza kufanya kazi. Wizara tunakamilisha Kanuni zitakazoiwezesha Sheria hii kufanya kazi. Sheria hii imetupa heshima duniani, imetuingiza katika nchi salama mtandaoni kwenda kuwekeza na kufanya shughuli. Kwakweli Mheshimiwa Rais ametutendea haki katika jambo hili na tuna sababu za kumpongeza na kulipongeza Bunge lako kwa kutunga Sheria hii. Sheria hii itakapoanza kufanya kazi tunahakika usalama mtandaoni utakuwa mzuri. Wakati tunakwenda kutunga kanuni tutawashirikisha wadau ili washiriki kuhakikisha kanuni hizi zinatungwa vizuri, zinaendana kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na kuhakikisha mtandao wetu unakuwa unakuwa salama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili niishukuru Kamati na nilishukuru Bunge lako. Inavyoonekana kwa kauli moja wameunga mkono uwamuzi wa kufungia simu ambazo haziko halali katika mtandao wa nchi yetu. Kwa mahesabu ambayo tumeendelea kuyatoa mpaka jana tulikuwa na simu takriban million mbili na kitu ambazo hazijahakikiwa. Tunaendelea kutoa hizi siku mpaka tarehe 13. Tunaamini kwa kauli moja, kwakuwa tumekubaliana kudhibiti uhalifu kwenye mtandao basi tunashukuru kwa endorsement iliyopatikana; na tarehe 13 Mwezi 2 saa kumi jioni kama kuna simu itakuwa haijahakikiwa hatutasogeza muda tutaifunga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa usalama wa mtandaoni unategemea Sheria, unategemea mifumo lakini unategemea pia usimamizi. Tumeongeza usimamizi kwenye baadhi ya maeneo, Sheria zimetungwa na tunaendelea kuzitunga na mifumo inaendelea kuwekwa. Hapa pametokea malalamiko na yamekuwa yakizungumzwa na Kamati imegusia. Bado kuna message nyingi ambazo watumia huduma za mawasiliano wanazilalamikia, kwamba zinatumwa kwao bila wao kutaka wala kuziomba; na message nyingi zinahusiana na biashara na biashara zenyewe za hovyo, biashara za waganga wa kienyeji mambo ya betting sijui mambo ya kuhamasisha biashara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria iko wazi, na kwenye hili nataka kuchukua nafasi hii kuwataka TCRA, nadhani tumevumiliana vya kutosha, sasa tuchukue hatua tukomeshe jambo hili. Watu wamelalamika sana inatosha, tunaharibu jamii yetu. Watu wanatumia taarifa za watu, wanawatumia message ambazo kwa kweli zimegeuka kuwa usumbufu. Hili jambo limezungumzwa kwa kina hapa na sisi kama Serikali tunalipokea, na kupitia TCRA hii ndiyo kauli ya mwisho, tunataka hili jambo likome. Tumezungumza, tumevumiliana, imefika wakati sasa inatosha. Watoa huduma za mawasiliano, kwasababu message, zinapitia kwao. Mtoa huduma ambaye ataruhusu jambo hili sasa tutachukua hatua na bila shaka ndiyo itakuwa suluhisho la jambo hili. Inatosha, message zimekuwa nyingi. Kwa hali ilivyo tukiendelea kuruhusu jambo hili nadhani tutakuwa hatuwatendei haki watumia huduma za mawasiliano.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupitisha Mfumo wa Anuani za Makazi, na bahati nzuri kamati imezungumza vizuri, kwamba mfumo huu utaendelea kujengwa, utaendelea kuhimarishwa na kuboreshwa. Tuko hatua za mwisho za mchakato wa kutunga kanuni, na pengine sheria za kuufanya sasa mfumo huu uwe katika matumizi ya kawaida. Sasa hivi unaweza usione effect yake kwa sababu bado hakuna kanuni za kuufanya utumike. Tunakoelekea huduma nyingi zitatolewa kwa kuzingatia pia Mfumo wa Anuani za Makazi; na hii itarahisisha sana utoaji wa huduma.

Mheshimiwa Spika, suala la mwisho kwenye ripoti imezungumzwa changamoto tuliyonayo hasa kwenye mipaka ya nchi yetu, suala la huduma za mawasiliano lakini pia suala la usikivu wa shirika letu la utangazaji.

Mheshimiwa Spika, pamoja na bajeti yake kuwa ndogo lakini hivi tunavyoongea tuko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha makubaliano kati ya TTCL na TBC ili kuwawezesha TBC watumie minara ya TTCL kupeleka huduma ili tukabiliane na changamoto ya uwekezaji wa minara kwa shirika letu la utangazaji. Tunaamini jambo hili likitekelezwa litaongeza usikivu wa shirika letu. Hivi leo tunavyoongea, tarehe 31/01/2023, ile minara 763 tenda yake imefunguliwa leo. Tunaamini baada ya hapa tutatengeneza mchakato mzuri. Niahidi mbele ya Bunge lako, siku tutakapowakabidhi wajenzi tutaomba kibali tukutane Wabunge wote tukiwa hapa ili tushuhudie kukabidhiwa hawa wanaokwenda kujenga, na kila mmoja amuone nani anakwenda kujenga kwenye eneo lake ili isaidie ufuatiliaji, na bila shaka itapunguza tatizo tulilonalo la Mawasiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono Hoja za Kamati. Nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye mapendekezo haya ya bajeti. Nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na timu yake nzima kwa kazi nzuri wanayofanya, najua wanapitia kwenye mawimbi wakati mwingine, lakini ndio kazi zenyewe zilivyo, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri hongera sana kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia niipongeze Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti nadhani wamefanya kazi nzuri sana ukipitia report yao wameweka mambo mengi ya msingi ambayo wameyashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, upande wa Serikali nipongeze uamuzi wa kufuta tozo mbalimbali mlizozifuta, ninaamini nyingi zitasaidia kurahisisha ufanyaji wa biashara katika nchi yetu, nadhani hili jambo ni zuri na ni jambo la kutiwa moyo. Sasa tuende mbele zaidi tukaangalie zile tozo ambazo zina positive impact kwa wafanyabiashara na impact yake ni kubwa zaidi, hizi ziko nyingi ziko 54; lakini nyingi ni ndogondogo sana na pengine madhara yake yanaweza yasionekane sana kwa hiyo tuende zaidi ya hapo tulipoenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru sana Serikali kwa kukubali pendekezo la kufuta tozo kwenye visima vile, visima vya watu binafsi nadhani uamuzi huu ulikuwa mzuri, ninaishukuru Serikali kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Mtama, lakini na kwa niaba ya watumiaji wa visima kwa sababu nadhani hii ilikuwa ni kero kubwa, Serikali imekubali, imelifuta naomba nichukue nafasi hii kuishukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sasa Mheshimiwa Waziri nadhani tuende mbali kidogo Kamati ya Bajeti imependekeza msamaha wa kodi kwenye ongezeko la thamani kwenye mitambo ya kuchimba visima vya maji. Kwa hiyo, pamoja na kufuta tozo lakini nadhani sasa fikirieni kwa sababu Mheshimiwa Waziri magonjwa mengi nchini hapa chanzo chake ni maji, lakini mitambo hii ikifutwa kodi, mitambo hii itatumika kuchimba visima, lakini pia itatusaidia kwenye kilimo kwenye kuchimba malambo. Kwa hiyo, ninaunga mkono pendekezo la Kamati ya Kudumu ya Bunge kwamba pamoja na kufuta tozo kwenye visima basi tuende mbali tufute pia VAT kwenye mitambo ya kuchimbia visima. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaunga pia mkono pendekezo la Kamati ya Kudumu ya Bunge wamezungumzia kwa kina mgawanyo wa bajeti yetu. Bajeti yetu kwa sehemu kubwa na Kamati imeeleza, imepeleka fedha nyingi kwenye maeneo ya ujenzi na miradi mikubwa tuliyonayo, sio jambo baya kuwekeza kwenye hii miradi. Lakini sekta ambazo zinahusishwa watu wengi katika nchi yetu ni sekta ya kilimo ndio inahusisha watu wengi sana, karibu asilimia 70 ya Watanzania wanajihusisha na kilimo, lakini kinazalisha ajira kwa asilimia 65, asilimia 85 karibia ya bidhaa tunazouza nje zinatokana na kilimo, lakini inachangia Pato la Taifa kwa asilimia 29 na kwa asilimia zaidi ya 100 chakula cha nchi hii kinategemea kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii ndiyo sekta ambayo ikiguswa inagusa maisha ya watu wengi na tungeweza kupambana na umaskini wa watu wetu kwa kiwango kikubwa. Ukiangalia mtiririko wa bajeti mwaka 2016/2017 kwa bajeti ya maendeleo tulitenga asilimia 1.38 ndio tukapeleka kilimo; asilimia 1.38, sekta ambayo ndio inabeba watu wengi.

Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 tukatenga asilimia 1.25, mwaka 2018/2019 tukatenga asilimia 0.81 na huu ni utengaji sio upelekaji wa fedha, mwaka 2019/2020 tukatenga asilimia 1.17 ya fedha za maendeleo. Sasa hili ndilo eneo kubwa na kupanga ni kuchagua, kama tunataka kushughulika na umaskini wa watu wetu, tunataka kushughulika na watu walio wengi mimi nilidhani vipaumbele vyetu na mgao wetu eneo kubwa la fedha zingeenda huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kama tumeshindwa kutenga fedha nyingi na upelekaji wa fedha kwenye sekta hiyo ambayo inagusa watu wengi unasuasua, mimi nilidhani ule utaratibu tulioanza nao mwaka 2016/2017 wa kufuta tozo nyingi kwenye eneo la kilimo ili itusaidie tungeendelea nao ingesaidia inge-replace hili ambalo tumeshindwa kulifanya la kutenga fedha nyingi kwenye sekta ya kilimo. Lakini safari hii tume-deal na tozo kwenye biashara, kwenye kilimo tumefumba macho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakumbuka tulikuwa tunatenga fedha hapa kwa ajili ya pembejeo, kuna wakati tulifikia mpaka bilioni 200 tumeziondoa, pembejeo hakuna hazipatikani, viwanda vya kutengeneza havipo sasa na bado tozo bado ziko nyingi, pendekezo langu ni kwamba tuende tukazipunguze.

Mheshimiwa Spika, eneo la pili; wigo wa wawalipa kodi kwa muda sasa imekuwa tukizungumza, kuna takwimu sina hakika kama bado ni hizo hizo kwamba inategemewa walipa kodi wako kama bilioni 14 wanaolipa ni milioni 2.5, kwa hiyo mzigo wa wawalipa kodi wengi ambao walitakiwa kulipa unabebwa na asilimia ndogo sana ya Watanzania. Sasa Mheshimiwa Waziri mimi nilidhani tungeanza hata kama ni kidogo kuupanua huu wigo wa wawalipa kodi tungekuwa tumepiga hatua fulani na wigo ungepanuka, nimemsikia mama yangu pale akizungumza hoja ya wafanyakazi, tunajua mshahara kidogo hatujapandisha maisha yao yanaendelea kuwa magumu.

Mheshimiwa Spika, mimi nilidhani tungekuwa tumepanua wigo wa walipa kodi tungeweza kushughulika kupunguza kodi hasa kwa wafanyakazi na hasa wafanyakazi wa chini. Ukichukua takwimu leo wafanyakazi wote nilisikia mama alizisema pale karibu shilingi bilioni 971 zinategemewa kutokea kwenye pay as you an ya wafanyakazi wa Serikali. Lakini wako wale wa chini kabisa walimu ambao ni wengi na ndio wanateseka tunategemea shilingi bilioni 194 tungezikata hata kwa asilimia 50 ambayo unapata shilingi bilioni 97, hizi tukazipeleka kwenye chanzo kingine ambacho tumekibuni huu mzigo ungepungua kutoka kwa wafanyakazi na hasa walimu.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi nadhani tungeianza hii hatua tulipo-introduce vitambulisho vile vya kitaifa lengo moja wapo ilikuwa ni ku-formalize sekta zetu lakini kwa kiasi gani tumeitumia imetusaidia kwa kiasi gani tusipotanua wigo wa wawalipa kodi tutaendelea kuwabebesha watu wachache mzigo mkubwa wa wawalipa kodi na kwa sababu mzigo unakuwa mkubwa wana-tendency ya kujitahidi kukwepa kwa sababu mzigo ni mkubwa sana. Kodi nzuri ni ile ambayo inalipika na inalipika kwa wakati, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nilikuwa napendekeza hebu tuanze basi tutoke hapa tulipo tuongeze wigo wa wawalipa kodi.

Mheshimiwa Spika, kwenye taarifa nilizozisoma hapa inaonesha kwamba sekta ya sanaa na burudani imekua kwa kiwango kikubwa, lakini ukweli sekta hii inakua kwa kudra. Sheria, kanuni na taratibu tulizonazo zinazosimamia sekta hii zimepitwa na wakati sana. Sasa lazima ifikie mahali Serikali twende tujikite tuzibadilishe sheria na taratibu zinazozisimamia sekta hii ambayo tunakubaliana kwamba inakua kwa kiwango kikubwa basi iendane na wakati, kwa sababu sheria tulizonazo zimepitwa na wakati na hazisaidii ukuaji wa hii sekta. Kwa hiyo mapendekezo yangu moja, tuangalie mgawanyo wa fedha tunaupeleka wapi kule ambako wapo watu wengi nadhani ndiko ambako tulipaswa kupeleka fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili ni vizuri tukaangalia namna ya kupanua wigo wa wawalipa kodi tusibaki na namba ile tunacheza nayo unarudisha, unajumlisha, unatoa mzigo unakuwa mkubwa sana. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana malizia.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Mtama kwa kuniamini na kunipitisha bila kupingwa kuwa mwakilishi wao ndani ya Bunge hili, nakishukuru pia chama changu, Chama cha Mapinduzi, kwa kunipa dhamana hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Kwa kuwa muda hautoshi, naomba nizungumze mambo mawili. Mpango huu ni mzuri sana lakini utafanikiwa tu ikiwa kutakuwa na fedha za kuutekeleza. Fedha zinapatikana kutoka kwenye makusanyo ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto kubwa sana inaendelea katika nchi yetu. Ukusanyaji wa kodi ni taaluma na katika historia ni taaluma ya muda mrefu sana. Changamoto tuliyonayo ni kwamba tumeamua kuacha kuwatumia wataaluma ambao ndiyo wakusanya kodi badala yake tunatumia Task Forces kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Task Forces kwa sababu siyo taaluma yao, wanachofanya wanakwenda kuua biashara. Kelele hizi zote unazozisikia ni kwa sababu tumeamua kuacha kutumia taaluma ya ukusanyaji wa kodi, tumeamua kutumia Task Forces kukusanya kodi na kwa sababu siyo taaluma yao wanachoangalia ni kufikia lengo walilowekewa. Kinachotokea ni kwamba wanakwenda kwa mfanyabiashara, hawajali maisha yake ya kesho, hawajali kwamba wanatakiwa wakusanye kodi leo wamuachie uwezo wa kuzalisha ili wakusanye na kesho. Tunafurahia matokeo ya muda mfupi; ni kweli tumefanya kazi nzuri ya kukusanya kodi, lakini haya matokeo tunayoyafurahia ni ya muda mfupi sana kwa sababu idadi ya biashara zinazofungwa ni nyingi mno, kesho hatuna ng’ombe wa kumkamua maziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali, hebu punguzeni habari ya Task Forces kukusanya kodi, siyo kazi yao, hawa wanakwenda kuua biashara. TRA ilianzishwa kwa kazi hiyo na watu wamesomea. Tukijiwekeza kwenye Task Forces kesho hatutakuwa na cha kukusanya kwa sababu siyo kazi yao. Nimeambiwa baadhi ya maeneo wanakwenda na draft ya kesi za uhujumu uchumi, wanawatisha watu, watu inabidi watoe fedha, wakitoa fedha wanafunga biashara zao. Sasa mwendelezo wa hiki tunachokifanya mwisho wake utakuwa nini? Ushauri wangu Serikali ondokeni kwenye Task Forces, rudini kwenye taaluma ya ukusanyaji wa kodi itatupa uhalali wa kuendelea kukusanya hiyo kodi kesho na kesho kutwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili, tumefanya vizuri sana kwenye kuungamanisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu kwenye Sekta ya Elimu. Tumetoa elimu ya msingi bila malipo kwa kipindi cha miaka mitano; siyo kazi ndogo. Hata tulipofanya uamuzi huu tulijua ni kazi kubwa. Nampongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa kazi nzuri waliyofanya ya kutekeleza jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ushauri wangu; tumetekeleza kwa kipindi cha miaka mitano, tumefanya vizuri lakini bila shaka umefika wakati tupitie changamoto tulizokutana nazo katika kipindi cha miaka mitano halafu tufanye marekebisho kwa baadhi ya maeneo. Hapa ntatoa mfano, tunatumia kigezo cha idadi ya wanafunzi kupeleka fedha, kigezo hiki nadhani kimepitwa na wakati, twende tutanue. Kwa sababu mtu mwenye watoto kumi na mwenye watoto 200 baadhi ya mahitaji yanafanana, ukimpelekea fedha ileile unamuua huyu mwenye watoto wachache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani ni vema Serikali tupitie upya, tuangalie hivi vigezo tunavyovitumia vya kupeleka fedha kusaidia elimu bure. Jambo hili ni jema lakini tupitie upya tuliboreshe, tulifanye vizuri ili tuongeze vigezo vya kupeleka fedha. Fedha za utawala zizingatie mahitaji ya kiutawala. Fedha za kuangalia mwenendo wa watoto, performance yao zifuate hivyo vigezo vingine lakini tuongeze idadi ya vigezo; nadhani hili jambo litatusaidia twende mahali pazuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nakushukuru kwa nafasi uliyonipa. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nichangie kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, na kwa niaba ya wananchi wa Mtama nitoe pole kwa familia ya Dkt John Pombe Magufuli kwa kufiwa na Mheshimiwa Rais. Lakini kwa wana CCM kwa kufiwa na Mwenyekiti wa chama chetu na kwa watanzania nitoe pole nyingi sana kwa kifo cha huyu mzalendo wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajisikia fahari kwamba nilishiriki ndani ya chama na nje ya chama katika mchakato wa kumpata Dkt John Pombe Magufuli mwaka 2015. Amefanyakazi nzuri kwa Taifa letu ameacha alama nyingi kubwa ambazo hazitasahaulika. Lakini ameacha mafunzo mengi kwa nchi yetu, kwa chama chetu, kwa bara la Afrika na hata dunia inajadili mafunzo aliyotuachia. Kwa hiyo, ninajisikia fahari kwamba nilishiriki mchakato wa kupatikana kwake, na namshukuru Mungu kwa maisha ya Dkt John Pombe Magufuli kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kukipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kusimamia vizuri mchakato wa mpito kutoka Rais Dkt. Magufuli kwenda kwa Mama Samia usimamizi mzuri uliofanywa na chama umethibitisha kwamba CCM bado ni chama bora sana kwa nchi yetu, kwa Bara la Afrika na duniani. Wamesimamia vizuri mchakato niwapongeze viongozi na chama changu. Siyo nchi nyingi zinaweza kusimamia mchakato wa namna hii wengine ingekuwa fujo na vurugu. Chama kimeonyesha uwezo mkubwa wa kuendelea kuiongoza nchi yetu kwahiyo nakipongeza chama changu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze pia vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuiheshimu katiba ya nchi yetu na kuisimamia vizuri hongereni sana Mabeho na wenzako kwa kazi nzuri mliyofanya katika kipindi chote cha mpito. Nchi yetu imepitia Awamu tano na sasa tuko Awamu ya Sita ya uongozi Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikaa miaka karibia 24. Awamu ya pili ya mzee Mwinyi, Awamu ya Tatu ya mzee Mkapa, Awamu ya Nne ya mzee Kikwete, Awamu ya Tano ya Dkt Magufuli na sasa Awamu ya Sita ya mama Samia Suluhu Hassan. Katika awamu zote hizi chama kimesimamia viongozi wake kufanyakazi nzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere alikuja mzee Mwinyi. Mzee Mwinyi Pamoja na kuendeleza mambo mazuri sana yaliyofanywa na Mwalimu Nyerere kuna baadhi ya mambo alifanya maboresho na marekebisho na ndiyo maana tukaenda vile tulivyokwenda. Alipomaliza mzee Mwinyi akaja mzee Mkapa akaendeleza mambo mazuri yaliyofanywa na mzee Mwinyi na akafanya baadhi ya maboresho na marekebisho pamoja na ndoto zake lakini tukasonga mbele na yale mazuri ya mzee Mwinyi na marekebisho aliyoyafanya mzee Mkapa tukasonga mbele nchi yetu ikapiga hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, akaja mzee Kikwete pamoja na ndoto zake za chama na mengine lakini alifanya baadhi ya marekebisho kwenye yale yaliyotokea wakati wa mzee Mkapa. Akaja Dkt Magufuli Awamu ya Tano amefanya mambo makubwa lakini alifanya marekebisho makubwa sana kwenye mambo yaliyotokea kwenye awamu zilizopita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho yale ndiyo yameipa heshima Tanzania yetu leo na tukamuunga mkono akafanya marekebisho na haikuwa nongwa hata kidogo. Amekuja Rais wa Awamu ya Sita mama Samia pamoja na ndoto nzuri na muendelezo wa ndoto na amesema hadharani tutaendeleza yale aliyoyaanzisha Dkt John Pombe Magufuli na sidhani kama kuna mtu anataka haya mambo yaachwe kama yako mahali ni marekebisho madogo madogo ambayo yanafanyika vizuri na mama Samia ameanza vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Awamu ya Sita pia kama zilivyofanya awamu zingine ataendeleza ndoto lakini kule ambako anapaswa kufanya maboresho ili mambo yatekelezwe vizuri nadhani tumpe ushirikiano ayafanye hayo maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mzee Mwinyi alituambia kila zama na kitabu chake zama za Mwalimu zilikuwa na kitabu chake, zama za mzee Mwinyi na kitabu chake, na wakati huo mzee Mwinyi alifanya marekebisho makubwa na haikuwa rahisi kutoka kwa mwalimu amekaa miaka 24 anakuja mzee Mwinyi anafanya marekebisho haikuwa rahisi na wakati mwingine anafanya marekebisho mbele yake anasema ruksa tumevutana na IMF sasa tukae mezani haikuwa rahisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mzee Mwinyi akatuambia kila zama na kitabu chake, tumekuwa na vitabu vitano sasa tunaandika kitabu cha sita wito wangu kwa viongozi Wabunge wenzangu wana CCM na watanzania tumsaidie mama kwa kumuunga mkono aandike kitabu cha awamu ya sita, tusigombane bila sababu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni yetu sote tumsaidie mama na yeye aandike kitabu chake tusimshike mikono kumwandikia kitabu tumuache aandike kitabu chake na ndugu zangu legacy haitetewi legacy inajitetea yenyewe na hasa ile inayofanywa na mtu kama Dkt. Magufuli legacy yake itajitetea itajisimamia kwa miaka unless mtu ana mashaka na legacy yake lakini kama hamna mashaka na legacy yake legacy yake itasikilizwa itasemwa itaombewa na sisi watoto wajukuu na vitukuu kwasababu haya aliyoyafanya watayakuta tu hatuna sababu ya kugombana hatuna sababu ya kutoana macho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa kiongozi kwenye chama nimesimamia Idara ya Maktaba na Nyaraka duniani kama kuna chama bora kime-document mambo mengi ya kutosha CCM ni karibia namba one kwa kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye document zetu tumesema kujikosoa na kukosoana ni silaha ya mapinduzi na kujiimarisha na siyo dalili ya udhaifu chama chetu kimeenda namna hiyo kwa miaka ya kutosha…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nape kengele ya pili imeshagonga ahsante sana nimeambiwa na katibu hapa

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja na naipongeza Serikali kwa uamuzi kwa uamuzi wa kuondoa TMX nendeni mkasimamie okoeni zao la korosho na ufuta hongereni kwa uamuzi huo ahsanteni sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi na kwa sababu ya muda naomba niende moja kwa moja na nina hoja moja tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chama cha Mapinduzi traditionally ni Chama cha Wakulima na Wafanyakazi, ndio base yetu; ndio social base ya chama hiki. Na Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni muhimu sana, sana, ikashughulika na wafanyakazi wa nchi hii kama mtaji muhimu wa Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nataka kuzungumzia jambo ambalo limezungumzwa na Wabunge kwa sehemu; lakini mimi nimeona nililete kwenye Wizara ya Utumishi. Jambo la haki na stahiki za walimu wa Tanzania. Nimeona nizungumzie hawa kwa sababu kwanza, ni karibia asilimia 70 ya watumishi wa umma wa nchi hii ni walimu, lakini ndio watu ambao tumewakabidhi watoto wetu na vijana wetu kwa kuwalea na kuwafundisha kulitengeneza Taifa letu tunakokwenda. Kwa hiyo, ni kundi muhimu kabisa muhimu sana, lakini bahati mbaya Wizara ya Utumishi na Hazina wamekuwa wakitoa nyaraka na taratibu ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa hazilitendei haki kundi hili kubwa katika watumishi wa umma wa nchi yetu. Nyaraka hizi na taratibu ambazo zimekuwa zikitumika kwa mfano kwa walimu zimezaa makundi yafuatayo:-

Moja, kuna kundi la walimu ambao walipewa barua za kupandishwa madaraja lakini stahiki zao hazikubadilika mpaka wakastaafu. Kwa hiyo mafao yao ya mwisho yameathirika sana na kundi hili lipo mtaani, kubwa! Wamepewa barua, stahiki zao hazikubadilika na hivyo mafao yao yameathirika kwasababu stahiki zao hazikubadilika.

Kundi la pili, walimu waliopandishwa madaraja kwa barua, lakini hakukuwa na mabadiliko kwenye stahiki zao kwa muda mrefu mpaka wamekutwa na barua zingine za kupandishwa madaraja wakati zile za awali hazikufanyiwa kazi. Kundi hili nalo lipo kubwa katika kada hii ya walimu.

Kundi la tatu, walimu ambao wamepandishwa madaraja au vyeo kwa makaratasi, lakini mpaka leo wamebaki na maandishi ya pesa kwenye makaratasi lakini stahiki zao hazijaguswa.

Kundi la nne na hapo nataka niguse mifano tu, walimu ambao walipandishwa madaraja kwa barua na hii nadhani ilikuwa mwaka 2013. Wakakaa nazo bila ya mabadiliko ya stahiki zao, baada ya muda ukaandikwa waraka ukafuta, kule kupandishwa kwao madaraja na bila sababu ya msingi na mimi nadhani ni baada ya kuona kuna mlimbikizo mkubwa Serikali ikataka kukwepa deni hili ikaandika waraka wa kufuta waraka wake ambao uliwapandisha hawa walimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, haya madaraja na stahiki zao sio hisani ni haki zao. Hivi inavyoendeshwa, inalifanya jambo hili ligeuke kuwa ni hisani kuwapandisha madaraja na kuwapa stahiki zao. Hili jambo si sawa, hatuwatendei haki walimu wa nchi hii. Ni matumaini yangu nimesikia Wizara wanasema kwamba wanapandisha madaraja watu ni karibu 900. Lakini kupandisha huku madaraja kusisahau hawa ambao tayari wameshaathirika kwa sababu ya mfumo mbovu ambao tumeutumia. Nyaraka tunazoziandika kutoka Utumishi, zisigeuke kichaka cha kupora haki za watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haki ndio itainua Taifa hili, hili kundi ni kubwa sana kulifumbia macho na kuja tu na hoja tu ya kupandisha madaraja peke yake hakutafidia haki ambazo zimepotea za haya makundi na haya ni machache inawezekana yapo mengi sana na jambo hili limezungumzwa hapa. Sasa mapendekezo yangu, naiomba Serikali ikiwezekana iunde Tume Maalum iende ikachunguze ili wale ambao tayari wamekwishaathiriwa na huu mfumo tuwarekebishie mambo yao hata kama tutawalipa taratibu lakini haki yao isipotee kila mmoja apate haki yake. (Makofi)

Mimi ni matumaini yangu wizara wamepewa vijana wadogo zangu; na nina hakika watafanyakazi vizuri, Mheshimiwa Mchengerwa na mwenzake nina aamini mtakwenda kutendea haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimemsikia Mheshimiwa Rais, akizungumza suala la haki, jambo hili ni haki ya wafanyakazi ukiacha maslahi yao ya kupandisha mishahara, lakini hata hiki ambacho ni haki yao, nataka kuiomba Serikali ya Chama cha Mapinduzi; chama cha wakulima na wafanyakazi, twendeni tukatende haki kwenye suala la stahiki za hawa wafanyakazi ambao tumewaacha, wananung’unika na msisahau Waheshimiwa Wabunge ndio hawa pia wamesimamia chaguzi zetu. Wamefanya kazi nzuri, wanafanya kazi nzuri ya kuwalea watoto wetu, hebu tusiache haki zao zikapotea.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi leo unaajiriwa, ukiajiriwa kwa teknolojia ya leo, likiingizwa jina lako kwenye kwenye mfumo kuna haja gani tena ya kuanza kuhangaika na taarifa kule chini! Tayari kishaingizwa kwenye mfumo tunajua baada ya muda fulani nitastaafu.

Leo kuna watu wanastaafu wanakaa kule mpaka wanakuwa wanywa gongo! Kwa nini? Kwa sababu hamuwapi haki zao za kuondokea kwenye vituo vyao vya kazi. Kila siku lete document hii, lete document hii, na nikushukuru, Mheshimiwa Naibu Spika asubuhi umelizungumza jambo hili, jambo hili lina umiza, tumeanza kutumia utaratibu wa kuhakiki, utaratibu wa kutaka nyaraka kama kichaka cha kupora haki za watu. Hizi haki zao zisimamiwe wazipate. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele imeshagongwa.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie kidogo kwenye Wizara hii ya Kilimo. Napongeza hotuba nzuri ya Mheshimiwa Waziri na nipongeze kazi nzuri inayofanywa na Wizara hii; Waziri na Naibu Waziri. Nadhani katika Wizara ambazo combination yake imekaa vizuri ni Wizara hii. Mawaziri wake ni wasikivu, lakini wana werevu mzuri, nami nina matumaini kwamba sekta ya kilimo itakwenda vizuri. Hongera sana Waziri na Naibu wako pamoja na Katibu Mkuu. Watu wapole na wasikivu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda, nataka nizungumze jambo mahususi kwenye korosho. Mwaka 2018 tulibadilisha sheria hapa ya tasnia ya korosho. Tulipofanya yale mabadiliko yalisababisha kufutwa kwa mfuko wa kuendeleza zao la korosho ambao ulikuwa unaitwa Mfuko wa Pembejeo, ambapo chanzo chake cha fedha ilikuwa ni tozo ya mauzo ya nje (Export Levy). Uamuzi ule ulipofanyika, wale waliokuwepo wanakumbuka, Serikali ilitoa ahadi hapa Bungeni kwamba inachukua zile fedha ambazo zilikuwa zikipatikana; na kwa sababu kile chanzo bado kipo, fedha zinapelekwa kwenye mfuko mkuu ili zikasimamiwe vizuri kwa hoja kwamba zilipokuwa kwenye huu mfuko zilikuwa hazisimamiwi vizuri.

Mheshimiwa Spika, makubaliano ilikuwa ni kwamba hizi fedha zikishaenda Mfuko Mkuu, zitarudi kuja kuendeleza zao la korosho kama ambavyo zilikuwa zikifanyika kwenye mfuko wa pembejeo. Kwa hiyo, kilichofanyika ilikuwa ni kubadili msimamizi. Sasa huu ni msimu wa tatu toka makubaliano hayo yafanyike na sheria hii ibadilishwe, bahati mbaya sana hii fedha haijarudi kwenye zao la korosho, haiendi kabisa. Hili ni la kwanza.

Mheshimiwa Spika, la pili, baada ya hii fedha kuchukuliwa, uzalishaji wa korosho ukashuka kutoka tani 320,000 ukaenda mpaka tani 200,000 na kitu, kwa maamuzi tu haya ya kuchukua huu mfuko. Baya kuliko yote, badala ya kurudisha hii fedha kwa wakulima, kilichofanyika, msimu uliofuata moja ya kazi iliyokuwa inafanywa na hii fedha ilikuwa ni kugharamia utafiti na kuendesha Bodi ya Korosho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ikaleta mapendekezo, ikaweka tozo kwa wakulima shilingi 25/= ya utafiti na shilingi 25/= ya kuendesha Bodi ya Korosho, badala ya kutumia ile fedha waliyoichukua, ile fedha haikurudi na ule mzigo akarudishiwa mkulima. Kwa hiyo, mkulima anakatwa shilingi 50/= kwa ajili ya utafiti na kwa ajili ya kuendesha Bodi ya Korosho. Huu ni udanganyifu. Tulipoahidiwa hapa Bungeni tuliambiwa hii fedha ingeenda, lakini sasa huu mzigo amebebeshwa mkulima.

Mheshimiwa Spika, baya zaidi, sasa hivi yako mapendekezo mengine ya kugharamia pembejeo kwa kumkata mkulima shilingi 110/= kwa kilo. Ahadi iliyotolewa hapa ni kwamba hii fedha ya Export Levy ndiyo ambayo ingerudi kuja kugharamia. Sasa kwa mahesabu ya kawaida, mwaka 2018 iliingizwa shilingi bilioni 37, wakati huo mfuko haukufanya kazi kwenda kugharamia pembejeo. Serikali ilipata mapato shilingi trilioni moja na zaidi, kwa kuingiza shilingi bilioni 37 tu. Mwaka huu makisio ya uzalishaji ni tani 280,000 mpaka 350,000, tunahitaji shilingi bilioni 55 tu. Sasa kwa nini tunataka kwenda kumbebesha huu mzigo mkulima badala ya kuchukua ile fedha ambayo mlituahidi hapa kwamba itakwenda kutumika vizuri? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi bilioni 55, tunazalisha zaidi ya trilioni moja plus! Ni maombi yangu kwa Serikali, naomba sana; na bahati nzuri Naibu Waziri wakati ule tuna mgogoro huo wa Export Levy hapa, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na alituunga mkono. Ni matumaini yangu kwamba kwenda kwake Serikalini hakujambadilisha kuliona hili jambo kwa mtazamo sahihi, tuchukue fedha ya Export Levy turudishe iende kugharamia korosho ili Serikali mpate.

Mheshimiwa Spika, kushuka kwa uzalishaji kumemuumiza mkulima kwa sababu uzalishaji umeshuka, lakini kumeiumiza Serikali. Sasa siyo vibaya kurekebisha. Ni ombi langu kwamba Serikali ifanye marekebisho badala ya kwenda kumkata mkulima, chukueni fedha, shilingi bilioni 55 kati ya shilingi bilioni 200 au shilingi bilioni 300, rejesheni huku tukomboe zao la korosho lisife. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mfuko huu ulipoondolewa na Bodi ya Korosho ilivunjwa, huu mwaka wa tatu. Zao ambalo ndiyo linaloongoza kwa kuiingizia fedha nyingi za kigeni nchi hii kuliko zao lolote, mwaka wa tatu hakuna bodi. Mkurugenzi wa Bodi, yuko anakaimu.

Mheshimiwa Spika, bahati mbaya mimi nadhani Mkurugenzi amepewa kazi kubwa kuliko uwezo wake. Hii kazi imemshinda, mtafutieni kazi nyingine, tuleteeni Mkurugenzi mwingine. Kwa sababu huyu Mkurugenzi anakwenda kule, anafika mahali akibanwa na wakulima anaanza kutoa majibu ya kiburi kabisa. Sasa zao ambalo ndiyo linawaingizieni fedha; mwaka wa tatu huu kuunda bodi tu inashindikana; tuna lengo gani na zao hili? Hili zao likifa tunapata nini? Tuundieni bodi, tutafutieni Mkurugenzi mwenye uwezo, tutengenezeeni mambo.

Mheshimiwa Spika, la tatu, mwaka ule wakati tunaanza kuhamasisha kulipeleka hili zao mikoani, wako wananchi waliohamasishwa kutengeneza miche ya korosho; na kati yao kwanza wengi hawajalipwa, lakini kati yao walikuwepo Watumishi wa Umma. Mkoa wa Lindi wako saba, nchi nzima wako 24. Wameingia mkataba na Bodi ya Korosho.

Mheshimiwa Spika, maajabu kabisa, wameshazalisha miche imechukuliwa imesambazwa, wanaambiwa wao hawakutakiwa kuzalisha. Kwa nini mliingia nao mkataba? Kwa nini mmechukua miche yao? Why don’t you pay them today? Uharamu unapatikana baada ya kuchukua miche na kusambaza. Eti ni Watumishi wa Umma! Kwani Mtumishi wa Umma akizalisha akapata hela ya ziada, dhambi iko wapi? Mimi nadhani hii ni roho mbaya tu ambayo haina sababu. Tengeni fedha, walipeni hawa watu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mapendekezo yangu, msimu huu ambao pengine muda wa kurekebisha sheria unaweza ukawa haujafikia na bahati nzuri Kamati imependekeza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

SPIKA: Malizia kwa sentensi moja.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, naipongeza Kamati kwa kupendekeza jambo hili, mfuko wa kuendeleza zao la korosho urudishwe. Kabla haujarudishwa, tupeni shilingi bilioni 55 mkalipie pembejeo, ile iliyobaki rekebisheni.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie kidogo kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Ardhi na nianze kwa kumpongeza Waziri na Naibu Waziri na timu yake nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya kwenye Wizara hii. Kama wenzangu waliotangulia wavyolisema, Wizara hii mwanzoni ilikuwa na kelele nyingi sana, lakini Mheshimiwa Lukuvi kwa uzoefu wake nadhani ameweza kuituliza, kelele zimepungua, hata kama bado yapo mambo machache lakini kwa kweli mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni, amefanya kazi nzuri sana. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Bunge la Kumi na Moja mimi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtama tulileta mapendekezo Serikalini ya kufuta shamba Na. 37ambalo lipo Maumbika Jimboni Mtama ambalo lilikuwa na hati Na. 5,438; shamba hili tuliliomba kwa muda mwanzoni, hati yake ikafutwa, baada ya muda ikabatilishwa ufuataji wake, sasa kwa niaba ya wananchi wa Mtama nimesimama kumshukuru.

Mheshimiwa Waziri Lukuvi kwa sababu baada ya mjadala naye Serikali imechukua uamuzi wa kulichukua hili shamba na kuwakabidhi Halmashauri ya Mtama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri na Serikali nawashukuru sana na usikivu wenu na wananchi wa Mtama wanashukuru kwa uamuzi huu wa kulirudisha shamba hili sasa lisimamiwe na Halmashauri mpya ya Mtama. Nikuhakikishe kwamba tumeanza utaratibu wa kupanga matumizi bora ya eneo hili na hivi karibuni tutakamilisha utaratibu wa mapendekezo yetu na tutayaleta Wizarani kwa ajili ya kuidhinishwa. Ni matumaini yangu kwamba kelele za watu wachache hazitawarudisha nyuma tena. Mmeshatukabidhi, msirudi nyuma. Mwanzoni mlirudi nyuma, ikatusumbua sana.

Mheshimiwa Niabu Spika, safari hii msirudi nyuma tena, tupo katika mchakato wa kupanga matumizi na tupo katika hatua ya mwisho kabisa. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba ulinde uamuzi wako ili tupate kupaendeleza mahali hapa kwa matumizi ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza pia Wizara hii kwa kuhamisha huduma zilizokuwa zinatolewa kwenye kanda kuzipeleka mkoani. Jambo hili limetupunguzia sana gharama wananchi, lakini naomba nitoe mapendekezo, kama mmeweza kutoka kwenye kanda kwenda mkoani, mnaweza pia kutoka mkoani kwenda wilayani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, umefika wakati baada ya kufanya kazi kwenye kanda na mkaona usumbufu ambao ulikuwepo na bila shaka mtaona tija iliyopatikana baada ya kuzitoa huduma za kwenye kanda kuzipeleka kwenye mkoa. Sasa Mheshimiwa Waziri nadhani twende zaidi, tuzitoe hata kama kwa kuanzia baadhi ya huduma na hasa huduma kama za upatikanaji wa hati hizi. Upatikanaji wa baadhi ya vitu tuutoe kwenye mkoa tuupeleke kwenye wilaya. Tutakuwa tumewasogelea sana watu na tutapunguza sana gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa kama wa Lindi bado ni mbali sana mtu kutoka Liwale kuja Lindi Mjini kuchukua huduma. Kwa hiyo, ni mapendekezo yangu kwamba kwa kuwa tumefanikiwa kupeleka kwenye Mkoa na umeona inafanya vizuri; na katika dunia hii ambayo Sayansi na Teknolojia imekua sana, tunaweza bado tuka-control kutoka mkoani lakini bado huduma fulani wasilazimike kusafiri kuzifuata mkoani, bali waende wakazichukue Wilayani. Hayo ni mapendekezo yangu, nami naamini kwa uzoefu wenu na uwezo wenu mnaweza mkalifanya hilo na tukasogeza huduma karibu na wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho nililotaka kulizungumzia ni suala la upimaji na upangaji wa miji yetu. Nimeona kwenye Kamati na nichukue nafasi hii kuipongeza iliyokuwa Kamati yangu ya zamani ya Ardhi wameliona hili jambo la utengaji wa fedha na kuzikopesha Halmashauri zetu zipime zenyewe. Jambo zuri lililofanyika hapa, mnawapa kwa zero interest, nadhani hili jambo ni zuri sana na bila shaka Serikali wameona, kwamba hii fedha wakipeleka, hata kwa hizi chache walizoanza nazo, wakifanikiwa kupima na kumilikisha, tayari ni mradi mzuri wa kuiingizia Serikali mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mapendekezo yangu; la kwanza, naiomba Serikali iongeze fedha, hizi Wilaya ni kidogo sana, ikiwezekana tu- roll hata nchi nzima kwa sababu itaongeza mapato kwa kiwango kikubwa sana. Kwa hiyo, eneo la kwanza fedha iongezwe. Eneo la pili Mheshimiwa Waziri nilikuwa napendekeza, kwa kuwa kasi ya ukuaji wa miji ni mkubwa, badala ya kwenda kwenye urasimishaji na bila shaka Waziri wa Fedha yupo na amenisikia, hili ni eneo zuri litatupatia fedha ya bure sana. Wape fedha ya kutosha waongeze Wilaya. Sasa pendekezo la pili miji inakua kwa kasi kuna mradi wa kurasimisha urasimishaji una matatizo yake kwa sababu unakuta watu wameshajipanga mnaanza kurasimisha inachukua muda na ni gharama.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ilikuwa kipaumbele cha hizi fedha pelekeni kwenye Halmashauri mpya ambazo miji yake ndiyo inaanza kukua na hapa naomba upendeleo mkubwa kwa Halmashauri yangu ya Mtama. Naomba tuletewe fedha, Halmashauri bado ni mpya, hatujatawanyika sana. Tukiletewa fedha, tutapima na kupanga vizuri bila gharama na tutajikuta tuna miji mizuri ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa namwomba Mheshimiwa Waziri jambo mahsusi, Mji wa Mtama wakati Mheshimiwa Hayati Dkt. Rais Magufuli anaamua kutupa Halmashauri, ule mji umepanuka. Bahati mbaya wakati wa kupanuka kuna mahali wakapanuka mji ukaenda ukachukua eneo la Tandahimba, nasi tukadhani ni eneo la Mtama. Wakati wa kupima sasa vipimo kuleta kutangaza GN ya Mji wa Mtama, tukakuta lile eneo ambalo wananchi wanapata huduma Mtama, tunajua ni wananchi wa Mtama miaka yote, tukajikuta wanawekwa nje. Karibia theluthi moja ya Mji wa Mtama ipo nje ya Mtama na ipo nje ya Mkoa wa Lindi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri ikiwezekana basi tuma watu wako waje waliangalie tatizo hili na kwa sababu limevuka suala la Jimbo, limevuka Wilaya, limeenda Mkoa, kwa hiyo, likotokea Wizarani itakuwa rahisi kulitatua. Watume watu wako waje waangalie, ikiwezekana tuone namna ya ku-accommodate. Kwa sababu wenzatu wa Tandahimba wala hawana shida, kwa sababu hili eneo wala hawakujua kama ni lao, isipokuwa GN ya miaka mingi inaonesha hili eneo lipo Tandahimba. Kwa hiyo, ombi langu Mheshimiwa Waziri tuma watu wako waje watusaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashukuru kwa kazi nzuri iliyofanywa, lakini nawapongeza kwa kusogeza huduma mkoani, sasa zipelekeni wilayani. Napongeza kwa kutenga fedha za upimaji na kuwakopesha Halmashauri na ninawaomba wale wanaokopeshwa wasimamie fedha zirudi ili na wengine tukope. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri nakuomba ukisimama, basi iingize Mtama nipate fedha kwa ajili ya kupima mji wangu mzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Naunga Mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nami nitumie dakika chake nichangie kwenye hotuba hii ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Kwa kipekee nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mwalimu wangu wa Sheria kwa kazi nzuri anayoifanya yeye na Naibu wake na pia watendaji kwenye Wizara hii, Katibu Mkuu na Taasisi wakiwemo Ngorongoro, TFS na wengine, hongereni kwa kazi nzuri. Wizara hii ilikuwa na kelele sana, lakini mmejitahidi kuituliza na nadhani mtasonga mbele vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii Mheshimiwa Waziri kukushukuru kwa kukubali Naibu Waziri aje kufanya ziara Jimboni kwangu na kutembelea maeneo yale ambayo yameathiriwa na wanyamapori hasa Kata ya Mnara na Chiponda. Naibu Waziri karibu sana Mtama, tunakupenda na tutakupokea kwa mikono miwili, utembelee maeneo haya na kuona jinsi tulivyoathiriwa na wanyamapori. Nami sina mashaka kwamba tutachukua hatua za kurekebisha maeneo haya na kupunguza athari zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza na kuishukuru Kamati kwenye hotuba yao wamegusia jambo ambalo ndilo nilitaka nilizungumze hapa; Jambo la sekta ndogo ya uwindaji wa kitalii. Kamati wamekiri kwamba sekta hii kidogo imetikisika, imeyumba. Takwimu huwa hazidanganyi. Ukiangalia namba zinaonesha wazi kwamba liko tatizo. Bahati nzuri jambo hili tulianza kulizungumza ndani ya Bunge hapa miaka kama minne au mitatu iliyopita tukaanza kutoa mashaka yetu kwamba jamani mnapokwenda mtapata matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tukizingalia takwimu, zinakubaliana na ripoti ya kamati kwamba sekta hii tusipochukua hatua itakwenda kufa na hapa nipitie takwimu chache. Mwaka 2013 sekta hii ilikuwa na wawindaji wa kitalii 1,550, leo ukichukua takwimu za 2018/2019 wameshuka mpaka wamefika 473. Kutoka 1,550 mpaka 473, hili ni anguko kubwa sana, tusipochukua hatua tunakwenda pabaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mapato ya Serikali, mwaka 2013 Serikali ilikuwa inapata mpaka dola milioni 27. Leo tumeshuka mpaka dola milioni nane. Hili ni anguko kubwa; 27 kwa 8. Mapato ya jumla ukikusanya tozo na vitu vingine tulikuwa tunakwenda mpaka dola milioni 100. Leo, milioni 25, maana yake tunaanguka. Mwaka 2013 tulikuwa na makampuni 60 yapo yanafanya kazi, leo yako chini ya 40. Maana yake tumeshuka kwa zaidi ya asilimia 50. Ukienda kwenye takwimu sasa za vitalu vyenyewe, vitalu ambavyo viko wazi sasa vinakaribia asilimia 50. Maana yake ni kwamba kuna anguko kubwa kwenye hii sekta na kama hatutachukua hatua za makusudi, Sekta hii itaanguka. Sekta hii kwenye Wizara ni eneo muhimu katika kufanya mchango wa Wizara kwenye uchumi wetu uendelee kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuiomba Serikali, ondokeni kwenye kuona kwamba mkishaamua jambo, hata kama linafanya vibaya mnatakiwa kuendelea nalo, nadhani siyo sawa sawa. Kila mara mnakuja, tunawaonesha takwimu, tunaonesha mwelekeo ulivyo, lakini kwa sababu Serikali mmeshaamua, mnaamua kuendelea hivyo hivyo, hata kama tunakwenda kuanguka. Mheshimiwa Waziri mkiendelea hivi, maana yake mnahujumu sekta hii; na mkihujumu sekta hii, mnahujumu uchumi wa nchi. Kama mapato yameanguka kwa kiasi hiki na bado hatuchukui hatua, liko tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumefikaje hapa? Kweli kuna mchango wa tatizo la Covid, lakini tulianza kuanguka kabla ya Covid na tukaanza kusema kwamba tunaanguka. Covid ilipokuja ikapiga msumari kwenye anguko. Sasa katika mazingira haya, mategemeo yangu ilikuwa ni kwamba tuchukue hatua, kwa sababu tukichukua hatua tutakwamua anguko hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vitalu hivi vinavyobaki wazi kila siku ya Mungu vinapoteza thamani yake. Wewe unajua katika vitalu vilivyobaki wazi leo karibu vitalu 14 havifai, maana yake tumepoteza rasilimali ya nchi. Kazi kubwa ya Wizara hii ni pamoja na kuhifadhi ndiyo kazi kubwa. Sasa kama uhifadhi unaharibika, tunachukua hatua tunakwenda kuharibu zaidi, mimi nadhani iko haja ya kuchukua hatua. Kwa hiyo, tumefikishwa hapa na nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maamuzi Serikali tuliyafanya ya kubadilisha mfumo wa ugawaji wa vitalu. Ni kwa nia njema na hata Kamati wamekiri; nia ile njema lengo ilikuwa ni kuongeza transparency, kupunguza rushwa, kuondoa maneno; nia njema, lakini Mheshimiwa Waziri ule mfumo mliouweka una upungufu ndiyo maana vitalu mnavipeleka mnadani vinakosa soko, vinabaki wazi, vinapoteza thamani. Kadri siku zinavyokwenda rasilimali hii inaharibika.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu; moja, nendeni mkapitie upya huo mfumo mliouanzisha. Kaupitieni upya mpunguze matatizo yaliyomo including kuongeza transparency. Hivyo mlivyoweka haitoshi, bado una upungufu mwingi ndiyo maana minada inafeli. Minada yote iliyofanyika, mnapeleka vitalu vingi, mnauza vichache, mnarudisha vingi. Hapa ni kuonesha kwamba kuna upungufu kwenye mfumo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ya pili, wale ambao wana vitalu tayari msiwapeleke kwenye mnada. Kwanza wamepitia wakati mgumu wa Covid, wamewekeza kwenye hivi vitalu, wameweka miundombinu na wanavilinda kwa sababu vile ambavyo havina watu mmeviacha, ulinzi hakuna, miundombinu hakuna, vinapotea, vinaharibika, tunapoteza mapato. Kwa hiyo, wale ambao wako kwenye vitalu, ombi langu ni kwamba waongezeeni muda wa kuendelea kupanga kwenye hivi vitalu. Rekebisheni mfumo mlioleta, vile vitalu tupu vipelekeni mnadani, endeleeni na utaratibu baada ya maboresho. Mkifanya hivi, naamini tutakuwa tume- save sekta hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo la tatu. Mmesema vizuri kwenye bajeti yenu kwamba mnakwenda kupitia sera, sheria, taratibu na kanuni mbalimbali malizojiwekea. Serikali ya Awamu ya Sita moja ya lengo kubwa ni kuvutia wawekezaji. Hebu nendeni mkazipitie upya tuendane na wakati na wakati huo tuangalie na mazingira mengine. Mheshimiwa Waziri, hili kundi kubwa ambalo tumelipoteza maana yake moja, limekwenda kwenye maeneo mengine. Kwenda kule, linaweza lisirudi. Sasa tusiporekebisha tutaendelea kuanguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ni matumaini yangu Serikali itachukua hatua tuiokoe Sekta ya Uwindaji hapa nchini. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipa nafasi, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa wasilisho nzuri la mapendekezo haya ya bajeti ya Serikali na kwa pongezi nilivyozisikia huu ni ushahidi kwamba Chama cha Mapinduzi kinalea vizuri sana. Maana Mheshimiwa Naibu Waziri alikua mwenyekiti wa vijana wa CCM kwa hiyo alilelewa vizuri, Mheshimiwa Waziri amekua Mweka hazina wa Chama cha Mapinduzi Taifa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi. kwa hiyo, ni ushahidi kwamba Chama chetu kinalea vizuri na matunda yake tunayaona, hongera sana Mheshimiwa Waziri na timu yako nzuri kwa kazi ambayo mmeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze Mheshimiwa Rais hii ni bajeti yake ya kwanza, Rais wa Awamu ya Sita na ni bajeti nzuri sana sana katika historia bajeti zetu hii ni bajeti nzuri na kama bajeti yake hii ya kwanza imefanyika hivi nadhani mama tukimpa bajeti kama 10 hivi nchi yetu itakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumuunge mkono kwa bajeti yake ya kwanza na bajeti zake tano za mwanzo halafu 2025 tumuongeze bajeti zingine tano ili mambo yetu yaende sawa sawa. Kwa tafsiri rahisi kabisa hii ni bajeti ya watu na Mheshimiwa Waziri umetutendea haki maana sisi hapa tumeletwa na watu umetuletea bajeti ya watu umehalalisha kurudi kwetu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya watu kwanini? Kwanza umegusa maeneo ambayo ni ya muhimu sana suala la barabara vijijini, suala la maji, suala la afya, suala la miundombinu ya elimu, haya ni maeneo makubwa yanagusa watu na kumekuwa na kelele ya muda mrefu ya kushughulika na maendeleo ya watu. Sasa umeya-identify jambo la kwanza, lakini la pili umependekeza vyanzo vya fedha ya kwenda kutatua mambo haya hili jambo ni kubwa sana na mimi naunga mkono mapendekezo ya Wabunge wengi kwamba hizi fedha tuziwekee wigo, tuzikusanye ndiyo lakini tuziwekee wigo zikafanye hii kazi uliyokusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na niwaombe Watanzania tuunge mkono na tulipe kodi ili tujivunie kujitawala ni kujitegemea na haya mapendekezo yanatupeleka kwenye kujitegemea badala ya matatizo haya kuendelea kutegemea fedha kutoka nje. Mheshimiwa Waziri na Serikali hii tunawaungeni mkono kwa mawazo haya mazuri na ninaomba Wabunge wote bila kujali tofauti zetu, mwisho wa siku tupige kura ya ndiyo ili tukajenge barabara tukapeleke afya tukapeleke elimu tukapeleke maji vijijini. Mheshimiwa Waziri hii kazi nzuri hii ni bajeti ya watu, mmetafsiri vizuri ukuwaji wa uchumi wetu kwenye maisha ya watu tunawaungeni mkono kwenye jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, nataka kupongeza uamuzi wa Serikali wa kuamua kuangalia upya finance ya miradi yetu mikubwa. Hili jambo ni kumbwa sana litasaidia kupunguza mzigo mkubwa kwa wananchi wa kawaida financing ya miradi yetu, tumeshaanza wenyewe vizuri hapa tulipo sasa tuangalie financing yake na kwenye hili Mheshimiwa Waziri tuweke nguvu tuhakikishe tunafanya credit rating ya nchi yetu itatusaidia sana kupunguza hali ambayo tunapambana nayo kwenye mikopo mbalimbali ambayo tumekua tukiomba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono credit rating ifanyike ni wakati sahihi tuko uchumi wa kati credit rating itatuweka mahali pazuri sana na tutapata fedha ya kuendeleza miradi hii. Kwa haraka sana nilitaka nizungumze eneo moja kubwa la hisa za Serikali kwenye makampuni, hisa za Serikali kwenye makampuni na hapa nazungumzia makampuni mawili TIPER na PUMA na bahati nzuri kuna fedha nyingi za kutosha huku, makampuni yote haya mawili Serikali ina hisa asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIPER tuna asilimia 50, na ORXY energy wana asilimia 50. Sasa nataka nizungumze namna ambavyo tunaweza tuka maximize hisa zetu zikatuletea vyanzo vingine vya mapato. Sasa hivi hapa TIPER tuna infrastructure ya matenki ya kuhifadhi mafuta. Sasa tusiruhusu wengine ndani ya Serikali humo humo wakatengeneza tena matenki mengine kuna hoja ya bandari kutaka kuingia huko hakuna sababu tutumie yale yale ya TIPER. Kuna hoja ya TPDS kwenda huku, kila mmoja atomize wajibu wake kazi hii ya kupokea haya mafuta na kuyahifadhi waachiwe watu wa TIPER.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hapa Mheshimiwa Waziri kuna jambo very specific, tokea TIPER imeanza MD wa TIPER amekuwa anatoka Ufaransa ambayo ni makubaliano na mimi nakubaliana. Lakini juzi imetokea fursa MD aliyopo anajiuzulu, wametangaza wameingia wazungu tatu, mhindi mmoja na Mtanzania mmoja, mtanzania kashinda kwenye mchakato baada ya kushinda kwa mujibu wa taratibu, wenzetu wanatakiwa kutuandikia Serikali tutoe consent yetu, consent tu tumekaa nalo, tunaangaika nalo na ni kwa roho mbaya tu, kashinda mtanzania, mtanzania akienda kwa faida ya nchi yetu anakwenda kuziangalia hisa zetu lakini tumeng’ang’ana nalo weee! Hivi angeshinda Mfaransa mngefanya vetting? Si mngetoa barua tu akaendelea ameshinda mtanzania roho mbaya mnambania ya nini na mkichelewa kujibu wataweka Mfaransa Watanzania hebu viongozi tuondoke kwenye roho mbaya, Mtanzania mwenzetu tumuunge mkono toweni consent ya Serikali aendelee, wamekaa wazungu wamemkubali sisi tunaweka roho mbaya hili jambo halikubaliki hii ni kwa TIPER. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa PUMA tuna hisa asilimia 50, Mheshimiwa Waziri tunaagiza mafuta hapa ya bulk kupitia PPPA lakini tunatangaza tender, wanaotuletea mafuta ni makampuni ya nje, hapa tuna kampuni yetu ya PUMA asilimia 50 ni Serikali yetu. Hivi ni kwanini tusiwatumie hawa hawa tukaagiza mafuta tukapata fedha lakini pia tukapata income tax kwa sababu hii kampuni iko hapa na sisi wenyewe Serikali tunapata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya sasa hivi tumewaachia makampuni ya nje ndiyo yanayoleta yakituletea tukishawalipa wanaondoka zao lakini na hakuna mtu hatatushangaa kampuni ya PUMA ni ya kwetu tuna hisa asilimia 50 lakini ina uwezo wa kufanya manunuzi ya kimataifa tuondoke kwenye kuangaika na hao twendeni tukaitumie kampuni yetu ya ndani tutapata fedha za ziada, tutapata mapato na mambo yetu yatakwenda vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, moja ninaunga mkono bajeti hii asilimia 100, bajeti safi twendeni tukaitekeleze na tumpe nafasi mama na waziri umefanya vizuri na naamini umeanza vizuri na baada ya muda uta-gain uzoefu wa kutosha utatupeleka mbele zaidi. Lakini kwenye financing ya miradi mikubwa twende kwenye credit rating itatutoa hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu twendeni tukaangalie matumizi ya hisa zetu kwenye makampuni yetu, na hizi hisa zetu zitatuongezea wigo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza kuongeza wigo wa kodi siyo idadi tu ni pamoja na ubora ukiwaongezea uwezo wale ambao wanakulipa kodi alikuwa anakulipa Shilingi 10 ukimuongezea uwezo anakulipa mia 200, unakuwa umeongeza wigo na hapa ndipo ambapo tunaiomba Serikali yetu ienda, lakini vinginevyo mimi naunga mkono ninampongeza Rais, kwa bajeti hii amelegeza vyuma sana tumuunge mkono aendelee kulegeza ili mambo yetu yaende, style aliyokuja nayo twende nayo tusonge mbele pamoja ninaunga mkono bajeti kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kidogo kwenye haya mapendekezo. Nianze kwa kuipongeza sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kwa kazi nzuri waliyoifanya, kwa kweli wamefanya kazi nzuri na mimi ni matumaini yangu kwamba Serikali watazingatia ushauri waliopewa na Kamati hii ya Bunge wamefanya kazi nzuri sana, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kushauri maeneo mawili makubwa, eneo la kwanza ni eneo la Deni la Taifa. Kwa taarifa zilizopo ukiangalia taarifa za Benki Kuu, hotuba ya Waziri na hata Kamati Kudumu ya Bunge ya Bajeti inaonekana Deni la Taifa limefikia trilioni 64, pamoja na kwamba taarifa zote zinasema kwamba deni hili bado ni himilivu lakini…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kidogo tu.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Halima.

T A A R I F A

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, sikuwa na nia ya kumuingilia Mheshimiwa Mbunge, lakini ninataka nirekebishe kidogo Deni la Taifa kwa mujibu wa taarifa ya BOT iliyotolewa mwezi Septemba ni Trilioni 78, Deni la Serikali ndiyo Shilingi Trilioni 64 na tukiongeza na Trilioni 1.3 tuliyochukua mwezi Septemba maana yake Deni la Serikali sasa hivi ni Trilioni 65.7 huko. Kwa hiyo, Mheshimiwa naomba uendelee na mchango wako mzuri. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Nape endelea na mchango.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaipokea, amefanya ufafanuzi ambao pengine nilidhani sikuwa na haja ya kwenda huko, lakini hoja yangu ni nini, kasi ya ukuaji wa deni hili pamoja na kwamba tunaambiwa deni bado ni himilivu kasi yake siyo kasi nzuri, kwa sababu linatupeleka mbele ya safari siku tutakapoanza kusema siyo himilivu utakuwa ni mzigo mkubwa usiobebeka na itakuwa ni shida kwa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipitie takwimu kidogo na hapa kwa kuwa Serikali inakopa kwa niaba ya wananchi na maana yake ni kwamba watakaokuja kulipa ni wananchi na Bunge tupo kwa niaba ya hao watakaokuja kulipa, nadhani ni vizuri tukafumbua macho tuangalie hii kasi inakotupeleka halafu tuwe wakweli tuambiane ukweli tuchukue hatua mapema kabla ya mambo hayajaharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtakumbuka Awamu ya Tatu tulihangaika na hili suala la Deni la Taifa na Awamu ile walichukua hatua ya kuzungumza mpaka tukafikia mahali pa kusamehewa baadhi ya madeni. Wakati ule awamu ile kwa miaka kumi zilikopwa dola Bilioni Tisa. Awamu ya Nne zikakopwa Dola Bilioni Saba kwa miaka 10, Awamu ya Tano kwa miaka Mitano mpaka Sita zimekopwa Dola Bilioni Tisa kwa miaka mitano mpaka sita. Bahati mbaya mkopo huu ambao nautathmini wa miaka mitano, sita asilimia 40 ni mikopo ya kibiashara ambayo moja ya sifa yake ina riba kubwa, lakini inalipwa kwa muda mfupi, kwamba inaiva mapema mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii imepelekea hali ilivyo kwa sasa kama hizi takwimu ni za kweli, katika mapato yetu kwa mwezi tunatumia zaidi ya bilioni 800 kulipa deni ambayo ni asilimia 44 ya makusanyo kwa mwezi. Sasa kama kasi itaendelea hivi maana yake ni kwamba kuna uwezekano mkubwa asilimia ya makusanyo kwa mwezi yakawa yanatumika ku-service madeni na matokeo yake yakaathiri shughuli zingine za utoaji huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili pamoja na kwamba inawezekana namba zilizowekwa kufikia kutostahimilika bado zinaturuhusu, lakini siyo vizuri kupuuza kwamba fedha tunazotumia kulipa madeni kwa mwezi ni hela nyingi ambazo zinaathiri shughuli zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninayo mapendekezo yafuatayo: Pendekezo la kwanza ni kwamba Awamu ya Sita wameanza vizuri sana kwa kuweka uwazi wa pesa walizokopa zinakwenda kufanya nini kwenye shughuli zetu na mfano mzuri ni hii 1.3 trilioni imewekwa mezani kila mmoja anajua mpaka muuza mchina anajua imekwenda wapi. Sasa pendekezo langu kwanza utaratibu huu uendelee, upongezwe, uigwe uendelee tuweke wazi yale tunayoyakopa tunapeleka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hizi za nyuma ambazo zimekopwa na hakuna uwazi mkubwa sasa tuende kufanya ukaguzi kwenye account ya Deni la Taifa tujue kilikopwa nini, kimeenda wapi, thamani yake nini, uhalisi wa miradi inayotekelezwa na thamani tuliyoambiwa iwekwe mezani ili tuige mfano mzuri uliofanywa na Rais Samia. 1.3 Trilioni imewekwa mezani kila mtu anajua, hizi zingine za kibiashara tuende tukague na sisi ndiyo walipaji kwa sababu sisi ni wawakilishi wa wale waliotutuma hapa, hili la kwanza la Deni la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kilimo. Tunasema huu mpango unatupeleka kwenda kujenga uchumi wa ushindani na shirikishi. Sasa nilitegemea kama kweli tunasema shirikishi nguvu kubwa ingepelekwa kwenye sekta ambayo inakusanya watu wengi haya maneno yangekuwa na uhalisia, hali ilivyo haya maneno hayana uhalisia na mimi ni maombi yangu kwa Serikali mtakapoleta mpango na Bunge hili wengi wameletwa humu na wakulima tukipitisha mpango ambao hauna nguvu kubwa kwenye kilimo tutakuwa tunawasaliti waliotuleta hapa na hili jambo siyo sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kinachangia asilimia 26 ya GDP yetu, lakini zaidi ya asilimia 70 au 80 ya Watanzania wameajiriwa kwenye Kilimo. Asilimia 100 chakula nchi, tunategemea kilimo; viwanda na maeneo mengine yote yanategemea kilimo. Sasa kama hali ni hii; ukiangalia miradi yote ya kielelezo, nitajieni mradi mmoja wa kielelezo ambao unashughulika moja kwa moja na kilimo, hakuna. Sasa kama hatushughuliki na kilimo, tunashughulika na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2013/2014 mlishafikia mahali tulikuwa tunatenga mpaka shilingi bilioni 200 kupeleka kwenye kilimo kama fedha za maendeleo. Leo bajeti hii tunayomaliza, tumetenga shilingi bilioni 80. Sasa badala ya kwenda juu, tunarudi chini, hii siyo sawa. Sasa mapendekezo; najua muda wangu unakimbia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba Serikali ilete mpango na bajeti inayojiungamanisha na walio wengi kwenye sekta yao. Tuanzie mahali rahisi sana; Ilani ya Uchaguzi inasema tunatakiwa mpaka 2025 tuwe na hekta 1,200,000 za umwagiliaji. Tuna 600,000. Mimi nilitegemea kwenye Mpango walau hata hekta 150,000 au 200,000 ingeonekana kama ndiyo mradi wa kielelezo wa kugusa walio wengi. Sasa ninyi hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi siipingi miradi hiyo, lakini ni kweli inagusa walio wengi masikini katika nchi hii? Hapana. Inawezekana inasaidia kwa pembeni, lakini hebu tubadilishe mwelekeo. Mwalimu Nyerere alituambia maendeleo ni ya watu, hata kama tutabishana. Kwa hiyo, pendekezo langu la kwanza, mtakapoleta Mpango, njooni na namna ya kupata fedha za kuweka walau hekta 200,000 au 150,000 ili tuanze hatua ya kufikia hiyo 1,200,000. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, tumezungumza sana hapa suala la kuwa na mfuko wa kusaidia, au mfuko wa ruzuku kwenye mazao. Dunia ikitikisika sisi wote tunayumba, kwa nini? Hatuna fedha ya kusaidia ruzuku kwenye mazao. Nilitegemea Mpango huu ungekuja na suala la Mfuko wa Ruzuku kwa mazoa yetu kama moja ya miradi elekezi ili tutoke hapa tulipo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye muswada huu muhimu ambao umewasilishwa. Nianze kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza maandalizi mazuri ya muswada huu, ni katika miswada mizuri, umechukua muda mrefu, lakini umeandaliwa vizuri na kwa hakika umejumuisha mawazo na michango na maoni ya wadau wengi, ndiyo maana ni katika miswada bora kabisa. Nachukua nafasi hii kuipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, nadhani amefanya vizuri sana kwa sababu Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe licha ya kuwa ni mwanasheria lakini ni mwanahabari, kwa hiyo, ameutendea haki muswada huu. Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe, nakupongeza na kukushukuru sana kwa kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu ukipewa tafsiri finyu unaleta matatizo katika mjadala. Wachangiaji wengi wamekuwa wakizungumza na pengine labda kwa bahati mbaya wanauchanganya Muswada huu wa Haki ya Kupata Taarifa na Muswada wa Huduma ya Vyombo vya Habari ambao kwa kweli ni miswada miwili tofauti.
Muswada huu wa Haki ya Kupata Taarifa uko chini ya Wizara ya Katiba na Sheria na upo Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari ambao uko chini ya Wizara ya Habari ambao utakuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wengi wamekuwa wakichangia kama vile huu ndiyo Muswada wa Huduma za Vyombo vya Habari, ndiyo maana michango mingi imekwenda huko. Sasa ama ni kwa bahati mbaya au kwa makusudi au kwa kutosoma vizuri na kuelewa ndiyo maana michango imekwenda hivyo ilivyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, muswada huu una mambo ambayo hayagusi moja kwa moja tasnia ya habari na haya ni ya muhimu sana na ndiyo maana tukiupa tafsiri inayofaa michango yetu itakwenda vizuri. Muswada huu moja ya eneo ambalo utaisaidia sana nchi yetu, muswada huu unatupeleka kwenye kuongeza uwajibikaji na hasa wa taasisi za umma na watumishi wake. Moja ya eneo la uwajibikaji ni kuhakikisha taarifa zinapatikana. Siyo kila taarifa inayozungumzwa na muswada huu inakwenda kutumiwa na vyombo vya habari, hapana. Muswada huu unazungumza haki ya mwananchi wa kawaida kupewa taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mwananchi ana haki ya kupata taarifa juu ya miradi ya maendeleo ya eneo lake. Kiongozi katika eneo, Mtendaji wa Kijiji, Diwani, Mbunge, muswada huu unamfanya Afisa wa Umma ambaye anatumikia umma awe na wajibu wa kutoa taarifa za miradi ya maendeleo ya eneo lake ambalo kwa kufanya hivi, itaongeza uwajibikaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukijikita na kudhani taarifa hizi zinazozungumzwa hapa ni taarifa ambazo zimelenga vyombo vya habari peke yake, nadhani tunataka kuupotosha Umma na siyo sawa sawa. Sasa anayeupinga Muswada huu, maana yake anapinga uwajibikaji. Tafsiri rahisi kabisa! Wakati huo tunapiga kelele ya uwajibikaji, tunatunga sheria itakayotusaidia kuwajibika zaidi, watu wanasimama wanapinga sheria hiyo isitungwe, maana yake wanapinga uwajibikaji kuongezeka katika nchi yetu. Na mimi nadhani ni vizuri tukaliweka sawa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inakuwenda kuondoa urasimu. Moja ya tatizo kubwa ambalo limekuwa likizungumzwa kwa muda mrefu, ni urasimu wa upatikanaji wa taarifa mbalimbali zinazowahusu wananchi, za maendeleo yao; za namna Ofisi za Umma zinavyofanya kazi. Kwa muda mrefu imekuwa ni kama hiari hivi. Ukienda kwenye Ofisi ya Umma unaweza kupewa taarifa au kutopewa, bila kujali ni mwandishi wa habari au sio mwandishi wa habari. Mwananchi wa kawaida anakwenda mahali anauliza, hivi mradi huu gharama yake ni kiasi gani? Usipokuwa na sheria ya namna hii, yule mwenye ile habari ana uhuru wa kutoa au kutokutoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii inakotupeleka ni kwenye kumfanya huyu afisa awe na wajibu wa kuhakikisha anampa taarifa huyu mwananchi wa kawaida. Kwa hiyo, tukiangalia tukaipa tafsiri ya kwamba tumelenga vyombo vya habari peke yake, nadhani tunakwenda kwenye ufinyu sana wa kutafsiri muswada huu, ambapo siyo jambo sawa na hatuutendei haki muswada huu. Nategemea Bunge hili liutendee haki muswada huu, unakwenda kujenga jambo la maana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ni nyenzo muhimu ya maendeleo; iwe ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, ndiyo maana muswada huu kwa kweli lengo lake ni kutupeleka huko. Sasa hivi hali ilivyo kabla ya hii sheria kupita, utoaji wa taarifa unategemea busara, unategemea utayari wa mtoaji na unategemea uelewa wa mtoaji na hili limekuwa tatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali inaleta Bungeni Muswada tuupitishe ili tusitegemee busara tena, tusitegemee utashi na utayari wa mtu kutoa taarifa. Mtu anayesimama kuupinga maana yake anataka turudi kule ambako watu wote tumekuwa tukilalamikia. Kwa hiyo, nadhani la kwanza ni vizuri tukaupa muswada huu tafsiri pana inayostahili Muswada huu, vinginevyo tutakuwa hatuutendei haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili; wale ambao sasa wamekuwa wakiupotisha muswada, wakidhani unagusa tu tasnia ya habari, huu muswada, mimi ni Waziri wa Habari na nimeupitia vizuri huu muswada na tumezungumza na wadau wa habari. Nilikwenda Mwanza nikakutana na wanahabari nikawaambia, nipeni maeneo mnayodhani yanakwaza tasnia ya habari katika huu muswada, wakayaorodhesha, tukazungumza na Waziri na ninataka nimpongeze Mheshimiwa Waziri, ameyazingatia maeneo karibu yote ambayo kwa kweli kwa namna moja ama nyingine yangekwaza tasnia ya habari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini muswada huu utasaidia sana kukuza tasnia ya habari kwa sababu mtoa taarifa mkubwa katika nchi yetu ni Serikali na vyombo vyake. Sasa sheria hii inakwenda kuilazimisha Serikali, inakwenda kuvilazimisha vyombo vya umma viwe na lazima ya kutoa taarifa kuwapa wanahabari. Sasa kuna jambo gani kubwa tunaweza tukaitendea haki tasnia ya habari kama kuitengenezea ulazima wa wao kupewa taarifa? Sasa tukileta hapa, watu wanasema hii hapana, hii hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani liko tatizo la kiwango kikubwa sana cha kutoaminiana ambacho ndiyo kinatufikisha hapa, watu wanabaki wanatoa mapovu, bila kuangalia jambo hili linakwenda wapi, hii ni shida. Ukiwa na watu ambao wanadhani muda wote ni lazima kufanya harakati, hata wakati ambapo mnataka kuzungumza mambo ya manufaa kwa nchi yenu wenzenu wanadhani mnafanya harakati. Hii ndiyo shida ambayo inatokea.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa watu wamezungumza, wanasema, aah, unajua siku hizi vyombo vya habari vinafungiwa hovyo na sasa wanatafsiri kwamba kama vile huu muswada unakwenda kumwongezea nguvu Waziri mhusika na wanasema Nape, kama vile Nape atadumu milele hapa. Nape yupo leo, kesho hayupo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme…
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa Mwaka 2016
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Muswada ulioko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mifumo inayoendeshwa kidemokrasia kama wa kwetu, baada ya uchaguzi, kazi ya Serikali iliyoko madarakani ni kutekeleza agenda waliochaguliwa na wananchi kuingia nayo madarakani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya ajenda kubwa ya Serikali ya Awamu ya Tano, ni kurudisha nidhamu ya utumishi wa umma katika nchi yetu. Hili tuliliahidi na ndio ilikuwa moja ya sifa ambayo Watanzania walituamini nayo, wakatupa kura nyingi tukachaguliwa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika kutekeleza ajenda mambo mawili ni ya muhimu sana. La kwanza, ni kuangalia sheria mlizonazo ni jinsi gani zinawasaidia kutekeleza ajenda ambayo mmepewa dhamana ya kuitekeleza.
Ndiyo maana Miswada ya namna hii inakuja ili isaidie katika kutekeleza agenda hiyo.
La pili, ni watu mnaowaweka kwenye maeneo mbalimbali ambao kwanza wanaamini agenda mliyonayo, lakini mbili wana uwezo wa kuitekeleza hiyo ajenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Kambi ya Upinzani moja ya kazi yao ya msingi ambayo nadhani wanaifanya vizuri, ni ya kujaribu kuzuia msifanye hayo mabadiliko yatakayowasaidia kutekeleza ajenda ili waje watumie mwanya huo kuwahukumu kwa wananchi wakati wa uchaguzi unapokuja. Pili, watahakikisha kila uteuzi mnaofanya ambao utawapeleka kwenye kutekeleza ajenda yenu wanaukosoa na kuupigia kelele vya kutosha ili msifanikiwe kutekeleza ajenda yenu. Kwa hiyo, walilolifanya si jambo la ajabu, ni jambo la kawaida na wanatimiza wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumzwa hapa uteuzi ambao umekuwa ukifanywa na Mheshimiwa Rais. Kaka yangu Mheshimiwa Tundu Lissu anajua kwa sababu ni mwanasheria, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 36, naomba niinukuu inasema hivi:-
“Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Katiba hii na ya Sheria nyingine yoyote, Rais atakuwa na mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais ana mamlaka ya kufanya uteuzi kwenye maeneo yoyote kwa mujibu wa Katiba hii. Kwa hiyo, uteuzi alioufanya hakuvunja Katiba hata kidogo, ameteua Wakurugenzi, ameteua Wakuu wa Wilaya hakuvunja Katiba lakini pia amezingatia principle ya kuteua watu ambao watakwenda kutekeleza ajenda ambayo ndiyo imemweka madarakani kwa sababu mwisho wa siku ndiye atakayekuja kuulizwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine kaka yangu Mheshimiwa Lissu anajua, amejaribu ku-twist maneno hapa kwamba Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Simbachawene lakini anajua huyu anaitwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, mwenye Wizara yake ni Rais. Kosa la Rais hapa ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwenye Wizara hiyo ni Rais, ndiyo maana ofisini kwake kuna Wizara mbili, haitwi Waziri tu, anaitwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, UTUMISHI na maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasema maneno haya tuyapuuze kwa sababu lengo lake ni kutaka kutotupeleka kwenye kutekeleza ajenda tuliyonayo na ni ajenda ya muhimu, tuna miaka mitano ya kutekeleza. Kazi ya kwanza tutengeneze na kurekebisha sheria zetu. Kazi ya pili, tuweke watu wenye imani na ajenda tuliyonayo na hao ndiyo watatupeleka huko tunakokwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nisisitize upotoshaji wa namna hii ni wa kuupuuza na sisi tusonge mbele. Rais amefanya sawasawa na aliowateua hakuvunja sheria, hakuvuja Katiba, wala hakupotoka popote…
Amefanya sawasawa kwa sababu tunataka kutekeleza ajenda na tuna sababu ya kusonga mbele katika hili. Wangesifia ingebidi tukae kujiuliza lakini kwa kuwa wamekosoa na kupiga kelele, uamuzi huu ni sahihi na tusonge mbele.
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba nichukue fursa hii kukushukuru tena kwa kunipa nafasi ya kufanya majumuisho ya mjadala kuhusu Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022. Jumla ya Wabunge saba wamechangia Muswada huu na naomba kwa heshima kuwatambua, Mheshimiwa Zahor Mohammed Haji, Mheshimiwa Miraji Mtaturu, Mheshimiwa Stella Fiyao, Mheshimiwa Engineer Mwanaisha Ulenge, Mheshimiwa Ally Mlaghila Jumbe, Mheshimiwa Innocent Bilakwate na Mheshimiwa Ahmed Yahya Abdulwakil.

Mheshimiwa Spika, natambua hoja nyingi zilizotolewa ni za ushauri ambazo niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tutazizingatia kwenye utengenezaji wa kanuni, lakini kwenye utelelezaji wa sheria ambayo tunaipendekeza kupitishwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitambue kazi nzuri iliyofanywa na Kamati ya Kudumu ya Miundombinu. Katika taarifa yao kwetu ambayo tumeipitia tumezingatia ushauri wao na niwahakikishie Mwenyekiti na Kamati yako kwa niaba ya Bunge wamefanya kazi nzuri sana ambayo imerahisisha kazi yetu kuendelea huko mbele.

Mheshimiwa Spika, pengine niguse hoja tatu kwa kifupi sana ambazo ni muhimu kuzitolea ufafanuzi. Hoja ya kwanza, aliitoa Engineer Ulenge, hoja ya haki ya marehemu, mtu ambaye hayupo tena duniani. Nataka niwahakikishie ukiangalia kifungu cha 30(4) kimetaja sio tu haki ya marehemu, lakini pia haki ya mtoto, haki ya mtu asiye na akili timamu, au mtu mwingine yeyote asiye na uwezo wa kutoa ridhaa, kwa sababu katika kulinda haki hizi tumetaka itolewe ridhaa. Kwa hiyo, inapotokea mtu ni marehemu au ni mtoto au hana akili timamu au hana uwezo wa kutoa ridhaa, sheria imependekeza na imetaja mzazi, mlezi, mrithi au wakili wake na kadhalika ambao wanaweza kufanya kwa niaba yake . Kwa hiyo jambo hili limezingatiwa.

Mheshimiwa Spika, ilikuwepo hoja ya suala la vyanzo vya mapato ambalo tumelijadili kwenye Kamati lakini na Wabunge wameligusia hapa. Kwanza inathibitisha utayari wa Bunge kutaka sheria hii itekelezwe na ndio maana wamekuwa concerned na vyanzo vya mapato. Jambo hili nalipongeza sana na limetufariji sana. Nilithibitishie Bunge lako katika ibara ya 51A-E, tumeorodhesha vyanzo vya mapato na mojawapo ni bajeti ya Serikali kupitia Wizara yetu ambayo itakuja hapa Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo niwahakikishie kwamba tuna hakika tume na vyombo vyake vitakwenda sawasawa kwa sababu bajeti itapita hapa, lakini tumeorodhesha vyanzo vile.

Mheshimiwa Spika, tumeweka pia uwezekano wa kuongeza vyanzo kwenye kanuni kwa maana ya kwamba mazingira wakati mwingine huwa yanabadilika. Kwenye sekta yetu ya TEHAMA fursa huwa zinaweza kutokea katikati kwa hiyo badala ya kujifunga vyote kwenye sheria tumeweka room ya kuwa na vyanzo vingine kwenye kanuni.

Mheshimiwa Spika, hapa pengine nigusie hoja ya utungaji wa kanuni. Kwanza nilithibitishie Bunge lako kwamba, Kanuni zitakazotungwa zitazingatia Sheria iliyotungwa kwa sababu haiwezekani kutunga kanuni ambayo haitaheshimu sheria ambayo Wabunge wameipitisha hapa Bungeni.

Mheshimiwa Spika, la pili, kanuni hizi tutawahusisha wadau ili kuhakikisha zinazingatia yale matakwa na hali halisi ya Sheria ambayo mmeitunga hapa. Wadau hao ni wengi na wanaweza wakawa hata mpaka Wabunge wenyewe. Hata hivyo, tunajua kupitia Kamati ya Sheria Ndogo za Bunge, kuna uwezekano wa kanuni hizi kupitiwa pia. Kwa hiyo ni uhakika kanuni hizi zitakuwa salama. Niwahakikishie kwamba tutatunga kanuni nzuri, zitazingatia Sheria lakini pia tutahakikisha tunawashirikisha wadau na kuhakikisha tumezingatia mazingira yote na kanuni hizi zitakuwa nzuri.

Mheshimiwa Spika, tumepokea pongezi nyingi kwa niaba ya Serikali na kwa kweli kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, sheria hii imeanza kuchakatwa miaka kama tisa iliyopita na haikuwezekana, lakini kwa usimamizi mzuri wa Rais Samia na Serikali ya Awamu ya Sita, imewezekana na leo tumeandika rekodi nzuri ya kuingiza nchi yetu kwenye nchi zinazo heshimu na kuzingatia ulinzi wa taarifa binafsi. Kwa kweli, niwashukuru Wabunge kwa uamuzi huu wa busara sana na uzalendo mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Sheria hii ukiacha mambo mengine ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya 2025, ibara ya 61B inayosema hivi:

“CCM itasimamia Serikali yake kuongeza faragha na usiri wa taarifa za wananchi katika mawasiliano kwa kukamilisha kutunga Sheria ya kuimarisha ulinzi wa taarifa na takwimu”.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi tulichokifanya hapa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, nawashukuru kwa kuunga mkono. Vile vile tulichofanya hapa ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 ambayo nayo inasisitiza ulinzi wa taarifa binafsi.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa na nawashukuru sana, mwelekeo wa duniani leo, mataifa makubwa na uwekezaji mkubwa hawaendi kuwekeza kwenye nchi ambayo haina sheria au mfumo unaolinda taarifa binafsi. Ukienda Ulaya wamekubaliana, kwa hiyo tumeathirika na kuna baadhi ya wawekezaji walishindwa kuja kwa sababu ya kutokuwepo kwa sheria hii. Kuna baadhi ya mikataba na makubaliano tuliyoingia duniani. Mnakubaliana ila wakitaka kuja wanauliza mna sheria ya kulinda taarifa binafsi kama hawana wanakwenda. Tumezidiwa na baadhi ya majirani zetu kwa sababu wenyewe walitangulia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo leo Bunge lako limefanya uamuzi wa kizalendo wa kuifanya nchi yetu sasa iwavutie wawekezaji hao ambao kwenye nchi zao wana sheria hii. Bila shaka sheria hii itakaposainiwa, tutaona mafuriko ya wawekezaji wakija na hasa kwenye sekta ya TEHAMA ambayo itazalisha ajira nyingi sana. Nchi zinazotuzunguka za SADC na Afrika Mashariki, uwekezaji bila kuwa na sheria hii, unakuwa mgumu. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumezingatia mawazo yao, ushauri wao na tutakwenda kuutekeleza kwenye kanuni na utekelezaji wa sheria hii.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.