Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel (43 total)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza naomba niulize, je, Wizara hawaoni kwamba sababu mojawapo inayoweza kusababisha malalamiko au kutotekelezeka kwa sera hii ni ile hali ya kuzi-upgrade hii vituo vyetu vya afya na zahanati zetu? Kwa mfano katika Manispaa ya Iringa, hospitali yetu ya Frelimo ilipandishwa hadhi kuwa hospitali ya Manispaa tangu mwaka 2013 lakini mpaka sasa inapokea mgao kama kituo cha afya. Katika hospitali ile tuna takribani akina mama 300 mpaka 350 wanaojifungua pale kila mwezi. Unaweza ukaona hiyo inachangia kwa sababu mahitaji ya watu wanaokuja pale yanakuwa makubwa kuliko mgao wanaoupata.

SPIKA: Yaani Mheshimiwa Hospitali ya Frelimo pale kila siku kumi wanajifungua?

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Ndiyo.

SPIKA: Endelea na swali lako Mheshimiwa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, kwa sababu hospitali yetu ya Frelimo, kwanza tulikuwa na Hospitali ya Wilaya imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya rufaa, kwa hiyo, wilaya tumepewa ile iliyokuwa kituo cha afya Frelimo kuwa hospitali ya wilaya. Kwa hiyo, ile hospitali yetu iliyokuwa ya wilaya imekuwa hospitali ya rufaa, hivyo, wagonjwa wengi sana wamekuwa wakienda pale na kwa kuwa bado tunapata mgao kama kituo cha afya imesababisha sasa wagonjwa wengi kuwepo pale na akina mama wengi wanaojifungua kukosa ile huduma bure. Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka, tangu 2013 jamani kwamba na sisi Iringa tupewe mgao kama hospitali ya Wilaya?

SPIKA: Ahsante sana, swali la pili fupi.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Spika, swali la pili, niombe tena Serikali ione, je, hii migao inayokuwa inakinzana yaani unaipandisha hospitali hadhi halafu unaipa mgao wa kile kiwango cha awali, hawaoni hiyo inaweza kuwa ni sababu mojawapo ya malalamiko kwamba Sera hii haitekelezeki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza alivyouliza swali lake ni suala ambalo tunahitaji tufuatilie tujue specifically kwamba kwenye hospitali yake mgao wake uko kwa namna gani.

Nikitoka hapa Mheshimiwa Mbunge tutakaa pamoja tuangalie ukweli wa hilo unalosema. Nimekwenda Hospitali ya Mbozi, wanatumia shilingi milioni 415 kwa mwaka kutibu kinamama na watoto, kwa hizi huduma zinazotolewa bure lakini wanapata OC kutoka Serikalini shilingi milioni 485 kwa mwaka, maana yake ukitoa hizo huduma wanabaki na zaidi ya shilingi milioni 60 kwa mwaka ambazo ni zaidi ya matumizi kwa huduma hizi ambazo zinatolewa bure.

Mheshimiwa Spika, hata ukienda Hospitali ya Mkoa wa Mbeya wamepewa dawa za shilingi milioni 53 pamoja na kuhudumia akina mama wakauza wakapata shilingi milioni 157 lakini mwisho wa siku wakaenda kununua dawa za shilingi milioni 29 maana yake ni chini hata ya dawa walizoziuza. Kwa hiyo, kimsingi ukiangalia tunahitaji tupate ushirikiano kwa Wabunge na viongozi wote ili tuhakikishe haya mambo tunaweza tukaya-solve kwa pamoja kwa sababu mengi ni ya kitendaji kule chini.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, lakini tunaenda kwenye bima ya afya kwa wote haya mambo yataweza kutatulika kwa urahisi zaidi.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kundi kubwa la watu wenye ulemavu wana vipato duni na hivyo inawapelekea kushindwa kumudu gharama za matibabu. Je, Serikali inaonaje ikiwatambua kama ilivyofanya kwa wazee na kuwapatia vitambulisho vya huduma za afya bila malipo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, swali la Mheshimiwa Mbunge ni swali nzuri sana, lakini kwa sababu tunaenda kuleta Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote, naamini wakati wa mjadala haya maswali yote na kuwahudumia watu wa namna hiyo tutaweza kupata namna ya kufanya. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, mgao wa fedha wa kununulia dawa kwa mwaka huu wa fedha zimeenda mara moja tu katika vituo vyetu vya afya na zahanati zetu na isitoshe fedha hizo zinakatwa juu kwa kwa juu kwenda kulipia deni sugu lililopo Bohari ya Dawa. Swali langu kwa Serikali, je, Serikali inamkakati gani kuhakikisha deni linalipwa na dawa zinapatikana katika zahanati na vituo vyetu vya afya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nataka kujua Serikali inampango gani kuhakikisha kwamba mgao wa fedha wa kununulia dawa haukatwi juu kwa juu kwenda kulipia deni hilo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO:-Mheshimiwa Spika,…

SPIKA: Mheshimiwa Waziri amesimama, Mheshimiwa Waziri, sijui mlivyokubaliana lakini tuanze na lile la kwanza.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, yes.

SPIKA: Aliuliza kwa nini dawa za shinikizo la damu hazitolewi katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya na wewe umejibu vizuri kwamba sasa hivi hata watu wenye Shahada za Udaktari sasa wanapangwa kwenye vituo vya afya, kwa hiyo mmekubali kwamba sasa dawa za shinikizo la damu zitatolewa katika vituo vya afya au bado hamjakubali?

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, msisitizo uliowekwa nikwamba dawa za shinikizo la damu zinatolewa kulingana na zinavyofanya kazi, lakini na athari zake. Kwa sababu kuna dawa ambazo zinaenda kugusa moyo moja kwa moja na kuna dawa ambazo hazigusi moyo. Sasa utoaji wake unazingatia utaalam na uwezo wa wataalam wenyewe. Kwa hiyo, wakati tunaamuliwa ndiyo maana sasa utaona wakati kunadawa sasa hivi mpaka sasa zinatolewa kwenye zahanati, vituo vya afya, lakini inakwenda mpaka kufika rufaa.

Mheshimiwa Spika, kuna dawa zingine haziwezi kutolewa huko kulingana na utaalam ulioko katika sehemu husika. Kwa hiyo, sasa tunakwenda kuboresha kushuka chini kuhakikisha sasa wataalam ambao walikuwa wanapatikana tu katika hospitali za wilaya na za mikoa wanaanza kushuka chini sasa kuwepo kwenye maeneo hayo. Pia kuna mwongozo mpya ambao umetengenezwa ambao utaenda sasa kusaidia hizo dawa ziweze kupatikana kila mahali, ndicho ambacho tulimaanisha.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la nyongeza, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Hawa Mchafu kwa sababu katika meseji nyingi ambazo nimekuwa nikirushiwa na Waziri na ambazo nilikuwa nazipata, tumepata meseji zake sana zinazokwenda kwenye service delivery. Bado narudi pale pale kwamba tunahitaji, ukiangalia nilieleza na nikasema kwamba umeona nimetoa mfano wa hospitali, nitoe Hospitali ya Katavi, tumekwenda Hospitali ya Katavi nao wamepewa dawa zenye thamani ya milioni 41, lakini wakauza hizo dawa pamoja na kuhudumia akinamama na watoto wakapata milioni 112, mwisho wa siku wakaenda kununua dawa za milioni…

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri swali alilouliza Mheshimiwa Hawa Mchafu kama la nyongeza ni national problem.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Yes.

SPIKA: Hela zinakatwa juu kwa juu…

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, sawa, nakuja hapo. Kwa hiyo ukiangalia dawa za milioni 22 maana yake amenunua chini ya pesa aliyopata MSD, kwa maana hiyo ni kwamba utakuta utekelezaji kule chini kuna uwezekano wa hospitali zetu kuuza dawa na kupata pesa ya kutosha kupeleka kule na kuweza kuhudumia wananchi. Sasa…
MHE. LUCY T. MAYENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa muda mrefu kwenye kundi hili la watu wenye matatizo ya akili baadhi yao wamekuwa wakipata matatizo ya kisheria na kuweza kuchukuliwa hatua mbalimbali ikiwemo kufungwa, lakini kwa sababu tiba hii na ugunduzi wa watu wa aina hii huwa inachukua muda mrefu sana, kwa maana ya kwamba, mtu anakuwa na matatizo ya akili, lakini uthibitisho kwamba, huyu anakuwa na matatizo ya akili unachukua muda mrefu. Je, Serikali sasa iko tayari kwa kundi hili maalum kwa matatizo haya waliyonayo wakaongeza muda wa jinsi ya kuwahudumia watu hawa, hasa wafungwa, lakini zaidi waweze kuwa na kitengo maalum cha kuhudumia watu hawa, ili badala ya kuteseka muda mrefu kwenye jela na mahabusu, basi waweze kupata huduma mapema ili kuweza kuchukuliwa hatua mapema?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa la nyongeza, lakini naomba kuongezea kidogo pale mwanzo kwenye vyanzo vya sababu zinazosababisha ugonjwa wa afya ya akili, ili ikibidi na sisi wenyewe tuwe mabalozi wa kuweza kudhibiti hivi vyanzo maana vingine ni vya kawaida kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zimetajwa sababu za kibaolojia ambazo ni vinasaba vile ambavyo mtu amekuwa ameumbwa navyo. Unaweza ukawa unavyo lakini usifikie stage ya kuweza kupata huu ugonjwa kutokana na mazingira unayoishi nayo katika jamii yako na wewe mwenyewe yanavyokuandaa kupata au kutokupata. Naweza nikatoa mifano hai hapa kuhusu matumizi ya vilevi kupita kiasi mfano bangi au pombe kupita kiasi, kama mwili wako katika maumbile yake unavyo vile vinasaba unaweza ukajikuta unaangukia kwenye ugonjwa wa kukosa akili. Kwa hiyo, inabidi jamii yetu tunakokwenda huko tuishi vizuri, matumizi ya kila kitu ni kwa kiasi, yasije yakakusindikiza kwenye kupata ugonjwa huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna watu wanawafanyia wenzao ukatili. Ukatili ukianza kufanyika kwenye maisha ya binadamu katika hatua zake zote siyo jambo jema. Sisi kama Waheshimiwa Wabunge ni mabalozi wazuri wakuweza kukemea vitendo vya ukatili maana vinaweza vikawapeleka kupata msongo hatimaye kupata ugonjwa huu wakawa hatari kwenye taifa letu na kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna masuala jinsi gani mwanadamu anachukulia maisha yake, zile changamoto, watu wanasema wana ugumu wa maisha, hili nalo ni suala la kukaa na jamii iweze kuchukulia positive changamoto mbalimbali na siyo kujiwekea msongo wa mawazo kufika huko kusikotakiwa. Dunia imeendelea sana nayo ni shida kwa watoto wetu wanapoangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala lile lingine la pili naomba nilipokee, kweli umuhimu huo upo. Tutajipanga kama Wizara kuona jinsi gani tunatoa huduma hiyo ya kuharakisha hayo mashauri yaishe yanayotokana na afya ya akili. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza, kabla sijauliza kwanza nikushukuru Mheshimiwa Naibu Waziri nimekuwa nikikusumbua sana kwa masuala ya afya, Mkoa wetu wa Iringa na wakati wote upo tayari. Naomba sasa nikuulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa kipimo hiki katika hospitali yetu ya Mkoa wa Iringa kumefanya wagonjwa wetu kupata matatizo makubwa na mateso makubwa kwa sababu ni lazima kwanza waje wafanye kipimo Hospitali ya Mkapa au Hospitali ya Muhimbili Dar es Salaam. Kwa wagonjwa wasio na uwezo wamekuwa wakipata mateso na kusababisha vifo vingi sana katika mkoa wetu wa Iringa.

Je, Serikali sasa iko tayari kuhamasisha sekta binafsi kwa kutumia miradi ya PPP ili iweze kufunga katika hospitali zetu kwa sehemu ambazo hakuna mashine hizo?

Mheshimiwa Spika, swali letu la pili, kwa kuwa kumekuwa na mfumo usio mzuri kati ya MSD, hospitali na vituo vyetu vya afya kuletewa madawa yasiyoombwa na kuacha yale ambayo wanayaomba. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akalizungumziaje suala hili la madawa katika hospitali zetu na vituo vya afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu si tu amekuwa akieleza matatizo ya afya yaliyoko kwenye Mkoa wa Iringa, lakini vilevile amekuwa akiyazungumzia matatizo ya watumishi wa Mkoa wa Iringa.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tunaenda kwenye utaratibu wa bima ya afya kwa wote, lakini Serikali ina utaratibu wa PPP. Sasa kwa kuunganisha hayo kwa sababu utaratibu wa PPP unahitaji umakini wake kutekeleza tusubiri wakati tutaona jinsi ya kufanya namna tuweze kuona namna gani ya kushirikiana na private sector ili kufunga mashine hizo kwenye hospitali zetu, lakini ieleweke tu kwamba Serikali bado ina mpango huo wa kufunga kwenye hospitali zote, na sasa hapa tulipo kuna mashine mbili ziko njia kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kwamba ameuliza kuhusu MSD, nalichukua wazo lake, ni wazo nzuri ambalo sasa Meneja wa MSD ataenda kulifanyia kazi kuhakikisha mawazo yake haya mazuri yanafanyiwa kazi kuhakikisha vinavyoagizwa ndivyo hivyo vinavyopelekwa kule. Lakini tunawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na ma- DMO wote (Waganga Wakuu wa Wilaya) wahakikishe wanaweka takwimu sahihi za magonjwa ili wanapokuwa wanaagiza wafamasia waagize vitu kwa uhitaji wa hospitali husika bila kuagiza kwa namna nyingine tofauti.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, ndani ya wiki hii tuhakikishe tutatimiza ile ahadi yetu ambayo ilivunjika, twende Iringa tukakae pamoja, tujenge uelewa wa pamoja tuje tutatue matatizo ambayo Wabunge wote wa Mkoa wa Iringa wamekuwa wakizungumzia dawa hasa na vilevile na Mbunge wa Iringa Mjini, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu yenye matumaini kutoka kwa Naibu Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kabla sijauliza, napenda kuwashukuru wananchi wa Mkoa wa Shinyanga hasa wanawake walioweza kunichagua na chama changu kuniteua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la kwanza la nyongeza; kwa kuwa ili hospitali iweze kukamilika na kuanza kufanya kazi ni lazima miundombinu yote iwepo kama maabara, X-Ray na mortuary. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba majengo mengine na miundombinu mingine inakamilika?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa tumeanza kuona jitihada nzuri za Wizara ya Afya katika kudhibiti wizi wa madawa na ubadhirifu wa madawa: Je, nini mkakati endelevu wa Serikali kuhakikisha kwamba wizi wa dawa unadhibitiwa na dawa zinapatikana muda wote? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, Mheshimiwa Mnzava ameuliza kuhusu majengo mengine. Kwa bajeti ya mwaka huu 2021 Serikali imetenga shilingi bilioni 4.5 kwa ajili ya majengo mengine ambayo ameyataja.

Vilevile imetenga shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya magonjwa ya mlipuko. Kwa maana kwa bajeti mwaka huu tunaokwenda kuanza, kuna shilingi bilioni 6.4 ambazo zinaenda kuelekezwa kwenye hospitali husika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ameuliza ni kwa namna gani tunaenda kudhibiti wizi wa madawa kwenye hospitali zetu. Kwanza, niseme tu kwamba tumepita na tumegundua kwamba watumishi wengi wa Wizara ya Afya wanafanya kazi nzuri sana lakini kuna wachache ambao wanafanya haya mambo ya ubadhirifu. Vile vile tumegundua kwamba wabadhirifu wamekuwa wakienda Mahakamani aidha, wanaishinda Serikali au kesi zinachukua muda mrefu. Kwa hiyo, tunaenda kimkakati sana kuhakikisha kwamba yeyote atakayepatikana hachomoki, ni lazima awajibike.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya miezi miwili, mtaanza kuona mkakati wa Wizara wa kuhakikisha moja kwa moja hayo mambo yamefutika, kwa sababu watu wako chini kuhakikisha kwamba tukianza kufanya hiyo kazi hakuna atakayechomoka na tunamaliza hilo tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nichukue nafasi hii kuipongeza Wizara ya Afya kwa kazi nzuri chini ya Mheshimiwa Dkt. Gwajima, lakini hivi karibuni Mheshimiwa Dkt. Mollel alifanya kazi nzuri pale Mount Meru Hospitali kwa ajili ya kurudisha zile fedha ambazo alitozwa yule mama ambaye alikuwa ametoka kujifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Hospitali ya Kitete Tabora bado inatoza fedha kwa akinamama ambao wamejifungua normal delivery na ushahidi upo. Je, msimamo wa Serikali ukoje ukizingatia katazo ambalo alilitoa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa Songwe na hiyo Sera ya Afya ambayo ametoka kuitamka Mheshimiwa Naibu Waziri? Nini msimamo wa Serikali kuhusu kuendelea kutozwa akina mama hao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; akinamama ambao wanashindwa kutoa hizo fedha ambazo zinaanzia Sh.30,000/= mpaka Sh.50,000/= katika normal delivery, huwa wanazuiliwa pale Hospitali ya Kitete Tabora Manispaa. Je, Serikali ina msimamo gani kuhusu wale akinamama ambao bado wanazuiliwa na watoto wao wachanga, hakuna kutoka mpaka watoe fedha hizo ambazo ni za kujifungulia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake huo mzuri kwa ukaribu kwenye eneo hili la Huduma ya Mama na Mtoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, msimamo wa Serikali bado ni ule ule wa kisera na miongozo na maelekezo ya Serikali, kama ambavyo nilishasema kwamba Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya wahakikishe wanasimamia utekelezaji wa sera hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini msimamo wa Serikali? Ukienda kwenye hospitali ambayo Mheshimiwa Mbunge anasema, mapato yao kwa mwezi huu wa Januari, 2021 ni shilingi milioni 73; mapato kutokana na Bima ni shilingi milioni 133, lakini Serikali imepeleka OC ya shilingi milioni 54 kwa mwezi wa Januari, 2021. Maana yake mapato yao kwa mwezi ni shilingi milioni 260. Ukitoa na matumizi ya akinamama na watoto, hizi za kutoa bure, ni milioni 13 point, ndiyo matumizi yao kwa mwezi Januari, 2021. Maana yake ukitoa matumizi mengineyo ni shilingi milioni 134, ukija ukijumlisha, wanabakia kuingia mwezi huu wa Februari, 2021 na shilingi milioni 120. Kwa maana nyingine hakukuwa na sababu yoyote ya kum-charge mama na watoto pesa yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ikipeleka OC ya shilingi milioni 54 kwenye hospitali hiyo kila mwezi, maana yake imeshawalipia hawa akinamama. Ukiondoa shilingi milioni 13 ina maana imebaki fedha nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaondoka pamoja na Mheshimiwa Mbunge kwenda Kitete, tukae site pamoja tupige hesabu na tuone. Tutakubaliana pamoja, tutakuja na way forward. (Makofi)
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naipongeza sana Serikali kwa kuweza kuweka mkakati madhubuti…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa mapambano dhidi ya malaria nchini Tanzania yalianza toka mwaka 1890; na wengi tunafahamu kwamba suala la malaria linatokana na mbu; kwa vile tunacho kiwanda kinachozalisha dawa ya viuadudu ambayo inamaliza kabisa mazalia ya mbu: Je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kuzitaka Halmashauri kutenga bajeti katika bajeti zao ili kuweza kununua dawa hizi kila Halmashauri iweze kudhibiti malaria kupitia kila Halmashauri? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa wenzetu toka nje ya nchi wanakithamini sana na kuona umuhimu wa kiwanda hiki na dawa hii inayozalishwa Tanzania: Je, Serikali kupitia Wizara hii inatoa elimu gani kwa wananchi kuhusiana na suala la dawa zinazozalishwa na kiwanda hiki kilichoko Kibaha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Maida kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni namna gani tutakitumia kiwanda ambacho kiko Kibaha kuweza kushirikiana nacho kumaliza tatizo la malaria? Hili tunalichukua. Vile vile ndani ya swali la kwanza ameuliza Halmashauri itafanyaje? Tutaenda kushirikiana na TAMISEMI na hasa kwa sababu kuna tozo ambazo zimekuwa zikitozwa kule Halmashauri zinazotokana na masuala ya afya, fedha hizo zinaweza zikatumika asilimia fulani, vile vile kusaidia kugharamia eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linaonekana linahusu elimu. Nafikiri kwenye strategic ya mwaka 2021 – 2025 kwa kweli tutakwenda kuwekeza kwenye eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge amelishauri. Tunachukua ushauri wake na tutaenda kuufanyia kazi kwa nguvu zote kabisa.
MHE. MWANTUMU M. ZODO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo. Swali la kwanza; je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka watumishi wengi zaidi katika Mkoa wa Tanga, hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Tanga ndio mkoa wenye halmashauri nyingi zaidi nchini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; utoaji wa huduma za afya kwa vituo vya Serikali unakabiliwa na changamoto nyingi tukilinganisha na vituo binafsi. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha huduma zinaboreshwa kwenye vituo vya Serikali ili kuongeza mapato ya Serikali? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika ajira 12,476, Serikali inaenda kuelekeza kwenye maeneo kama aliyoyataja ndio kipaumbele kitakuwa, ukiangalia Mikoa kama Kigoma, Mtwara, Songwe na mingine ambayo kwa kweli ni mikubwa, lakini kuna upungufu mkubwa zaidi, itakuwa ndio priority ya Serikali. Kwa hiyo, tunachukua ushauri wake na utaenda kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile swali lake la pili ameuliza kwamba, alitumia neno mapato kwenye eneo upande wa Serikali. Ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba, ukiangalia kwenye vituo vyetu vya Serikali, hasa ukiangalia kwenye eneo la bima tu, ukiangalia kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge utaona. Tukichukua hata zahanati tu, tuliwahi kuchukua moja, kwenye zahanati tu ya kawaida ambayo wanalipwa bima kidogo ukilinganisha na mkoani, unakuta wanaingiza milioni 84 kwa mwaka, lakini Serikalini wanaingiza 420, lakini ukigawa kwa idadi ya watumishi Serikalini tulijua walikuwa 187 huku kwenye private walikuwa 17, lakini utakuta kwa mwaka wanaingiza shilingi 5,300,000/=, lakini huku serikalini tena mkoani wanaolipwa zaidi wanaingiza shilingi 2,000,000/=

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunafikiri kuna umuhimu wa kwenda kufanya kazi kuhakikisha productivity ya watu wetu inaongezeka. Tukiongeza kwenye eneo la productivity maana yake hata kuna mahali ambapo prpductivity ndio inasababisha ionekane kwamba kuna upungufu, lakini upungufu sio halisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuna eneo la watumishi; tutaenda kuchukua modal ya Wizara ya elimu. Wizara ya elimu wameshirikiana vizuri sana na private sector kwamba, private sector wana shule, lakini na Serikali ina shule, lakini wamekuwa wanashirikiana vizuri sana bila kuwepo anayenyonya upande huu. Hivyo, kwenye afya tutaenda kudhibiti hasa kwenye eneo la kwamba, unakuta kuna watumishi wakati wa kufanya kazi Serikalini wako eneo la private sector wakati wameajiriwa ndani ya Serikali. Nalo hilo litaenda kufanyiwa kazi kwa nguvu na litatusaidia sana kuweka mambo sawa. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM M. NYOKA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; Je, lini Serikali itafanya ukarabati mkubwa kwenye majengo mengine yaliyo chakavu zaidi katika Hospitali hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; uchakavu wa majengo ya hospitali hiyo yanakwenda sambamba pamoja na uchakavu wa vifaa tiba, ikiwemo ultra sound, Mashine ya kufulia na vifaa vingine. Je, Serikali haioni umuhimu wa kununua vifaa hivyo katika hospitali hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nilikuwa naongea na Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo ananiambia alimtembelea juzi kabla ya kuja Bungeni. Kama alivyotembea amejionea yeye mwenyewe kwanza jengo ambalo limejengwa hilo la magonjwa ya dharura, lakini alijionea ukarabati mzuri uliofanyika kwa mapato ya ndani kwenye magonjwa yanayoambukiza ambayo sasa wagonjwa wenye matatizo ya kupumua wamelazwa mle ndani na Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo mengine kwa mtindo ambao sasa jengo ambalo linamalizika mwezi Oktoba umefanyika.

Mheshimiwa Spika, pia akumbuke kwamba pamoja na hilo kwa juhudi za Wabunge wa Mkoa wa Ruvuma wakiongozwa na Mheshimiwa Jenista Mhagama, walianzisha mchakato wa kupata hospitali mpya kabisa ya mkoa, ambapo kule Mwenge - Mshindo wameweza kupata heka 276 kwa ajili ya kujenga hospitali mpya ya mkoa. Waziri wa Afya alituma watu wa kwenda kuangalia eneo, lakini ikaonekana kuna watu sita walitakiwa kufidiwa na ikafanyika tathmini ikaonekana inatakiwa milioni 700 kwa ajili ya kufidia. Sasa Waziri wa Afya ameagiza hebu tuhakiki hiyo milioni 700 kwa watu sita kwa nyumba za udongo ni nini. Kwa hiyo, mimi na Mheshimiwa Mbunge tutakwenda kuangalia tujihakikishie hilo ili sasa tuanze michakato ya kupata Hospitali mpya kabisa ya Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu vifaa tiba; Mheshimiwa Mbunge atakumbuka, Bunge lililopita alikuja akilalamika kuhusu x-ray yao iliyoharibika ambayo ilikuwa ina shida ya battery na ilikuwa imeagizwa nje na imeshafika sasa na x-ray inafanya kazi. Tunampongeza sana Mbunge kwa juhudi zake hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshapeleka milioni 348 MSD, zipo cash pale ambazo ni fedha, tukimaliza hapa tukutane mimi na Mheshimiwa Mbunge ili tuwasiliane na Uongozi wa Hospitali na Mkoa ili tuweze kupanga kulingana na mahitaji anayoyasema…

SPIKA: Ahsante sana.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, lakini Rais wetu amepeleka direct kwenye akaunti yao milioni 110, nayo hiyo haijapangiwa chochote, kwa hiyo tunaweza vilevile kupanga kuelekeza kwenye maeneo anayoyasema.

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, nashukuru ahsante.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, pia kuna milioni 130 kwa ajili ya Kiwanda cha Majitiba, kwa hiyo kazi inaendelea vizuri.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na Mungu akubariki.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kumekuwa na changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa dawa katika zahanati zetu na vituo vya afya. Je, Serikali ina mpango gani wa kuyaruhusu maduka ya dawa ambayo yamesajiliwa kutoa huduma ya upatikanaji wa dawa ambazo wagonjwa wameandikiwa kupitia Bima ya Afya?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Serikali ina mpango gani wa kuanzisha upatikanaji wa Bima za Afya kwa wajasiriamali wadogo na wananchi wenye vipato duni kulipia Bima za Afya kwa awamu lakini vile vile kuendelea kupata matibabu? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza swali ambalo ni muhimu sana hasa kwa mustakabali wa afya ya Watanzania. Swali la kwanza, Serikali ina mpango gani wa kuruhusu maduka yanayouza dawa kutumia bima. Mpango huo upo na una utaratibu wake ili kuweza kuruhusiwa kufanya hivyo. Kwa hiyo, kimsingi mpango huo upo labda kama kuna eneo la kuboresha na kuongeza ufuatiliaji zaidi ili kuhakikisha kwamba yanafika sehemu nyingi. Hilo tutaenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni kuhusu wajasiriamali wadogo na kuhakikisha watu wanapata bima ya afya. Sisi tunachofikiri leo kwa sababu kwenye bajeti hii tunaenda kujadili Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote, tuko tayari kupokea mawazo yenu na kupokea namna nyingi ambazo tunaweza tukaboresha hii huduma.

Hata hivyo, tunawashauri kwa sasa kuna hicho kitita ambacho kinatumika kwa wajasiriamali ambao hawajajisajili kwenye makundi maalum ambayo yanaangalia umri, ukubwa wa familia na kadhalika, tunamwomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwahamasisha wajiunge kwa hilo, lakini wazo lake la kwamba tunafanyaje waweze kujiunga kidogo kidogo nalo hilo ni wazo tunalolichukua, wakati tunajadili huu muswada mpya wa sheria tuone tunalifanyaje na wakati hata mwingine kwenye simu na vitu vingine ili wazo lako ambalo ni zuri liweze kutekelezeka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARTHA N. GWAU: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini nilikuwa na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, la kwanza. Je, ni mamlaka gani hasa inayosimamia uingizaji wa zebaki nchini?

Mheshimiwa Spika, lakini kingine, Serikali iko tayari kutenga fedha kwa ajili ya kwenda kutoa elimu ya madhara ya kemikali hiyo ya zebaki kwa wananchi wanaojihusisha na uchimbaji wa madini, hususan Mkoa wangu wa Singida, Ikungi na Wilaya ya Iramba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza swali lake la kwanza ni mamlaka gani inayohusika na kusimamia uingizaji wa kemikali hizi nchini:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye swali la msingi, ni Mkemia Mkuu wa Serikali, lakini ili tuweze kufanikiwa kwenye hili ni suala ambalo linahitaji kushirikisha mamlaka mbalimbali. Kwa hiyo, kikubwa ni kwamba, kupitia Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mamlaka mbalimbali ambazo zinahusika zitashirikishwa, ili kuhakikisha kunakuwepo na udhibiti wa kina.

Mheshimiwa Spika, lakini swali lake la pili. Je, Serikali ipo tayari kutenga fedha kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu suala hilo:-

Mheshimiwa Spika, ni swali zuri, na nafikiri iko tayari na kwa sababu tunahitaji kwakweli kutoa elimu pamoja na kudhibiti kwa maana ya kuwasajili watu kama hao wanaoingiza, lakini vilevile kuna umuhimu wa ufuatiliaji, ili zebaki isiweze kuingia kwa njia za panya. Lakini wakati huohuo kwenda kutoa elimu hasa kwenye maeneo ya madini ambayo wanachimba dhahabu, kwenye makaa ya mawe ambao wanahitaji kutumia zebaki. Wakati huohuo kwenye hospitali zetu ambazo vilevile zenaki inatumika, kuhakikisha kwamba, wakati wa ku-despose hivyo vitu vinakuwa disposed vizuri. Vilevile kuwajulisha wananchi namna nzuri ya kutumia, lakini kununua vifaa ambavyo wakati wachimba madini wanapokuwa wanatumia basi kuwe na mashine na vifaa maalum ambavyo vinasababisha hivyo vitu visiweze kutoka na kuingia kwenye jamii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri swali lake Serikali iko tayari na nafikiri kwa ajili ya kufanya hatua hiyo fedha zinahitajika.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ilianza kama zahanati mnamo mwaka 1920 ikapandishwa daraja ikawa Kituo cha Afya mwaka 1922, ikapandishwa daraja ikawa Hospitali ya Mkoa mwaka 1956, mwaka 2011 ikapanda daraja kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Hospitali hii inahudumia Wilaya zote saba za Mkoa wa Kilimanjaro, lakini ina upungufu wa Madaktari Bingwa hususani upande wa wanawake.

Je, Serikali inasema nini kuhusu kuongeza madaktari bingwa wa Hospitali hii kwa sababu huduma stahiki wananchi wa Kilimanjaro hawazipati kutokana na ukosefu wa madaktari na madaktari bingwa?

Kutokana na miundombinu hii iliyoanza tangu mwaka 1920 ni kweli kabisa hospitali ile imechoka, mazingira…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa uliza swali.

MHE. ZUENA A. BUSHIRI: Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kujenga majengo ambayo yana hadhi ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake mzuri sana hasa kwenye eneo la hospitali hiyo, lakini kwa ufuatiliaji wake mzuri hasa kwenye huduma ya akina mama na watoto. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kuhusu Madaktari Bingwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mawenzi hospitali hiyo mpaka sasa ina ma-specialist, tisa lakini specifically idara anayoisema Mheshimiwa Mbunge ambayo inahitajika kuwa na Madaktari Bingwa wanne ina Daktari Bingwa mmoja. Kwa hiyo, ninamuahidi Mheshimiwa Mbunge wakati tunajipanga kwa mwaka huu kwa maana ya ajira za mwaka huu Hospitali ya Mawenzi itakuwa mojawapo ya hospitali za kipumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sivyo tu kwamba kuna ma-specialist tisa, lakini kuna baadhi ya Idara kama Idara ya Mifupa ambayo haifanyi vizuri sana, tutaenda kufanya kazi kubwa kwenye kuboresha hasa kuweka kwenye vifaa, lakini kuelekeza utawala wa hospitali ili usimamie vizuri eneo hili liwe kufanya kupunguza rufaa kwenda KCMC.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pilli ni kuhusu miundombinu kwamba hospitali ni ya muda mrefu na kuna majengo ambayo yamechakaa na mengine kabisa hayafai kutumika. Ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema na baada yeye kuja Wizarani, Mheshimiwa Waziri wa Afya alituma timu wiki mbili zilizopita, wameshakwenda Mawenzi na sasa wako kwenye hali ya kuangalia yale majengo ambayo hayafai kabisa na michoro imeanza kuchorwa ili kuja na mawazo ya namna gani tunaweza kuboresha hospitali hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini kuna suala la ardhi pembeni ya Hospitali ya Mawenzi kuna ardhi ya Manispaa ambayo tunaweza tukafikiria namna ya kushirikiana na Manispaa kama inawezekana, lakini ukiangalia ramani yamwaka 1959 Hospitali ya Mawenzi na ukiangalia mabadiliko ya 2009 utaona kuna maeneo fulani ya hospitali hiyo ambayo vilevile hayaonekani kwenye ramani nayo yatashughulikiwa kuhakikisha sasa tunaenda kuja na mkakati ambao hospitali hiyo itaboreshwa vizuri sana, ahsante sana.
(Makofi)
MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kama alivyoainisha Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa upande wa figo, kama Taifa tumepiga hatua kubwa sana pia kwa kutumia wataalam wetu wa ndani.

Hata hivyo, utakubaliana nami kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa sana la magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari, moyo na figo. Sasa swali langu la kwanza, kwa Serikali, ni lini mchakato huu wa kuandaa huu Muswada utakamilika kama alivyoonesha sasa hivi tunatumia utaratibu wa Kimataifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Muswada huu utaletwa hapa Bungeni ili kutupa nafasi sisi ambao tuko tayari kuchangia viungo vyetu kama vile figo tuweze kufanya hivyo? Sheria hii itaruhusu sasa wale wenzetu ambao wanafikia mwisho wa maisha yao wataweza kuchangia viungo vyao kama vile figo na moyo ili kuwasaidia Watanzania wenzetu wenye uhitaji wa viungo hivyo waweze kuboresha afya zao na kuendelea kujenga Taifa letu. Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo amekuwa akifuatilia sana huduma za watu wake wa Iringa. Amekuwa akiwasiliana na sisi sana, hasa wagonjwa wake wanapokuwa Bugando, Muhimbili, KCMC na kwingine amekuwa akifuatilia kwa karibu sana. nadhani ndiko alikojifunzia kwamba, haya matatizo yanatakiwa yashughulikiwe haraka sana kwasababu, yanasumbua wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake ni kwamba, ni lini?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwasababu kama nilivyosema kwamba, tuko sasa kwenye hatua ya kukusanya maoni ya wadau. Kwa hiyo, kwenye Bunge la mwezi wa tisa tutaleta muswada kwa ajili ya kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini niliombe Bunge lako Tukufu kwamba, suala sio kwamba tu sisi kuja na sheria ya kuweza kuruhusu upandikizaji na kuvuna viungo. Suala ni kwamba, ni kwa nini imeongezeka tatizo la watu kuharibika figo na matatizo ya moyo, hilo ndio swali kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Wabunge wenzangu kwa sababu sauti zao zinafika mbali na zinaheshimiwa na wananchi zile za taratibu za kuzuia matatizo ya figo, za kuzuia kupata magonjwa ya moyo. Tutakapokuja Wizara na mkakati na mtaona wakati wa corona tulikuwa na mkakati mzuri ambao mmetusaidia endeleeni kutuunga mkono ili kuzuia watu wasipate haya matatizo.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, KFW Germany wamekuwa wakitoa huduma hiyo tangu mwaka 2013 mpaka 2018 mwishoni Mkoani Tanga, lakini 2019 mwanzoni ndipo walisitisha huduma zile na kuweza kupeleka mikoa mingine. Naomba kujua sababu gani imesababisha KFW Germany kuacha kutoa huduma ile ya mama na mtoto Mkoani Tanga na kuhamishia sehemu nyingine?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili. Mwaka 2017 Serikali kwa mara ya kwanza ilianzisha upasuaji kwa watoto wenye upungufu wa usikivu nchini Tanzania, yaani wanafanyiwa upasuaji na wanapata mashine ambayo ni cochlear implant surgery machine, lakini accessories ama spare parts za mashine hizo zimekuwa ni ghali sana kwa wananchi wa kawaida kuweza kuzi-afford. Betri moja la mashine ile ambayo ni rechargeable ni zaidi ya laki tano, lakini ukienda kwenye…

NAIBU SPIKA: Swali Mheshimiwa.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, Serikali sasa ione haja ya kuvigiza vifaa hivyo nchini na wananchi waweze kununua kupitia Serikali, ili kuweza kushusha bei ya ununuzi kwasababu India ni rahisi sana. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba kujibu maswali yake mawili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni kwamba, kwa nini, sababu iliyofanya ule mkataba ukavunjika wa elfu mbili maana mkataba ule ulikuwa ni wa kipindi maalum 2012 ambao umeanza kama anavyosema 2013 na mpaka 2018, lakini nafikiri anauliza sababu iliyofanya:-

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ya kwanza ambayo sisi tunaijua ilikuwa ni mkataba wa wakati maalum, lakini nimuombe Mheshimiwa Mbunge tutafuatilia vizuri zaidi kwasababu inawezekana kulikuwa na uwezekano wa kuongeza mkataba na ukaweza kusitishwa. Tutaenda kufuatilia pamoja na yeye ili tujue na nitampa taarifa kwamba, ni nini kama kuna uwezekano wa kufanya lolote tuweze kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kufuatia hilo najua amekuwa akipata shida sana na umekuwa ukija wizarani kwa ajili ya akinamama wa Mkoa wa Tanga kuchajiwa hela. Mimi na wewe tutatafuta muda tuende tukaangalie tatizo liko wapi tulishughulikie haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili lilikuwa ni suala la upandikizaji wa viungo, watu wenye shida ya usikivu, upandikizaji ili waweze kusikia:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikwambie kwamba, Serikali yetu ukweli watu walikuwa wanapelekwa nchi za nje kwenda kuweza kupandikizwa hivyo viungo na walikuwa wanatumia zaidi ya milioni 100 kwa mtu mmoja. Lakini sasa Tanzania vimeshanunuliwa vifaa na upandikizaji huo umeanza kwenye hospitali yetu ya Muhimbili na ndicho anachozungumzia Mheshimiwa ambayo bado ni changamoto kwasababu, kununua tu vifaa vyenyewe ni zaidi ya milioni 40 ili kuweza kumpandikiza mtu huyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunaenda vilevile kuja na Muswada wa kupanga gharama za vifaa tiba na dawa hatuna muongozo wa kudhibiti bei za vifaa hivyo, mtu anajiamulia tu kuuza bei anayoitaka. Lakini kwasababu Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alitoa bilioni 80 juzi kwa ajili ya kununua vifaa tiba tutaenda kuzingatia kwenye eneo hilo tuhakikishe Muhimbili wana vifaa hivyo kupitia MSD.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, mbele ya Rais kwa maana ya Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Mheshimiwa Waziri Ummy alituhakikishia kwamba itakapofika mwezi Julai, 2020 hospitali hiyo itakuwa imekamilika. Serikali inasema nini kwa Wanakatavi kutokana na ahadi hizi zisizotekelezeka? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili Mkoa wa Katavi umbali kutoka Katavi ikitokezea amepatikana mgonjwa, anahitaji tiba na madaktari bingwa ama umpeleke Mbeya, Mwanza au Dar es Salaam. Umbali huu ukiwa salama na katika mazingira ya amani unaweza ukaenda bila matatizo, lakini ukiwa katika hali ya mahtuti, umbali unakuwa ni mrefu zaidi. Serikali inasemaje katika namna ya kuwanusuru Wanakatavi kuja na suala zima la dharura nikizingatia yapo maeneo mengine hospitali zimejengwa kwa fedha ambayo ni zaidi ya hiyo bilioni tisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji mkubwa sana wa hali ya afya ya Mkoa wake na Wabunge wa Mkoa huo kwa sababu wamekuwa wakija Wizarani na nakumbuka alikuja pamoja na Wabunge wenzake. Waziri wa Afya alinituma nikaja Mkoani kwao, ni kweli kama Mbunge anavyosema kwa rufaa tu pale kwao wanatumia shilingi milioni 250 kwa mwaka kwa ajili ya ambulance tu kupeleka watu rufaa. Kwa hiyo, anachosema ni kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anasema hospitali hiyo iliahidiwa kumalizika mwaka jana na bahati mbaya haijafanyika kama ahadi ilivyokuwepo. Kama unakumbuka tulikwenda Wizarani na tayari Waziri wa Afya ameunda timu na imechunguza sababu ambazo zimesababisha hizi hospitali zichelewe na sababu hiyo utaletewa Mheshimiwa Mbunge. Vilevile tumeshatengeneza strategy ambayo kwa uhakika kabisa Januari, 2022 hospitali hiyo inakwenda kumalizika ili kuondoa wananchi katika adha hiyo ambayo tayari ulishakwenda kunionesha Mkoani kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili umezungumzia umbali, tulipokwenda mkoani kwako ulielezea suala la ramani ambayo mlitaka hasa kwenda kwenye hospitali za kanda. Ile ramani ambayo ulikuwa unaizungumzia Mheshimiwa Mbunge, tayari Waziri ameshakaa na timu yake na hata yale mapendekezo yenu ya kupunguza rufaa hasa kuelekea kwa hospitali za kanda inatafutiwa suluhisho na itafanyiwa kazi vizuri kama ambavyo mlitegemea ifanyike Wabunge wa Mkoa wenu. Ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini sasa Serikali italeta mashine za CT-scan na MRI kwa ajili ya Hospitali za Mikoa hususan Mkoa wa Manyara kwa kuwa gharama ni kubwa za wagonjwa wa magonjwa makuu kwenda kwenye Hospitali za kKnda? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kutoka Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema hata kwenye bajeti ya mwaka huu Serikali imejipanga, siyo tu kuweka CT-Scan kwenye hospitali za kanda, bali pia kwenye hospitali za mikoa. Tayari Hospitali ya Mkoa kama Mwananyamala; na sasa hivi tunavyozungumza nilikuwa naongea na Meneja wa MSD, kuna CT-Scan mbili ambazo ziko njiani kwa ajili ya kufunga kwenye hospitali mbili za mikoa; na jinsi fedha zitakavyokuwa zinapatikana, Serikali itahakikisha kwamba hospitali zote za mikoa zinapata CT-Scan na hasa tutazingatia umbali kutoka CT-Scan moja kwenda nyingine ili kuhakikisha kwamba zinawekwa kwenye angle ambazo zitapunguzia wananchi adha ya kwenda mbali kufuata CT-Scan.
MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, napenda kuishukuru Serikali kwa ujenzi na swali langu la nyongeza ni kwamba, kwa kuwa ujenzi huu umechukua muda mrefu na kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Katavi bado wanaisubiri kwa hamu sana hiyo Hospitali ya Mkoa. Je, Serikali inatoa commitment gani kutoa pesa zilizobaki bilioni 5.8 kwa ajili ya kumaliza ujenzi wa hii hospitali? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Mkoa wa Katavi tumejenga vituo vingi sana vya afya, lakini pia tunazo hospitali tatu tumejenga kwenye Wilaya zetu tatu za Mkoa wa Katavi pamoja na zahanati. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutuletea vifaa tiba kama vile vifaa vya upasuaji, ultrasound na kadhalika kwa ajili wananchi wakati wakiwa wanasubiri hiyo hospitali iishe waweze kuhudumiwa kwenye vituo vya afya pamoja na hizo hospitali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze Wabunge wote wa Mkoa wa Katavi, kwa kweli wamekuwa wakifuatilia suala la afya kwenye mkoa wao kwa kina sana na nawaelewa sana kwa sababu ni mojawapo ya mikoa ambayo ni migumu kufikika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kwamba ni lini sasa Serikali kwenye hospitali ambazo zimejengwa itapeleka vifaa tiba. Kama ambavyo Wabunge wanajua Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa bilioni 80 kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba. Kwenye hizo bilioni 80 mojawapo ya vipaumbele ambavyo tayari tumeviweka ni hospitali ambazo Mheshimiwa Mbunge amezitaja hapa. Kwa hiyo, kwa uhakika kabisa tutafanya hivyo. (Makofi)
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida imechukua muda mrefu sana kukamilika. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi waweze kupata huduma nzuri za afya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumeeleza kwenye Hospitali ya Mkoa ya Katavi, kwa ujumla kwenye Hospitali zetu za Mikoa kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi, Serikali kwenye bajeti ya mwaka huu imetengwa bilioni 57 ambapo kwenye bajeti hiyo mojawapo ya hospitali ambayo imetengewa bajeti ni Hospitali ya Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada tu ya bajeti hii sasa tunaenda kuanza kazi hiyo. Naomba mimi na yeye tupange kwenda kwenye Hospitali ya Mkoa wa Singida tuangalie mambo mengi kwa sababu vilevile kuna suala la wao kutoka kwenye ile hospitali ya mjini kuhamia kwenye hiyo hospitali inayojengwa. Ahsante. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupata nafasi. Ningependa kujua ni lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe iliyopo Vwawa Ilembo itakamilika kwa sababu ilikuwa ianze kufanya kazi mwaka 2020? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anakumbuka yeye alikuja akanieleza suala hilo na nilikwenda kwenye ile hospitali. Ninachotaka kumwambia jengo la OPD na maabara limeshakwisha lakini sasa jengo ambalo liko kwenye level ya msingi linajengwa ni jengo la wazazi ambalo nalo linaendelea na Waziri Mkuu alikuwa amepanga ziara ya kwenda kuzindua hayo majengo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye bilioni 80 iko kwenye bajeti ya kuweka vifaa kwenye hilo jengo la wagonjwa wa nje. Kwa hiyo, mara tu baada ya Bunge hili ratiba ile ya Waziri Mkuu ya kwenda kulizindua itakamilika na kazi itaanza kwenye hospitali wakati majengo mengine yanaendelea kuingizwa kwenye bajeti. (Makofi)
MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hii ni ya Rufaa ya Mkoa na ukisoma vitabu vya bajeti kwenye mwaka uliokwisha ilikuwa inahudumia wagonjwa karibu 75,000; mwaka huu ambao tunaumalizia wameongezeka wamefikia 96,000 na ni ongezeko la karibu asilimia 13. Lakini pia vitu vya kawaida kabisa kama nyuzi za kushona, kama giving set, vitu vya kawaida kabisa kwa ajili ya huduma ya akinamama havipatikani na ni Hospitali ya Rufaa.

Je, Serikali inatoa commitment gani kuhakikisha vitu hivi vya kawaida kabisa vinapatikana wakati tunasubiri ukamilishaji wa jengo hilo la mama na mtoto?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge Priscus Tarimo kwa jinsi ambavyo anafuatilia kwa umakini sio tu hospitali yetu ya Mawenzi, lakini na Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya KCMC hasa kwenye maeneo ya miundombinu, lakini kwenye kuwatetea na kufuatilia maslahi ya watumishi wa hospitali zetu hizi zote mbili.

Swali lake ni kwamba ni lini Serikali itahakikisha kwamba vifaa vinapatikana, ametaja nyuzi na vitu vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo huko nyuma mmesikia Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan mwezi wa pili alitoa shilingi bilioni 43 kwa ajili ya vifaa tiba na dawa, lakini mwezi wan ne alitoa shilingi bilioni 80 kwa hiyo, ukijumlisha ni kama shilingi bilioni 123 zimetolewa kwa ajili ya eneo hilo la huduma ya tiba. Kikubwa ni kwamba ndani ya mwezi mmoja vifaa hivyo vitakuwa vimefika kwa sababu vimenunuliwa viwandani na hilo tatizo litakwenda kuisha na hospitali yetu itakuwa na vifaa vyote ambavyo vinahitajika. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali nyingi za Halmashauri zimebaki bila kumalizika na kwa bahati mbaya Serikali imekuwa na tabia ya kupeleka fedha na mwisho wa bajeti inazichukua. Jimbo la Mbulu Vijijini hospitali imefikia asilimia 95 kumalizika.

Je, ni lini Serikali itarudisha shilingi milioni 300 ilizozichukua ili hospitali ile iweze kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tatizo ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Mbunge Massay limetokea kwenye Wilaya nyingi hapa nchini, hata ikiweko Wilaya yetu ya Siha.

Mimi ninachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge tukimaliza hapa, hebu tutoke mimi na wewe twende Hazina tuangalie ni nini kimetokea na waweze kusuluhisha hilo tatizo liweze kufanyiwa kazi na fedha hizo zipatikane kazi hiyo imalizike ambayo ni asilimia tano imebaki ili hiyo hospitali ianze.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa hii nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbozi lenye wakazi 300,000 halina hospitali, linategemea vituo viwili vya afya kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake, lakini katika hivyo vituo viwili vya afya cha Itaka na Isansa havina vyumba vya kulaza wagonjwa, havina wodi za kulaza wagonjwa. Sasa pamoja na kwamba tuna madaktari wazuri wa kufanya upasuaji mkubwa katika hivyo vituo vya afya wananchi wanakosa huduma kwa sababu hawana vyumba vya kulaza wagonjwa.

Sasa nini mkakati wa Serikali wa kujenga wodi za kulaza wagonjwa kwenye hivyo vituo vya afya viwili vya Itaka na Isansa ambavyo vinategemewa katika Jimbo la Mbozi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kwa Mheshimiwa Mbunge ni kweli kwenye Hospitali yake ya Wilaya ya Mbozi kwanza miundombinu ni michache, lakini sasa hivi ndio inatumika kama Hospitali ya Mkoa na sasa tumeshamalizia majengo ya Hospitali yao ya Mkoa. Kwa hiyo, mzigo ulioko kwenye Hospitali ya Wilaya ya Mbozi ambao ilikuwa inaubeba kama Hospitali ya Mkoa sasa utahamia kwenye hospitali ya mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ni kweli kwamba ili kuboresha huduma na kupunguza adha ya wananchi kufuata huduma mbali ni vizuri vituo vya afya viweze kusimamiwa. Kwa hiyo, mimi nafikiri Mheshimiwa Mbunge ni tukitoka hapa Bungeni tukae mimi na wewe, ili uweze kuleta vituo vya afya ambavyo umevifikiri tuangalie kama tayari tumeviingiza kwenye bajeti, kama hatujaingiza tutaweza kuingiza kupitia Global Fund ili viweze kufanyiwa utekelezaji.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi narejea kwenye lile swali la msingi la Hospitali ya Mawenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Hospitali ya Mawenzi ilipandishwa hadhi ikawa Hospitali ya Rufaa na kule Moshi hakuna Hospitali ya Wilaya. Ni lini Serikali itatujengea Hospitali ya Wilaya ili iweze kuhudumia watu wa Jimbo la Moshi Vijijini, Jimbo la Vunjo na Manispaa ya Moshi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa ndugu yetu, Profesa Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Wilaya ya Moshi Vijijini haina hospitali ya wilaya na ndio maana hata baadhi ya ambulance kwa ombi la Mbunge ambazo zilikuwepo pale Mawenzi zimetolewa zikapelekwa kwenye vituo vya Moshi Vijijini ili kusaidia wananchi kutokana na hiyo adha ambayo anaisema.

Mimi nafikiri Mheshimiwa Mbunge kuna umuhimu wa kukaa sasa na kuangalia jiografia ya Moshi Vijijini kwa sababu ukiiangalia jiografia yake kwanza ni milimani, lakini imezunguka Mji wa Moshi Mjini; muangalie sehemu nzuri kijiografia ambayo inafaa halafu hatua stahiki zianze kufuata sasa kuanzia kwenye Halmashauri yenu kuja Mkoani - RCC, ili iweze kufika TAMISEMI na mwisho wa siku kazi hiyo iweze kufanyika.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaishukuru Serikali kwa majibu mazuri; nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ugonjwa hautasubiri mpaka mpango huu mzuri wa bima ya afya kwa wote ukamilike, na kwa kuwa miongozo ambayo inatolewa na Serikali kiuhalisia haizingatii na watendaji; ni nini kauli ya Serikali kwa watendaji hawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ikumbukwe kwamba wakati wa Bajeti ya Wizara hii ya Afya, Mheshimiwa Waziri wakati akihitimisha hotuba ya bajeti yake alisema kwamba Serikali imeandaa utaratibu mzuri wa matibabu kwa wazee, ambapo alisema kwamba zitaandaliwa tisheti nzuri ambazo zitahamasisha utoaji wa huduma bora kwa wazee.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali inaonaje mpango huu mzuri ukawajumuisha na watu wenye ulemavu?

Kwa mfano kama tisheti hizi zitaandikwa mzee kwanza, basi iwe mzee kwanza na mtu mwenye ulemavu, lakini pia kama itaandikwa kwamba tuwajali wazee basi tuwajali wazee na watu wenye ulemavu.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL). Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kusema kwamba ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema, kwamba ugonjwa na matatizo hayasubiri mswada kutengenezwa. Lakini kama ambavyo unajua kwamba kwa sasa kwenye hospitali zetu; na kwenye eneo hilo anachotaka kujua Mheshimiwa Mbunge ni tamko gani linatolewa. Kwa sababu kwa kweli pamoja na kuwepo na sheria na vitu, vingine inawezekana kuna maeneo ambayo haizingatiwi maelekezo ya Serikali kwa mambo ambayo kwa sasa yapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mimi niseme na nitoe ari kwamba, kwanza agizo, Waganga Wakuu wa Mikoa na Ma-DMO wanapokuwa wanazunguka; cha kwanza kwenye CCP zetu na kwenye supervision zao wahakikishe kwamba wamekagua na kuhakikisha kwamba hizi haki zimezingatiwa. Pia kuwaomba kupitia TAMISEMI Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala kusimamia suala hilo ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni kuhusu suala la kuunganisha huduma za watu wenye ulemavu pamoja na huduma za wazee. Kama ambavyo tayari Mheshimiwa Waziri ameshazindua hili suala la tisheti na kuzindua huo mkakati wa kuweza kuboresha huduma za wazee kama ambavyo mmeona kwenye vyomba vya Habari; tunachukuwa wazo lake kwamba hilo suala liende kuunganishwa pamoja na suala la watu wenye ulemavu.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali inawaambia nini wananchi hasa wazee wenye kadi za Bima ya Afya pindi wanapokwenda kupata huduma na kujibiwa dawa wakanunue madukani; nini majibu ya Serikali juu ya hili?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kutokana na ongezeko kubwa la zahanati vijijini changamoto kubwa ni upatikanaji wa dawa, vifaa tiba kwa maana ya vipimo na waganga. Nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana bila usumbufu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, ni kweli concern ya Mbunge anayoisema ndiyo concern kubwa ambayo imeonekana kwenye eneo la CHF ambayo wananchi wengi wamekuwa wakienda na wakifika kwenye kituo wanakutana na tatizo hilo la upatikanaji wa dawa pamoja na daktari kumwandikia na CHF ni kwamba haiwezi kumsaidia mtu huyu kupata kwenye maduka mengine dawa zaidi ya kwenye kituo husika.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana sasa hivi Serikali umesikia moja; Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 123 kwa ajili ya kuboresha eneo la dawa, maana yake sasa wakienda vituoni watakutana na dawa. Lakini umemsikia Waziri wetu kwa sababu suala la upatikanaji wa dawa vituoni ni zaidi tu ya fedha zenyewe kupatikana ndiyo maana umemsikia Waziri wetu wa Afya pamoja na Waziri wa TAMISEMI wameanza kufanya kazi kubwa sana kwenye eneo la uadilifu kuhakikisha kuna accountability kwenye eneo zima la dawa. Kwa hiyo hilo ndilo jibu la swali lako la kwanza.

Mheshimiwa Spika, lakini swali la pili ni upatikanaji vilevile wa dawa na vifaa tiba vituoni; nalo linajibiwa na swali la kwanza kwa sababu tukishakuwa na shilingi bilioni 123 ambayo Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshazitoa kimsingi tutakuwa tumetatua hilo tatizo. Lakini vilevile sasa tunapokwenda kwenye Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote maana yake hata tukiingia watu wote wakapata bima ya afya inayofanana na hizi ambazo wafanyakazi wa Serikali wanazo hata kama watakosa dawa kwenye kituo chake, kuna maduka ya dawa ambayo yanatumia Bima ya Afya ambayo ni hii kubwa ya Taifa kwa hiyo tatizo hilo la dawa litaondoka.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, kwa sababu Mheshimiwa Waziri katika jibu lake amesema kwamba wanaruhusu kuwahakiki wazee na kwa sababu mfumo wa kuhakiki wazee haujawa rasmi, mmewaachia Halmashauri na ndiyo unakwamisha wazee wengi kutokupata huduma hii kwa kigezo cha kutokusajiliwa.

Ni nini hatua ya ziada ya Serikali kuhakikisha wazee wote wanasajiliwa katika muda ambao umepangwa ili wapate haki yao ya matibabu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL):
Mheshimiwa Spika, labda nijibu swali zuri la Mheshimiwa Mbunge, moja; nachukua concern yake kwa sababu ameonesha kuna tatizo kwenye eneo zima la utambuzi wa wazee. Kwa hiyo tutaenda kukaa kuona ni namna gani tunaweza kuboresha hilo eneo hasa la utambuzi wa kujua ni nani mzee na nani siyo mzee.

Lakini kwa sababu tunakwenda, suala hapa ni tiba ni ku-access tiba tunapokwenda kwenye Muswaada wa Bima ya Afya kwa Wote kimsingi hilo litakuwa lipo contained kwenye utaratibu mzima, kwa hiyo, halitakuwa tatizo.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nishukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini nina swali la nyongeza.

Kwa kuwa hospitali ile ni kongwe na mpaka sasa hivi kwenye Hospitali ya Ligula Mtwara haina x-ray machine, lakini katika suala hilo la kutokuwa na x-ray machine huduma za theatre kwa ujumla wake hazipo.

Je, ni lini Serikali sasa itaamua kututengenezea masuala mazima ambayo yanahusu package hiyo ya x-ray machine pamoja na jengo la theatre? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, je, ni lini Serikali itaratibu suala zima la kutuletea Madaktari Bingwa ambapo tunashida ya Madaktari Bingwa wa Watoto, Madaktari Bingwa wa Koo ambao vifo vinasababisha kuwa vikubwa sana kwenye hospitali yetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Hassan Tenga kwa ufuatiliaji wake wa kina sana kwa suala zima la Hospitali ya Mkoa, lakini sio tu Hospitali ya Mkoa, ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwenye Wilaya yake.

Swali lake la kwanza ni lini hospitali hiyo itapata x-ray, lakini pamoja na vifaa vya theatre. Kama ambavyo nimekuwa nikisema hapa Rais wetu miezi michache iliyopita alitoa shilingi bilioni 123 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na dawa na hospitali yake hiyo ipo kwenye bajeti kwa ajili ya vifaa husika ambavyo ameulizia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili analoulizia ni suala ambalo mimi na yeye kama ambavyo nimemuomba la madaktari kupelekwa kwenye hospitali yake; na ni ukweli kwamba kuna tatizo la madaktari kwenye maeneo mengi tu sio eneo la kwake na kuna makakati huo sasa wa ajira mpya ambazo zinakuja tunamfikiria lakini mimi na yeye kama tulivyopanga tutakwenda kwenye hospitali yake kufuatilia Hospitali ya Mkoa tutakwenda pamoja tutaona tatizo ni kubwa kiasi gani tuone tunafanya nini kuhamisha sehemu nyingine ili madaktari waweze kusaidia eneo hilo.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize Hospitali ya Wilaya ya Hai imekuwa na changamoto kubwa sana ya majengo mpaka ninivyozungumza hatuna jengo la mama na mtoto, hatuna jengo la pharmacy, hatuja jengo la maabara kakini pia work way za kuwasiliana kwenye majengo haya hatuna.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutujengea majengo haya? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kaka yangu Saashisha Mafuwe kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwenye Wilaya ya Hai hasa kwenye kufuatilia miundombinu tu sio tu ya Hospitali ya Wilaya, lakini zahanati zake lakini vituo vya afya na Hospitali ya Machame ambayo ni DDH, ni ya kanisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja kuna kazi kubwa sana inafanywa na Waziri wa Afya Mheshimiwa Dorothy Gwajima pamoja na Waziri wa TAMISEMI dada yetu Ummy Mwalimu ya kuhakikisha tunapata resources kupita sources zingine ili tuweze kukamilisha miradi kama hiyo ambayo anaisema ambayo inawezekana haijaingia kwenye bajeti kubwa ambayo sasa tumeipitisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Saashisha tukitoka hapa twende pamoja, tuangalie mkakati huo wa Mawaziri wetu wawili tuone ni namna gani inaweza kufanyika kupitia Global Fund, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana; kwa kuwa Serikali imeendelea na ukarabati wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa, nataka kujua tu ni nili itakamilisha ukarabati huo ili kuondoa adha inayojitokeza katika suala la kupata huduma ya afya katika Mkoa wa Singida? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tulishakwisha kusema hapa kwa bajeti ya mwaka 2021/2022 zimetengwa zaidi ya shilingi bilioni 57 kwa ajili ya kufanya ukarabati na ujenzi katika hospitali mbalimbali za rufaa hapa nchini hospitali aliyoitaja Mheshimiwa hapa ni mojawapo ya hospitali ambayo ipo kwenye mpango huo.

MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusu Hospitali ya Rufaa ya Ligula tuna ujenzi wa Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara ambao naishukuru Serikali imekamilisha kwa awamu ya kwanza; je, Serikali imejipangaje kuanza ujenzi awamu ya pili ya hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo amekuwa karibu sana kufuatilia ujenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwenye bajeti ya mwaka huu ni moja wapo ya hospitali ambazo zimetengewa fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi na kumalizia baadhi ya unit ambazo ilikuwa hazijamaliziwa, ni hospitali aliyoitaja.
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la x-ray katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Ligula mimi niliuliza hilo swali Bunge lililopita Naibu Waziri wakati ule Mheshimiwa Ndugulile aliniambie x-ray machine ya Mkoa wa Mtwara ipo bandarini, leo majibu ya Naibu Waziri anaongea as if hakuja kitu kabisa. Mimi nataka tu kujua ile x-ray yetu ambayo tuliambiwa ipo bandarini ime-evaporate au vipi? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze dada yangu mpambanaji kwa swali lake zuri ambalo linahusu wananchi; moja ni kwamba anasema kwamba x-ray hiyo ilikuwa ipo bandarini na mpaka sasa haijafika kwenye eneo husika. Nikuombe dada yangu tukimaliza maswali hapa twende mimi na wewe tukakae pale tufuatilie hiyo x-ray na tuweke utaratibu iweze kufika mapema inapotakiwa, ahsante sana.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; nafahamu kwamba utaratibu wa kuomba fedha kwa awamu ya kwanza ya ukarabati umeshakamilika. Swali langu langu kwa Serikali: Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili ukarabati uanze?

Swali la pili: Je, Serikali ina mpango gani wa ziada kuhakikisha kwamba ukarabati wa majengo haya chakavu ya Milembe unakamilika katika awamu hii na awamu ijayo ya mwaka wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O MOLLEL): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Mbunge, ni kweli kwamba kuna utaratibu ambao tayari umefanyika, lakini wakati utaratibu huo umefanyika imeonekana kwamba kwa kweli unahitajika ukarabati mkubwa sana na vile vile baadhi ya majengo kubomolewa na kujengwa upya, kwa hiyo, ikahitajika kufanyika tathmini kwa sababu fedha nyingi zitahitajika zaidi.

Mheshimiwa Spika, mara tu baada ya huu upembuzi kufanyika, kwanza kazi ambayo ilikuwa inaendelea itaendelea kufanyika, lakini tunahitaji ifanyike kazi kubwa zaidi kwa maana ya kuingia kwenye bajeti ya mwaka kesho 2022 ili ujenzi mkubwa ufanyike na ukitambua kwamba pale Mirembe inaenda kuwa taasisi kamili, sasa iko kwenye wakati wa kuunda muundo. Maa yake kutakuwa na ongezeko la kibajeti na wataweza sasa kuandika proposal zao binafsi ili kufanya research na pengine ile taasisi kuwa kubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Ahsante.
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Sisi Kusini nadhani magonjwa haya kwa sababu ya korosho hayapo.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya aliwahi kutembelea kusini. Katika ziara yake, tulimpa maombi ya kusaidiwa kukarabati kituo cha afya kikongwe kuliko vyote katika Jimbo la Mtama ambacho kinahudumia zaidi ya kata sita na ahadi hiyo ilitolewa. Sasa nataka kujua ni lini tutapata fedha ili tusaidie kuboresha huduma katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Nape, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kama ambavyo amesema tulikwenda na vilevile baada ya hapo aliandika barua kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya na Mheshimiwa Waziri wa Afya aliwasiliana na TAMISEMI. Nataka kumhakikishia kwamba kituo hicho kimeingizwa kwenye bajeti na kimetengewa shilingi milioni 500 na baada ya fedha kupatikana kazi itaanza. Nami baada ya kumaliza Bunge, twende pamoja ili tusisitize na mambo mengine ambayo tuliyapanga wakati ule kuyafanya. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Ni kweli Hospitali hiyo ya kanda imeanza kutoa huduma, lakini lengo la Hospitali ya Kanda ni kutoa huduma za rufaa. Huduma hizo hazijaanza kwa sababu hakuna vifaa na hakuna madaktari bingwa. Sasa swali langu: Ni lini vifaa na madaktari bingwa wataletwa katika hospitali hiyo kwa sababu hiyo ndiyo shida yetu sisi watu wa kusini hususan Mkoa wa Mtwara? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Ukiangalia mazingira ya nje ya hospitali ile, bado yapo shaghalabaghala, ni lini yatawekwa katika mandhari ambayo inaendana na mandhari ya hospitali? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri sana; na kweli mawazo mazuri aliyoyatoa ndiyo mwelekeo wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwanza hospitali hiyo imeanza na ni kweli bado watumishi hawajafikia idadi aliyoisema. Tumegawa uanziswaji wa hiyo hospitali. Ukiangalia hospitali yenyewe sasa ina umri wa mwezi mmoja na siku nane, lakini tumegawa uanzishwaji wake kwa phase tatu, maana yake tumeanza phase ya pili ambayo sasa wanaenda kuwekwa watumishi.

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya hospotali hiyo na tayari shilingi bilioni tatu zimeingia kwa ajili ya kununua CT-Scan na MRA. Kuna specialist mmoja na mwezi ujao wanapelekwa 4 ili wafikie 5. Mpaka mwezi wa Pili ambapo tutaenda kwenye Phase ya tatu ya uanzishwaji wa hospitali, tutakuwa na watumishi 217. Kwa hiyo, Mheshimiwa ukitembelea mwazi wa tatu utakuta imeanza kama ulivyotaka wewe.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kuhusu mazingira ya Hospitali. Kweli nimeyaona na mimi wakati jiwe la msingi linawekwa, bado mazingira yaliyozunguka siyo safi. Wakati tunaendela kwenye phase hizi, tunaendelea kuhakikisha vile vile na usafi unafanywa.

Mheshimiwa Spika, OC imetengewa shilingi milioni 600. Kwa hiyo, watatumia kwa ajili ya kuhakikisha mambo mengine yanakuwa sawa na kufikia lengo ambalo Wana- Mtwara wangetegemea kuona.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Spika nashukuru. Nami napenda kuiuliza Serikali: Ni lini itaimarisha utoaji wa huduma kwa magonjwa yale ambayo yalikuwa hayapewi kipaombele; magonjwa ya kitropiki, kwa maana ya neglected tropic diseases kwenye hospitali hii ya Kanda ya Kusini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, kwanza ukisikia tunaanzisha specialists mbalimbali, tunazungumzia magonjwa yote hayo. Ukisikia tunasema tunaongeza watumishi, ni kwa kuzingatia hayo. Ndiyo maanda unaona sasa kuzunguka nchi nzima, utaona kila Mkoa sasa unafanya wahamasa kuhusu magonjwa ambayo ameyazungumzia. Juzi Arusha nilimwakilisha Waziri wa Afya kwenye kuzindua swala hilo kitaifa. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimwulize maswali mawili madogo ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amezingatia eneo moja tu la uchimbaji wa dhahabu: Je, Serikali ina mpango gani wa kubadili matumizi ya zebaki inayotumika katika vifaa vya afya ikiwemo katika ujazaji wa jino?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Je, zebaki inayotumika katika huduma za afya kama vile kipima joto kwa maana ya thermometer ama wakati wa kujaza jino kwa maana ya amalgam, ina athari gani zinapotumiwa na binadamu; na je, athari hizo zinapatikana baada ya muda gani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili mazuri ya Mheshimiwa Mbunge mwenzangu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, matumizi ya vitu vyenye mercury kwenye kutibu meno; moja, kwa mercury ipo dozi maalum ambayo kuna mahali inapofikia ndiyo inaweza kuleta athari. Hata hivyo ni kweli kwamba kuna baadhi ya watu wakizibwa meno kwa kutumia amalgam hiyo yenye mercury, wengine wanapata allergy.

Kwa hiyo, wakati mwingine watu wanaweza wakafikiri ni madhara ya mercury, lakini ni allergy kwa sababu kuna watu wenye allergy na baadhi ya mambo. Mpaka sasa, kwa kutibu meno, inatumika na haijaonesha madhara ambayo unadhani yanatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna options mbalimbali za kutumia na utafiti unaendelea kuona namna ya kupata kitu chenye strength ile ile ambayo amalgam ilikuwa inafanya ili waweze kuitoa, lakini kwa kweli mpaka sasa kitiba haina shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, amezungumzia thermometer na vifaa vingine vya tiba ambavyo vina mercury, tunafanyaje? Kikubwa ambacho mpaka sasa hata kwenye madini kinafanyika, kwenye vifaa vyote vya tiba na hata dawa, suala kubwa hapa, ni kwa namna gani unafanya disposing na control mechanism zinavyohaibika na zile thermometer unazi-dispose kwa namna gani? Ndiyo maana kuna utaratibu maalum wa namna ya ku-dispose vifaa tiba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea na utaratibu wa kuhakikisha thermometer na vifaa vingine vyote vinavyotumia mercury vinakuwa under control na vikiharibika ile disposing mechanism inafuatwa ili kutunza mazingira na kutunza afya ya binadamu. Ahsante. (Makofi)
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matumizi ya zebaki, hasa Kanda ya Ziwa, sehemu ambazo wanachimba madini imekuwa ikisababisha ongezeko la wagonjwa wa Kansa ya Shingo ya Uzazi: Je, Serikali imeshafanya utafiti kuthibitisha kwamba zebaki ndiyo chanzo cha ongezeko la magonjwa ya kansa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba hata ukienda Ocean Road imeonekana kwamba wagonjwa wengi wenye matatizo ya kansa wanatokea Kanda ya Ziwa. Hayati Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli aliwahi kuagiza ufanyike utafiti ambao bado majibu yake hayajaja ili kuthibitisha nini hasa chanzo cha tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachofanyika kwa sasa ni kwamba kwanza kuna sababu nyingi ambazo zinasababisha kansa ya kizazi. Kwa hiyo, hatuwezi kusema specifically ni hilo. Kikubwa, tunashirikina na Wizara ya Madini kupitia taasisi yake kuhakikisha sasa wanapochenjua madini, wale wachimbaji wadogo na wakubwa kunakuwepo na control ya kutosha kuhakikisha kwamba haiendi kwenye mazingira na vilevile haiendi kufika maeneo ambayo binadamu wanatumia maji na vitu vingine. Hilo ndiyo tunaendelea nalo kwa sasa.
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza maswali yangu ya nyongeza, siafiki takwimu za Serikali kwa sababu Covid ilisambaa nchi nzima na kwa watu 725 ukigawanya tu kwa mikoa 31 maana yake kila mkoa wamekufa watu 23 ambayo haina mantiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kama nchi tulisimamisha mwaka mzima, Machi, 2020 mpaka Machi, 2021 kutoa takwimu. Kwa hiyo, hizi taarifa za takwimu siyo za ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa maswali yangu ya nyongeza mawili; la kwanza, moja kati ya changamoto kubwa ilikuwa ni upimaji, kwa sababu ilikuwa lazima upime ndiyo ujue huyu mtu amekufa na Covid ama hajafa na Covid; sasa Mheshimiwa Waziri ameeleza vizuri sana juu ya mkopo wa shilingi bilioni 466 toka IMF, lakini hivi vitu alivyoviainisha hapa hakuna hata sentensi moja inayozungumzia ujenzi wa maabara ama uwepo wa maabara kwa ajili ya kupima Covid ama virusi vingine vinavyoashiria ama vinavyofanania na hivyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka aniambie, kwa sababu tunaishi na Covid-19 na virusi vinavyofanania na hivyo vitakuja, ni fedha kiasi gani katika mkopo huu wa shilingi bilioni 466 tutapeleka kwenye eneo la maabara specifically; na siyo hizi maabara sijui X-Ray, hizo zinatoa viashiria tu, kwamba kuna homa ya mapafu? Hilo ni la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na dawa, nili-intend hapa kuuliza, tiba za asili za Tanzania kwa kiwango kikubwa sana zimechangia kutibu madhara yanayotokana na Covid. Imesaidia sana; na hizi ni fursa kwa watu wa tiba za asili kwa nchi, kwa ukanda na dunia: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka Serikali iniambie, mpaka sasa, kwa sababu kila siku mnajibu mnafanya tafiti, mmeshagundua ni tiba gani za asili ambazo ni sahihi kwa Watanzania watakaopata maradhi ama Virusi vya Covid ili wakiugua tujue protocol ya matibabu ni hii; na siyo sasa hivi kila mtu anakunywa kivyake mpaka tunakunywa sumu? Ni lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie tu rafiki yangu kwamba hii ni sayansi. Kama ni sayansi, inahitaji akili kubwa kuweza kuyaona hayo na siyo hisia za kwenye ma-corridor. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie tu kwamba Bugando, Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia amepeleka vifaa vya maabara vya kupima Corona vyenye thamani ya shilingi bilioni nne na mlinisikia nikisema. Kibong’oto ambayo ndiyo taasisi yetu ya magonjwa ambukizi, imepelekewa vifaa vyenye thamani ya shilingi bilioni sita na maabara inajengwa kwa thamani ya shilingi bilioni 14. Maabara yetu ya Taifa nayo inayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujue virus siyo mdudu mpya. Ni mdudu mpya kwenye genetic makeup lakini sayansi ni ile ile. Kwa hiyo, maabara ni zile zile, mashine ndiyo zimetofautiana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kuhusu tiba ya asili. Kwanza hatujaacha tiba ya asili. Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ametoa shilingi bilioni 1.2 imeenda NIMR kwa ajili ya kuchakata dawa zetu zilizoonekana kwamba zinatusaidia na kuziweka vizuri. Vilevile kwenye fedha hizi ambazo nilikuwa nazitaja, shilingi bilioni 466, imetengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya utafiti ule mkubwa na mgumu kwa ajili ya kuja na chanjo yetu ya Kitanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa ninachoweza kumwambia Mheshimiwa, haya ya kisayansi huwa ni magumu, nawaachia wanasayansi. Unahitaji super computing system kubwa kuziona; hii siyo ngwini yaani, unajua. Kwa hiyo tulia. (Makofi)
MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami pamoja na majibu mazuri kabisa ya Daktari msomi, mwanasayansi Mheshimiwa Mollel, nina swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huko nyuma tulikuwa tunaona Serikali ikishiriki katika kampeni mbalimbali tunapokuwa na magonjwa haya ya mlipuko na magonjwa mengine. Kwa mfano tuliwahi kuwa na kampeni ya kutokomeza Malaria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu, ni upi mpango wa Serikali kutumia wasanii wetu katika kuhamasisha, lakini pia kutoa elimu zaidi kwa wananchi hasa makundi ya vijana katika kupambana na Ugonjwa huu wa Uviko-19? Kwa sababu tunaona katika awamu hii kama wasanii hawajatumika sana katika eneo hili? Ni upi mpango wa Serikali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mbunge ni muhimu sana; na kweli kwa kutumia wasanii wanaweza wakatufikishia vizuri sana ujumbe, lakini kikubwa ambacho kinaendelea sasa hivi ni kuhakikisha kwamba badala ya kutumia wasanii kutoka juu, tunapeleka kabisa huduma iende ikafanyike na jamii yenyewe kule chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, imeonekana kwamba, ukiangalia fedha tulizonazo, ukitumia sana wasanii hawa wakubwa, ambao bado tunaendelea kuwatumia na tutawatumia jinsi watakapohitajika, lakini kwa kupeleka kule chini huduma inafika kwa urahisi zaidi kwa lugha inayoeleweka na watu wa jamii iliyoko eneo husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana tumesema tutakwenda kule na tukifika kule Umasaini tutawatumia wasanii walioko kule, lakini tutatumia redio na lugha zilizoko kule ili waweze kupata kirahisi na ili ujumbe ufike. Ila hatuna lengo la kuwaacha wasanii, isipokuwa tunatafuta namna ya kutumia hela kidogo kwa kufanya kazi kubwa zaidi. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wakati Mheshimiwa Waziri anajibu maswali ya nyongeza, alisema wamefanikiwa kupeleka vifaa vya maabara kwenye maeneo mawili. Nchi yetu ukichanganya na Zanzibar ina mikoa 31, kwa Bara ni 26: Je, hamwoni kwamba hiki ni kikazi kiduchu kwa tatizo kubwa ambalo limetukumba la Covid? Ni lini mtahakikisha hizo maabara zinakuwepo nchi nzima na siyo hizi mbili ambazo zimetokana na pesa ya mkopo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo niliyoyasema ni mifano tu. Nataka nimweleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba toka Uhuru tumekuwa na CT- Scan mbili tu kwenye nchi hii, kwenye hospitali za mikoa mbili tu, lakini amekuja leo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kupata 29 ambazo zina gharama kubwa kuliko mashine za kupima Corona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka tu kumhakikishia ni kwamba tuna uwezo huo, mpaka leo tunapoongea hivi Mount Meru Hospital wanapima, Mbeya wanapima, kila mahali tutafikiwa. Kwa hiyo, usiogope, kazi inapigwa. Sisi tuendelee kusherehekea, karibuni upande huu kumenoga. (Kicheko/Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu ya Serikali yaliyotolewa hapa, bado kuna tatizo kubwa, hasa kwenye vituo vyetu vya afya, huduma hii imekuwa ngumu sana kwani akinamama wanapokwenda kujifungua wameendelea kutozwa hela na watoto chini ya miaka mitano wanapokwenda pia kupata huduma wameendelea kutozwa fedha. Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ni nini hasa kinakwamisha huduma hii au sera hii isitekelezwe?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika vituo vyetu vya afya kumekuwa na upungufu mkubwa sana wa dawa na vifaa tiba. Je, Serikali ina mkakati gani sasa kuhakikisha kwamba vifaa tiba na dawa zinapatikana katika vituo vyetu vya afya ili watoto wetu na akinamama wanapokwenda kujifungua waweze kupata huduma hiyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, nilijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Regina Ndege kwamba kwa kweli tumeshafanya uchunguzi wa kutosha na kujua kwamba tatizo hilo lipo, ndiyo maana straight forward tumetaka kuwaelekeza wanaohusika kufanya kazi yao. Hata kwenye presentation ya semina iliyofanywa jana kwa Wabunge wote na Wizara ya Afya tulionesha kwamba exemption ile ya akinamama na watoto inachukua asilimia 0.1 mpaka 10.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo maeneo ambayo ni 0.1 ni maeneo yale ambayo kwa kweli unakuta akinamama walitakiwa kupewa hiyo huduma bure na hawapewi; tutakwenda kuboresha kwa nguvu kuhakikisha kwamba huduma inapatikana. Ndiyo maana tumeleta vilevile kwenu ili tushirikiane kwa pamoja ili kuweza kutatua tatizo hilo.

La pili, kwenye eneo la dawa; kwenye eneo hili, Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan alishatoa bilioni 16 na najua Kamati inakwenda siku ya Jumapili, kimejengwa kiwanda kule Njombe ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha vidonge vyote vya kutosha nchi nzima kwa siku mbili tu na kimeshafika asilimia 98 kukamilika.

Mheshimiwa Spika, tayari Rais wetu, mama Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya bilioni 185 kwa ajili ya kununua dawa. Tukijumlisha na uelewa ambao jana tulipeana Wabunge wa kusimamia upotevu wa dawa, wanaweza kuona tuna items zaidi ya 400 za dawa, lakini tumechunguza tu items 20 ndani ya mwaka mmoja kuna upotevu wa bilioni 83. Maana yake tukishirikiana kwa pamoja sisi na viongozi tuliotaja hapa huko mbele tutaweza kufika hatua nzuri na dawa zikapatikana kwenye maeneo yetu. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nami niulize swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi; hii sera ni ya muda mrefu na haitekelezeki. Wabunge mnajua kwenye majimbo yetu, akinamama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano hakuna matibabu bure. Sasa Mheshimiwa Waziri anasema atatoa miongozo, kama hakuna kitu cha kumbana mambo ni yaleyale.

Je, kwa nini kusiwe na sheria kwamba ni lazima akinamama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee wapate matibabu bure ili wazee wasiweke tiba ya kisaikolojia tena, wakienda hospitali wapate matibabu bure? Sera imekuwepo haitekelezeki, leteni sheria kama mna dhamira njema.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge na ndiyo maana umekuwa mkali sana kwenye suala zima la bima ya afya kwa wote. Nataka kukuhakikishia tukienda kutekeleza agizo lako la suala la bima ya afya kwa wote, haya mambo yatakuwa ni historia. Kwa wakati huu miongozo iliyopo tutaendelea kuifuatilia na kusisitiza, lakini Mheshimiwa Ester Bulaya aendelee kushirikiana na sisi ili tuweze kufanya hilo litekelezeke. Ahsante sana. (Makofi)