Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Dr. Godwin Oloyce Mollel (25 total)

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatoa bila malipo huduma za uzazi wa mpango na za afya kwa Wajawazito na Watoto chini ya umri wa miaka mitano kama Sera ya Afya inavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ni mara ya kwanza kusimama hapa mbele, nitumie fursa hii kumshukuru Mungu, kushukuru Chama changu, kumshukuru Rais wetu kwa kutupa nafasi hii. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Siha kwa kuendelea kuniamini lakini nimshukuru mke wangu kwa kuendelea kunipa ushirikiano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Sera ya Afya ya mwaka 2007, ukurasa wa 19, kifungu 5.3.4 ambacho kinahusu Afya ya mama na mtoto na Tamko la Sera Kipengele (c) Sehemu ya (i), inaelekeza huduma bila malipo kwa Huduma za Afya ya Uzazi na Watoto chini ya miaka mitano. Baadhi ya maeneo wamekuwa wakifanya kinyume na tamko la kisera na hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa pale wananchi wanapotoa taarifa. Katika kipindi cha mwaka 2015-2020, Serikali ilitoa huduma kwa wenye uhitaji bila malipo likiwemo kundi hili zenye thamani ya bilioni 880.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hayo, Wizara inawaagiza Waganga Wakuu na Mikoa na Wilaya ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa sera na miongozo ya afya katika ngazi ya mkoa na halmashauri kutimiza kikamilifu majukumu yao kwa kushughulikia haraka kero na malalamiko ya wananchi pia utekelezaji wa suala hili ambalo siyo tu ni tamko la kisera lakini pia ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambacho ndicho chama kilichounda Serikali. Ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-

Je, ni kwa nini dawa za shinikizo la damu hazitolewi katika ngazi ya zahanati na vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma,Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, dawa za kutibu shinikizo la damu zimegawanyika katika makundi kulingana na namna zinavyofanya kazi na athari zake,hivyo basi utoaji wake unazingatia utaalam na uwezo wa kitaaluma, ndiyo maana kuna dawa hutolewa katika ngazi za Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya, Hospitali za Rufaa na Hospitali ya Taifa.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha ushauri mzuri wa Mheshimiwa Mbunge unatekelezeka, Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli imepeleka wataalam wengi wenye shahada ya udaktari mpaka ngazi ya kituo cha afya kwa lengo la kuhakikisha huduma nyingi na bora kama ulivyoshauriwa na Mheshimiwa Mbunge zinapatikana kuanzia ngazi ya chini na pia dawa hizi zimehusishwa katika mwongozo mpya wa matibabu nchini ili ziweze kutumika mpaka ngazi ya kituo cha afya na zahanati.
MHE. LUCY T. MAYENGA (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) Aliuliza: -

Nchi yetu imekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa Afya ya Akili: -

(a) Je, nini chanzo cha ugonjwa huo?

(b) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wagonjwa hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, afya ya akili ni ile hali ya mtu kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwemo utambuzi, uzalishaji wa mali, kutunza familia na kumudu shughuli za kijamii. Magonjwa ya akili ni pale mtu anaposhindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwa ni pamoja na kushindwa kumudu shughuli za kijamii, kujitunza, hisia na utambuzi ambapo sababu za magonjwa haya ni mchanganyiko wa sababu za kibaiolojia, kisaikolojia na kimazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa haya, Serikali imefanya yafuatayo: -

(1) Kuandaa Sheria ya Afya ya Akili ya Mwaka 2008 ambapo sheria hii inatoa mwongozo na utaratibu wa namna ya kuwapokea na kuwahudumia watu wenye ugonjwa wa akili.

(2) Kuandaa Sera na miongozo ambapo wagonjwa wa afya ya akili ni miongoni mwa makundi maalum ambayo huduma zake zinaweza kutolewa kwa msamaha kwa watu ambao hawana uwezo.

(3) Serikali inahakikisha kuwa huduma hizi zinatolewa katika ngazi zote za huduma za afya kuanzia kwenye jamii, ngazi ya afya ya msingi, mkoa, kanda, mpaka hospitali maalum ya Taifa ya afya ya akili.

(4) Kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu za afya ya akili kwenye vituo vyote vya huduma za afya.

(5) Kuongeza udahili wa wanafunzi wa uzamivu (Masters) katika masomo ya wagonjwa wa akili.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI Aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Mkoa wa Iringa mashine ya CT-Scan?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Kabati, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa uwepo wa huduma za kibingwa za vipimo vya mionzi kwa kutumia CT-Scan. Katika kuzingatia umuhimu huu tayari ilishakamilisha kufunga mashine hizi kwenye Hospitali za Kibingwa Taifa, kanda na Hospitali mbili za Rufaa za Mikoa zilipata mashine hizi mnamo Desemba, 2020 ambazo ni Mwananyamala na Sekou Toure.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa zoezi hili ni endelevu, Serikali inaendelea kuziwezesha hospitali zingine zote za Rufaa za Mikoa ikiwemo Iringa kufunga mashine hizi kwa kadri ya upatikanaji wa rasilimali fedha za utekelezaji wa mpango huu.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa wodi ya wazazi utaanza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christina Christopher, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga ni miongoni mwa Hospitali za Rufaa za Mikoa zinazoboreshwa. Napenda kumjulisha Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba Mshauri Elekezi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi ameshapatikana, ambaye ni Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Aidha, hatua inayoendelea hivi sasa, ni mchakato wa zabuni ya kupata mkandarasi atakayefanya kazi ya ujenzi, ambapo ujenzi huo unategemewa kuanza mwezi Machi, 2021. Mradi huu utatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani.
MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA Aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo la hospitali ambazo zinaendelea kutoza fedha akinamama wanaojifungua kwa njia ya kawaida?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Adamson Mwakasaka kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Sera ya Afya ya mwaka 2007, Ukurasa wa 19, kifungu 5.3.4 ambacho kinahusu afya ya mama na mtoto na Tamko la Sera Kipengele (c) Sehemu ya (i), inaelekeza kuhusu huduma bila malipo kwa Huduma za Afya ya Uzazi na Watoto chini ya miaka mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2015 - 2020 Serikali ilitoa huduma kwa wenye uhitaji bila malipo likiwemo kundi hili, zenye thamani ya shilingi takriban bilioni 880. Hivyo, Wizara inasisitiza watoa huduma wote kuzingatia utekelezaji wa tamko hili la kisera.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie fursa hii kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa tayari Wizara imewaelekeza na kuwataka Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri ambao ndio wasimamizi wakuu wa utekelezaji wa Sera na Miongozo ya Afya katika ngazi ya Mikoa na Halmashauri kutimiza kikamilifu majukumu yao kwa kushughulikia haraka kero na malalamiko ya wananchi ikiwemo vituo vya kutolea huduma za afya kuacha kuwatoza fedha wajawazito na watoto wanapofika kituoni kupata huduma.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH Aliuliza: -

Pamoja na jitihada zinazofanywa na Serikali za kupambana na ugonjwa wa Malaria, bado ugonjwa huo unaendelea kuwaathiri wananchi wakiwemo watoto: -

Je, Serikali inaweza kutuambia hatua zilizofikiwa za kutokomeza ugonjwa huo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitekeleza afua na kazi mbalimbali za kudhibiti ugonjwa wa malaria nchini na kufanikiwa kupunguza kiwango cha maambukizi ya Malaria kutoka zaidi ya asilimia 40 mwanzoni mwa miaka ya 2000 mpaka asilimia 7.5 mwaka 2017.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara inatekeleza Mpango Mkakati wa Malaria (National Malaria Strategic Plan 2021 – 2025) ambao umeweka malengo ya kupunguza kiwango cha Malaria kutoka asilimia 7.5 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025. Lengo mahususi ni kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria ifikapo 2030.
MHE. MWANTUMU M. ZODO Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukabiliana na upungufu wa Watumishi wapatao 16,000 kwenye Sekta ya Afya nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Mzamili Zodo, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Tanga, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto ya upungufu wa watumishi katika sekta ya afya ambayo kwa kiasi kikubwa hivi sasa imetokana na mahitaji mapya yanayotokana na ujenzi na upanuzi wa hospitali za rufaa za kanda, mikoa, ujenzi wa hospitali za Halmashauri, ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto ya uhaba wa watumishi ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita 2015 hadi 2020 Serikali iliajiri watumishi wapatao 14,479 na zaidi ya watumishi 565 walipatiwa ajira za mkataba kwa kugharamiwa na makusanyo ya vituo vya kutolea huduma za afya. Pia katika mwaka wa fedha 2020/2021 sekta ya afya inatarajia kuajiri jumla ya watumishi wapya 12,476.
MHE. MARIAM M. NYOKA Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuifanyia ukarabati mkubwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa ni ya muda mrefu na majengo yake yamechakaa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariamu Madalu Nyoka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ukarabati wa majengo chakavu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kwa kubomoa majengo chakavu manne; jengo la Masjala ya zamani, choo cha nje cha wagonjwa, jengo la viungo bandia na jengo la zamani la huduma za kifua kikuu, kwa ajili ya kujenga jengo la kisasa la wagonjwa wa dharura ambalo limefikia asilimia 95. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi 630,340,507.00, ambapo hadi sasa fedha hiyo imetolewa yote. Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba, 2021. Ahsante.
MHE. JANETH E. MAHAWANGA aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wajasiriamali wadogo kupata Bima ya afya kupitia utaratibu wa vikundi ambao ulikuwa msaada mkubwa sana kwenye jamii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janeth Elias Mahawanga, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya inatoa kitita mahususi cha mafao kwa makundi maalum ya wajasiriamali ambao wamejirasimisha shughuli zao kupitia mwamvuli wa jumuiya au vyama vyao vilivyorasimishwa.

Mheshimiwa Spika, makundi ya wajasirimali yanayonufaika na utaratibu wa bima ya afya ni pamoja na makundi ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika 225 vyenye idadi ya wanachama 6,196; vikundi 17 vya umoja wa wamachinga; wajasiriamali wadogo; wachimbaji wa madini; wavuvi; na mamalishe ambavyo vina idadi ya wanachama 2,315; na vikundi vya umoja wa madereva bodaboda, malori na daladala ambavyo vina idadi ya wanachama 303.

Mheshimiwa Spika, kwa makundi ya wananchi ambao ni wajasiriamali lakini hawamo katika mwamvuli wa jumuiya za wajasiriamali zilizorasimishwa, Mfuko umeanzisha vifurushi vya bima ya afya vya hiari ambavyo vinazingatia umri, ukubwa wa familia, aina ya huduma na gharama halisi za matibabu nchini ambapo hadi tarehe 31 Machi, 2021 wanachama 32,343 wameshajiunga na mpango huu.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya kwa jamii na kwa kutambua matatizo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameainisha na Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiyaainisha, Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambayo itawasilishwa Bungeni mwezi Juni, 2021.
MHE. MARTHA N. GWAU aliuliza:-

Je, ni kiasi gani cha Zebaki kinaingizwa nchini kila Mwaka?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martha Nehemia Gwau, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka 2019 kiasi cha Zebaki kilichoingizwa nchini kilikuwa ni tani 24.42, ambapo mwaka 2020 kilikuwa ni tani 22.

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba zebaki ni kemikali inayotakiwa kudhibitiwa kwasababu ina madhara ya afya ya binadamu kama vile kusababisha upofu, kutetemeka viungo, kupoteza kumbukumbu, kuharibika ngozi, tatizo la ini na figo.

Mheshimiwa Spika, hivyo basi Serikali, kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeendelea kuchukua hatua za kudhibiti uingizaji wa Zebaki kwa kuwasajili wale wanaoingiza Zebaki nchini na kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka sheria.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza:-

Je, lini Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Mawenzi litakamilika na kuanza kutoa huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbuge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto ambalo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha dhilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 3.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya vifaa na vifaatiba. Aidha, huduma zitaanza kutolewa baada ya kukamilika kwa ujenzi na ukamilishaji usimikaji wa vifaa ifikapo Januari, 2022.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo vya binadamu kama vile figo na moyo kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa zimeanza kutoa huduma ya uvunaji na upandikizwaji wa figo nchini tangu mwezi Novemba, 2017 kutoka kwa wachangiaji walioridhia. Hadi sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza figo 62 na Hospitali ya Benjamin Mkapa imepandikiza figo 18. Aidha, kwa upande wa upandikizaji wa moyo, Serikali inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya upandikizaji wa viungo nchini kama ambavyo Mbunge ameainisha, Serikali imeandaa Muswada wa Kutunga Sheria itakayoongoza taratibu za uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa viungo ambayo ipo kwenye hatua ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau. Hata hivyo, kwa kuwa huduma zimeanza kutolewa, kwa sasa nchi inatumia miongozo ya kimataifa inayosimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo.
MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE aliuliza:-

Mwaka 2018 KFW Germany walisitisha udhamini kwa huduma za Afya kwa Mama na Mtoto Mkoani Tanga: -

(a) Je, ni juhudi gani zimefanyika kuhakikisha Mdhamini huyo anaendelea na udhamini wake Mkoani Tanga?

(b) Je, Serikali ina mpango gani kupata Mdhamini mwingine?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Eng. Mwanaisha Ng’anzi Ulenge, Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya KFW ilianzisha mpango wa Bima ya Afya kwa akinamama wajawazito na watoto. Mpango huo ulitekelezwa kwa makubaliano ya kipindi maalum toka 2012 hadi 2018. Mpango huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa dhana na umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali inakamilisha Rasimu ya Muswada wa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ambao utawasilishwa Bungeni mwezi Juni 2021, swali la Mheshimiwa Mbunge lenye kipengele (a) na (b) litaenda kupata suluhisho. Hata hivyo, Serikali inaendelea kuwahamasisha wadau mbalimbali katika kuchangia miradi ya Sekta ya Afya, ikiwemo Bima ya Afya kwa Wote.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa Katavi kwani ujenzi huo unakwenda kwa kusuasua?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi ambapo kwa sasa ujenzi umekamilika kwa wastani wa asilimia 70. Ujenzi kwa upande wa maabara umefikia asilimia 98 na jengo kuu la hospitali umefikia asilimia 42. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.82 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.97 kimetolewa na kutumika.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha wa 2021/2022, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 57 kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali za Rufaa za Mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 5.85 zitatumika kukamilisha ujenzi huu ifikapo Januari 2022.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa Hospitali ya Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa hospitali ya Mkoa wa Katavi umekamilika kwa wastani wa asilimia 70, ambapo ujenzi kwa upande wa maabara umefikia asilimia 98 na jengo kuu la hospitali umefikia asilimia 42. Mradi huu unagharimu jumla ya shilingi bilioni 9.82 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 3.97 zimetumika na bilioni 5.85 zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2021/2022 na zitatumika kukamilisha ujenzi huu ifikapo Januari, 2022. Ahsante.
MHE. PRISCUS J. TARIMO aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali wa kukamilisha Mradi wa Jengo la Mama na Mtoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambao umeanza tangu mwaka 2008/2009 bila kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa niaba ya Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Priscus Jacob Tarimo, Mbunge wa Moshi Mjini kama ifuatavyo;-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo la kuwahudumia mama na mtoto katika Hospitali ya Mawenzi umekamilika kwa asilimia 70. Mradi huo unagharimu jumla ya shilingi bilioni 10.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi bilioni 5.3 kimetolewa na kutumika.

Aidha, kiasi cha shilingi bilioni 5.2 kimetengwa kwa mwaka 2021/2022 ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 3.6 zitatumika kukamilisha ujenzi na kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kitatumika kununulia vifaa tiba na ujenzi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo Januari, 2022.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaandaa utaratibu mzuri wa matibabu kwa watu wenye ulemavu wakati ikisubiri Bima ya Afya kwa wote?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL). alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeweka utaratibu wa kuwatambua watu wenye ulemavu kupitia Kamati za Watu Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya kijiji na kuwaunganisha kwenye vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kulingana na mahitaji yao. Aidha, kupitia mipango kabambe ya afya ya halmashauri Serikali imeendelea kuwatengea rasilimali kulingana na mahitaji yao. Mfano kwa walemavu wa ngozi wanawezeshwa mafuta ya kuzuia jua (Sun Cream) ambayo kwa sasa hutengenezwa katika Hospitali ya Kanda ya KCMC, na bidhaa hii imeingizwa kwenye orodha ya bidhaa za afya zinazosambazwa na Bohari ya Dawa (MSD).

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetoa miongozo ya miundombinu ya kutolea huduma kwa kuzingatia haki za watu wenye ulemavu. Pia, Wizara imeendelea kutengeneza miongozo na mafunzo kwa watoa huduma ili kuwezesha na kuboresha utoaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mswada wa Bima ya Afya kwa Wote unakuja, hii ni fursa muhimu sana kwa sisi Wabunge kutengeneza sheria nzuri zitakazolinda haki za watu wenye ulemavu. Ahsante.
MHE. SHAMSIA A. MTAMBA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia wazee hasa wa vijijini bima ya afya ikiwemo ya CHF inayotolewa na Halmashauri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shamsia Azizi Mtamba, Mbunge wa Mtwara Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, huduma za tiba ni haki ya msingi ya wazee wote. Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa matibabu hususan kwa wazee wasiojiweza nchini kwa kuanzisha madirisha kwa ajili ya matibabu kwa wazee. Serikali imeendelea na zoezi la utambuzi wa wazee na kuwapatia vitambulisho vya matibabu. Hadi kufikia Machi, 2021 jumla ya wazee 2,344,747 wametambuliwa sawa na asilimia 87 ya makadirio ya wazee wote nchini. Kati yao wanaume ni 1,092,310 na wanawake ni 1,252,437. Aidha, wazee wasio na uwezo 1,087,008 na wamepatiwa vitambulisho vya matibabu bure na wazee 856,052 wamepatiwa kadi za matibabu za Afya ya Jamii yaani CHF.

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na kukamilisha rasimu ya Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ili kuwezesha wananchi wote wakiwemo wazee kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha kwa mfumo rasmi na ulio mzuri zaidi. Ahsante.
MHE. HASSAN S. MTENGA aliuliza: -

Majengo mengi katika Hospitali ya Mkoa wa Mtwara yamechakaa; je, ni lini Serikali itaanza ukarabati wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Hassan Seleman Mtenga, Mbunge wa Mtwara mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara - Ligula ni moja kati ya Hospitali za muda mrefu hapa nchini ambazo miundombinu yake imechakaa sana. Katika jitihada za kuboresha miundombinu ya Hospitali hiyo, kwenye bajeti ya 2020/2021 kiasi cha shilingi milioni 201 kimetolewa kwa ajili ya ukamilishwaji wa jengo la kuhifadhia maiti ambalo ujenzi wake umekamilika na vifaa vimenunuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha shilingi bilioni moja kimetengwa kwa ajili ya ukarabati wa Majengo ya Wagonjwa wa Nje (OPD), wodi za wanaume na wanawake, upasuaji, wodi ya uangalizi maalum na kichomea taka. Ukarabati huo unatarajiwa kukamilika Machi, 2022. Ahsante.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Hospitali ya Wagonjwa wa Afya ya Akili ya Mirembe ambayo Miundombinu yake imeharibika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alice Karungi Kaijage, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kumtumia Wakala wa Majengo (TBA) imeanza upembuzi yakinifu wa majengo yatakayofanyiwa ukarabati pamoja na yale yatakayobomolewa na kujengwa upya. Aidha, kupitia upembuzi huo Serikali itabaini gharama halisi za ujenzi na
ukarabati wa Hospitali hiyo. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba, 2021.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -

Je, ni lini Hospitali ya Kanda ya Kusini itaanza kutoa Huduma kwa Wananchi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Mlapo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Kanda ya Kusini Mtwara imewekewa jiwe la msingi tarehe 26/07/2021 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango na huduma zimeanza tarehe 1 Oktoba, 2021. Ahsante.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta teknolojia mbadala ili kunusuru afya za wananchi wanaotumia zebaki kwa matumizi mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na taasisi zake, ipo kwenye mpango wa kutafuta teknolojia mbadala na tayari vikao vya pamoja na taasisi zinazohusika na uchimbaji wa dhahabu vinafanyika ili kupata teknolojia isiyohitaji zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu na hivyo kuondoa athari za kiafya kwa jamii na mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa elimu juu ya matumizi sahihi, kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa katika siku za usoni matumizi ya zebaki ni dhamira ya Serikali katika kulinda afya ya jamii na mazingira. Ahsante.
MHE. HALIMA J. MDEE aliuliza: -

(a) Je, tangu janga la Corona lianze ni Watanzania wangapi wamepata maambukizi; wangapi wamekufa; na wangapi wamepona?

(b) Je, ni fedha kiasi gani zimetengwa na Serikali na zimefanya nini na wapi katika kukabiliana na janga hili?

(c) Je, nini kinapelekea gharama za kupima Covid- 19 kuwa kubwa na ni dawa gani zilizofanyiwa uchunguzi na kuthibitishwa kuwa zina uwezo wa kuzuia au kutibu Covid-19?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a), (b) na (c), kama ifuatavyo: -

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo zimeathirika na mlipuko wa Ugonjwa wa Covid-19. Hadi kufikia tarehe 25 Oktoba 2021, idadi ya Watanzania 26,164 ndio waliothibitika kuwa na maambukizi. Kati ya hao, 725 walifariki na 25,330 walipona.

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani kiasi cha shilingi bilioni 158 zimetumika kununua vifaa mbambali ikiwemo mitambo 19 ya kuzalisha hewa ya oxygen yenye uwezo wa kuzalisha mitungi 200 hadi 300 ambapo mitambo saba tayari imeshasimikwa na 12 ipo katika hatua ya usimikaji. Fedha nyingine zilinunua PPE, dawa, vifaa, vifaa tiba, vitendanishi pamoja na magari 105 ya kubebea wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Sekta ya Afya imepokea kiasi cha shilingi bilioni 466.78 ambazo zitatumika katika kupambana na Uviko-19 ikiwemo kujenga na kusimika vifaa katika majengo ya matibabu ya dharura (EMD) 115, ujenzi wa wodi za uangalizi maalum (ICU) 67, ununuzi wa magari 253 ya kubebea wagonjwa, magari nane ya damu salama, usimikaji wa mitambo 10 ya kuzalisha hewa ya oxygen, vitanda 2,700 kwenye vituo 225 vya kutolea huduma za afya, kununua na kusimika mashine 95 za X-Ray, CT-Scan 29, mashine 4 za MRI pamoja na kufanya tafiti sita kuhusu tabia za virusi vya korona.

(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama halisi ya kumpima mgonjwa mmoja ni Dola 135 na Serikali sasa inatoza Dola 50. Hivyo Serikali inachangia Dola 85.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti mbalimbali zimefanyika duniani kuhusu dawa, ila hadi sasa dawa zilizopo zinatumika kutibu tu madhara yatokanayo na virusi. Hata hivyo kilichothibitika kwa sasa kusaidia kuondoa vifo ni chanjo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. REGINA N. QWARAY aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kusimamia kikamilifu Sera ya Afya ili akinamama wajawazito na watoto wasitozwe gharama katika vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Regina Ndege Qwaray, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, licha ya kuwepo kwa sera na miongozo inayotaka huduma itolewe bure, kumekuwepo na malalamiko ya baadhi ya wananchi walio katika makundi hayo katika maeneo mbalimbali kudaiwa fedha katika vituo vya umma vya kutolea huduma. Ili kuepukana na malalamiko hayo, Serikali inawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, Bodi za Afya na watoa huduma za afya kutekeleza Sera na miongozo inayohusu matibabu bure kwa mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano katika maeneo yao.

Mheshimiwa Spika, pia Serikali inawakumbusha Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi kuwa ni jukumu lao pia kusimamia miongozo inayotolewa na Serikali. Ahsante.