Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:- Hospitali ya Mkoa wa Iringa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nyumba kwa ajili ya madaktari bingwa na hivyo kusababisha madaktari hao kuishi mbali na hospitali:- Je, ni nini mkakati wa Serikali kutatua changamoto hiyo?

Supplementary Question 1

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize maswali madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake lakini pia niendelee kumshukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Iringa, Dkt. Mwakalebela kwa kazi nzuri sana ambayo amekuwa akiifanya katika hospitali yetu kutokana na changamoto nyingi zilizopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mkoa wetu wa Iringa unakabiliwa na ajali nyingi sana lakini kipindi kirefu hatuna daktari bingwa wa mifupa pia hatujawahi kupatiwa daktari bingwa wa watoto toka hospitali ile imeanzishwa. Tuna wodi kubwa sana katika hospitali yetu ya Mkoa kuliko hospitali zote za Nyanda za Juu Kusini.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri sasa anatupa ahadi gani wananchi wa Mkoa wa Iringa kutokana na changamoto hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, naomba niipongeze Serikali yetu hii ya Awamu ya Tano kwa ujenzi wa Hospitali za Wilaya katika nchi yetu. Mkoa wetu una upungufu mkubwa sana wa watumishi takriban asilimia 70 inawafanya wauguzi na madaktari kufanya kazi kwenye mazingira magumu sana. Je, nini mpango wa Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ritta Kabati, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Ritta Kabati amekuwa anafanya kazi nzuri sana ya kufuatilia masuala mbalimbali ya afya katika Mkoa wa Iringa. Kwa kweli amekuwa anatufuatilia sana sisi ndani ya Wizara na tunashukuru kuona kwamba ni mdau mkubwa sana katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza linahusiana na kwamba kuna upungufu wa madaktari wa upasuaji wa mifupa pamoja na madaktari wa watoto. Hilo kama Serikali nakiri lakini sasa hivi Serikali inafanya mkakati wa kufanya mafunzo ya madaktari bingwa takribani 100 mwaka jana tumesomesha, mwaka huu tunasomesha madaktari wengine zaidi ya 100. Wwale watakaomaliza mafunzo na tumeweka utaratibu kwamba madaktari bingwa ambao wanasomeshwa kwa fedha za Serikali baada ya kuhitimu masomo yao, sisi Serikali tutawapangia wapi wanatakiwa kwenda kufanya kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi madaktari hawa watakapomaliza masomo yao basi Mkoa wa Irinnga utakuwa ni moja ya mikoa ambayo tutawapa kipaumbele. Hawa madaktari ambao amewaongelea ni madaktari wa kipaumbele ambao na sisi tumeweka msisitizo kuhakikisha kwamba tunawapa mafunzo na hospitali zote za Rufaa za Mikoa zinakuwa na madaktari bingwa hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ameuliza ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba tunaongeza rasilimali watu. Ni kweli hili jambo tunalo na katika mwaka huu ambao unaisha sasa, Serikali imeajiri watumishi zaidi ya 11,000 kuziba mapengo mbalimbali ambayo yamekuwepo na ajira mpya. Serikali kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) pamoja na Ofisi ya Rais (Utumishi), tunaendelea kufuatilia vibali kuhakikisha kwamba tunapata wataalam wa afya kwa ajili ya maboresho makubwa ambayo tumeyafanya kwenye vituo vya afya na ujenzi wa hospitali za Wilaya ambazo tunaendelea kuzijenga kwa sasa kote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na changamoto hii ya watumishi, kwa kweli watumishi wetu wa afya wanafanya kazi kubwa sana na nzuri katika kuwahudumia Watanzania. Rai yangu katika mikoa yote ikiwa ni pamoja na Mkoa huu wa Iringa ni kuhakikisha kwamba viongozi wa Serikali na viongozi wa vyama wanatengeneza mazingira wezeshi kuhakikisha kwamba watumishi ambao tunawapeleka kule basi wanatengenezewa mazingira wezeshi ya kuweza kufanya kazi zao vizuri.