Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Marwa Ryoba Chacha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Serengeti

Primary Question

MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Barabara inayojengwa kuunganisha Mkoa wa Mara na Arusha inasuasua sana, kwani tangu ilipoanza kujengwa 2013 mpaka leo hata kilomita 50 zimeshindwa kukamilika. (a) Je, Serikali ina mkakati gani dhidi ya ukamilishaji wa barabara hii? (b) Je, ni lini wananchi waliofanyiwa tathmini watalipwa fidia zao?

Supplementary Question 1

MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika sana kiukweli majibu haya hayaridhishi hata kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulienda Serengeti na Naibu Waziri pamoja na Kamati ya Miundombinu, Naibu Waziri gari lake lilipata pancha mara nne, matairi manne. Tukampa spare zikaisha mpaka raia wananchi wakampa spare, hali ni mbaya kwa wananchi wa Serengeti. Ukiangalia barabara imeanza kujengwa tangu 2013, miaka sita (6) imepita kilomita 50 hazijakwisha; Je, itachukua miaka mingapi kumaliza kilomita 80 kutoka Sanzate mpaka Mugumu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wananchi wa Mugumu kwenye hiyo kandokando ya barabara walishafanyiwa tathmini na kila mtu anajua analipwa shilingi ngapi, ni lini watalipwa fidia zao?

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ryoba Chacha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, pamoja na masikitiko yake lakini niruhusu nimpongeze sana Mheshimiwa Ryoba kwa namna anavyofuatilia hasa miradi hii ya barabara. Ni kweli niseme tu kwamba barabara hii kwa historia ni barabara muhimu, hizi kilomita 452 mimi nimeipita hii barabara ina changamoto zake. Kwa historia Marehemu Baba wa Taifa alikuwa akipita barabara hii akitokea Arusha miaka ile, kwa hiyo ni muhimu na sisi kama Serikali tunaiangalia kwa macho mawili. Niseme tu pamoja na kuwa ujenzi huu umekwenda kwa hatua hiyo ya kusuasua lakini kama nilivyosema na kwa kweli kwa ushirikiano wa Wabunge wa Mkoa wa Mara nimejibu wiki juzi swali la Mheshimiwa Agness Marwa na wiki iliyopita nimejibu swali la Mheshimiwa Getere kuonesha umuhimu wa barabara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba Mheshimiwa Ryoba avute subira, lakini niseme tu kwamba kama commitment nilivyosema hapa na namna tunavyosimamia vizuri sasa pamoja na kuchelewa lakini barabara hii itakamilika na kama nilivyokuwa nikizungumza hapa, kwa hiyo tunaisimamia vizuri itakamilika vuta subira.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kilomita 452 tuko asilimia 41 ya commitment ya barabara, kwa Mradi huo wa Makutano Juu – Sanzate kilomita 50. Kama nilivyosema kutoka Sanzate – Natta kilomita 40 tuko hatua ya manunuzi, lakini pia kwenye bajeti Natta – Mugumu kilomita 45 tumeitengea bajeti na ujenzi wa eneo la Wasso – Sale kilomita 49. Utaona asilimia 41 tunaendelea kuisogelea kuweza kuikamilisha barabara hii, kwa hiyo avute tu subira Mheshimiwa Ryoba tutaisimamia vizuri barabara hii ili iweze kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali lake kuhusu tathmini ya wale wananchi; kama nilivyosema, kiutaratibu tunatakiwa tulipe kabla ya ujenzi kuanza. Kwa hiyo tutazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizokuwepo, Sheria ya Ardhi, Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, wananchi watalipwa haki yao kulingana na sheria, kwa hiyo avute tu subira kabla ya kuanza ujenzi wananchi hao watalipwa mara moja.

Name

Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Primary Question

MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Barabara inayojengwa kuunganisha Mkoa wa Mara na Arusha inasuasua sana, kwani tangu ilipoanza kujengwa 2013 mpaka leo hata kilomita 50 zimeshindwa kukamilika. (a) Je, Serikali ina mkakati gani dhidi ya ukamilishaji wa barabara hii? (b) Je, ni lini wananchi waliofanyiwa tathmini watalipwa fidia zao?

Supplementary Question 2

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba niulize swali la nyongeza, naamini kwamba kwa watu wale ambao wanategemea usafiri wao wa maji kivuko ni barabara. Sasa kwa kuwa kivuko ni barabara nataka kuzungumzia kivuko cha Lindi ambacho kinatoka Msinjaili kuelekea Kitumbikwera. Kivuko hiki ni muhimu sana kwa usafiri wa watu wa eneo lile. Sasa kivuko kile kimeshawahi kuharibika na kikapotea kikaelekea maeneo ya mbali. Kutokana na kupotea huko tunamshukuru Mungu hakikuweza kusababisha ajali ya kuua watu. Kwa kuwa kivuko hiki kinaharibika mara kwa mara; Je, Serikali ina mpango gani wa kututengenezea kwa uhakika ili kivuko hiki kiendelee kutumika katika eneo husika? (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mama yangu amekuwa akifuatilia sana mambo mbalimbali hasa kwenye Mkoa wa Lindi, kwa hiyo nitumie nafasi hii kumpongeze. Niseme tu kwa ufupi kabisa tunafahamu umuhimu wa kivuko hiki na tunafahamu namna kivuko hiki kinavyowahudumia wananchi wa Lindi. Tumefanya kwa kweli maboresho makubwa sana katika eneo hili, tumetengeza eneo la maegesho ya kivuko, tumetengeneza nyumba kwa ajili ya abiria wanaovuka kwenda ng’ambo kule. Niseme tu kwa tatizo la kivuko hiki kweli kimekuwa na matatizo kidogo na tumefanya ukarabati mkubwa lakini nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kwa sababu Bunge hili limetupitishia fedha za kutosha kwa ajili ya kuongeza vivuko katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapatazama pale, itakapokuwa imewezekana tutabadilisha injini ya kivuko hiki, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga ili tuone kwamba changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza na zinaendelea kujitokeza tutaendelea kuzitatua na kuziondoa kabisa. Kwa hiyo wananchi wa Lindi wawe na subira lakini niwape comfort tu kwamba, tumejipanga vizuri tutafanya maboresho makubwa pamoja na ile barabara ya kule ng’ambo tutaifanyia matengenezo ili wananchi baada ya kuvuka waweze kwenda na shughuli zao bila kikwazo chochote. Ahsante sana.