Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Wilaya ya Muheza ina utajiri wa uzalishaji wa matunda kama machungwa, maembe, machenza, mafenesi na kadhalika:- Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda Wilayani hapo cha kutengeneza juisi na kuwaondolea usumbufu wakulima hao wa kutafuta soko?

Supplementary Question 1

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, Kumbukumbu za Bunge (Hansard) zinaonesha kwamba swali hili liliwahi kuulizwa mara nyingi na Wizara imekuwa ikitoa maelezo tofauti tofauti ikiwapo na kusema kwamba machungwa ya Muheza siyo mazuri wakati machungwa ya Muheza sasa hivi ni mazuri, tunatumia mbegu ya Valencia, Washington na Msasa na kwamba machungwa hayo yanapelekwa Kenya na kutengeneza juice ya Del Monte. Swali langu la kwanza, Mheshimiwa Waziri atanithibitishiaje kwamba hii Kampuni ya SASUMUA HOLDING ni kweli inataka kujenga hicho kiwanda Mkoa wa Tanga? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ninao wawekezaji ambao wanataka kufanya Muheza iwe kituo cha matunda. Mheshimiwa Waziri atanithibitishia kwamba wawekezaji hao hawatapata usumbufu nitakapowaleta kwake? Nashukuru.

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Answer

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, unapoulizwa swali na Mheshimiwa Mbunge ambaye amewahi kuwa Kamanda halafu ni Balozi inakuwa shida kumjibu. Nimezungumza na watu wa TAHA (Tanzania Horticultural Association) kupita Mkurugenzi Mkuu wao Jacqueline na nimezungumza na SASUMUA HOLDING, vifaa vyao kama earth equipment vimeshafika Kwamsisi, nimeviona na wamenihakikishia. Jambo la kukupa amani ya moyo Mheshimiwa Adadi ni kwamba mimi na wewe pamoja na Waziri, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba na Mheshimiwa Mboni, Mbunge wa Handeni tutapanga twende pale tuone shughuli zinazofanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tuna shughuli ya msingi kwamba yule mtu anataka outgrowers hekta 3,000 na yeye mwenyewe hekta 17,000 na anasema atawapa service. Kwa hiyo, ni jukumu lako Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote wa Tanga mkiongozwa na Mheshimiwa Mboni, mimi na Waziri mwenzangu pacha twende pale tuone Kashenamboni, tuamini au tusiamini mimi na wewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo ninalolipenda kuliko yote ni hili swali lako la pili kwamba niko tayari. Leo nina shughuli tena shughuli pevu, nakuomba kesho uniache nipumzike Jumatano walete wawekezaji wako, hakikisha Tanga hakuna vikwazo, mimi saini yangu natembea nayo.

Name

Mary Pius Chatanda

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Wilaya ya Muheza ina utajiri wa uzalishaji wa matunda kama machungwa, maembe, machenza, mafenesi na kadhalika:- Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda Wilayani hapo cha kutengeneza juisi na kuwaondolea usumbufu wakulima hao wa kutafuta soko?

Supplementary Question 2

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Waziri, amesema kuna wawekezaji ambao wanakusudia kuwekeza pale Kwamsisi, natoa pongezi kwa sababu kiwanda kile kinakuja katika Mkoa wetu wa Tanga. Kwa kuwa ndiyo wanatarajia kuanza kulima hayo mazao ambayo yatalisha kiwanda hicho, je, haoni ni wakati muafaka kwa matunda yaliyopo sasa na hasa ikizingatiwa kwamba Serikali imeshasema itafufua kwanza viwanda vilivyokuwepo hasa kiwanda kilichokuwepo pale Korogwe, ni kiwanda kidogo lakini kinaweza kutengeneza juice kikafufuliwa hicho kwanza wakati tunasubiri kiwanda kikubwa?

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Answer

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, waambie wanipige taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mary Chatanda ameuliza maswali mawili katika moja. Ubora wa matunda au matunda tuliyonayo na hii kampuni ya Kwamsisi ambayo itachukua miezi 18 mpaka ianze kutengeneza juice, jibu lake ni hivi, kuna kampuni nyingine inaitwa Sayona inajenga kiwanda sehemu ya Tanga karibu na Chalinze, itachakata tani 25,000 za matunda yoyote, hii itakuwa inakidhi haja wakati sisi tunasubiri hiki kiwanda cha SASUMUA. Kwa nini SASUMUA hawezi kuanza, yeye analenga kuanza na mananasi na wanasema wataalam kwamba nanasi litakapopandwa linahitaji miezi 18 kuweza kukomaa. Kwa hiyo, yeye ana masharti yake na utaalamu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la Korogwe kwamba kiwanda kipo na bahati nzuri ameuliza swali siku nzuri, namuagiza Mkurugenzi Mkuu wa SIDO aende Korogwe na mtaalam wa TIRDO watathmini ni kitu gani kinahusika halafu Halmashauri yake ambaye yeye ni Diwani tuje tuangalie ni namna gani ninyi mnaweza kuhamasisha Wanatanga ili muweze kukiendesha, viwanda vingine siyo vya Serikali. Ni nini tatizo, hiyo ni kazi yangu nitabaini, spare atanunua wapi wataalam wangu watamwambia, ni viwanda vya shilingi milioni 60 au 80, halmashauri mnavimudu.

Name

Pascal Yohana Haonga

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Mbozi

Primary Question

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:- Wilaya ya Muheza ina utajiri wa uzalishaji wa matunda kama machungwa, maembe, machenza, mafenesi na kadhalika:- Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda Wilayani hapo cha kutengeneza juisi na kuwaondolea usumbufu wakulima hao wa kutafuta soko?

Supplementary Question 3

MHE. PASCAL Y. HAONGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Waziri swali dogo. Ni lini Serikali itaacha kuagiza toothstick maana tuna miti mingi ya kutosha kule Mbeya na sehemu nyingine. Ni lini Serikali itaacha kuagiza toothstick? Ahsante sana.

Name

Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Answer

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika mambo yanayoninyima raha ni kama kuona watu wanaagiza toothpick. Mimi nimeleta bajeti yangu hapa lakini haina maana hata ningeisoma kwa mbwembwe namna gani kama ninyi msipoikubali. Ninyi Wabunge mniambie kwamba toothpick zisipite Dar es Salaam muone kama zitaingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtambo wa kutengeza toothpick ni dola 28,000, ni jukumu lako Watanzania kuwekeza. Kuna Mtanzania mmoja, nawaomba asiyetaka kuwekeza kwenye viwanda na nimelisema mara tatu, kuna Wabunge, kuna watu wanakuja kila siku wanataka kuwekeza, Mtanzania anayeagiza toothpick anaagiza container 100 ni mtu wa Makete. Mtambo wa kutengeneza toothpick ni dola 28,000. Kuna Mbunge Mheshimiwa Lema anafuatilia kuleta mtambo wa toothpick kupeleka Kilimanjaro. Watu wanahangaika, msikosoe, msilalamike twende tufanye kazi. Toothpick inatumia mabaki ya miti haitumii ubao, the reject, the unwanted material ndiyo inatumika. Tuchangamke, twende wote kwenye behewa la viwanda msibaki nyuma. Viwanda ni vita Bwana Msigwa twende kwenye viwanda. Toothpick mkiamua zisiagizwe hazitaingia, TBS ni yangu nitazizuia lakini na ninyi muwekeze watu wanapenda toothpick.