Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Faida Mohammed Bakar

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR aliuliza:- Je, ni sababu gani zimekwamisha uanzishwaji wa Benki ya Wanawake kwa upande wa Zanzibar?

Supplementary Question 1

MHE. FAIDA MOHAMMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi kwa kuunganisha Benki hii ya Wanawake pamoja na Benki ya Posta Tanzania. Kwa nini naipongeza? Naipongeza kwa sababu Benki ya Wanawake Tanzania ilikuwa katika maeneo machache hususani Dar es Salaam na maeneo mengine, haikuwa katika mikoa yote, lakini Benki ya Posta iko kila eneo la Tanzania hii, naipongeza sana Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu lipo hapa, katika hiyo Benki ya Posta ya Tanzania kuna akaunti moja inaitwa Tabasamu kwa ajili ya wanawake. Nadhani watu wengi hawaielewi, leo Mheshimiwa Naibu Waziri atueleweshe hapa. Je, hii akaunti ya Tabasamu imewasaidia kwa kiwango gani wanawake wa Tanzania katika kuwainua kiuchumi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

Name

Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Answer

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la moja la nyongeza la Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Dada yangu Mheshimiwa Faida kwa kuwa yuko mstari wa mbele kufuatilia maslahi mapana ya wanawake wa Tanzania. Niwapongeze sana wanawake wa Zanzibar kwa kutuletea kifaa hiki na kinafanya kazi sawasawa kwa ajili yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nalisema hili kwa sababu hata swali lake aliloliuliza, kauliza specific ili wanawake waendelee kufahamishwa nini faida wanayopata baada ya Benki ya Wanawake Tanzania kuunganishwa na Benki ya TPB.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumefungua akaunti ya Tabasamu ni sahihi kabisa, Dada yangu Mheshimiwa Faida na akaunti hii maalum imefunguliwa kwa ajili ya wanawake wa Tanzania pekee, waweze kuhudumiwa kama wanawake kama walivyokuwa wakihudumiwa na Benki yao ya Wanawake Tanzania. Kwa hiyo, huduma zote zile zinatolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nyongeza katika akaunti hii ya Tabasamu kama lilivyo jina lake, tunataka kupeleka Tabasamu kwa mwanamke wa Tanzania. Tunahitaji mwanamke wa Tanzania awezeshwe kupata mkopo wenye riba nafuu, awezeshwe yeye peke yake siyo lazima awe kwenye kikundi kama ambavyo mabenki mengine yanafanya, aweke akiba yake kidogo kidogo apate mkopo nafuu na aweze kufanya shughuli zake za ujasiriamali, afanye shughuli zake za kiuchumi na za kijamii kwa ajili ya maslahi yake yeye mwenyewe binafsi na maslahi mapana ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa wanawake wa Tanzania, tuitumie akaunti hii ya Tabasamu ndani ya Benki yetu ya Posta. Imeanza vizuri na sisi tuko tayari kuwahudumia wanawake wa Tanzania kwa sababu Serikali ya Chama cha Mapinduzi inawajali Watanzania na hasa wanawake. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.