Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Primary Question

MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:- Barabara ya Tabora – Mambali – Bukumbi – Shitage - Tulole mpaka Kahama ipo katika mpango wa Serikali wa kujenga barabara za lami nchini:- (a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza? (b) Kumekuwa na mvutano wa wapi barabara hiyo ingepita baada ya kufika Mambali, mapendekezo ya Bodi ya Barabara ya Mkoa ni kuwa barabara hiyo ipite Bukumbi, Shitage, Tulole na kuunga Kahama; Je, Serikali inatoa msimamo gani baada ya mapendekezo hayo ya Bodi ya Mkoa wa Tabora? (c) Je, ni lini kipande cha barabara hiyo kitachukuliwa na TANROADS?

Supplementary Question 1

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile kipande cha barabara hiki cha Mambali – Bukumbi – Shitage - Mhulidede mpaka Kahama kupitia Tulole ni muhimu sana kiuchumi kwa sababu ya biashara ya mikoa miwili hiyo; Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
Swali la pili, ni lini uchambuzi yakinifu na usanifu utaanza kwa ajili ya barabara hiyo? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

Name

Elias John Kwandikwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ushetu

Answer

NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia hii barabara, barabara hii ambayo anaizungumza kutoka Mambali – Bukumbi- inakwenda mpaka Mhulidede ni barabara ambayo inapakana na Jimbo la kwangu kule Ushetu. Kwa vile amekuwa akifuatilia barabara hii imewezesha hata kile kipande cha kilometa 21 nilichokitaja kwenda Tulole hadi Kahama Mjini ili kuleta ulinganifu na kuleta maana kimeanza kuhudumiwa.
Mheshimiwa Spika, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuunganisha mikoa na mikoa na kuunganisha mikoa na nchi jirani. Kwa vile kazi inaendelea vizuri nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa maeneo ya Bukumbi, Mhulidede, Mambali na majirani zake kule upande wa Bukene kwamba baada ya kazi nzuri ya kuunganisha mikoa sasa nguvu kubwa itaelekezwa kuunganisha barabara hizi ambazo zinaunganisha wilaya na mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge avute subira baada ya kuwa kazi nzuri ya kuunganisha mikoa na nchi za jirani ikikamilika basi zoezi la usanifu kwa kipande hiki cha barabara kutoka Mambali ambacho kimsingi kitapunguza umbali wa mtu anayetoka Tabora kwenda Kahama kwa takribani kilometa 50.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuvute subira tutakuja kufanya usanifu na kuweza kujenga barabara hii. Usanifu utaanza baada ya kuwa tumejipanga vizuri na kuhakikisha kwamba, sasa tunafanya muunganiko wa sehemu hii ya barabara.