Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Daimu Iddi Mpakate

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kusini

Primary Question

MHE. DAIMU I. MPAKATE aliuliza:- Katika Mji wa Tunduru yako mabango mengi yanayoelezea ununuzi wa madini jambo linaloashiria upatikanaji mkubwa wa madini kutoka kwa Wachimbaji wadogo wadogo ambao hawatambuliwi kwa mujibu wa sheria:- Je, ni lini Serikali itawatengea maeneo ya kuchimba madini na kuwatambua Kisheria Wachimbaji hao wadogo wadogo?

Supplementary Question 1

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, naishukuru Serikali kwa kutenga eneo la Mbesa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia wale wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwawezesha kimtaji na kuwajengea mtambo wa kuchenjulia madini ya shaba ili waweze kusafirisha yakiwa yamechenjuliwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Tunduru kama alivyojibu kwenye swali la msingi ina mabango mengi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mtaalam wa kufanya valuation ya madini haya ya sapphire ili Halmashauri ipate takwimu sahihi za usafirishaji wa madini? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante.

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Answer

NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wachimbaji wengi wa madini wanahitaji kusaidiwa kimtaji kama alivyosema na hasa kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani wa madini (value addition). Nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii Serikali inaifanya kwa umakini kwa sababu tuna historia mbaya hapo nyuma.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo walivyopatiwa mitaji kupitia ruzuku fedha nyingi sana hazikutumika kwa malengo yaliyokuwa yamekusudiwa. Kwa hiyo tunaangalia utaratibu mzuri zaidi kupitia mradi wetu wa SMRP kuona kwamba tunawasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wachimbaji wa Tunduru.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba tupeleke Mtaalam wa valuation Tunduru kwa ajili ya kufanya uthamini wa madini ya vito, tunalichukua jambo hili na tunalifanyia kazi. Vile vile tutaandaa watu baada ya Tume ikishakuwa imekamilisha kazi zake za kuchukua watalaam ili tuweze ku-station mtu mmoja kwa ajili ya kufanya valuation pale Tunduru.