Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Joseph Roman Selasini

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Rombo

Primary Question

MHE. JOESPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. PASCAL Y. HAONGA) aliuliza:- Shule za Watu Binafsi zinatoa huduma ya elimu kama zilivyo Shule za Umma, lakini kwa muda mrefu zimekuwa zikikabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwa ni pamoja na kodi ya majengo (property tax), tozo ya fire, kodi ya ardhi na kodi nyinginezo:- (a) Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuondoa baadhi ya kodi zisizokuwa na tija ambazo zimekuwa kero kwa shule za watu binafsi? (b) Je, Serikali haioni ni wakati sasa wa kuzipatia ruzuku shule binafsi kwa sababu zinashirikiana na Serikali kupunguza tatizo la ajira?

Supplementary Question 1

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, nnakushukuru na nashukuru kwa majibu ya Serikali. Kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza naomba tu jina la muuliza swali lisomeke kama Pascal Yohana Haonga siyo Pascal Yohana Hasunga. Baada ya masahihisho hayo kidogo naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, mara nyingi Serikali imekuwa ikizungumzia na kutoa matamko kuhusu ada zinazopangwa na shule za binafsi ikionesha kana kwamba Serikali ina mpango wa kuweka kiwango fulani cha ada bila kuzingatia gharama ambazo shule hizi zinaingia katika kusomesha wale watoto na kuendesha shule zao. Je, kwa nini Serikali isiwaachie wamiliki wakapanga hizi ada wenyewe ili wazazi ambao wanaweza wakamudu ada hizo waenda kwenye shule bila kikwazo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mara nyingi shule zinapanga taratibu zao za namna ya kuwafanya hawa watoto waweze kufaulu, kwa mfano, kuwawekea mitihani kutoka kwenye daraja fulani kwenda kwenye daraja fulani, lakini Serikali pia inaonesha haifurahishwi na jambo hili. Je, kwa nini Serikali isiache hizi shule zikapanga utaratibu wa kuwafanya hawa watoto waweze kufaulu kulingana na sera na taratibu za shule zenyewe? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Name

William Tate Olenasha

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngorongoro

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Serikali kutoingilia maamuzi ya shule za binafsi katika kuamua ada. Naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sasa Serikali inaendelea na majadiliano na sekta binafsi ya namna bora ya kuratibu suala hilo badala ya Serikali yenyewe kutoa maelekezo ya gharama ambazo zinatakiwa zilipwe.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu shule za binafsi zinaendeshwa na watu binafsi, lakini vilevile kwa sababu ni biashara na ni biashara ambayo maana yake mtu anayetaka kwenda kununua au kupata hiyo huduma yeye ndiyo aangalie uwezo wake, tunafikiri bado kuna busara ya kuendelea kujadiliana nao namna bora ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na gharama ambazo zinahimilika badala ya Serikali yenyewe kuanza kutoa bei au gharama elekezi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili kwamba Serikali isiingilie taratibu za shule binafsi za kuweka viwango vya ufaulu. Wakati tunatambua kwamba ni kweli ni vizuri sekta binafsi katika uendeshaji wa shule ikaachiwa nafasi ya kuamua wenyewe namna wanavyodhibiti ubora. Ni kweli kwamba udhibiti wa ubora ni suala la kisera na kisheria, kwa hiyo, haiwezekani Serikali ikakaa moja kwa moja ikaruhusu kila mtu ajiamulie namna anavyodhibiti ubora katika shule yake.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa sasa ilichoamua ni kwamba tutaendelea kushirikiana na Umoja wa Wamiliki wa Shule Binafsi ili kuangalia namna ya kuboresha sheria na taratibu zilizopo ili ziwawezeshe kupata ubora ule, lakini bila kuvunja sheria za elimu kwa sababu hata kama shule ni za binafsi, lakini ni nchi moja, Serikali ni ile ile, sheria ni zilezile, hatuwezi tukaruhusu kila mtu akajiamulia anavyotaka kwa sababu siyo kila mwenye shule binafsi amekuwa akitumia uhuru huo vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya wanafunzi wamefukuzwa shule kinyume na sheria, kuna wengine wanakaririshwa kwa kuonewa, kuna wanafunzi unakuta wa Form Four wanafukuzwa shule tu kwa sababu hajafikia kiwango fulani. Tunachosema ni kwamba tutaendelea kuwaruhusu kuboresha hayo mazingira, lakini sheria na taratibu lazima tuzifuate na ndiyo maana tunaendelea kufanya nao mjadala kwa pamoja.