Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Masoud Abdalla Salim

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Mtambile

Primary Question

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM aliuliza:- Imebainika kuwa ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) umeendelea kuathiri jamii ya Watanzania. Je, Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa TB?

Supplementary Question 1

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nina maswali mawili ya nyongeza.
Katika majibu yake Mheshimiwa Waziri, amesema kwamba wamekuwa na teknolojia mpya ya upimaji na ugunduzi wa vimelea vya TB kwamba sasa ndani ya masaa mawili badala ya siku tatu.
Napenda kujua nini hasa mkakati wa Serikali wenye kutoa kampeni maalum ya elimu ambayo itaweza kuenea kwa kasi zaidi katika maeneo ya migodi, viwanja vya michezo, mikusanyiko ya wavuvi pamoja na mikusanyiko ya wasafiri?

MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, inaonekana kwamba mkakati wa kukabiliana na tatizo hili ni kwamba ndani ya taratibu hizi za kibajeti, fedha hizi wameachiwa wahisani ambao ni Wazungu. Matatizo ni ya Watanzania, ugonjwa ni wa Watanzania, lakini matibabu ni kwa wahisani wafadhili, Wazungu.
Napenda kujua, kwa nini Serikali imetenga shilingi bilioni 33.3 na ni fedha za nje, hakuna hata senti tano ambayo ni fedha za ndani ambapo fedha hizi za nje huwa hazitolewi kwa wakati na wakati mwingine hazitolewi kabisa. Kwa nini Serikali isipange mkakati wake wa kuweka fedha za ndani badala ya kutegemea fedha za wahisani? (Makofi)

Name

Dr. Faustine Engelbert Ndugulile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kigamboni

Answer

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Masoud kwa kuwa amekuwa ni mfuatiliaji mzuri sana wa masuala ya afya, TB pamoja na masuala ya UKIMWI. Nakupongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri ambayo umeendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijielekeza katika maswali yake ya msingi, ni kwamba sasa hivi Serikali baada ya kuona kwamba tumekuwa na changamoto kubwa sana katika utambuzi wa makundi maalum ambayo wengi wamekuwa wanaathirika kama nilivyoyataja katika majibu yangu ya msingi, tumeelekeza juhudi mahususi katika masuala ya makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakumbuka, mara nyingi ugonjwa huu wa UKIMWI umekuwa ni ugonjwa pacha vilevile wa ugonjwa wa UKIMWI. Sasa hivi mikakati ambayo tunayo, kwanza tumejielekeza kutoa elimu kwa njia mbalimbali kwa vyombo vya habari pamoja na mitandao ya jamii. Vilevile sasa hvi tuna mkakati mahususi wa kuwatafuta wagonjwa wa TB katika migodi. Sambasamba na hilo, katika mikakati yetu tumetengeneza mikakati jumuishi kati ya ugonjwa wa UKIMWI na ugonjwa wa TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tumeanza kijielekeza mahali pengi ambapo tunaweza tukapata wengi kwa pamoja na hususan wanaume. Tumeelekeza nguvu kwenye migodi, tumeelekeza nguvu kwenye kambi za uvuvi na sasa hivi tunataka twende mbali sana katika upande huu wa UKIMWI, hata kule ambapo wanaume wanakuwa katika bar, msishangae na sisi tukiwa tunapita kule tunawaomba kufanya upimaji wa masuala ya UKIMWI pamoja na masuala ya TB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali lake la pili alilielekeza katika suala la fedha akihoji kwa nini Serikali na katika kitabu pale inaonesha kwamba kuna fedha za nje na kwa nini sisi kama Serikali hatujaweka fedha za ndani. Naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 kufikia shilingi bilioni 269 katika mwaka wa fedha 2017/2018 na katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge mmetupitishia hapa juzi, bajeti ya dawa imeongezeka mpaka shilingi bilioni 270. Katika hiyo bajeti, ni kwa ajili ya dawa, vitendanishi na vifaatiba na ndani ya hiyo tumetenga shilingi bilioni tano kwa ajili ya ugonjwa wa TB. (Makofi)