Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mariamu Nassoro Kisangi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Katika Jiji la Dar es Salaam kuna Viwanda vingi ambavyo vimebadilishwa matumizi yake na kugeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia vifaa mbalimbali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvirejesha viwanda hivyo kwenye matumizi yake ya awali?

Supplementary Question 1

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ambayo yamenitosheleza, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri wazi kuwa kuna baadhi ya viwanda viliuzwa na kubadilishwa matumizi; na kwa kuwa sera ya Tanzania ni kutaka tupate Tanzania ya viwanda; je, Serikali inatoa tamko gani sasa kwa hao wanunuzi na wafilisi wa hivyo viwanda wasibadilishe matumizi na badala yake waendeleze viwanda kama Serikali yetu inavyotaka?
Swali la pili, kwa kuwa wanawake wa Dar es Salaam, Lindi na Mtwara walikuwa wanapata ajira kubwa sana katika viwanda vya kubangua korosho vya TANITA, leo hii viwanda hivyo vimewekwa kuwa maghala na maeneo ya kuweka matakataka tu mengine; hususan wanawake wa Mbagala, Kongowe, Temeke, Kurasini, Tandika, wote walio wengi walikuwa wanapata ajira katika kiwanda cha TANITA cha Mbagala; je, Serikali ina mpango gani wa kuvifufua viwanda vya TANITA vya kubangua korosho ili wanawake walio wengi waweze kupata ajira katika viwanda hivyo? (Makofi)

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na viwanda ambayo vimebadilisha matumizi, niseme tu kama ambavyo nimesema awali. Lengo la Taifa ni kuhakikisha kwamba viwanda vinatoa ajira. Kwa hiyo, tusingependa kusema moja kwa moja kwamba ni marufuku kubadilisha matumizi kwa sababu inawezekana biashara iliyokuwepo wakati huo, kulingana na mtaji na mashine zilizopo yawezekana haiendani na wakati wa sasa. Tunachotaka ni kwamba viwanda hivyo viendelee kufanya kazi hata kwa kuangalia bidhaa nyingine ambazo zinaweza zikazalishwa hapo na kuendelea kutoa ajira.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna wale ambao wakati viwanda vinabinafsishwa, waliandika maandika na wakapewa masharti maalum ya kuendeleza viwanda hivyo. Wengine hawajatekeleza kabisa masharti hayo na matokeo yake, viwanda hivyo vimehujumiwa na vingine vimekuwa hata mashine zake hazipo. Tunawaambia ole wao, tutapitia kimoja hadi kimoja na wale ambao wataonekana kwamba hawajakidhi matakwa ya mikataba, naamini Serikali itachukua hatua kali inayostahili.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kiwanda ambacho ni cha TANITA, niseme tu kwamba sambamba na maelezo uliyoeleza Mheshimiwa Mbunge pia sisi tutatembelea lakini la msingi kama ambavyo nimesema awali tungehitaji kuona kwamba viwanda vyetu vinafanya kazi yenye tija na kuweza kutoa ajira kwa watu wengi zaidi ikiwemo akina mama.