Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Dr. Raphael Masunga Chegeni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JUMANNE K. KISHIMBA) aliuliza:- Mfumo wetu wa elimu unaonekana kuchangia mfumuko wa matatizo ikiwemo kujenga mazingira ya udanganyifu na wizi wa mitihani hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kufutiwa matokeo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumpima mwanafunzi kwa kutathmini tangu shule ya msingi na kuoanisha na mtihani wake wa mwisho ili kupata uhalisia na uwezo badala ya kumpima mwanafunzi kwa kigezo cha mtihani wa siku moja?

Supplementary Question 1

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, hoja ya swali la Mheshimiwa Kishimba ni kwamba kumekuwa na utaratibu wa kumtahini mwanafunzi kwa mtihani wa mwisho na wakati mwingine unakuta mwanafunzi pengine zile siku za mwisho anakuwa na matatizo ambayo yanamfanya ashindwe kufaulu vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia maendeleo ya mwanafunzi huyu ili kusudi maendeleo yake yawe ni sehemu ya mtihani wake wa mwisho ili kuondoa mchanganyiko huu?
Swali la pili, kwa vile kumekuwa na wizi wa mitihani mara kwa mara na hii inachangiwa kwa sababu wanafunzi wanajiandaa kwenda kushinda mtihani badala ya kujua namna ya kujibu mtihani.
Je, Serikali inatafuta mbinu gani mbadala za kuwasaidia vijana badala ya kukariri kufanya mtihani, wafanye mtihani kwa kuelewa namna ya kushinda mtihani?(Makofi)

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia matokeo endelevu yaani mwanafunzi amekuwa akipimwa katika muda wake anaokuwa darasani, vilevile hata wale wanaofanya shughuli za vitendo, kwa mfano wale wanaosoma masomo ya ufundi wamekuwa wakienda kwenye mazoezi wanafuatiliwa na pia shughuli za vitendo zimekuwa zikichangia asilimia 30 niliyosema katika mitihani ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mtihani wa mwisho ni kweli ndiyo unakuwa na nafasi kubwa zaidi kwa ajili ya hiyo asilimia 70; endapo mwanafunzi amepata tatizo siku ya mwisho ya mtihani, taarifa huwa zinatolewa na kuweza kuangalia kwamba alikuwa kwenye mazingira gani. Wakati mwingine mwanafunzi anashauriwa asifanye mtihani kama hali yake kwa mfano itakuwa ni ya ugonjwa ili aweze kurudia na kufanya mtihani wakati mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wizi kwa kiwango kikubwa Serikali imeweza kudhibiti tatizo hilo, nanyi mtakuwa mashahidi katika kipindi hiki, hasa toka tumeingia halijawahi kutokea tatizo la wizi wa mitihani. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ningependa kuweka msisitizo kwenye suala la wizi wa mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulihakikishia Bunge lako kwamba Serikali imedhibiti suala la wizi wa mitihani na kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani, ambapo baadhi ya Walimu ama huwa baada ya kufungua zile karatasi za mitihani wanaenda pembeni wanawaandalia wanafunzi majibu na kuyapeleka katika chumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali imekuwa pia makini katika kuhakikisha kwamba inaangalia kwa karibu usimamizi wa mitihani na wote ambao wanakuwa wanajihusisha na udanganyifu katika mitihani hatua zimekuwa zikichukuliwa na zitaendelea kuwa zinachukuliwa.(Makofi)

Name

Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JUMANNE K. KISHIMBA) aliuliza:- Mfumo wetu wa elimu unaonekana kuchangia mfumuko wa matatizo ikiwemo kujenga mazingira ya udanganyifu na wizi wa mitihani hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kufutiwa matokeo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumpima mwanafunzi kwa kutathmini tangu shule ya msingi na kuoanisha na mtihani wake wa mwisho ili kupata uhalisia na uwezo badala ya kumpima mwanafunzi kwa kigezo cha mtihani wa siku moja?

Supplementary Question 2

MHE. DOTO M. BITEKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi mzuri wa mitihani ni pamoja na kuwalipa stahiki zao wasimamizi wa mitihani wakiwemo walimu pamoja na askari, lakini mwaka 2015 walimu walisimamia mtihani ya kidato cha nne wakakopwa fedha zao, fedha hizo mpaka sasa hawajalipwa. Ninaomba kujua ni lini walimu hao watalipwa fedha zao walizokopwa wakati wanasimamia mitihani? (Makofi)

Name

Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mwaka 2015 tulikuwa na deni ambalo walimu walisimamia mitihani walikuwa hawajalipwa na deni lile baada ya uhakiki lilikuwa karibuni shilingi bilioni 6.4. Ninapenda kuzipongeza baadhi ya Halmashauri hasa kuna Halmashauri maalum zingine zilifanya initiative ya kulipa zile fedha karibu shilingi bilioni tatu ziliweza kulipwa, hivi sasa tuna deni ambalo ni outstanding karibuni shilingi bilioni 3.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba deni lile tulipeleka Hazina na liko katika hatua ya mwisho kwa wale watu ambao hawajalipwa watalipwa pesa zao.

Name

Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JUMANNE K. KISHIMBA) aliuliza:- Mfumo wetu wa elimu unaonekana kuchangia mfumuko wa matatizo ikiwemo kujenga mazingira ya udanganyifu na wizi wa mitihani hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kufutiwa matokeo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumpima mwanafunzi kwa kutathmini tangu shule ya msingi na kuoanisha na mtihani wake wa mwisho ili kupata uhalisia na uwezo badala ya kumpima mwanafunzi kwa kigezo cha mtihani wa siku moja?

Supplementary Question 3

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa swali la Mheshimiwa Kishimba linafanana kabisa na changamoto ya udanganyifu wa mitihani yaani thesis and dissertation kwa wanafunzi wa shule ya Uzamili na Uzamivu elimu ya juu.
Je, Serikali imejipangaje kuwa na mfumo mahsusi katika kudhibiti ubadhilifu wa mitihani kwa maana ya kuwa na mfumo mathalani central system plagiarism test? Ahsante.

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika masuala haya ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafanya mtihani na wanapimwa kwa kiwango wanachostahili kwa kadri ya kuwapima uelewa wao, Serikali tumeendelea kufanya hivyo. Kwa upande wa vyuo vikuu hasa kwa upande wa wanapofanya maandishi yao, niseme thesis kwa mfano, kweli kumekuwa kunajitokeza udanganyifu wa watu kuomba ama kufanyiwa na watu, wakati mwingine kunakili maandiko ya watu wengine waliopita kiasi kwamba mtu anakuwa hajafanya kazi yake na kupimwa kwa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaliona hilo na tumeshaandaa mfumo kiasi kwamba kila mtu akishamaliza andiko lake litakuwa linapitishwa humo kiasi kwamba likioanishwa litajulikana kwamba huyu ameiba kutoka kwa andiko la mtu mwingine. Ikizingatiwa katika mfumo huu wa digital watu ni rahisi kuiba. Kwa hiyo tumeshaona namna ya kudhibiti eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya sekondari ngazi mbalimbali tunafanya uhakiki. Kwa mfano, mara hii ya mwisho hata sisi wenyewe Mawaziri tumekuwa tukitembelea baadhi ya shule za kidato cha sita kuona kwamba taratibu na sheria zinazingatiwa katika sehemu za mitihani. Mfano, safari hii nimeenda shule ya Ifunda na shule ya Iringa Girls. Hivyo tunasimamia kikamilifu.

Name

Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JUMANNE K. KISHIMBA) aliuliza:- Mfumo wetu wa elimu unaonekana kuchangia mfumuko wa matatizo ikiwemo kujenga mazingira ya udanganyifu na wizi wa mitihani hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kufutiwa matokeo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kumpima mwanafunzi kwa kutathmini tangu shule ya msingi na kuoanisha na mtihani wake wa mwisho ili kupata uhalisia na uwezo badala ya kumpima mwanafunzi kwa kigezo cha mtihani wa siku moja?

Supplementary Question 4

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Pamoja na kuwa lugha yetu ya Taifa ni kiswahili lakini kumekuwa na mkanganyiko katika mfumo wetu wa ufundishaji wanafunzi. Shule nyingi za Serikali kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba wanafundisha kwa kiswahili lakini wakifika sekondari wanaambiwa wazungumze lugha ya kiingereza. Sambamba na hilo, tatizo hili liko kwenye vyuo vyetu vya Serikali ya Mitaa hususan Hombolo. Masomo yote yanafundishwa kwa kiingereza ilhali watu hawa wanaenda kusimamia watu ambao hawajasoma.
Je, Serikali haioni ni muhimu kubadilisha mitaala hii kuondoa mkanganyiko huu katika sera ya ufundishaji?

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza tunamshukuru kwa kuwa ni mdau wa kiswahili na kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kuwa Balozi wa Kiswahili Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ya msingi kiswahili imekuwa ndiyo lugha ya kufundishia na kiingereza inakuwa kama somo. Tunafanya hivyo kwa sababu tunaamini Watanzania wengi lugha ya kiswahili japokuwa ni lugha ya pili, lakini wana uelewa zaidi na hivyo kuwawezesha kuelewa vizuri elimu yao ya msingi katika lugha ambayo wamekuwa nayo. Hali kadhalika tunapokwenda kwenye sekondari ndipo sasa wanapotumia lugha ya kiingereza kama lugha ya kufundishia na kiswahili kama somo na hiyo sasa inaenda vilevile kwa upande wa zile shule zinazotumia lugha za kiingereza toka awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu hakatazwi kuweka msisitizo katika lugha ile ambayo anafahamu inaeleweka na wanafunzi kwa uzuri zaidi ili kumfanya yule mwanafunzi kile kilichofundishwa aweze kukitafsiri katika lugha yake iliyo rahisi na kukielewa vizuri zaidi. Ieleweke kwamba lugha pekee siyo maarifa. Lugha pamoja na yale maarifa unayofundishwa ndiyo yanayomfanya mwanafunzi kuwa imara na kuweza kutumika katika nyanja mbalimbali zinazohitajika. (Makofi)