Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Primary Question

MHE. AIDA J. KHENANI aliuliza:- Wananchi wengi Sumbawanga hawana hati miliki; aidha, kumekuwa na changamoto nyingi katika kupata hati hiyo hali inayowafanya wananchi kukata tamaa.- Je, ni gharama kiasi gani zinazohitajika ili kupata hati miliki?

Supplementary Question 1

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Pia nashukuru kwa ufafanuzi alioutoa Naibu Waziri ambao utaleta mwanga kidogo kwa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga wameamua sasa kufuata utaratibu ili wapate hati, shida yao siyo kumiliki tu hati, ziwasaidie kwenye taasisi pia za kifedha, lakini hati zimekuwa zinachelewa sana. Hamuoni kwamba kuendelea kuchelewa kwa hati hizo mnawanyima fursa wananchi wa Manispaa ya Sumbawanga na Mkoa wa Rukwa masuala ya maendeleo kwa sababu wanakosa mambo muhimu hasa katika taasisi za fedha?
Swali la pili, Maafisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga wanajitahidi sana kwa jitihada zao kuwafuata wananchi kwenda kupima maeneo, lakini wanakabiliana na changamoto za usafiri, pamoja na vitendea kazi vingine kwenda kupima ardhi.
Je, Serikali hamuoni kuna umuhimu zaidi wa kuwapa kipaumbele ili wale wakafanye kazi kwa mujibu wa sheria ili wasipate malalamiko kama yanayoendelea kwa sasa?

Name

Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Answer

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza amezungumzia ucheleweshaji utaratibu wa kupata hizo hati pengine unakuwa ni mrefu na ni kinyume na utaratibu. Pengine Mheshimiwa Aida bado yuko na mawazo yale ya zamani, kwa sababu sasa hivi kama ambavyo tulieleza kwenye bajeti iliyopita ndani ya mwezi mmoja kama umekamilisha malipo yako vizuri, unapata hati yako, hakuna tena usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda zetu zote Nane zinatoa hati hizo tumeishaweka wataalam kule wako wanafanya kazi hiyo. Kama huko kwake bado hilo linafanyika, nadhani siyo sahihi, na mimi siamini kama linafanyika hivyo kwa sababu utendaji wa Wizara kupitia Kanda zake unakwenda kwa utaratibu na mujibu wa sheria ambavyo tumewawekea, hivyo hakuna tena suala la ucheleweshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Maafisa Ardhi kukosa usafiri na vitendea kazi, naomba tu nitumie fursa hii watendaji hawa ambao wako katika Halmashauri ni jukumu la Halmashauri kuweza kuona ni jinsi gani watu hawa watafanya kazi. Wizara tuna-support yale ambayo yako nje ya uwezo wa Halmashauri. Hii ni Idara kama Idara zingine, kama Idara ya Elimu, Idara ya Afya wanakuwa na usafiri, wanawekewa bajeti zao kila mnapopanga. Mnashindwa nini kufanya hilo kwa Idara ya Ardhi, kwa sababu sehemu nyingi kila unapoenda unakuta Idara ya Ardhi ile ni ombaomba, wakitaka kwenda field mpaka wabembeleze gari sijui la Elimu, lakini ni jukumu la Halmashauri husika kui-treat Idara hii sawa na Idara zingine. Kwa sababu ndiyo kwanza wanaofanya zile kazi ambazo inawezesha Idara zingine kuweza kufanya kazi zao kwa ukamilifu vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe kwamba mbali na Wizara kusaidia, ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha kwamba tunapoweka bajeti zetu, katika kupanga vitendea kazi pamoja na kwamba vina gharama lakini lazima tukadirie. Wizara pia inakwenda kuweka utaratibu kwenye maeneo ya Kanda zetu kutakuwa na vifaa vya upimaji kule ambavyo vitasaidia katika Halmashauri zetu. Kwa hiyo, tusaidiane Halmashauri na Wizara ili tuwarahisishie kazi hii na wao waweze kufanya kazi zao kwa ukamilifu.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri sana, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge niwape experience kidogo kwa swali la nyongeza hili kwamba hati hazitayarishwi na Wizara, hati zinatayarishwa pale kwenye Halmashauri. Sasa nawaombeni ninyi Waheshimiwa Wabunge mkirudi majumbani kwenye Halmashauri zenu mfanye tu ujanja ambao nimegundua wanafanya.
Meshimiwa Naibu Spika, nimekuta Kibaha pale hati zinaanza kuandaliwa pale Wilayani makaratasi, hata lile jalada la hati linatengenezwa pale sisi tunakuja kusaini tu huku mwisho. Mkienda kwenye Masjala za Hati kwenye Wilaya zenu zote, mtakuta hati zile zimetayarishwa ziko kwenye mafaili haziendi kokote.
Waheshimiwa Wabunge, hebu kila mmoja aende kwenye Masjala ya Ardhi ya Halmashauri yake, utakuta hati zimeshaandikiwa, watu wameshalipa wametengenezewa na yale majalada ya kaki halafu zimewekwa pale miaka miwili mitatu. Hazifiki kwa Makamishna wa Wizara ya Ardhi kusaini kwa nini? Ndiyo kazi tunayoifanya sisi wenzenu kuja kwenye Majimbo yenu kuja kuangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sasa wote muwe ma-auditor muende kwanye masjala za ardhi mkaziondoe zile hati ambazo zimekaa mle, watu wanataka zikae muda mrefu wasahau halafu waweze kubadilisha wampe mtu mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, naomba mtusaidie kwenda kwenye masjala, mfanye ukaguzi watu wote ambao majalada yameshaandikwa yafike kwa Makamishna wapewe hati zao, tunataka mwezi mmoja tangu mtu amelipia apate hati yake. (Makofi)