Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Mohamed Omary Mchengerwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rufiji

Primary Question

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:- Sheria zinatoa ridhaa kwa watu kuwinda ndani ya hifadhi:- Je, Serikali inachukua hatua gani kutoa ridhaa kwa wananchi waishio maeneo ya hifadhi kupata ruhusa kisheria ili kuweza kuvua samaki ndani ya mabwawa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma kwa wanakijiji waishio maeneo ya hifadhi hususan Kata za Mwaseni, Mloka na nyingine?

Supplementary Question 1

MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wananchi waliokuwa na umri wa kuelewa mambo, mwaka 1956 Mwalimu Nyerere aliahidi ujenzi wa Bwawa la Stiegler‟s Gorge ili kuweza kutatua tatizo la umeme. Bwawa hili lingejengwa pale katika Kata ya Mwaseni. Ahadi hii ina miaka 61.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kufahamu kama ahadi hii ya Mheshimiwa Waziri aliyotuahidi hapa ujenzi wa mabwawa katika Kata za Mwaseni, Kipugira, Kilimani pamoja na Mkongo itachukua pia miaka 61 au itakuwa muda mfupi kidogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Wizara ya Maliasili na Utalii inachangia pato la Taifa asilimia 19 na Rufiji yetu iko ndani ya hifadhi kwa zaidi ya nusu ya Rufiji, yaani square kilometer 6,500 ipo ndani ya hifadhi ya Maliasili na Utalii. Naomba kufahamu, mchakato wa ujenzi wa vyoo katika eneo la Selous pale Rufiji, leo hii watalii wanajisaidia katika maeneo ya hifadhi bila kuwa na vyoo. Naomba kufahamu, hili pato la Taifa mgawanyo wake ukoje katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii ili kuweza kusaidia wanyama hawa ambao wapo ndani ya hifadhi ikizingatia kwamba watalii wetu leo hii wanajisaidia sehemu ambazo ni za wazi bila kujisaidia eneo la vyoo.

Name

Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Answer

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza la wasiwasi au mashaka ya kwamba pengine hata ahadi hii tuliyoitoa hapa inaweza ikachukua muda mrefu ule alioutaja zaidi ya miaka 60 akifananisha na suala la mradi wa Stiegler‟s Gorge; kwanza nataka tu nimpe taarifa kwamba mradi wa Stiegler‟s Gorge akileta swali ambalo ni mahsusi kwa mujibu wa Kanuni za Bunge litajibiwa vizuri sana na Wizara ya Maji kwa sababu lina majibu sahihi kabisa na mahsusi ya kwa nini imechukua muda mrefu kiasi hicho kutekeleza mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na majibu haya ya utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa matano; kwanza napenda nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, kwamba hivi ninavyozungumza, kutokana na jitihada zake, wananchi wa Jimbo lake wanaelekea kupata majawabu ya changamoto kubwa hii ya kupata maeneo ya uvuvi hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi karibuni kwa sababu ninavyozungumza sasa hivi tayari mawasiliano yameshafanyika kati ya Wizara yangu na Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji. Tumeshabadilishana uzoefu na taarifa na tayari tuna makisio ya awali ya gharama za ujenzi wa mabwawa hayo matano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kutokana na kiwango cha fedha kile ambacho tumekiona katika hatua za awali, tunafanya mapitio ili tujue ukubwa wa mabwawa yale lakini pia tujue namna ya kuyajenga ili kuweza kutumia gharama ambazo zitakuwa zina unafuu, lakini bado tufikie malengo ya kuweza kuwapatia mabwawa hayo wananchi.
Kwa hiyo, wananchi wa Rufiji wasiwe na wasiwasi, Mheshimiwa Mchengerwa anawapigania na watapata maeneo ya kuvua samaki mbadala nje ya Hifadhi ya Selous. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili; ni kweli utalii unachangia asilimia zaidi ya 17 katika pato la Taifa; lakini pia niongeze kwamba robo ya upatikanaji wa fedha za kigeni katika muda wa miaka mitatu mfululizo lilitokana na pato linalotokana na utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu changamoto aliyoisema ya eneo la maingilio ndani ya hifadhi, changamoto ambayo inaleta usumbufu kwa watalii, nataka kusema kwamba changamoto hii imeshamalizika kwa sababu tayari ni miongoni mwa mambo ambayo tumeyapa kipaumbele hivi karibuni, yale ambayo tunatakiwa kuyashughulikia kwa haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua unapokuwa na changamoto kuna nyingine ni kubwa sana zinahitaji labda jitihada kubwa na rasilimali nyingi, lakini hizi nyingine ndogo ndogo kama hii, hizi ni quick wins, kwa hiyo, tunazifanyia utaratibu wa haraka. Nataka nimhakikishie kwamba kabla mwaka huu haujakwisha, tutakuwa tumetatua tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.