Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Salome Wycliffe Makamba

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SALOME W. MAKAMBA aliuliza:- Serikali kupitia Mawakala wake wa Maji katika Mkoa wa Shinyanga imepandisha bei ya maji kwa takribani asilimia 100 kwa unit na service charge. Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza bei ya huduma ya maji ili wananchi waweze kumudu gharama za huduma hiyo na pia kuwavutia zaidi wawekezaji viwandani ili waendelee na uzalishaji?

Supplementary Question 1

MHE. SALOME W. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, majibu ya Mheshimiwa Waziri hayaridhishi. Anaongea habari ya gesi asili Shinyanga yaani mpaka gesi asili ije kufika hizi ni ndoto na kwa kweli tutaendelea kuumia na bei ya maji. EWURA hawajaenda kufanya consultation, hawajaenda kuongea na wananchi, wamepandisha bei ofisini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Maji ya Shinyanga na Kahama wametengeneza muungano wakaweka kitu kinaitwa SHUWASA na kazi ya SHUWASA ilikuwa ni kuboresha usambazaji wa huduma ya maji katika Wilaya hizi mbili. Badala yake SHUWASA sasa hivi wanauzia maji Mamlaka ya Kahama na ya Shinyanga ambapo watumiaji wa mwisho wanaumizwa na bei kubwa kwa sababu ya kuwepo na mtu wa katikati. Waziri ana mpango gani wa kujaribu ku-standardize suala la bei ya maji katika wilaya hizi mbili kwa sababu hali hii inawaumiza wadau na wawekezaji wanakimbia kwa sababu hakuna huduma? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, nikimnukuu Mheshimiwa Rais Magufuli kwenye kampeni zake alisema atahakikisha akiingia madarakani nchi nzima tutapata maji na kama tukikosa maji atawageuza ninyi Mawaziri kuwa maji, lakini mpaka leo hamjawa maji. Shinyanga ni Kata nane tu za Wilaya ya Kahama Mjini ndiyo zina maji wakati Kata 12 zote mpaka leo hazijapata maji, watu wanahangaika wanatumia maji taka na inatishia kuleta milipuko ya magonjwa. Ni lini watatimiza mpango wa kutandaza mtandao wa maji katika Wilaya hizi mbili ili watu waepukane na magonjwa? Ahsante sana.

Name

Eng. Gerson Hosea Lwenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Wanging'ombe

Answer

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge pamoja na jazba aliyokuwa nayo wakati akiongea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimfahamishe kwamba masuala ya kupandisha bei yapo kisheria. Huyu mdhibiti ambaye anaitwa EWURA ipo procedure ambayo lazima aifuate. Kwa hiyo, procedure ya kupandisha bei ilifuatwa, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Spika, pia naomba afahamu kwamba jurisdiction ya SHUWASA ni katika Mji wa Shinyanga kule Kahama wana mamlaka nyingine ambayo inashughulikia Kahama. Kwa hiyo, tunayo mamlaka ambayo inaleta maji SHUWASA kwa bulk halafu SHUWASA sasa ndo inafanya distribution.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hoja kubwa hapa ungesema tu kwamba unaona bei iliyowekwa ni kubwa, hilo ni jambo ambalo tunaweza tukazungumza. Ndiyo maana kwenye majibu tumesema kwamba nusu ya gharama za uendeshaji wa SHUWASA ni kulipa bili za umeme. Kwa hiyo, bili za umeme zikishushwa definitely na bili ya maji itashuka. Tukasema kwamba uzalishaji wa umeme kwa mfano kama tunatumia nishati ambayo inalazimisha bei ya umeme ishuke basi hata bei ya maji itashuka, ndiyo hoja ambayo ulikuwa umeuliza kwenye swali la msingi.
Mheshimiwa Spika, lakini pia ukielezea suala la kwamba mpaka sasa upatikanaji wa maji maeneo mengi hakuna, lakini ni lazima Mheshimiwa Mbunge afahamu tulipitisha bajeti mwaka huu na tumepanga fedha za kutekeleza miradi na kila Wilaya inaendelea kutekeleza. Sasa akilizungumza kwa ujumla inakuwa vigumu kuelewa swali lake tulijibu vipi. Nataka awe specific na swali kwamba ni Wilaya ipi na ni mradi upi ambao haujakamilika. Serikali inaendelea kukamilisha miradi kulingana na mpango ambao Wabunge mlipitisha.
Mheshimiwa Spika, naomba nitambue Mheshimiwa Masele ndiye aliyeuliza swali kwa Mheshimiwa Rais kuhusu bei za maji.

Name

Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Primary Question

MHE. SALOME W. MAKAMBA aliuliza:- Serikali kupitia Mawakala wake wa Maji katika Mkoa wa Shinyanga imepandisha bei ya maji kwa takribani asilimia 100 kwa unit na service charge. Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza bei ya huduma ya maji ili wananchi waweze kumudu gharama za huduma hiyo na pia kuwavutia zaidi wawekezaji viwandani ili waendelee na uzalishaji?

Supplementary Question 2

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Spika, nikushukuru. Naomba niulize swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa TANESCO wameondoa service charge na hawa ndiyo wanatusaidia kusukuma maji katika vyanzo vyetu lakini wenzetu wa Wizara ya Maji kwenye bili zetu za maji bado kuna service charge. Je, ni lini hii service charge itaondolewa kwa wananchi wetu kwa sababu kwa kweli ni gharama kubwa pamoja na bili hizi ambazo zimepanda?

Name

Eng. Isack Aloyce Kamwelwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Katavi

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali moja dogo la Mheshimiwa Gekul kuhusu ni lini tutaondoa service charge kwenye bili za maji. Mpango huo tumeuanza na kwa sasa Mkoa wa Iringa meter reading haisomwi tena na watendaji, meter reading hakuna kwa sababu tumeweka mita za LUKU. Ukitaka maji unakwenda kulipia kwa kutumia mfumo uliopo, unapata maji kama jinsi ambavyo unanunua umeme. Kwa kufanya hivyo, sasa hivi Mkoa wa Iringa bado muda kidogo hakutakuwa na service charge. Kwa hiyo, tukifanya hivyo nchi nzima service charges zitaondolewa.