Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 3 Sitting 32 Energy and Minerals Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa 260 2016-05-30

Name

Leonidas Tutubert Gama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Primary Question

Umeme ni muhimu sana kwa maisha bora ya wananchi, lakini wananchi wa Songea Mjini hawana uhakika wa umeme kutokana na kutegemea zaidi umeme wa jenereta na ule kidogo unaozalishwa na Shirika la Masista Chipole:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa Gridi ya Taifa toka Njombe/Makambako?
(b) Je, Serikali inafahamu kuwa watu wengi wanashindwa kuja kuwekeza Songea kutokana na kukosa umeme wa uhakika?

Name

Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Answer

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu a na b kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kufikisha umeme wa Gridi ya Taifa mkoani Ruvuma kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea. Kazi za mradi huu na utekelezaji wake umeshaanza na zimegawanyika katika sehemu kuu mbili:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilometa 250 kutoka Makambako hadi Songea. Kazi hii pia inahusisha pia upanuzi wa kituo cha kupooza umeme kutoka Makambako, lakini pia ujenzi wa vituo vipya vya kupooza umeme katika Mji wa Madaba pamoja na Mji wa Songea. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018 naitagharimu dola za Kimarekani milioni 34.68 lakini pia shilingi bilioni 15.41.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 900. Lakini pia wateja wa awali 22,700 katika vijiji 120 vya Wilaya ya Ludewa, Njombe Mjini, Njombe Vijijini, Wanging‟ombe katika Mkoa wa Njombe wataunganishiwa umeme. Kadhalika kazi hii itajumuisha pia katika wilaya za Mbinga, Namtumbo, Songea Mjini na Songea Vijijini katika Mkoa wa Ruvuma. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2017 na itangarimu dola za Marekani milioni 37.63 na shilingi bilioni 6.51.
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Ruvuma umeimarika kwa siku za hivi karibuni. Na hii ni kutokana na kufunguliwa kwa vituo mbalimbali vya kuzalisha umeme, ikiwa ni pamoja na vituo vya umeme vya Donya (megawatt 0.5), Mbinga (megawatt 2.5), Namtumbo (megawatt 0.4) Songea (Megawatt 4.5) na Tulila (megawatt 5) vilivyofikisha jumla ya megawatt 12.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya juu ya umeme kwa Mji wa Songea ni megawatt 4.7, na uwezo wa uzalishaji ni megawatt 9.5, hivyo kuwa na ziada ya umeme wa megawatt 4.8. Ni matumaini ya Serikali kuwa kukamilika kwa
mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya Makambako kwenda Songea kutamaliza kabisa tatizo la changamoto za umeme na kufufua fursa za uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla wake.