Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 19 Sitting 1 Water and Irrigation Wizara ya Maji 9 2020-03-31

Name

Hawa Abdulrahiman Ghasia

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Mtwara Vijijini

Primary Question

MHE. HAWA A. GHASIA aliuliza:-

Tatizo la maji Mkoani Mtwara limeendelea kuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mkoa huo:-

(a) Je, mradi wa kutoa maji mto Ruvuma hadi Mtwara Manispaa umefikia hatua gani?

(b) Je, ni lini Serikali itapeleka fedha za ukarabati wa Mradi wa Maji wa Mbuo Nkunwa?

(c) Je, ni nini hatma ya Mradi wa Maji Makonde?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Jimbo la Mtwara Vijijini, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu wa mradi wa kutoa maji katika chanzo cha maji cha Mto Ruvuma kwa ajili ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuajiri mtaalam atakayefanya usanifu wa kina na kuandaa makabrasha kwa ajili ya kuanza utekelezaji katika mwaka wa fedha 2020/2021. Mradi huu ni mkubwa, ukitekelezwa utakuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara.

(b) Mheshimiwa Spika, ukarabati wa mradi wa maji Mbuo – Nkunwa unaendelea kufanyika na Mkandarasi anaendelea na kazi. Mpaka sasa bomba la njia kuu lenye urefu wa kilomita 3.6 limelazwa na wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji.

Pia mkandarasi amechimba kisima kingine kipya ili kuongeza kiasi cha maji. Kazi ya kufunga miundombinu ya bomba la mtandao wa maji inaendelea. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Aprili, 2020. Usimamizi wa mradi huu unafanywa na wataalam wa ndani (force account) wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mtwara (MTUWASA).

(c) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa mradi wa Makonde, Serikali imepanga kufanya ukarabati kwa awamu. Awamu ya kwanza ya ukarabati inaendelea ambapo tayari njia ya bomba kuu yenye urefu wa kilomita 17 kutoka chanzo cha maji Mitema hadi Mjini Newala imekamilika.

Mheshimiwa Spika, kazi ya ufungaji wa pampu inaendelea ili majaribio ya mradi yafanyike kwa ajili ya Mji wa Newala. Aidha, katika awamu hii upo mpango wa kuongeza njia nyingine kubwa kutokea Mitema hadi eneo la Nambunga ambapo tenki lenye uwezo wa lita milioni tano litajengwa na maji yatasambazwa katika Mji wa Newala na vijiji jirani. Awamu ya pili itahusisha ukarabati wa mtandao wa mabomba katika eneo la Tandahimba ili kutoa huduma ya maji ya uhakika.