Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 53 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 469 2019-06-26

Name

Victor Kilasile Mwambalaswa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Primary Question

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-

Miaka ya karibuni samaki aina ya Ngege (Pelege) katika Ziwa Rukwa wamepungua na kudumaa na hii ni kutokana na uchimbaji wa dhahabu Wilayani Chunya na Songwe ambao mara nyingi ulihusisha zebaki.

Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya utafiti katika Ziwa hili?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka ya nyuma samaki aina ya ngege katika Ziwa Rukwa walikuwa wanakuwa wakubwa kutokana na kuwa walikuwa hawakabiliwi na changamoto zinazowakabili sasa.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) katika mwaka huu wa 2019 kwenye Ziwa Rukwa, ilibainika kuwa kuna udumavu na upungufu wa samaki katika ziwa hilo na hasa kwa samaki wa jamii ya ngege. ngege aina ya Oreochromis rukwaensis ambaye ni wa asili katika ziwa hilo wamepungua zaidi kulinganisha na ngege aina ya Oreochromis esculentus ambao wamepandikizwa. Udumavu na upungufu wa samaki katika ziwa hilo unasababishwa na changamoto zifuatazo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, uchafuzi wa mazingira utokanao na kuongezeka kwa shughuli za binadamu kama vile:-

(i) Kuongezeka kwa idadi ya mifugo inayotegemea ziwa kupata maji ya kunywa na pia malisho ya mifugo hiyo pembezoni mwa ziwa;

(ii) Kilimo kisichofuata taratibu karibu ama pembezoni mwa ziwa;

(iii) Uchimbaji wa madini ya dhahabu ambapo zebaki, (mercury) hutumika kuchakata dhahabu hizo; na

(iv) Ongezeko la matumizi ya petrol katika machimbo ya dhahabu ambapo petrol hiyo yaweza kusababisha madini ya risasi (lead) kuingia ziwani.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, uvuvi haramu ambao wavuvi hutumia makokoro na nyavu zisizoruhusiwa; Uvuvi haramu usiozingatia taratibu za kulinda rasimali za za uvuvi na mazingira unaendelea kushamiri katika eneo hilo. Uvuvi huo unahusisha makokoro na nyavu zisizoruhusiwa kama vile matumizi ya vyandarua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sampuli za minofu zimechukuliwa katika Ziwa Rukwa zinaendea kuchakatwa ili kujua kiwango cha zebaki na risasi katika minofu ya samaki na pia kuangalia kiasi hicho kama kipo ndani ya viwango vinavyokubalika na Shirika la Afya Duniani (WHO).