Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 53 Enviroment Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira 463 2019-06-26

Name

Yussuf Salim Hussein

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Chambani

Primary Question

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-

Je, Serikali inafaidikaje na rasilimali ya miti ya mikoko iliyoanzia katika Ukanda wa Pwani ya Tanga mpaka Mtwara?

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa misitu ya mikoko ni pamoja na kuwa mazalia na makazi ya viumbe wa baharini; nan i moja ya vivutio vya utalii nchini; na ni mfumo ikolojia unaosaidia kuondoa kiwango kikubwa cha hewa ukaa (carbon sequestration) ambayo ingeweza kuongeza kiwango cha joto la dunia na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi. Aidha, misitu hii huhifadhi fukwe na mazingira ya bahari kwa kuzuia uharibifu utokanao na mmomonyoko wa fukwe na kingo za bahari, hivyo kuokoa mali na maisha ya makazi ya wakazi wa Pwani kutokana na vimbunga, dhoruba na mawimbi ya bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile misitu hii husaidia kuchuja udongo, uchafu na sumu zinazoweza kutiririshwa na maji yanayoingia baharini ambayo huchangia kuharibu matumbawe ambapo ni makazi ya mazalia ya samaki wa aina mbalimbali. Kwa hiyo, miti ya mikoko ina umuhimu kwa Taifa kama sehemu muhimu ya hifadhi ya ikolojia, huipatia jamii chakula na kipato kupitia shughuli za ujenzi, ufugaji nyuki na kuongeza pato la kaya pia ni chanzo cha mapato kwa Serikali kupitia vibali vya kuvuna miti ya mikoko na biashara ya utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa misitu ya mikoko nchini, misitu hii imekuwa ikihifadhiwa tangu kabla ya uhuru kwa kuchukua hatua ikiwemo kutunga sheria ijulikanayo kama The Tanganyika Forest Laws and Rules Handbook ya mwaka 1947. Baada ya uhuru Serikali imeendelea na jitihada za kuhakikisha mikoko inalindwa. Mwaka 1987 Serikali ilipiga marufuku ukataji wa miti ya mikoko hadi mwaka 1991 ulipoandaliwa mpango wa usimamizi wa mikoko. Chini ya mpango huu, misitu ya mikoko imeendelea kuhifadhiwa na ukataji wake hufanyika kwa kibali maalum kutoka Wakala wa Misitu Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuhifadhi misitu hii, Tanzania inachangia katika malengo ya kidunia ya kupunguza hewa ukaa na kupunguza athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi. Kwa kuzingatia umuhimu wa rasilimali hii, nawasihi wadau wote wakiwemo wananchi wa maeneo ya Pwani na Serikali zote za Mitaa kushirikiana katika kuitunza na kuihifadhi kwa manufaa ya Taifa.