Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 15 Sitting 47 Justice and Constitutional Affairs Katiba na Sheria 397 2019-06-18

Name

Saed Ahmed Kubenea

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Ubungo

Primary Question

MHE. SAED A. KUBENEA aliuliza:-

Serikali ilitangaza kuwa wanasheria wote walioko kwenye mashirika ya umma watafanya kazi chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupunguza gharama za uendeshaji wa kesi na kuwapa ufanisi kwenye ufuatiliaji wa kesi zinazofunguliwa dhidi ya Serikali.

(a) Je, utekelezaji wa agizo la Serikali kuhusu mawakili binafsi kutosimamia kesi za Serikali limefikia wapo?

(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kilichookolewa tangu mashirika ya Serikali yaache kutumia mawakili wa nje?

Name

Dr. Augustine Philip Mahiga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Answer

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Saed Ahmed Kubenea, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yaliyofanywa kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2018 yaliyopitishwa na Bunge lako tukufu, yaliwezesha kufanya wanasheria wote katika utumishi wa umma kuwa chini ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Mabadiliko hayo yalitokana na Tangazo la Serikali Na. 50/2010 lililotambua kuwepo kwa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ambayo amepewa jukumu la kusimamia, kuratibu na kuendesha mashauri yote ya madai ambayo Serikali inashtaki au inashtakiwa.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali tayari imeshatoa maelekezo kwa Wizara na Taasisi zote za Serikali kuwasilisha mashauri yote ya madai dhidi ya Serikali katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uratibu, usimamizi na uendeshaji.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uwezeshaji wa Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa sasa mashauri yote ya madai dhidi ya Serikali yanasimamiwa na ofisi hii isipokuwa kama itaonekana kuwepo kwa ulazima wa kuhusisha mawakili binafsi. Hii hutokea iwapo mashauri husika yamefunguliwa katika mahakama za nchi za nje zisizokuwa za Kimataifa ambazo kwa baadhi ya nchi sheria zake za ndani na taaluma ya uwakili haziruhusu mawakili wa nchi nyingine kufanya shughuli za uwakili hasa uwakilishi mahakamani ndani ya nchi husika.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, inapotokea hitaji la kutumia mawakili binafsi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali hulazimika kutoa kibali cha Serikali cha kuajiri Wakili kutoka ndani ya nchi hiyo itakayoshirikiana na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika kusimamia uendeshaji wa shauri husika.

Mheshimiwa Spika, kuwepo kwa ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kumesaidia kupunguza gharama zilizokuwa zinalipwa na wakili binafsi ambazo kwa tathmini ilifanyika uendeshaji wa kila shauri moja hapa nchini zilikuwa hazipungui shilingi 5,000,000 na kwa upandea mashauri yaliyofunguliwa nje ya nchi gharama za kumlipa wakili kwa kila shauri ilikuwa hazipungui dola za Marekani 300,000 mpaka 2,500,000 kwa kila shauri.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika hotuba yangu ya bajeti 2019/2020 kwa mwaka 2018/2019 Serikali iliokoa kiasi cha shilingi 9,018,957,011 ambazo zingelipwa kwa mawakili binafsi. Ninapenda kulithibitishia Bunge kuwa Serikali itaendelea kuokoa fedha nyingi zaidi ambazo zitasaidia kuleta maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea na kazi ya ukusanyaji wa mashauri yote ya madai kutoka kwa Wizara na Taasisi zote za umma/Serikali. Zoezi hili litakapokamilika litasaidia kufanya tathmini ya kina na kupata thamani halisi ya fedha zilizookolewa na Serikali kupitia maboresho haya mapya. Ahsante.