Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 6 Water and Irrigation Maji na Umwagiliaji 80 2019-09-10

Name

Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MARIA N. KANGOYE Aliuliza:-

Kumekuwa na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuelekea Mikoa ya Shinyanga na Tabora vyenye mitambo yake chanzo cha maji kule Ihelele Wilayani Misungwi, aidha maeneo yanayozunguka mitambo hiyo na yanayopitiwa na mabomba ya mradi huo hayana maji safi na salama.

Je, nini mpango wa Serikali kusambaza maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria kwa wananchi wa vijiji vya Mkoa wa Mwanza hususan maeneo yanayopitiwa na bomba hilo?

Name

Jumaa Hamidu Aweso

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Pangani

Answer

NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maria Ndila Kangoye, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa wa Victoria, Serikali ililenga kufikisha maji katika miji ya Kahama na Shinyanga na vijiji vyote vilivyopo kando ya bomba kuu la kusafisha maji. Kwa wakati huo vijiji vilivyokidhi na kuingizwa katika mradi huu vilikuwa ni vijiji vilivyopo umbali usiozidi kilometa tano kwa kila upande wa bomba kuu. Hivyo, jumla ya vijiji 39 vikiwemo vijiji vitano vya Mawile, Ilalambogo, Lubili, Isenengeja na Ibinza vya Wilaya ya Misungwi katika Mkoa wa Mwanza viliunganishwa na vilianza kupata huduma a maji tangu uendeshaji wa mradi ulipoanza mwezi Februari, 2009.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chanzo cha maji na mitambo ya kusafisha maji kwa mradi wa Kahama - Shinyanga iko katika kijiji cha Nyang’ohomango. Aidha, eneo hilo pia linapakana na vijiji vya Lubili, Isesa, Igenge na Mbalika. Kwa kutambua umuhimu wa maeneo haya kuwa na huduma ya majisafi na salama kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali ilianza ujenzi wamradi wa maji vijiji vya Nyang’ohomango, Isesa, Igenge na Mbalika kwa gharama ya shilingi bilioni 6.1.

Aidha, fedha za kutekeleza mradi huu zinatolewa kwa asilimia mia moja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inatarajiwa kuwa baada ya ujenzi huo kukamilika, jumla ya wananchi 14,606 wa vijiji hivyo na mifugo yao watanufaika na huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kukamilika kwa mradi huu kutawezesha pia kuunganishwa kwa mradi wa maji unaoanzia kwenye kijiji cha Mbalika kwenda katika mji wa Misasi katika Wilaya ya Misungwi ambao pia utahudumia ziadi ya vijiji kumi.