Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 4 Investment and Empowerment Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu 40 2019-09-06

Name

Sikudhani Yasini Chikambo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuza:-

Serikali imekuwa ikitoa mikopo kwa wafanyabiasha kupitia Baraza la Uwezeshaji:-

(a) Je, ni vigezo vipi vinatumika katika kutoa mikopo hiyo?

(b) Je, ni wafanyabiashara wangapi ambao wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma?

Name

Stella Ikupa Alex

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WENYE ULEMAVU) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua tatizo kubwa la mitaji linalowakabili wananchi wa Tanzania na hasa wajasiriamali, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ilisaini makubaliano maalum na Benki ya TPB na Taasisi ya UTT Microfinance kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wajasiriamali. Chini ya makubaliano hayo, miongoni mwa vigezo vya msingi vilivyopaswa kuzingatiwa na waombaji ni kama ifuatavyo:-

(i) Wafanyabiashara wanapaswa kujiunga katika vikundi vya VICOBA au SACCOS kwa ajili ya kupeleka maombi yao ya mikopo;

(ii) Kikundi kinapaswa kuwa na usajili, Katiba na Sera za uendeshaji wa kikundi; na

(iii) Kikundi kinapaswa kuwa na Ofisi inayotambulika, uongozi, mfumo mzuri wa utunzaji wa kumbukumbu za kihasibu na akaunti ya benki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maombi yanayokidhi vigezo husika hupelekwa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa ajili ya kuombewa dhamana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Agosti, 2016, Serikali kupitia Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lilidhamini mikopo yenye thamani ya Sh.542,844,500 ambapo jumla ya wajasiriamali 729 wamenufaika na mikopo hiyo Mkoani Ruvuma kupitia Benki ya TPB. Aidha, Baraza lilidhamini pia mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 kwa SACCOS mbalimbali mkoani humo kupitia Benki ya CRDB. Hata hivyo, Baraza limedhamini wajasiriamali katika mikoa mingine pia ndani ya nchi ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwezi Juni, 2019 kiasi kilichorejeshwa na wajasiriamali waliokopeshwa kwa dhamana kupitia Benki ya TPB ni Sh.430,292,635.60 sawa na asilimia 79.3. Hivyo, natoa wito kwa wakopaji waliosalia, kukamilisha marejesho ya mikopo yao ili Baraza liweze kuwahudumia wafanyabiashara ama wajasiriamali wengine wenye uhitaji.