Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 3 Information, Culture, Arts and Sports Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo 39 2019-09-05

Name

Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza:-

Michezo mingi ikiwemo mpira wa miguu inapata ufadhili sana hapa nchini kupitia kampuni mbalimbali binafsi na za Kiserikali:-

Je, ni lini Serikali itahakikisha ufadhili unapatikana kwenye michezo inayohusu wanawake hususan michezo ya ngumi kwa wanawake?

Name

Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nisahihishe dhana ya kwamba michezo inayowahusisha wanaume inapata “ufadhili sana” nikinukuu maneno aliyotumia Mheshimiwa Mbunge, kuliko inayowahusisha wanawake. Mfano hai ni Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu upande wa Wanaume kwa msimu wa 2018/2019 ambayo ilikosa udhamini na kusababisha matatizo makubwa ya maandalizi na usafiri kwa timu zote 20 zilizoshiriki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ufadhili haushinikizwi na Serikali bali ni suala la hiari upande wa wafadhili ambao huchukua hatua hiyo wakishaziona fursa za kibiashara na kijamii upande wao. Wajibu wa Serikali ni kujenga mazingira rafiki ya ufadhili huo bila kujali jinsia. Hivi sasa Tanzania ina Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu kwa Wanawake ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Vinywaji ya Serengeti Breweries kupitia bia yake ya Serengeti Lite.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa riadha, Kampuni ya Multichoice imekuwa mstari wa mbele kudhamini wanariadha bora wanaojitokeza na kuandaa makambi ya mazoezi bila ubaguzi wa jinsia. Kampuni ya SportPesa pekee imejitokeza kumfadhili Mwanamasumbwi Mwakinyo aliyekuwa namba 174 kwa ubora Duniani katika uzito wake, baada ya kumtwanga Eggington wa Uingereza, wakati huo namba akiwa 8 kwa ubora duniani. Hakuna kigezo kingine kilichotumika na SportPesa kumfadhili Mwakinyo zaidi ya weledi aliouonesha katika mchezo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kuwaomba wadau wote wa michezo nchini wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, kusaidia kushawishi makampuni, taasisi na wadau wenye uwezo kifedha, kudhamini na kufadhili maendeleo ya michezo yote nchini ukiwemo mchezo wa ndondi upande wa wanawake.