Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 16 Sitting 3 Enviroment Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira 32 2019-09-05

Name

Mwantum Dau Haji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Primary Question

MHE. MWANTUM DAU HAJI aliuliza:-

Kasi ya mmomonyoko wa ardhi na uhaba wa udongo katika Visiwa vya Unguja na Pemba inatishia uhai wa Visiwa hivyo:-

Je, ni hatua zipi za makusudi zimechukuliwa katika kuvinusuru Visiwa hivyo?

Name

Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Answer

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), naomba nichukue fursa hii sasa kujibu swali la Mheshimiwa Mwantum Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Visiwa vya Unguja na Pemba vina maeneo takribani 148 yaliyoathirika na mabadiliko ya tabianchi (Pemba 125 na Unguja 23). Athari hizi ni pamoja na mmomonyoko wa fukwe na kuingia kwa maji ya bahari katika mashamba na makazi ya watu. Ili kuvinusuru visiwa hivi dhidi ya athari ya mabadiliko ya tabianchi, Serikali imechukua hatua mbalimbali kupitia miradi inayofadhiliwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mradi wa kujenga uwezo wa jamii kuhimili athari ya mabadiliko ya tabianchi (LDCF) ambao umetekelezwa mwaka 2012 - 2018, shughuli zifuatazo zimefanyika: Ujenzi wa kuta mbili za mita 25 kila moja katika eneo la Kisiwa Panza - Pemba na ujenzi wa makinga bahari (gloynes) matano ya wastani wa urefu wa mita 100 kila moja katika eneo la urefu wa mita 538 Kilimani
– Unguja; upandaji mikoko Pemba maeneo ya Kisiwa Panza hekta 200, Tumbe hekta 10, Ukele hekta 7 na Tovuni hekta 1; na upandaji mikoko Unguja maeneo ya Kisakasaka hekta 8 na Kilimani hekta 1.4.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kupitia Mradi wa Kupunguza Uhalibifu wa Ardhi na Kuongeza Uzalishaji wa Chakula katika Maeneo Kame nchini mwaka (2017 - 2022), shughuli zifuatazo zinategemewa kufanyika katika maeneo ya Micheweni, Kata ya Micheweni na Kiuyu Maziwang’ombe ambazo ni: Kujenga makinga maji katika mashamba (dykes) ili kuzuia maji ya bahari kuingia katika mashamba; kutoa elimu kuhusu kilimo kinachokabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mashamba darasa; upandaji wa miti ili kuhifadhi udongo na kutunza mazingira; na uanzishaji wa biashara ndogo ndogo ili kuwezesha jamii kuwa na shughuli mbadala za kujiongezea kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi; kudhibiti mmomonyoko wa udongo; na kukabiliana na uhaba wa udongo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.