Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 6 Livestock , Fisheries, Agriculture, Food Security and Cooperatives Wizara ya Mifugo na Uvuvi 73 2020-02-04

Name

Dr. David Mathayo David

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Same Magharibi

Primary Question

MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza:-

Serikali iliahidi katika Bajeti ya mwaka 2012/2013 kujenga malambo, majosho na kisima kirefu kwa ajili ya Wananchi wafugaji wa Kata ya Ruvu Jimbo la Same Magharibi?

Je, ni lini ahadi hiyo itakamilishwa?

Name

Abdallah Hamis Ulega

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkuranga

Answer

NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mhe. Dkt. David Mathayo Mbunge wa Jimbo la Same Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia bajeti yake pamoja na program mbalimbali imeendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya maji ya mifugo katika maeneo mengi ya ufugaji hapa nchini ili kupunguza tatizo la maji hasa wakati wa kiangazi kikali. Katika Mwaka huu wa Fedha 2019/2020 Wizara imetenga fedha Jumla ya shilingi 700,000,000 kwa ajili ya kujenga visima kumi na kukarabati mabwawa kumi katika mikoa kumi Tanzania Bara. Katika utekelezaji wa mpango huo, kisima kimoja kinatarajiwa kuchimbwa katika Wilaya ya Same, hususan Kata ya Ruvu ili wafugaji waweze kupata maji kwa ajili ya mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka huu wa fedha 2019/2020 Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kukarabati majosho 161 nchi nzima ili kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe, mbung‟o na wadudu wengine. Mpaka sasa, majosho 46 yamekamilika, majosho 95 ukarabati unaendelea na majosho 20 ukarabati bado haujaanza. Aidha Wizara imejenga josho moja la kisasa Wilayani Bariadi. Pia Halmashauri mbalimbali zinakarabati majosho 288 na zinajenga majosho mapya 84. Kwa Halmashauri ya Same josho moja linakarabatiwa na Wizara katika Kata ya Ruvu-Muungano na matatu yanakaribatiwa na Halmashauri yaliyopo kwenye vijiji vya Mwembe, Bangalala na Mkonga. Mikakati ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mifugo inaendelea kadri fedha zinapopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Napenda kuchukua fursa hii kutoa rai kwa halmashauri zote hapa nchini ikiwemo Halmashauri ya Same kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kujenga, kukarabati na kuendeleza miundombinu ya mifugo katika maeneo yao kwa kutumia fedha zinazopatikana kutokana na makusanyo ama tozo za mifugo.