Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Question

Term Session Sitting Sector Ministry Qn No Date
2015-2020 Session 18 Sitting 1 Industries and Trade Viwanda na Biashara 10 2020-01-28

Name

Saada Salum Mkuya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Welezo

Primary Question

MHE. DKT. SAADA MKUYA SALUM aliuliza:-

Je, ni nini kinasababisha baadhi ya bidhaa zinazozalishwa Zanzibar kupata vikwazo kuingia katika soko la Tanzania Bara?

Name

Eng. Stella Martin Manyanya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nyasa

Answer

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saada Salum Mkuya, Mbunge wa Welezo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa nchi yetu ni moja hatutegemei kuwepo kwa vikwazo vya kibiashara kutoka upande mmoja wa Muungano kwenda upande mwingine. Kinachojitokeza ni changamoto chache za kisheria, kanuni na taratibu ambazo hata hivyo zimewekewa utaratibu mahsusi wa kushughulikia. Utaratibu wa kushughulikia changamoto hizo hufanyika kwa njia ya vikao vya ushirikiano wa kisekta ambapo Ofisi ya Makamu wa Rais imetoa mwongozo wa sekta za pande mbili za Muungano kujadili changamoto kupitia vikao kuanzia ngazi za wataalam, Makatibu Wakuu na Mawaziri na kushauri mamlaka za maamuzi.

Mheshimiwa Spika, chini ya utaratibu huo, sekta ya viwanda na biashara kwa nyakati tofauti imekuwa ikipokea kujadili na kutafutia ufumbuzi changamoto za biashara zilizoibuliwa kutoka pande zote mbili za Muungano, baadhi ya bidhaa zilizowahi kushughulikiwa chini ya utaratibu huo ni pamoja na kuku, maziwa na bidhaa nyinginezo.

Mheshimiwa Spika, namwomba Mheshimiwa Mbunge tuendelee kuwasiliana na kushirikiana katika kushughulikia kwa pamoja changamoto ambazo huenda zikajitokeza ili kuimarisha Muungano wetu na kukuza biashara kwa maslahi mapana ya wananchi wetu kupitia biashara.